Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, April 14, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-40



‘Sio hongera ya kesi, bali ni hongera ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’

‘Bosi kazi gani umenipandisha cheo, .....?’ nikauliza nikiwa na hamasa ya kujua,

‘Nimekupigia simu kukupa ushauri tu, sio kwamba sikupendezewa na taarifa hiyo, nimefurahi sana, maana hayo ni maendeleo,...’akasema

‘Bosi mbona mimi sijaelewa, sijui lolote....’nikasema

‘Basi kumbe nimekuwa mmbea,...huenda sikutakiwa nikuambie mapema, ila ninachotaka kukuambia ni maswala ya kukushauri tu...’akasema

‘Bosi ina maana kazi hiyo sio hapo kwako?’ nikauliza

‘Hayo tuyaache, ninachotaka kukuambia ni kuwa, uwe makini kwani dunia sasa imebadilika, usione mtu anakujali, ukaona huyo ni mtu mwema sana kwako,...inawezekana ikawa hivyo, lakini ni mmoja kwa mia...’akasema

‘Wapo wanadamu watakuchekea, ukaona ni wema sana kwako, lakini moyoni kwake ana inda,...’akasema

‘Bosi ...’nikataka kumkatiza

‘Nisikize, wewe tumekaa pamoja, nakufahamu sana,..nimekuona kama mdogo wangu, kwahiyo inabidi nikushauri huko unapokwenda,...ni kwema, kuna masilahi mazuri, lakini ....’akatulia

‘Bosi kwani ninakwenda wapi...?’ nikamuuliza

‘Watakuambia wenyewe,....nahisi sikutakiwa nikuambie,..muda utafika utaambiwa....’akasema.

‘Hapana bosi, nimuhimu niambiwe, kwanini ..’nikaanza kulalamika, na mara nikasikia mlio wa simu kukatika...

‘Sio hongera ya kesi, bali ni hongera ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’

******

‘Sio hongera ya kesi, bali ni hongera ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’

Haya maneno ya bosi wangu yaliendelea kujirudia kichwani kwangu, yalikuwa maneno yenya ujumbe fulani, na niliona ajabu simu yake kukatika ghfal, na hata nilipojaribu kumpigia tena ikawa haipatikani, na mdada akaniangalia na kusema;

‘Mambo ya digitali hayo, nimeshakuambia hutakiwi kuongea na mtu yoyote wa nje kwa hivi sasa, nahisi hao ni watu wa usalama wanafanya vitu vyao, kwani wenyewe wameshafika....’akasema mdada akiangalia saa yake.

‘Ili iweje,hawajui kuwa huyo ninayeongea naye ni bosi wangu,....’nikasema

‘Kwao wao hawawezi kuwa na uhakika wa kila mtu, hawawezi kubahatisha, na ni nani atamfahamu huyo bosi kuwa hana lolote dhidi ya hao watu, ni maswala ya kiusalama, wao wanafahamu zaidi, ...’akasema

‘Lakini hata hivyo, mimi naingiwa na wasiwasi, bosi anasema nimepata kazi mpya ni kazi gani hiyo ambayo hata mimi siifahamu?’ nikauliza na kabla hajatamka kitu mlango ukagongwa na mdada akasema

‘Subiri, nahisi ndio hao wameshafika, natumai wao wenyewe watakupa jibu la swali lako, kazi nyingine hazitangazwi ovyo...’akasema na kuelekea mlangoni, akawa anaongea na mtu aliyekuwa nje, yeye akiwa kasimama mlangoni, baadaye akaniambia;

‘Unahitajika kwenye chumba cha mkutano, ....’akasema na kwa muda huo nilikuwa nimeshavaa nguo rasmi, ambazo aliniletea mdada, nikasimama  bila kuleta ubishi nikafanya kama alivyoniagiza mdada nikaelekea huko kwenye chumba walichokiita ni cha mkutano.

Nilipofika mlangoni mdada, akanishika begani, akaniangalia kwa jicho ambalo nilihisi kama vile anaona keshanipata, na kwahiyo mipango yake imakamilika, lakini sikumuelewa, lile jicho lina ujumbe fulani, ...akageuka kuangalia pembeni akasema

‘Kila-laheri...’akaondoka kwa mwendo wa kasi kama anawahi jambo, hakugeuka nyuma na mimi nikafungua ule mlango na kuingia ndani...

‘Ilikuwa ni ofisi iliyokamilika, na inaonyesha inatumika, maana humo ndani kulikuwa na kila kitu cha kiofisi, na humo nilimkuta mtu mmoja akiwa anapanga vitu mezani, na aliponiona akaacha na kunisogelea akanyosha mkono kunisalimia;

‘Karibu muheshimiwa...’akaniambia na kunifanya nishituke, toka lini mimi nikawa muheshimiwa, name nikanyosha mkono tukasalimiana, halafu nikasogea hadi kwenye kiti alichonielekeza, akasema;

‘Wakuu wameshafika, wanakuja muda wowote , cha muhimu wanachotaka kufanya ni taratibu za kupata mfanyakazi mpya kutokana na nafasi iliyoachwa wazi na marehemu...’akasema

‘Marehemu! Marehemu yupi huyo?’ nikauliza nikishituka maana kupewa kazi ya marehemu inashitua kidogo, sikuwa nimehisi lolote kwa wakati huo

‘Huyu aliyefariki hivi karibuni humkumbuki wa kitengo cha ushuru...’akasema

‘Oh, sikujua hilo, lakini mimi badi nipo kwenye kesi, na kesi yenyewe wananishuku kuwa mimi huenda nahusika...sasa iweje tena niwe katika watahiniwa wa hiyo nafasi,...isije ikawa ni mtego...., hata hivyo, mimi nimesomea mambo ya uhasibu....’nikasema

‘Kazi ni hizo hizo bwana, ni bahati imekuangukia, usije ukaijutia,..cha muhimu ni sifa wanazozitaka wao, ...swala la kesi hilo wanalifahamu sana, na kama ungekuwa katika kashifa yoyote wasingelikuchukua, watakuwa wamegundua kuwa huhusiki, na nahisi katika kuchunguza kwao, kuhusu hiyo kesi, ndio wakagundua kuwa wewe unastahili, vinginevyo watakuambia wao wenyewe,....’akasema na kunikabidhi makabrasha

‘Soma hayo maelezo yatakusaidia kwenye usaili wao,...mimi sina zaidi nimemaliza kazi yangu, kama kuna kitu unahitajia kwa sasa, au swali loloye niulize,..’akasema na mimi sikujua nimuulize nini, nikabakia kimiya na yeye akasema;

‘Mimi nakutakia kila la heri...’akasema na kuendelea kupanga panga vitu mezani, halafu akaondoka, na haikupita hata dakika moja mlango ukafunguliwa, wakaingia watu wawili waliokuwa wamevalia suti za bei mbaya, waliangalia huku na kule, kama kuhakikisha kuwa mambo yapo sawa, na mmojawapo akasema;

‘Oh, umeshafika mhasibu..’ilikuwa sauti nzito, na mimi kwa muda huo nilikuwa nimesimama nikijua ndio waheshimiwa wenyewe, na mmojawapo akanisogelea akiwa na chombo fulani, akanipitishia halafu akasema;

‘Ok, upo salama,..naomba hiyo simu yako...’akasema na akaichukua ile simu yangu akaikagua, na baadaye akamwambia mwenzake;

‘Ni ile ile, haina kitu...’akasema na mwenzake, akaipokea na kikagua, halafu akasema

‘Ok, labda ni maingiliano,..tutaona huko mbele, lakini hakuna lolote baya, waache waingie tu...’akasema na haikuchukua muda wakatoka, na mara wakaingia jamaa wengine wawili, hawa walikuja na makabrasha yao mikononi, wakaniangalia na kusema;

‘Oh, umeshafika mkuu,.....?’ akauliza mmojawapo na mimi nikasema

‘Nimeshafika mkuu.....’nikasema na wote wawili wakanisogelea na tukasalimiana na wao wakajitambusliha kuwa ni maofisa uajiri, na kazi yao kubwa ni kunifanyia usaili, ili kukamlisha taratibu za kumpata mfanyakazi wa nafasi iliyobakia wazi,

‘Kama unavyojua kuna nafasi iliyoachwa wazi kwenye idara zetu za ushuru, na kwa utaratibu nafsi hii inatakiwa itangazwe, na hilo limeshafanyika, na wengi wameomba nafasi hiyo ukiwemo wewe mwenyewe...’akasema na mimi nilitaka kusema sijawahi kuomba hiyo nafsi lakini nikabakia kimiya

‘Sisi kama wataalamu wa kumpata huyo mtu tumeshafanya uchunguzi wetu unaostahiki, na tumerizishwa na wewe kuwa unafaa kuziba hilo pengo, na kilichotuleta hapa ni kukamlisha taratibu zetu tu..baadaye huenda ukaonana na wakuu kwa utambulisho zaidi...’wakasema

‘Nashukuru....’nikasema nikijiuliza hao wakuu ni akina nani, na haya mambo mambo yanakwenda hata mimi mwenyewe kufahamu, lakini niliona nivute subira tu.

‘Wakati uchunguzi wa kesi ya hayo mauaji, ndipo tulipogundua kuwa wewe  unafaa sana kuziba pengo la marehemu,...na kiukweli, kesi yako inahakikiwa, umeshikiliwa kwasababu ya kukutwa kwenye tukio, ...hilo linafanyiwa kazi na wahusika..usiwe na shaka nalo...’akasema

‘Cha muhimu ni kuwasikiliza watu wako, kwani kufanikiwa kwako kumetokana na juhudi za hao watu wanaokudhamini,...na zaidi ni kutoka kwako, kwani utakuwa na miezi mitatu ya majaribio,....ni matarajio yetu kuwa wewe utafanya kazi kama alivyofanya marehemu, ujue kuwa nafasi hiyo nyeti sana, sio rahisi kupatikana na sio rahisi kupewa watu ovyo ovyo....’akasema

‘Nitajitahidi kutimiza wajibu wangu kama inavyostahili....’nikasema huku moyoni nikijipa moyo,japokuwa sikuwa na uhakika, ni kazi gani hasa nastahiki kuifanya.

‘Sasa unatakiwa kujaza hizi fomu hapa, ukimaliza, tutakuwa tumekamilisha kazi yetu....’wakasema na mimi nikakabidhiwa hizo fomu, nikazisoma kwa makini, ni mkataba wa ajira, una maelezo mengi sana,...niliyapitia kwa haraka, na kule kwenye nafasi za maelezo binafsi,....nikajaza kila kitu baadaye nikawakabidhi , wakaniuliza maswali mbalimbali, ya kiutendaji, nami nikawajibu kadri niwezavyo, na mwisho akaniambia

‘Haya ndugu kazi yetu tumemaliza, ....nimeambiwa kuwa kuna mtu anakuja muonane naye mara moja, muongee naye kwa haraka kidogo, kutokana na muda, kwani baada ya hapo unatakiwa kuonana na wakili wako,  kwahiyo usubiri hapa....’akasema na wakaondoka, 

Nilibakia peke yangu kwa muda, baadaye mlango ukafunguliwa, na aliyeingia alikuwa ni mchumba wangu

‘Hivi Wewe unanifanya nini...’akaanza kulalamika

‘Kwanini unasema hivyo,?’ nikamuuliza na aliponiona nilivyovalia na chumba chenyewe akaduwaa, na kusema

‘Oh, kumbe ni kweli...’akasema

‘Ni kweli kuhusu nini?’ nikauliza

‘Baba kaniambia kuwa umepata kazi mpya na sasa hutakuwa na kisingizio tena kuwa huwezi kunioa mpaka ujenge, ufanye nini, ...kwani wamesema utapewa nyumba , gari,....oho, tumshukuru mungu...’akasema akionyesha furaha ya hali ya juu, na moyoni nikawa namuona mdada kasimama nyuma yake, akionyesha huzuni

‘Usianze kufurahi , wakati hata sijajua kuwa hiyo kazi ipoje, je nikikataa, maana siwezi kupewa kazi yenye mitego na masharti, hawa watu siwaelewi..’nikasema

‘Utakuwa mtu wa ajabu sana, wenzako nafasi kama hizo wanazitafuta, wewe unasema utaikataa, sikuelewi....’akasema

‘Kwanza nikuulize baba yako mumeongea naye saa ngapi, kakupigia simu?’ nikamuuliza

‘Ndio kanipigia simu....’akasema akianiangalia kwa makini

‘Kwanini unaniuliza hivyo?’ akauliza

‘Naona kila kitu anakifahamu yeye mapema tu,hata sijui anahusika vipi na haya yote.....’nikasema

‘Baba huwa anafahamu mambo mengi ya nchi hii, anakwenda na wakati, ni mtu wa serikali, ana majukumu yake hata mimi siyajui...’akasema

‘Mhh, haya ...niambie ulisema unataka kuongea na mimi, naomba mambo mengine tuyaongee tukiwa huko nje, hapa sio mahali pazuri pa kuongea chochote, na nimepewa muda mchache wa kuongea na wewe....’nikasema

‘Ni kuhusu huyo mdada, ...ni muhimu sana umuelewe mapema, haaminiki huyo mwanamke,kama usipokuwa makini utajiingiza kwenye matatizo....’akasema

‘Usijali, huyo ni mfanyakazi mwenzamgu, hana matatizo kabisa....hilo lisikuumize kichwa...’nikasema kwa kujiamini

‘Na huko unapokwenda kufanya kazi mtakuwa naye?’ akaniuliza

‘Wapi, ...sijajua wapi,...lakini sijui, ,...yeye ana kazi yake, .....’nikasema huku na mimi nikiwaza kuwa ina maana kweli nitakuwa mbali na mdada, nitakosa uchakaramu wake, nikamwangalia mchumba wangu ambaye kwa muda huo naye alikuwa akiniangalia kwa makini

‘Umebadilika kweli siku hizi...’akasema

‘Nimekuwaje?’ nikamuuliza huku nikiangalia saa yangu, nikijua sina muda wa kuongea naye, na nilikuwa na mambo mengi ya kuongea na huyu mtu, ili asije akaharibu.

‘Umekuwa mweupe, unazidi kupendeza, ..halafu, hueleweki,.....’akasema

‘Naona huna la muhimu kwa sasa, nimeambiwa kuna watu wanakuja kuonana na mimi, ni vyema ukaondoka, ...’nikasema

‘Unanifukuza..’akasema akiniangalia kwa mshangao

‘Huoni nipo kwenye ofisi za watu, na kuna wakubwa wanakuja kuongea na mimi, nisingelipenda wakaja kukuta humu.....’nikasema

‘Ndio vizuri wajue kuwa mimi ndiye mchumba wako wa halali, sio huyo mwanamke wako, anayekuzuzua...hivi kwanini mwanamke kama huyo anakusumbua kichwa chako....’akasema na mara mlango ukagongwa

Nikageuka kuangalia mlangoni, na mchumba wangu akanisogelea kusimama karibu yangu, akasema

‘Nataka wakija unitambulishe kuwa mimi ni mchumba wako....’akasema
Na mara mlango ukafunguliwa, akaingia wakili akiwa pamoja na mdada,....


Ni mimi: emu-three

No comments :