Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, April 2, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-35


‘Kwahiyo tunakwenda wapi?’ nikamuuliza mdada akiwa anaendesha gari kwa mwendo wa kasi, akageuza uso wake na kuniangalia halafu akaangalia mbele, na kusema;

‘Kwanza ni kwenda kujipongeza mengine baadaye..’akasema huku akitabasamu, na alivyokuwa akiendesha, utafikiri yupo kwenye mashindani.

‘Huu mwendo wa nini, huoni ni hatari....?’ nikamuuliza na yeye akatabsamu, na kusema

‘Unaijua hatari wewe...tulia mwanaume wee, ajabu kabisa mwanaume kuwa muoga hivyo, huu sio mwendo mbaya...lazima tuwahi mapema, kuna mapangilio maalumu huko, na huenda tunasubiriwa...’akasema

‘Na akina nani tena?’ nikauliza

Surprise...’akasema huku akitabasamu

‘Mimi leo nisingelipenda kukutana na watu, akili yangu haijatulia,...’nikasema

‘Basi kwa hali kama hiyo, ...unahitajia kitu kama hicho ...cha starehe, ukitoka hapo unaanza upya, cha muhimu, akili yako iachane na hayo, ...sahau kabisa...’akasema

‘Lakini ....’nikaanza kulalamika, na yeye akageuka mara moja kuniangalia  akasema;

‘Usitake kuniuzi, sikiliza ninachokuambia kwa masilahi yako mwenyewe, unasikia ‘akasema

‘Sijisikii kabisa kukutana na watu, hapa nilipo nahisi kama nipo uchi...’nikasema

‘Nakushauri kitu, kama huna la maana la kuongea kwasasa ni bora unyamaze, hadi tufike huko ndani, mimi nina imani utafurahi tu, utayaondoa hayo yote yaliyopo kichwani mwakoi...’akasema huku akizidi kukanyaga mafuta, ulikuwa mwendo mkali sana.

Nilikaa kimiya, sikutaka kuongea tena, nikatuliza kichwa changu na mara akili yangu ikajikuta inakumbuka mazungumzo haya;

‘Mimi naondoka, nimefikia kwa shangazi ,nilikuja jana,nikaambiwa upo na mazungumzo na wakili wako, nikaulizia, kuhusu kesi yako...wakawa hawaniambii cha maana..hata hivyo,nimeshaambiwa kuwa unashughulikuwa kuhusu dhamana yako,...

‘Sasa, siwezi kwenda kwako, unapoishi, unafahamu taratiu na mile zetu, kwa vile hatujafunga ndoa ,siwezi kwenda huko kwako unapoishi, nimefikia huko kwa shangazi yangu,....’

‘Shangazi yako yupi huyo, anaishi wapi hapa mjini...?’

‘Karibu na hiyo hoteli kubwa ya inayoitwa,...aa, Kajificheni...’

‘Oh,kumbe mna ndugu yenu hapa mjini, na anaishi karibu na hiyo hoteli mbona simfahamu, yupoje, mbona hatujawahi kukutana naye, huyo ndugu yako ananifahamu mimi..?’

‘Anakufahamu sana...’;

Mhh,kumbe ni shangazi yake , ndiye anayempelekea umbea huko kijijini, na inaonekana ana 
nifahamu sana, na huenda ameshaniona mara nyingi nikiwa na mdada, na......oh, sasa natakiwa kuwa makini,...sasa nitafanyaje na huyu mdada ndio kaniganda, nikisema niachane naye, anaweza kupandisha na hata kuyatuma hayo mapicha yake mabaya..sasa...

‘Hili sasa ni janga, kweli nimumbuka....’nikajikuta nikisema kwa sauti na mdada akaniangalia kwa makini na kusema

‘Unaongea peke yako au unaongea na mimi....?’ akaniuliza

‘Naongea peke yangu....’nikasema

‘Utachanganyikiwa, wanasema mimi nina matatizo ya kiakili,....kumbe tupo wengi, hahaha, inabidi na wewe uende ukamuone mtaalamu wa magonjwa ya akili....’akasema

‘Mimi matatizo yangu, sio kihivyo....’nikasema

‘Huenda pia ikasaidia kwenye hii kesi....’akasema

‘Kwa vipi...?’nikauliza nikimwangalia kwa kauli hiyo.

‘Kama kweli una matatizo hayo ya ya akili, itakuwa kama mimi, walipothibitisha kuwa kweli mimi nina matatizo hayo, unaona ilivyokuwa, waliogopa hata kunishika, wakaogopa, ...kuwa nikipandisha huko mahabusu hakutakalika......hahaha, ...watu waoga jamani, ...mmh japokuwa ni tatizo, lakini namshukuru mungu, kumbe kila kitu kina umuhimu wake....’akasema .

‘Lakini hilo ulilo nalo sioni kwanini waliite ni tatizo ...kwani huo ni ugonjwa wa akili, ..’nikasema kama nauliza

‘Wewe una utaalamu gani wa kulisemea hilo, hayo ni maswala ya wataalamu wa mambo hayo, madocta bingwa wamelithibitisha hilo,...sio kwamba napendelea hivyo, kwani kiujumla hiyo hali inanotesa sana ikianianza, na ikiisha ninakuwa mwili wote unauma.... sipendi kabisa hiyo hali,...lakini sasa utafanyaje, na...inafikia muda, natamani kumpata wa kumlaumu, ..hata hivyo sitamlaumu nani..’akasema

‘Wanaume...’nikasema kwa utani

‘Haswa, ni kweli, ....hata hivyo, ...hata sijui nifanye nini hii hali ipoteee, ndio nimeshauriwa niolewe, nikishaolewa, hii hali itakwisha kabisa....’akasema

‘Oh, ...kumbe...’nikasema

‘Ndio hivyo, na natakiwa niolewe na mtu ninayempenda,...na hisia zangu zimeshanionyesha huyo mtu ni nani, ndio maana hata kutokee nini, siwezi kukuumiza wewe...’akasema

‘Ina maana ....’nikasema na kukatisha

‘Yah, ndio hivyo, ...lakini hayo tutakuja kuyaongea baadaye, tumalizane na hili lililopo mbele yetu, hata hivyo, kwasasa , hatutakiwi kuwaza mambo mengine, nimekuambiaje...?’ akawa kama ananiuliza

‘Ni muda wa kustarehe...’nikasema

‘Ndio hivyo....kwa ajili yako,...nimeambiwa nisinywe pombe,  lakini nashindwa kujizuia, nikinywa pombe mara nyingi naishia kwenye matatizo,..na nashukuru siku nilizowahi kwenda na wewe umegeuka kuwa msaidizi na mlinzi wangu muhimu.....’akatulia na kuniangalia

‘Kwahiyo leo, leo ni lazima tunywe unaonaje dear...?’ akauliza

‘Hapana, mimi siwezi kunywa, na nilikuwa nakushauri kitu..., kwanza mimi sijaoga, sijajiweka sawa, nimetoka jela, na ujuavyo kule, usafi ni wa shida, nahitajia muda wa kuoga, na kujiweka sawa,...najisikia vibaya sana kwenda sehemu kama hizo nikiwa hivi...itanipa  wakati mgumu...’nikasema

‘Ile ni hoteli, ina kila kitu, hebu angalia hapo nyuma ya gar kuna nini?’ akaniuliza na mimi nikageuka nyuma ya gari kuangalia, niliona mfuko,...

‘Kuna nini?’ nikauliza huku nikiuangalia ule mfuko kwa makini.

Surprise....lakini usijali, kila kitu kipo sawasawa, ukifika hapo hotelini, utapata huduma zote, ni siku ya furaha leo, maana tumeweza kufanikisha jambo muhimu sana, sio rahisi kama unavyofikiria wewe,..’akasema

‘Ni kweli....’nikasema

‘Wewe huwezi kujua kwa jinsi gani jambo hilo lilivyokuwa gumu,....nimehangaika sana na huyo wakili, yote hayo ni kwa ajili yako, uone jinsi gani ninavyokupenda, je nikuulize, tangu upate haya matatizo huyo anayeitwa mchumba wako aliwahi kuja, au hata kukupigia simu? ‘akaniuliza.

‘Alishawahi....’nikasema baada ya kusita kidogo

‘Kufanya nini?’ akauliza na mimi nikatabasamu na kusema;

‘Kufanya yote,...kupiga simu, kuja kuniona...na kuangalia kama anaweza kusaidia lolote...’nikasema na akawa kama kashituka na kusema

‘Mhh, kumbe ni kweli.....’akasema na kutulia kama anawaza jambo fulani, na mimi nikamuuliza

‘Kweli kuhusu nin?’ nikamuuliza

‘Kuwa huyo mtu, alionekana hapa mjini....’akasema

‘Oh, umejuaje, ni nani alikuambia, kwani unamfahamu?’ nikamuuliza

‘Tatizo lako bado upo dunia nyingine, ..sasa hivi dunia ni kijiji, nilishapata taarifa hiyo, lakini sikuitilia maanani, kwa vile aliyeniletea taarifa hiyo, alikuwa na mambo mengi ya kuniwakilishia, ...mmh, inanipa muwasha washa, ....ok, hebu niembie,  huyo mtu bado yupo hapa mjini?’ akaniuliza

‘Sina uhakika....’nikasema

‘Huna uhakika, mbona unaongea kama huna raha, ...hukupendezewa na ujio wake?’ akaniuliza

‘Sikutarajia na sikupenda afahamu hili tukio...’nikasema

‘Ndio maana nakuona upo dunia nyingine, tukio kama hili linajulikana na watu wengi, iweje mtu wako wa karibu kama huyo ashindwe kufahamu,  ningeliona ajabu kama angekuwa kimya, hata asije kukuona,.... ikizingatiwa  kuwa huyo ni mtarajiwa wako....’akasema kwa sauti isiyo na furaha.

‘Wasiwasi wangu ni kuwa kama bado yupo hapa mjini, anaweza kunifuatilia, na hii inaweza kuleta mchafuko nisioutaka...’nikasema

‘Hilo unalo...’akasema na kutulia kimiya.

‘Mhh, haya bhana,...’nikasema

‘Kumbe ndio maana upo hivyo,..nimekupata,....’akasema na akawa kama hana raha, na mimi nikawa kimiya, ...akasema;

‘Hata hivyo, kwani wasiwasi wako ni nini..kuwa huyo mchumba wako atatuona tukiwa wawili?’ akaniuliza

‘Mhh...wewe huni kuwa hilo ni tatizo?’ nikamuuliza

‘Unaona, hilo ndio tatizo la kuchukua visicha vya kijijini, mnawaharibu mabinti wa watu, na kuwahadaa, kiakili wanakuwa hawajui hata maisha yanavyokwenda, ...'akasema

'Hayo ni mawazo yako...'nikasema

'Ok, sawa ni mawazo yangu, ....hata hivyo yeye bado mdogo, atakuwa anaelewa, kuwa mimi ni mfanyakazi mwenzako, na isitoshe, mimi ndiye msaidizi wako wa hii kesi,kwahiyo kuwa pamoja na mimi sio tatizo, labda awe na lake jambo, na kama lipo lake jambo, ni bora afahamu mapema, kuwa yeye na wewe basi....’akasema

‘Eti nini,....?’ nikauliza nikionyesha mshangao, na yeye akaniangalia akiwa katoa macho, na kusema;

‘Ina maana hukunielewa nilivyokuambia mwanzoni , kuwa sitaki kusikia maswala ya ndoa yako....usitake kunichanganya, umesikia, kama unataka mengine nisikie tena hiyo kauli,...’akasema na kuwa kimiya, niliogopa kuongea naye, asije akabadilika,...

Tulifika kwenye hiyo hoteli, na moja kwa kwa moja akalipeleka gari ndani kabisa, kuna sehemu maalumu ya kuweka magari kwa wanachama, na yeye ni mwanachama, na alipolisimamisha akatoka na kunifungulia, akasema

Here we are...’ akasema akishika mkoba wake kwa mkono mmoja, na mkono mwingine kashikilia mlango wa gari lake...akanitupia jicho la haraka na kusema;

‘Leo hii wewe ni mtu muhimu sana, ni lazima nifanye hivi, usione ajabu,...’akasema

‘Nashukuru sana....’nikasema

‘Usijali, ujue kuwa leo ni kufurahi kwa kwenda mbele, sitaki kusikia kingine zaidi ya furaha,....’akasema na mimi nikawa kimiya tu.

‘Unasikia nilichokuambia, tafadhali sana, usije ukafanya lolote la kuiharibu hii siku...nakuaptia ukifanya hivyo, utanibeba, ...’akasema akinyosha nyosha nguo yake na kujiangalia kwenye kiyoo kilichokuwepo, kwenye mkoba wake.

‘Nitajitahidi kufanya hivyo....’nikasema

‘Haya, ...natumai umenielewa mpenzi...’akasema na kunisogelea, tukawa tumesimama sambamba, yeye akiwa mkono wangu wa kushoto, tulitulia kidogo, mara akapitisha mkono wake kunishika kiunoni,..nilishituka kwani sikutarajia hich kitendo, akanishikilia na kuegemeza kichwa chake begani kwangu, halafu akasema;

‘Sikiliza nikuambie kitu, sasa hivi sahau yote, akili yako iweke kwenye furaha, ...’akasema na mimi nikajitahidi kutabasamu, na hapo nikawa najitahidi kuuondoa mkono wake, kwani kwa mahali kama pale sikutaka afanye hivyo, niliangalia huku na kule nikiwa na wasiwasi, na yeye akawa anajaribu kunishika zaidi, na aliponiona nahangaika kuuondoa mkono wake, akachekea  na kusema;

‘Hahaha masikini mhasibu, napenda hiyo eeh, ....kumbe na wanaume nao wapo hivyo,...acha hiyo mhasibu, usiniaibishe bwana...,’akaniangalia moja kwa moja usoni, halafu akasema;

‘Nikuambie kitu, wewe ukiwa na wasiwasi hivyo, na huo uwoga wa kinafiki, unapendeza sana, nataka uwe hivyo hivyo, hadi hapo utakapoweka pete kwenye kidole hiki.....’akasema akinionyeshea kidole chake, na muda huo alikuwa ameniachilia, na mimi nikaweza kupumua kidogo, tukaanza kutembea kuelekea mlango wa ile hoteli.

NB: Mtihani, mtihani, mitihani, baba yangu anaumwa, ....naomba dua na maombi yenu kwa wingi, mwenyezimungu amsaidia apone,  kwa uwezo wake yeye muumba wa kila kitu.


WAZO LA LEO: Hisia za wanadamu hutofautiana, hasa katika kupokea taarifa nzito, kuna wengine nafsi zao zinaweza kujenga ujasiri, wa kuweza kupokea lolote na wana uwezo wa kuhimili hali yoyote ile, wao wamejaliwa kuwa na mioyo migumu, lakini wapo wengine wenye mioyo dhaifu,...huenda ni kutokana na nakama za kimaisha, au madhila mbalimbali ya maisha yao, kwao wao, jambo dogo huwa ni kubwa,..hawana uwezo wa kuvumilia..hayo ni maumbile...Cha muhimu hapa ni kuwa na hekima ya jinsi gani ya kutoa taarifa nzito kwa wengine, kwani jambo dogo tu linaweza kuathiri afya ya mtu.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Fantastic goods from you, man. I've consider your stuff prior
to and you're just too fantastic. I really like what you have acquired right here, really like what you are saying and the way during which
you are saying it. You're making it enjoyable and you still take care of to keep it
sensible. I can't wait to read much more from you. That is really a terrific
site.

Also visit my site: best diet plans sacramento