Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, March 24, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-32
Wakati mpelelezi wa kesi yangu akiondoka, na muda huo huo, wakili aliyependekezwa na mdada naye akawa anaingia, na mpelelezi akaniambia, kuwa sijampa taarifa ta kazi aliyonipa, kichwani nilibakia nikiwaza ni kazi gani aliyonipa, na kabla sijapata jibu, wakili pendekezo la mdada akawa ameshafika, na kuniambia;

‘Mdada anasema hivi, huhitaji wakili mwingine,...huyu wakili wako hakufai, uachane naye, vinginevyo, ....’akaanza kuongea kabla hatujasalimiana

‘Vinginevyo nini...?’ nikajiuliza kichwani, sikumuuliza yeye, nilibakia kimiya, nikimsubiria yeye anataka kusema nini, na alipoona nipo kimiya akasema;

‘Mdada kanituma kuwa mimi ndiye nitakayekuwa wakili wako tu, ili tuweze kuyaweka mambo sawa,unakumbuka tumeshaandikiana mkataba na tayari nimewakilisha nyaraka zangu zote kwa wahusika kuwa mimi ndiye nitakuwa wakili wako ....’akasema

‘Sijakuelewa kwanini mfikie maamuzi hayo...unakumbuka mara ya mwisho kuonana na wewe nilikuambia nini, kuwa wewe utashirikiana na wakili mwingine,...sasa kwanini mnachukua maamuzi wenyewe, bila hata kunishirikisha...?’ nikamuuliza

‘Mimi ni wakili na kazi yangu ni kufanya anavyotaka mteja wangu, na mtu aliyenifuata kuwa anahitaji wakili ni mdada, kwahiyo namsikiliza yeye, na kwa vile tunafahamu wewe uko sehemu kama hizi, hutakuwa na nafasi ya kufuatilia, .....usijali ndugu...’akasema

‘Sijawaelewa kabisa mnafahamu huyu wakili mwingine kafanya nini kwangu, tangu asubuhi tupo na wakili huyu mwingine akihangaika kunitetea, ..leo hii mnakuja na taarifa kuwa hatakiwi, mnataka mimi nimwambie vipi,...kuwa yeye hatakiwi tena, wakati nimeshaingia mkataba naye, na unafahamu ni gharama kubwa kuvunja mkataka,.. hata hivyo kwasababu gani za msingi?’ nikauliza.

‘Mkataba gani mlioingia naye,hajawakilisha chochote kwa msajili wa kesi hii, na  sizani kama mumeshaandikishana lolote, sijaona hilo,....sikia haya ninayofanya ni kwa manufaa yako,tunahangaika kwa ajili yako, unatakiwa utilie sisi tufanya kazi hayo ya kuvunja mikataba, na gharama muachie mdada na mimi tutayaweka sawa....’akasema

‘Mimi sielewi kwanini ni lazima nimuondoe yeye, kwanini wewe usiondoke...?’ nikasema na yeye akaniangalia kwa sura ya kushangaa, halafu akasema kwa sauti ya kawaida sio ya kukasirika, inaonekana jamaa huyu hakasiriki haraka, au ndio mbinu zake za kikazi;

‘Sababu kubwa ni kuwa huyo wakili wako hajui kesi za mauaji zinakwenda vipi..kesi kama hizi zina mitihani yake, usizani polisi wao watakubali kirahisi tu kuwa hauhusiki, angali iliyotokea kwa mdada, hana kesi, ....kwanini, sio rahisi hivyo, sisi tunajua ni kitu gani cha kufanya...’akasema

‘Kwanini hana kesi wakati tulikuwa naye, wakati alama za vidole zipo kwenye hiyo bastola, wakati yeye inawezekana kabisa huenda alipochanganyikiwa ndiye aliyemuua huyo mtu...msitake niseme sana...’nikasema na yeye kama kawaida yake akasema;

‘Fikira za watu na jinsi wanavyohisi ni tofauti na ushahidi uliopo,...hata hivyo, hilo halikuhusu kinachotakiwa kwa sasa ni kuangalia jinsi gani na wewe utaondokana na kesi hii, maana inavyoonekana wewe ndiye muhusika mkuu....’akasema

‘Ina maana mumehamisha kesi ya Mdada kwangu mimi nionekane niye muuaji, no way...nawaambia hivi hili sitakubali, mkitaka nianza kuropoka ovyo, fanyeni hivyo...’nikasema kwa hasira.

‘Nikuambie kitu, uwe makini katika kauli zako,..unasikia, na ni muhimu ukaliweka hilo kwenye akili kuwa mimi kama wakili ndiye ninayebeba dhamana yako, kuhakikisha kuwa kesi hii inakwisha, kwa vipi, hilo niachie mimi...nimeshamaliza kwa mdada, ...sasa nakuja kwako, ...’akasema na mimi nikakaa kimiya nikiwaza

Inawezekana huyu jamaa ni jembe, amewezaje kumaliza hii kesi kwa mdada, hata haijafikishwa mahakamani, anadai mdada hana kesi tena,....oh, kweli, hebu nimsikilize nisije nikajifanya mjanja nikaozea jela, kwanza mimi nitapungukiwa na nini, awe yeye ni wakili wangu au huyo mwingine,..mimi sitoi pesa yoyote...oh, ngoja nisubiri.

Wakali huyo akawa keshatoa makabrasha yake na kila mara alikuwa akinitupia jicho, na mimi nikawa kimiya nikiwaza, halafu nikasema;

‘Ina maana kweli mdada hana kesi tena,ajabu kabisa...’nikajikuta nasema kwa sauti, na jamaa akaniangalia halafu akatabasamu, na kusema;

‘Huamini eeh, ...hahaha, ndio maana mdada akanitafuta mimi, ....utaamini hapo kesho ukiona upo nje kwa dhamana, ...japokuwa kuimaliza kesi yako kwa sasa ni vigumu, maana muuaji hasa hajapatikana, na wewe ili uachiwe huru, ni mpaka mu-uaji apatikane, na hiyo ni kazi ya polisi, sio mimi....unaonaeeh, ....’akasema sasa akitulia kwenye kiti.

‘Lakini mimi sioni ubaya huyo wakili mwingine akiendelea kuwepo, ili wewe ukihangaika upande mwingine na yeye anahangaika upande mwingine, ukumbuke huyo ni wakili wa kampuni yangu, ana haki ya kujua ni nini kinachoendelea...’nikasema

‘Nimekuambiaje kwanza huyo wakili hana uzoefu na kesi na za mauaji,..kesi hii haiendeshwi kama kesi za ofisini,..ina mitego yake, na ukiijulia, huwezi kunaswa, nikuambie ukweli, mimi nawafahamu hawa maaskari wetu na udhaifu wao....labda wamlete askari mgeni ambaye simfahamu,lakini kama ni hawa hawa ambao ninao kila siku..kesi hii itaisha kienyeji tu...’akasema

‘Pili kutokana na kauli ya Mdada nyie wawili,mna mambo yenu....’akasema na kuniangalia na nikataka kumuuliza mambo gani, kabla sijamuuliza hivyo akasema;

‘Aaah, hayo mambo yenu, mnajuana wenyewe, kasema siyo ya kumueleza kila mtu, hata mimi mengine siyafahamu lakin kuna muda inawezakana nikahitajika kuyafahamu baadhi ili niweze kufunika kombe mwanaharamu apite,....sasa ni bora kama ni mambo yenu ya siri, yakajulikana na watu wachache tu wanaoaminika,...’akasema

‘Mambo gani tena hayo anayosema mdada, mbona sina mambo yoyote na yeye, cha muhimu ni hii kesi, sizani kama kuna mambo mengine yanayohusiana na hii kesi,...sikumbuki, unajua mdada ana mambo mengi, asije akanitumbukiza kwenye mambo yake, na kusema nahusika, hapana hilo sikubali, eti nikuulize ni mbona gani hayo anayosema mdada...?’ nikauliza

‘Mnafahamiana wenyewe, mimi sijui, kama unayahitaji, basi,muulize Mdada...kama kuna umuhimu huo, ...lakini tusipoteze muda kwa hilo, hilo sio muhimu kwa sasa....’akasema

‘Lakini kama sio muhimu, kwanini ukaligusia, nina haki ya kufahamu ni mambo gani ambayo mdada anasema ni ya siri, ....’nikasema

‘Kama unahitaji hivyo, basi, mtakaa na mdada, mtaongea naye atakueleza, kama nilivyokuambia hata mimi mengine siyafahamu, ila nafahamu jinsi gani tutaimaliza hii kesi,...’akasema

‘Kwakweli mnanichanganya, hata sielewi, ..napelekwa kama bendera...’nikajikuta nikisema.

‘Huenda kama hivyo, basi ukitoka kesho, mtapanga mkutane na mdada, ili akuelezee lengo na nia yake ni nini, lakini kwanza cha muhimu, kabla ya yote ni wewe ukubaliane na huo uamuzi wa wewe kuwa na wakili mmoja ambaye ni mimi,.....ili tumalize hii kesi tuendelee na mambo mengine..’akasema

‘Mimi bado sijaelewa kwani hujanipa sababu ya msingi, siwezi kumwambia wakili ambaye ananihangaikia siku ya ngapi sasa, ...hivi nyie mnafahamu, kafanya nini leo, kapambana na huyo mpelelezi ....’nikasema

‘Kapambana nini bhana, kafanya nini na huyo mpelelezi! ....acha maneno matupu, hivi unafikiri dunia ya leo utaongea maneno matupu tu, ueleweka, siku hizi kinachoongea ni ....’akaonyeshea kwa vidole, kuashiria `pesa’ na mimi nikajitahidi kutabasamu, akaendelea kusema;

‘Nikuambie ukweli, hata kama kaongea na kuweka mistari ya sheria ya kuona kuwa huna hatia, lakini kama hajawarizisha hawa watu wenye njaa zao,...hujafanikiwa kitu, ....hawa watu hawa, wanatoka nyumbani hawajui familia yao itakula nini, wengine wamebakiza miezi michache tu wastaafu, hawana hata kibanda cha kuishi, ukimwambia nitakujengea nyumba, ..unafikiri atasema nini...akili ni mali....’akasema na kushika kichwa.

‘Una maana una...ho-nga....’nikasema

‘Hamna kitu kama hicho Tanzania, huwezi kumhonga mtu, unasikia hicho kibwagauzi kuwa rushwa ni adui wa haki...mpokea na mtoaji wote wana makosa au sio, kwahiyo hakuna mtu anayetoa au kupokea rushwa, ...’akasema

‘Sijakuelewa....’nikasema

‘Tunachofanya ni kusaidiana...huyu ana shida, anataka kuweka mambo yake sawa, huyo ana family problems, anahitaji ada za watoto, yule anataka kujiandaa kustaafu, na wewe una shida zako, unataka utoke ukaifukizie shilingi, tufanyeje hapo,...tunasaidiana, ...ili haki itendeke, ndio kazi yetu ndugu....’akasema akionyesha uso wa kutabasamu au kunisanifu.

‘Mhh, hiyo kali...hata nyie, ...’nikasema.

‘Sasa nikuambi  ukweli huyo wakili wako unayesema kafanya kazi toka asubuhi, hajafanya lolote, sana sana ni kuwapotezea maaskari wa watu muda wao, hakuna lolote alilolifanya, mimi nimeshaongea na mkuu wa kituo, kanielewa...’akatulia na kuangalia saa yake, hakuwa na wasiwasi, akasema;

‘Kwanza huyo mzee wa watu anataka kwenda likizo, akaweke mambo yake sawa, unafahamu anahitaji kustaafu mwakani,kapigika kweli, miaka nenda rudi, anajitolea yeye na ofisi, muda wa kustaafu umefika hana hata kakibanda utamuonea huruma, jamani, kwanini wanawafanyia hivi hawa watu...’akasema na kutulia

‘Nikuambia ukweli, watu wema, wanaojitolea na kutenda yaliyo haki, katika nchi hii ndio wanabakia kuwa masikini,....mshahara hauna tija, hauwasaidii lolote, ...kama mtu akijifanya hana njia nyingine ya kipato, akala mezani kwake, ataambulia kustaafu, huku anawaza kama ningelijua..kama ungelijua wakati upon je ya ofisi, wanasubiri ufe ndio wakulipe hicho kinachoitwa kinua mgongo, ...hakuna kitu hapo...’akasema na kufunua funua makabrsha yake.

‘Anyway, tuaacha hayo watu husema kufa-kufaana, au sio, niliweza kwenda kuongea na mkuu huyo,...na alipoisoma hii kesi, kaona kabisa ni kesi ya kubambikiwa, ...haina mshiko,mzee huyu ana uzoefu wa siku nyingi, kagundua kabisa kuwa kuna watu wamecheza mchezo mchafu,....haoni kwanini usipate dhamana, ni mtu mnzuri sana yule mzee, ..., kesho dhamani inatolewa, lakini hata hivyo kwa masharti...’akasema huku akigonga gonga kwa vidole kwenye meza.

‘Masharti gani hayo?’ nikauliza nikiwa na mashaka, maana huyu mtu anaonekana kuwepa pesa mbele, kutokana na maelezo yake, sio mtu wa pesa ndogo, sijui mdada anatakuwa kamlipa shilingi ngapi.

‘Kwanza ukubali kuwa mimi ndiye nitakuwa wakili wako pekee, na mengine yatafuata baadaye, ukishakubaliana na hili ambalo ni muhimu sana, kwa mustakabali wa maisha yako ya baadaye, basi mengine niachie mimi na mdada...’akasema

‘Mimi naona ni bora niendelee na wakili huyo, kwani kateuliwa na kampuni, ..naona kuna muelekeo mwema, lakini sio nyie,...nikimkataa ajira yangu inaweza kuwa hati hati, kuna leo na kesho.’nikasema na yeye akaniangalia kama haamini anachokisikia, akatabasamu na kugeuka kuangalia huku na kule, halafu akasimama na kutulia kwa muda

‘Akachukua simu yake, na kuanza kupiga namba, halafu akasema;

‘Naona hujanielewa, labda nifanye hivi...’akasema huku akiweka simu sikioni, halafu akasema kwa sauti ndogo;

‘Yah, ni mimi, hebu ongea na mtu wako anaonekana hajaelewa, sina muda wa kupoteza hapa....’akasema na mara akanikabidhi simu, na sauti ya Mdada ikasikika ikisema;

‘Unasema nini, hebu nipe niongee naye...’akasema na mimi nikawa nimeshaiweka simu sikioni mwangu, na kusema;

‘Unasemaje mdada...’nikasema kwa sauti iliyochoka

‘Hivi wewe unataka nini, unafurahi kukaa hapo rumande na kesho ulitakiwa kwenda gerezani unalifahamu hilo, tumehangaika leo kutwa hadi kwenda kwa mkuu wa kituo, tumemsomesha mpaka ameelewa, na zote ni juhudi za huyo wakili, sasa unasema humtaki huyo wakili, unataka nini, unataka ukawe mke wa wafungwa, hebu amuka mwanaume wewe,....’akasema kwa sauti isiyo ya ukali

‘Sasa sikiliza hapo una mawili umkubali huyo wakili, ambalo huna jinsi labda kama umechoka kuishi,..ukifanya hivyo kesho dhamana ipo wazi, hutaenda gerezani utakuwa raia japokuwa kesi ipo mbele yatu, ama umkate huyo wakili, ukashikane na huyo wakili wa kampuni ambaye yupo nje, analala na mke wake, ....wewe utakwenda kunyea ndoo, sijui na mengine ya huko, na ukumbuke kabisa nakupa kama tahadhari....’akatulia kidogo

‘Tahadhari gani?’ nikauliza

‘Kama ukienda huko gerezani, sizani kama utarudi,...sijui,...’akasema

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Masikini mhasibu....oho,..kwanini kwanini....’akasema kwa sauti ya kunioenea huruma.

‘Lakini mbona unakuwa kama unanilazimishia kwenye jambo nisilolielewa, kuna nini mdada, ...hivi kweli una nia njema na mimi,...’nikasema

‘Kama nisingelikuwa na nia njema na wewe ningeliacha ukafungwe, na hata kunyongwa, ....wewe ndiye unayejulikana kwa sasa kuwa umemuua huyo mtoza ushuru, wana ushahidi wa kutosha, kama hujaambiwa uelewe hivyo,...’akasema

‘Kwa ushahidi gani, ?’ nikauliza

‘Mhh, unataka uone huo ushahidi eeh, subiri ukifika mahakamani utauona, nakuambia ukweli, ukikanyaga kile kizimba, bila ya msaaa ya huyo wakili wetu, unakwenda kufa jela, kifungo cha maisha ya kuua bila kukusudia....’akasema

‘Haiwezekani, lakini mimi sijafanya hivyo, watakuwa wananionea bure, hata wewe unafahamu, kwanini wasikuchukue wewe...’nikaanza kuongea na yeye akanikatiza na kusema

‘Silly boy,....shut-up...sikiliza kwa hali ilivyo wewe kwasasa huna ujanja hapo, ni bora utoke nje, ukajue jinsi gani ya kujitetea kuliko kukaa huko ndani,watakuharibu akili zao kwa maneno ya kujifanya wanakujali, kumbe lengo lao ni kutafuta vyeo,...nakuhurumia sana, hasa afya yako, na maisha yako ya baadaye.....’akasema

‘Na nikuambie ukweli, kama utaenda gerezani kama mahabusu, kuna watu wameshawekwa wa kukumaliza, wanaona wewe ni mzigo , wewe ni tatizo wanahisi umeingilia anga za watu, wenye mirija yao ya pesa, na kinachowashangaza ni wewe kujihusisha kwenye mambo yao, wanahisi unafahamu mengi....huenda wewe ni shushu...’akasema

‘Watu gani hao...mbona sikuelewi, mbona wewe ndiye chanzo ya yote haya?’ nikauliza nikilalamika

‘Haina haja ya kuwafahamu,hata mimi siwafahamu,....cha muhimu ni kusikiliza ninachokuambia,..ili usipoteze muda wako, muda ni muhimu sana haukungoji, unahitajika kujijenga, nyumba yako ya huko kijijini inakusubiri, na mchumba ndio huyo, nasikia kaja juu, sijui...sasa akiona huo upuuzi wako, na kusikia upo jela, unafikiri atachukua hatua gani,....nasikia alishapeleka kesi ya kubakwa...mliimaliza kienyeji, sasa anakwenda kuifufua,..unaona ilivyo....’akasema

‘Hebu achana na mambo yangu...mchumba wangu anahusika vipi, na tafadhali usimwambie lolote, kuwa nimeshikwa, unasikia mdada...’nikasema

‘Nisimwambie, wakati baba yake anafahamu..hahaha. unalo hilo, ..sasa unasemaje?’ 
akauliza

‘Lakini mdada huyu wakili mwingine keshaanza....’nikataka kusema

‘Mimi sitaki kusikia kuhusu huyo wakili mwingine, huyo mtu hataweza kufanya lolote kwenye hii kesi, namfahamu sana, kwanini hunisikilizi mimi, .....niliamua uachane naye kwa vile ni wakili wa maswala ya kiofisini hana uzoefu na kesi za mauaji, ...’akasema kwa haraka.

‘Mbona anafahamu sana,wewe hujui tu, huyo kesi kama hizo ndio fani yake, lakini hakutaka kujishughulisha nayo, kwasababu zake za kifamilia, lakini kasema yupo tayari kunisaidia kwenye hii kesi, ndio nikaona ili kesi hii imalizike mapema, nitawachukua wote wawili, sio tatizo hapo lipo wapi,...’nikasema

‘Kwahiyo wewe unasema na upo tayari huyo wakili aone uchafu wako uliowahi kuufanya, na ukumbuke huyo ni wakili wa kazini, kwahiyo hayo machafu yako yatajulikana hadi kazini, upo tayari kwa hilo..?’ akaniuliza

‘Uchafu gani unaoongelea unaohusikiana na hii kesi?’ nikamuuliza

‘Unaniuliza nikukumbushe,unataka nikukumbushe, ok, ok....oh, tatizo hiyo simu uliyo nayo hapo sio ya kwako, lakini ukinilizamisha naweza kufanya hivyo,.....kama upo tayari basi nitamtumia uchafu wako huyo wakili akuonyeshe, upo tayari,, ...’akasema

‘Mdada mbona unachanganya mambo, ...huu sio mda wa kutishana na mambo hayo, mimi hapa nilipo sijui hatima yangu ni ipi, umekuwa ukiniingiza kwenye mambo nisiyoyaelewa, unataka nini kwangu...’nikasema kwa kulalamika

‘Ndio maana nikamtafuta mtu ambaye namfahamu, anajua ni nini kinatakiwa kifanyike kwa wakati kama huu, bila kuathiri mambo mengine,....nisikilize  kwa makini, umeshafua nguo huna budi kuyaoga hayo maji, ...huna ujanja,..., kuanzia sasa wakili wako ndio huyo, huyo wakili wa kampuni achana naye.....’akasema

‘Mhh, hata sijui nifanye nini...’nikasema

‘Masikini mhasibu, hata hujui ufanye nini, ...sasa ama hujui ufanya nini , mimi nitakuoneyesha ni nini cha kufanya, ...kwanza kama huwezi kumweleza huyo wakili wa kampuni kuwa hatakiwi, niachie mimi nitaongea naye..’akasema

‘Hapana, nitaongea naye mimi mwenyewe.....’nikasema

‘Masikini mhasibu, pole sana...ok, tumelewana hadi hapo, haya hilo la kimueleza nakuachia wewe, kesho utapata dhamana yako, na tutaanza kuangalia mambo mengine, na ujue kuanzia sasa sitaki kusikia mambo yoyote kuhusu huyo wakili wa kampuni, unasikia ...’akasema na kutulia

‘Pili kuanzia sasa wewe ni mtu wangu, sitaki kabisa kusikia mambo ya uchumba wako na mchumba wako, ...sasa hivi wewe utanisikiliza mimi,umenielewa, mhh, masikini mhasibu, mbona unakuwa kama sio mwanaume...’akasema kama mzaha, hakujua jinsi gani nilivyokuwa najiskia vibaya, nilishaanza kumuhisi vibaya mdada, na nikawa najaribu kumtoa rohoni, lakini..oh, sijui kanipa nini...

‘Sawa....nimechoka na kashifa zako....’nikasema na kumkabidhi huyo wakili simu, na  yeye akaipokea huku ananiangalia machoni, na alipoipokea akaiweka sikioni huku bado anaendelea kuniangalia akawa sasa anangea na mdada, halafu akageuka na kuniambia;

‘Unasikia, sasa naenda kumalizia mambo, nisainie hii karatasi, ya makubaliano, sitaki tena kusikia kuhusu huyo wakili wako mwingine, kuna mambo kidogo naenda kuyamaliza kuhusu hii dhamana yako.’akasema na kunipa karatasi, nikasaini hata bila kuangalia kumeandikwa nini.

‘Safi, sasa tupo pamoja, nikitoka huko kwa maswala ay dhamana, nitakwenda kuonana  na yule mpelelezi anayechunguza hii kesi, anaonekana kichwa ngumu haelewi , ndio hao hao, watakazeekea ofisini, na kujikuta hawana hata kibanda ya kufia,...nimeshaongea naye, lakini kuna mambo hatujakubaliana, na haya yote nahisi yanataka msukumo....’akasema

‘Msukumo gani, una maanani pesa zinahitajika,..?’ nikamuliza

‘Ndio maana unatakiwa umsikilize mdada,...nikuambie ukweli bila kufanya hivyo, huwezi kutoka kwenye hii kesi, wenzako wana ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa ulihusika, na wewe ndiye uliyemuua huyo mtoza ushuru,....unaona hapo, wewe utajikinga vipi kwa hilo, bastola ina alama zako za vidole, ......’akasema na kuangalia saa yake.

‘Sawa, mimi nawasikiliza nyie, lakini ninawaonya, kama.....mna ajenda nyingine dhidi yangu....’nikasema na kutulia, sikusema zaidi, na yeye akaniangalia, akasimama na kunyosha mkono, kuniaga,na kusema;

‘Usijali, ..hii ni kesi ndogo sanai, ....wewe utaona vumbi langu kuanzia kesho..’akasema na kuondoka zake.

********

Wewe utaona vumbi langu...

Kesho yake, sikuonana na wakili yoyote asubuhi na wala mchana, na nikaona ikifika jioni huenda nikasafirishwa wenda gerezani, ...lakini ilipofika jioni, akafika yule askari mpelelezi, akasema anataka kuongea na mimi

‘Siwezi kuongea na wewe bila kuwemo wakili wangu, unalifahamu hilo..’nikasema

‘Sikiliza hili ninalotaka kuongea na wewe ni kwa masilahi yako,....na kuhusu huyu wakili wako, mpya, uliyeamua kumchukua, ...’akasema

‘Wakili gani?’ nikauliza

‘Huyo wakili aliyekuchagulia mdada, hivi kweli, unamfahamu historia yake, utendaji kazi wake?’ akaniuliza

‘Si-sifahamu kwani vipi?’ nikauliza nikigugumia nikajua mambo sasa yameharibika

‘Huyu mtu ni miongoni mwa mawakili wanaotiliwa mashaka, katika utendaji wao,...inasadikiwa ana mambo yasiyotakiwa, huenda anashirikiana na makundi mabaya, yakiwemo ya biashara haramu,..hakujawahi kupatikana ushahidi dhidi yake, lakini,.....uwe makini naye’akasema

‘Kama unajua hivvyo kwanini huweki pingamizi, ili na mimi niweze kuachana naye?’ nikamuliza

‘Hiyo sio kazi yangu ila nakupa kama angalizo, akili kichwani mwako,...nimeifuatilia kesi yako, na nimegundua mambo mengi sana, na kama upo tayari kushirikiana nami, basi tutaweza kulimaliza hili na huenda tukaweza kulimaliza hili kundi....lakini...’akasema na kusita kuendelea

‘Kundi gani hili,...na kakini nini ?’ nikauliza

‘Kuna kundi limezuka hapa mjini, nia na makusudio yao, ni kuwatisha matajiri kwa kuwategea mambo mabaya, na kuyatumia mambo hayo kwa ajili ya kujipatia mali, ....ni aina ya blackmail...na tunahisi mdada yupo nyuma na hilo...’akasema

‘Huyu mdada niyamfahamu, hapana mnamsingizia,...hata hivyo, mimi sina uhakika na hilo..’nikasema huku nikiangalia chini.

‘Inawezekana ukawa mmoja wa wahanga wake, ndio maana unakubali kufanya kila anachokitaka, ....ufahamu kuwa hilo ni kosa kubwa, na ukigundulikana, utafungwa, na ukichanganya na hii kesi, sizani kama utaweza kuokoka, kirahisi...’akasema

‘Umeshaongea na mdada?’ nikamuuliza

‘Nimeshaongea naye mara nyingi tu....ni mjanja sana, dharau nyingi,, na baya zaidi hataki kushirikiana nami, hakubali kuongea na mimi moja kwa moja, anamuachia wakili wake...na wakili wake, ni ni hao hao...lakini hili tukio ndilo litawezesha kulisambaratisha hili kundi, ....ndio maana nataka kuongea na wewe...’akasema

‘Kuhusu nini, mimi sina cha kuongea...’nikasema

‘Sikiliza, mdada keshaongea na mkuu wa kituo na huenda ukapewa dhamana, lakini nakuonya kuwa kutoka kwako humu, huenda ikawa ni tiketi ya kutafuta kifo chako, nimechunguza na kugundua kuwa hao watu wanataka kukumaliza, kwa vile wanahisi unafahamu mengi kuhusu kundi lako,...’akasema

‘Kundi gani gani , mbona kila mara unanielezea kuhudu kundi...mimi sina ufahamu wowote kuhusu hilo kundi...’nikasema

‘Kundi hilo, limejengwa na watu mashuhuri tu, lina mawakala kila sehemu nyeti, zikiwemo sehemu hizi za usalama, huwezi amini hata mimi siwaamini watu ninaofanya kazi nao, ...ndio maana nataka tuwe kitu kimoja, ujitolee kwa ajili ya taifa lako...’akasema

‘Kwa vipi...?’ nikamuuliza

‘Nitakuelezea, ...na kabla ya hilo, nataka nifanye juhudi usitoke kwanza humu ndani, nataka niweke pingamizi usipate dhamana...’akasema

‘Mhh, mbona sikuelewi,....’nikasema

‘Tutaongea kesho, ngoja nione jinsi ya kufanya, ...nakuacha ulifikirie hili, na ili tuweze kufanikiwa unatakiwa uniamini, na uwe tayari kuniambia kila kitu, hasa kumuhusu mdada...kila kitu unachojua kuhusu yeye ...na hata kama kuna kitu kawahi kukufanyia , wewe unatakiwa uniambie...kwa ajili ya kulimaliza hili kundi....’akasema .

‘Aaah, hakuna kitu alichowahi kunifanyia, hata hivyo...’nikataka kusema jambo lakini nikasita yeye akasema

‘Usijali, nafahamu ni kwanini, bado hujajiamini, hata mimi imefika hatua simuamini mtu, namuona kama kila mtu anahusika,....lakini hakuna jinsi, inabidi lifanyike jambo, na nahisi muda wa kulifanya umefika,...’akasema

Na baadaye akaondoka, na kuniacha nikiwa hata sijui nifanye nini..nikajikuta nikisema mwenyewe;

‘Masikini mimi,....mmh, masikini mhasibu

NB: Ndio hivyo tena, sijui nyie mwasemaje


WAZO LA LEO: Ukweli na haki, ni daraja la juu la mtu muadilifu, na ni ngumu sana kufikia daraja hilo, kama utafikia hatua hiyo ya kuwa wewe ni  mkweli kwa kauli na vitendo, na unayofanya ni ya haki tupu, basi wewe utakuwa kwenye daraja kubwa la mtu muadilifu na mwaminifu. Ni nani ana uwezo huo?...Tusidanganyane, kila mtu nafsi inamsuta, ...

Kama ni hivyo,basi tukubali kuwa yote tunayopata ni kutokana na huruma na neema za aliyetuumba, kwahiyo basi,inatubidi tumshukuru sana muumba wetu,... kila kukicha tufanya hivyo, na kila kukichwa,usiku ukaingia, tumuombe sana msamaha muumba wetu,...

Ni mimi: emu-three

No comments :