Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, April 11, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-39


'Mbona unaniangalia kama umeona shetani....’ilikuwa sauti ya mdada akiwa kasimama mlangoni akiwa amevalia sweta zito, kuonyesha kuwa alitokea kulala, na hakutaka ubaridi umuingie, alionekana sio mtu wa kutoka, na mkononi alikuwa na mkoba wake mkononi.

‘Mbona umewahi hivi, mimi sijajiandaa....’nikasema nikijikagua

‘Nimekuja tuongee kidogo kabla hujakutana na hao watu.....’akasema

‘Watu gani?’ nikauliza nikitoa macho ya mshangao, maana sikumbuki kuambiwa kuwa leo nitakutana na watu

‘Leo utakutana na watu muhimu sana,ambao pamoja na mengine, ni kukuweka sawa, na huenda wakaja na taarifa nzuri kwako...’akasema

‘Taarifa gani, kuwa kesi imefutwa au?’nikauliza nikiwa na hamasa

‘Watakuambia wenyewe, cha muhimu ni kujiweka sawa kwa wageni wa heshima, sio wageni wa ovyo, hao ndio wanaojua hali halisi yah ii nchi, wanaweza kukugeuza leo ukawa mtu mwingine kabisa, au kukupoteza, usionekane tena hapa duniani..’akasema

‘Mhh, sielewi...ina maana wao wanauwezo wa mungu? ’nikauliza kwa mshangao.

‘Usiulize maswali kama sio msomi, swali gani hilo, nilichoongea hakimgusi mungu, mwenyezimungu ana uwezo wake, mimi nazungumzia mamlaka ya hapa duniani, ya hapa kwetu....’akasema na kuniangalia, mimi nilikuwa nina wasiwasi kuwa sasa hivi kuna mtu atagonga mlango.

‘Kuna mtu unatarajia kuonana naye mbona hutulii...nimekuambia nataka kuongea na wewe...’akasema

‘Mhh, hapana,sio kitu ...ila mimi nataka kwenda nyumbani kwangu kuna mtu alinipigia simu kuwa,kuna watu walifika kwangu, wanatoka kijijini wanataka kuonana na mimi...’nikasema

‘Walikuja nyumbani kwako,...lakini siwanafahamu kuwa bado umeshikiliwa na polisi au?’akauliza kwa mshangao

‘Ndio walikuja nyumbani kwangu haponilipopanga..sina uhahika kama wanafahamu lolote, lakini..’nikasema nikikwepa kuangalia naye nay eye akanikatisha kwa kusema;

‘Nakuomba uachane na hao watu, na huko kwako upasahau kwa sasa, ulishaambiwa kuna watu wanakuwinda, na nyumbani kwako ni lazima kutakuwa na watu wanakusubiria, upo kwenye hatarani inabidi kuwa na tahadhari, kwa hivi sasa huwezi kujua ni nani yupo nyuma yako..unalifahamu hilo,....’akasema

‘Hata hivyo ni lazima niende huko mara moja, kwani hao wageni inaonekana kuwa wanafahamu kuwa nimeshapata dhamana, ndio maana wakafika kuniona,nitachukua tahadhari uasijali kwa hilo...’nikasema

‘Unataka kuonana nao sasa hivi?’ akaniuliza akionyesha kukerwa na maelezo yangu hayo

‘Ndio...ni muhimu sana’nikasema

‘Hapana, huwezi kuondoka kwa hivi sasa, hata baadaye..., kwa leo haitawezekana, ....’akasema

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Nimeshakuambia kuwa leo ni siku muhimu sana kwako,unahitajika kukutana na hao watu, ukimalizana nao, ukakubaliana nao, basi ukitoka hapo utakuwa huru kwenda unapotoka, tutaangalia na muda...hata hivyo baada ya hapo utahitajika pia kwenda kuonana na wakili , ukumbuke kuwa kesi bado haijafutwa, japokuwa jalada lako la kesi lipo kwa waheshimiwa...’akasema

‘Lakini nina mambo yangu binafsi...na ni muhimu kwangu mimi, sijafungwa, nipo huru au? ’nikasema

‘Ndio upo huru, lakini uhuru wako kwa sasa una masharti, kwanza hebu niambie una mambo gani muhimu kama ulivyosema binafsi unayoyahitajia...au ndio hao wageni unaosema wamefika kutoka huko kijijini, ...au una jingine,?’ akaniuliza

‘Pamoja na hayo...’nikasema nikionyesha kutokuwa na furaha

‘Sikiliza kuanzia sasa, hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa, unatakiwa uniweke wazi kwa kila jambo unalotaka kulifanya, kumbuka kuwa mimi ndiye mdhamini wako, ...’akasema

‘Nafahamu hilo, na sina nia mbaya,nitajitahidi kuchukua tahadhari, ni lazima nitoke humu ndani haraka,...’nikasema nikijiandaa kuondoka huku nikiangalia mlangoni

‘Utoke humu ndani haraka!? Wewe mtu vipi, kwanza unaonekana kuna mashaka-mashaka, unaogopa nini, kuna hatari yoyote umeihisi au kuna jingine,hebu niambie ukweli?’ akaniuliza akiniangalia kwa makini

‘Sio jambo la hatari, ni huo ugeni tu, ni muhimu kwangu....’nikasema

‘Huo ugeni ni kuhusu huyo mchumba wako, au sio?’ akaniuliza na kunifanya nishituke, nikamuuliza

‘Nani kakuambia ni kuhusu mchumba wangu?’ nikamuuliza kwa mshangao na yeye akacheka kwa dharau, na kusema;

‘Nakuomba uwe muwazi kwangu, yaani muda wote unahangaika kumbe ni kuhusu huyo mtu,...nikuambie ukweli, hakuna mtu anayeruhusiwa kuonana na wewe hadi hapo,hao waheshimiwa watakapoondooka,...ni maswala ya usalama, hao watu ni watu muhimu, ...siwezi kukueleza kila kitu lakini huyo mtu wako hawezi kuonana na wewe.......kwa sasa’akasema

‘Mhh, mbona mnanikwaza...’nikasema

‘Ukumbuke kuwa sasa hivi, kila unalolifanya linachunguzwa, ...wao wana utaalamu wao, hawawezi kuja kuonana na wewe bila kujua usalama wao, ndio maana ukawekwa hapa,...hata hivyo hata mimi ninayekudhamini, natakiwa nikuchunge kama ninavyochunga mboni yangu ya jicho...’akasema na mimi nikamwangalia kwa macho ya mshangao

‘Kwahiyo, kama ni kuhusu yeye, huyo binti gani sijui, hawezi kuja kukuona kwa hivi sasa, kama anavyotaka yeye...hataambiwa hivyo moja kwa moja...’akasema

‘Kwa vipi, na na.....’nikaanza kuhisi wasiwasi

‘Tulizana, usitake kuharibu mambo, tuna nusu saa ya kujiandaa, kabla waheshimiwa hawajafika, ninachotaka kukuambia ni kuwa hao watu sio watu wa mchezo, wakija unachotakiwa ni kukubaliana nao kila kitu, after all, ni kwa faida yako, sioni kwanini ukatae...’akasema

‘Mimi sielewi, kwanini yote hayo siambiwi, sifahamu , kila jambo naperekeshwa tu, kwani kuna nini mnanitafuta mimi, hebu niambie ukweli mdada, yote haya ni ya nini, na kwanini mimi?’ nikauliza

‘Ipo siku utakuja kufahamu, na nahisi muda unakaribia,..usijali..subira huvuta heri, na baada ya yote hayo, huenda ukafurahi, cha muhimu usiniangushe,...’akasema na kuangalia saa yake, halafu akageuka kunitizama, akiwa na uso usio na tabasamu, alionekana yupo kikazi zaidi, akaangalia kitandani na kuona vile vifaa, akasema;

‘Hivyo vifaa ni muhimu sana kwako kwa hivi sasa, vina maana yake....usiviweke ovyo, na ukijiandaa tunatakiwa tutoke hapa, kuna ofisi ipo chumba cha pili yake...’akasema na mimi nikageuka kuangalia yale mawani, simu na saa, nilikuwa nimeviweka kitandani

‘Unasema hivyo vifaa ni muhimu sana, wa nini kwangu mimi, kama ni mtego,mimi...sivihitaji....’nikasema kwa sauti ya kukata tamaa

‘Utavihitaji tu,....usiwe na wasiwasi mwanaume wewe, mimi nakuhakikishia utavipenda,na hakikisha unakuwa mchangamfu ukija kukutana na hao wageni,...wakifika utakaa ongee nao, mimi sitakuwepo wakati mnaongea, kwahiyo unatakiwa kujiamini,...unasikia wewe mwanaume?’ akasema

‘Sijui...’nikasema na yeye akaniangalia kwa uso wa kushangaa, akanisogelea na kunishika kidevuni

‘Wewe mwanaume vipi wewe, hebu amuka,usiniangushe bhana,...’akasema na huku akichezea kidevu changu kwa vidole.

‘Unajua mdada, sikuelewi...’nikasema

‘Mhasibu,tupo kazini hapa, usitake nibadilike...haya yote yanafanyika kwa ajili yako, ujue kesi yako haijafutwa, na hao watu ndio wanaoweza kuifuta hiyo kesi, kama hutaonyesha ushirikiano nao, ujue,...utasahaulika...nakuonya kwa mara ya mwisho...’akasema na alipotaja kuhusu kesi nikashituka, nikasema;

‘Baba mkwe wangu anasema anashughulikia hii kesi, sielewi kwa vipi?’ nikauliza

‘Mimi sijui,..na hata hivyo mimi sitaki kuongea maswala ya baba mkwe wako hapa, huyo mtu kanipigia simu leo asubuhi, akaanza kunishutumu, eti naingilia ndoa ya binti yake,...simuelewi huyo mzee, kwanza kanipa kazi nimfanyie, hajui naifanya vipi, anakimbilia kusema nimeitumia nafasi hiyo kukurubuni, hivi kweli mzee huyo ana akili, hanielewi kabisa...’akasema

‘Lakini mengine naona kama yana ukweli,au sio..’nikasema

‘Hahaha...na wewe upo upande wake,..sikiliza si baba mkwe wako au nani, wewe na mimi ni kitu kimoja, huyo kwasasa achana naye, hana maisha ya maendeleo na wewe, mimi natakiwa kukujenga ili ufanane na wanavyotaka hao watu, ..hata hivyo,...nilishakuambia wewe ni wangu,hunielewi..’akasema

‘Huwezi kulazimisha penzi,...’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya kuelegeza, halafu akatabasamu, na kusema;

‘Una uhakika na hilo, tukifungua moyo wako hapo, hakuna kingine zaidi yangu, tusitake kupoteza muda na mambo hayo kwasasa, ila baba mkwe wako kanichafua, na hawezi kunitishia mimi,...’akasema

‘Kakutishia kasema nini...?’ nikauliza

‘Eti nikiendelea kufanya hivyo,atahakikisha ananiharibia maisha yangu, kwani anafahamu siri zangu zote,...yaani mzee huyu keshasahau fadhila zangu, hajui bila mimi asingelijua mambo mengi, ...anapenda kunitumia tu akiwa na shida zake, zikiisha keshanisahau...’akasema

‘Unakutumia eeh, ndio maana akakutumia kunichunguza mimi ?’ nikamuuliza

‘Nilifanya hivyo kwa vile nilihitajika pia kuendelea na mipango yangu mingine, inayokuhusu wewe, la sivyo, nisingelifanya anavyotaka yeye...’akasema

‘Mipango gani?’ nikauliza

‘Ndio hiyo inafikia hatima yake leo..ukikutana na hao watu, utafahamu...utakuja kunishukuru,...’akasema

‘Nikushukuru kwa kuniharibia amani ya maisha yangu, wewe unafikiri nitaongea vipi na baba mkwe, kama umemzuia binti yake asionane na mimi, na sijui umemfanya nini...’nikasema

‘Hajafanywa kitu...yupo chumba fulani anakusubiri, lakini atakusubiri mpaka atachoka,na mwisho wake ataondoka....’akasema

Mara simu yangu ikalia, nilipoangalia nikaona ni namba ya bosi wangu, nikamwangalia mdada, na mdada akaniangalia na kuuliza

‘Ni nani huyo?’ akaniuliza

‘Ni bosi....’nikasema

‘Oh, bosi, bosi wako wa kampuni, aah, achana naye, nikuambie ukweli, kuanzia sasa, huyo utamsahau....’akasema.

‘Kwanini unasema hivyo?’ nikauliza huku simu ikiendelea kuita, na yeye akaniashiria kwa mkono kuwa niipokee hiyo simu. Nikasema

‘Samhani, ngoja niongee naye....’nikasema

‘Ongea naye...lakini hukutakiwa kuongea na yoyote kwa hivi sasa, ....ok, ongea naye....’akasema akiangalia saa yake, na mimi nikaiweka hewani simu ya bosi, na bosi alianza kwa kusema;

‘Hongera sana..’akasema nikajua kuwa huenda ananipa hongera ya kupata dhamana, nikasema;

‘Lakini kesi bado haijaisha....’nikasema

‘Sio hongera ya kesi yako, kesi yako nasikia haina nguvu sana, mimi nakupa hongera ya kupata kazi mpya, ...’akasema

‘Kazi mpya kazi gani hiyo...?’ nikauliza na kumwangalia mdada, na mdada akawa anatabasamu tu, inaonekana alikuwa anafahamu ni kitu gani kinachoendelea , bosi akasema;

‘Lakini uwe na tahadhari, sio kila king’aacho ni dhahabu, na sio kila anayekuchekea ana nia njema na wewe....

NB: Hongera mpendwa kwa kuwa nami, naishia hapa kwa leo je wewe unasemaje? Tumalize kisa, umechoka,?


WAZO LA LEO: Ni kweli kila mmoja anatafuta, ili kupata riziki na maisha bora,lakini zipo njia ambazo sio sahihi, na zipo kazi ambazo sio halali,na hizo wakati mwingine zina mvuto wa masilahi mazuri,kwani kazi haramu haziishi hamu. Tahadhari tu, tusivutwe na tamaa za kupata na kuchuma kwa haraka kwani mwisho wake ni mbaya. 
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

ilipofikia naona siielewi hata nimeshasahau kule maisha ya bosi imekuwa na mzunguko sana

Yasinta Ngonyani said...

Yaani ni kama vile nilikuwa nasoma kitabu na mara nikashtuka eti mwisho ..aahhh emu-thre..Mimi sijachoka kabisa. Je unaposema "tumalize kisa" unamaanisha kivipi?