Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, March 4, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-20


Yaliyotokea kwa mdada yalifanya nimuonee huruma sana, japokuwa sikuwa nafahamu undani wa yaliyomkuta, lakini nilihisi kuwa yatakuwa ni mabaya sana. Na hali hiyo ya kujiuliza ni kitu gani kilimpata, ilinifanya niingiwe na hamu sana ya kukutana na mdada, ikiwezekana anisimulie yeye mwenyewe aliyokutana nayo utotoni, ..nahisi ni utotoni, lakini hilo nahisi halitawezekana

‘Sasa ni nani atanisimulia kuhusu masahibu yake,...au nimuulize bosi...’nikajikuta najiuliza mwenyewe.

`Kitu cha ajabu, ukimuuliza ni nini kiliwahi kumtokea, au kwanini anawachukia wanaume, anaghadhika sana,.....na sasa huyo, anakuwa kama mtu aliyepagawa au mtu aliyepandisha mashetani,...mhh, nahisi kuna tatizo, sasa nifanye nini...?’ nikajiuliza.

Wakati naendelea kujiuliza, kumbukumbu za yaliyotokea muda uliopita zikaanza kunirejea akilini,....
                   

                   **********

Baada ya mwanadada kutoka na ule mnyororo, aliniambia nimfunge, na kitu kilichokuwa kikinishangaza ni ile hali ya kubadilika kwa sauti, yeye ana sauti nzuri ya kuvutia ya kike, lakini muda ule akawa kama mwanamke anayeigiza sauti ya kiume.

Ninasema kuigiza, kwasababu mimi naifahamu vyema sauti mdada, kwahiyo akiongea sauti nyingine, nitajua anaigiza, na hususani kuongea sauti ya kiume..lakini sauti iliyotoka kwa mdada, kama humjui, utasema ni mwanaume anaongea, kwani ilikuwa sauti nzito na ya kutetemeka ya mwanaume haswa.

‘Nifunge huu mnyororo haraka...’sauti nzito ikatoka na wakati huo mdada alikuwa haniangalii usoni

‘Eti nini,.....’nikauliza nikionyesha mshangao, ule mnyororo ni mnzito, lakini kwa jinsi alivyokuwa kaushika mkononi mwake, ulionekana kama kitu kidogo kwake..kitu ambacho kilinifanya nione ajabu sana, kwani namfahamu mdada, pamoja na ujasiri wake, lakini mikono yake haijashupaa kubeba vitu vizito.

‘Nimesema unifunge hunielewi, kwanza wewe ni nani....?’ akaniuliza na kunikabidhi ule mnyororo, ni kama mtu anakutupia na kwa vile ikujiandaa nao nikajikuta napepesuka, na kabla sijaushike vema akaninyoshea mikono yake, huku akiangalia pembeni.

‘Mimi sikuelewi, mdada...’nikasema bado nikiwa sina uhakika, akilini mwangu bado nilijua ni ule utani wake, na alipoona nimeduwaa akauchukua ule mnyororo na kunichapa nao...ni mnyororo mrefu wenye nguvu, na jinsi alivyouinua ule mnyororo na kunichapa nao, ni kama mtu kashika kitu kidogo,lakini kwangu mimi niliipata pata ..

Nilijikuta naserereka, ...na kwenda kujigonga kwenye ukuta, na kabla sijakaa sawa akanijia, na ule mnyororo ukiwa hewani,...alikuwa akitoa sauti ya mngurumo kama ya simba, nilipoona hivyo, niliinuka haraka pale nilipokuwa nimelala nikigugumia maumivu, nikajizoa zoa, na kuangalia mlango upo wapi,, kilichofuata hapo ni mbio,...

Na kwa vile nilikuwa nakimbia huku nageuka kumwangalia, siamini ninachokiona na kutokea, huku nina wasiwasi, woga umenijaa,nikajikuta najigonga kwenye kizingiti cha mlango, nikadondoka, haraka nikainuka, nikashika kitasa na kuufungua huo mlango, nikatoka, huku nyuma nikasikia sauti ya kicheko cha kukera.

‘Hahahahaha....halafu mnajiita wanaume...bahati yako....’ ilikuwa sauti ya kukwaruza ya mauzi, na mimi sikuangalia nyuma, nikawa nimeshatoka nje, ...na kwa jinsi nilivyokuwa naogopa, sikuweza hata kuongea na mlinzi, nililiendea pikipiki langu na kumkuta yule mlinzi akiwa kasimama karibu nalo, huku akiwa kalishikilia.

‘Pikipiki lako zuri, siku naomba uniazime kidogo, nikumbukie enzi zangu, unajua nilishawahi kuwa na pikipiki......’akasema na mimi sikumsemesha nikampiga kikumbo, akaserereka pembeni, nikalidandia pikipiki langu na kwa haraka nikaliwasha na kuondoka kwa mwendo wa kasi sana uliomfanya huyo mlinzi abakie akiniangalia kwa mshangao.

‘Vipi wewe ni adabu gani hiyo ...mbona unanisukuma, halafu unaondoka bila kuaga...kuna nini, weweeeh,....’akawa anaongea lakini mimi sikusubiria, nikawa nimeshalisukuma geti kwa ile pikipiki,na kwa vile alikuwa hajalifunga vyema, likafunguka na kwa haraka nikatika nje ya jengo hilo, na kunifanya kidogo niwe amani,nikaendesha pikipiki langi kwa mwendo wa kasi hadi nyumbani.

‘Huyu mdada ana mashetani nini, mmh, au kachanganyikiwa na madawa, lakini haiwezekani, ina maana kapata wapi zile nguvu, siamini, sasa...duuh, ...’ndivyo nilivyosema, na sikutaka hata kuwaliwazia zaidi maana kwa muda huo kichwa kilishaanza makeke yake.

‘Dawa ya hiki kichwa ni kulala....’nikasema, huku nikawazia nimpigie simu bosi, lakini nikaona ni bora ni nyamaze tu, nikapanda kitandani, na kujiegemeza huku nikijaribu kuvuta subira, huku nikijizuia kwenda kutafuta kinywaji.

‘Ukianza kusikia maumivu ya kichwa, kunywa maji mengi, jitahidi kutafuta usingizi...’nikakumbuka ushauri wa dakitari, na mimi nikainuka na kuchukua gilasi ya maji, nikayanywa, nikaongeza tena na tena...halfi kidogo kwa mbali nikasikia unafuu fulani.

‘Kitapona tu....’nikasema huku nikijizuia kukumbuka yaliyotokea, lakini kwa upande mwingine wa akili, kuna hali inaniuliza nifanya nini, maana huyo ni mfanyakazi mwenzetu nahitajika kumsaidia,...na wakati nawaza hivyo, kwa ajabu kabisa nikashikwa na usingizi. Usingizi ulionishika sio wa kawaida, ....

‘Nilikuambia nikusaidie nikupe dawa ya huyu mtu anayekusumbua, hukutaka,sasa unaona, na bado ...’sauti ikasema.

‘Dawa gani?’ nikauliza nikisikia sauti ikiniambia, sikumuona huyo mtu zaidi ya sauti

‘Yakuondokana na hayo unayopambana nayo..’sauti ikasema

‘Mimi sihitaji dawa, na kama unaona nahitaji dawa bai nipe hiyo dawa, kama unayo...’nikasema

‘Dawa yenyewe ina masharti....’ile sauti ikasema

‘Masharti gani?’ nikauliza

‘Unatakiwa uchague mawili, umuoe au umuue huyo...’sauti ikasema

‘Nimuoe,au nimuue nani?’ nikauliza kwa mashaka, na ile sauti ikawa kama inaguna , halafu ikasema.

‘Huyo anayekusumbua..’ sauti ikasema

‘Ni nani huyo anayenisumbua....?’ nikauliza na mara ...

Moyo ukawa unanienda mbio, na kuhisi kitu kikigonga kichwani kwangu, na mlio kama wa mtu anayegonga mlango, lakini ule mlio ulikuwa mkubwa wa kunifanya kichwa kiume, nikashituka, kumbe nilikuwa naota, nikasimama haraka kutoka kitandani, nikatulia nikwaza nilikuwa naota nini.

Mlango ukagongwa kwa haraka haraka, ...kumbe kulikuwa na mtu anagonga mlango, ndiye aliyenifanay nizindukane kwenye ndoto hiyo ya ajabu;

‘Nani wewe unayegonga...’nikauliza.

‘Ni mimi mtu wa usalama ....’sauti ikasema na sikutaka kuuliza zaidi, nikaenda kwenye mlango na kufungua mlango,maana nilifunga na funguo.

Nilipofungua mlango nikakutana na jamaa alikuwa mrefu, na mwili wake ulionekana shupavu, nahisi atakuwa mtu wa mazoezi,, nikamwangalai usoni, na yeye akawa akaniakzia macho, nikasema;

‘Habari yako ndugu...nikusaidie nini...?’nikamsalimia, na kumuuliza swali, maana sikutaka maongezi na mtu, nilikuwa na mambo yangu mengi kichwani. Mara yule mtu akatoa kitamblisho na kuema;

‘Mimi ni askari usalama nilikuwa na maongezi na wewe kidogo...’akasema huyo mtu.

‘Kuhusu nini?’ nikauliza nikiwa na mashaka, na akili yangu linituma kuwa huenda mdada, kapatwa na madhara.

‘Kuhusu mashitaka yaliyoletwa kwetu, kuwa kuna kundi limejitokeza, kundi hilo linatishia amani....’akasema na kunifanya nipumue kidogo, kuwa sio swala la mdada.

‘Kwahiyo umeona mimi ni mmoja wa hilo kundi?’nikamuuliza

‘Tunajaribu kuwahoji watu mbali mbali, ili tupate ushirikiano, wa raia wema, huenda katika maongezi yetu tunaweza kuligundua hilo kundi...ni kwa usalama wetu sote..’akasema na mimi sikutaka kubishana naye zaidi nikasema;

‘Sawa karibu ndani, lakini mimi sijui lolote kuhusu kundi lolote....’nikasema na kumpisha aingie ndani, na yeye kwanza aliangalia kushoto, halfu kulia kwa haraka sana, halafu akaingia ndani.

‘Nakumbuka tulishawahi kukutana kabla...’akasema

‘Wapi?’ nikauliza huku nikijaribu kukumbuka kama kweli sura hiyo nimewahi kuiona mahali, lakini sikuwa na kumbukumbu yoyote kuhusu yeye, kwangu alionekana mgani kabisa.

‘Kwenye hoteli ya Kajificheni, ukiwa mdada mmoja..’akasema na hata hivyo, sikuweza kumkumbuka, nikasema;

‘Inawezekana, lakini mimi sikukumbuki kabisa..’nikasema.

‘Unaweza usinikumbuke, maana ile siku ulikuwa umelewa sana, na nilitaka kuingilia kati, nihakikishe umefika nyumbani kwako salama, lakini ulikataa, ukasema huyo dada ni mchumba wako....’akasema na kujaribu kukumbuka kama kweli nilifanya hivyo, lakini sikukumbuka kabisa.

‘Nilisema hivyo mmh, sikumbuki kabisa, na hata hivyo, sizani kama ni mimi nahisi kama umekosea, labda alikuwa mtu mwingine....!?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Inawezekana usikumbuke kwa vile ulilewa sana...kulewa kwa namna ile sio kuzuri, maana watu wabaya wanaweza kuchukulia nafasi hiyo kukufanyia lolote baya, na sikupenda walivyokuwa wakikifanyia wale watu...’akasema na mimi nikaona huyu mtu anaweza kuniletea matatizo nikasema;

‘Samahani kuna jingine, maana najiandaa kutoka, ...kuna jingine la kuniula mkuu...?’ nikamuuliza huku nikipiga miayo ya kulazimisha.

‘Nimeanzia hapo kama kukuweka sawa, sijakuuliza maswala ya msingi, ...’akasema

‘Maswali gani ya msingi, unataka kuniuliza..?’ nikamuuliza

‘Kwanza, nikuulize wewe una mahusiano gani na mdada...’akaniuliza na kunifanya nianza kuona mashaka, nikahisi kuna kitu kimemtokea mdada, huyu mtu alitaka kunianzia mbali.

‘Hayo ni maswala binafsi, nafikiri sitaweza kukuambia lolote kuhusu hilo...’nikasema.

‘Ndio ni maswala binafsi lakini yanaweza yakatusaidia sisi, unafahamu sisi lengo letu ni jema kabisa na tunafahamu lipi ni jambo binafsi, na tukiambiwa tnafahamu jinsi gani ya kuliweka ili liwe siri, ...nikuondoe wasiwasi kuwa mahusiano yenu ya ndani hatuna maana nayo sana, cha msingi ni kunijibu, ili niweze kuendelea na maswali mengine.

‘Yule ni mfanyakazi mwenzangu,...’nikasema.

‘Sawa hilo nafahamu, zaidi ya ufanyakazi, ...nikuambie ukweli, kuna jamaa wawili nilikuja kuwauliza hivyo hivyo, wakanijibu hivyo hivyo, lakini baadaye nikawaona wpo mitaani, wanalalamika kuwa huyo mdada, kasababisha wao kusimamishwa kazi kwa muda, hata hivyo, bado waliendelea kuficha siri, siri ambayo tunaifahamu, tunachotaka tu ni ushahidi...’akasema.

‘Ushahidi gani mnautaka, kuna mtu kauwawa, kuna jambo limetokea,..?’ nikauliza.

‘Kama nilivyokuambia, kuna kundi, lenye nia mbaya, kwa jamii, na lenyewe inavyoonekana, linawalenga watu wenye uwezo, wakidai kuwa watu hao ni mafisadi,...sasa kama ni mafisadi, kama wanavyodai, kwanini wasishitaki...kinachofanyika na kuwasumbua raia wema,...nafikiri hapo kidogo nimekuweka sawa, ili uelewe lengo langu...’akasema

‘Kwahiyo unahisi mdada anahusika na hilo?’nikauliza

‘Hapana, sijasema hivyo, ndio maana natafuta ukweli, wa tetesi za watu...’akasema.

‘Tetesi za watu....ina maana watu wanasema hivyo?’ nikauliza.

‘Wanashindwa kusema hivyo moja kwa moja, maana wanaogopa, na hawajasema moja kwa moja kuwa ni mdada, na lengo letu ni kutafuta ukweli, ..’akasema.

‘Kwahiyo wewe unachunguza maneno ya mitaani, ...nilifikiri kuna mtu kashitakia, na ndio unafanay uchunguzi....’nikasema.

‘Sikiliza ndugu yangu, ikuulizi kwa ajili ya maneno ya mitaani, kuna hilo tatizo, lipo kwenye jamii yetu, limeshawakuta watu wengi,...na kila ninamuhoji, huwa anaweza keshakutwa na hayo matatizo, au anakuja kukutwa na hayo matatizo, cha msingi ni kutoa ushirikiano ili hili tatizo liishe...’akasema

‘Tatizo gani, mbona hujalisema...mimi sikuelewi, sijaliona tatizo hapo, na kwanini mimi ?’ nikauuliza.

‘Kama nilivyokuambia, kuna kundi limezuka, la watu kujifanya waandishi wa habari, au madalali, watu hawa wapo kila sehemu maalumu, wamejipanga, ...na kwa vile wamejikita kila nyanja, wanakuwa ni wepesi kuchota taarifa za watu, hasa wageni,kwa minajili ya kuwatisha na kuwaibia....wanachofanya wao ni kubuni kashfa, na kuipandikiza kwa watu wanaowalenga, na kuitumia hiyo kashfa kujiingizia kipato kisicho halali, wanadai pesa,...au chochote....’akasema.

‘Mna uhakika na hilo?’ nikauliza

‘Tuna uhakika nalo ndio maana tunafanya uchunguzi, ili tupate ushahidi, tatizo ni kuwa wahanga wa hayo yote hawataki kusema ukweli,kwa jinsi walivyofungwa, na hapo inatuwia sisi vigumu, kulisambaratisha hilo kundi, hakuna ushahidi wa moja kwa moja...’akasema

‘Sasa hiyo ni kazi yenu, ...fanyeni kazi yenu, lakini mimi siwezi kuwasaidia kwa hilo maana sijui lolote...’nikasema.

‘Una uhakika na hilo...?’ akaniuliza

‘Una maana gani kusema nina uhakika?’ nikamuuliza.

‘Wewe uandishi wa habari, ndio fani yako?’ akaniuliza na kunifanya nishituke, akawa analikunjua gazeti na mimi sikumpa muda nikasema

‘Uandishi wa habari..mimi sio mwandishi wa habari, mimi ni mhasibu...tafadhali naomba uondoke...’nikasema na yeye akatabasamu na kusema

‘Nitaondoka, hapo utakaponiambia ukweli, ....wewe kazi ya undishi wa habari, umeupatia wapi....?’ akasema akibadilika sura.

*********
 Bosi alipofika alisema mdada anaendelea vyema, na atakuwa na siku mbili zaidi za mapumziko, kabla ya kuweza kuja kazini,...

‘Oh, kwahiyo mliweza kuongea?’ nikamuuliza

‘Yah, of course , mimi na mdada tunaongea vyema kabisa kuachia maswala ya kikazi, lakini mambo yake ya nje, alipotokea , ananisimulia sana, kwahiyo namfahamu kuliko mtu yoyote...’akasema bosi.

‘Kwahiyo kumbe unafahamu mambo yake ya siri, anayoyafanya...’nikajikuta nimesema.

‘Inawezekana mengine asiniambie, maana sio kila kitu unaweza kumwambia kila mtu, kuna mambo unaweza kumwambia huyu au yule hata kama ni rafiki yako, bado utakuwa na mipaka ya mambo yako ya siri...’akasema.

‘Nilikuwa na hamu ya kusikia kuhusu maisha yake ya huko nyuma, ilitokeaje mapaka akawachukua wanaume..’nikasema

‘Ipo siku nitakusimulia, kama yeye mwenyewe akitaka nifanye hivyo, vinginevyo kwasasa ninalokuomba ni kutokumuulizia hayo...kwa ajili ya usalama wako...’akasema

‘Mhh, kwa hali hiyo utanifanya nimuogope sana mdada..japokuwa...mmh...’nikatulia

‘Japokuwa mhhhh, nini tena, sema ukweli, japokuwa umetokea kumpenda ...au?’ akauliza bosi huku akitabasamu.

‘Siwezi kusema hivyo bosi, ukumbuke mimi nina mchumba wangu, siwezi kumsaliti mchumba wangu,...,ila tu,...mhhh, kiukweli, nimetokea kumzoea sana mdada,...sio kawaida yangu kuzoeana na akina dada, kama nilivyomzoea mdada, moyoni kwangu namuona kama eeh,tuseme, dada yangu...’nikasema.

‘Nimekuelewa, uipate shida,...hata yeye kasema hivyo...’akasema bosi na kucheka kidogo.

‘Unasema hata yeye kasema hivyo, ina maana mlikuwa mnaniongelea mimi?’ nikauliza nikiwa na mashaka.

‘Ilitokea hivyo, tukakuongelea kwani aliuliza kuwa upo salama, umeweza kufika kazini, na nilipomuuliza kwa vipi awe na wasiwasi na wewe, akasema huenda alipochanganyikiwa, aliweza kukuumiza...nikamuuliza ina maana wakati anachanganyikiwa ulikuwepo, akasema ndio, ulikuja wakati yupo kwenye wakati mgumu, kama angelijua unakuja,angekuzuia...’akasema bosi

‘Hivyo tu....?’ nikauliza nikimwangalia bosi.

‘Hivyo tu una maana gani,..ulitarajia tuongee nini zaidi, kama kuna mengine ambayo unahisi ulitaka tuyaongee, haikutokea hivyo, ila alichoniotuma kwako wewe ni kuwa ujitahidi sana upitie kwake leo hii ukitoka kazini,...’akasema na mimi moyo ukaanza kunienda mbio, na kwa wasiwasi nikasema;

‘Lakini bosi umesema yeye hataki wanaume wamkaribie..sasa huoni najipeleka kwenye tatizo...?’nikasema.

‘Cha msingi ni wewe kuchunga ulimi wako, ongea mengine, lakini usimuulize maswali yaliyomtokea akiwa mdogo...ndilo la msingi, mengine ni maswala yenu binafsi mimi siwezi kuwaingilia, ila...kama kuna lolote, unahisi unahitajia msaada wangu kimawazo, mlango upo wazi,...na mapema ni bora zaidi, kabla hali haijawa mbaya...’akasema bosi

‘Kwanini unasema hivyo bosi, ....?’ nikauliza
‘Kusema hivyo kwa vipi tena, ni ushauri wangu kwako...ulitaka nikushauri vipi?’ akaniuliza

‘Nafikiria hiyo kauli uliyosema kuwa, kabla hali haijawa mbaya...’nikasema

‘Ni hisia zangu tu, maana kila siku naona kama vile wewe unajiiingiza kwenye matatizo, na akilini mwangu, ninahisi kuna jambo linakukabili, lakini hutaki kuwa muwazi kwangu..ni hisia tu, sio zaidi, ...’ akasema bosi.

‘Mhh, hapana bosi, hakuna kitu....’nikasema kwa sauti ya kutokujiamini.

‘Unaikia, nikuambie ukweli, ilivyo, na kawaida, ukiona upo kwenye hatari, unahisi hali sio nzuri, ni bora ukamuona dakitari haraka iwezekanavyo,..ili ujikinge, sio usubiri tatizo litokee ndio uende kutibiwa...’akasema bosi.

‘Lakini mimi siumwi...’nikasema.

‘Yah, kuumwa sio lazima ugonjwa, kuna matatizo ya kijamii, yenye mlengo mbaya, kuna vikwazo vya kimaisha, kuna majaribu ya hapa na pale, unaweza ukajikuta upo kwenye hatari, au unahisi hatari inaweza kutoke,....kwa majambo kama hayo, kuna watu wazuri wa kusaidia..mfano kama ni makosa ya kisheria, kuna watabibu ambao ni wanasheria, hao ndio madakitari wa hayo matatizo....sisi tuna mwanasheria wetu, wa kampuni,kwa sasa, hana kazi nyingi, tunaweza kumtumia...’akasema bosi.

‘Kwanini mwanasheria,...mimi sijafanya makosa yoyote ya umhitajia mwanasheria..’nikaanza kujitetea.

‘Sijasema una makosa...ila kama unahisia kuna tatizo linaweza kutokea au upo njia panda, ya kisheria, au kuna vitisho, vinavyoweza kukutumbukiza kwenye mattizo ya kisheria, ni bora ukajihami...’akasema bosi

‘Sawa nimekuelewa bosi,...kama nitakuwa na matatizo, sitasita kufanya hivyo,..’nikasema

‘The sooner the better.. wahi mapema kabla mambo hayajaharibika...’akasema na kuingia ofisini kwake.

Siku hiyo ilikwenda haraka sana, maana nilikuwa na kazi nyingi za kimahesabu,  na wakati napeleka taarifa za mahesebu kwa bosi, bosi akaniambia.

‘Ngoja nikusimulie kidodo, nakumbuka sehemu iliyopita tuliikatisha, na ni vyema tukamalizia sehemu hiyo muhimu kabla hatujaingia kwenye ehemu nyingine ya masiha yangu yalivyokuwa, au una kazi nikuache, tukutane kesho,...?’ akaniuliza

‘Nimeshamaliza kazi bosi, ....nipo tayari.kusikiliza.’nikasema

‘Na tukimaliza, usisahau kumpitia mdada....’akasema bosi akiangalia saa yake.

‘Mhh, nitaangalia, kama ni lazima nitakwenda kumuona, hamna shida....’nikasema

‘Kama una wasiwasi tutaongozana...’akasema

‘Hapana  sina wasiwasi bosi, , nitakwenda tu kumuona, kama ananihatajia..’nikasema

********

‘Kwanini mumemchelewesha huyu mtu....?’ aliuliza dakitari akionyesha wasiwasi kwani alisema kichwa cha mtoto kilishaanza kujitokeza, na hiyo ni hatari.

Hakuna aliyeweza kumpa jibu, na mume wangu akagizwa beseni na vifaa vingine, na mimi nikawekwa kwenye hilo beseni na kunikimbiza leba na hapo kiakili nikawa mimi na mungu wangu , kipindi hicho mume wangu alikuwa katumwa kwenda kununua baadhi ya vifaa vilivyohitajika kwenye duka lao, japokuwa alikuwa anaumwa lakini kutokana na hali yangu ilibidi kuumwa kwake akusahau.....

Tuendelee kuanzia hapo......

Namshukuru mungu, alinipa subira na kunisimamia kwani licha ya hatari iliyokuwepo kuwa huenda tukampoteza mtoto, lakini kwa uwezo wa muumba, baada ya dakika tano nikajifungua kichanga, ....nilitulia na kumshukuru mungu pale niliposikia kilio cha mtoto.

‘Hongera umejaliwa mtoto wa kiume...’ilikuwa sauti ya mkunga, na akaniletea kitoto hicho usoni,..nikakiangalia huku nikiwa sina nguvu hata ya kuinua mkono. Mkunga akakiondoa kichanga kile kwa ajili ya kukihudumia.

Baadaye ,mume wangu ambaye alitumwa baadhi ya vifaa alirejea, na mkunga akamwambia;

‘Wewe muda wote ulikuwa wapi, umeshachelewa...’akasema na kumfanya mume wangu abakie mdomo wazi,akihisi kuna hatari, docta aliyekuwa akimuhudumia mtoto, akamwangalia mume wngu, na ili kumuondoa wasiwasi, akakinua kile kichanga, na kumuonyesha, akisema

‘Hongera mzee, mumepata mtoto wa kiume, hana matatizo yoyote...’akasema huyo dakitari, na mkunga akacheka na kusema;

‘Mwanaume alishaanza kuabdilika....hongera bwana...unaruhusiwa kumkaribia mke wako...’akasema

 Mume wangu kwa furaha akasogea kwa dakitari na kumpokea yule mtoto, lakini dakitari akasema asubiri kidogo, kuna huduma anafanyiwa huyo mtoto kwanza, basi mume wangu alikaa karibu yangu akiwa anamwangalia mtoto anavyokuwa akihudumiwa na dakitari.

Baadaye tulikabidhiwa mtoto wetu, na mume wangu akawa habanduki karibu yangu akionyesha uso wenye furaha, na huku tukisubiria chakula, tukitarajia chakula cha mzazi kitaletwa kutoka huko nyumbani, lakini hadi inafika jioni, hakukuonekana dalili ya mtu kuleta chakula.

‘Mke wangu hapa naona hakuna dalili ya mtu kuleta chakula..’akasema

‘Sasa utafanya nini?’ nikamuuliza

‘Inabidi nikanunue chakula cha gengeni, hakuna jinsi hapa....’akasema

‘Pesa unazo...maana ?’ nikamuuliza na yeye bika kusubiria maelezo yangu akaondoka, nilimuonea huruma maana nafahamu kabisa anaumwa, lakini anajikaza tu.

Baadaye alirudi akiwa kabeba chakula cha gengeni na kwa mara ya kwanza nilikula chakula bila kujua kilitoka wapi,nikamshukuru mume wangu, na kujiathidi kula, ili maziwa ya mtoto yapatikane, kwani kichanga kilishaaza kudai haki yake .

Na ilipofika saa moja za usiku ndio wifi yangu akaja na chupa ya uji, akiwa kanuna, inavyoonekana hakupenda kufanya hivyo, ilikuwa kama kalazimishwa, akafika na kuitoa ile chupa iliyokuwa na uji, akaiweka juu ya meza, akaanza kuondoka, na alipofika mlangoni akawa kama kasahau kitu akageuka na kuniangalia, akasema

‘Hongera mzazi, umeleta mtoto gani?’ akauliza, nafikiri aliuliza hilo swali kwani alijua kuwa akifika nyumbani ataulizwa swali kama hilo na atakuwa hana majibu sahihi, japokuwa nina uhakika huenda kaka yao, yaani mume wangu atakuwa keshawaambia, na nahisi ndiye aliyemlazimisha kuleta huo uji.

‘Mtoto wa kiume...’nikasema

‘Mtu wewe una bahati kweli...unaujulia sana utaalamu wenu, maana wa kwanza jike, wa pili dume, unatupangilia eeh,..mmh, kweli mumechanjia, lakini usifikiria mimi bado nina furaha na wewe...nina usongo na wewe, kwa jinsi ulivyomfanyia mama yangu, mimi bado nawazia jinsi gani ya kukufanya...’akasema

‘Wifi hayo yametoka wapi tena...’nikasema

‘Ngoja urudi nyumbani, ...utajua yametoka wapi tena...ninahangaika usiku na mchana kutafuta dawa yako....labda nife, lakini nikiwa hai hivi hivi tutapambana....’akasema na kufungua mlango, akaondoka, hakutaka hata kumuangalia mtoto.sikujali, nilishaanza kuwazoea.

Nililala hapo hospitali siku hiyo na kesho yake, tukaruhusiwa kurejea nyumbani, na akilini mwangu nikisema, narudi kwenye uwanja wa vita...

NB: Itakuwaje

WAZO LA LEO: Kuna majanga yakitokea kwa mwanadamu, huleta athari kubwa kwenye ubongo wa mwanadamu, na matokea yake yanaweza yakaharibu mfumo mzima wa akili, mwili na utashi wa kufikiri. Kuna vyanzo vya matatizo hayo, na vingi vinaanzia utotoni, kwenye ajali, kubakwa na vitu kama hivyo.

Jamii sasa zinaharibika, na ukichunguza sana, chanzo kikubwa ni malezi, ukiukwaji wa haki za watoto, watoto wanakosa elimu, wanakosa malezi bora. Elimu sasa ni kwa wenye kipato,kuna tofauti kubwa inayoanzia hapa, hili haliangaliwi sana, ....jamii kubwa inakosa haki hizi, ...Tusipoangalia vyanzo vya matatizo haya, tukakimbilia kutibu, itakuwa hatujafanya lolote.


Ni vyema tukaangalia chimbuka la mmonyoko wa maadili, tukaangalia tatizo hili linaanzia wapi, na ni ukweli usiopingika kuwa tatizo hili linaanzia kwa watoto wetu wanaokosa haki zao za masingi. Tusipoziba ufa, tusipomkunja samakini akiwa mbichi,...tujue kuwa yanayotoea kwa wenzetu ipo siku yatakuja kutokea hapa kwetu.
Ni mimi: emu-three

No comments :