Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 13, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-25


Katika maisha yangu naogopa sana silaha hasa bunduki, na bastola, na sikutarajia kabisa ipo siku moja na mimi nitakutana nayo, na mbaya zaidi, ikielekezwa kwangu,...moyoni nikawa najenga taswira ya kuwa nimeshapigwa risasi nipo sakafuni natapa tapa...hasa niliposikia milio karibu mitatu ikitokea humo ndani...

Tuendelee na kisa chetu...

‘Yupo chumba gani?’ sauti ikanishitua nikiwa nimezamatulipofika ndani na mimi hapo nikajifanya sijui wapi alipo, nikasema
‘Sina uhakika, mimi sijui yupo chumba gani....’ nikasema na nikakatishwa na kipigo cha kitako cha ile bastola, jamaa alikuwa akipiga kweli...nikahisi maumivu na haraka nikanyosha kidole kuelekea chumba alipo mdada,

‘Haya tangulia twende huko huko...’akasema akinisukuma kwa mguu wake, na mimi nikatembea kwa kupepesuka, nikielekea huko ndani huku nikiwa na wasiwasi nikijua sasa naenda kukutana na simba aliyejeruhiwa, kwani nimjuavyo mdada kama atakuwa kapandisha ikianza mambo yake ni bora ukutane na huyo simba aliyejeruhiwa....

Nikakifikia kitasa cha mlango na kwa mkono unaotetemeka, nikakishika hicho kitasa cha mlango na kukinyonga, na huyo jamaa alipoona nachukua muda kukizingusha akakishika mwenye na kuufungua ule mlango halafu kwa nguvu akanisukumia ndani na yeye akawa nyumba yangu bastola ikigusa kichwa changu.

Na mimi nikiwa bado na wasiwasi nikatizama kitandani ambalo nilijua kuwa mdada kalala,...na ilionyesha hivyo, kuna mtu kalala, kajifunika gubi gubi,
‘Haya mwamushe wewe mwenyewe....’akasema na mimi nikasogelea kitanda, na kujaribu kutikisa tikisa, lakini kimya...

‘Una uhakika kuna mtu kalala hapo?’ akaniuliza

‘Ndio, yeye anaumwa, kwahiyo nahisi kapitiwa na usingizi kutokana na madawa anayokunywa...’nikasema na jamaa akanisukuma pembeni, akasogelea kitandani huku kashikilia bastola tayari kwa lolote akalivuta lile shuka kwa nguvu....

Ilikuwa kama mlipuko, ilikuwa kama kishindo...na kilichofuata hapo ni vurugu, haikuchukua dakika, nikasikia sauti mbili za risasi zikilia, nikajua kuna mtu kafa, nikajihakiki kama sio mimi, nilipoona naweza kugeuza shingo, nikajua nipo salama,...nilimuona yule jamaa akiwa sakafuni, huku kajaa damu usoni, nikageuka kuangalia,...mdada alikuwa na damu zinamtoka begani....

‘Toa hii maiti humu ndani....’sauti ikasema nikageuka kuangalia pale alipolala jamaa, kweli alionekana kama maiti, uso umeharibika, umekuwa kama umekwaruzwa na chombo maalumu, na asilimia kubwa ya ngozi ya usoni haipo.

Huku natetemeka, nikamshika yule jamaa, na kuanza kumuinua, na mdada akaona ninachelewa akamshika kama mtu anayeshika kitu kidogo, akamrusha kwa kupitia mlangoni, na nikasikia kishindo cha mtu akidondoka kama gunia. Sikuamini, ..

Unajua kama unamfahamu mdada, na hicho kilichotokea ni vitu viwili tofauti, kwani alichofanya ni kama mtu kuchukua kilo chache kwenye kiroba uinue na kurusha kutoka chombo hiki hicho kigunia kidondokee sehemu nyingine, varandani...

Nikageuka kumuangalia mdada, nikamuona akitembea kuelekea mlangoni na mimi kwa haraka nikaindea bastola iliyokuwa sakafuni, ile naishika tu, nikahisi kitu kikigonga kichwani mwangu, ..nikapoteza fahamu kwa muda.

Sijui ulipita muda gani, ....ninachokumbuka ni kuwa nilifungua macho yangu kwa shida na kumuona mdada, akiendea ile bastola aliyokuwa sakafuni, na kuishika mkononi, hapo nikajua umauti ni wangu sasa, mdada atatumaliza wote, nikageuka kuangalia mlango, nikauona mlango upo mbali,...lakini nikasema kimoyo moyo, ni bora nikimbie hata nikifa nijue nilikuwa na jitetea,...

Nilihesabu moja mbili tatu...nikatoka mbio, ...nilipofika sebuleni pale alipodondokea jamaa nikamuona anajiinua kumbe bado yupo hai, mimi nikamwambia

‘Kimbia hapa hakukaliki tena....’nikasema

‘Nimeshakufa, imebakia nini, lakini ni lazima nife na mtu,...’akasema huku akijitahidi kuinuka, na mimi sikusubiria, nikachomoka mbio kuelekea nje....

Wakati nipo nje, ndio hapo nikasikia tena sauti ya mlio wa risasi,...na ukelele wa mtu akilia maumivu,...nikahisi kuwa huyo analia maumivu ya risasi, keshakufa, sijui ni nani, mdada au huyo jamaa, mimi hapo sikusubiria mbio..kuelekea kwenye pikipiki langu, nilipolifikia, nikasikia sauti ikisema nyuma yangu

‘Simama hapo hapo ulipo...’nikasinyaa.


*********
Sehemu hii nilisimuliwa nikiwa nimeshikiliwa kituo cha polisi, alipokuja kunitembelea bosi, na alianza kwa kusema;

‘Pole sana na majanga,... atakuja wakili wa kampuni kuona jinsi gani ya kukusaidia, unahitajika kumuelezea kila kitu, ukumbuke, niliyowahi kukuambia kabla kuwa kama kuna tatizo la kisheria, tunahitajika kuwatumia watu wenye ujuzi nayo,lakini hukutaka kuwa muwazi,  ..’akasema bosi akiniangali jinsi nilivyonyong’onyea, nilikuwa kama mtu aliyenyeshewa, na hajala kwa muda mrefu, nikatulia huku nimeinamisha kichwa chini.

‘Haya majanga haya yanakukuta, sijui utafanya nini kukabiliana nayo, lakini hujachelewa wakili wetu atakuja kukusikiliza, na atatupa ushauri wake, vinginevyo, mimi sijui nikusaidieje, kama wewe mwenyewe hukutaka kujisaidia,  ...’akasema huku anaangalia saa yake.

‘Umesikia nilivyokuambia lakini...?’ akaniuliza alipoona bado nipo kimiya

‘Mhh, nimekusikia bosi,  nitamwambia kila kitu....lakini bosi,mdada anaendeleaje ?’ nikauliza

‘Hata sijui ...kama yupo hai au vipi, nimewauliza watu wa usalama, lakini hakuna aliyetaka kuniambia ukweli mpaka sasa, wanasema bado wapo kwenye uchunguzi wataongea wakishamalisha uchunguzi wao, ....mpaka sasa sijui ni nini hasa kilitokea na kuna nini kinaendelea..’akasema bosi

‘Kwahiyo hufahamu kabisa habari za mdada....?’nikamuuliza na yeye akasema.

‘Kwa hivi huhitajiki kupaniki...kifupi sifahamu bado, lakini nitafahamu muda sio mfupi,., cha muhimu, ni kujaribu kukumbuka kila kitu kilichotokea hapo, na pili, kukumbuka mambo muhimu ambayo huenda yanahusiana na hilo,...ila kwa sasa kwa kukuweka sawa ili kichwa chako kitulie, kidogo, nataka nikumalizie sehemu hii mwisho ya simulizi langu, ..’akasema

‘Mhh, bosi unafikiri kichwa changu kipo hapa...sijui kama nitaweza kusikiliza, maana haya yaliyopo mbele yangu ni makubwa, naona kama nimebebeshwa mzigo nisiouweza...’nikasema

‘Hilo sio shida, akili inahitajika kutulia,...na ukumbuke matatizo yanapotokea, cha muhimu, ni kuhakikisha kuwa akili na mawazo yako hayafikirii matokea mabaya, yawe yanalenga matokeo mazuri, kwa kujipa moyo, ....ili mwili na akili zisianze kuchoka na kukata tamaa...’akasema bosi

‘Nia na lengo langu ni kukupa ujasiri kuwa katika maisha ya taaabu, ukavumlia, ukajitahidi, mwisho wa siku utafanikiwa,....ndio maana nataka kukumalizia sehemu hi muhimu ili nawe uwe na ujasri fulani akilini mwako....’akasema bosi

‘Kama unana hivyo, sawa...’nikasema

‘Unakumbuka nilikuwambia kisa cha maisha yangu ni kirefu, na sehemu tuliyokuwa tukienda nayo ni sehemu ya kwanza, na sasa ndio naimalizia...nitakusimilia hitimisho la sehemu hii ya kwanza ambayo ni mwanzo wa sehemu ya pili, huku tukimsubiria huyo wakili wetu...ili tuone atakusaidia vipi...’akasema

‘Lakini bosi mimi sionu umuhimu wa wakili, kwani mimi nina kosa gani,maana mimi....mhh,  ...sijui kilichotokea nilipoona mdada kabadilika, nilikimbia, huko nyuma sijui kulitokea nini....’nikasema.

‘Hayo utamwelezea wakili sio mimi, au hutaki nikumalizie kisa changu, maana huenda hutapata muda wa kukisikia tena, ....’akasema na mimi nikamwangalia kwa mashaka.

‘Kwanini unasema hivyo bosi...?’ nikamuuliza nikianza kuogopa.

‘Kwa jinsi kesi yenyewe ilivyo, nahisi hutakuwa na muda wa kutulia na kusikiliza mpaka kesi yanyewe iishe, sasa hatujui itachukua muda gani,....kesi yenyewe imeshagubikwa na mauji...sio kesi ya mchezo...’akasema bosi

‘Mauji! Unasema mauaji,, ..ni nani kafa...?’ nikauliza kwa mashaka huku nikitoa macho ya uwoga, na yeye akaniangalia na kusema;

‘Ngoja nikumalizie kisa changu kwanza....akija wakili atakuelezea yeye mwenyewe kile unachohitajika kukijua na wewe utamsimulia hayo yaliyotokea ....usimfiche kitu, kama kweli ulifanya hivyo, au ....’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;

‘Kufanya nini bosi, mimi sijui,...sijafanya kitu bosi....’nikasema sasa nikianza kuogopa.

‘Usiwe na shaka, wakili akija atasikiliza,...ninachotaka kwa sasa ni kukutuliza kichwa chako, usipotulia na kuweza kutafakari vyema, unaweza ukajikuta kwenye wakati mgumu,...’akasema bosi

Nikawa sina jinsi ila kutulia na kumsikiliza bosi akimalizia kisa chake....

*******

‘Siku zikawa zinakwenda na maisha yakawa yanaendelea na juhudi zangu, zikaleta matunda nikawa na maendeleo mazuri maduka yangu yakawa yamesheheni viti, na wateja wakawa wanajazana, kwani nilikuwa nafahamu ni kitu gani mteja anahitajia, jinsi gani ya kumvuta mteja, hayo niliyasomea na niliweza kuyatekeeleza katika biashara zangu.

Wakati hayo yanaendelea pia maisha ya ndani nyumba yalikuwa yakiendelea kwani nilijikuta nina mimba nyingine, na hii nilikuwa nimejiandaa nayo, kwahiyo sikuwa na shaka nayo, kwahiyo niliweza kujipangia taratibu zangu za kikazi bila kujichosha na bila kusimangwa na mtu

Ukumbuke kuwa nilishapeleka maombi ya kazi, na kuwa muda niliona kama vile sitaweza kuipata hiyo kazi kwani muda ulishapita, lakini nilishangaa siku moja naletewa barua ya kuita kwenye usailikwani, kule nilipopeleka maombi ya kazi, nikajibiwa kuwa nahitajika kufika kwa ajili ya kufanyiwa usahili.

Kwa vile nilishaanza kazi za biashara, na nilishajenga uzoefu wa kukutana na watu mbali mbali, kwenda huku na kule, kwa ajili ya kufanikisha maswala ya biashara, hali hiyo ilinijenga kuwa na ujairi wa kuongea na kila mtu, kwahiyo hilo la kuitwa kwa usahili halikunipa mashaka.

Kuna kitu nilijifunza katika maisha, ambacho kinanisaidia mpaka leo ni tabia kujiamini. Ukiwa unajiamini katika jambo lolote ni rahisi sana kufanikiwa, na kujiamini kunatokana na kuwa na uhakika na kile unachotaka kukifanya, na ili uwe na uhakika nacho ni lazima uwe unakifahamu,kama hukifahamu uione soo kuuliza, au kama ni kitu cha kusomea nenda kasome.

Kitu kingine nilichojifunza ni kujituma, unapokusudia jambo, kujituma kunakupa mori, usifanye kitu kama umelazimishwa, fanya kwa uhakika, kwahiyo nilipoamua kutafuta kazi, nilikuwa nimejihakikishia kuwa ninaweza, na sio natafuta kwa ajili ya kupata pesa tu, lakini pia ni kwa  vile nilijua kuwa ninaweza kuifanya hiyo kazi.

Pamoja na kuwa maiha yangu yalipitia kwenye mitihani hiyo,ambayo ingeweza kuharibu hata utashi wa kufikiri na kusimamia mambo yako itakiwavyo,  lakini kwangu mimi haikuwa hivyo, nilijua kabisa kusoma ni nguzo muhimu katika mafanikio yenye tija,kila muda nilipokuwa napata nafasi, sikuacha kusoma, nilikuwa najikumbusha yale niliyowahi kujifunza shuleni na vyuoni, kwahiyo sikuwa nimejisahahau sana.

Kitu kingine kilichoweza kunisaidia ni lugha, shuleni nilikuwa nimejitahidi sana kujua lugha, nah ii ilikuja kunisaidia sana katika hughuli za kibiahara, maana ukiwa mfanyabiashara unatagemea kukutana na watu tofauti, na lugha ya kimataifa ni kiingereza, na hilo nililijua nikawa nimejiandaa nalo,...na ukikumbuka, kama nilivyoelezea awali, darasani nilikuwa nafanya vizuri sana, kwahiyo pamoja na changamoto hizo za kimaisha uwezo wangu wa kitaaluma ulikuwa pale pale.

 Nikajiandaa kwa taratibu hizo, nilishauliza natakiwa nijiandae vipi kwa waliobahatika kuajiriwa, na pia kupitia makabrasha mbali mbali kwenye mitandao, na vitabu, na kwa jinsi walivyonielezea wenzangu niliona ni kazi rahisi, kwani hayo ya kuongea na wateja, jinsi gani ya kumfanya mteja avutike na kujiona ni mtu muhimu ndiyo ilikuwa kazi yangu, kwahiyo hayo sikuwa na mashaka nayo, mimi nilikuwa nayafahamu vyema.

Basi siku hiyo nikajiandaa na kwenda huko kwenye kampuni yenyewe, nilitarajia kuwa nitakuta watu wengi, wakiwania hiyo nafasi lakini ikawa kinyume chake,ilikuwa kama walishanifahamu kabla, wakanihoji maswali yao, na walivutika sana na mimi, na walisema wameshaniona ninafaa, lakini kwa vile kuna wengine wanatahiniwa, nisubiri nyumbani wataniita.

Siku moja nikapigiwa simu na mtu maarufu wa kampuni niliyowahi kufanyiwa usahili, kwajili ya kazi ,nilifika haraka bila kuchelewa na nikapewa barua ya kukubaliwa kufanya kazi kwenye kampuni hiyo, ilikuwa moja ya kampuni kubwa zya tiketi za ndege na nilianza tu baada ya kujifungua na kumaliza arobaini kama kawaida yetu.

Sasa naamini kuwa pamoja na shida, pamoja na dhuluma za dunia, ma madhaidi yetu, tunatakiwa tusikate tamaa, na usiangalia kuwa wewe ni jinsia gani, kuwa kwa vile wewe ni mwanamke hutaweza, hiyo sio kweli, ukiwa na ukamlifu wa mwili, hata kama huna ukamlifu huo, lakini una akili za kufikiri vyema, utafanikiwa tu, cha muhimu na kujibidisha, na akilini jenga hoja, kama wenzangu wanaweza kwanini mimi nishindwe.

Hutaamini, mimi saa ni mmoja wa wanawake wanaoweza kujiendesha wenyewe, nina maduka, nina miradi na kampuni ambayo nitakuja kuelezea kwenye sehemu ijayo jinni gani nilivyofanikiwa kufikia hapo, nayo ilikuwa na changamoto zake.

Mimi kama binadamu, huwa pia nina mapungufu yangu, kwahiyo hayo ni lazima nije kuyaelezee pia, kwani mimi sio malaika, nilipofanikiwa kuna muda na mimi nilianza kujiona, nikaanza hata kumzarau mume wangu nikamuona mtu wa chini...’akasema na kutabasamu.

‘Inatokea kibinadamu, kwasababu mimi nina uwezo nina pesa, yeye kidogo, sio sawa na mimi japokuwa na yeye alikuja kujiwekeza kidogo, kukawa na changamoto zake...yote hayo ni mapungufu ya mwanadamu, na tutakuja kuyaona kwenye sehemu ya pili ya simulizi letu, kama mambo yako yakienda vyema ...’akasema bosi na mara akaja mtu na kusimama karibu yetu

Bosi akaniangalia halafu akamgeukia yule mtu, na baadaye akanianglia mimi na kusema;

‘Huyo ndio wakili wetu, ...’akaniambia na mimi nikainua kichwa kumuangalia, huku mwili ukianza kuhisi joto...damu ikianza kwenda mbio, nikijiuliza ina maana sasa natakiwa kusema kila kitu, hata siri zangu..WAZO LA LEO: Ukweli na haki ndio msimamo sahihi, ili uweze kafanikiwa, ili uweze kuyashinda majaribu, ili uweze kufanikiwa, simamia kwenye msimamo huo, sema kweli, na tenda yaliyo haki.

Ni mimi: emu-three

No comments :