Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, April 29, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-47


‘Mlinzi wa mdada ameshakamatwa , yupo mikononi mwa polisi....’akasema mpelelezi, nilipokutana naye tena, safari hii alikuja rasmi akiwa na kibali cha kuonana na mimi.

‘Mhh,kakamatwa! Alikuwa wapi?’ nikauliza

‘Amewaambia polisi kuwa alipatwa na dharura ,alitumiwa ujumbe kuwa mtoto wake aliyekuwa kijijini anaumwa, na bahati mbaya simu yake ikaibiwa, kwahiyo hakuweza kuwasiliana na bosi wake, ...inawezekana alikuja na hadithi ya kutunga au ni kweli ilitokea hivyo, polisi hawakutaka zaidi, nia yao ilikuwa ni kumkamata tu kwani wao kama wanavyodai,walishakuwa na ushahidi kuwa ndiye aliyehusika na hayo mauaji ya mtoza ushuru.

'Na mlinzi huyo hakuwa na jinsi, akakamatwa na kumweka mahabusu, na baadaye kwa haraka wakamfikisha gerezani sehemu yenye ulinzi mkali...’akasema

‘Oh, mbona wamemfanyia haraka hivyo, inaonekana kweli wana ushahidi wa kutosha na hawataki kupoteza muda, ...au kufanya makosa...’nikasema

‘Ndivyo walivyosema, na hakutakiwa kuonana na mtu yoyote, hata wakili wake alizuiwa kwa muda, na wakili huyo alikuja kuonana na mteja wake baadaye kabisa...’akasema

‘Hiyo sio haki.....au sio?’ nikauliza huku nikishindwa kuficha furaha yangu moyoni kuwa hatimaye kesi yangu itakuwa imeshafutika kabisa.

‘Wakati mwingine inabidi ifanyike hivyo, ili kupata taarifa nyeti,..kabla hazijachaachuliwa, japokuwa kwa huyo mlinzi, walishachelewa, ....’akasema

‘Kwa vipi,...wamechelewa kwasababu gani?’ nikauliza

‘Jamaa alishajipanga, anafahamu aseme nini, na alishajua ni kitu gani polisi watamuuliza, sizani kama wanajambo jipya dhidi yake, ....’akasema.

‘Kama ni hivyo, kwanini sasa waseme kuwa wana uhakika kuwa ndiye aliyefanya hayo mauaji?’ nikauliza

‘Polisi ndivyo wanavyosema, na wamesema safari hii hawataki utani tena ni lazima haki itendeke,kwani wana ushahidi kamili wa kumbana huyo mlinzi,kuwa yeye ndiye aliyemuua mtoza ushuru, na hawataki kumchelewesha, watamfikisha huyo jamaa mahakamani haraka iwezekanavyo....’akasema

‘Hebu niambie kwa uchunguzi wako wewe, je ni kweli huyo mlinzi ndiye aliyafanya hayo mauaji, kwa uchunguzi wako wewe uligundua nini, hebu niambie ulivyoona wewe ilikuwaje siku ile....?’ nikamuuliza

‘Jinsi ilivyotokea, ukichunguza kwa makini ni tukio lililopangwa kwa utadi wa hali ya juu, sio kwa bahati mbaya,.....huyu jamaa aliyekuja kumuona huyo mlinzi wa mdada, alifika na kutoa amri, na mlinzi akatii bila kupoteza muda, ...kama angeluwa hawajawasiliana au hawajuani, au ni swala la kupewa chochote, kungelikuwa na maongezi ya kubishana ....lakini haikuwa hivyo,...’akasema

‘Pili huyu mlinzi alipotoka pale getini, hakuingia ndani moja kwa moja, alichofanya yeye ni kuelekea kwenye gari la mdada, na humo alijua kuna kitu gani ambacho angeliweza kukitumia, japokuwa kulikuwa na vyombo vingine, lakini yeye alichagua nyundo. Hii nyundo ina maana gani, ....’akatulia kidgo.

‘Siwezi nikathibitisha hilo, kuwa huenda nyundo ilikuwa na maana fulani, lakini kwa haya makundi kila jambo lina ishara zake, na baada ya tukio hilo, hiyo nyundo ilitoweka, huyo mlinzi hakuwahi kuirudisha hapo, au kuonekana sehemu yoyote....Hapo utaona kama ni kitu kilichokuwa kimepangiliwa, kwa namna fulani....’akasema

‘Unavyosema alikuja huku kwenye maegesho magari, kauli yako inanifanya niwazie mengine, ni kama vile upo kwenye hayo maegesho na huyo mlinzi akafika eneo hilo ulipokuwepo wewe,hebu nifafanulie vyema hapo?’ nikauliza

 ‘Alipofika kwenye eneo la magari, akaingia kwenye gari la mdada, ...akitumia ufungua bandia, akafungua mlango na kuingia ndani ya hilo gari, alikaa kidogo, na kutoka akiwa kashikilia hiyo nyundo, akaichomeka kwa nyuma, kama wanavyofanya watumia bastola...

‘Haraka akasogea kwenye madirisha na kuanza kuchungulia ndani,...nahisi alikuwa akihakiki usalama, na baadaye akatoa pisipisi,.....unaona kwenye ule mfuko, alichukua na pisipisi, ambayo ndiyo aliyoitumia kupachulia kiyoo cha lile dirisha, akasogeza kiyoo, nahisi hilo dirisha, lilikuwa halifungi vyema au alishalilegeza kabla...’akasema

‘Akaingia kwa kuruka dirishani,i...’akasema

‘Halafu ikawaje?’ nikamuuliza

‘Sijui yaliyotokea huko ndani...’akasema na mimi nikamwangalia kwa mashaka, nikauliza

‘Hebu niambie ukweli, ...unavyoongea ni kama vile ulikuwepo kwenye tukio,...’nikasema

‘Ni kweli...mimi nilikuwepo kwenye eneo hilo.....’akasema na kunifanya nibakie mdomo wazi

‘Kweli, ina maana ulikuwepo!!!....’nikamaka

‘Ndio maana nikawa nakusisitiza useme ukweli,...kwani ukweli mwingi naufahamu, ...’akasema

‘Kama ni hivyo, kwanini hukuwaambia polisi?’ nikauliza

‘Mimi nafanyakazi kivyangu, ...lakini mwisho wa siku ni lazima yote hayo wayafahamu polisi, kwa hivi sasa sijamaliza kazi yangu, bado nakusanya ushahidi wangu, kwa kazi yangu maalumu.....’akasema

‘Wewe unamfanyia nani hiyo kazi?’ nikamuuliza

‘Nchi yangu....’akasema

‘Hata polisi wanafanya kazi kwa ajili ya ncho yao au sio?’ nikauliza

‘Halikadhalika,..... lakini kila mmoja ana malengo yake...’akasema

‘Hebu niambai zaidi kuhusu huyu mlinzi, kwa jinsi alivyoipata hiyo silaha, ....hiyo nyundo?’ nikamuuliza.

‘Ni kama nilivyokuelezea, aliipata kutoka kwenye gari la mdada....’akasema

‘Ehe....’nikasema

‘Japokuwa mimi baadaye mimi nilipata nafasi ya kuingia kwenye gari la mdada na kuangalia vyema, ndipo nikagundua mkoba uliokuwa na vifaa vya ujenzi, humo kulikuwa na msumeno, misumari, na vifaa mbali mbali vya ujenzi, ina maana mdada, alikuwa kaviweka hivyo vifaa kwa ajili ya kumpelekea fundi, ....’akasema.

 ‘Kwanini Polisi hawakuligundua hilo?’ nikauliza

‘Polisi wana malengo yao na mimi nina malengo yangu totauti,...sio kila kitu ni muhimu kwao, mimi nafanya kazi kwa undani zaidi kuhakikisha napata kiini cha haya matatizo, ili ning’oe mti na mizizi yake, ...kwahiyo kazi yangu ni polepole na kwa umakini zaidi,na kila kitu kilichotokea kwangu ni muhimu, ....’akasema

‘Lakini huoni kwamba kama ungeshirikiana na polisi ungeliwarahishia kazi yao..’nikasema

‘Yah..ni kweli, lakini kwa hali ilivyo, ni bora iwe hivi,...’akasema

‘Kwahiyo uliona kabisa huyo mlinzi akiingia kwenye hilo gari na kutoka, akaingia kwenye hiyo nyumba kwa kupitia dirishani na kutoka lakini hufahamu ni kitu gani kilitokea huko ndani?’ nikauliza

‘Yah...huko ndani nisingeliweza kufahamu maana mimi nilikuwa nje, na nilikuwa sehemu ya kujificha, nisingeliweza kutoka na kuangalia huku na kule,...na ukumbuke baada ya muda, polisi nao walishafika kwenye hilo eneo, kwahiyo mimi nilitakiwa nitafuta mwanya wa kutoka hapo kwa haraka, sikupenda kukutana na hao watu, ...’akasema

‘Lakini ni watu wa idara yako...’nikasema

‘Yah, ...hata kama ni watu wa idara yangu, lakini malengo yetu ni tofauti....’akasema

‘Kwahiyo wewe ulimuona mlinzi wakati anatoka kutoka ndani ?’ nikauliza

‘Nilimuona wakati anatoka, ..alitoka kwa njia hiyo hiyo aliyoingilia, akiwa na mfuko mkononi kuonyesha kuwa kabeba kitu fulani, ....’akasema

‘Kitu cha namna gani,..kwa mtizamo wako?’ nikauliza

‘Kitakuwa sio kitu kikubwa,....nahisi inawezakana ikawa CD’s, au hivi vifaa vidogo vya komputa vinaweza kubebe kumbukumbu nyingi..’ akasema

‘Kwahiyo kumbe alijua ni kitu gani anakitafuta, ....kwani angelijuaje hicho kifaa?’ nikauliza

‘Huyo mlinzi ameenda shule,...na anafahamu sana maswala ya komputa, ni fundi wa mambo mengi sana, akiwa jeshini, alikuwa fundi mzuri, lakini kwa matatizo ya kiafya aliacha kazi, akaenda kutibiwa, na aliporudi hakutaka kuendelea tena na kazi hiyo ya jeshi, akawa mlinzi wa watu binafsi,....amefanya hiyo kazi sehemu mbali mbali, na hakuwahi kufanya jambo lolote baya.....’akasema

‘Mhh,....nahisi sio kazi hiyo ya ulinzi peke yake, nahisi ana kazi za siri...’nikasema na mpelelezi akaniangalia kwa haraka na kusema

‘Seehemu niliyokuwepo, ilinifanya nisione mengi, nilijaribu sana kuchunguza, lakini sikuweza kupita kwa mbele ya nyumba, kwani kama ningelifanya hivyo, huyo mtu aliyeachwa getini, angeliniona...’akasema

‘Mimi najiuliza,  wewe uliwezaje kuingia na kutoka bila kuonekana ...?’ nikamuuliza

‘Kwa muda mwingi,mimi nilikuwa nje...., na nilikuwa upande wa nyuma, niliingia kipindi kile kile wakati mlinzi anaongea na huyo jamaa mwingine. Huyo jamaa alivyokuwa amevaa usingeliweza kumtambua ni nani,...alikuwa kavaa kofia pana, alilolishusha na kuficha uso,....na akavaa koti refu  utafikiri anajikinga na mvua...’akasema

‘Unasema  kwa muda mwingi ulikuwa nje ya hilo jengo,...kwahiyo ulimuona huyo mtu akifika,...huyo mtu aliyeongea na mlinzi na wakafanya waliyoyafanya,  je huyo mtu alifika kwa usafiri gani, kwa mguu au kwa pikipiki?’ nikauliza

‘Ndio nilikuwepo hapo nje, nikijaribu kuchunguza mambo yanayoendelea humo, na nilishasikia kuwa mdada ni mgonjwa,...na wewe umo humo ndani, ....’akasema

‘Kwahiyo ulifika hapo kutaka kufanya nini?’ niamuuliza

‘Nilishagundua kuwa kuna jambo linaloendelea hapo,...nilifika hapo nikimfuatilia mtoza ushuru,...nilitoka naye mbali, akiwa anafuatiliwa na vijana wangu, na hadi alipofika hapo...’akatulia na ilionyesha alikuwa akificha baadhi ya maelezo.

‘Wakati nipo hapo nje, ndio akatokea huyo mtu, ambaye alifika bila usafiri wowote, alifika akitembea kwa kujiamini tu, akafika kwenye hilo geti na kugonga mlango, na mimi nikavutiwa naye, wka jinsi alivyokuwa amevaa, nikasogea, karibu, japokuwa hawakuniona, nikawa napiga mahesabu ya kuweza kuingia humo ndani....’akasema

‘Ukawa unapiga mahesabu ya kuingia humo ndani, ili ufanye nini, kwani ulishajua ni kitu gani kinaweza kutokea,?’ nikauliza

‘Sikuwa ninajua kuwa hayo yote yanaweza kutokea, ila mimi nilikuwa namfuatilia mtoza ushuru, kujua ni kitu gani kilichomleta kwa mdada, ....na sasa akaja huyu mtu asiyefahamika, nikahisi kuna kitu...’akasema

‘Sasa uliingiaje humo ndani...?’ nikauliza

‘Yule mlinzi alipofunguliwa mlango, yule jamaa akawa kasimama kwa muda kidogo, halafu aaingia kwa ndani,wakawa wanaongea kwa muda mfupi tu, ni kiasi cha kutoa maelekezo..mimi kwa haraka, nilisogea hadi pale mlangoni na kuwachungulia kwa nje...

‘Yule jamaa alipoingia, alisimama ndani, akiwa kanipa mgongo, na mlinzi akawa kasimama huku kaangalia jengo, mlengo wa nyumba yam dada, ilivyoonyesha huyo jamaa ni mtu muhimu sana kwa mlinzi, kwani mlinzi alionyesha kunyenyekea, kwa jinsi nilivyomuona, kwahiyo hata ile akili ya kuangalia huku mlangoni haikuwepo kwa muda huo...’akasema

‘Ok, kwahiyo huenda ni bosi wake, au aliwahi kuwa bosi wake...’nikasema

‘Yawezekana...’akasema

‘Wakati wanaongea, yule mlinzi kwa haraka akakimbilia kuelekea kwenye jengo, na mimi nikasukuma mlango taratibu, na kupata upenyo wa kupita...nilimuona huyo jamaa akiongea na simu, na  muda huo alikuwa akiangalia yule mlinzi anavyotembea kwa haraka kuelekea eneo la jengo, hapo hapo sikupoteza muda, nikapita pale mlango kwa haraka, nikawa naambaa ambaa upenuni mwa michongoma,..

‘Kama huyo jamaa angeligeuka nyuma, angelioniona, lakini nilicheza na bahati nasibu kuwa hatageuka kwa haraka, na kweli ikawa hivyo, nikatembea hadi kwenye maegesho ya magari nikajificha huko...na ndipo nikamuona yule mlinzi akifungua mlango wa gari la mdada...

*******

Mlinzi alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, na kusomewa mashitaka yake, na yeye akayakana yote kuwa yeye hajamuua mtoza ushuru, kwa hiyo ikapangwa siku ya kesi.

‘Sisi tumeshakamilisha ushahidi wetu, hatuna shaka..’alisema muendesha mahitaka alipoulizwa,  na alipoulizwa mshitakiwa kuwa ana wakili , yule mlinzi akasema

‘Ndiye ninaye wakili wangu, lakini nashangaa kwa jinsi wanavymzuia kuonana na mimi, ...’akasema na hakimu akasema huyo mshitakiwa ana haki ya kuonana na wakili wake, na muendesha hayo mashitaka akasema hilo linafanyika....

Kwahiyo tarahe ya kesi ikapangwa,...

******

Wakati hayo yanaendelea ndani ya familia ya baba mkwe, kulikuwa na kikao maalumu cha wanafamilia, kwenye kikao hicho alikuwepo shangazi, mchumba wangu, na ndugu wengine, na wakili wa baba mkwe na ndugu mmoja aliyetambulikana kama mtaalamu.

NB:Naona kama tunaingia kwenye hitimisho la kisa chetu, ...mahakamani, je haki itatendeka?


WAZO LA LEO: Mara nyingi madhalimu wanaogopa ukweli na haki, kwani katika ukweli na haki madhambi ya ufisadi hayana nafasi, na ndio maana mara nyingi madhalimu,hutumia nguvu nyingi, na uwongo na poropoganda potofu ndio sera zao. Lakini kwa vyovyote iwavyo, miali ya nuru ya ukweli na haki itapenya kwenye giza nene la dhuluma zao, na mwanga wa haki na ukweli utaleta matumaini kwa wanyonge. 
Ni mimi: emu-three

No comments :