Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, April 1, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-34


 Sikuamini kuwa kweli nimetolewa , japokuwa ni kwa dhamana,  na hata nilipotpka nje, bado nilikuwa na wasiwasi, nikawa nageuka nyuma, nikihisi kuwa nitaambiwa nirudi. Kwa ujumla kipindi masiku niliyokaa hapo mahabusu kilikuwa ni kipindi cha mateso kwangu ambacho sikuwahi kukutana nacho kabla....

Hata hivyo, ni kweli nimepata dhamana, je ndio itakuwa nafasi ya kuweza kupigania ukweli wa hili jambo, ili haki itendeke, kwa vipi, sikuwa na uelewi kwa muda huo, nilihisi kuwa na wasiwasi zaidi, na nikajikuta nikiangalia huku na kule, kama kumtafuta mtu nisiyemfahamua ni nani....

Kwa ujumla aliyefanya hayo yote hdi dhamana kupatikana ni wakili aliyetafutwa na mdada, akishirikiana na mdada mwenyewe, sikuelewa ni kwa jinsi gani waliweza kulifanikisha hilo..na kwa muda huo , sikujali sana ni hilo, kuwa ni jinsi gani walifanya,mimi nilikuwa na jambo jingine lililokuwa likinisumbua, kuwa sasa naingie kwenye mtego mwingine, ukweli, ...

'Sasa naumbuka....'nikajisemea kimoyoni..

Tuendelee na kisa chetu......

Wakati nipo na mdada, tunaongea kumbe wakili naye alishafika, yeye alipita moja kwa moja kwa wahusika, kufuatilia hatua za mwisho za hiyo dhamana, hakukuwa na kipingamizi kwani wakubwa walishapitisha, kwahiyo, wale wahusika wa hapo walichofanya ni kuweka kumbukumbu zao sawa kuwa kweli nilikuwepo hapo na nimeachiwa kwa dhamana.

Nilipomaliza kuongea na mdada, nikarudi mahabusu...nikiwa sijakuwa na uhakika wa dhamana hiyo japokuwa mdada alinigusia kuwa imeshapiitishwa. Kwahiyo niliporudi ndani, nikawa nimetulia nikisubiria tu.

Haikuchukua muda nikaitwa na kuambiwa niende sehemu ya kuchukua vitu vyangu, kwani nimeshakubaliwa dhamana yangu..sikuamini kuwa kumbe ni kweli,...basi nikafanya hivyo, na baadaye akaja wakili, tukawa tukatoka naye hadi sehemu ya kusubiria mambo mengine ambayo yalikuwa hayajakamilika, na hapo tukawa tunaongea na huyo wakili

‘Bahati yako, hukupelekwa huko gerezani, ungepelekwa huko kazi yake ingekuwa pevu, maana huko bwana, kutoka kwake ni mpaka twende mahakamani...na jamaa wa kule sio wote ninaofahamiana nao, kazi yetu hii inakuwa rahisi kama unafahamiana na watu...na watu sio kila mtu...’akasema huyo wakili huku akitikisa kichwa. Mimi niligeuka kumwangalia, na nilipoona yupo kimiya nikasema;

‘Mhh, hata  hivyo mpaka sasa sielewi kinachoendelea....’nikasema na kugeuza kichwa kuangalia mblele halafu nikageuka kuangalia huku huku na kule, nilikuwa kama namtafuta mtu, au kuonyesha mashaka fulani.

Ni kweli, moyoni nilikuwa sijiamini,...na hata hivyo sikuwa na uhakika hasa ni kitu gani ninachokiogopa au kuwa na wasiwasi nacho, je ni kutokuamini kuwa niko angalau huru kwa muda, au kuna jambo jingine linanisumbua kichwa changu. Nahisi nilikuwa naona aibu, nahisi, kama vile naogopa kufaminiwa, japokuwa sipo kwenye tendo la kufamaniwa, kiukweli, nilikuwa kwenye wakati mgumu, na Wakili aliponiona jinsi ninavyohangaika, akaniuliza;

‘Naona kama hujatulia, una wasiwasi gani?’ akauliza

‘Wasiwasi eeh, umeonaeeh!? Mmh, , ..hapana, siunajua tena, ni lazima ukiwa sehemu kama hizo, unakuwa kama hujiamini vile, hivi wewe ulishawahi kufungwa, kama hivi...?’nikasema na kuuliza

‘Hahahaha, Unaonaeeh,.....ndio hapo uone umuhimu wetu, kama sio sisi ungelikuwa wapi, ....hahahaha, mimi bwana kama nikufungwa ningelishafungwa sana, lakini ujanja, na kutumia hii....ndio maana sijawahi kufanywa hivyo.....’akacheka kwa sauti ya kitajiri, huku akigusa kichwa chake kwa kidole, kuashiria kuwa anatumia akili, na huku akinipiga piga mgongoni kwa kiganga cha mkono wake.

‘Mshukuru sana mdada, amefanya kazi kubwa sana, huyu mwanamke sio mchezo anajiamini na anaweza, japokuwa mimi ni wakili wake, lakini bila ya juhudi zake, na kujotolea kwenda kuongea na watu mashuhuri, tusingelifanikiwa kabisa, ....nimekuwa naye sambamba, nikifuatilia yale mambo ya kisheria,na kumshauri hili na lile, lakini mwanamke huyu ni jembe ....’akatulia na kusimama, kama vile kasahau kitu, halafu akanigeukia na kusema;

‘Yule wakili wa kampuni yako aliwahi kuja tena,...?’ akaniuliza

‘Hajawahi,....’nikasema nikijiuliza hata mimi ilikuwaje , huenda aliongea na mdada,akamueleza kuwa hahusiki tena.

‘Nikuambie ukweli kama ungelibakia na huyo wakili wako wa kampuni, ambaye ninayemfahami, ni wale watu, wanaotaka kufuata utaratibu, .....wewe kwenye nchi zeutu hizi utafuata utaratibu, ...hao wasimamizi wenyewe wa utaratibu hawafuati utaratibu, wewe ujifanya unafuata utaratibu utakesha...kuna wakati unatakiwa uchukue maamuzi magumu, japokuwa sio utaratibu...’akasema

‘Ina maana....?’nikasema

‘Ninachotaka kukuambia ni hivi, kila mara unatakiwa uangalie alama za nyakati, unafahamu...., ukiona kunastahili hiki fanya hivyo, dalili zitajionyesha, ..cha muhimu ni kuiiamini, angalia dalili kwanza kama kuna uwezekano, kama hakuna angalia mbadala wake, hii ni nchi yetu tunajijua wenyewe, akili ichanganye, tumia bongo, ....’akawa kama anaonyesha kichwa chake kwa kidole.

‘Sasa kwa hili lako, nimelisoma kwa makini, kiujumla, hakuna ushahidi wowote wa kuwabana nyie, ndio, bastola ina alama zenu za vidole, lakini kwa hali hiyo, sio ajabu, ....cha muhimu hapo ni muda wa tendo, muda wa mdada kupoteza fahamu....hapo inabidi kumshukuru docta....’akatulia

‘Muda ....muda na muda ambao wewe ulitoka nje, ...utakuta mauaji yale yalifanyika muda ambao wewe haupo na mdada keshapoteza fahamu,....ndio muda ambao jamaa alipigwa risasi,...hapo muda unawabana,wameshindwa kuweza kuliunganisha hilo...’akaulia

‘Ama kwa ushahidi mwingine uliopatikana,huna mshiko, hauna vigezo...na ukilinganisha na matukio yenyewe, unakuta nyie mpo salama, kuna jingine la msingi, ....’akageuka kuangalia nyuma.

‘Lipi hili?’ nikamuuliza

‘Kuhusu huyo mtu mwingine, aliyekuwa na ndevu,hilo ndilo polisi wanalitafuta , huyo mtu ni nani, na wao wameshikilia kuwa ndiye muuaji,.swali kubwa hata mimi najiuliza,huyo mtu ni nani,na kwa hivi sasa ni bora asipataikane kwanza ...akipatikana tu kuna mawili,yeye akawa muhusika, au akalta matatizo, hata hivyo huenda kupatikana kwake, kukaimaliza hii kesi, au kuzua balaa jingine....’akasema

‘Huyu mtu hawezi kuwa ndiye muuaji, kumbuka, wakati mimi natoka sikuwahi kuona mtu mwingine yoyote, niliwaacha mdada na marehemu...’nikasema

‘Atakuwa alijificha, na inaonekana anamfahamu sana mdada na matatizo yake hayo, kwahiyo alikuwa anajua nini anachokifanya, ndio maana hamkumsogelea, au atakuwa kafanya namna ambayo hisia za mdada zisingliweza kumnasa, hayo yanawezekana,  hata hivyo kwa jinsi docta anavyosema, hata kama angejificha wapi, mdada akiwa katika hali hiyo angemuona, kwani anakuwa na hisia kama za mbwa, ananusa na kujua chochote kilichopo karibu yake, ...’akasema

‘Kwahiyo...unataka kusema nini hapo?’ nikauliza

‘Hapo ni kitendawili,...tega ni tege, na mteguaji sio kazi  yetu.hiyo ni kazi ya polisi...tuwaache wao wafanye kazi yao, ...na hapo inanituapa muda wa kujipanga vyema, .unaonaeh, ndio maana tunataka tukae pamoja tuone hilo tutafanyaje ikiwa hivi au vile,...kwani hatima ya yote hayo, kuna kusimama mahakamani...una ona hapo,...’akasema

‘Mimi bado nashindwa kumuelewa huyo mtu mwingine, mbona anakuwa ni jinamizi, mimi nilikuwepo mle ndani sikumuona, hapana, siamini, mna uhakika kulikuwepo na mtu mwingine humo ndani....?’ nikauliza

‘Nimeshakuambia hilo halituhusu kwa sasa, hiyo ni kazi yao,...unafahamu....wakati wanahangaika hivyo,...sisi tunafanya yetu, kwa ujumla, hapa hakuna kesi kabisa dhidi yenu, kama kweli mliyoniambia ndivyo ilivyokuwa, basi kesi hapo hakuna, vinginevyo, labda muwe mumenidanganya,...’akasema na kuonyesha mkono wa ushindi.

‘Mdada yeye anasema nini kuhusu huyu mtu wmingine?’ nikamuliza

‘Mdada, mhhh, achana anye huyo, tatizo ni kwako,...hata hivyo, ya mdada yaache pembeni kwa sasa, hayakuhusu usijichanganye kabisa na kuhusu yeye....’akatulia

‘Mdada ana kinga ya kitaalamu, kwa kipindi hicho hakuwa yeye,  kama wanataka wamtafute huyo aliyekuwa ndani yam dada kipindi hicho, sawa, ....unajua vitu kama hivyo visikie tu, mashetani kuapagawa , kuchanganyikiwa, mmmh, hata mimi siamini...’akatulia kama akiwaza jambo.

‘Mimi mwenyewe nilipiga kichwa hapo, nikaongea na docta, docta wakeeeh,mmmh, kanihakikishia mambo hayo yapo na yanatambulikana kitaalamu, yapo kwenye kundi la watu wenye matatizo ya ubongo, akili, yeye  anaweza kuhakiki hilo kitaalmu, ,.....unaona hapo, ndio maana yeye mambo yake tulimaliza kirahisi tu, ...kwenye sheria mtu mwenye matatizo ya akili, hana hatia, anakinga..hahaha, haya mambo ukiyajulia, unapeta...’akasema.

‘Kwa namna hiyo vyovyote iwavyo, mimi ndiye ninayebakia hapo, kuwa nastahili kujibu kesi, kwa vile mdada hayupo tena...?’ nikauliza nikionyesha wasiwasi.

‘Mhh, usiumize kichwa chako kwa hilo, hiyo ni kazi yao,na kazi yangu kukutetea,...kuna watu wanalipwa kwa kazi hiyo, hatuna haja ya sisi kumiza kichwa saaana, mimi nitakachofanya ni kucheza na vipengele vya sheria...wenyewe wanasema mambo mazuri hayatai haraka, au sio, sasa sisi tunakuwa kama yule ndege mla mizigo, hana pupa, anasubiri udondoke tu, ....unaona hapo..’akasema akionyesha kweli hana wasiwasi.

‘Mhh, ni lazima niwaze, kwa hilo....’nikasema

‘Unasikia sana, ukiwaza jambo ukaumiza kichwa kuwa huenda itakuwa hivi au vile, ukaumia sana, hata kabla ya muda wake, ikafika huo muda kweli ikawa ndio upande wa kuumia, huoni kuwa utakuwa umejiumiza mara mbili....ni bora usibiri, kama nikuumia, utaumia huo muda ukifika, na kama ni kupata hutakuwa na hasara,...unapata kwa faida tu....unaona hapo, sijui kama unanielewa....’akasema akiniangalia. Na aliponiona nipo kimiya akasema;

‘Kila kila kwa wakati wake, ..unaonaeeh,   wenzako walijipanga kulifanya hilo, sio kwamba wamekurupuka tu, kwahiyo, hapo unatakiwa utumie akili, lakini usiumize akili kihivyo, waachie wanastahiki kuumiza kichwa, wafanay hivyo, sisi tunakuwa kama huyo ndege mla mizigo, ....unaona hapo...hicho kwa ujuma ni kitendawili...’akasema

‘Lakini vyovyote iwavyo ni lazima haki itendeke, muuaji apatikane afikishwe kwenye vyombo vya haki..’nikasema

‘Na hiyo sio kazi yako,...nisikie sana hapo,  na hiyo sio kazi yangu, mimi kazi yangu ni kukutetea wewe, nihakikisha wewe,...hushitakiwi, na ukishitakiwa, unashinda kesi,...hakuna swala la kushindwa kesi hapa...., ‘akatulia akawa kama anawaza.

‘Sizani kama unanielewa, nikuambie ukweli, hawa watu hawana kesi dhidi yako, wamekushikilia tu, ili waonekana wanafanya kazi,...wanachofanya kwa sasa ni kuvuta muda, .....kwa hali hiyo mnyonge atakayeingia kwenye anga zao, ndio huyo anakuwa chambo...wewe wakakuona ni chambo hawakujua kuwa nyuma yako yupo mdada.....’akatulia kidogo.

‘Sasa kwa vile taratibu zao za kufanya kazi mimi nazifahamu, ...huhitajiki tena hapo kusubiri taratibu ...hapo hakuna cha kufuata utaratibu, kama alivyotaka kufanya wakili wenu wa kampuni,..nikuambie ukweli, huyo wakili wenu angekuchukua muda sana kulifuatilia hili, kwani ndio hao watu wa  kufuata taratibu, na bongo kwa hilo, ooh, `ngoja, subiri, silioni zitakuwa nyingi, usipojulia utasaga makalio, uskisubiri, utamaliza soili za kiatu ukifuatilia, wewe huku unasota jela ...’akagonga gonga kiatu chini.

‘Mhh, unaonekana wewe unaufahamu sana na mambo haya, hujali kuvunja sheria?’ nikamuuliza

‘Nani kavunja sheria, ....mimi hata siku moja sivunji sheria, nafuta muelekeo wa sheria, sheria inaweza ikapindishwa, ....kwa makusidi maalumu, mimi ninachofanya nikufuatilia jinsi inavyokwenda,..kwa mfano  leo hii walishapanga kukupeleka huko gerezani, ...sasa ahpa ungefanya nini,..mtu usie na hatia ungelienda kusota jela, utaumia, na huenda wakakumaliza huko huko....utakaa kimiya, utasubiri, utaratibu, ...hapo ni akili kichwani mwako...’akasema akiniangalia kwa makini.

‘Kwahiyo una maana....’nikataka kusema na yeye akanikatisha na kusema;

‘Nikuambie ukweli  kama isingelikuwa juhudi zangu na uzoefu wa mambo haya, usingelipewa hii dhamana, ...ndio maana mdada aliliona hili mapema, huyu dada ni kichwa, anajua kuyasoma mambo, sio kwamba hakutaka huyo wakili wenu aifanye hii kazi, ....angaliacha afanye kwa vile na yeye alikuwa na kesi yake,lakini akaona umuhimu wako, wewe ni mfanyakazi mwenzake, na hayo yaliyotokea yalitokea wakati nyie mnamjali ....’akasema.

‘Mhhh, ...ni kweli, nisingelienda hap ohayo yote yasingelitokea, na .....’nikatulia kidogo na baadaye nikasema

‘Haya mimi nawasikiliza nyie maana mambo yamekuwa ni kama mgeni kwenye nchi ngeni hata hujui uende wapi....’nikasema

Baadaye aliitwa na akawa anaongea na muhusika wa maswala ya dhamana, na kupewa amsharti, na mimi nikawa nasikia anachoambiwa, na baadaye akasaini, kitabu cha humo, na wakakabidhiana nyaraka, na walipomaliza hilo zoezi, yule wakili akanijia na kuniambie tuondoke...

‘Ulisema wewe unakuwa kama mgeni kwenye nchi ngeni au sio?’ akaniuliza

‘Ndio kwa hali ilivyo....’nikasema huku tukitembea kuelekea nje.

‘Ndio hivyo, sisi tutakuwa wenyeji wako...usijali, cha muhimu ni kusikiliza na kufuata yale unayoelekezwa hadi hili tatizo liishe, maana hapo ni mwanzo tu....bado kesi haijafika mahakamani, bado...sijui yatakayofuata baadaye, maana mwenye kovu usizani kapoa....’akasema na kuanza kutembea na mimi nikawa namfuatilia nyuma, kwa mwendo wa hatua za kuhesabu.

 ‘Hata hivyo muheshimiwa,  dhamana ni kitu kingine,...haitanisaidia sana, ukilinganisha na kesi yenyewe, nikuulize ,.... vipi kuhusu kesi yenyewe, umejipanga vipi, .....maana ninaweza kutoka kwa dhamana, kesi ikaja nikaonekana nina hatia, wakati mimi sijafanya hilo kosa...’nikasema

‘Hilo limeshafanyiwa kazi, usijali...ni kazi ndogo tu, kama nilivyokuambia, polisi wenyewe wamechanganyikiwa, ....ni kitendawili, ...maana jinsi ilivyotokea na vielelezo walivyo navyo, wanajikuta hawapati muafaka wa pamoja, wao wenyewe wamajikuta wakigawanyika makundi mawili kila mmoja akiwa na dhana yake....hapo ndipo wanapokosea....’akasema

‘Sasa itakuwaje...?’ nikauliza

‘Cha muhimu ilikuwa wewe utoke kwenye anga zao, ili tuweze kuliangalia hili swala kwa pembeni, kwani mambo mengine yanakuwa magumu wewe mlengwa unapokuwa haupo nasi,... huwezi kujua huko wanakuuliza kitu gani,...polisi wana mbinu,...na huwezi kusema hili limewashinda inawezekana ni moja ya mbinu zao, mhalfu wameshampata....lakini wanasubiri wakati muafaka, ndio maana nasema sisi tusimuize kichwa, ilimradi tunafahamu hatuna kosa....

‘Ndio maana tunataka uwe karibu nasi, ili tujue utaongea nini, ...wakati ukifika,...mimi nawafahamu sana hawa watu wanaweza  hata kutumia nguvu kukulazimisha kuongea..ukiwa kwenye mikono yao, au kusaini nyaraka wanavyotaka wao,hilo pia linawezekana...kwahiyo ni muhimu uwe nje, ili tuwe na uwezo wa kukudhibiti,....’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo...mnataka kunidhibiti mimi kwa vipi?’ nikauliza

‘Hapa ndipo mdada alipocheza, kunitafuta mtu kama mimi, kichwa cha vipengele vya sheria, ...’akasema huku akitembea kwa madaha.

‘Sikiliza ndugu,usiumize kichwa chako kabisa, wewe mwenyewe utakuja kugundua hilo baadaye, ....kwa hivi sasa ni wewe uwe kwenye anga zetu, na mambo ya usalama nini na nini..inabidi kuyaangalia..anyway, usijali sana, maana kiukweli, kama ilivyosikika kutoka kwao wenyewe ni kweli, kuna watu wanaweza kukumaliza kama wakiona unafahamu jambo litakalowaingiza matatani...hilo linawezekana...’akasema na kusimama na mimi nikasimama karibu yake.

‘Hivyo basi tunahitajika uwe sehemu ambayo tutahakikisha, haitokei hivyo, wanadai kuwa, upo kwenye hatari, kuna watu wanataka kukunyamazisha kwa hali yoyote ile...anyway, mimi sina uhakika sana na hilo, cha muhimu ufike nyumbani,kwangu kwa hapo nimeshamaliza kazi yangu...’akasema

‘Mhh, hapo sasa mnanitisha ina maana hakuna utaratibu wowote mliopanga wa kuhakikisha usalama wangu kama kweli hicho kitisho kipo,.....?’nikauliza

‘Tumalipanga hilo, .... tumeona kwa vile kuna hii kesi na sisi ndio tumekudhamini, inabidi ukae karibu na sisi, yaani karibu na eneo ambalo nitaweza, au watu wangu wataweza kukuona na kuhakiki nyendo zako, unafahamu hii kesi ina ugumu wake, hasa inapifikia kwenye sehemu hii ya kudhamini mtu,..’akageuka kuniangalia.

‘Kwanza wewe mwenyewe unaweza ukaingiwa na wazo la kijinga, ukaamua kutoroka,au watu wakaja kukufanyia lolote, huwezi jua,..na mimi ndiye mdhamini wako, na lolote likitokea mimi nitakuwa matatani, kwahiyo mimi nikaonelea  ukae sehemu maalumu, ambayo mimi na watu wangu tutaweza kukuona na kuhakiki usalama wako....’’akasema

‘Sehemu gani hiyo maalumu, kwasababu mimi siwezi kuishi mbali na nyumbani kwangu, kwanza kwa hivi sasa nataka twende nyumbani kwangu...’nikasema

‘Nyumbani kwako??..., wewe una nyumba hapa mjini?’ akaniuliza kama ananishangaa, na mimi nikasema;

‘Sehemu nilipopanga...ni kweli, sina nyumba hapa mjini’nikasema na yeye akatikisa kichwa na kusema;

‘Ndio kama ni muhimu kufika huko ulipopanga hakuna shida, nitakupeleka huko uchukue unachokichukua, ...halafu tunakwenda kukuonyesha wapi, unapostahiki kukaa, hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa, ili na mimi nijirizishe...’akasema

‘Kwanini muwe na wasiwasi na mimi, nawahakikishia kuwa mimi siwezi kutoroka, na sina mtu wa kunihatarishia maisha yangu, ,msiwe na wasiwasi na mimi...pia mimi ni mfanyakazi, nina kazi yangu,..’nikasema

‘Ni muhimu niwe na uhakika, ...hata hivyo, mengi mtaongea na mdada, tuone jinsi gani ya kufanya, ila ningekushauri ufanye kama nilivyokuagiza, sitaweza kuhakiki usalama wako ukiwa mbali na mimi,niamini ninayokuambia, nina uzoefu na mambo haya...usalama wako kwa sasa, nahisi pia upo matatani, japokuwa sitilii maanani sana, lakini lisemwalo lipo, ..kama halipo, hutapungukiwa kitu ukiwa umejihami...’akasema

‘Una maana kusema hivyo...?’nikauliza

‘Mimi kazi yangu ilikuwa ni kuhakikisha nafanikisha unatolewa kwa hao watu, na hilo nimelifanya, hata hivyo, sheria inahitajia nihakikishe upo salama, na uwepo kesi ikianza...unaona hapo, ndio maana sitaki lije litokee jambo, niharibu sivii yangu...na nahisi kuna watu wapo nyuma yako, kuna watu wanaoenkana kukufuatilia, sina uhakika kuwa ni watu wenye mlengo mwema, .....’akasema

‘Watu gani hao...?’ nikauliza

‘Utaongea zaidi na mdada, ila ninaloweza kukuambia ni kuwa uwe makini, na kama ingelikuwa ombi langu...’akasema

‘Ombi gani?’ nikamuuliza

‘Ukakae sehemu niliyokuchagulia mimi, ili niweze kuhakiki usalama wako....’akasema

‘Mimi hata sijui nifanya nini kwa maelezo yako tu, nahisi kuna jambo lipo, na huenda hata wewe unalifahamu, na inanifanya nisiwaamini, wewe na watu wako, nona kama mna ajenda ya siri dhidi yangu...’nikamwambia

Anyway, hayo mtaongea na mdada, mtakavyokubaliana mimi sina shaka...nimekuelezea hilo ili uone hali halisi, hapo ni wewe kutumia akili yako, kulitafakari hili nililokuambia..., unafahamu dunia hii ione ilivyo, sio kila king’aacho ni dhahabu, sio kila anayekuchekea ni mtu mwema kwako....wenzako tunajua ni nini cha kufanya kwa muda wake, wakati mwingine inabidi, utumie mbinu ya kuuma na kupiliza ilimradi mambo yaende sawa, siku zinakwenda...’akasema

‘Mimi sikuelewi una maana gani hapo....., ujue wewe ndiye wakili wangu, na usalama wangu upo kwenye mikono yako, unakumbuka ulivyoambiwa na huyu mtu aliyekukabidhi kuwa mimi ni mtu wao na usalama wangu kwa sasa upo mikononi mwako, na ulikubali kuwa utahakikisha nipo salama kwa ajili ya hiyo kesi, leo unaniambia mambo kama hayo....’nikasema

‘Kwani nimekuambia nini kibaya...nimekutonya tu, ili na wewe utumie akili yako, kama upo tayari ukakae sehemu niliyokuchagulia mimi, lakini kama bado unahisi ni bora ukakae kwako haya....ila ninalokuambia ni kuwa uwe makini....’akasema

‘Kuwa makini kwa vipi,?’ nikauliza

‘Mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu, nitafanya kila kitu ambacho kinaweza kutambulikana kuwa niliwajibika juu yako, lakini kuna mengine ni juu ya uwezo wangu, sheria unalifahamu hilo, sitaweza kuhukumiwa kwa hayo, yanayofahamika....kwahiyo ikitokea hayo, ambayo ni juu ya uwezo wangu sitaweza kualaumiwa...’akasema

‘Kama yapi?’ nikauliza

‘Nimekushauri ukakae sehemu ninayotaka mimi, ili niweze kuhakikisha usalama wako, umepinga, na ukiwa kwako, unaweza ukafanya mambo ambayo, sitaweza kuhakiki, chakula chako, maji yako...na mengineyo, mimi siwezi kujua unakula nini, unakunywa nini, utakwenda wapi, na linguine muhimu sana, nakuonya.....usipende kwenda kwenye majumba ya starehe kwa sasa, au kutoka sehemu zisizojulikana....’akasema

‘Mimi siwezi kufanya hivyo....najua nina kesi kubwa mbele yangu, mimi sana sana nitakwenda kazini tu...’nikasema

‘Safi kabisa, na mimi nitajitahidi kuhakikisha usalama wako upo, kuna walinzi watakuwa karibu yako, sio lazima uwajue...’akasema.

Tukawa sasa tumefika kwenye gari lake, na mara nikasikia honi ya gari, ..tukageuka kuangalia , mdada alikuwa kwenye gari lake, akaonyeshea ishara ya kutuita, na kwa haraka wakili huyo akaanza kutembea kule kulipokuwa na gari la mdada, mimi nikabakia nimeduwaa, nikaona mdada anaonyeshea ishara kuwa na mimi niende.

Tulifika pale lilipokuwa gari la mdada, akasema

‘Muheshimiwa huyu mtu naondoka naye mimi, ...’akasema

‘Mhh, lakini sijamalizana naye...na..ali...’akasema

‘Usijali, ...’akasema mdada huku akiniashiria mimi niingie kwenye gari lake....na yule wakili akabakia ameduwaa , na mimi sikuwa na la zaidi.....nikamwangalia wakili, na yeye akageuka pembeni...

NB: Kwa leo inatosha eti?..ila mtandao ni ishu!


WAZO LA LEO: Kusoma kunatusaidia kujua jambo kwa usahihi wake, au kwa uhakika, unaposomea nyanja fulani, unakuwa na upeo mpana zaidi wa hiyo nyanja, au taaluma uliyoisomea, lakini sio kwamba utafahamu kila kitu kinachohusiana na hilo jambo,kama binadamu tunaweza kuwa na walakini,na mwingine akawa anafahamu zaidi, au kwa njia tofauti, lakini kwa mantiki hiyo hiyo ...kwahiyo basi tukubali kukosolewa, kuelekezwa, au hata tukiambiwa kuwa hapo tumeteleza tuwe ni  wepesi, kusikiliza kwa masilahi mema ya lile jambo. 

Ni mimi: emu-three

No comments :