Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, April 10, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-38


Ni kipindi nimesharudi hotelini kwangu, na kuanza kushangaa simu niliyopewa, mawani nilishaiweka pembeni, hamu yangu kubwa ilikuwa hiyo simu, ambayo ilikuwa na kila kitu kilichopo kwenye laptop.

‘Hii ni zawadi yako kijana, kwa kuja kujiunga nasi, na humo tutaweza kuwasiliana nawe...’niliambiwa na jamaa mmoja aliyeniletea hiyo simu, na mdada akanionyeshea ishara kuwa nipokee.

‘Pamoja nayo, tunakukabidhii hii saa, uhakikishe unavaa wakati wote, kwani muda ni muhimu sana, bila kujua muda, huwezi kufanikiwa mambo yako...’akaniambia huyo jamaa na kunivalisha hiyo saa mkononi.

Vitu vyote hivi niliviona vya thamani sana, na niliogopa nisije kupewa gharama ambayo sitaweza kuilipa, nikamwangalia mdada, na mdada akatabsamu na kusema;

‘Sasa umekamilika,....kilichobakia ni wewe kutoa tamko...’akasema

‘Tamko la kukubali kuwa upo tayari kujiunga na kundi, na hilo sio lazima utamke, ila matendo yako, kazi zako, na majukumu utakayopea ndio yatawahakikishia wahusika kuwa upo kwenye kundi...uwajibikaji, ni muhimu sana...unatakiwa kila mwezi uonyeshe juhudi zako kwa kutoa kiasi fulani kwenye kundi....’akasema

‘Kiasi fulani?’ nikauliza

‘Kundi litaendelea vipi bila kuwa na mfuko,....hayo utayafahamu hatua kwa hatua...’akasema

‘Lakini....’nikaanza kuongea na mdada, akanionyeshea ishara kwenye vifaa nilivyopewa, akasema

‘Uwe na kauli ya ujasiri, na kujiamini, usipinge au kulalamika...’akasema

Niliviangalia vile vifaa, simu, saa na mawani, nikajua vyote hivyo ni sehemu ya mipango ya kuniingiza kwenye kundi nisililolifahamu, na sijui kazi yao ni nini...nikatulia nikisubiria, na mara sauti ikasikika,..

‘Kwenye miwani yako hiyo, utasikia kila kitu...’akasema mdada, na kweli, nilisikia sauti ikitoka, ni kitu kama hotuba, mtu alikuwa akiongea, kuwashukuru waliohudhuria, na kupongeza juhudi za kundi, akasema;

‘Pamoja na kupoteza mwenzetu mmoja, lakini usemi wetu ni kata mti panda mti, ....tuna furaha kuwa tuna kizazi kipya, wapo wanachama wapya wamejiunga, ....na wengine wapo kwenye mafunzo maalumu, ili waweze kujua wajibu wao,tuna wenzetu wengi wameshaingia kwenye sehemu nyeti, kwahiyo tumeimarika kabisa...natumai baadaye hao wote watakuwa watu muhimu kwenye kundi. Lakini pia tukumbuke uhai wa kundi ni michango yenu...kila mahali unapokuwepo, ujue unachomeka mirija yetu....

‘Hupotezi kitu hapo, kwani unachoiingiza ni kingi zaidi ya kinachotoka, lakini ni lazima tuwe na akiba maalumu kwa shughuli za utawala,tuweze kuwekeza kila eneo,....miradi yetu inaendelea, na huenda tukawa kundi la kwanza afrika katika uwekezaji,..bado tunasifika kwa ufadhili, kila mwanachama wetu anafadhili mambo makubwa kwenye taifa, na hilo ndilo lengo letu.

'Dunia yangu, ndio ndoto yetu, na hili litafanikiwa kama kila eneo kutakuwa na mtu wetu, kwahiyo hatutakuwa na kizuizi kila tunapotaka kufanya mambo yetu...hilo linakaribia kukamilika...

‘Pamoja na hayo zipo changamoto,...wapo wasiotutakia mema,wanataka kuziba mirija na juhudi zetu, wapo wasaliti, wapo ambao hawawajibiki, hilo ni lazima lifanyiwe kazi ili iwe fundisho,...mwenzetu aliyeondoka, ni mmoja wa watu waliojaliwa, lakini hakujali kundi, hakukumbuka wapi alipotoka, tukaondoa kinga yetu,....mnaona yaliyomkuta..

‘Kumbukeni kujiunga hapa ni huru tu, ila kutoka hakupo, ukitoka, tunakusindikiza kuzimu, natumai hayo mnayaelewa...zaidi ya hayo ni kuwatakia sherehe njema, na makaribisho mema kwa wanachama wapya, .....’mara kukawa kimiya,

Nilibakia kimiya nikijiuliza huyo aliyekuwa akiongea ni nani, mbona haonekani, na kwanini iwe siri kiasi hicho, nikageuka kumwangalia mdada, na niliona kama anaongea na mtu, kwenye simu yake, alipomaliza akasema;

‘Nimeambiwa nikuambie kuwa file la kesi yako lipo mikononi mwa wahusika, wanalifanyia kazi,na huenda baada ya wiki hivi kesi hiyo itakuwa haipo, lakini kwanza ni wewe uonyeshe kujali....’akasema

‘Nionyeshe kujali kwa vipi?’ nikauliza

‘Kwenye simu yako hiyo, kuna fomu ya kujaza, utaijaza na kuelelezea kila kitu wanachokihitajia, ukimaliza unatuma kutokana na maelekezo, baada ya hapo utakuwa ukipewa maelezo ni kitu gani ufanya, ukumbuke, hayo yote ni siri yako.....’akasema mdada

‘Mhh....’nikaguna

‘Usigune baba, ndio unaanza hapo, baada ya mwezi utakuwa unanukia umwenzetu,.....’akasema na kusimama, akaangalia saa, na kusema;

‘Ni muda wa kujichanganya, simama tutembee, kuna vitu vya kufahamu, usione hiki ni chumba, upande wa pili kuna maonyesho mbali mbali, kama ulivyosikia kundi hili ni wafadhili wakubwa, sio kuwa wanatania, ....’akasema

Tulitoka na kuelekea upande wa pili

**********

‘Mbona tangu jana nakutafuta hupatikani?’ ilikuwa sauti ya mchumba wangu aliyeniamusha toka usingizini, simu yake ilikuwa imeita mara nyingi, nilipuuzia kuipokea lakini ilipoita tena na tena, nikaona niipokee

‘Nilikuwa na mawakili, na watu wanaosimamia kesi yangu...’nikasema

‘Asubuhi hii, ?! Jana nimekupigia wee, hupatikiani, leo, asubuhi, nimepiga mara nyingi tu, simu inaita hupokei, upo nanani hapo ulipo?’ akaniuliza

‘Nipo peke yangu...nimeshakuambia, nilikuwa kwenye mkutano na mawakili, na nililala usiku sana, mawazo na mambo mengi yalinifanya nichelewe kulala,...’nikasema

‘Kwahiyo upo wapi, nyumbani kwako au umelala wapi?’ akauliza

‘Hapana...’nikasema

‘Hapana nini, mbona sikuelewi, upo wapi sasa..?’ akauliza

‘Sikiliza sio muhimu sana, kujua wapi nilipo, tutaonana kesho...’nikasema

‘Jana ulionekana ukija kwenye hoteli, ...au sio, ndio huko mlipokutana na hao watu wako, wanaokudanganya,..na kwanini  ni lazima mkutanie kwenye hoteli...?’ akauliza

‘Nani kakuambia nilikuwa hoteli?’ nikauliza

‘Kwahiyo unataka kunificha, basi nikuambie ukweli, jana wakati nilikuja pale polisi uliposhikiliwa, na wakati nafika bahati mbaya mkawa mnaondoka, tukawafuatilia, hadi mlipoingia kwenye hiyo hoteli kubwa...’akasema

‘Ulikuwa na nanii?’ nikauliza

‘Nilikuwa na shangazi, na sasa hivi nipo hapa hotelini....nilikuwa na baba...’akasema

‘Ulikuwa na baba yako!? Baba yako amefuata nini huku?’ nikauliza

‘Alikuja kwenye mkutano wao, na kwa vile nipo huku, alinitumia ujumbe kuwa hatakuwananafasi ya kuja huko kwa shangazi, kwani ana wageni anaongea nao, akaniita nije nionane naye mara moja, yeye sasa hivi anaondoka...’akasema

‘Mkutano...?’ nikauliza kwa mshangao

‘Ndivyo alivyoniambia...’akasema

‘Ulifanyika wapi na ilikuwa muda gani?’ nikauliza

‘Alisema ulifanyika Usiku, mimi sijui saa ngapi lakinini muda wa usiku....’akasema

‘Oh, ..lakini hapa kwenye hoteli kuna kuwa na mikutano mingi..’nikasema

‘Mimi sijui hayo....alisema ulikuwa mkutano muhimu sana kwao, walikuwa wanakaribisha wanachama wapya, na kuomboleza kupoteza mwanachama wao mmoja, baba bwana hapumziki, kila siku mikutano...’akasema

‘Oh,.....’nikajikuta nikiguna

‘Mbona unaguna,ninakusumbua,  kwanza hebu niambie wewe sasa hivi upo wapi, nataka kuonana na wewe.....’akasema

‘Leo haitawezekana...’nikasema

‘Kwanini, na mimi nina ujumbe wako muhimu...’akasema

‘Ujumbe gani kutoka kwa nani?’ nikauliza

‘Kuhusu huyu mwanamke unayetembea naye....’akasema

‘Mwanamke gani huyo?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi

‘Tatizo lako unafikiri mimi ni mtoto mdogo,unafikiri nimekuja hapa mjini kukaa tu, ni lazima na mimi nihangaike,...’akasema

‘Kwanini uhangaike..?’ akauliza

‘Niangalia nitasaidia nini kwenye kesi yako....’akasema

‘Kwanini ujisumbue, kesi yangu ni ngumu, inafanywa na mawakili, wewe huwezi kusaidia kitu....’nikasema

‘Nani kakuambia siwezi kusaidia kitu, ndio maana nataka kuja kukuona, nimegundua jambo, japokuwa baba anasema halina uhakika, lakini ni kweli kabisa...’akasema

‘Umegundua jambo gani?’ nikamuuliza

‘Kuhusu huyo mwanamke wako mwenye mashetani ....’akasema

‘Mwanamke gani, kafanya nini?’ nikamuuliza

‘Hata nikikuambia sasa hivi huwezi kuamini, lakini ni kweli kabisa, huyu anahusika, ndio yeye  aliyemuua huyo jamaa, halafu katumia mbinu ili ionekane ni wewe uliyefanya hivyo....’akasema

‘Wewe acha maneno yako haya...utafungwa...una ushahidi gani ?’nikasema kwa kunong’ona, na akanifanya nisimame, nilitaka hata kukata simu asiendelee kuongea, lakini haikuwezekana.

‘Hahaha, unaogopa eeh, kwa vile ni mpenzi wako,shangazi anafahamu kila kitu,sasa wewe cheza na hii familia, tuone kama utafanikiwa...’akasema

‘Sikiliza...’nikataka kuongea na yeye akasema

‘Mwanzoni nilikuwa simuelewi baba, alivyokuwa akisema hakuamini, ....nilimkatalia kabisa, lakini haya niliyosikia sasa, yananifanya nianze kuamini kuwa, wewe una mwanamke huku mjini, na huyo mwanamke na huyo huyo....’akasema

‘Hayo ni mawazo yako, ....’nikasema

‘Lakini yana ukweli, nimeanza kumwamini baba, nimeshamwambia kuwa nina mashaka na wewe, yeye kanipa tumaini kuwa, anakufuatilia, kasema sasa hivi upo mikononi mwake, keshajua mambo yako yote, anasubiri muda muafaka, .....’akasema

‘Sikiliza....tutaongea kesho, nakuomba tafadhali.....’nikasema

‘Baba wakati anafuatilia kesi yako, amegundua kuwa, huyo mwanamke ameshakurubuni, na huwezi kusema lolote juu yake, anakuperekesha kama garo bovu, ...lakini muda wako unakaribia, angekuacha uoze jela, ila kakustahi kwa vile umezaa na mimi...’akasema

‘Unasema baba yako anafuatilia kesi yangu, nani kakuambia yeye anafuatilia kesi yangu?’ nikamuuliza kwa sauti.

‘Unafikiri isingelikuwa baba, ungepata hiyo dhamana,...na hiyo kesi kwa vile ni ya kubambikiwa, yeye anaweza kuhakikisha inakwisha juu kwa juu...’akasema

‘Tutaongea kesho....’nikasema nikitaka kukata simu

‘Kesho naondoka, lakini kabla sijaondoka nataka kuonana na huyo mwanamke wako, nimueleze wazi kuwa wewe ni mchumba wa mtu…..,wewe ni muhini uliyeniharibia maisha yangu, na kama anataka kukurubuni, kwa umalaya wake, ajue atakuangamiza, mimi sitakubali...’akasema

‘Nakuomba tafadhali....’nikasema

‘Huna haja ya kuniomba...kesho nikiondoka, nataka uniambie utaratibu wetu wa ndoa ni lini,.....’akasema

‘Tutaongea kesho

‘Kesho kwanza nataka kuonana na huyo hawara wako,sijui kama mpo naye hapo au yupo nyumbani kwake, mimi sijali, nimeshafahamu nyumbani kwake, nitakwenda kuonana na yeye....’akasema.

Wakati huo huo, upande mwingine wa chumba, mdada akiwa na furaha, aliinua uso na kuangalia saa ya kitandani, na alipoona ni muda wa kuamuka, akijinyosha akiwa bado kitandani, na baadaye akatupa shuka pembeni, huku akilini akisema;

‘Mambo sasa yameanza...hakuna kupoteza muda sasa...huyu mtu sasa ni wangu, iliyobakia ni kuhakikisha anafanya kila ninachotaka,....’ akasema na kuelekea bafuni.

Huku kwenye chumba kingine mazungumzo yalikuwa yakiendelea, mhasibu akiwa katika wakati mgumu na mchumba wake, alitaka kukata simu, lakini aliogopa kuonekana anamzarau mchumba wake, akasema;

‘Tafadhali nakuomba usiende huko, utajitakia matatizo...’nikasema

‘Mimi siogopi mashetani yake, nitapambana nayo, hata mimi nina mashetani zaidi yake..kwanza niambie upo wapi, nije nikuone sasa hivi...’akasema na nikasikia kama sauti inaongea karibu yake , nikauliza

‘Unaongea na nani?’ nikauliza kwa hasira na wivu ukatanda moyoni

‘Naongea na shangazi....’akasema

‘Ndiye huyo anayekudanganya au sio....?’ nikasema

‘Nimwambie hivyo...’akasema

‘Mimi naongea na wewe, kwanini umwambie,..ina maaana mpo naye hapo, mlikuja naye,sikiliza....’nikasema na yeye akasema

‘Ndio nimekuja naye, alikuja kumsalimia kaka yake, na kumbe upo humu humu hotelini, , nimeshagundua, ina maana umelala humu humu na huyo hawara wako sio,...nakuja huko huko nionane naye...’akasema

‘Nina mkutano na wakili, sina muda wa kuongea na wewe kwa leo....’nikasema

‘Nimesema nakuja huko huko,....’akasema na kukata simu.

Mara nikasikia mlango wa chumba changu ukigongwa, nikashituka, maana sikutegemea mgeni yoyote muda kama huo, nikajiweka sawa na nilipoona nipo tayari kukutana na huyo mgeni, nikaelekea mlangoni, kabla sijashika kitasa cha mlango, mlangu ukafunguliwa .....

NB: Oh, tuishie hapo kwa leo


WAZO LA LEO: Inapofikia hatua wapenzi, wanandoa wanaanza kudanganyanya ujue hapo kuna tatizo, kwani uaminifu ni nguzo muhimu ya upendo wa kweli...sasa hiyo nguzo muhimu inavunja , tutarajie nini hapo...

Ni mimi: emu-three

No comments :