Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, March 15, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-26


 ‘Sasa niambie ukweli ulivyokuwa, niambie kila kitu, bila kunificha ili nione nitafanya nini.. sijapata taarifa yoyote kutoka polisi, lakini kuna mtu wangu atanifahamisha, ni nini kinachoendela, na wakati tunasubiria,..ni vyema nikajua ni kitu gani kilitokea....’akasema wakili huo, na mara bosi yeye akainuka na kusema;

‘Mimi naona niwaache, nafika ofisini, halafu nitakuja kujua mumefikia wapi, sijui swala la dhamana, maana kama walivyosema, hutakaa hapa inabidi aende gerezani, hayo nakuachia wewe wakili,jitahidi dhamana ipatikane....’akasema

‘Niende gerezani kwa kosa gani, mimi sina kosa..’nikajitetea

‘Yote inategemea wewe,..... hatujui polisi wana ushahidi gani na kulitokea nini, kwani wamejitahidi kuficha habari zote, hakuna anayefahamu kilichotokea ni wewe ambaye ulikuwepo kwenye hilo tukio unaweza kutuelezea , muelezee wakili,sio mimi...’akasema bosi.

‘Lakini mimi sijui zaidi...nimeshakuambia bosi..’nikasema

‘Ongea na wakili, ujue yeye ndiye atakayekusaidia, kauli yako haitasaidia kitu , huenda ukaongea jambo likawa ndio kitanzi chako....huyo hapo wakili, mimi sina ninaloweza kukusaidia, usiposhirikiana na wakili wetu huyo, usije ukajilaumu...’akasema bosi.

Mimi nikamwangalia bosi, na alipokuwa akiondoka, niliona ni kama mzazi, anakuacha baada ya kufanya kosa, na ulitegemea yeye akusaidia, lakini kumbe hata yeye hana uwezo nalo, nikajua sasa nijipange kivyangu, hata hivyo, sikuwa tayari kuelezea kila kitu kwa masilahi yangu binafsi

Bosi alipondoka nikabakia mimi na wakili...nikamwangalia, akifungua makabrsha yake, na akawa anaandika jambo, kabla haajanza kunihoji,akachukua simu yake, yenye sehemu ya kurekodi sauti, akaiwasha na kuiweka mbele yetu, halafu akaniangalia na kusema;

‘Haya kama alivyosema bosi wako, nataka unieleze kila kitu, na ni vyema, ukaniambia wewe na mdada, wewe na huyo mtoza ushuru mnafahamiana vipi...kwanza elezea siku hiyo ya tukio ilikuwaje..

Nikamuelezea kwa kifupi kuwa mimi nilifika kwa mdada na bosi kwa ajili ya kumjulia hali na tukaona kuna umuhimu wa kumsaidia, kwahiyo tukapanga tukae naye, baadaye bosi akaondoka, na mimi nikabakia na mgonjwa

‘Wakati bosi wako anaondoka mdada alikuwa hajaamuka?’ akaniuliza

‘Ndio alikuwa hajaamuka...’nikasema

‘Mhh, alipoondoka bosi wako wewe ulikuwa wapi muda wote, ulikuwa ndani na mgonjwa au ulikuwa sehemu nyingine?’ akaniuliza

‘Nilikuwa chumba cha maongezi, ambapo tulikuwep hapo tangu awali, mimi na bosi, na bosi alipoondoka niliendelea kukaa hapo,...japokuwa mara kwa mara nilikuwa naingia chumbani kwa mdada kuchungulia kama kaamuka, ...’nikasema

‘Ni muda kama unakumbuka vyema, mdada alizindukana, kutoka kwenye nguvu za dawa alizopewa,au ulijuaje kuwa kaamuka?’ akaniuliza

‘Kuna muda nilikuwa naongea na simu, ...nahisi ndio muda alizindukana..’nikasema

‘Kwanini unasema unahisi...?’ akauliza

‘Kwasababu nilipokwenda kama kawaida yangu kuangalia chumbani kwake, nilikuta hayupo..’nikasema

‘Ulikuta hayupo, una maana gani kusema hivyo?’ akauliza

‘Nilikuwa naongea na simu, nikamaliza, lakini kuna muda nilihisi kun kitu kimelia, au  mtikisiko wa kitu, ndipo nikaenda chumbani kwake, nikakuta hayupo kitandani, nikajua labda yupo chooni, lakini huko napo hakuwepo, nilipotoka kwenda chumba chake cha makitaba nikamkuta yupo anaangalia laptop yake, nahisi kuna kitu alikuwa akifanya....’nikasema

`Ulikuwa ukiongea na nani kwenye simu?’

‘Na hilo natakiwa kuongea, mambo mengine ni ya kwangu binafsi...’nikasema

‘Kwa hali ilivyo, huna budi kuongea kila kitu hata kama ni mambo yao binafsi, mimi nitakushauri kuwa hili uongee a hili usiongee, muda wake ukifika, ...ni muhimu sana ukaniambia kila kitu...’akaniambia

‘Nilikuwa naongea na mchumba wangu...’nikasema

‘Mchumba wako yupo wapi,?’ akaniuliza

‘Yupo huko kijijini...’nikasema

‘Mlikuwa mnaongea nini hasa...maana mdada aliweza kuamuka, na usiweze kufahamu, huenda alisikia mlichokuwa mkiongea, na huenda ikawa na sababu ya tukio zima, ndio maana nakuuliza ili niweza kujua lipi ni lipi ni muhimu kwa wakati kama huu...’akaniambia

‘Alikuwa akinikumbushia kuhusu ahadi yangu ya ndoa...ni maswala hayo, na mimi nikamwambia nipo kwenye maandalizi,..na niliposikia huo mlio, au mtikisiko, nikaacha kuongea naye, nikakimbilia chumbani kwa mdada kuangalia kumtokea nini...’nikasema

‘Wewe na mdada mpoje, kuachia mbali maswala ya kufanya kazi pamoja, hamna urafiki wa karibu?’ akaniuliza

‘Sio kihivyo...hapana, yeye ni mfanyakazi mwenzangu tu, ...’nikasema na wakili akaniangalia kwa makini.

‘Ni muhimu ukaniambia ukweli, kwani polisi watafanya uchunguzi wa nyendo zako, watagundua yote, na mimi usiponiambia ukweli, nikaongea jambo, ambalo ni tofauti na walivyogundua wao, tutaonekana sisi ni waongo....unielewe hivyo, ...’akaniambia

‘Ndio hivyo mimi na mdada, ni ukaribu wa kikazi tu, sina zaidi na yeye....’nikasema nikimkwepa tusiangaliane.

‘Hamjawahi kufanya jambo jingine tofauti na maswala ya kikasi, mkawa mumeshirikiana wewe na mdada,..?’ akaniuliza

‘Hapana sijawahi kufanya hivyo, mimi na mdada tunajuana kazini tu, tukitoka kila mtu na lake...’nikasema

‘Una uhakika na hilo?’ akaniuliza.

‘Ndio hivyo kwanini nikufiche....mimi nina mchumba wangu na kama nilivyosema nilikuwa naongea naye kwa ajili ya maandalizi ya harusi, ...sina mambo mengine na mdada.

‘Huwa mkitoka kazini hamkutani mahali mkaongea mkanywa, mkala...?’ akaniuliza

‘Kwa mara chache sana....lakini sio kwa kuzoeana kiundani , hapana...’nikasema

‘Ujue kila ninachokuuliza kina maana yake, usitake nije kupata taabu ya kutafute ukweli, ni vyema ukasema ukweli, ili unirahisishie kazi...ufahamu mimi sifahamu chochote kuhusu wewe na mdada, na tukio zima, na natakiwa nikitoka hapa nikafanya uchunguzi ...’akasema

‘Uchunguzi wa nini na mimi ninachokuambia ndio ukweli wenyewe....’nikasema
‘Nikuulize tena, kuacha maswala ya kikazi, wewe na mdada hamna mambo mengine mnayoshirikiana naye?’ akaniuliza

‘Hakuna...na kwanini mdada, kwani yupo kuna nini kimetokea kwake, ...hajambo yupo hai...?’ nikajiukuta nauliza maswali mengi.

‘Majibu yake tutayapata hivi karibuni....cha msingi kwa sasa nikujua ukweli wa tukio zima, na wewe na mdada mpoje, wewe na huyo mtu mwingine mnajuana vipi na kulitokea nini siku hiyo ya tukio...’akasema

‘Haya hebu turudi siku hiyo ya tukio,..ulisema uligundua kuwa mdada yupo chumba cha maktaba, ulipotoka kwenda kumuangalia au sio?’akauliza

‘Ndio.....’nikasema

‘Alikuwaje, maana huyu mtu alikuwa mgonjwa,na sasa kaamuka yupo anafanya jambo kwenye laptop yake, ulimuonaje ?’ akaniuliza

‘Alikuwa safi tu, huwezi kutambua kama ni yule aliyekuwa akiumwa, na ndipo nikamuuliza hali na tukaanza kuongea mambo mengi tu, ...’nikasema

‘Mliongea nini hasa ...?’ akaniuliza

‘Mambo mengi ya kimaisha kwani yeye ni mfanyakazi mwenzangu na tumezoeana kwahiyo mnapokutana mnakuwa na mengi ya kuongea, siwezi kusema kila kitu...’nikasema

‘Sikiliza, ...wewe umeniambia kuwa wewe na mdada mnajuana kikazi zaidi, sasa hivi unasema kuwa mliongea naye mambo mengi zaidi ya kimaisha, ...’akasema akikunja uso kuonyesha kuwa ninamficha jambo.

‘Kuongea ni kitu kingine, mnapokuwa ofisini mnaongea mengi japokuwa hamna mahusiano nje, mkitoka hapo kila mtu na lake...’nikamwambia

‘Uwe makini na kauli zako..hapo moja kwa moja nimegundua kuwa kuna kitu unanificha,....inaonekana wewe ni mdada mpo zaidi ya kikazi...’akasema

‘Wewe wasema hivyo, ....kwa mdada ni mwepesi kumzoea kwasababu ni mcheshi,na nivyo ilivyokuwa kwangu, lakini sio ukaribu hadi mambo nje ya kazi,....’nikamwambia

‘Mliongea maswala ya kimaisha kama yapi, kuwa unajenga kuwa una mchumba kuwa kuhusu nini hasa?’ akaniuliza

‘Kama hayo, alitaka kujua mipango yangu ya kimaisha nikioa,...utani mwingi, ukikutaa na mdada tunaongea mengi kama tumezoeana sana, lakini sio kihivyo...’nikasema

‘Mkaongea hivyo mpaka saa ngapi, au hamkulala kabisa mkawa mnaongea tu?’ akaniuliza

‘Hapana tuliongea kwa muda, baadaye akamalizia kazi zake na yeye akaenda kulala..’nikasema

‘Alipokwenda kulala wewe ukabakia hapo makitaba au ulikwenda wapi?’ akauliza

‘Nilikwenda chumba kile nilichokuwa awali, hadi asubuhi, na ndipo...’nikataka kusema akanikatisha

‘Subiri usiende mbio,...’akasema

‘Wakati unaongea na mdada, ni kitu gani hasa alikuambia anakifanya maana anaumwa na mara kaamuka na kitu cha kwanza ni kukimbilia laptop yake...?’ akauliza

‘Kwakweli mimi sijui maana nilijaribu kadri niwezavyo nisimsumbue, au kumuuliza swali litakalomkwanza na kama tulivyoambiwa na docta, tusimkwaze, kwani akikasrikia, ndio anakuwa sio yeye tena...’nikasema

‘Sio yeye kama vipi anakuwaje, akikasirika..?’ akaniuliza

‘Hayo naomba uje umuulize dakitari wake, ana nafasi nzuri ya kukuelezea vyema zaidi yangu..’nikasema

‘Ok, sawa nataka unieleze kwa mtizamo wako, hayo ya kitaalamu sawa, nitamuuliza dakitari lakini wewe unasema akikasirika anakuwa kama sio yeye, ina maana ulishawahi kuona akiwa hivyo,...ni mara ya ngapi kuwa hivyo, ...kama ulivyosema anakuwa kama sio yeye...?’ akauliza

‘Mhh, ilitokea mara ya kwanza wakati naongea naye, nikamuuliza maswali ambayo nahisi hakuyapenda,..yakamkumbusha maisha yake yaliyopita,..na ndivyo inavyokuwa akikumbuka maisha yake yaliyopita anabadilika kabisa, anakuwa mtu mwingine tofauti na anaweza kufanya jambo baya....hata...’nikatulia

‘Hata kufanya nini?’ akauliza

‘Hata kujeruhi, kupiga na kufanya lolote baya....’nikasema na hapo akageuka na kuangalia saa yake, mara simu yake ikalia, akaiangalia, na kuniambia;

‘Samahani naongea na simu,..na wakati naongea, hebu jaribu kukumbuka vyema, maana hadi hapo sijapata kitu cha kuweza kukusaidia wewe...ndio tunaweza kusema mdada alibadilika akafanya yaliyofanyika, lakini.....’akatulia na kuangalia simu yake ambayo ilikuwa bado inaendelea kulia

‘Ok, samhani,...’akasema na kuweka simu yake sikioni na akawa anasikiliza kwa muda, bila kusema kitu, baadaye akasema;

‘Sawa nitakupigia baadaye, ....’akasema na kunigeukia

‘Sasa mambo yameiva,....’akasema

‘Kwa vipi unasema hivyo?’ nikamuuliza

‘Hii sasa ni kesi ya mauaji..’akasema

‘Mauaji ya nani?’ nikamuuliza nikianza kuhisi wasiwasi, na shinikizo la damu likaanza kupanda

‘Mtoza ushuru kauwawa...kwa kupigwa risasi,...na bastola yake mwenyewe, na kwa ushahidi wa alama za vidole, wewe na mdada mnahusika..’akasema

‘Kwa vipi mimi sikuwahi kuishika hiyo bastola...?’ nikauliza na kujitetea

‘Umeishika..., hizo alama zako za vidole zingefikaje kwenye hiyo bastola, hapo inabidi uniambie ukweli ulivyokuwa, ukinificha nitashindwa jinsi gani ya kukusaidia,....’akaniambia.

‘Mimi nilitaka kuichukua, na wakati nataka kufanya hivyo, nikapigwa na kitu kichwani na kupoteza fahamu, sikuwahi kuishika kabisa...’nikasema na ndivyo ninavyokumbuka hivyo, nilishangaa kusikia kuwa alama zangu za vidole zipo kwenye hiyo bastola.

‘Kwa mujibu wa polisi, wao wamepima na kukuta alama zilizopo kwenye hiyo bastola ni za kwako, na za mdada, na marehemu, hakuna alama nyingine...’akatulia na kuniangalia.

‘Mimi nina uhakika sikuigusa kabisa...’nikasema na huyo wakili alionekana haniamini akatikisa kichwa kutokukubaliana na mimi, akasema;

‘Ni muda wa wewe kuniambia ukweli ilikuwaje, ukinificha ujue sasa kitanzi, ni chako...mdada atajitetea kuwa ana matatizo ya akili,..lakini wewe utajitetea vipi, wakati alama za vodole vyako zimeonekana kwenye hiyo bastola....’akasema na kutulia.

‘Nakuapia ....mimi sikuigusa kabisa hiyo bastola, sijui kwanini alama za vidole zionekane kwenye hiyo bastola...’nikasema, na yeye akaniangalia kwa makini, halafu akasema;

‘Mhh, sizani kama kesi hii itakwenda vyema, naona nimtafaute mtu mwingine, ....ungeniambia ukweli wote, ningekubali kuishughulikia, lakini naona kabisa unanificha,..sitaki lawama,..’akasema

‘Sasa unataka nikuambie uwongo...’nikasema halafu yeye akasema;

‘Mimi ninakupa dakika tano za kufikiria,.....kuna mtu nampigia simu nikimaliza kuongea naye, nataka uniambie kila kitu..vinginevyo, mimi naosha mikono.’akasema na kusogea pembeni na akawa anampigia mtu simu.

Nikabakia nikijiuliza nifanye nini, maana nikiongea ukweli, nitakuwa nimharibu kabisa mahusiano yangu na mchumba wangu, na baba mkwe, hatakuwa radhi na mimi, na mengine ya kwangu na mdada yatajulikana, yale mapicha mabaya yatatakiwa kama ushahidi....hilo siwezi kufanya hata siku moja

‘Lakini nisiposema ukweli..itaonekana nimeshirikiana na mdada kwenye mauaji...kwa hiari yangu, kitu ambacho sio kweli...sasa nifanye nini.’nikawa najiuliza huku muda ukikimbia kuliko maelezo, na wakili akawa kamaliza kuongea na simu, akanisogelea na kusema
‘Haya ongea ukweli..ulivyokuwa na mahusiano yako na mdada....’akasema

NB: Zawadi kidogo ya wikiend


WAZO LA LEO: Usiogope kusema ukweli,hata kama kwa kusema hivyo,utaumia, ukificha ukweli ukasema uwongo, hata ukija kusema ukweli tena, uaminifu wako utakuwa umepungua, hutaaminika tena. 


Ni mimi: emu-three

No comments :