Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, February 26, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-18


Kwa mara ya kwanza nilianza kuingiwa na wasiwasi na mambo ya mdada, nilijiona nimewekwa kama ngao, na kutumiwa kama mpini wa shoka, ...nikawa kila mara nikiikia simu,naogopa nikijua inatoka kwa mdada, na hata nilipopigwa na watu wengine, nilihisi kuwa ni yeye, nikawa naogopa kupokea.

Kutokana na hiyo hali nikaona ni bora niongee naye nione jinsi gani nitaweza kuondokana na hiyo hali,lakini nitamuanzia vipi, kwani nafahamu kabisa nikijifanya ni mnyoge kwake, ndio atazidi kuvimba kichwa na kuzidi kunizihaki, na nikijifanya ni mkali kwake, anaweza kuniumbua kwa kuyatuma hayo mapicha mabaya, .

'Kwahiyo nifanyeje...?' nikajiuliza.

Simu yangu ya mkono ikalia, nikashtuka hadi kuidondosha chini, na nilipoangalia mpigaji nikaona ni matangazo ya biashara ya makampuni ya simu. Kwa hali iliyofikia, ninaweza kushikwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, kwani mawazo, wasiwasi, na kutokujiamini, vilikuwa vimeteka hisia yangu, japokuwa kichwa kilikuwa hakiumi kama zamani, naona kilishaanza kuniachia.

'Sasa nifanyeje,....?' nikaendelea kujiuliza

'Au nikatae kumtii, nione kutatokea nini, mhh, hilo siwezi, nafahamu kabisa kwa mdada nikikataa, muda huo huo atayatuma hayo mapicha.

 Nikashika kichwa nikiwaza, halafu nikawa naongea peke yangu kwa kusema;,

'Au niongee na baba mkwe wangu nijaribu kumuelezea hali halisi, ili hata mdada akipeleka hayo mapicha, ajue jinsi gani ya kunisaidia, lakini je ataniamini ...hilo la kuongea na wakwe zangu, nililiona halifai kabisa ni kujiabisha...namfahamu sana baba mkwe, ataniuliza maswali mengi ambayo yatakuja kuniumbua.

Wakati nawaza hili na lile mara akilini, nikakumbuka onyo  kutoka kwa wale wahanga wawili wa huyu mdada;

‘Kama ulishaingia kwenye mitego yake, jaribu kukataa, hebu jaribu ili uone atafanya nini..mwenzangu hapa alijaribu, ...huko kwao akienda sasa hivi anaingia usiku, mtaa wote wanamfahamu kuwa ana.....

Mtaani kote wanamfahamu kuwa ni nani....’ hapa alikuwa na maana gani, kuna nini alifanyiwa huyu jamaa, ....huenda alifanyiwa mabaya zaidi yangu...'nikawa naongea  peke yangu.

'Mhh, hebu niangalie , mfano nikimkatalia, atakachofanya ni kupeleka hizo picha kwa baba mkwe, baba mkwe kwa vyovyote ataniuliza, nitamuambia nini, nitamuambia ni uwongo, mmh, yale mapicha yalivyo yanaonyesha kila kitu, lakini baya zaidi, nafahamu kwa kunikomoa atayasambaza hayo mapicha kwa kile anayemfahamu kuwa ni mtu muhimu kwangu, hadi kwa mchumba wangu,...oh, nimekwisha, ...

'Mhh, hapa sasa sina ujanja..'nikasema
'Baya zaidi baba mkwe anamtumia mdada kunichunguza nyendo zangu, kwahiyo anaaminika zaidi ya kwangu, kwahiyo kwa mdada ni rahisi kabisa kuniharibia maisha yangu...haiwezekani, ni lazima nifanye jambo, ni lazima niyanyamazishe haya mambo,...na ili nifanikiwe, ni mpaka nijua wapi alipoficha hayo mapicha.

'Ni lazima nitafute dawa ya hili tatizo,...sasa ni dawa gani?' nikajiuliza na kujiuliza swali hilo hadi nikahisi kichwa kinazunguka.

Wazo likanijia kuwa huenda kayahifadhi hayo mambo yake kwenye simu yake na kwahiyo nimvizie akiwa ofisini niichukue simu yake bila kujua nifute kila kitu...lakini sizani kama simu yake hiyo inaweza kuhifadhi hayo madude yote, ni lazima kahifadhi kwenye mtandao. Kama ni kwenye mtandao itakuwa ni vigumu sana, kwani ni mpaka nijue anavyoingia. ...simu ilinishitua, ulikuwa ujumbe wa maneno unaingia, nikaufungua nikiwa na tahadhari, ulikuwa ukisema;

‘Jiandae, jamaa kama hataleta pesa leo, kama alivyoniahidi, kesho natoa kubwa lake..uwe makini na nyendo zako..’ujumbe hauna namba, nikafahamu kabisa unatoka kwa mdada, hapo nikazidi kuchanganyikiwa

‘Sasa nifanyeje,...’nikajiuliza na baadaye simu yangu ikaita, nikapokea,

‘Ujumbe huo ni muhimu, kuwa makini, ...hata hivyo naona aklainika, nimemtumia kombora moja, kashikwa na kimuhe muhe, .'akasema na mimi nikawa kimiya.

'Sasa sikiliza nataka uje hapa hotelini haraka, nimepanga kukutana naye huyu mtu, kasema atauleta huo mzigo wangu hapo, lakini simuamini, .....’akasema

‘Sasa mimi nije kufanya nini, ....?’ nikauliza nikitamani nizame ardhini.

‘Hivi nilikuambia nini, ...unatakiwa uifanyie kazi pesa unayoipata, pesa haipatikani kirahisi kihivyo...uje haraka, sitaki maswali...’akakata na mara ujumbe wa simu ukaingia, nilipofungua nikakutana na yale mapicha mabaya, kwa haraka nikajiandaa na kuondoka kuelekea huko hotelini.

‘Sasa naona ili niweze kufanikiwa kumpata huyu mtu, ni lazima niwe karibu naye, nikigundua tu ni wapi anaficha siri zake, basi nitahakikisha nazifuta zote, halafu na mimi naanza kivyangu,..ikibidi ni lazima niwe ninafika nyumbani kwake, kitu ambacho sikukipenda, siku zote nakwepa sana kuonekana nyumbani kwake.

‘Ni lazima nijenge rafiki wa uwongo, ...nitagundua ni wapi anaficha huo uchafu wake...’nikasema kimoyo moyo, huku nikiwa nimeshatoka nje, na kama kawaida nikakutana na mzee mwenye nyumba.

‘Kama kawaida yako na leo una dharura...’akasema

‘Ndio mzee...’nikasema

‘Nikuambie ukweli, kama huyo mtu anakusumbua niambie nitakusaidia,..mimi najua dawa zao watu kama hao....’akasema

‘Mtu gani huyo mzee?’ nikamuuliza

‘Huyo anayekuita muda kama huu, mimi nafahamu mambo mengi...maana huyo mtu atakufanya usiwe na amani katika maisha yako, na nahisi ni mwanamke...’akasema

‘Mzee, ni mambo ya kikazi tu...’nikasema huku naondoka.

‘Mambo ya kikazi eeh, kazi gani za usiku, unanitaia mahaka wewe mtu, isije nikawa naficha jambazi kwenye nyumba yangu, ...kila siku usiku una dharura,..ni lazima niwaambie polisi wakufuatilie...’akasema huyo mzee mwenye nyumba lakini sikumsikia kwani nilishaondoka kuelekea huko aliponiitia mdada.
*********  

Kesho yake nilifika ofisini mapema, nikiwa bado na usingizi, sikutaka hata kukumbuka mambo ya jana, na nilielekea moja kwa moja kwenye ofisi yangu, na humo nikakaa na kuinamisha kichwa ili nipunguze usingizi, na kweli usingizi ukanipitia, tena wa nguvu ...

‘Nikuambie dawa ya huyu mtu..?' nikaulizwa

'Dawa gani ...?' nikauliza

'Ya huyo mtu anayekusumbua ....dawa yake ni ndogo tu,....’sauti ikaniambia nikageuka kumwangalia huyo mtu, kwani alikuwa akiongea akiwa nyuma yangu. Nikageuka ili nimuone huyo mtu, ...lakini nilipogeuka ikuona mtu yoyote, nikasikia tena nyuma yangu, akiuliza swali hilo hilo, na safari hii nikamuuliza

‘Dawa yake ni nini?’ nikamuuliza lakini nilichosikia ni kicheko, kicheko kiliendelea kwa muda kwenye kichwa changu mpaka nikajisikia vibaya, na ghafla nikashituka,

‘Wewe vipi unalala ofisini mpaka unaota,..ndoto za mchana mbaya, ndoto kama hizo zinaweza kukuashiria jambo la kweli, ...kwani unatafuta dawa ya nani?’ akaniuliza bosi.

‘Dawa, dawa gani?’ nikauliza kwa mshangao huku moyo unanienda mbio,

‘Wakati naingia, bahati nilikuwa naongea na simu, kuna mtu alikuwa akinichekesha kwenye simu,...'akasema.

'Anakuchekesha kuhusu nini?' nikauliza huku nikijaribu kuweka akili yangu sawa.

'Anasema kuwa yule jamaa wa mamlaka ya ushuru, kakosana na mke wake, ndani ya hiyo nyumba, hakukaliki, na huenda wakaachana, na wakiachana, ina maana huyo jamaa hana kazi, mke wake ndiye aliye,mpigia debe hadi kupata hiyo kazi....’akasema bosi.

‘Kwasababu gani?’ nikauliza

‘Si kuhusu ile kashfa ya kuonekana huko kwenye mahoteli akifanya uchafu wake, ...mke wake kasema atachunguza mpaka ajue ukweli wake...’akasema bosi.

‘Oh, ndio imekuwa hayo...’nikasema nikimwangalia bosi kwa mshangao.

‘Dunia hii kuna mambo,mhasibu ukioa tulia na mke wako, kwani hao wanawake wengine wana nini cha zaidi, kitu ni kile kile, cha muhimu ni kuambizana ukweli, kufundisha, wewe unafahamu hiki mfundishe mwenzako, wewe unataka hivi muelekeze mwenzako, ni kazi rahisi tu ...h'akasema bosi.

'Kwahiyo unahisi ni hayo tu...?" nikajikuta nimeuliza hivyo.
'Zaidi ya hayo, kuna watu wametumia mwanya huo,kutafuta pesa, kuna watu wajanja, na si ujanja, ni utapeli...'akasema bosi.

'Ina maana akitoa pesa yatakwisha?' nikauliza

'Nijuavyo mimi, pesa za watu kama hao hazitohi, na watu kama hao, wanahitajia pesa nyingi sana, maana wanamfahamu kuwa ni mtu wa kuchezea pesa, ....’akasema bosi.

‘Ina maana watu wanafanya hayo kwa ajili ya kupata pesa, hawaogopi, ...?’ nikauliza

‘Wanaogopa,lakini wamechukua hatari hiyo mikononi mwao, ...wapo tayari kufa, na mara nyingi wanawatumia watu wengine, wahusika huwa hawajitambulishi, na hata wakijitambulisha, ni lazima kuwe na mtu kati, anayetumiwa kama mpini wa shoka...’akasema

‘Mpini wa shoka?’ nikauliza huku nikijaribu kukumbuka hayo maneno nimeyasikia wapi.

‘Eeeh, ili shoka likate mti, ni lazima liwekewe mti...unaona, ili huyo mtu afanikiwe ni lazima atumiwe watu...sasa hao watu wanaotumiwa ndio wanakuwa kwenye hatari, mwenzao anayeneemeka keshajipanga, anajua jinsi gani ya kujilinda, wajinga ndio waliowao....’akasema bosi.

‘Mhh, sasa hiyo hatari....sijui watafanya nini kumkwepa mtu kama huyo...’nikasema kama nauliza

‘Tatizo la ammbo hayo ukihajiingiza kutoka inakuwa ni vigumu, maana ukijitoa, wahusika watakutilia mashaka, kuwa unaweza kuwauza, kwahiyo kujitoa kwako ni kuuwawa....’akasema bosi

‘Unasema kweli..mungu wangu...’nikasema huku nikisimama na bosi akaniangalia kwa mashaka, na kuniuliza

‘Vipi kwani, mbona unanitisha...?’ akauliza bosi

‘Hapana bosi nimesahau flash yangu nyumbani na ina vitu muhimu sana...’nikadanganya, na bosi akaniangalia bado akiwa na uso wa kunishangaa

‘Haah, yaani...oh,  umenishtua kweli kweli,...ulivyotoa hayo macho,...utafikiri kuna kitu kibaya umesikia, utadhania unahusika na hayo tuliyoongea, au mhaibu unahusika nini...?’ akaniuliza akiniangalia kwa wasiwasi.

‘Hapana bosi... kuhusika kuhusu nini, ...hapana sio hivyo...’nikawa najiuma uma.

‘Sikiliza mhasibu, usiwe na wasiwasi na kazi, kama ni hiyo flash, na ina vitu muhimu huhitajii kushituka hivyo,..., baadaye utaiendea, ila kama kuna kitu kingine ni bora ukaniambia mapema iwezekanavyo, ili tuone jinsi gani ya kusaidiana,...’akasema.

Kuna wakati moyo wangu ulitaka nimuambie bosi wangu kila kitu ili nione kama anaweza kunisaidia, lakini nilichelea, maana sijui bosi na mdada wanajuana vipi zaidi, naona kama vile, bosi anamlea huyo mdada kama mdogo wake, ...

‘Leo nitajaribu kumwambia kidogo...’nikasema kimoyo moyo.

‘Sikiliza mhasibu kama kuna tatizo kubwa, na unaona upo hatarini niambie mapema kabla halijafika kubaya, maana ukiingia kwenye matatizo makubwa, mimi sitaweza kukusaidia, wakati ni sasa...’akasema

‘Bosi, nitakuja kukuambia tu...lakini..sina matatizo, ni kuchoka tu...’nikasita.

 ‘Huna matatizo kweli wewe, kwanza nimekukuta umelala, unaota,..unaweweseka, unaonekana haupo sawa, .....sasa tuanongea, ghafla umebadilika, na kutoa jicho la uwoga, ni kama vile umeona kitu cha kutisha, niambie ukweli una tatizo gani...?’ akaniuliza na mara mlango ukagongwa, akaingia mdada.

‘Bosi samahani nilikuwa anomba ruhusa kidogo, nimesahau flash yangu nyumbani,...’akasema na bosi akaniangali, na kusema

‘Wote mumesahau flash, mbona mna mambo...’akasema bosi

‘Nani mwingine kasahau flash...?’ akauliza mdada, na bosi hakusema kitu akageuka kuingia ofisini kwake, nikabakia na mdada, na mdada, akaniangalia kwa mashaka, akanisogelea na kunionyeshea kidole, akasema;

‘Ole wako.....uje kutoa hata kauli moja, ...utaumbuka, na utakuja kujijutia katika maisha yako yote...’akasema

‘Kwani vipi?’ nikauliza nikionyesha wasiwasi.

‘Nimesikia bosi akikuambia umweleze una tatizo gani, sasa ropoka, uone ...nafanya haya kwa kukusaidia, ile pesa itumie haraka, maana pesa kama hizo, hazina muda,...’akasema na kunifanya nikumbuke zile pesa alizonipa jana

Mara simu yangu ya mezani ikaita, nikainua kusikiliza alikuwa bosi akaniita ofisini kwake na mdada akanisogelea na kunifinya, hadi nikasikia maumivu, halafu akaniogelea na kunishika, akawa kama anataka kunikumbatia, akasogeza mdomo wake karibu yangu, akama anataka kunibusu, nikawa nimetulia, .hakunigusa, lakini mapigo ya moyo yalikuwa yanakwenda mbio kupita kiasi, akaniachia ni kunisukuma;

‘Hahahaha....’, akacheka na kukiweka kidole chake kwenye mdomo wangu na  kusema;

‘Masikini mhasibu anatia huruma....’. akafungua mlango na kuondoka, na mimi nikainuka kuelekea kwa bosi.

*******
`Vipi umeshakaa sawa, maana ulikuwa haupo sawa,..’ akasema bosi.

‘Nipo sawa bosi, naona usingizi umekwisha niliamuka asubuhi sana, na nilipofika hapa nikaona nipunguze usingizi, na wakati nimelala ndio nikawa naota ndoto mbaya...’nikasema

‘Ina maana ni ndoto ndio ilikuwa inakusumbua vile....pole sana, maana kuna ndoto nyingine zinatisha, au kuna jambo umefanya, maana wewe sasa naanza kukutilia mashaka...’akasema bosi.

Mimi akilini mwangu kauli ya mdada ikawa inanijia akilini;

‘huku nikikumbuka kauli yam dada ; Ole wako.....uje kutoa hata kauli moja, ...utaumbuka, na utakuja kujijutia katika maisha yako yote...

`Hakuna kitu bosi, niamini,...’nikasema

‘Sawa... kama una uhakika na hilo mimi siwezi kukushurutisha, ila kumbuka mapema ni bora kuliko kuchelewa, kama kuna jambo unalohisi linaweza kukuletea majanga uniambie ,...tuna mwanasheria, anaweza kukushauri kama unaona ni la hatari...’akasema bosi.

‘Bosi mwanasheria wa nini, hakuna kitu bosi...’nikasema.

‘Haya ngoja nikusimulie kisa changu huku unafikiria, ....tuanze pale nilipoishia, pale alipokuja mfanyakazi wa nyumbani na kusema ni funge duka...’akasema..........

‘Dada funga duka haraka twende nyumbani.....’akasema huku kashikilia kichwa na anaonekana kama anataka kulia, nikamuuliza kuna tatizo gani

‘Kwani kuna nini?’ nikamuuliza.

Yule mfanyakazi akasema wifi yangu alimchukua mtoto wangu na kumfungia nje na mvua kubwa ilikuwa inanyesha...

‘Unasema nini, ooh, sasa mtoto yupo wapi...?’nikamuuliza huku nahangaika kutafuta ufungua, nilishachanganyikiwa na nguvu zilikuwa zimeniishia kabisa, miguu yote ilikwua inatetemeka.

Kwa hali ile, sikukumbuka hata kufunga duka, nilikuwa nimechanganyikiwa na kujikuta naacha kila kitu kama kilivyo na kukimbia nyumani na nilipofika nilimkuta mtoto anatetemeka nje ya mlango huku kalowa kupita maelezo niliumia sana na nililila kwa uchungu kweli.

‘Mtoto wangu..jamani...kwanini mnanifanyia hivi, hivi huyu kiumbe wa mungu kawakosea nini....’nikamshika na kumkumbatia ili mradi apate ujoto, nikawa nimemshika hivyo hivyo huku nakimbilia ndani. Mtoto hakuweza hata kutoa sauti, huenda alilia mpaka sauti ikamkauka.

Kibinadamu sikutarajia kabisa hilo linaweza kutokea,na wala sikutegemea kuwa shangazi mtu, anaweza kufanya hivyo kwa mtoto wake,maana shangazi anasimama sehemu ya baba, ...kweli kumbe mwenye kovu usizani kapoa, kumbe abdo wenzangu wana yao moyoni.

Nilimchukua mtoto na kukimbia naye ndani nilikuwa nimeshajawa na khofu nikijua kuwa sasa nampoteza mtoto. Nilikuwa mara kwa mara nikimwangalia na kila nikimtupia jicho naona hali yake ni mbaya mbaya...siwezi hata kuelezea.

Nilimvua zile nguo zilizolowana na mvua, na kumvalisha nguo zingine na niliona hazitoshi, nikachukua na sweta, na nikamlaza kitandani, na kumfunika na blanketi nilikaa mda huku nalia, kama mtoto, niligeuka kumwangalia mtoto wangu nikaona sasa anapumua kwa shida sana. Nilipoona hivyo, nikasimama, miguu haina nguvu, nikainama kumtikisa, niliona kama ndio anakata roho,.

Alipanua mdogo kama anataka kulia lakini sauti ikawa haikutoka, halafu akalegea na kutulia kimiya, ......

‘Oh, mungu wangu, mtoto wangu anakufa, ...nisaidie mungu wangu, nimekosa nini oh.....’nikasema huku machozi yananitoka, na kila ninachofanya hakifanyiki, mfukoni sina kitu, pesa kidogo niliyokuwa nayo nimenunulia vifaa vya dukani, nitafanya nini...na nilipotoka kule sikuangalia kama kuna akiba yoyote, nikachanganyikiwa, hata hivyo nikaona hakuna jinsi ni lazima mtoto apalekwe hospitalini...mvua bado nje inanyesha kumbwa.

Nikamwangalia mtoto, bado anapumua lakini kwa shida sana..., nikaona nisitapoteza mtoto, nikakimbia kama mwehu kutoka nje, bila kujali mvua na kuanza kutafuta usafiri wowote, ili niweze kumpeleka mtoto hospitali baada ya kuhangaika sana baba moja msamaria mwema aliniona akashangaakuniona ninavyohangaika na mvua ikininyeshea;

‘Wewe mwanamke vipi mbona unakimbia huku na kule kwenye mvua?’ akaniuliza kwa sauti.

‘Wewe niache tu, masikini mtoto wangu anakufa..nifanyeje jamani....’nikasema na yeye akaniuliza;

‘Hebu nieleze mtoto kafanya nini...?’ akaniuliza na mimi kwa haraka nikamuelezea ilivyokuwa.

‘Dada yangu usijali nitakusaidia....mimi nina usafiri...’akasema na mimi nikageuka kumwangalia kwa macho ya kushukuru.  Na hapo akaingia kwanye geti la nyumba yake na mara nikaona gari linatoka, kumbe alikuwa na gari, akatoka nalo, na kuniambia;

‘Haya haraka panda twende nyumbani kwako...’akasema na mimi bila kujali nilivyolowana nikapanda kwenye gari, tukaanza kurudi kuelekea kwangu,...maana kwa kuhangaika kutafuta gari nilishafika mbali.

Tulirudi hadi nyumbani kwangu na nikamkuta mtoto yupo vile vile, na hali ilikuwa mbaya zaidi, nikambeba, nikatoka naye nje, tukaingia kwenye gari na tukaelekea huko hopitalini, mtoto alikuwa anazidi kuwa na hali mbaya......

NB: Je ilikuwaje

WAZO LA LEO: Kwa vyovyote iwavyo, hasira na chuki zetu zisiguse watoto , watoto hawana makosa katika mambo yenu ya kimaisha, mtoto hana dhambi, inashangaza watu wanagombana, na hasira zao wanazipeleka kwa watoto, huo ni unyama, uliokithiri.


Watoto ndio jamii, ndio kikazi, taifa letu kutokana na wao, tunatarajia kupata viongozi wetu, tukiwalea vyema, tunaijenga jamii, iliyo na upendo na amani, na kupata viongozi waadilifu,kinyume chake tutarajie shida, uhasama chuki na vita....tukumbuke kuwa watoto ni taifa la leo, kesho na siku sijazao.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hey there! I know this is kind of off topic but I was wondering which blog platform are you using
for this site? I'm getting tired of Wordpress because I've had issues with
hackers and I'm looking at options for another platform.
I would be fantastic if you could point me in the direction of a good platform.