Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, May 2, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-48


 Wakati hayo yanaendelea,  familia ya baba mkwe ilikutana, wao kama familia waliamua kufanya kikao maalumu cha wanafamilia cha dharura chenye ajenda moja ya jinsi gani ya kumsaidia mgonjwa wao, kwani penye wengi kuna mengi, lengo ni kama kuna njia nyingine zaidi ya hiyo ya kutibiwa hospitalini, je kuna nini kilichomfanya ndugu huyo afikie mahali hapo, na kama wanandugu wao wachukue hatua gani..

Ndani ya kikao hicho, walihudhuria ndugu wa baba mkwe akiwemo shangazi, mtoto wa baba mkwe ambaye ndiye mchumba wangu, na jamaa wengine wanashibana na familia, pia alikuwemo wakili wa baba mkwe na akaalikwa jamaa mmoja mgeni kabisa katika familia hiyo…...

Kati ya hao ndugu wanaoshibanana hiyo familia mmojawapo alikuwa ni rafiki yangu, ndiye aliyekuja kuniambia jinsi kikao kilivyofanyika;

‘Nakuambia haya kama rafiki yangu uwe na tahadhari kwani hali ya hatari imetangazwa, wewe na mdada, mumewekwa kama maadui wakubwa wa familia hiyo..’akaniambia

‘Usijali, yote yatakwisha na ukweli utadhihiri, na ikifikia hapo wote watarudi nyuma na kugundua kuwa, haki  na ukweli wakati wote una nguvu zaidi ya dhuluma…hebu niambie waliyoyaongea huko kwenye kikao chao ni yapi, au ni siri yenu?’ nikamuuliza.

‘Nitakuambia walichoongea, lakini halahala, usije kumwambia mtu yoyote kuwa mimi ndiye niliyekuambia haya ninakuambia unasikia, wao wananiamini sana kama mwanafamilia, sasa usije ukanivurugia uaminifu wangu, tupo pamaja…’akasema.

‘Siwezi kukusaliti rafiki yangu, …tupo pamoja kama kawaida yetu wewe lete maneno...’nikasema na yeye ndio akaanza kuniambia jinsi kikao kilivyofanyika na yaliyoongelewa;

‘Kikao kilianza kwa kiongozi wa familia ambaye ni mdogo wake baba yako mkwe, yeye alianza kutoa taarifa ya kusudio la kukutana kwao…’akawa anajaribu kuiga sauti ya huyo mtu kwani rafiki yangu huyu anapenda sana kuchekesha;

Alipomaliza kuongea akadakia shangazi yako maana huyo ni mama mdomo, visinipite,akaanza kuongea hata kabla mwenyekiti hajamruhusu kuonyesha yeye anajua zaidi…

‘Jamani hali ya ndugu yetu ni kama mlivyoisikia, ni mbaya sana,kwa maelezo ya mtaalamu ni kuwa kakumbwa na shetani, na bahati nzuri niliposikia hivyo kuwa kaka kadondoka na kupoteza fahamu, nilimpigia simu jamaa yangu huyu hapa, kwa utambulisho huyu ni mtaalamu anaifahamu sana kazi yake, na habahatishi, uliza watu watakuambia…’ akasema shangazi akimtambulisha huyo mtu mgeni

‘Yeye anafahamu, na nilipomuambia akawa keshafahamu tatizo ni nini, na alisisitizia tusimuwahishe kaka hospitalini kwanza, nikawaambia watu wa karibu wa kaka, unajua tena watu wanaojiona ni wa kisasa,hawakunisikia, na mtaalamu akafika kwa haraka, ili tumuwahi kaka  kabla hajapelekwa hospitalini…..’akasema shangazi.

‘Watu wabishi bwana, tunafika wameshamchukua kaka kumkimbiza hospitalini na magari yao,..lakini hata hivyo hakikuharibika kitu, kwani tulikimbilia huko huko hospitalini, na mtaalamu akanipa dawa za kuwahi kumpaka kabla hawajamuwekea madude yao..kazi ikawa kwa madocta,eti keshaingizwa eisiyuuu….’akasema shangazi

‘Jamani sio kila ugonjwa ni ugonjwa wa kukimbilia hospitalini, mtuulizege kwanza, ilitakiwa lifanyike jambo jingine kabla, na huenda yangeliishia hapo hapo nyumbani na asingelifikishwa huko kabisa, wengi waliniona mtu wa ajabu sana, lakini mimi nafahamu mengi, maana nawasiliana sana na hawa watu wanaoitwa wataalamu, na wazee wa zamani....’akasema shangazi

‘Ni hiyo dawa niliyompaka,japokuwa nilimkuta wameshamuwekea madude yao ilisaidia kidogo, na mtaalamu aansema kama tungelimuwahi kabla hajafikishwa hapo, angelimaliza kazi, kwani hilo tatizo sio kama wanavyosema wao, alikumbwa na pepo mbaya, …..ule mshituko, mapigoya moyo yakapanda, ...’akatulia akimwangalia jamaa yake huyo aliyetambulikana kama mtaalamu,. 

Jamaa huyo kwa muda wote alikuwa kainama tu, akitikisa kichwa kama kukubali hivi, kavaa kofia lenye manyoya ya kila aina ya ndege…anatisha usoni.

Kiongozi wa familia akaona amkatishe shangazi kwanza, kwani akimuachia kikao chote kitakuwa chake, akasema;

'Samahani kidogo dada, ni vyema tukamsikiliza kwanza wakili nahisi ana ujumbe muhimu kwetu, akimaliza utaendelea na maongezi yako, maana ni muhimu sana...'akasema huyo kiongozi wa kikao, na shangazi akatulia, na wakili aliyekuwa katulia akiwa kashika kichwa na kuonyesha kuwa na mawazo na kuangalia makabrasha yake, akainua kichwa na kusema;

'Tuendelee kuna kitu nakimalizia kwanza,...'akasema na kiongozi wa familia akasema;

‘Hali ya mzee wetu bado sio nzuri, japokuwa keshaanza kuonyesha matumaini, ila kwa hivi sasa ni vyema, akaachwa na kutulia, sisi tuchukue majukumu yake yale tunayoyaweza, kwa hali kama ile hatakiwi kujua chochote kinachoendelea, japokuwa madakitari wanasema alipozindukana tu kidogo alitaka kuongea na wakili wake,...’akasema kiongozi wa familia akimwangalia wakili, na wakili alipotajwa mara ya pili akasema;

‘Ni kweli nilikwenda kuonana naye, na mengi aliyoweza kuniambia ni maswala yetu mimi na yeye, ni ya kikazi zaidi, sitaweza kuyaongea hapa,tuongee mengine tu, hayo niachieni mimi na mzee ...’akasema, na kiongozi wa familia akasema;

‘Sasa, haya tumuache wakili ana mambo mengi ya kufikiria, ila kama mlivyosikia, ndugu yetu huyu japo anaumwa, lakini kazi kwake wakati wote ipo mbele, hajali hata afya yake, hajli hata umri wake,...hili linazidi kummaliza siku hata siku,...sasa kama wanandugu tunahitajika kumsaidia...’akasema

‘Ni kitu gani kilitokea hadi hali hiyo ikamkuta baba yangu, maana nijuavyo mimi, baba hana matatizo ya shinikizo la damu, mimi sijawahi kusikia, yeye ni mkakamavu mtu wa mazoezi ....?’ akauliza Binti,mchumba wako.

‘Hiyo hali inaweza kutokea kwa yeyote hata kama hana shinikizo la damu, hata kaam ni mtu wa mazoezi, inaweza kutokea tu, pale unapojikuta umesongwa na mawazo, au ukapata mshituko fulani,....akili nayo hufika sehemu ikagoma kufanya kazi, mapigo ya moyo yakashinikizwa, ni tatizo tu, hutokea tu, na huwezi jua huenda baba yako alikuwa na matatizo hayo kabla, lakini hakuwahi kuwaelezea...’akasema wakili wa baba mkwe.

‘Sio shinikizo la damu hilo, mimi namfahamu sana ndugu yangu, nyie mkitaka kujua zaidi, muulizeni huyu mtaalamu niliyekuja naye, atawaambia kila kitu....'akasema shangazi akimuangalia huyu mtu anayeitwa mtaalamu

'Lile ni shetani, alikumbana na pepo mchafu, aliyetumwa, kwa ajili ya kumuangamiza...’akasema shangazi,alipoona huyu mtu katulia haongei kitu na wakati huo wakili alikuwa akitabasamu , na kabla shangazi hajaendelea mwanafamilia mmoja akaingilia na kuuliza;

‘Madakitari wao wanasemaje, baada ya kupelekwa huko?’ akauliza huyo mwanafamilia mwingine ambaye alikaa karibu na wakili.

‘Wanasema ile hali mbaya imeshaondoka, sasa hivi wanacheza na kushusha shinikizo la damu ambali wanasema lilipanda sana...dakitari anasema kuna kitu kilitokea, ambacho kilimshitua sana mzee, au kuna shinikizo fulani...'akasema huyo jamaa na wakili naye akaongezea kwa kusema;

'Ni kweli, hata dakiatari aliniulizia kuna kitu gani kilitokea kwa huyo mgonjwa , kwani hali kama ile, ina sababu zake, je wakati hali hiyo inatokea kulikuwa na maongezi gani, ni nani alikuwepo, sikuweza kumjibu, maana tukio hilo limetokea mimi sipo naye....’akasema wakili

'Unaona mnazunguka tu mkikwepa ukweli niliowaambia...'akasema shangazi na mwanafamilia mwingine akauliza

‘Unahisi kuna jambo baya alilisikia, au kuna kitu kilimpandisha hasira, na ni nani alikuwa naye wakati hali hiyo inatokea ....?’ akauliza mwanandugu huyo, akimuangalia wakili.

‘Unajua mzee ana shughuli nyingi, nilishamshauri kuwa aachane na majukumu mengine, lakini kama umjuavyo mzee, kila kitu anataka akifanye yeye, au akifuatilie yeye mwenyewe,, kiukweli kwa umri wake alitakiwa awaachie majukumu watu wengine lakini mzee ni mtu asiyependa kupumzika,...hilo ndio tatizo lake, japokuwa kwa namna nyingine inamsaidia kwani anaweka mwili na akili yake iwe inafanya kazi...’akasema wakili.

‘Lakini nahisi kuna jambo limetokea ambalo limemshitua mzee, sio bure, baba sio mtu dhaifu kihivyo...’aksema mchumba wako.

‘Hivyo nyie hamumuamini hayo ninayowaambia huyu mtaalamu, amesema kaka kakumbwa na shetani mbaya, pepo mbaya...nyie mtakuwa mnajidanganya na madakitari wenu, eti shinikiza la damu, hivi mambo kama haya yalipokuwa yakitokea kwa mababu zetu kulikuwa na vipimo kama hivyo...mambo kama hayo yalitokea, na wao walijua ni sababu gani, na watu wakatibiwa, siku hizi mnakimbilia mahosipitalini, mnawekewa madude gani sijui...mnaona yanayowakuta....’akasema shangazi.

‘Lakini shangazi hilo ni tatizo linalojulikana ni shinikizo la damu,linafahamika kitaalamu, na lina taartibu zake za kiutibabu....’akasema wakili.

‘Jidanganyeni tu na mambo yenu hayo, ...hilo sio shinikizo la damu, kama asingelikuja mtaalamu akaliondoa hilo pepo kabla hajafikishwa huko, tungelimpoteza kaka kabisaa,....’akasema shangazi.

‘Mimi najiuliza wakati hali hiyo inatokea alikuwa na nani, alikuwa akifanya nini, huyo mtu ndiye muhimu wa kutuambia, iwe ni pepo au shinikizo la damu, lakini mimi naona kuna umuhimu wa kujua chanzo kilianzia wapi, ...ni lazima kuna jambo...’akasema jamaa mwingine.

‘Hayo hatuwezi kuyafahamu kwa sasa, ni mpaka mwenyewe aje kuyazungumza kama atapenda kufanya hivyo....’akasema wakili

‘Sasa sisi tufanye nini kama wanafamilia....?’ akauliza mtu mwingine

‘Tulipize kisasi kwa yoyote aliye nyuma ya hili, bila kufanya hivyo hawa watu watazidi kutuchezea, kumbuka enzi za kaka, hakuna mtu aliweza kumchezea, walikuwa wakimuogopa, sasa sijui hiki kidudu mtu kimetokea wapi..’akasema shangazi

‘Kwanini kisasi , kwani kuna kitu gani cha kulipiza kisasi?’ akauliza wakili akionyesha mshangao.

‘Mimi nafahamu kuwa kaka ana shughuli zake nyingi tu, na alikuwa na watu anawaamini, akawapa majukumu, sasa hawa watu wamekuwa wakimgeuka, na kufanya mambo yao mabaya huku wakimsingizia kaka yangu, lakini hili tukio la yeye kudondoka na kupoteza fahamu ni la ghafla, na huenda hakuwa na mtu...’akasema shangazi.

‘Hayo ni yakusikia, naomba hayo tusiyazungumze, na wala tusijitie kwenye matatizo ya kulipiza kisasi kwa jambo ambalo halina uhakika, hata yeye kasema tusifanye lolote kwa sasa mpaka hapo atakapotoka hospitalini...’akasema wakili

‘Mimi nasema hayo nikiwa na uhakika,kuna watu wapo nyuma ya haya, ambao sasa wanatumia mbinu hizo za kuwatupia wenzao mashetani, wameona njia nyingine hazifanikiwi...’akasema shangazi

‘Uhakika gani ulio nao shangazi kwa hayo unayoyasema.....shangazi mimi nilikuwa na ombi kuwa kama kuna mambo unayohisi yamefanyika ni vyema ukamwambia wakili ili ayafahamu, na aangalai jinsi gani ya kufanya, lakini hayo mambo ya mashetani, mimi siyaelewi,...’akasema mchumba wako na shangazi akamgeukia wakili na kusema;

‘Kwanza yupo mdada, huyu anajifanya kujua sana, kuna mambo kayatengeneza kwa kaka yangu ili kaka aonekana ana fanya biashara haramu, hilo ni muhimu ulichunguze na uangalia jinsi gani ya kumshitaki huyu mtu, kama ndivyo mnavyotaka, hili niliwahi kuongea na kaka, lakini kama mnavyomfahamu kaka, hajali, na anasema hakuna anayeweza kumfanya lolote,sasa unaona matokeo ya dharau zake....’akasema

‘Hayo naombeni tuyaache, tusiende mbali kiasi hicho, mimi nitaongea na mzee, nitajua ni jinsi gani ya kufanya...’akasema wakili

‘Wewe fanya kazi yako, na sisi kama wanafamilia ni lazima tufanye kazi yetu, ni lazima hawa watu, mdada, na huyo mkwe wa uwongo, huyo mchumba wako, ambaye anajifanya ndumila kuwili, hawa watu wawili na wakili wao...ni lazima tupambane nao...’akasema

‘Kwa vipi, mimi sioni kwamba wana ubaya kihivyo, ...’akasema mchumba wako

‘Wote hao lao moja, nia na madhumuni yao ni kumuangamiza ndugu yangu, na wanafanya hayo wakidhania sisi tumelala, hatujui wanachokifanya, sasa ni muda wa kuwaonyesha kuwa na sisi tupo macho, ni lazima tuwashughulikie....’akasema shangazi

‘Ina maana hata mhasibu anahusika?’ akauliza mchumba wangu

‘Saana, tena huyo ndiye mbaya zaidi maana ni ndumila kuwili,  yeye ndiye mtoa taarifa kutoka ndani ya familia yetu, na kuwapelekea hao watu wake, hebu niambie siku ya tukio la kumuua mtoza ushuru, huyu mhasibu alikuwa wapi,  si alikuwa kwa mdada, wakifanya ufusuka wao na kupanga mipango yao,...’akasema

‘Shangazi una uhakika?’ akauliza mchumba wako.

‘Kama unabisha nenda kawaulize polisi, wao kwa mdomo wao wanasema mhasibu alikuwa kalala kwa mdada usiku wa tukio, na asubuhi akataka kukimbia wakamdaka, hata yeye ukimuuliza hawezi kukataa, atakachosema kujitetea ni kuwa mdada, alipandisha, na nijuavyo mimi hilo shetani la mdada likipanda, linachukiwa wanaume, sasa hebu niambie kwanini yeye aliweza kubakia humo asidhurike...’akasema shangazi

‘Shangazi una uhakiika na hayo?’ akauliza mchumba wangu

‘Unataka uhakika gani wewe binti, hivi mimi unaniona mtoto wa juzi,...kabla ya kukuambia haya, nikuambie ukweli, nilishafanya utafiti, wa kisasa, na huu wetu wa kumtumia mtaalamu, huo wenu wa kisasa, nimeongea na maaskari wanaohusika, wakaniambia yote...’akasema

‘Polisi wanaweza kukuambia mambo kwa nia ya kuficha ukweli, ukweli wote wanaufahamu wao wanasubiri kuuelezea kwenye mahakama...’akasema mjumbe mwingine, na wakati huo wakili alikuwa akiongea na simu na watu wake, hakutaka hata kusikiliza hayo maongezi, lakini hakuondoka.

‘Tangu tatizo hilo lianze, niwaambie ukweli, sijakaa chini, nimehangaika hadi kwa hawa wataalamu, ndio maana nikamlete huyu mtaalamu awathibitishie mwenyewe....’akasema kwa kujiamini.

‘Shangazi haya yanayoendelea hapa hayahusiani na imani zako za giza, wenzako wanatumia mbinu za kisasa...’akasema mchumba wako.

‘Tatizo lenu nyie mnajifanya mumesoma, na ujinga wenu huo ndio unaofanya muumie na kujikuta mnahangaika, wakati matatizo mengine hayahitaji mambo yenu ya kisasa,..sikiliza mimi nimeshatembea kwa wataaalmu zaidi ya mmoja, na wote wameniambia hayohayo...’akasema

‘Hayo hayo yapi...?’ akaulizwa na mjumbe aliyeonekana kuyaamini sana hayo anayooongea shangazi.

‘Wote wameniambia...mhasibu anatembea na mdada kwasababu shetani lake linamkubali, vinginevyo, angeshaangamizwa, kwani shetani la mdada halina urafiki na wanaume...’akasema shangazi.

‘Na hao wengine, wakili wao, na wengine, wengi tu, nia yao kubwa ni kuhakikisha ndugu yangu hawezi kufanya kazi anazozifanya, wanasema anaweka kiwungu, keshastaafu bado anang’ang’ania madaraka...kwahiyo wanataka wamuondoe kwa nguvu...’akasema

‘Makubwa hayo, ....sasa ukaambiwa tufanye nini, au huyu mtaalamu ndio kaja kuyamaliza, maana hapo tunatakiwa kujifunga au?’ akauliza huyo mjumbe.

‘Kazi za kisheria tumuachie mwanasheria, na kazi za kifamilia na mambo yetu tunatakiwa tufanye wenyewe,  hawa watu tuwashughulikie kwa kila njia, ni lazima waokote makopo, na kuzalilika, kama huyo mchumba wako anajiona kidume cha kutembea na kila mwanamke, basi tuhakikishe, bakora yake haifanyi kazi, hilo niachieni mimi....’akasema shangazi akimwangalia huyo jamaa aliyembulishwa kama mtaalamu, na huyo jamaa akatingisha kichwa kukubaliana.

‘Shangazi, mbona umekwenda mbali hivyo, ...’akalalamika mchumba wako

‘Kuna njia nyingine ya kibabe zaidi,...mimi nawafahamu wahuni wote wa mjini, wengi ni marafiki zangu kutokana na kazi zangu za hapa na pale,hawa watu ukiwalipa pesa ndogo tu, wanahakikisha hawa watu wanazibwa mdomo...na sio kuzibwa mdomo tu, ni kuhakikisha wanasahaulika kabisa....’akasema shangazi

‘Kwanini tufikie huko shangazi, kwanza hatuna uhakika na hilo,  na ukumbuke mhasibu ni baba wa mtoto wangu...’akalalamika mchumba wako.

‘Sikiliza wewe mtoto ni nani bora kati ya huyo mhasibu aliyekubaka, na baba yako?’ akaulizwa

‘Baba yangu ni bora...lakini...’akasema

‘Lakini nini tena...hakuna zaidi ya wazazi wako, baba yako katamka waziwazi, mhasibu mdada, na kundi lake wamemsaliti...sasa unataka uelewi vipi tena, hapo, nikuulize je upo tayari baba yako aangamizwe na watu wenye roho mbaya hata kama ni mchumba wako?’ akauliza

‘Kwakweli sipo tayari hata kama ni nani,..lakini cha muhimu ni uhakika wa hilo, je ni wao kweli, je yeye anahusika, au wanamsingizia tu, nakumbuka shangazi mwanzoni ulisema mhasibu anasingiziwa mambo mengine, ...’akasema binti

‘Unataka uhakika wako hile eehe, basi nenda chumba cha wagonjwa mahututi ukamuone baba yako akipumulia mashine, kama kweli una huruma na baba yako pambana na hao waliomfanya awe hivyo,hata kama anasingiziwa, lakini yupo na hao watu, wote watawajibika, mimi kwa hivi sasa sijali...’akasema kwa hasira na Binti alipotaka kusema akamnyoshea mkono kumnyamazisha na kuendelea kusema;

‘Kama mapenzi yamekughilibu akili yako, kiasi hicho, basi ujue mimi sitakuwa na wewe, tutakosana kabisakabisa, kwanza mtu mwenyewe ameshakuonyesha moja kwa moja kuwa ana hawara, unataka nini tena, achana naye, wanaume wapo wengi wazuri, pia sisi tutataifisha mali yote, keshaiandikisha kwa mtoto na wewe, ana nini tena, mjini shule, kama hujui rudi kijijini ukajipange ...’akasema

‘Shangazi, mimi sijakataa, ila ni vyema tukawa na uhakika, kwasababu wao wana mawakili,na wanafuata sheria, au wanafanya huku wakijua jinsi gani ya kujikinga kisheria, kwahiyo na isis tuwe makini kwa hilo....’akasema

‘Uhakika gani unaoutaka wewe, ina maana huniamini mimi, ....huyu hapa ndiye mtaalamu anayeaminika, anaitwa kila mahali kuwadhibiti watu kama hao, hakimshindi kitu, ...kama mnabisha anaweza kuwathibitishia mwenyewe hapa ...’akasema akimuonyeshea yule jamaa ambaye kwa muda mwingi alikuwa kimiya,akitikisa kichwa kukubali au kukataa, utafikiri hawezi kuongea, na alipotajwa akainua kichwa na kukitikisa mara nyingi.

Watu wote waligeuka kumwangali, na yeye akawa ametoa macho kama mtu aliyeoona kitu cha kutisha, akatikisa kichwa chake tena mara nyingi, na kuhema kwa haraka haraka, alikuwa kama anaona kitu cha kutisha, nay eye anajaribu kukikwepa, halafu kwa sauti ya juu akasema;

‘Mdada, ana shetani lenye nguvu sana, haingiliki kirahisi, ...mdada ana nyota kali sana, mdada, ana nyota na nguvu ya utawala, huyu mwanamke sio mchezo,sivyo kama mnavyomuona, kajivika ngozi ya kondooo, ..huyu atawaangamiza....haaaaah...na kundi lake lote linamtegemea yeye,....haaaah, ’akasema

‘Sasa tufanye nini?’ akaulizwa

‘Kwanza ni kumuondoa huyu mtu haraka iwezekanavyo, japokuwa ni kazi ngumu sana, kama nilivyowaambi huyu mtu ana nyota kali ya utawala na nguvu, sasa kama kuna njia nyingine mnaifahamu nyie ifanyeni kwa haraka, mimi siwezi kuwaambia ni njia gani, sina mamlaka na mambo hayo na nionavyo naona kama mumeshachelewa, lakini jaribuni…., mkichelewa na …mumeshachelewa,….jaribuni,...’akasema akiwa kama anaangalia hewani

‘Tusaidie mtaalamu, tufanye nini....?’akauliza shangazi

‘Fanyeni mfanyalo,...uwezo wa kumfanya lolote upo mikononi mwenu, sio kwetu, ila kwa tahadhari, huyu mtu mkimuachia mtamalizwa nyie, keshaanza kazi, mmoja baada ya mwingine atadondoka, mtapotezana, mtafungwa, mbele yenu kunaonekana mtando wa giza,gizaaa....’akasema na kutulia kimiya huku jasho likimtoka kwa wingi .

Kilipita kitambo, na yule mtu akatulia na kuangalia huku na kule, akainuka akijaribu kutikisa kichwa kama kuondoa vitu kichwani mwake,halafu akahema, na alipotulia, vyema, akainua kichwa na kumuangalia shangazi akasema;

‘Mimi naondoka, kama mumesikia mliyoambia fuateni, mimi naondoka nina safari leo hii hii, hata hivi sasa nimeshachelewa kuna mteja nahitaiika kumuona, ...’akasema

‘Lakini mtaalamu umetuacha njia panda, tufanye nini…?’ akauliza shangazi

‘Kazi iliyobakia ni ya kwenu wenyewe,siwezi kuwadanganya..mnahitajika kuhangaika kweli kweli, kunaonekana kuna jambo limejificha ndani ya familia yenu gumu sana kulitatua, linahusiana na mambo mabaya….’akasema

‘Mambo mabaya, kama yapi?’ akauliza shangazi

‘Hayo siwezi kuyataja, ila inaonekana sheria inawaandama,kuna ukiukwaji wa sheria na mlifanya hivyo awali wakati nyota yenu  inang’ara lakini sasa imeshafifia, …mna wakati mgumu sana wa kujisahihisha,..inabidi muhangaike kwelikweli,sio mchezo hapo, kwangu mimi sina cha kufanya…’akasema

‘Kwahiyo huwezi kutusaidia kwa hili?’ akauliza jamaa mwingine

‘Mhh,kiukweli, siwezi kuingilia huko, kila kazi ina mipaka yake, mipaka yangu inaishia hapo, huko kwenye sheria, uvunjasji wa sheria, na ….hapana, huko mimi siruhusiwi kabisa kupagusa, nina mafungamano na masharti makali ya kazi yangu,...fanyeni mlichoambiwa kabla hamjachelewa...mimi naondoka, sina muda tena hapa…’akasema na kuanza kuondoka

Wanafamilia walibakia wakiangaliana, na shangazi akasema;

‘Mnaona, kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na tunatakiwa tufanye jambo kwa haraka, mimi namfahamu sana huyu mtu, hasemi uwongo,na kama jambo halina muafaka, atawaambia ..’akasema shangazi

‘Kwa mtizamo swala hili la ndugu yetu halina ujanja, ni swala la kisheria, basi mimi naona tumuachie mwanasheria.....’akasema ndugu mwingine

‘Yeye afanye kazi yake kisheria na sisi tuhangaike kivyetu, ….niliwaambia toka wali,sio swala la kisheria tu, mumesikia wenyewe, ..., kazi imeshaanza, na tusipojitahidi tutampoteza ndugu yetu hivi hivi, hatujui ni nani atafuata, ila mimi sikubali,mimi nitahangaika juu chini...’akajipiga kifua kama kutamba.

‘Shangazi,...mbona haya mambo ni ya kutisha,...mmh, ....’akasema mchumba wako.

‘Ni ya kutisha kwa vile nyie vijana mnayapuuzia, ..., lakini nina uhakika haya yote ni mambo ya mdada, na shetani lake, kama alivyosema mtaalamu kuwa nyota yake kwa sasa ina nguvu, lakini kuna  namna ya kuivunja nguvu, nitakwenda kwa mtu mwingine….’akasema shangazi

‘Lakini nilivyomsikia vyema huyu mtaalamu tatizo hapo ni uvunjaji wa sheria, ..mimi naona muhimu ni kumuachia wakili apambane nalo sizani kama ni mambo ya kishirikiana….’akasema mtu mwingine akimuangalia wakili, wakili yeye muda mwingi alikuwa akisoma makabrasha yake.

‘Yeye afanye kazi yake kisheria,na sisi……tutafanya yetu…’akasema shangazi

‘Mhh hapo sielewi kitu, wewe shangazi unataka tufanye nini?’ akauliza mchumba wako

‘Kulipiza kisasi kwa hawa watu, maana nila wao hili tatizo lisingelikuwepo, huyu mchumba wako na mdada ni lazima tuwafanyizie…, lakini adui mkubwa ni huyo anayetaka kukunyang’anya mchumba wako…’akasema

‘Mhh,mimi naona mambo haya ni kuyatisha,hata mimi sasa naanza kuogopa, nina wasiwasi na baba, sijui kafanya kitu gani kibaya, lakini baba ni mchapakazi, hataki utani, sizani kama anaweza kuvunja sheria, …..’akasema.

‘Unaonaeeh, mimi ndio hapa nasema ni lazima tufanye kazi..sasa nakuuliza kwa mara ya mwiho je upo tayari kukosa yote, mchumba na wazazi wako, maana haitaishia kwa ndugu yetu, itakuja na sisi sote wanafamilia, hebu niambie upo tayari kukosa yote...’akasema shangazi na binti akainuka kama anataka kuondoka.

‘Unataka kwenda wapi, tulia hapa, usitake kuharibu mambo…kama unapanga kwenda kuongea na huyo mchumba wako, kuanzia sasa ni marufuku kuonana naye, hutakiwi kuongea na huyo mtu kabisa, mpaka tumalize kazi yetu, unanisikia, huyo ni mbaya wako, ni adui wa hii familia,tunatakiwa tupambanae naye na washirika wake,...’akasema shangazi

‘Sasa tufanye nini?’ akauliza jamaa mwingine

‘Kwasasa niachieni hiyo kazi mimi…kazi ya kisheria ipo mikononi mwa mwanasheria,wakili wa kaka atafuatilia, mengine yapo mikononi mwetu, kuna msaada nahitaji kutoka kwanu, hasa wa kifedha, ikishindikana sina budi kuongea na kaka japokuwa sio wakatii muafaka wa kuongea naye, ni azima niongee naye kinamna, nahitajia msaada wake, ...’akasema

‘Msaada wa kitu gani?’ akauliza mwanasheria akiwa kasimama akitaka kuondoka huku akiangalia saa yake.

‘Ninachohitajia kwa sasa ni pesa, pesa nyingi, kuna watu natakiwa kuwapa hii kazi, na hao watu hawawezi kuifanya hii kazi kwa pesa ndogo, nataka pesa nyingi sana....’akasema shangazi.

‘Unataka wafanye kazi gani?’ akauliza wakili akimwangalia kwa mashaka…

NB: Haya vita imeanza, kesi imeanza, je haya yataishia wapi


WAZO LA LEO:Ukweli unauma,hasa unapogusa masilahi yetu,hakuna atakyekubali kuwa mali aliyo nayo ni ya ufisadi, hata kama ni kweli kaipata kwa ufisadi au kwa njia ambazo sio za halalimtu kama huyu atatafuta kila namna ya kuhalalisha ufisadi wake huo hata kama ni kwa kubadili mikataba na kugeuza vifungu vya sheria vilivyopo, hata kama ni kwa kunukuu maandishi matakatifu kwa namna ya kuhalalisha ufisadi wake huo, ...mara nyingi dhuluma hujaribiwa kulindwa kwa dhuluma, lakini hala hala, dhuluma ikidumu sana, kinachofuata ni maasi, amani inakuwa haipo tena, kwani dhuluma haidumu ikidumu inadumirisha.

Ni mimi: emu-three

No comments :