Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, April 9, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-37


‘Wewe nenda kaoge, leo nitakufungua macho kidogo tu,...uonge dunia inavyoliwa, kwa mrija, cha muhimu kwa sasa ni muonekano nadhifu,kaoge, ukitoka nguo hizo hapo,nataka leo uvae itakawavyo na wao, ...kwani huko kuna uvaaji wake,...’akasema

‘Uvaaji wake kwa vipi?’ nikauliza

‘Kila kitu kipo tayari, wewe ni kuvaa tu, hizo kwa vipi hazina maana, ukimaliza kuoga, nguo utazikuta hapo kabatini, mimi nakusubiria nje, kuna mtu nataka kumpigia simu, fanya haraka kidogo, muda umekwenda, ...nataka leo angalau kidogo uone starehe za hii dunia ,...’akasema

‘Umesema huko kuna uvaaji wake, mimi hapo ....’nikaanza kuongea

‘Hebu jail muda kwanza, kwani unataka kujua nini...?’ akauliza.

‘Mengi tu, ulishaniambia kuwa nikitaka kujua au kupata mengi, ni mimi nikubali, kila mara unaniweka hewani, mimi sitapenda kwenda huko mpaka niwe na uhakika nakwenda wapi na kufanya nini...’nikasema

‘Hahaha, masikini mhasibu, unafahamu ni kweli, unalozungumza, siwezi kukulaumu,lakini ukiuchunguza moyo wako ndani, unataka, na kila mmoja anataka kuwa mtu fulani, au sio...sizani ungelipenda kuwa kama ulivyo, sasa leo nataka nianza kukufunda kwa vitendo....’akasema

‘Mhh, kwa vipi?’ nikauliza

‘Kwanza nilishakuambia kuwa kila mmoja anataka kupata, lakini ili upate, unatakiwa ujitoe, uhangaike, ...na hapa ni pagumu, kuna mitihani yake, kuna kujitoa muhanga, kuna mambo mengi yanahitajika ili upate jambo, sio kila jambo ni rahisi tu, hasa kupata mali....mmh, kuna wengine wanafikia kutoa makafara,kujitoa mhanga na vitu kama hivyo, na ukiangalia nia na lengo ni kupata...’akatulia akiangalia saa yake.

‘Hapa, kwa hawa watu, wanajinsi ya kumpima mtu, kuna mambo mengo unaweza kukutana nayo, na hata kuumizwa, na wengine hupoteza maisha kabisa, wakasahaulika,hayo ni kwa ajili ya kukupima imani yako,je unaweza...’akatulia

‘Mimi sikuelewi,...ina maana unaniingiza kwenye mambo ya ushirikina?’ nikamuuliza

‘Ni nini maana ushirikiana?’ akauliza kwa mshangao

‘Mambo kama hayo ya kafara,...siumesema mwenyewe...’nikasema

‘Hata kwenye dini kuna kafara, au sio...kafara sio lazima ufanye ushirikina, ni ile hali ya kujitoa kwa hali yoyote, hata ikibidi kutoa damu...ili kuondoa vikwazo...wenzako hapa wameiweka hii kafara kisayansi zaidi, siwezi kukuambia zaidi, lakini cha muhimu ni kuamini kuwa baada ya hapo utapata....’akasema

‘Utapata nini?’ nikamuuliza nikiwa bado nimesimama na yeye akiwa kasimama akiwa tayari kuondoka.

‘Kwani watu wanatafuta nini katika hii dunia..?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho ya kunishangaa

‘Mhh, uhai, na, ...’nikawa najiuma uma na yeye akasema

‘Ni mali, utajiri, na maisha bora, au sio?’ akawa kama ananiuliza

‘Yah, ndio hivyo, inategemea kwa vipi, kwahiyo unataka kusema nini...?’ nikamuuliza nay eye akaangalia saa , inaonekana nilikuwa nampotezea muda, lakini hapo hapo hakutaka kunilazimisha kitu ambacho sio kawaida yake, nikahisi kuna kitu muhimu sana kwangu mimi kuwepo huko.

‘Kwahiyo,?...unaniuliza  hapo, ....jibu unalo wewe mwenyewe, ..usingelitoka huko kwenu kijijini kuja kutafuta kazi hapa mjini,..kama hoja ni maisha tu, hata kijijini yapo, hata kijijinu riziki ipo tu, ungelikaaa huko huko kijijini ikajipa,au sio, lakini ulihangaika hadi hapa,...unaona hoja hapo...’akasema

‘Ndio maana nauliza kwahiyo unataka mimi nifanye nini..?’ nikamuuliza

‘Ninachotaka wewe kwanza ni kuona, ni kufuta huo utongotongo,ilivyo kihalisia ukiona utaamini,...na nina uhakika kama una akili yenye kutafakari,utafanikiwa, na kufanikiwa huko hakutakuja bure bure , maana kila mtu kapewa akili, kila mtu ana kipaji chake chenye thamani tu tatizo ni kuwa hatujijua..’akasema

‘Mhh, , ...’nikaguna na yeye akasema

‘Hakuna cha kuguna hapo, ...kinachohitajika ni kukitafuta kipaji chako, kile chenye thamani, ukitumie, wewe unajiona una akili ya kuweka mahesabu sawa, au sio?, lakini inawezekana isiwe ndio kipaji chako, wenzako wana ujuzi wa kukitafuta kipaji chako,....kitajulikana ukitaka, na kujiunga kwenye kundi, wao wanakushauri ni nini cha kufanya, watakitumia kipaji chako na wewe mwenyewe utashangaa,..,’akasema

‘Unapsema wanzako, hao ni akina nani?’ nikamuuliza na yeye akanitupia jicho na kutabasamu, akasema;

‘Hayo maswali yako uwe makini nayo,....’akasema na kutulia kwa muda, halafu akasema

‘Nikuambie jambo katika hii dunia, kuna watu wapo kwenye makundi mbali mbali, wapo wengi tu huku na kule,wao wanaamini kuwa ni wanachama wa kundi fulani, wameamini tu, na wanatumiwa tu, lakini hawajui kuwa wanatumiwa kwa masilahi ya wengine,...

'Kiukweli watu hao wapo kama bendera kufuata upepo, wanajiita wanachama, ...waulize chama ni nini, kina nini ndani yake, madhumuni yake nk...hawajui kabisa, lakini wanaamini kuwa ni wanachama....unaona hapo, sasa mimi sitaki uwe humo kama wao, nataka uwe humo kama mtendaji...’akaniangalia kwa makini na mimi nikatulia

‘Mtendaji...?’ nikajiuliza na yeye akajifanya kama hakusikia na kusema;

‘Lakini kwenye vyama, au makundi, ili mambo yaende vyema, ni lazima hao watu wawepo...’akasema na kuniangalia moja kwa moja usoni, na mimi nikawa nimetulia tu.

‘Ninasemea hao, bendera fuata upepo, wapiga makofi, wapiga kura,...ili waweze kuwaficha watu maalumu,maaliwatani, matajiri, ambao kazi yao inaitwa ufadhili, ..’akatabasamu.

‘Hivi kweli mkono utatoa tu, hakuna kitu kama hicho, mkono utoao ndio unaopewa...hapi ndio hawa wenzetu walipojikita, wanaitwa wafadhili, lakini mumo ndimo wanapofanyia mambo yao...ni muhimu sana hapo, nimejifunza mengi hapo....’akatabasamu.

‘Dunia hii ukiwa na akili, haki ya mungu huwi masikini, ...nakuambia hilo, ukiwa masikini umetaka mwenyewe,’akatikisa kichwa kama kukubali jambo.

‘Sasa katika hilo kundi kuna watu wapo tu, wanatumiwa tu, ili neno likamlike, ambalo wengi wanalifahamu kama demokrasia...,si ndio hivyo?’ akaniuliza

‘Yah, ndio hivyo...’nikasema

‘Siasa hiyo bwana,  ndio maana kuna kitu kinaitwa ni nini, wengi wape,...bila kuwa na hao wengi, hawo watu maalumu hawatapata kitu, watashindwa kufanya mambo yao...kutokana na hao watu wengi, ndio ufadhili wao unapoonekana,..sasa kiujumla, ...kila mmoja anatakiwa kufika huko..lakini kwa spidi yake, ...kama wewe utaamua kulala haya...’akasema na kuniangalia na mimi nikabakia kimiya

‘Utaona kama ni ndoto fulani ya kufikirika,...lakini mimi nimeifanyia kazi hiyo kivitendo, na matokeo yake mnayaona, ...haya wa kusema ni ndoto waache waendelee hivyo hivyo, hebu niembie ukweli, wewe unanionaje kwa sasa, angalia mwenyewe, hivi sasa,nina nyumba nzuri, nina gari nzuri, ..nina miradi mingi tu,hata mingine bosi haifahamu ....naanza kupanda daraja, lakini ili ufike huko nahitajika kumpata mwenza wa kufikia mahala fulani,mwaminifu anayejua kutunza siri, lakini hayo sio muhimu kwa sasa ....’akatulia

‘Unasema mwenza, una maana mume au?’ nikamuuliza

‘Mhh, jibu hilo unalo mwenyewe....’akatulia na kuniangalia kwa makini.

‘Sasa kwenye nadharia hiyo, ni lazima kuwe na watu, ...wengi tu, wasiojua ni nini kinachoendelea, lakini ni wanachama, wanaamini hivyo,..ni muhimu kujaza wafuasi wengii kwa ajili ya kuombea misaada, wengi tu hata kama hawajui nini kinachoendelea, ilimradi ni washabiki tu, hawa wengine watakuja kusaidia kwenye kutoa makafara, kwenye kupiga kura,na vitu kama hivyo...geresha-geresha za namna hiyo, ni, ujanja ujanja,mbinu za aina yake...watu wanalimbikiza, wanatajirika, huku wewe umelala, ndugu yangu amuka...’akasema.

‘Sikuelewi,.....’

‘Kwasasa hutanielewa,....utakuja kunielewa tu, ...ila muda ni muhimu sana, kumbuka, hao ndio wameshikilia file lako la kesi yako,....nakudokezea tu...natumai hapo utanielewa, ni lazima ukubali huna ujanja, ina maana kweli wewe hutaki kufikia kwenye kundi la mwenzetu....  mwenzetu ni hatua ya juu sana..

‘Hahahaha, hata mimi mwenyewe sijafikia huko,.....samahani nimeongea sana, hata nisivyostahili kukuambia, nenda kaoge...’akainuka na kutoka, na kuniacha hapo chumbani. Nikabakia nimeduwaa, nikijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu na mara nikakumbuka usemi wa wakili wa kampuni....

‘Inawezekana upo ndani ya hilo kundi bila ya wewe mwenyewe kujijua, ukawa unatumiwa, lakini anyway, yote ni wewe tu, nikuambie ukweli, ni ukweli wako tu, ndio utakaoweza kukuokoa,....’

‘Ukweli wangu...!,ukweli upi huo...’ nikajiuliza

‘Ni ukweli wako tu ndio utakaoweza kukuokoa vinginevyo, utaniambia...’

 Maneno haya yaliendelea kunirudia kichwani, hadi namaliza kuoga, nikavaa zile nguo nakuonakana mtu mwingine kabisa...nikatabasamu, na mara mdada akarudi na aliponiona nimeshavalia, akatabasamu na kusema,...

Sasa upo tayari,...chukua mawani haya meusi, hii ni moja ya alama za kundi...nahisi watakuamini, japokuwa , nina imani wewe bado hujajiamini....na nakuonya usipokubali, sizani kama watakupa nafasi ya kufikiri mara mbili, watakufanya kafara .....’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo?’ nikamuuliza

‘Usijali, ...cha muhimu ni kuwa na mimi, na ukubali kuwa mimi ni mtarajiwa wako,  vinginevyo, huenda ukawa historia....’akasema na hapo hapo nikakumbuka yale maneno ya mwisho ya yule wakili;

‘Nikuambie ukweli, ni ukweli wako tu, ndio utakaoweza kukuokoa,vinginevyo, itabakia historia kuwa kulikuwa na mtu kama wewe.....’

NB: Naishia hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Kujiamini katika mambo yetu yawe ya kikazi au maongezi tu, ni muhimu sana, lakini huwezi kujiamini  hivi hivi tu, ni vyema kwanza kufahamu ni kitu gani unachokifanya(kukiongelea), kwa kukisomea au kwa kukifanyia utafiti , usiongee kiubishi tu wakati huna rejea zozote za matendo au za maandishi. 

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

Mnyonge mnyongeni lkn mpeni haki yake, unastahili pongezi mkuu, una vitabu vingapi, mbona hakuna tangazo kwenye blog yako?

Anonymous said...

HONGERA

Anonymous said...

Kwa kweli uko juu, nitakupa hongera sana, kipaji chako ni cha hali ya juu.