Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, April 17, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-42Binti aliondoka kwa hasira, baada ya kuongea na baba yake kwenye simu, na kuniacha nikiwa nimeduwaa, hasa kutokana na kauli yake pale alipokuwa akiwasiliana na baba yake, kuna maneno yalinifanya nihisi kuwa kuna jambo limetokea huko kwa baba yake;
Wapi,....kwani wewe upo wapi,?’

‘Lakini ulisema umerudi nyumbani kijijini,....’

‘Oh, kwanini, kuna nini kimetokea?’

‘Baba ....una uhakika na hilo ...unasema kuwa wamekugeuka,...akina nani?’

‘Msaliti mkubwa wewe..utaona.....’

‘Msaliti mkubwa, wewe...’ hivi haya maneno yalikuwa yakielekezwa kwangu,au kuna mtu mwingine, na huenda alikuwa akielekeza hizo shutuma kwangu, kwa jambo gani nililolifanya hadi nipewe shutuma hizo, au ni kuhusu mdada labda...

‘Yawezekana ikawa ni kuhusu mdada, huenda, wamegundua kuna kitu kinaendelea kati yangu mimi na yeye, au mdada keshatuma hizo picha mbaya kwa huyo mzee, lakini mdada hawezi kufanya hivyo, sasa ni kwanini niitwe msaliti, labda sio mimi..’ nikawa najiulza maswali mengi,

‘Ngoja niingie huko huko ndani nikamsikilize mdada, ni lazima anafahamu ni kitu gani kinaendelea, ... nahisi kuna tatizo kubwa sana....’nikasema na kurudi kule kwenye hiyo ofisi ambapo nilimuacha mdada na wakili, na nilipoingia nilimkuta mdada akiongea na simu

‘Hali yake inaendelea vipi?’ akauliza mdada kwenye simu, na aliweka spika ya nje, kwahiyo unasikia huyo mtu wa pili anasema nini, nafikiri alifanya hivyo, ili wakili wake asikie ni kitu gani wanaongea na huyo mtu mwingine.

‘Hali yake hadi sasa haijajulikana, kwani aliingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, ni mshutuko, na inawezekana ikawa ni kiharusi...lakini yote tunasubiri taarifa ya dakitari..’sauti ikasema.

‘Kwahiyo pia inaweza ikawa ni mshituko tu, ...na kupoteza fahamu, sio lazima iwe ni kiharusi, namfahamu sana huyo mzee, ni mtu wa mazoezi, lakini, ooh, binti yake anafahamu?’ akauliza

‘Sizani kama anafahamu, maana nilivyosikia alikuwa chumba cha mkutano akiongea na mchumba wake..kwani hujaonana na huyo binti, kwani anakutafuta sana.’sauti ikasema,na mdada akamwangalia wakili, hakuniangalia mimi, ni kama vile hakujua nimeshaingia.

‘Alikuwa hapa, nimeshaonana naye, sina uhakika kama  ameshaondoka,..hebu subiri kidogo....’akasema alipogeuka na kuniona akaniuliza;

‘Huyo mwanamke wako yupo wapi?’ akaniuliza

‘Wa nini tena, ...mwenyewe ulikuwa unashinikiza aondoke, sasa tena unamuhitajia, wa nini?’ nikamuuliza nikionyesha kutokujali.

‘Baba yake kapatwa na mshituko, kadondoka na kupoteza fahamu, sasa hivi kakimbizwa hospitalini, ndio maana nataka kufahamu wapi lipo,...’akasema

‘Unasema, nani, mzee wake, haiwezekani, wapi hiyo imetokea?’ nikauliza nikionyesha mshituko na mshangao, na mdada akawa kashikilia ile simu, akaiweka hewani na kusema;

‘Nitaongea na wewe baadaye, fuatilia kwa makini, kwani nahisi kazi imekwisha....’akasema na kuiweka simu yake mezani, akaniangalia na kusema

‘Unauliza wapi imetokea, huyu mzee, alipatwa na mshituko huo akiwa humu humu kwenye hili jengo..kwenye ofisi nyingine...’akasema

‘Lakini nijuavyo mimi, huyu mzee kesharudi kijini...’nikasema

‘Ndio hivyo, jua hivyo hivyo,..anyway, ni muhimu kama binti yake hajafahamu ikatafutwa jinsi y kumfahamisha, maana huyo ni mzazi wake, na hatujui uhimili wake, japokuwa anaonekana mkorofi, je wakili unasemaje?’ akauliza

‘Kwani umemuacha wapi huyo binti?’ akauliza huyo wakili

‘Mimi ninachoshangaa ni kuwa, muda mchache tu, huyo binti alikuwa akiongea na baba yake, kwenye simu, na sikuweza kufahamu wameongea nini, ila kunaonyesha kuwa kuna tatizo, yeye alipomaliza kuongea na simu, akaondoka kwa haraka, hakutaka hata kuniambia lolote.....’nikasema

‘Nahisi alipomaliza kuongea naye, ndio akapata taarifa zilizomshitua, ...nahisi ndivyo ilivyotokea,...kakutana na mambo mengi kwa wakati mmoja, ya kifamilia, ya kikazi, na mambo yake binafsi, akashindwa kuhimili, ..’akasema mdada.

‘Hili sasa linaweza kuathiri mambo mengi, lakini kwa upande wetu, ni nafasi pia ya kujipanga vyema, na ni muhimu kujiandaa kwa lolote lile...’akasema wakili.

‘Mhh, kweli linaweza kuharibu mpango wote, hata hivyo, ni jambo gani lililompelekea huyo mzee kupatwa na mshituko, na muda huo alikuwa akiongea na nani, ni muhimu sana hilo tukalifahamu...’akasema mdada

‘Huyo mtu wako hajafahamu zaidi, inabidi umuulize, ili tujue ni nini cha kufanya, ....’akasema wakili

‘Mhh, kweli safari hii mzee kapatikana, na ujanja wake wote huo, kashindwa kupambana na kashikashi za mihamaniko ya dunia, nilishamuambia kuwa hayo anayoyafanya yatampeleka pabaya, lakini alijiona hawekaniki, sasa...sijui, lakini, jamani mwili wa binadamu sio mali kitu, kama namuona vile...’akasema mdada kwa sauti ya huruma

‘Kwani imekuwaje, na kapata taarifa gani mpaka apoteze fahamu?’ nikauliza nikiwa nahangaika kumpigia mchumba wangu lakini simu yake ilikuwa haipatikani.

‘Hayo na mengine tutayafahamu baadaye, huna haja ya kumpigia simu mtu, unataka kumpigia nani?’ akauliza mdada

‘Ni lazima nifahamu , huyo binti, atakuwa wapi, je keshapaa taarifa....’nikasema

‘Hilo kwa sasa lisubiri, sisi tuendelee na yetu, maana haya yetu hayasubiri mtu, kesi bado hajatenguliwa, yaliyopo ni maombi tu, kisheria, bado tuna kesi mahakamani, na mtu aliyekuwa akiibeba ndio huyo, taabani....’akasema wakili.

‘Ina maana huyo mzee, ndiye aliyekuwa akinisaidia, mbona mumesema ni nyie...?’ nikauliza

‘Hata kama ni yeye, lakini ni kutokana na juhudi zetu, na shinikizo zetu, bila sisi yeye asingelifanya lolote, kwanza alishakuona ni msaliti...’akasema mdada

‘Msaliti, msaliti wa nini?’ nikauliza nikikumbuka kauli ya mchumba wangu.

‘Kwani hilo ni siri, yule mzee, ana masikio,yanayosikia kila kitu kinachoendelea, hasa kwa watu wake muhimu, ana macho yanayoona mbali, kuliko unavyofikiria wewe..sioni ajabu kulifahamu hivyo, japokuwa yeye mwanzoni alilichukulia kuwa ni sehemu ya utendaji wangu, kwa kazi aliyonipa.....’akasema

‘Kazi gani aliyokupa..?’ nikamuuliza

‘Kukuchunguza wewe....hivi hilo nalo ni swali la kuniuliza,....wewe mwanaume, fahamu kuwa hadi kufikia hicho cheo, ni kutokana na mimi, taarifa zangu kwao, na kuonyesha kuwa wewe ni mtu unayeweza hiyo kazi,...labda wapo wengine, mimi sijui, lakini kwa pendekezo langu, mimi niliona kuwa unafaa.....kwa jinsi wanavyotaka wao....’akasema

‘Mimi sikuelewi mdada, kwani wewe ni nani kwao, unafanya kazi gani, ..?’ nikamuuliza

‘Hayo maswali haya maana kwa sasa...mimi ni katibu muhutasi wa kampuni ya bosi wako, inatosha wewe kufahamu hivyo, mengine ni uchakaramu wa mjini, ukiwa mjanja hulali njaa, huoni, nilivyokusaidia, ni ujanja wa mdomoni na akili ya kupangilia maneno, na mengine kidogo...’akasema akijiangalia mwilini

‘Jamani muda unakwenda, naona tufanya chochote,....kama vipi niachieni nifanay nionavyo ni vyema kwani kwasasa hata sijui kama mumejiandaa kwa lolote lile...’akasema wakili

‘Ni kweli, kwani akili yangu haipo sawa kwa sasa, ni muhimu nikafahamu kama huyo mzee anaumwa, ili na mimi nikamuone’nikasema

‘Hakuna aliyesema anaumwa,..na hilo tukio halitakiwi kufahamika, ujue hilo, ...usije ukakurupuka hapa na kukimbilia huko, sijui wapi, ukasema kauli kama hiyo....’akasema mdada

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Hayo ni maswala ya kiusalama zaidi, kwanza jiulize kwanini bado yupo hapa, na wewe unafahamu kuwa yupo huko kijijini, hata mtoto wake, mwenyewe hafahamu hilo,...huyo sio mwenzako...haya mambo yana utaratibu wake, usije ukaropoka ovyo...’akasema mdada.

‘Kwahiyo mnasemaje?’nikauliza

‘Kwanza hapa kunahitajika vielelezo , kwa mfano huyu mhasibu alifika hapo kwasaabbu gani,..na aliondoka muda gani, ...kitu ambacho ni muhimu sana, pia kuhusu huyu mtu mwingine, ni nani,..unajua hili limekuwa kitendawili kwa hawa wapelelezi.....’akasema

‘Lakini unahisi ndiye aliyemuua huyo jamaa?’ aakuliza mdada

‘Kwa asilimia kubwa inaoneka ndiye aliyefanya hivyo,...na akipatikana basi sisi hi kesi haipo tena...’akasema

‘Kitu kinachoulizwa na wengi, unajua dunia hii ni kijiji, watu wameshafahamu kuwa mhasibu amependekezwa kwenye hiyo nafsi, waandishi wanauliza ni kwanini, wakati yeye ni mshukiwa,... unaona hapo, ndio maana nahisi mzee, alipokabiliwa na haya maswali akaanza kuzongwa na shinikizo la damu,...’akasema mdada

‘Sizani kama ni kuhusu hoja hiyo, hata hivyo mzee, yeye hahusiki kwenye uteuzi huo, yeye alipendekeza tu, na kwa vile wanamuamini ndio maana wakalikubali pendekezo lake, mimi nahisi kuna jambo jingine limejificha hapo...lakini, hata hivyo huyu mzee, nahisi ana jambo, mimi simwamini sana, eti wakili, hivi huyu mzee unamuamini sana?’ akauliza mdada

‘Mimi namwamini sana, ni mtu aliyefanya kazi yake kwa uhodari, na haat ukiangalia sehemu alizokuwa akifanya kabla ya kustaafu, alikuwa mchapakazi,na ndio maana serikali inaendelea kumtumia kwenye shughuli mbali mbali, mimi sioni kama ana tatizo....’akasema wakili

‘Yah, ni iwe hivyo....lakini hisia zangu zinanituma vingine, sijui, ...wakati mwingine, nahisi ni kwa vile tumechefuana kuhusu binti yake, lakini wakati mwingine, nahisi kuna jambo limejificha,...na ni lazima nilifahamu....’akasema mdada

‘Ili iweje, mbona unaingilia kazi za watu,....?’ nikamuliza mdada

‘Kazi za watu.....nimeshakuambia sisi ni mission town, mambo kama hayo ndiyo yanatufanya tuishi hapa mjini, tuonekane watu....ni hatari lakini salama...’akasema mdada akiandika kitu kwenye kitabu chake cha kumbukumbu.

‘Sasa je vile vielelezo vinavyohitajika kwa mwanasheria mwendesha kwa ajili ya hii kesi vitapatikana...anavihitajia leo, ili ajirizishe, pili ni kuhusu tukio lenyewe, ni lazima tuliangalie kwa jicho jingine..’akasema wakili

‘Hivyo vitapatikana hakuna shida, mimi mtoto wa mjini, wewe nipe muda, hiyo ni kazi ndogo sana kwangu, ngoja niwasiliane na vijana wangu, nione wamefikia wapi...’akasema mdada

‘Lakini mimi naona hiyo ni kazi ya polisi, nakumbuka mlishaniambia hivyo...’nikasema

‘Kwa muda ule ndivyo ilitakiwa iwe hivyo, lakini kwa hali inavyokwenda ni muhimu na sisi tujiandae kwa lolote lile, kwani sasa imeshatangazwa hali ya hatari, kila mtu anajiangalia yeye mwenyewe kwanza, serikali imeshaamuka, ....’akasema mdada

‘Kwani kuna nini kinachoendelea, unafahamu hadi sasa sijui haya yote ni kwa ajili gani, hebu nipeni ufununu?’ nikauliza na mdada akamwangalia wakili, na wakili akasema;

‘Sikiliza ndugu, hicho cheo ulichopewa, sio bure, kuna watu wana masilahi nacho,na ndicho kimeleta kizaa zaa, na mambo mengi yameshaanza kuwekwa hadharani, kwa hivi sasa uwe makini kwa hilo, pili, ni vyema tukajipanga kisheria, hatujui ni kitu gani kinaendelea mpaka sasa...’akasema mwanasheria

‘Sawa mimi sina shida, maana kwangu mimi ni sawa tu kiwepo au kisiwepo , mimi tayari nina kazi yangu, sikufikiria kama nitapewa wadhifa kama huo,na sehemu nyeti kama hiyo..’nikasema

‘Ni lazima ukipate, ni muhimu sana...’akasema mdada

‘Kwa hali ilivyo naona ni hatari, naweza kuambiwa yote yaliyotokea ilikuwa kwa ajili ya mimi kuipata hiyo kazi, ...sipendi hali kama hiyo, ni bora nifanye kazi yangu ya kawaida tu, kuliko kufanya kazi ya kuniweka roho juu...’nikasema na mdada akaniangalia kwa muda halafu akasema

‘Wewe ni mwanaume, unatakiwa uwe ngangari, usiogope, wakati mwingine, inabidi ufanye kazi za hatari, ili kuweza kufika mahali fulani, usiogope, kuna watu wengi wapo nyuma yako, cha msingi ni kutusikiliza..’akasema mdada na kumwangalia wakili

‘Sasa unaweza kuandika chochote, ili nipate muda wa kufuatilia hivyo vielelezo?’ akamuuliza wakili

‘Kama mnataka iwe hivyo, niachieni nifanye kazi yangu, ..siunajua mambo yenyewe yalivyo, natakiwa nikae ni wale watu, niwaweke sawa, baadaye, haat nikiomba kuoanana na mwendesha amshitaki, inakuwa haina ugumu tena.....’akasema wakili

‘Huyo mwendesha mashitaka, kama unataka mimi naweza kuonana naye, ila uwe nyuma yangu, ..nafahamu jinsi gani ya kumpata...’akasema mdada na mimi nikamwangalia kwa mashaka, kwa jinsi anavyojiamini

‘Unaweza kufanya hivyo?’ nikauliza na mdada akaniangalia huku akionyesha uso wa kutabasamu akasema

‘Katika dunia hii ukijiamini, hakuna kisichowezekana,mimi naweza kuonana na yoyote yule, na nikaongea naye shida zangu, na mara nyini nafanikiwa,...hilo sina shaka nalo, cha muhimu ni kuwa na uhakika na hicho ninachotaka kuongea na huyo mtu....ukweli, uwazi, na kujiamini, vinanisaidia sana...’akasema mdada na mara simu yake ikalia, akaiangalia na kuipokea

‘Niambie...’akasema na kuanza kusikiliza kwa muda, bila kusema neno, baadaye akasema

‘Kazi nzuri, kwahiyo, keshatoka na anaendelea vizuri, ila hatakiwi kuonana na watu,je ni nani aliongea naye kwa mara ya mwisho?’ akauliza

‘Mpelelezi, yupi huyo?’ akauliza

NB: Haya yalitokea na yanaendelea kutokea katika jamii zetu, tuone ni nini kitafuata baada ya hapo, je mhasibu ataipata hiyo kazi, ni kwanini mzee akashikwa na mshituko, na huyo mzee ni nani...


WAZO LA LEO:Dhuluma inaposhika hatamu, haki inapotea, watendaji wanakuwa wagumu kutimiza wajibu wao, ukiangalia kwa makini sababu kubwa ni hali ngumu. Wenye nacho wanakuwa hawatosheki, wanataka zaidi na zaidi,na kujiwekea namna ya kupata zaidi na zaidi na ili wapate inabidi kuchukua hata kile kidogo cha wasio nacho, haki inakwenda kwa wasiostahiki...Haki ikipotea, amani haitakuwepo, hata kama tutajidanganya kwa nguvu za dola.
Ni mimi: emu-three

No comments :