Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 20, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-30


‘Kuna mgeni wako....’askari wa hapo kituoni akaja kuniambia.

Nilisimama kwa haraka, nikiwa nimebadili na kuvaa shati, nikijua leo nitakutana na watu mbali mbali,nguo nilizokuwa nazo awali zilikuwa zimechafuka sana, nikaomba niletewe nguo nyingine. Hapo nikiwa angalau, msafi, nikatoka kwenye kile chumba cha mahabusu nikiwa kama kuku aliyemwagiwa maji, nilitamani nitoke mle kwa haraka ili angalau nipate hewa safi nje, kulikuwa na joto mbu, na harufu mbaya, ....kweli ndio maana watu wakitoka sehemu kama hizi huishia kuugua magonjwa ya vifua...,

Nikatoka pale na kuelekea kwenye meza ya kusubiria wageni, sikuona mtu zaidi ya askari waliokuwepo humo tangu jana, wakimalizia muda wao ili waje askari wengine wa zamu. 

Nikatulia kumsubiria huyo wakili aliyeletwa na mdada, na mara nikasikia sauti ya mtu anakuja nyuma yangu, nikageuka,...

‘Mimi ni askari upepelezi ninayechunguza kifo cha mtoza ushuru...’ilikuwa sauti ya huyo mtu ambaye mwanzoni nilijua ndio huyo wakili aliyeletwa na mdada lakini kumbe ni askari wa idara ya upelelezi.

‘Siwezi kuongea lolote na wewe mpaka aje wakili wangu....’nikasema nikigeuka kuangaliana na huyo askari,aliyekuwa kavalia kiraia, japokuwa wajihi wake, na anavyoonekana huwezi kumkosea kuwa ni askari, mwili wake, umejengeka hivyo.

‘Kwa taarifa na kumbukumbu zetu, hujatuletea jina la wakili wako, na tuna haki ya kukuhoji, hadi hapo utakapotuletea jina la wakili wako..’akasema huku akinikaribia pale nilipokuwa nimesimama.

‘Wakili wangu yupo tena wapo mawakili wawili, hivi sasa namsubiria wakili wangu wa pili ili kuweka mambo sawa,...kwahiyo kama unataka kuongea na mimi naomba umsubiri kwanza huyo wakili wangu...’nikasema

‘Kama nilivyokuambia, hatujapata jina la wakili wako, na tumetoa muda wa kutosha kusubiria, tangu jana nilitaka kuongea na wewe, lakini nikasikia kauli kama hiyo hiyo,....sisi tunahitaji kukuhoji, ili tuweze kufanya kazi yetu,....’akasema.

‘Na mimi ni haki yangu kuwa na wakili...’nikasema

‘Kinachotakiwa hapa ni wewe kutoa ushirikiano ili tuweze kuifikisha hii kesi mahakamani haraka iwezekanavyo, hivi unapenda ushikiliwe hivi mpaka lini, tulitakiwa leo tukupeleke huko gerezani, wewe umekaa hapa kwa siku ngapi,.....huoni kama vile umepata upendeleo, sasa ni vyema tukaongea, sina maswali mengi kwako, kwani mengi tumeshayaongea,..tunataka tuyamalize haya ili haki itendeke, sisi kwa upande wetu tuna ushahidi wa kutosha, ni mambo machache tu tunahitajia kuyafahamu kutoka kwako...’akasema

‘Sijawakatalia hilo, lakini na mimi ni haki yangu kuwepo mtu atakayehakikisha natendewa haki, naye ni wakili wangu, maana mumenikamata bila makosa, na nina mashaka mnaweza kunihukumu kwa makosa ambayo sikuyafanya..’nikasema

‘Hatuwezi kufanya makosa hayo, kwasababu kila kitu kitaonekana mahakamani, kama huna makosa kama unavyodai hakimu yupo, atahakikisha haki inatendeka, ndio maana kabla ya hukumu kuna mpito wa kesi, kuhojiana na ushahidi unawekwa mbele ya mahakama,....’akasema huku akitoa makabrasha yake kama anataka kuhakiki kitu.

‘Nakuelewa sana, ....na sipingi kuhojiwa na nyie, lakini ni muhimu wakili wangu awepo,...itakuwa na maana gani mimi niwe na wakili, halafu mje kunihoji bila ya yeye kuwepo, na najua sasa hivi atakuwa njiani anakuja, huenda ni foleni za magari, ndio zimemchelewesha....’nikasema .

‘Wakili wako huyo ni nani?’ akaniuliza
Na kabla sijamjibu, mara nikasikia mtu akiulizia kwa nje, na haikupita muda akaja askari na kusema wakili wangu amefika

‘Unaona huyo ndiye wakili wangu, nahitajia niongee naye kwanza kabla hujanihoji..’nikasema na yule askari akawa hakupendezewa na hoja yangu akasema;

‘Huku ni kupoteza muda, ...’akasema na kuangalia saa yake, na baadaye akainuka kuondoka, na akapishana na jamaa mmoja, aliyekuwa akiingia, wakaangaliana na huyo askari akawa kama anashanga, halafu akaendelea na safari yake.

Mimi nikawa nimetulia ili kupata utambulisho wa huyo mtu,....na huyo mtu akaja hadi pale nilipokuwa nimesimama, na akaangalia kwenye meza iliyokuwa na viti viwili,akanionyeshea ishara ya kuwa tukae, nikajua huyo ndiye wakili ambaye kaletwa na mdada. Tukakaa kwenye na yeye kwanza aliweka mkoba wake kwenye hiyo meza akaangalia saa yake, halafu akaniangalia na kunyosha mkono ili tusalimiane.

‘Pole sana mkuu, najua upo kwenye wakati mgumu, lakini usikonde mimi nimekuja na mambo yote tutayaweka sawa, unafahamu kazi hizi ni fani za watu, sio kila mtu anaweza kuzifanya, nimeshashikilia kesi za watu wengi, ambao walikuwa matatani, lakini nikazisimamia kitaalamu kabisa, na nashukuru wengi wameokoka na kitanzi...’akawa anafungua mkoba

‘Kwa kuanzia nataka tuelezane mambo machache tu, ili kuokoa muda, maana natakiwa kwenda kusimamia dhamana yako....kwahiyo, kwa vile mengi nimeshaongea na mdada, wewe unachotakiwa ni kuwa sambamba na jinsi nitakavyowalekeza,...ili msije kuongea tofauti, ni muhimu sana hilo....’akasema na mimi nikawa kimiya tu.

‘Hii kesi ni ngumu, na inaweza kukutia hatiani kama tusipokuwa makini, japokuwa hujafanya hilo kosa,kwa jinsi nilivyoongea na mdada.....’akasema

‘Hebu nielezee kidogo, ili nikuweke sawa, pale alipokwenda kukutana na huyo jamaa,..ukampa ule mzigo uliopewa na mdada, je alitoa bastola hapo hapo..au ilikuwaje?’ akauliza na mimi nikawa kimiya kwa muda halafu nikamwambia ilivyokuwa.

‘Hakutoa bastola hapo hapo, mimi niligundua ana bastola pale nilipokuwa naelekea ndani, pale aliponistua akiwa nyuma yangu, kwani wakati nilipomkabidhi ule mzigo wake, nay eye kunikabidhi mzigo wake, yeye aliekea kwenye gari lake nikajua anaondoka...’nikasema.

‘Unaona hapo....polisi, wanasema ulipomkabidhi mzigo, na kugundua kuwa ulichompa sio sahihi ndio akatoa bastola...’akasema

‘Sio kweli, mimi nimeonga nao mara mbili, nikawaambia hivyo hivyo...’nikasema

‘Ndio maana unatakiwa uongee ukiwa na wakili wako, wao wanaweza kugeuza maneno yao kwa manufaa yako..hilo nilitalisimamia..’akasema

‘Unafahamu,.... polisi wameshakusanya ushahidi wao wa kutosha, na wewe ni mtuhumiwa namba moja, ukishirikiana na mdada...ndivyo ilivyo kunapotokea kesi kama hizi, ...hata kama huhusiki ilimradi ulikuwepo kwenye tukio, halafu kukawa na alama za vidole kwenye silaha iliyotendea kosa, oooh, huna ujanja hapo, ni lazima, utashukiwa kuwa wewe ni mtendaji wa hilo kosa,...wao ndivyo wanavyofanya kazi zao, lakini ukikutana na watu kama sisi, ambao, tunatetea watu kama nyie, hupati shida, cha muhimu ni ushirikiano, ....’akatulia kidogo akifungua makabrasha yake.

‘Kwanza kabisa huu ni mkataba wa kukubali kuwa mimi ndiye wakili wako....ili niwakabidhi hao wahusika, ni utaratibu tu, ...na kesi kama hizi unaweza ukaweka mawakili zaidi ya mmoja, ..lakini kwa hii ya kwenu, nitaimaliza peke yangu, tena mapema kabisa...’akasema.

‘Kwahiyo kumbe alishapokea huo mzigo, na alipofika kwenye gari, akagundua kuwa huenda haujakamilika, au sio wenyewe, hapo akachukua bastola na kuja kwako, wewe muda huo hukujua kuwa jamaa anakuja na bastola, na kwa muda huo mlinzi alikuwa wapi?’ akaniuliza

‘Atakuwa alikuwa kwenye kibanda chake cha ulinzi..’nikasema

‘Kwahiyo kwa matendo hayo, hakuona chochote...?’ akauliza

‘Sina uhakika na hilo, ungemuuliza huyo mlinzi mwenyewe, nahisi itakuwa hivyo, maana sijasikia maelezo yake kwa upande huo kutoka kwa polisi....’nikasema

‘Hamna shida, nilitaka kuhakiki baadhi ya maeneo...na..na, kipindi unapigwa na kitu kigumu nyuma, hukuweza kabisa kumuona huyo aliyekupiga ?’akaniuliza

‘Sikumuona, kwanza mimi nilihisi ni mdada, lakini niliposikia kuwa nimepigwa na kitu kama nyundo, ndio nikaona sio yeye, ni lazima kulikuwa na mtu mwingine,...’nikasema

‘Na hukuwahi kuishika hiyo bastola kabisa?’ akaniuliza

‘Sikuwahi, maana nakumbuka, kabisa wakati nanyosha mkono kuishika ndio nikapigwa na kitu kugumu kichwani kwa nyuma, na mkono wangu ndio ulikuwa unaikaribia hiyo bastola,lakini sikuishika kabisa nina uhakika huo...’nikasema

‘Labda wakati unadondoka mkono wako uliigusa...’akasema

‘Hapana, kwa jinsi nilivyokuwa ...mkono wangu, hasa alama za vidoleni ...unaweza kufanya mazoezi mwenyewe, ukaona, nilinyosha mkono hivi...bastola ilikuwa mbele kidogo, nikama unajinysha hivi....mkono upo kwa mbali na hiyo bastola, kwahiyo ukadondoka kwa kupoteza fahamu utakuwa mbali kabisa na hiyo bastola, sikuishika,...alama za vidole, zikafikaje....na wanasema ni karibu vidole vyote...’nikasema

‘Hapo, kuna kitu hapo....ndio maana wanasita kuchukua hatua yoyote...’akasema

‘Kwanza kabisa nikuambie ukweli, huyo mtu aliyeuwawa, alikuwa na maadui wengi sana,...pili, angalia mazingira yenyewe, yalivyokuwa, wewe na mdada mlipigwa na kitu kizito kichwani mkapoteza fahamu,...hii ni kuashiria kuwa kulikuwa na mtu mwingine ndani aliyefanya hivyo...unaona eeh...’akasema huku akifungua fungua kwenye makabrasha yake, na mimi sikuwa nimesaini ule mkataba wake kwa muda huo, nilifanya kama nasaini, lakini nikaufunga na kuuweka pembeni.

‘Tatu, kuna mtu aliyekuwa na ndevu, kwa taarifa ya mlinzi, huyu mtu ni nani, hawajamgundua mpaka sasa huyo mtu,....na huyo mtu anaweza akawa ndiye muuaji....ndio maana mpaka sasa wamekushikilia tu, ulitakiwa muda kama huu uwe gerezani, sio hapa,....wanaogopa kufanya hivyo,kwani hawana ushahidi wa kuwatia nyie wawili hatiani.....’akasema.

‘Sasa sikiliza huyo mpelelezi hapo nje anataka kukuhoji, mimi nimeshamwambia kila kitu waniulize mimi....lakini kwa vile ni kesi ya mauaji, ni muhimu sana wakuhoji, na sio mara moja, wanaweza kukuhoji mara nyingi tu, lakini wanatakiwa wafanya hivyo, mimi nikiwemo, ...’akasema

‘Mhh, sasa nafikiri umenielewa....’akasema

‘Sijui.... mimi nakusikiliza wewe, ...’nikasema

‘Hakuna kesi hapa, usiwe na wasiwasi kabisa, mimi nataka kwenda kusimamia dhamana yako maana ni haki yako kisheria,...wanadai wanakushikilia kwa usalama wako, eti wanahisi unaweza ukauliwa na ndugu na jamaa za marehemu...’akasema

‘Kwahiyo mimi nifanyeje, maana mtu wa usalama anataka kunihoji tena, ....nimeshamuambia siwezi kufanya hivyo bila wakili wangu kuwepo, ....’nikasema

‘Umefanya vizuri sana, usijali, nimeshaongea naye, na ...ngoja kidogo...’akachukua simu yake na kumpigia mtu simu halafu akageuka kuniangalia, halafu akasema;

‘Ameshakubali,...nitaisimamia tu hakuna shaka, mmmmh, wewe ni wangu, malipo ni kama nilivykuonyesha kwenye hiyo ankara, kwanza inabidi nipate hiyo pesa ya awali kwa ajili ya ada za kisheria, pili kwa ajili ya mizunguko ya hapa na pale, na tatu, kwa ajili ya kuwalipa vijana wetu, ....’akasema

‘Hamna shida, ..usijali bosi wangu...’akasema na kugeuka kuniangalia, akasema;

‘Unaona huyo mtu keshaondoka, alikuwa akiongea na bosi wako...hakuna kitu hapa usijali kabisa, .....’akasema huku akifunga makabrasha yake, na mimi nikaona nimchokoze;

‘Sasa huyo muuaji wa kweli tutampataje?’ nikamuuliza

‘Hiyo sio kazi yako, hiyo sio kazi yetu, ni kazi ya polisi, na watu wao, hili lisikuumize kichwa kabisa, wakimpata wasipompata ni juu yao,...na inavyoonekana aliyefanya hivyo alijua ni nini anakifanya, sio rahisi kupatikana ....’akasema

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Kwasababu mpaka sasa hawajapata fununu yoyote kumhusu huyo mtu, pili, wamejikuta wamewashikilia nyie, huku wana ushahidi ulionyesha kuwa hamuhusiki, tatu,.....muda, katika kesi kama hizi jinsi muda unavyokwenda ndivyo muhusika wa hayo mauaji, anavyozidi kutokomea...sijui, labda wana fununu, au wameshamfahamu ni swala la muda tu, maana polisi nao wana utaalamu wao...’akasema

‘Wewe unaweza kuhisi ni nani aliyefanya hivyo?’ nikamuuliza

‘Siwezi kuhisi mtu, kazi yangu ni kuwatetea watu...sikiliza huyu mpelelezi akija kwako msimamo wako uwe ndio huo huo, kuwa hutaongea mpaka mimi niwepo, nafikiri tumeshaelewana,....’akasema akichukua ule mkataba akawa anaupitia, halafu akasema;

‘Mhh, mbona hujasaini kukubali kuwa mimi ndiye wakili wako....ni muhimu kiutaratibu....’akasema akinionyesha sehemu ya kusaini, na mimi nikachukua peni na kuweka sahihi yangu, halafu nikasema;

‘Kuna wakili mwingine mtashirikiana naye, ...’nikasema

‘Wakili gani mwingine .....?’ akauliza kwa mshangao, na kabla sijatoa maelezo akasema;

‘Wakili mwingine wa nini, haina haja ya kuweka wakili wawili, mimi nina jinsi yangu ya kufanya hii kazi, sipendi kuingiliwa, anaweza asikubaliane na utaratibu wangiu,..nikuambie kitu usipate taabu ya kuweka wakili mwingine.mimi nipo hii kesi ndogo sana kwa jinsi ilivyo, japokuwa ni kesi kubwa kwa utaratibu wake...’akasema

‘Mhh, hatakuingilia kabisa kwenye utaratibu wako, yeye atakuwa na mpangilio wake, na wewe endelea na mpangilio wako, hilo nakufahamisha tu...’nikamwambia na alikuwa kasimama, sasa akakaa kabisa, alionekana kutokuridhishwa na hilo, akasema;

‘Mdada anafahamu hilo?’ akaniuliza

‘Inawezekana, lakini hata yeye ana wakili wake, na wewe pia, au?’ nikamuuliza

‘Ndio...mimi ni wakili wa kumshauri tu,..ana wakili wake wa kuisimamia hiyo kesi,  lakini hata hivyo, yeye anahitajika kuwa hivyo, ...ok, ngoja nitaongea naye, lakini kwa jinsi nilivyoongea na mdada, hakusema una wakili mwingine, alisema wewe huna wakili anayefaa kwa kesi kama hizi, ...na tukakubaliana hivyo kuwa mimi ndiye niishike hiyo kesi, na aliponisimulia nikaona ni kesi inayowezekana,...’akasema

‘Mimi ndiye mwenye hii kesi, japokuwa tunahusika wawili, lakini inapofika kwenye utetezi kila mmoja anakuwa na mzigo wake, kwa hali ilivyo nimeona niwe na mawakili wawili, na nimeshakubaliana naye tayari, na hivi sasa anafuatilia mambo fulani fulani, ....’nikasema
Alionekana kusita, na baadaye akauliza;

‘Huyo wakili mwingine ni nani?’ akauliza huku akiwa kashikilia pen kichwani kama anawa jambo

‘Ni ....wakili wetu wa pale kazini,....’nikasema na yeye akatulia kidogo, na baadaye akasema;

‘Huyo hana ujuzi na kesi kama hizi, ..namfahamu sana, yeye ni mtu wa kesi za ajira, mikataba ya kikazi, na maswala ya kimaofisini tu ...sikiliza achana naye, hili swala niachie mimi, na mdada, kesi hii haina kitu, ni kesi ndogo sana, ....’akasema

‘Nimeshaingia mkataba naye siwezi kumkatalia tena, ...labda nikukutanishe na yeye muongee mtakavyokubaliana mimi nipo tayari, kwani ninachotaka mimi ni kuhakikisha kesi hii inakwisha haraka iwezekanavyo...’nikasema

‘Hapana siwezi kukutana na huyo mtu...’akasema huku akijiandaa kuondoka

‘Kwahiyo basi tumekubaliana hivyo...wewe utaendelea kwa upande wako, na huyo wakili mwingine atakuwa anasimamia upande wake, hata hivyo mwisho wa siku ni bora mkutane, ili kusijekuwa na mgongano...’nikasema

‘Hapana, ....hilo halitawezekana, mimi kukutana na huyo mtu, hatutaelewana.... kama ni hivyo inabidi nikaongee kwanza na mdada, ...’akasema akiondoka na wakati anatoka nikasikia mtu akiniulizia, nikajua ni wakili wetu wa kazini, moyoni nikasema;

‘Sasa naanza kuifurahia hii kesi...’nikasema na mara wakili wa kazini akaingia, huku akigeuka geuka nyuma, nahisi alikuwa akimwangalia huyo wakili aliyetoka, na baadaye akaniuliza

‘Huyu ni nani?’ akaniuliza

‘Ndiye wakili aliyemleta mdada...’nikasema

‘Haiwezekani...!’akasema kwa mshangao

‘Kwanini....?’ nikauliza

NB: Kwanini, sijui..tusubiri sehemu ijayo.

WAZO LA LEO: Kufanya kazi kwa ujanja ujanja ukijifanya kuwa unaielewa hiyo kazi, kwa ajili ya kuingiza kipato tu, ni sawa na kutapeli, na utapeli ni wizi. Kuna watu siku hizi wanajiita misheni town, kazi yao ni ulaghai, kila kitu wanajua wao,...tuwe makini na hawa watu.

 Hata maofisini wapo watu ambao hawajui fani fulani, lakini kwa ajili ya kuingiza kipato, wanajifanya wanajua hiki au kile, na kuzifanya kazi ambazo sio fani yao, matokea yake ni kuziba nafasi ya watu waliosomea hizo fani. Kuingiza kipato kwa ujanja ujanja, tunadhulumu haki za watu wanaostahiki.

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Mmmhhh...kesi yake inaanza kuleta msisimko...sijui ilikuwa shida gani na huyo wakili?....wazo la leo ni fundisho kwa wengi.....