Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 6, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-22



Docta alipotoka, akatuambia mdada, anatakiwa kupumzika, dawa alizopewa ni za usingizi, kwahiyo atalala sana, lakini inahitajika akiamuka kuwe na mtu anayemfahamu;

‘Cha muhimu akiamuka kuwe na mtu wa karibu anayefahamu matatizo yake, na akwepe sana kumuuliza mambo ambayo yatarejesha kumbukumbu zake nyuma...’akaema docta, na nikamwangalia bosi, nikijiuliza je yeye ndiye atakaa na mdada, au kuna ndugu zake wengine.

‘Mhh, kiujumla ndugu za mdada wapo mbali, na mimi ndiye mtu wao wa karibu kwa sasa,...sijui nitafanyaje, lakini anyway, nitaangalia nitakavyoweza...’akasema bosi.

‘Kila siku ninapokuja hapa nasahau kuuliza, maana wakati mwingine unaweza kuuliza swali ukajuta kwanini uliuliza, inategemea na mtu,...lakini sasa naona niwaulize, hivi huyu binti anaishi na nani hapa?’ akauliza akimwangalia bosi, na kuniangalia mimi, halafu akageuka kumwangalia bosi.

‘Mwanzoni alikuwa akiishi na ndugu yake, na ndugu yake, aliondoka kwenda kusoma, kwahiyo akabakia mwenyewe, na mfanyakazi wake wa ndani, ....mfanyakazi wake, kwasasa yupo likizo hajarudi..na huenda asirudi tena....’akasema bosi.

‘Kwanini asirudi tena, kafukuzwa?’ akauliza docta

‘Hapana hajafukuzwa, aliondoka akiwa kaomba kwenda likizo, na akiwa huko ikaja taarifa kuwa kapata mchumba, kwahiyo anatarajia kuolewa,na akiolewa ina maana ndio basi tena ...’akasema bosi na docta akawa anaiangalia ile nyumba na kusema;

‘Maana naona hii nyumba ni kubwa sana,ni nyumba ya kifamilia,..na hali yake ilivyo ni vyema akawa na mtu, vinginevyo....labda akalazwe, na akilazwa kwa matatizo kama hayo, itabidi apelekwe chumba cha wagonjwa wenye matatizo ya akili...na sizani kama atakubali...’akasema docta.

‘Kwani unahisi tatizo hilo ni kubwa sana kiasi hicho, cha kulazwa, nakumbuka mwanzoni ulisema hilo tatizo ni la muda tu litakwisha....?’ akauliza bosi.

‘Mhh, kutokana na hali hiyo,...siwezi kusema kuwa hali ni mbaya,kama angelikuwa anafuata masharti, huenda hilo tatizo huenda lingelikuwa limekwisha...’akatulia kidogo, na baadaye akasema;

‘Kwa jinsi inavyojionyesha, tatizo kujirudia tena na tena, ingelifaa, na ni muhimu, akakaa hospitalini ambapo atapata usimamizi wa kutosha, tatizo ni kuwa kwa hivi sasa kila anayekuja au hata akiwa na maongezi na wenzake, kuna ile hali ya kuuliza, maisha yaliyopita, ilikuwaje, kwanini...na hujui nani atamuuliza nini, bila kujali kuwa hilo analomuuliza litamkwaza au vipi...’akasema docta.

‘Wewe ndiye dakitari wake, na mtaalamu wa mambo hayo, na wewe ndiye unayeweza kumshauri hivyo, ...sizani kama ukimwambia akalazwe kwa ajili ya uchunguzi zaidi anaweza kukataa,....’akasema bosi,

‘Nimeshamwambia hivyo, akakataa kata kata, na kudai kuwa yeye sio mgonjwa, na hayo yanayotokea sio kusudio lake,...lakini anahisi, kama anavyodai, kuna dawa ambayo akiipata atapona kabisa....’akasema docta.

‘Dawa gani tena ambayo anaijua yeye, mimi nijuavyo wewe ndiye unayestahili kumpatia hiyo dawa...?’ akauliza bosi.

‘Hayo matatizo yake ni ya kiakili zaidi, na wakati mwingine, anavyoona yeye anaweza kukipata kitu,kikawa ni dawa, na kweli akikipata kinaweza kumsaidia,...kwa maono yake, kutokana na hisia hizo za kichwani, maana pale alipo anaweza kuona vitu ambavyo sisi hatuvioni, vinajengwa kwenye ubongo wake,..kutokana na msongo,wa mambo yanayokutana kwa kasi, na kushindwa kuhimili.....’akatulia kidogo akiangalia saa.

‘Lakini docta, wengine wanasema huenda ana mashetani, sijui hilo unatuambieje?’ akaulizwa.

‘Kuna maswala ya imani za watu, hayo kila mtu ana yake, lakini kuna maswala ya ugonjwa na unajulikana kisayansi...hilo alilo nalo, sio swala la mashetani...’akasema

‘Kwa, jinsi mwili ulivyo, na kila sehemu ya mwili ina kazi zake....ubongo ni sehemu muhimu ya mwanadamu ambayo ndio kiongozi wa kila kitu kwenye mwili wa mwanamu, kila jambo ili lifanyike ni lazima taarifa zifike kwenye ubongo...kwahiyo sehemu hiyo ni muhimu sana kwa mwanadamu na hauhitajiki kubughudhiwa...sasa kuna matukio yanaweza kuathiri sehemu hiyo nyeti,na kumfanya binadamu abadilike kabisa, afikie hatua kuwa kama mnyama...’akasema.

‘Siwezi kukataa kuwa kuna mambo hayo ya mashetani, lakini sio wakato wote hali kama hiyo ikawa ni hayo mashetani, ni muhimu sana ukaangalia upande wa vipimo vya kitaalamu, kwani huenda ni tatizo linalotibika kwa dawa za kawaida, ukilichelewesha linaweza lisitibike tena, ...mwisho wa siku utahangaika na hao waganga, na usipone kabisa...’akasema.

‘Kwahiyo ulivyomuona wewe ni tatizo la kawaida linalotibika, au kunatakiwa njia nyingine?’ akaulizwa.

‘Linatibika...cha muhimu pamoja na madawa, lakini masharti yake ni muhimu, tunaweza tukatumia dawa nyingi , lakini kama hatukufuata masharti, ikawa ni kazi bure....huyo kwa sasa anahitajia utulivu wa akili, na nashauri, kama angelipata mume muelewa, ingelikuwa ni bora zaidi...lakini awe muelewa, awe ni mtu anayemfahamu, awe mtu mvumilivu, mwenye hekima...’akamwangalia bosi, na baadaye akaniangalia mimi, mimi nilikuwa kimiya tu

‘Tumekuelewa docta, hayo ni maswala ya ushauri, maana hatujui yeye ana mipangilio gani kichwani mwake, lakini pamoja na hayo, wewe kama dakitari wake, ungekuwa mshauri mnzuri kwake, ukamshauri hilo na mengine, akisikia kutoka kwako, inakuwa na nguvu zaidi...’akasema bosi.

‘Yote hayo nimeshamwambia mapema kabisa,lakini kutoka na hayo yaliyomkuta huko nyuma ambayo ndio chanzo cha haya yote, bado nafsi yake haiamini kuwa mume ni mtu muhimu kwake...bado kajenga hisia kuwa mume ni mtu mbaya kwake, na kwake mume ni adui...sasa anahitajika mtu kuivunja hiyo hali....sijui...kuna mtu anamtaja taja sana, mhasibu, ni nani huyo?’ akauliza docta, na bosi akaniangalia na kutabasamu.
‘Anamtaja kwa mabaya, au kwa ....?’ akauliza bosi

‘Kwa mazuri, inaonekana anampenda sana huyo mtu, sijui yupoje, lakini hata kama anampenda, huyo mtu kabla ya kukubaliana na mdada, ni vyema akamfahamu, na kufahamu matatizo aliyo nayo na cha muhimu akiwa naye asije akajaribu kumghadhibisha, akamrejeshea machungu ya nyuma..huyo binti anahitajia kupetiwa na kuengeuliwa kama mwali mbichi...’akasema docta na kutasamu...

‘Tumekuelewa docta, tutajitahidi kumshauri, na huenda akampata mtu kama huyo, japokuwa wanaume wa namna hiyo ni nadra kuwapata, wengi, wanapooa, wanajua kuwa huyo mke kakamilika, anaweza kila kitu...hawaangalii madhaifu ya kibinadamu kuwa huyo naye alilelewa, na katika malezi kuna kutofautiana..’akasea bosi

‘Ni kweli...umesema kweli, natumai ukikaa nao, yeye mgonjwa na huyo atakayebahatika kumuoa ukawafunda, wanaweza wakasaidiana na taizo hilo likaisha kabisa...kama kuna janga lilitokea huko nyuma, ni bora lisitajwe..kabisa, mkitaka huyo mtu asipone, na ageuka kuwa mnyama mnyama,...mjaribu kuchimba alichowahi kufanya...’akasema docta.

‘Kwanini unasema hivyo docta?’ akauliza bosi

‘Kuna hawa watu wa usalama, mara kwa mara wananijia niwaelezee kuhusu aliyowahi kufanya huyo mgonjwa, nahisi wanahisi kuna jambo baya aliwahi kufanya...’akasema

‘Je ni kweli lifanya?’ akauliza bosi

‘Siwezi kusema kwa uhakika,....sio kazi yangu na hizo ni siri za mgonjwa, ...kama yapo, msije mgamgusia, au kumuulizia, hilo ni jambo muhimu, lakini pia, asijihusishe na madawa ya kulevya, pombe ....nilishamkanaya sana hilo...na zaidi, asije akajiingiza kwenye mambo ya kuhatarisha maisha yake nay a watu wengine....damu kwake, ni moja ya viashiria vya kumkubusha majanga yaliyowahi kumtokea..’akasema docta

‘Damu, ina nini damu....?’ akauliza bosi

‘Cha muhimu, ni kuwa asije akaingia kwenye mapigano, akamtoa mtu damu, au yeye kutolewa damu, ...ni vitu ambavyo akiviona anakumbuka jambo....sasa ni vyema, asijiingize kwenye makundi mabaya, yatakayoleta umwagaji damu...ni hayo kwa leo, nyie mumeshamuelewa natumai mtakuwa na moyo wa kumsaidia, kwani wewe umeshaoa...?’akaniluza docta swali la kunishitukizia na kunifanya moyo wangu uende mbio, niliogopa hata kumjibu, nikasema;

‘Nipo mbioni....’nikasema.

‘Nikuanavyo wewe ungemfaa huyo dada,...’akasema na mimi nikajitahdi kutabsamu na bosi akawa ananiangalia kwa jicho la kujiiba kuona kama nitasema kitu, na docta akageuka kuondoka.

 Dakitari alipoondoka tukabakia mimi na bosi, wakati huo tulishaingia ndani nyumbani kwa mdada, na mdada alikuwa kalala kwenye sofa, naona docta alipendekeza alale hapo kuliko kulala chumbani kwake na kwa vile hatukutakiwa kumsumbua, tukaingia chumba cha maongezi, na bosi akasema;


‘Inabidi hapa tupange zamu,...kwanza naanza mimi, maana baadaye natakiwa kufika kuiangalia familia yangu, ..baadaye utashika hiyo zamu, ..kama itakuwa bado, tutaangalia hiyo kesho ni nani anaweza kukaa na yeye...’akasema bosi

‘Lakini mimi ni mwanaume, na kama ujuavyo kwasasa hataki wanaume, karibu yake,..huoni nikiwa naye peke yangu muda huo, akizindukana kunaweza kutokea tatizo..’nikaanza kujitetea

‘Umeshafika hapa mara mbili kuonana na yeye kwa namna hiyo ni kuwa umeshajenga akili ya kutambua ufanye nini kwa mtu kama huyu...usikwepe majukumu. Kukwepa majukumu ni uzembe,..na uzembe wa namna hiyo hauna tija. Katika maisha yako ukiwa mtegeaji, kuwa mwenzangu atafanya, au nitafanya kesho, au kutafuta viingizio, hutafanikiwa kabisa katika maisha, yako na ukifanikiwa hutajiamini, hutakuwa na amani moyoni....’akasema bosi

‘Jitume kila inavyowezekana, kila jambo la kufanya jione wewe unastahili kulifanya, kuliko mwenzako, na kama ni la kitaalamu basi mtafute muhusika, ..ile kuhangaika kumtafuta huyo mtaalamu, hapo umejituma, na umetimiza wajibu wako, ..lakini kujifanya huhusiki na usihangaike, hata kumtafuta mtaalamu, ujue wewe una kasoro, na huo ni uzembe, na uzembe ni zambi...’akasema bosi

 ‘Kwahiyo bosi, ...sasa ni saa...’nikaangalia saa

‘Kama huna haraka sana, nikusimulie sehemu muhimu kwenye sehemu hii ya kwanza katika mfulululizo wa visa katika maisha yangu....’akasema bosi

‘Nitafurahi sana,....’nikasema.

*******
‘Katika simulizi la maisha yangu, kuna sehemu hii ya kwanza ambayo tunaenda nayo, ikielezea machungu niliyoyapata toka utotoni hadi kuolewa,....na sasa tupo kwenye sehemu ya mwisho ya sehemu hii ya kwanza, ambapo nimeshaanza maisha ya kujitegemea, nimeshaamua kujitosa kwenye ulingo wa kuwa muwekezaji..’akaanza kunisimulia

 ‘Ni hatua ya namna yake, kuamua kuwa sasa najiwekeza, naanzisha biashara yangu, na ukumbuke ni mama mwenye familia, na majukumu hayo bado ni yangu. Inahitajia ujasiri fulani, wa kujituma na mimi najituma, sikulala, nikawa nahangaika, najibidisha kwenye shughuli zangu,..

Hata hivyo pamoja na hayo, ile kasumba ya kuajiriwa, kupata kazi, bado nilikuwa nayo, nilikuwa mara kwa mara nikitamani nipate kazi ya kuajiriwa japokuwa nilikuwa an hizo biashara zangu..na hii ni hulka ya wengi..hasa unapokuwa umesoma.

Japokuwa mimi kwa bahati mbaya, nilisoma kwa vipande vipande kutokana na yaliyonikuta huko nyuma kwa wazazi wangu, hata hivyo, nilikuja baadaye kusoma hadi chuo, kwahiyo nilikuwa na vyeti vinavyoniwezesha kuajiriwa,..

Pamoja na akili ya darasani, lakini pia akili ya uzoefu, akili ya majanga, akili ya matatizo, ikawa ni mwalimu wangu mkubwa, nikajifunza kuwa matatizo, yanaweza kutumika, kuwa sehemu ya zana za kufanyia kazi, ..huwezi amini hilo, kwani nahisi kama isingeliwa hayo matatizo huenda nisingelifanya hayo niyoyafanya..

 Basi nilipomuendea yule rafiki yangu na kumuomba mkopo, na yeye akawa tayari kunikopesha, ila kwa sharti moja kuwa ni lazima nimuhusishe mume wangu, nikafanya hivyo.

Nilifahamu ni kwanini, alihitajia mpaka nimuhusishe mume wangu, maana mkopo, una masharti yake, na mojawpo ni ushahidi, unaweza ukawepo ushahidi wa maandishi, lakini ni muhimu kukawepo watu wa kudhamini ....ikizingatia kuwa mimi ni mke wa mtu basi mume wangu anawajibika kufahamu hilo, nikamuelewa na mimi nikaenda kuongea na mume wangu.

‘Mume wangu kama unavyoona, duka sasa linachanganya, lakini mtaji wetu ni mdogo sana, tunahitajika kuongeza bidhaa, lakini hatuna pesa..’nikasema.

‘Sasa tufanyeje, kama hakuna pesa, basi tuendelee hivyo hivyo, hadi hapo tutakapoweza kupata pesa nyingi, au wewe ulikuwa na wazo gani?’ akaniuliza.

‘Tukope pesa....’nikasema.

‘Unasema tukakope..., hapana, mimi naogopa sana madeni,..nilishawahi kukukopa, na kushindwa kulipa, matokea yake nilinyang’anywa kila kitu ndio maana ulinikuta sina kitu, .....’akasema.

‘Ulikopa bila malengo, usikope,....ukiwa hujajipanga, kwanza kabla ya kukopa, panga ni kitu gani cha kufanya, je kinalipa, ili uweze kupata hayo marejesho...usikope kwanza ndio upange, panga kwanza kabla ya kupata huo mkopo. ....’nikamwambia mume wangu.

‘Sawa haya niambie, utakopa wapi, ujue sisi hatuna dhamana, na ndugu zngu hawawezi kukubali nyumba yetu ichukuliwe kama dhamana,na nafahamu kabisa ukienda benki watahitaji dhamana...?’ akaniuliza.

‘Dhamani ni mimi na wewe...’nikamwambia.

‘Ni yale yale...mimi nina nini hapa....usinipe shinikizo la damu, na vidonda vya tumbo, ...’akasema

‘Ni hivi, nimeshaongea na rafiki yangu mmoja, yeye kidogo kajiweka vyema, na yupo tayari kutukopesha, anachohitajia ni wewe kukubaliana na mimi, na ukawa shahidi, basi mambo mengine, niachie mwenyewe,...usiwe na wasiwasi..’nikamwambia.

‘Unataka mimi nikawe shahidi, wakati sina mbele wala nyuma...hapana,kama unakopa kopa kwa malengo yako, usiniweke rehani..’akasema

‘Sikiliza mume wangu, duka umeliona lilivyo, je wateja wapo hawapo?’ nikamuuliza

‘Nimeona wapo,....lakini nijuavyo ukikopa tu, mambo yanaanza kubadilika...’akasema

‘Hizo ni imani za kukata tamaa,...cha muhimu ni kuwa tuna sehemu ya biashara tayari, na sehemu hiyo ina wateja, ina maana, tuna soko tayari..., na tayari tuna nini cha kufanya, ikiwa na maana kuwa tuna bidhaa, kinachohitajika ni kuongeza juhudi, ..huo mtaji utatusaidia sana, wewe mwenyewe utaona...’nikamwambia .

‘Sawa nimekubali, unataka nifanye nini, tuongezane kwa huyo rafiki yako?’ akaniuliza

‘Ndio maana yake...’nikamwambia,

 Kesho yake tukaenda kwa huyo rafiki yangu, na taratibu zote zikakamilika nikapata huo mkopo na kuongeza bidhaa na kazi ikapamba moto. Hali ikaanza kuwa nzuri, na kila siku tukaweza kununua kifaa hiki au kile kwa ajili ya nyumbani, na nyumba ikakamilika kila kitu muhimu kikawepo.

 Akilini mwangu bado nilikuwa na wazo la kuajiriwa, maana nilisoma, sasa elimu yangu itakuwa ni hivyo hivyo tu, hapana nikajiwa na wazo la kutafuta kazi ya kuajiriwa. Nikawa hivyo, na bila kupoteza muda, nikaanza kutuma maombi sehemu ninazozitaka.

Wakati nasubiria hayo maombi ya kazi, bado nilikuwa najituma kwenye biashara zangu Hata hivyo nikaona sijakamilika ili niweze kufuatilia biashara zangu na kufuatilia baadhi ya mizigo nahitajia kuwa na usafiri wangu. Nikiona wenzangu wana magari yao, hawahangaiki sana, na mimi nikasema ni lazima na mimi niupate huo usafiri, nikaweka malengo na juhudi.

Wazo hili la kuwa na gari lilikuja kama amasa fulani, na kwa vile muda huo nilishalipa deni, na hatua tuliyofikia ilikuwa io haba,nikapiga mahesabu yangu nikaona tunaweza kununua gari, na tukiwa na gari tutakuwa tumepunguza gharama nyingi za kukodi gari wakati wa kuagiza bidhaa, ni kweli nikatafuta gari, na haikupita muda, tukalipata...tukawa na gari.

‘Huwezi amini, ...kila siku ikawa ni neema, kila hatua  na malengo yake, ...nilipopata gari watu hawakuamini, wale mawifi, na ndugu za mume wangu bado wakawa na imani ile ile kuwa huenda huyu mtu sasa anatumia uchawi ,.....mpaka katajirika, je inawezakana kweli uchawi ukamtajirisha mtu,...kama ingelikuwa hivyo, basi wengi wanye tabia hiyo wangelikuwa na maendeleo makubwa. Tembelea sehemu zenye imani hizo, uone kama wana maendeleo, hakuna kitu.

Nikiwa na gari, nikaweza kufanya mengi, hata hivyo akilini mwangu bado nilikuwa na ile ndoto ya kuajiriwa kwenye kampuni kubwa kubwa,...nikaendelea kutuma maombi ya kazi, huku biashara zangu zikiendelea, nina watu nimewaajiri sasa, wanaonisaidia kuuza duka, na sio duka, nilishaanzisha jingine, nikawa na maduka mawili...dhiki ikaanza kupotea, kidogo kidogo....

NB: Je baada ya dhiki huja nini...mambo bado hapo, tutamalizia sehemu hii baadaye, tukiubiria sehemu ya pili kwenye simulizi, sehemu itakayoonyesha changamoto, na mitihani ya kuwa nacho....unacho, na unajiona wewe ni zaidi ya mume wako..


WAZO LA LEO: Maendeleo huja kwa maarifa, kujituma, na kuwa na malengo ya kusonga mbele, usirizike na hapo ulipo, jitahidi kuongeza kipato kwa kubuni njia mbadala, na mikopo ni njia mojawapo ya kuwekeza zaidi. Lakini tuchukue mikopo tukiwa na malengo tayari. 

Ni mimi: emu-three

No comments :