Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, February 3, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-7


Nikiwa kwenye pikipiki yangu nikielekea sehemu ambayo nafahamu Mdada bado yupo hapo, mara nikakutana na gari dogo, hilo gari likakatisha mbele yangu na kunifanya nisimame kwa ghafla, nikaanza kulalamika, kwa hasira

‘Wewe vipi unataka kuniua ni udereve gani huo...’nikasema huku nikiwa tayari kuteremka kwenye pikipiki yangu niende kuzozana na huyu dereva, na huyu mwendeshaji wa hilo gari, bila wasiwasi, akafungua mlango wa gari lake, na taratibu akanifuata pale niliposimama, alikuwa kavaa mawani makubwa,akanisogelea, akayavua yale mawani yake.

‘Oh, ni wewe afande, samahani, lakini ulivyofanya sio sahihi,wewe ndiye unayesimamia uendeshaji sahihi wa magari na leo unanifanyia mimi hivi, ..huoni ungesababisha ajali...’nikasema na yeye akawa ananiangalia kwa dharau, halafu akasema;

‘Nataka kukuonyesha kuwa unachokifanya, kitakuja kukuharibu, ujue kuna watu na watu, sasa angalia sana...’akasema huku akiwa kashikilia usukani wa pikipiki yangu.

‘Afande mimi sijakuelewa...’nikasema

‘Unanielewa sana, ...kwanza nikuulize Mdada yupo wapi?’ akaniuliza na hapo nikajua kumbe mwanzangu anaongelea kuhusu aliyekuwa mchumba wake.

‘Anaumwa, kwa taarifa nilizozipata anaumwa...’nikasema

‘Anaumwa au, kasakamia mipombe, ndio maana haweze kuja ofisini, nakuonya tena achana na huyo mwanamke, huyo mwanamke tunamfahamu sisi tuliomkaribisha huu mji,...’akaniambia.

‘Lakini mbona mimi sina mahusiano na yeye, mahusiano yangu mimi ni yeye ni kikazi zaidi...’nikamwambia.

‘Na iwe hivyo, ila yeye anasema kuna kidudu mtu hapo ofisini kwake,ana kamba mguuni, huyo kuku mshamba, ndiye anayetaka awe mchumba wake, sasa sijui kama ni wewe au ni nani mwingine, yoyote yule ajue kuwa huyo mtoto nimemgharamia mimi, hadi akapendeza, na sasa anajiuona kafika,hajafika....’akaniambia na akawa kama anakagua pikipiki yangu.

‘Afande mimi sijakuelewa, ...kwasababu nasikia wewe na huyo binti mumeshaachana, na wewe umesema huna habari naye tena, ulilitamka hilo mbele ya watu wenye heshimza zo, sasa iweje bado unadai ni mtu wako?’ nikamuuliza

‘Kwahiyo unataka kushindana na mimi?’ akaniuliza

‘Aaah, kwanini nishindane na wewe afande, ...sijasema mimi namtaka huyo mwanamke, mimi mbona nina mchumba wangu, ...’nikasema.

‘Mchumba wako, ungelikuwa na mchumba wako, ungelikesha na huyo mwanamke kwenye nyumba ya wageni...unafikiri mimi sijui kinachoendelea kati yako na yeye, nakushauri kwa nia njema, achana naye, ....vinginevyo, huyo mchumba wako atajua kila kitu, na hiyo kazi inayokuweka hapa mjini utaikosa, ....sio hivyo tu, unaweza ukaozea jela..huyo mwanamke ukamkosa na maisha yako ya baadaye yakaishia jela, huyo mwanamke hakufai,...’akaniambia.

‘Sawa afande mimi nimekuelewa,na nimeshakuambia mimi sina mahusiano ya kimapenzi na huyo binti....’nikasema.

‘Sawa tutaona ukweli wa kauli yao,  ila mimi nakupa siku tatu, nikikuona upo na huyo binti, utalifahamu kabila langu, huwa sisi hatutushii, nitakupiga, tunapiga kwanza , kwaheri....’akasema akinipiga begani kwa ngumi, ni kipigo kidogo, lakini nilihisi kama bega linataka kuachana na mwili,....yeye akaingia kwenye gari lake akaondoka, na mimi nikawa najiuliza nifanye nini...mara simu yangu ikaita..

‘Unakuja ....nimeambiwa na bosi unakuja, upo wapi?’ ilikuwa sauti ya mdada.

‘Ninakuja, umeshajiandaa , maana sitaki kupoteza muda?’ nikamuuliza

‘Unataka nijiandae vipi, hapa nilipo nina khanga moja tu, nataka tumalizie pale tulipoishia jana...’akasema.

‘Ina maana huumwi?’ nikamuuliza nikitaka kugeuza pikipiki nirudi kazini/

‘Ninaumwa sana, na docta wangu ni wewe,ndio maana bosi akakutuma uje kwangu, ...’nikasema.

‘Wewe huna maana kweli, ina maana huumwi, unamdanganay bosi...’nikasema.

‘Hivi wewe kwanini hutaki kunielewa, yaani huoni kuwa yote haya nayafanya kwa ajili yako, hivi wewe ni mwanaume kweli, angalia wanaume wenzako wanavyofanya,ujilinganishe na wewe. Ua wewe sio riziki.....’akasema kwa sauti kama ya mgonjwa.

‘Sikiliza Mdada, huko unapokwenda ni kubaya, hayo matusi yako siyapendi, nakuo,mba tuheshimiane, ...’nikasema kwa hasira, na kauli yake ilinikera, na moyni nikawa naingiwa na jaziba, ya kumuonyesha mimi sivyo hivyo anavyonifikiria.

‘’Kama umekasirika, onyesha hasira zako kwa vitendo, wanaume hawabembelezwi kihivyo, mimi nina mashaka na wewe...’akazidi kunikera.
‘Mdada, naomba tuheshimiane, wewe hujui unaniweka katika hali gani, ...’nikasema.

‘Nakuweka katika katika hali gani!..., sikiliza usijione wewe ni wa maana sana, wapo wanaume wananitafuta usiku na mchana, hivi wewe una nini cha kuringia, ndio huyo mchumba wako wa kijijini,mshamba kama wewe...nakuambia hivi , usipofanya nitakavyo mimi nitakatumia hako kashamba kako huu upuuzi wako, nasikia baba mkwe wako mtarajiwa ni mkali sana, .....’akasema.

‘Hayo yamefika wapi, na umeyapata wapi mambo ya mchumba wangu, nakuomba usinichafue, nitukane mimi upendavyo, lakini sio hawo,...usitake kumchokoza nyoka shimoni...’ nikasema kwa hasira.

‘Hahaha, eti nisimchokeze nyoka shimoni, hivi na wewe unaweza ukajiona una nguvu sana, au una uwezo gani,...wala usitamke maneno kama hayo, huna lolote, kama umenishindwa mimi, ujue huna lolote,...sasa unakuja au unapoteza muda tu hapo...?’ akauliza kwa hasira.

‘Nakuuliza kwanza huyo baba mkwe wangu umemjuaje, nakuona unanichimba?’ nikamuuliza, maana sijawahi kuongea na yoyote kuhusu mchumba wangu, au baba makwe wangu, yupo vipi. Ni kweli baba mkwe wangu ni mkali sana, na hadi kufikia kunikubalia niwe mchumba wa binti yake nilipata shida sana, na akanikubalia kwa masharti makubwa sana na mpja ya masharti ni kuwa nisije kumpotezea muda binti wake, nisije nikaonekana nina mahusiano na wanawake wangine.

‘Mzee mimi naahidi mbele yako, sitakuwa na mahusiano na wanawake wengine, binti yako nampenda sana, hakuna mwingine, atakayeweza kunibadili akili yangu, ...ngoja nijiweke sawa, tutafunga naye ndoa hivi karibuni...’nikamwambia.

‘Mimi nakuchunguza, popote utakapokuwa ujue kuna watu wangu wanakuchunguza nyendo zako, sasa ujifanye mjanja,...binti yangu nimemlea katika maadili mema, na atakusubiri, hadi hapo ytakapokuwa tayari, ole wako, itokee vinginevyo, ...’akaniambia na kweli mzee huyo anaogopewa sana, kutokana na wadhifa wake serikalini.

 Sasa kusikia huyo Mdada anamtaja, akashangaa, kamjuaje huyo mzee, huenda huyo mzee, keshatuma watu wake huku alipo, na akakutana na huyo mdada, wakati anawaza hayo mdada akasema;

‘Mimi nakufahamu sana, kuliko unavyofikiria wewe, ....jana nimepata kitu muhimu sana, ambacho akikiona baba  mkwe wako, ...ohoo. sisemi mengi, akiziona hizi picha, sijui kama huyo mchumba utampata tena, na jela inakungoja, ...’akawa kama anauliza.

‘Sikiliza mdada, mimi narudi ofisini, nitamwambia bosi kuwa wewe huuwmi,...’nikasema huku nikigeuza pikipikii yangu kurudi ofisini.

‘Unasema nini, hivi wewe una akili kweli, yaani sasa umevimba mapembe unapinga amri ya bosi wako, kakuambia uje unipeleke hospitalini, wewe bado upo njiani, umazubaa, unataka nini, hutaki kazi eeh...nakupa dakika kumi kama hujafika hapa, nampigia bosi wako simu na picha ya upuuzi wako juu....’akasema.

‘Ili iweje, nifukuzwe kazi, ndivyo unavyotaka, na maswala ya mchumba wangu hapa yanakujaje, kwanini husemi kuhusu mchumba wako, ambaye muda mchache aliopita alikuwa nami hapa, akinionya kuhusu wewe...’nikasema.

‘Tatizo lako wewe bado mshamba, unatishwa na mwanaume mwenzako unakubali, ina maana yeye ana nini ambacho wewe huna, wewe mwanaume gani, utaerevuka lini, ina maana mimi mwanamke ndiye ninayekuelekeza njia, kweli wewe sasa unanitia aibu, nimeshajiandaa, nakusubiri, tena fanya haraka, nisije nikapoteza fahamu, ....’akasema na kukata simu.

Nilikuwa bado nimesimama nikiwa nashindwa nifanye nini, nirudi ofisini au nienda kwa Mdada, na akilini sauti ya aliyekuwa mchumba wake, ilikuwa ikinitisha,;

‘...vinginevyo, huyo mchumba wako atajua kila kitu, na hiyo kazi inayokuweka hapa mjini utaikosa, ....sio hivyo tu, unaweza ukaozea jela..huyo mwanamke ukamkosa na maisha yako ya baadaye yakaishia jela, huyo mwanamke hakufai,....

Niliamua kutii mari ya bosi wangu, nikaenda moja kwa moja hadi kwenye ile nyumba ya wageni, kwani nilijua huyo Mdada bado yupo hapo, na nilitakiwa kwenda kulipa pesa za watu, kama nilivyoahidi

Nilipofika, sikupanda juu, nikampigia Mdada kuwa nimeshafika, nipo chini, nalipa pesa za watu, yeye akaniambia anahitaji mtu wa  kumshika mkono, maana hawezi kutembea.

‘Madada, hebu ...’nikataka kujitetea, na yeye akasema.

‘Unapoteza muda, panda huku juu, kwanini hunielewi...’akasema na mimi kwa hasira nikapanda huko juu, nikagnga chumba chake, hakuitikia, nikagonga tena, kukawa kimiya, nikafungua mlango, nilimkuta amelala kitandani.

‘Ina maana hujajiandaa?’ nikamuuliza

‘Unataka nijiandae vipi,..nilikuambiaje kwanza tumalize ile kazi tuliyoianza jana,...’akasema huku akiondoa shuka alilokuwa kajifunika,..sikuamini, na mara mlango ukagongwa.

‘Oh, nani huyo tena, a..’akauliza mdada, na mimi nikageuka, kuangalia mlangoni, mlango ukafunguliwa, na aliyekuwa kasimama mlangoni ni afande.

‘Hongera ....sikujua kuwa umejificha hapa, na ndio mipango yenu, badala ya kuwa kazini, mnakuwa kwenye nyumba za wageni, muda kama huu,...’akasema huku akiwa kashika kiuono.

‘Hivi wewe mwanaume unanitafuta nini,....’akasema mdada

‘Umesahaueeh, ni nani aliyekuingiza hapa mjini, umesahau eeh, ni nani aliyekufanya upendeze, na kuonekana mrembo, lao hii, ndio unatembea ni huyo bwege....sikiliza mimi sikuja hapa kuzozana na wewe,ninachotaka ni gharama zangu, nataka kesho uondoke kwenye nyumba yangu, unasikia,.....na mengine yatafuata baadaye...’akasema

‘Usinitishe wewe, nyumba gani yako kwako, hebu nenda ardhi udai kuwa hiyo nyumba ni ya kwako, ina jina lako....hivi wewe unaniona mjinga sana, au...ulipotoa vipesa vyako, nilikuomba, siulikwua unanishaua mwenyewe tu, na ni pesa gani uliyonipa ambayo ingeweza kujenga nyumba kama ile...nina hati ya mkopo wa benki, ambayo inathibitisha hilo, ....’akasema na yule afande akageuka kuniangalia, na kusema;

‘Unasikia..huyo ndiye mdada, kuna kitu anatafuta kutoka kwako, mimi nakiri kuwa nimekuwa mjinga wake, lakini sitakubali yaishe hivi hivi....yoyote atakyetumbukiza mguu kwake, atalipa hizo gharama,....upo tayari?’ akaniuliza

‘Mimi hayanihusu...’nikasema na kuanza kuondoka.

‘Wewe unakwenda wapi, bosi kakutuma nini, unataka kuniacha hapa, ni nani atanipeleka nyumbani?’ akaniuliza na mimi nikamwangalia huyo afande, na huyo afande akaanza kuondoka.

Nikageuka kumwangalia mdada, ambaye bila kujali alinuka pale kitndani akiwa uchi, na kuelekea bafuni, ....

*********

Ilikuwa asubuhi, wakati bosi alipoingia alinikuta nipo kwenye meza yangu nikiwa kwenye dimbwi la mawazo, nikiwazia picha aliyonitumia mdada, ikionyesha siku ile alipotaka kunifanyia ujanja wake, na ilikuwa ni bahati sana , kwani ilishafika hatua ambayo nilishaamua kufanya atakavyo, aliyekuja kuniokoa ni muhudumu, alifika na akiniambia pikipiki yangu ipo sehemu isiyoruhusiwa.

Nikazindukana kiakili, na haraka nikajiruudi, na kumshukuru sana huyo muhudumu kimoyoni, kwani kama isingelikuwa yeye, huenda ningeliingia kwenye mtego wa huyo Mdada, lakini hata hivyo, kumbe mdada, alishachukua picha za tukio hilo, na picha hizo zipo wazi, hauwezi kukataa, zinaonyesha wazi, nikiwa na dhamira ya zati ya kutenda tendo hilo ....

‘Huyu mwanamke ananitaka nini, ana nini anakihitaji dhii yangu, sizani kwamba ni mapenzi tu, sizani kama ananipenda kama anavyodai yeye, nahisi kuna jambo jingine analitafuta kwangu, ..’nikawa nawaza.

Nikaangalia hiyo picha na kukumbuka sauti ya maneno yake aliponipigia simu baada ya kunitumia hizo picha, alisema;

‘Hii ni moja ya picha ambayo natarajia kumtumia baba mkwe wako, unaona jinsi ilivyotoka vizuri, je akiiona unafikiri atasema nini...ole wako, nakupa siku tatu, utimize lile nililokuambia, kuanzia sasa mimi ni mpenzi wako, ukitaka niwe wa siri, fanya nitakavyo, lakini kama unataka nidhirishe wazi kwa watu, endelea kunikaidi...’akamaliza.

‘Lakini kwanini unanifanyia hivyo?’ nikamuuliza

‘Kwasababu na kupenda, na moyo wangu hautatulia mpaka uwe mpenzi wangu...’akasema

‘Lakini mimi nina mchumba tayari, nimeshakuambia hilo...’nikasema na yeye akacheka na kusema.

‘Mimi na yeye ni nani zaidi, hebu angalia sura yangu na yeye, ...huyo ni mchumba tu, unaweza ukaachana naye, ...’akasema.

‘Siwezi kufanya hivyo,...’nikasema.

‘Utaweza tu, hilo nakuahidi, labda nisiwe hai...’akatamka na kukata simu.

Bosi alinisalimia na kuingia ofisini kwake baadaye akaniita, na kuniuliza habari za jana, kwani jana niliporudi sikumkuta, alikuwa katoka na hakurudi kazini,

‘Nilipofika alisema anajisikia vizuri, hahitaji kwenda hospitalini, alishakunywa dawa...’nikamwambia.

‘Nilijua tu huenda ni ulevi, ...ok, sasa ngoja nikusimulia kisa changu kidogo, maana baadaye natoka nina kikao na wenzangu , kama nitawahi kurudi tutaendelea...’akasema

‘Sawa bosi..’

‘Unakumbuka tulipoishia, siku ile nilipopigwa na ndugu zangu ....’akaanza kusimulia

******

Waliponiona nimepoteza fahamu huku damu zikinitoka kwenye tundu za puani mdomoni, ...wakashituka, wakajua wameshaniua,..wakaniachia na kumwita dada yangu wa kambo kuniangalia;

‘Nyie mbona mumeua...’akasema huyo dada, lakini wakati huo sikimsikia, nilihadithiwa hivyo.

‘Hajafa huyo anajifanya kama kafa ili tusiendelee kumpiga..’akasema mwingine.

‘Hebu muangalie, kama kafa, tunalo, ...’akasema mwingine.

‘Tukamwagie maji, ili hizi damu zisionakena...’akasema mwingine.

‘Na haya majeraha je?’ akauliza mwingine.

‘Atajua mwenyewe, si kajitakia, ...tutaishije na mwanamke malaya humu ndani..’akasema mwingine.

Wakati huo kwa mbali nilishaanza kupata fahamu, hata wakati wananiinua kunipeleka bafuni, nilikuwa nimeshazindukana, lakini mwili mzima ulikuwa ukiuma, na damu bado zilikuwa zinatoka, na wakamuita mfanyakazi wa ndani ili amsaidia dada huyo wa kambo kuniosha hayo majeraha.

Waliponimwagia maji nikasikia nguvu ikinireja japokuwa bado, nilikua na maumivu makali sana mwilini kutokana na majeraha, walipohakikisha damu zimesita kutoka, wakanichukua hadi chumbani, na huko wakanifungia, bila hata ya kujali kunipeleka hospitalini, yule mfanyakazi alinipa dawa za kutuliza maumivu. Nikawa najiuliza ni kwanini nipigwe kiasi hicho, kuna kosa gani nimelifanya hadi kupata kipigo kama hicho, sikuweza kupata jibu.

Nilikaa mle ndani chumbani huku nikishindwa hata kulia, ila nilikuwa naumia ndani kwa ndani,nikiwaza na kuwazua, hicho kipigo cha masaa yote hayo, kama wanapiga mwizi kilikuwa cha sababu gani, baadaye mlango ukafunguliwa, na yule mfanyakazi wa ndani akaniambia ninaitwa na baba na mama, nikajikongoja hadi hapo varandani, niliwakuta baba na mama wamekaa wanaongea,  hawakuniuliza kwanini natemeba hivyo, wakaanza moja kwa moja na aliyeanza kuongea ni baba ;

‘Sisi tumeona uondoke hapa nyumbani, tumeona urudi ukakae na mama yako mzazi huko kijijini...’akasema

‘Mimi nimekushindwa kuishi na wewe, sitaki kuja kulaumiwa kwasababu ya tabia yako chafu....’akasema mama wa kambo.

Na kweli nikatafutiwa usafiri wa siku hiyo, na kwa haraka nikasafiri kwenda huko kijijini kwa mama huku mawazo yakiwa pale pale kuhusu sababu gani hasa iliyofanywa nipate kile kipigo cha masaa yote yale, nilifanya kosa gani kubwa , kiasi cha kupigwa kama mwizi,, tena wanaonipiga ni kaka zangu, je walitaka kuniua, na kwanini mara kwa mara walikuwa wakinipiga mateke ya tumboni,....

Nilipofika kwa mama kijijini, ile kumuona tu, nikaanza kulia, nililia sana, na mama akajaribu kinisihi nisilie kwani yote ni maisha, na maisha yana mitihani mingi.

‘Mwaanngu usilie, kama wamekukatisha shule, ipo siku utasoma, shule zipo tu,...’akasema mama akijua kuwa kilio changu ni kwasababu ya kukatishwa shule.

‘Mama naona heri nikae huku huku tu,maana nikirudi huko wanaweza kuniua’nikasema.

‘Usijali tupo pamoja,...japokuwa sina uwezo wa kukusomesha lakini ipo siku utasoma, kwani kuna nini cha zaidi mbona upo hivi, uso kama umevimba, ulikuwa unapigana?’ akaniuliza.

‘We mama acha tu, sitaki hata kukusimulia nisije kukuumiza moyo wako, namuachia mungu...’nikasema, na kweli sikutaka kumuhadithia mama, kwani niliogopa nitazidi kumuumiza, wakati yeye ana matatizo mengi ya kimaisha, niliona hayo mateso yawe mimi na hawo walionifanyia na mungu peke yake ndiye atawalipa, nikakaa kimiya.

 Siku iliyofuata nikashangaa ugeni ukifika nyumbani, walikuwa baba na mama wa kambo, na walipofika tu, wakaitisha kikao, na mimi nikaitwa;

‘Nimeamua kuitisha hiki kikao maalumu, ili kuliongelea swala la huyo mtoto wako, nafikiri keshakuelezea mengi, na anaweza akakudanganya kutokana na tabia yake chafu,...’akasema baba.

‘Mhh, mbona mnanitosha, hajanieleza jambo baya, zaidi ya kukatishwa shule, na hilo limeniuma sana, kwanini mumkatishe mtoto shule, tena ikiwa imebakia muda mchache tu, amalize...’akalalamika mama.

‘Ina maana yeye hajakuambia sababu ya kukatishwa shule, ...hawezi kusema maana ana madhambi mengi sana...’akasema mama.

‘Mtoto wako ni muhuni, akienda shuleni hasomi, kazi ni kufanya umalaya, ndio maana nikaamua kumsimamisha shule..’akasema baba, na mama akaniangalia kwa mashaka, hakuamini maneno hayo , akaniangalia kwa macho yaliyojaa mshangao.

‘Jana tu, ndio tulipata madhambi yake kwa undani, na ni makubwa zaidi ya tulivyofikiria,na ndio maana tukaamua kumleta huku haraka iwezekanavyo,...’akasema baba.

‘Jana kuna mtu katupigia simu, kutuelezea yote anayoyafanya huyu binti, hata mimi mwanzon I sikuamini, lakini huyo mtu aliyetupigia simu ni mtu mwenye heshima zake, akasema kuwa huyu  binti ana mahusiano na kijana mmoja wa kutoka huko moshi, anayeishi maeneo ya huko tulipo....’akasema baba

‘Hivi hayo mnayoniambia ni kweli,...ina maana huyu mtoto wangu kabadilika kiasi hicho?’ akauliza mama kwa mshangao.

Mimi pale nilipokuwa nimekaa, nilishikwa na butwa, sikuamini, kwakweli nilishtuka sana , maana huyo mvulana, sikuwa na mawasiliano naye tena, baada ya kufukuzwa shule, muda mwingi nilikuwa nyumbani, hayo wanayosema yametoka wapi...

‘Na isitoshe, katika umalaya wao huo, alifikiwa akapewa mimba, na kuitoa...’akasema mama wa kambo, na kauli hiyo ilimfanya mama ashituke hadi kuangusha kikombe alichokuwa kakishika mkononi, mama akaniangalai kwa macho yaliyojaa uchungu, woga, na kukata tamaa, na mimi nilipomuona mama alivyoshituka na jinsi slivyokuwa akiniangalia, nikaona nijitetee, na kusema;

‘Mama sio kweli, wananisingizia sijawahi kufanya hivyo....’nikasema na mama akaninyamazisha kwa mikono , na kusema;

‘Mimi siwezi hata kuamini, ina maana mtoto wangu ndiye kabadilika kisai hicho, ...sio mtoto wangu ninayemfahamu ....hapana,..hapana...’akasema mama huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa huzuni, alionekana kubadilika usoni, na nilihisi anaweza akadondoska kwa shinikizo la damu, ndio maana sikupenda kabisa kumwambia mambo hayo.

‘Kama mnabisha, ushahidi upo, mimi nimeona ni heri ukamkague mwanao mwenyewe,nendeni na mke mwenzako mkakague, ili uhakikishe mwenyewe, maana nafahamu utasema tunamsingizia..’akasema baba.

‘Mimi naona hilo litakuwa jambo sahihi...’akasema mama wa kambo akijiamini, nahisi alikuwa na uhakika kuwa kweli nimeitoa hiyo mimba, na mimi ni mlaya, lakini kwa upande mwingine,nikakumbuka hicho kipigo, walichkuwa wakinipiga, kililenga nini, huenda walifanya vile ili niumizwe,lakini yote nikamuachia mungu.

‘Lakini mimi naona hilo sio jambo jema, hata kama imetokea huyo ni mtoto wetu cha muhimu ni kukaa naye tumkanye tumelekeze...’akasema mama, huenda na yeye alishanihisi vibaya, kuwa huenda ni kweli ni yeye ataadhirika kuwa mimi ni muhuni, mimi nikasema;

‘Wazazi wangu mimi sijawahi kufanya hivyo...’nikasema.

‘Mwanangu una uhakika..?’ akaniuliza mama.

‘Mama mimi sijafanya kama wanavyodai wao...’nikajitetea nikiwa nalia kwa huzuni

‘Unasikia alivyomuongo, ..sasa ili uthibitishe uwongo wake,kama hujawahi kufanya hivyo, itaonekana, mchukueni huko ndani mkamkague, mimi nina uhakika na hilo....namfahamu sana huyu mtoto wako, ni malaya, ananitia aibu mimi...’akasema baba
.
 Kwakweli, kauli hiyo ya baba iliniuma sana,alipoonyesha kuwa ni kweli kuwa mimi ni muhuni, malaya, na nimetoa mimba, na zaidi anataka nikaguliwe,chuki dhidi ya baba ikanijaa, lakini moyoni nikamuonea huruma, kuwa baba anashinikizwa katika mambo ambayo hayajui, ipo siku atafahamu ukweli,..nafahamu kabisa kwa hivi sasa sio yeye, yote hayo ni kwasababu ya mama wa kambo.

Basi wazazi wangu hawo mama na mama wa kambo wakanichukua hadi chumbani, wakaniambia nijiandae, nikaenda bafuni nikaoga, na baadaye niakrudi hapo chumbani, nikawekwa mkao wa mama mja mzito anayetaka kujifungua, ili eti nikaguliwe..

Nilikubali kuzalilishwa hivyo, ili moyo wao urizike, nilifanyiwa huo uchunguzi na mama yangu mzazi na mama wa kambo....baba akiwa anasubiri taarifa...

NB: Je kuligundulikana nini, je ni kweli mpendwa alikuwa katoa mimba


WAZO LA LEO: Tukwepe kutoa kauli za kashifa kwa wenzetu bila kuwa na ushahidi nazo, hasa kauli za umalaya, uchawi, wiz ink, kauli kama hizi ni nzito sana, ni nyepesi kuzitamka mdomoni lakini ni kauli zinaziumiza sana hasa kwa mtu ambaye hajawahi kuzitenda.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hello there! This is my 1st comment here so I just wanted to give a quick shout out and tell you
I truly enjoy reading through your articles.
Can you recommend any other blogs/websites/forums that go over the same subjects?
Thanks!
My homepage ; myanmar airways