Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 27, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-33


Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu sana, nikawa na mawazo mengi sana...ni kila mara mara niliishia kutaka kujua hatima ya kesi yangu, je  itakuwaje...na nilichanganyikiwa sana, nilipopigiwa simu na baba mkwe

Ilikuwa nimepumzika, wakati alipofika askari na kusema kuna mtu anataka kuongea na mimi kwenye simu, nikajua huyo anaweza kuwa mdada, nikaiweka sikioni ile simu
‘Ndio, nimabie....’nikasema

‘Kuna mambo mengi nimeyasikia juu yako, nilitaka kuhangaika ili kesi yako iishe mapema,lakini kwa hayo niliyoyasikia, nimekata tamaa kabisa,...hebu niambie ukweli wewe na mdada mna mahusiano gani...’ilikuwa sauti ya baba mkwe, iliyonifanya nishituke na kutaka hata kupiga magoti

‘Oh, baba..mkwe.....shi...shikamooo...’nikasalimia

‘Shikamoo na wewe, umsikia swali langu?’ akaniuliza

‘Hapana,....’nikasema

‘Hujasikia swali langu?’ akaniuliza tena

‘Mzee mimi sina lolote na huyo dada, yeye ni mfanyakazi wetu tu..hakuna zaidi.....’nikasema

‘Mfanyakazi wenu uende kukaa kwake usiku kucha,..au unafikiri mimi sifahamu, nafahamu fika n kitu gani kilitokea huo usiku....’akasema

‘Wengi wamsikia tu...mimi na bosi wangu tulikwenda pale kumjulia hali , tukakuta amezidiwa ndio tukapanga tumsaidie kama mfanyakazi mwenzetu, na ndio huyo marehemu akatokea, ..kifo chake hakuna aliyekitarajia, hata sijui ni nani kamuua...’nikasema

‘Ninachotaka kukuambia ni kuwa, hayo ya mahusiano yako na mdada yamefikaje kwa binti yangu, ...?’ akauliza

‘Mzee mbona sikuelewi, ni nani kamuambia uwongo huo, ..hakuna mahusiano yoyote , labda ni watu wanataka kutogombanisha tu, ni fitina tu....’nikasema nikihisi labda mdada katuma mapicha yake mabaya, lakini hilo sizani kama mdada anaweza kufanya hivyo.

‘Sasa sikiliza kwa makini,...nilishakuambia mapema, kuwa nilichelea kukuweka ndani kipindi kile ulichomharibu binti yangu, baada yaw ewe kukiri kuwa utamuoa huyo binti, na nisaidie kukutafutia maisha, ..hiyo kazi nimehangaika mwenyewe, bila yaw ewe kujua, ....kuipata hiyo kazi ni kutokana na mimi kukupigia debe,....’akasema

‘Nashukuru sana mzee...’nikasema

‘Sasa kama kuna ukweli wa hayo, na jinsi binti yangu alivyoyapokea hayo, nahisi kachanganyikiwa, sijui...lakini nakukanya , nafikiri unanifahamu,....nalifuatilia hilo kwa 
karibu sana, ...nikifuatilia kesi yako inakwendaje, ....’akasema

‘Mzee, usiwe na shaka, hakuna lolote , mimi najiapnga kesi ikiisha tu, nafika kijijini, kufanga ndoa, unaona nyumba ile,..hata jina nimeandika jina la mchumba wangu kuonyesha kuwa namjali, hakuna...’nikawa naongea, kumbe simu ilikuwa imeshakatika mzee hayupo hewani,...

Basi nilipotoka kuongea na mzee nikawa nawaza sana, nikiwa namuwazia huyo mchumba, namfahamu sana, ni binti asiyejua kuvumilia machungu, kitu kidogo kitamsumbua sana,..sikutaka kabisa aje kusikia lolote linalotokea huku kijijini.

********

 Niliingia kwenye chumba ninachokaa, nikiwa na mawazo sana nikajitahidi kuyapima maneno ya wakili aliyetafutwa na mdada, ambaye alinithibitishia kuwa yeye ataweza 
kuhakikisha kuwa dhamana yangu inapatikana.

‘Kama dhamana ikipataikana ni lazima nifanye juhudi ya kulimaliza hili tatizo, sitaki tena kuwa mtumwa, sitaki tena...’nikatulia nikiendelea kuwaza;

‘Ina maana kweli huyu wakili anaweza kulifanya hili kama alivyosema kuwa anaweza kufanya dhamana ikapatikana na hata kuimaliza hii kesi haraka iwezekanavyo, mhh, sijui kwa vipi, lakini aliposema kuwa kesi kwa mdada haipo tena, nikaingiwa na wasiwasi, kuwa huenda kinachotumiwa hapo ni pesa, lakini iwezekanaje..siamini..

Na huyu mpelelezi anakuja na sera yake, ya kuwa mimi nijitolee kwa ajili ya taifa langu, niakumbuka maneno yake, akisema,...

‘Kundi hilo, limejengwa na watu mashuhuri tu, lina mawakala kila sehemu nyeti, zikiwemo sehemu hizi za usalama, huwezi amini hata mimi siwaamini watu ninaofanya kazi nao, ...ndio maana nataka tuwe kitu kimoja, ujitolee kwa ajili ya taifa lako....

Kauli hii ilinitia motisha nikawa nakumbuka masomo ya shuleni kwenye kipindi cha siasa na historia, kuhusu watu mashuhuri, waliojitolea kwa ajili ya mataifa yao na kuweka historia, japokuwa wamekufa lakini hadi leo wanazungumziwa, nikajiuliza hivi na mimi kwanini nisiwe kama wao...

‘Kwa vipi niwe kama wao, ni nani ataniona, ....ina maana nijitolee kwena gerezani, nikataabike, nikitoka niseme nimefanya hivyo kwa ajili ya taifa langu....hakuna kitu kama hicho...kwanza wamejipanga kuniulia huko huko gerezani, .....mmh, sikubali’nikasema

‘Sasa nifanyeje, nitoe siri zangu kuwa mdada alinifanyia mambo mabaya, na ndio maana nashindwa kusema lolote lakini hata hivyo ni kweli kuwa nafanya hayo kwa ajili ya mashinikizo yam dada, au kuna kitu kingine...?’ nikajiuliza

‘Kitu kingine kama kipi, mhh, labda ni kwa vile nimetokea kumpenda au nimezimia wake....sijui, lakini mdada kaumbika,...mmh, ndio maana hata mtoza ushuru aliingia kichwa kichwa...na sasa ni marehemu, na mimi je....’nikasema na nilipomkumbuka mtoza ushuru, nikajaribu kukumbuka jinsi ilivyotokea siku ile..

‘Nakumbuka kabisa nilitoka mle ndani, mtoza ushuru akiwa hai, japokuwa alikuwa anajikongoja, nahisi ni kwasababu ya jinsi mdada alinyomrusha na kumbwaga chini kama gunia, ...kwa hali ile kama wewe sio mpiga miereka unaweza ukavunjika mifupa, ...hata hivyo jamaa alionekana kukomaa, kwani aliweza kusimama na kuanza kujikongoja kutembea,....sasa aliuwawa vipi kwa risasi,...siwezi kujua maana nilishatoka nje...’nikasema

‘Kwa jinsi ilivyokuwa, ...mdada anahusika moja kwa moja, kwani nilimuacha yeye na huyo mtoza ushuru, na mdada ndiye aliyekuwa na hiyo bastola...inawezekana pia huyo mwtu mwingine alikuwa kajificha mahali, baada ya kunigonga mimi kichwani na hiyo nyundo, na alipoona nimezimia, akamgeukia mdada....

‘Hata hivyo, kinachonishangaza ni jinsi gani huyo mtu mwingine, ambaye nahisi ni mwanaume, alivyoweza kumsogelea mdada...nijuavyo mimi akipandisha huwa hataki mwanaume amsogelee, na nakuwa na hisia za ajabu sana, hata kuona kitu kinachokuja nyuma, ...huenda mtu alikuwa kajificha, na akamtokelezea mdada kwa nyuma kwa haraka sana, sasa huyo mtu alikuwa kajificha wapi, mbona mimi sikumuona?’ nikajiuliza

‘Atakuwa ni nani huyu mtu, na aliingia saa ngapi, na kwanini mlinzi asimuone, mhh, kwa vyovyote atakuwa katumia mbinu za hali ya juu kumpita mlinzi, na kuingia ndani bila kuonekana,huyo mtu sio wa kawaida ...sasa atakuwa ni nani?’ nikajiuliza bila kupata majibu
Ilikuwa kama marue rue, mwili ukaniisha nguvu, na mara nikazama kwenye usingizi, na kujikuta nimesimama katikati ya miti iliyofungwa kama magogo, na mimi nimefungwa bara bara...nikajiuliza kwanini nimefungwa hivyo

‘Unahukumiwa kwa kosa la kuua ...’nikaambiwa

‘Mimi sijamuua mtu..’nikasema

‘Tuthibitishie kama hujaua.....’nikaambiwa, na sikuwa na cha kuthibitisha, maana hata hilo kosa lenyewe al kuua, sikulitambua,...nikakaa kimiya

‘Umeshindwa kuthibitisha unanyongwa...’sauti ikasema

‘Lakini mimi sijaua..’nikajitetea

‘Thibitisha kama kweli hujaua...’sauti ikasema

‘Sina cha kusibitisha maana hata sijui nimemuua nani..’nikasema na mara ukaletwa mwili, uliofunikwa, na kuambiwa, unamuona uliyemuua....unataka kumuona ni nani?’ nikaulizwa

‘Ni...ha..pa...ni nani?’ nikauliza na mara ukafuniliwa, na nilipoona sura yake nikapiga ukelele na kuzindukana kwenye usingizi, niliamuka huku nikiwa nahema, moyo ulikuwa ukienienda kwa kasi, na sikutaka hata kuikumbuka hiyo ndoto, nikainuka pale nilipokuwa nimelala, na kunyosha nyosha viuongo

‘Hiyo ni ndoto sio kweli...’nikasema, na mara kukapambazuka na asubuhi ikaingia nikiwa sina raha, na ile ndoto ilinitawala sana kichwani, na nikawa najiuliza kwanini itokee vile, kwa nini nionyeshwe kuwa nimemuua mtu ambaye hata hahusiki na yote yanayotokea, nikajiathidi nisikumbuke lakini..

`Mhasibu kuna mgeni wako....’nikaambiwa

‘Ni nani?’ nikauliza nikiwa na hamasa , hasa ya kujua majaliwa yangu.

‘Utamjua ukifika huko...’nikaambiwa na huyo askari, na mimi kwa haraka nikatoka hadi sehemu ya wageni, na nilipofika hapo, nilimuona mtu kakaa kwenye kiti, lakini alikuwa kanipa mgongo, sehemu kubwa ya chini ilifunikwa na meza, alikuwa ni mwanamke, kwa pale alipokaa sikuweza kumuona vyema, hadi nilipomkaribia,na nilipofika karibu yake akageuka;

‘Oh ni wewe!, umefuata nini huku?’ nikauliza kwa mshangao, huku nimeduwaa, na huyo mgani akasema;

‘Ina maana ulitaka nisije,na kwanini hukutaka kuniambia kuwa umefungwa kwa kesi ya mauaji?’ akauliza

‘Mimi sijaua...’nikasema nikiwa bado nimesimama mbali nay eye, utafikiri namuogopa, na yeye akiwa kageuza kichwa, halafu akaendelea kuangalia mbele, kwahiyo nikawa namuangalia kwa pembeni. Nikasogea hadi pale alipokaa, na yeye alipohisi nipo karibu yake akasema;

‘Mimi sijui kama umeua au la, lakini kwa namna moja au nyingine unahusika,wasingakukamata kama hukuhusika japo kuwa karibu na tukio....niambie ukweli kuna nini kilitokea hadi kufikia huko?’ akaniuliza

‘Ni bahati mbaya ilitokea tu, ni kwamba siku hiyo nilikuwa kwenye tukio,tulikwenda kumuona mgonjwa, na tukiwa hapo, ndio hayo mauaji yakatokea, na wakati yanatokea mimi nilishatoka nje, kwahiyo hata sijui yalitokeaje...’nikasema

‘Huyo mgonjwa ni nani?’ akauliza kwa haraka

‘Ni mfanyakazi mwenzetu...’nikasema

‘Ni mwanamke au?’ akauliza tena kwa haraka

‘Ndio ni mwanamke...’nikasema nikijua jibu hilo litaleta dhana mbaya, hata hivyo nisingeliweza kumdanganya hapo, yeye akageuka na kuniangalia usoni na kusema;

‘Unaonaeeh, kumbe ni kweli,...mhh, nimeamini sasa, watu walikuwa wakiniambia mengi nikawa nayapuuzia, sasa nimesikia moja kwa moja kwenye kinywa chako,..’akasema

‘Wamekuambia nini hao watu, nilishakukanya kuwa usiwasikilie wambea, ukikaa kwenye makundi yenu mara nyingi kuna kudanganyana,....’nikasema

‘Walioniambia wala sio watu unaowafikiria wewe, ni watu wenye hekima zao tu, kuwa kuna mwanamke anakuzuzua, anakufanya husiki lolote,...nasikia hata kazi hazifanyiki vyema mbele ya huyo mwanamke, sijui kakupa nini...’akasema

‘Ni nani kakuambia hayo mbona sio kweli, usiwasikilize wambea hao, wafitinashaji wasiotutakia mema,,...hebu niambie ni nani kakuambia uwongo huo...?’ nikamuuliza nikijaribu kufanya kama nakasirika.

‘Ni nani kaniambi hilo sio muhimu kwa sasa, na kauli yako ichunge sana, unawatusi watu wazima, ambao wana heshima zao, na wasingelisema hilo kama hawana uhakika nalo,...mimi ninachotaka kwa sasa ni kusikia kauli yako ili nijue kuwa wewe ni mkweli au ni mwongo, na ukinidanganya, siku nikigundua,sitakuamini tena..je ni kweli au si kweli?’ akaniuliza

‘Ni kweli au si kweli kuhusu nini...?’ nikamuuliza

‘Kwani tulikuwa tunaongea nini, au nia yako ni kuleta ubishi wako , usio na msingi, hivi hata huo usomi wako, hakusaidii kitu...mimi nimekuuliza kuhusu huyo mwanamke, yupo au hayupo, ni kweli au si kweli, kuwa kuna mwanamke anayekuzuzua, hadi ushindwe kifanya kazi...?’ akaniuliza

‘Kama yupo ni wewe, hakuna zaidi yako....’nikasema na yeye akatabasamu na kuangalia pembeni , halafu akasema;

‘Nakuuliza tena hayo niliyoambiwa kuhusu huyo mwanamke ni kweli au si kweli?’ akageuka na kuniangalia akiwa kakunja uso kuashirikia kwa hataki utani.

‘Sio kweli, hakuna kitu kama hicho, ahadi yangu ipo pale pale, mimi nipo huku mjini kwa ajili ya kutafuta maisha yetu mimi na wewe, na haya yaliyonikuta ni katika harakati za kuhangaika, ...kumbuka nilivyokuambia, wewe ni mchumba wangu, hakuna mwingine anayeweza kuniingilia....’nikasema

‘Una uhakika na kauli yako hiyo?’ akaniuliza

‘Ndio nina uhakika.....kwanini unasema hivyo, una shaka gani na mimi, inakuwa kama vile kuna kitu umekigundua na unataka kuhakikisha,...kuna nini kinaendelea maana mpaka ufunge safari kuja huku, bila hata ya taarifa, nahisi kuna jambo?’nikamuuliza
‘Sikiliza , mimi nimepanga kuja hapa kukuambia ukweli, kuwa kama kuna lolote linaendelea kati yako na huyo mwanamke, nijue mapema, nisiendelea kuumia, kwani nimeshaumia vya kutosha, nimevumilia vya kutosha,...’akasema

‘Hakuna ukweli hapo.....’nikasema na yeye akanikatisha na kuendelea kuongea;

‘Ukweli upo, ila huwezi kuukubali,..sasa nakuambia ukweli, kuwa nikija kugundua, niliyoyasikia, kuwa ni kweli,nitakachokifanya ujue wewe ndio sababu,...ukumbuke kuwa, umeniharibia mipangilio yangu yangu, nilitakiwa na mimi niwe nasoma vyuoni kama wenzangu, ...ningelikwua na kazi nzuri, ukanikatishia ndoto yangu....’niliona machozi yakimtoka,

‘Lakini tulishaongea hayo, kwanini unazidi kujisononesha...’nikamwambia.

‘Mimi nimeganda huko kijijini, unafahamu sheria za baba, kosa nililolifanya limekuwa kisingizio kwa kila kitu, sina haki tena ya kufanya lolote, haya ni kutokana na wewe, nimeganda huko kijijini nikikusubiri wewe, na wewe umewapa ahadi wazazi wangu kuwa tutafunga ndoa hivi karibu, je hiyo ndoa tutafunga huko jela, ukienda kufungwa, ndoa itafungiwa wapi, hivi mtoto wako atakuwa na raha,akisikia baba yake ni mhalifu, hivi hilo wewe hulifikirii... ...’akasema akionyesha uso wa huzuni.

‘Lakini mimi sio mhalafu..’nikajitetea

‘Sio mhalfu, ungelikuwa sehemu kama hii, ..mimi naona hata aibu, kusikia hayo ninayoyasikia, na sasa ndio hivyo tena, unashutumiwa kwa mauaji,...yote mambo mabaya mabaya,...kwakweli sitafurahia, watoto wetu wayasikie haya...no bora nisiwepo kabisa...’akasema

‘Mpenzi wangu mbona unasema hivyo, usije ukafanya jambo baya, tafadhali...usije ukawafanya mtoto awe mkiwa, ajisikie vibaya,...oh, mbona unanitisha, nimeota ndoto mbaya, na wewe unongea hayo hayo...hapana, nakuomba, ...tafadhali, uniamini mimi...sijafanya hayo wananisingizia tu....’nikasema nikijaribu kumshika begani, akaondoa mikono yangu, na kujisogeza mbali na mimi.

‘Sikia kauli yangu...iliyonifanya nije hapa,kama wewe unasema umeota, basi mimi karibu kial siku naota ndoto mbaya, kukuhusu wewe,.... kama umeota ndoto mimi nafanya jambo, basi ujua ni kweli, sitanii,mimi nitafanya kweli....nimekuja hapa kuhakikisha mwenyewe...’akasema na kusimama.

‘Mimi naondoka, nimefikia kwa shangazi ,nilikuja jana,nikaambiwa upo na mazungumzo, nikaulizia, kuhusu kesi yako,nimeshaambiwa kuwa unashughulikuwa dhamana yako,...kwa vile hatujafunga ndoa mimi na wewe,siwezi kwenda huko kwako, nitakuwa huko kwa shangazi yangu,....’akasema

‘Shangazi yako yupi huyo, anaishi wapi hapa mjini...?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi, huku moyoni nikisema kumbe ana ndugu yake anaishi huku, basi atakuwa ndio yeye kapeleka umbea huko kijijini

‘Karibu na hiyo hoteli kubwa ya kajificheni...’akasema

‘Oh,...kuna ndugu yenu hapo karibu na hiyo hoteli mbona simfahamu, yupoje, mbona hatujawahi kukutana naye, ananifahamu mimi..?’ nikasema nikionyesha wasiwasi...

‘Anakufahamu sana...’akasema na kunifanya niangalia chini, na yeye akawa anaondoka, huku akisema;

‘Ndio hivyo, sitakaa sana, nilikuja kukupa pole, na kutokana na hali niliyoiacha huko nyumbani siwezi kuendelea kusubiria hapa, sitakaa sana, kesho au keshkutwa naondoka, japokuwa sijajua ukweli wa jambo lenyewe na ni nini...’akasema na kugeuka kuniangalia.

‘Na baya zaidi, sijui  hatima yako itakuwaje, maana kesi za mauaji haziishi leo au kesho, lakini hata hivyo, nitajua kwa kupitia kwa baba, ili nione mambo yamekwendaje, baba kasema ni kesi ngumu sana, maana hata kama hukuhusika kwa hayo mauaji, lakini inaonekana kama umjichanganya na makundi haramu,...hebu niambie ni kundi gani hilo ulilojichanganya nalo?’ akauliza

‘Hakuna kitu kama hicho, mimi sijajichanganya kwenye kundi lolote, nasikia tu kwa watu, kuwa kuna makundi haramu, ....hili tukio limenikuta tu, kwa vile nilikuwepo siku hiyo, kwa huyo mgonjwa, lakini mimi nina imani kuwa yatakwisha tu....’nikasema

‘Au ndio huyo mwanamke kakuingiza kwenye makundi mabaya...?’ akauliza

‘Mwanamke, ....mwanamke yupi, unayemuongolea,....una maana huyo mfanyakazi mwenzetu, au..’? nikamuuliza nikiwa na mashaka, maana aliponiambia kuna shangazi yake hapa akribuni, kanifanya nisijiamini tena.

‘Unamfahamu sana...’akasema

‘Hapana kama ni huyo, sio kweli, huyo ni mfanyakazi mwenzetu, na kama yupo kwenye hayo makundi mimi sijui, na sizani, sio kweli...hata hivyo, ni nani huyo kakudanganya..hivi mimi unanionaje, kuwa ni mwepesi kughilibiwa, eeh,... usisikilize maneno ya watu, yasiyokuwa na ukweli...!’ nikamwambia huku kicjhwani nikiwaza mbali sana.

‘Lisemwalo lipo, kama halipo lisingelisemwa, ...nyie wanaume mnatufanya sisi wanawake hatujui mnayoyafanya, mnasahau kuwa hao mnaofanya nao ni wanawake kama sisi,kama ni wanawake, mnaofanya nao, nabado mnaona wao hawajui, hamuoni kuwa mnajidanganya wenyewe, msitufanye wajinga wakati ujinga mumeuanzisha nyie...’akasema

‘Hayo ni maneno yako, na mara nyingi ni ya kusikia, na kiukweli sio sahihi, ukiyachukulia juu juu, utajiumiza mwenyewe, achana nayo niamini mimi, ninayekuambia....’nikasema

‘Haya....za mwizi ni arubaini, ipo siku nitayajua tu, na ni bora uniambie ukweli sasa hivi, kuwa ilitokea bahati mbaya, ulilewa ukapitiwa,  ...kuliko nije kufahamu baadaye, na iwe ni kweli,...kwakweli, ninavyoota ndoto mbaya, sijui nitakalolifanya, maana nimeumia sana, na sitapenda kuendelea kuteseka tena, lolote nitakalolifanya ujue ni wewe....na hata baba nimemwambia, nimechoka na kusimangwa...’akasema na kuinuka kuondoka

‘Lakini tulishakubaliana, tukayamaliza hayo, wanaokusimanga mwisho wake watachoka, wewe kaa na msimamo wako ukijua mimi nipo kwa ajili yako,...usidanganyoke na maneno ya watu, niamini mimi...unataka nikuambieje...’nikamwambia na yeye akawa akibenua mdomo wa kuzarau hayo maneno yangu.

‘Sikiliza nikuambie, usije kufanya jambo lolote la kujiathiri, kwa kitu ambacho hakipo, ho watu ni...waongo, wafitina, nakuomba tena sana, maana sasa unanitosha.....’nikasema huku ile taswira ya ile ndoto ikawa inanijia akilini na kujawa na wasiwasi, kuwa huenda ile ndoto ilikuwa na ujumbe fulani ambao unaweza kuwa ni kweli, ....oh,sasa nifanya nini na mimi nipo jela...

‘Mungu naomba isiwe hivyo, ...naomba isiwe hivyo, sio kweli ile ilikuwa ni ndoto tu....’nikawa nimeinama nikiwaza kwa muda, mrefu, hata sikujua nimekaa pale kwa muda gani, hadi nilipohisi mtu akinishika mgongoni, nikainua kichwa nikijua ni huyo mchumba wangu karudi tena, nikaanza kusema;

‘Nakupenda mchumba wangu tafadhali usifa....’nikakatiza maneno pale uso wangu ulipokutana na sura ya mtu mwingine, aliyenifanya moyo wangu uwe kama umelipuka,kwa kimuhe muhe, nikahisi akili ikibadilika..nikujikuta nikisema kwa kigugumizi..

‘Ume..mu..oona,....’nikasema kwa kigugumizi, huku nikiangalia mlangoni.

‘Nimemuona nani wewe, mimi nimekuja kukuchukua mwenyewe, dhamana yako imakubaliwa....na nataka tukitoka hapa tupitie kwenye hiyo hoteli ya kajificheni tujipongeze...’ilikuwa sauti ya Mdada.

NB : Nilikwanza kidogo na malaria, na walionipa pole na kuniombea dua nawashukuru sana, tupo pamoja.


WAZO LA LEO: Ni rahisi sana kumshutumu mwenzako ubaya, na hata kujirizisha kuwa upo sahihi kwa shutuma japokuwa na wewe ni mkosaji mkubwa, lakini inakuwa vigumu sana, kujishutumu wewe mwenyewe, na kuwa mkali ukikosolewa, au kushutumiwa, hata kama tunajijua kuwa tuna makosa.

Ni vyema tukajenga tabia ya kukosoana tukifanya yasio sahihi, lakini kwa mtizamo wa kujiangalia nafsi zetu kwanza, kwani sisi sote ni wakosaji, hakuna aliyemkamilifu.
Ni mimi: emu-three

No comments :