Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, January 22, 2014

Mkuki ni kwa Nguruwe-65-mwisho
‘Sasa ni ajenda ya mwisho, ajenda ya kusikia kauli na maamuzi ya wanandoa ambao ndio waliotuweka hapa, kwa namna nyingine tunaweza kuiita ajenda hii kuwa ni ajenda ya hukumu ....na hapa mimi sitaingilia sana, maana wanandoa waliosababisha hiki kikao wapo hapa, na walishapata muda wa kukaa pamoja na kulijadili kwa mapana.....’akasema mwenyekiti.
‘Japokuwa nilisikia kuwa bado hakujakuwa na maafikiano, lakini kwa vile tupo kwenye kikao cha wengi, na penye wengi hapaharibiki neno, natumai tutalimaliza hili swala kwa amani na upendo, ikishindikana mimi mwenyekiti nipo, itanibidi nitumie rungu langu la uenyekiti...kulimaliza hili tatizo,...

Tuendelee na hitimisho la kisa hiki...........

**********
‘Katika ajenda hii ya mwisho, tutaangalia jinsi gani, tutaweza kuwasaidia hawa wanandoa waliotuita hapa, ...mimi hapa ni mwenyekiti, lakini pia ni mzazi wao, lakini ni vyema, nikarudi kulielezea hili kama mzazi yoyote yule bila kujali kuwa yule pale ni binti yangu,,...

‘Kama mnakumbuka kikao kilichopita ilibidi tuendeshe jambo hili la kifamilia kama kesi ili tuone haki inatendeka, kwa vile mlalamikiwa hakukubali wala kukiri kosa lake, kwahiyo tukaona ni vyema tukaliangalia hili jambo kwa undani zaidi, ikabidi mpaka tuanze kutoa ushahidi hadi kukapatikana ukweli mzima, ambao ulikwenda hadi kuvuka mipaka ya kifamilia na ndio maana tukahirisha kiko chetu hadi hii leo..

‘Sasa basi mimi kama mwenyekiti, inabidi nilisimamie hili kwa hekima zote ili mwisho wa siku tukimalize hiki kikao kwa kushikana mikono ..bila kinyongo...ila natoa kama angalizo, kuwa hii ni familia yenye maadili yake, kama kuna mtu anaona kuwa hataweza kuishi nasi, kwa kufuata sheria zetu za kifamilia, basi awe huru kuondoka, hata kama ni mtoto wangu wa kumzaa,...ni vyema tukaanza kuweka kutii amri na sheria kuanzia kwenye familia, ni hili liwe wazai kwani, hatutaki kumlazimisha mtu,...

Hata hivyo, taratibu za familia ndogo, yaani za mke na mume zitaendelea kutumika,haina maana kuwa familia kuu ikiamua hili ndio kila kitu kinafuatwa hivyo, hapana, mke na mume wanaweza kujenga taratibu zao za kuishi, kama walivyofanya hawa wenzetu, na sisi kama familia kuu hatustahili kuwaingilia, maana kila familia ina mambo yake, ilimradi tu zisikiuke misingi mizima ya itikadi za familia kuu, kama kuvunja sheria za nchi, kukiuka misingi ya ndoa na vitu kama hivyo....

‘Sasa basi wazee walisema, yaliyopita ni ndwele tugange yajayo, yaliyotokea yawe ni fundisho kwetu, na tuape kuwa hatutarudia tena,tusameheane na kukiri kuwa tulikosea, na hatutareeja ujinga huo tena, kwani tumeshafinywa, mtu mzima ukifinywa, ona aibu, jirudi, eti jamani, ni aibu kwa haya yaliyotokea...miezi mitatu, ya heka heka, na jela, imetufundisha mengi, nyie mliokamatwa mumejionea wenyewe..’akasema mwenyekiti huku akimwangalia mume wa familia.

‘Hebu mwangalia mume wa familia alivyochongeka, ....ni taabu tupu, kwanini tufanye haya, tukijua kuwa ni makosa, tunamkomoa nani, ...baba, sasa ni wakati wako wa kurudisha mwili wako, ukae utulie ujipange vyema, muishi vyema na mkeo wako na familia yenu...

‘Kama ulivyoona hata mahakamani walikunyoshea kidole na kukupa onyo, na ulitakiwa ufungwe, lakini wakili wetu akafanya juhudi za ziada, akirejea maadili na tabia za familia kuu, matendo yetu mema ya kifamilia yakachukuliwa kukulinda wewe, ina maana kuachiwa kwako kunatokana na kumbukumbu za matendo yetu mema, maadili yetu mema yamukusaidia, sasa mimi kama mwenyekiti nikiwa hai sitakubali uadilifu wetu uporomoke tena, ...nawaomba kama wanafamilia  tuitunze hiyo kumbukumbu,...’akasema mwenyekiti.

‘Naona nimeongea sana, sasa ni wakati wa kumpisha mke wa familia, ambaye kikao kilichopita alitakiwa kusema yake, kutoa hitimisho ya haya yote, natumai kipindi hiki kifupi umeweza kukaa na kutathimini, umeweza kukaa na mwenzako mkayaongea vyema, ...na kwahiyo wewe kaam mdhulumiwa, unayo haki yako, na hatutapenda mwanafamilia kudhulumiwa....kama kuna mtu anadhulumiwa, aliweke wazi, sisi tupo tutaangalai haki iko wapi.

‘Mke wa familia, tunakuomba uondoe jaziba, najua umeumia sana, lakini yote ni maisha, kwenye wema, na wabaya wapo, na halikadhalika kwenye wabaya na wema hawakosekani, toa maamuzi yako yenye hekima na busara, kwani wewe ndiye uliyekuwa mlalamikaji, ni kweli kikao kiliona kuwa ulitendewa isivyo halali, na tuliona kuwa tuiachie katiba yenu ifanye kazi, lakini kama wanafamilia tulilijadili hili, tukaona kwanini misisameheane mkayasahau yaliyopita na kuganga yajayo...’akasema mwenyekiti.

‘Nakumbuka kikao kilichopita tulimpa nafasi mlalamikiwa ajitetee, na kuelezea hisia zake, leo hatuna nafasi naye tena, leo ni siku ya mke wa familia kuongea yake na pia kutoa maamuzi yake, kwani imeonekana kweli kuwa mke wa familia ulitendewa isivyo haki, kwahiyo kwa upendeleo una pewa  nafasi mbili, ya kwanza ni kumsamehe mume wako....

‘Kusameheana ni wajibu wa kila mwanadamu, ukikosa na kukosewa hatuna budi kusameheana, akayashau mabaya aliyotendewa,...na mnafika mahali mnasema haya tuanze moja, hata ikibidi kwenda fungate tena, mkakumbuka enzi zile za mapenzi ya awali, inasaidia...lakini yote ni maamuzi yako kama utakubaliana nalo, basi sisi kama wanfamilia, tutawashikanisha mikono, na tutamaliza mambo haya kwa amani na salama hilo ndilo kama wazee wenu tunalihitajia...’akasema mwenyekiti.

‘Lakini kuna nafasi ya pili, ambayo mimi kama mwenyekiti, sitaipendekeza sana, japokuwa nyie mlikubaliana kwenye katiba yenu iwe hivyo, ...kuwa atakayekiuka mambo fulani, ambayo mimi kwenye familia kuu nimeyaita matendo hayo kama kashifa, basi moja kwa moja ndoa inakuwa haipo..kama katiba yenu inavyosema, na mkosaji anawajibishwa, kwa kukosa kila kitu...mmmh, ni adhabu kubwa sana,inabidi muifikirie vyema, maana ni nani yupo asilimia mia kuwa hafanyi makosa hayo hata kwa siri, sijui ....’akatulia mwenyekiti na kumwangalia mke wa familia.

‘Naona nisipoteze muda, mke wa familia uwanja ni wako, ...’mwenyekiti akamwangalia mke wa familia, na mimi kama mke wa familia, nikamwangalai huku nikitafakari maneno yake, lakini akilini mwangu nilikuwa na yangu, kwanza nikasimama na kusema

‘Naomba niongee nikiwa nimekaaa, ...mwenyekiti naomba kibali chako....’nikasema na mwenyekiti akatabasamu na kusema;

‘Nyie vijana bwana, mbona mnachoka mapema, haya wewe kaaa, hata ukitaka lala, lakini sema yale yaliyo moyoni mwako, uwanja ni wako....’akasema mwenyekiti.

‘Nilitaka nisimame, lakini kama wenzangu walivyofanya kwa leo, nitaongea nikiwa hapa hapa, mtanisamehe kidogo.

‘Namshkuru sana mwenyekiti kwa kunipa nafasi hii, ambayo, imekuwa kama vile mtu yupo kwenye chumba cha mtihani baada ya maandalizi ya muda mrefu. Ni kweli nimekuwa nikijianda kwa siku kadhaa nyuma hasa baada ya kikao kilichopita, na leo ndio natakiwa kusema kile nilichokuwa nikijiandaa nacho, kwa siku zote nilizokuwa peke yangu, nimekuwa nikijiandaa kwa kuangalia nije niseme nini, kwani maamuzi tayari yalishajionyesha,...lakini sio kusema tu, lakini sio maamuzi tu, ni pamoja na kuhakikisha kuwa hili jambo linakwisha kwa amani na upendo....’nikageuka kumwangalia mume wa familia.

‘Pamoja na yote hayo, mume wa familia alipotoka rumande, huko alipokuwa ameshikiwa na polisi, nilijaribu kukaa naye ili nione jinsi gani tutasaidiana kulitatua hili,...ni jambo gumu kuliamua peke yako, unaweza ukalitatua kwa jaziba, kwa hasira, mwisho wake ukija kutulia ukaja kujijutia, na ni rahisi kuliongea kwa maneno ya haraka, lakini madhara yake ni makubwa, ....ndio maana nimekuwa nikiliwazia sana.

‘Tulipoweka makubaliano, yetu, kila mmoja aliyapokea kwa furaha, na mimi sikutarajia kuwa mwenzangu angelikuja  kuyafanya hayo aliyoyafanya,sikuamini, na ilichukua muda sana kulikubali kichwani, inafikia hatua unaona kama unaishi na watu wawili tofauti, na kwa ujumla nimekwazika siri, kwani sikujua kuwa unaweza ukaishi na mtu, mkachangiana naye kila kitu, ukampa moyo wako wote, kumbe mwenzako hayupo nawe kabisa, kumbe mwenzako anaye anayempenda, wewe upo kwa ajili ya kutumika tu...’nikatulia huku nikionyesha uso wa huzuni.

‘Nimejaribu kuongea na mwenzangu ili nione vipi tutasaidiana hili, kama binadamu, sikutaka kuwe na unyonge, kuwa kwa vile mimi nina hali hii au ile, ...kwahiyo nilimtaka ajitoe, aseme anataak nini, atoe ukweli wake ulio moyoni...lakini haikuwa rahisi...’nikainama kama nasoma kwenye karatasi.

‘Kwani ujumla kama mlivyoona, nia na malengo ya mwenzangu na mwenzake, ilikuwa ni kupata maisha mazuri, sio mapenzi hasa hasa, ...kwahiyo wakatumia hadaa, wakajipatia mumena mke, wenye kile walichokitaka, lakini nafsini mwao bado kulikuwa na mapenzo , upedo wao wa asili. Nimeshasikia wengi wakisema waume au wake zao sio wale waliokuwa wanawapenda kiasili, yaani sio wapenzi wao wa asili, lakini walikuja kupendana na waume au wake zao , na kusahau yale mapenzi yao ya asili..na wangi wamefanikiwa, nikajiuliza kwanini sisi isifanikiwe...

Sasa nilitarajia kwa mwenzangu kuwa huenda itakuwa hivyo,na nilipoongea naye akasema anahitaji nafasi ya pili, kwani keshajifunza, na yupo tayati kuishi kama mume mwema. Mimi sina uhakika na hilo, japokuwa wazazi wangu wamenithibitishia hivyo, kuwa kwa mwanaume ikishatokea hivyo, basi hujifunza na hataweza kurudia makosa tena, ..mmh, ukishaumwa na nyoka kila ukiguswa na unyasi utashituka,...’nikageuka kumwangalia mume wa familia.

‘Nilipoongea na mume wa familia alipotoka jela ili kutaka kujua ni nini maamuzi yake baada ya tukio zima hili, nikimtolea mfano wa mpenzi wake wa asili ambaye kakiri makosa na kawa tayari kuchukua maamuazi magumu,...namsifu sana, kweli amekomaa kiutu uzima, hongera zake na namuombea mola afanikiwa katika maisha yake..

‘Mimi nikamuuliza mwenzangu,  je na yeye ana msimamo gani, ..akaniambia msimamo wake ni ule ue, kuwa ndoa yake haitavunjika, nikamuuliza je makosa aliyoyafanya hayaoni,nilimuuliza kimtego kuona moyoni kwake, anakiri kuwa kakosea, bila kujua mtego wa swali langu yeye akasema alifanya hivyo akijua kuwa anawajibika kama mume wa familia.....kwakweli ilinivunja nguvu...’

‘Hebu angalieni hilo jibu katikati ya mstari kwa hekima..kweli mtu baada ya kukosea,angelitoa kauli hiyo...nikaona bado kumbe mwenzangu anaona kuwa alichofanya ni sahihi,na kwahiyo hali hiyo huenda inaweza ikatokea tena....

‘Kama ni kweli, mtu umekosea ulitakiwa kukiri kosa na kuomba msamaha, lakini hilo halikuwahi kutokea hadi tunafika hapa, haljafanikiwa, kwani hata hayo maswali niliyokuwa nikimuuliza mwenzangu, aliona kama ninamkera, sasa ni mimi niliyekosea au ni yeye aliyekosa, je ni nani anastahili kumbembeleza mwanzake, ni mkosaji au ni yule aliyekosewa...niliona bado kuna tatizo, na huenda hilo ni tatizo sugu...

‘Kwa majibu ya swali hili, imenifanya nifikirie mara mbili je ni nini mstakabali wa maisha bora ya mume na mke, ni, nini mstakabali wa watoto, ili waje wajifunze maisha bora, tabia njema, kutoka kwa wazazi wao..ndio hivyo kutumia ubabe, na kukosa na usiambiwe umekosa, ..hapana hatuendi hivyo....’nikamwangalia mwenyekiti, na mwenyekiti alikuwa katulia akijifanya anaandika andika.

‘Wazazi wangu nawashukuru sana kwa hekima zenu, kwakweli najisifia kwa kuwa  na wazazi kama nyie, kwani mnafahamu jinsi gani ya kuishi na watu, kwani baada ya haya yote nilitarajia mungelikuwa na hasira na kuniambia kuwa mimi nimejitakia,kwani mlishanikanya lakini sikuwasikia, nibebe mzigo wangu mwenyewe, lakini baada ya yote haya mumekuwa mstari wa mbele, mkiniomba haya tuyamalize kwa amani,..ikibidi turejeane...kama mke na mume...

Nimewaelewa sana, na mimi kama binadamu nahitajika kujirudi, kusamehe na kuangalia kuwa kweli kuna kuteleza, kuna kukosea, na mnaweza mkayasahihisha makosa yenu mkaendelea mbele..nimelikubali hilo, ...’nikatulia.

‘Kabla ya kutoa maamuzi yangu, mimi nimefikiri sana, nikaona kuna haja ya kufanya yafuatayo, kwa vle mume wa familia lengo lake kubwa ni mali, lengo lake kubwa ni kupata utajiri, lengo lake ni kuwa na hali nzuri, basi, mimi kwa rizaa yangu mwenyewe nimekubali kumuachia kampuni yake, ...achukue hisa zote, na amilikishwe moja kwa moja kama kampuni yake. Mimi sitakuwa na hisa tena kwenye kampuni hiyo, ina maana ni mali yake...hilo mimi nimeliamua kwa moyo wangu wote, kuonyesha mapenzi yangu kwake..

‘Kwa kufanya hivyo, sasa yeye ni tajiri, kwani ana kampuni ambayo ni yake...’nilimuona mwenyekiti akiniangalia kwa macho makali, maana wazo kama hilo niliongea na wao wakalipinga, lakini mimi nikaona ndio njia pekee ya kumsaidia mume w familia.

‘Mimi nitabakia na kampuni yangu na hisa za mume wangu zitaondolewa kwa vile nimeshamkabidhi kampuni yake awe yeye ndiye mumiliki, na sitajhusisha na kampuni yake tena...ila nilitaka yeye kwa rizaa yake mwenyewe, awauzie baadhi ya hisa washirika wake, ...hasa aliyekuwa rafiki yangu,... na pia amuuzie, mpenzi wake wa asili baadhi ya hisa...,ili wao pamoja wafanye kazi kwa ushirika, hii itawasaidia wote, na ile ndoto yao ya kupata utajiri itakuwa imekamilika,..natumai wakiwa pamoja wataweza kufanikisah mambo yao bila wasiwasi..

‘Mimi nimeona tusaidiane kwa hilo, ili kila mwenye nacho amsaidie na mwenzake, kwani huenda haya yote yasingelitokea kama watu tungelipendana, wale walio nachoa wakawasaidia wale wasio nacho, na kupandishana,...ingelikuwa ni dunia ya upendo na amani..

 ‘Lakini pamoja na yote hayo, nafahamu kuna watu hawatosheki, nafahamu mtaka nyingi nasaba, anaweza akakosa yote, kama bado mume wa familia hajatosheka na hilo..sijui nitamsaidiaje, mimi kwa mtizamoo wangu, kama hariziki na hilo,  itabidi twende mahakamani, ili haki yake ipatikane,...na mkataba wetu upo wazi utasimama kama ushahidi, na kama itafikia hatua hiyo, basi, sitarudi nyuma tena, ...mkataba utafanya kazi yake na yeye hatakuwa na haki ya kupata kitu chochote, sasa ni uamuzi wake...’nikasema na kumwangalia mwenyekiti.

Mwenyekiti akatulia kwa muda halafu akaniuliza, ...’mbona hatujakuelewa, hatujasikia maamuzi yako, au hayo ndio maamuzi yako..., ?’

‘Nilisema kabla sijatoa maamuzi yangu,nilitaka niyaweke hayo wazi, nilitoa hayo kama utangulizi, kabla sijatoa uamuzi wangu, ...nimefikiria sana, na moyoni nimeshasamehe yote yaliyotokea, na walionikosea nimeshawasamehe, akiwemo mume wangu, ....kama binadamu yeye anastahili kusamehewa, natumai hatarejea makosa kama hayo tena.

‘Kama alivyosema mwenyekiti, kusamehe ni wajibu wangu, ni hilo nimelitimiza, na nilishamwambia mwenzangu kuwa sina kinyongo naye, lakini nataka kuayasema haya hasa kuhusiana na ndoa yangu, baada ya yote hayo na kuyapima yote kwa makini zaidi, mimi nimegundua mengi, ambayo yatanifanya nitoe maamuzi yangu kama binadamu, natumai mtanielewa,....’nikatulia na watu wakaguna, kukawa kimiya.

‘Nikiwa na maana kuwa ndoa ni ya mke na mume, ni mafungamano yenye usawa, kila mmoja anawajibika kutegemeana na hali yake.

 ‘Nilishaongea na mwenzangu na kumtaka asome katiba yetu vyema, ili sije akasema mimi nilikuja kubuni Katiba nyingine, lakini alikataa, yeye alikuwa kaninunia tu, na kubakia kuniangalia kwa macho ya hasira na chuki,na alipoanza kuongea alikimbilia kunilaumu mimi na wazazi wangu kuwa ndio tumesababisha haya yote, hadi akawekwa ndani....jamani hivi ni sisi tuliofanya hivyo, au ni matendo yao mabaya... je kwa hayo aliyoyatenda ni nani angelistahili kumkasirikia mwenzake...sikumuelewa...’nikatikisa kichwa.

‘Ina maana kweli mtu hajajifunza kwa hayo yaliyotokea, kuwa yeye ndiye mkosaji, yeye  ndiye aliyestahili kuomba msamaha, na kunyenyekea kwangu, na kwa hawo walioathirika kutokana na matendo yake machafu, kamuharibia mtoto wa watu mipangilio yake ya maisha...hilo halioni,...yote kwake anaona ni kuwa hay a aliyoyatenda sio sahihi, lakini yeye anaona alivyotenda ni sawa tu kama anavyodai kuwa alifanya hayo akijua anawajibika kama mwanaume,...kwa mtizamo huo ninakuwa na mashaka, ,...

‘Huenda mwenzangu bado haajtosheka, huenda mwenzangu bado anahitaji muda wa kujirusha na kila mwanamke anayempenda, huenda nafsi yake ilikuwa haijatulia, ndio hivyo tena, yeye alinioa tu kwasababu kuna kitu alikitaka,mali, lakini mali haiji hivi hivi, inabidi tufanye kazi, ndivyo nilivyokuwa nafanya mimi, nilijitahidi kumjenga afahamu hivyo, natumai atayakumbuka maadili yangu kwenye kazi, akiwa kama kiongozi mkuu, atajua kwanini nilikuwa namfanyia hivyo....’nikamwangalia na yeye akawa ananiangalia kwa macho ya zarau.

‘Sasa mimi nimeona nimpe kile alichokuwa akikitaka, natumai moyo wake utarizika, na huenda akatulia, ..huenda, akawa mume mwema, na kuweza kujenga familia yake kwa amani na upendo, maana watu wa namna hii hawatosheki bwana, lakini sasa atafanya hivyo akiwa anataka nini,...’nikatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Mimi nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kutimiza wajibu wangu,sikuwahi kuvunja masharti makubwa ya ndoa hata siku moja, ina maana mimi nilikuwa mjinga, au sikuwa na vishwawishi vya hapa na pale. Wapo watu walikuwa wananikera, lakini mimi nilifahamu kabisa kuwa ni mwanandoa, na ndoa ina masharti yake, ...nikayatimiza, ina maana mimi nilikuwa sina hisia za kibinadamu.

‘Kwakweli kila nikiliwazia hilo ninaumia sana, kwa ujumla nimekwazika kupita kiasi, nimezalilika, hasa pale ninapoambiwa sikuweza kutimiza wajibu wangu ndio maana mwenzangu akafanya hayo...hamfahamu jinsi gani mwanamke anavyojisikia pale mume wake anapotembea na wanawake wengine wakati yeye ni mke wa ndoa, inaumiza mtu kisaikolojia, unajiuliza mawali mengi, hivi mimi nina kasoro gani, hivi..hivi...unaumia...’nikasema kwa machungu.

‘Lakini mungu ni mkubwa ukweli mara nyingi una nguvu, ukweli ukadhihiri, ukweli ukajileta, na mabo yakawa ahdharani, kumbe  hayo waliyapanga hata kabla hawajaingia kwenye ndoa, walichokuwa wanakitafuta ni sababu tu,...mimi,nakubali , ndio, kama binadamu hata mimi nilikuwa na madhaifu yangu, kama alivyodai, kuwa mara nyingine sikuwa karibu naye, kutimiza wajibu wangu wa kindoa, lakini hilo lilikuwa swala la kuongea, mimi ningemuelewa....hakuniambia, hakulalamika mbele yangu, akafanya aliyoyafanya...lakini hicho ni kisingizio tu, walishayapanga hayo kabla, wakishirikiana na mwalimu wao...

‘Udhaifu wangu, haukuwa wa kuvunja masharti makubwa ya ndoa, ni yale ya kibinadamu na kwenye mkataba tuliyaanisha hayo, yapo mapungufu ya kibinadamu, yanasameheka,....sio hayo aliyoyafanya yeye, ya kukiuka miiko ya ndoa, na kwenda kuzini nje, hadi kupata watoto, hawo watoto wanadai haki yao, kwanini walizaliwa hivyo, na wengine wanatelekezwa, kwa tamaa za watu wasio na maadili, hawa watu tutaishi nao mpaka lini, kwanini kusiwe na njia ya kuwawajibisha,...’nikasema na kumwangalia binti wa hiari wa wazee wangu, aliyekuwa mfanyakazi wangu wa ndani, alikuwa bado hajaondoka.

‘Na nimesahau jambo moja la muhimu sana, huyu binti wa hiari, nimeamua kuwa nitamuajiri kwenye kampuni yangu, nitaangalia jinsi gani ya kumsaidia,....maana alikuwa katika mikono yangu na yote yalitokea kwenye nyumba yangu, mimi nabeba mzigo huo nitamsomesha na nina imani baada ya miaka mitatu atakuwa tofauti...namjenga rafiki mwingine...sitachoka kusaidia watu pale inpowezekana....’nikasema.

Baada ya kusema hayo, ... ...,  kama ilivyoanishwa kwenye mkataba wetu wa hiari, na kutokana na ushahidi uliotolewa mimi nimeona ndoa yetu ifikie kikomo na kila mmoja aangalia ustaarabu mwingine, kwani hata bila kauli yangu hiyo ndoa ilishavunjika, kwani kama mtu umekiuka makubaliano ya ndoa, akazini, na mungu akatoa ushahidi, akapatikana mtoto, tunataka nini tena, ni dhahiri kuwa ndoa haipo tena...mwenyekiti alisema kama mtu hajatenda dhambi hiyo akitokeze, mimi najitokeza, sijafanya dhambi hiyo...mungu ni shahidi wangu...kwahiyo natimiza wajibu wangu, kwa kusema ndoa haipo, sheria ichukue mkondo wake.

Maamuzi yangu ya kuachana na mume wangu, ni kuonyesha upendo wangu kwake, kuwa mimi najali utashi wake,...kuwa yeye ana mpenzi wake wanayependana naye sana, ambaye alitamani awe naye, lakini kutokana na nakama za kimaisha, walishindwa, sasa wanazo mali, sasa wao ni matafjiri, wanaweza kuishi kwa raha, nafiki ndoto ya sasa imetimia, au sio wenzangu...sasa wana mali, ...kwanini nisiwape nafasi hiyo,sitaweza kuwadhulumu kwa hilo, ndoa yangu na mume wa familia imekwisha, na nashukuru mungu kwa yote hayo, na sio nasema hivyo kuwa nina kinyngo tena, hapana nimeshawasamehe...

‘Ninachkifanya hapa ni kuwa sitaki kuwatendea dhuluma kwa vile walikuwa na hali hii au ile, nimechukua maamuzi haya magumu, kwa vile nampenda sana mume wangu, na nataka arikie na nafasi yake...’nikatulia kidogo.

‘Kama mlivyoona, mimi nilikuwa na mume ndani, nikijua kuwa mwenzangu yupo na mimi kumbe alikuwa akinivunga, na kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa....sasa muda umefika, yeye na mchumba wake wa asili wapo huru, baada ya taratibu zote za kuvunja ndoa yangu, talaka na kila kitu, wao watakua huru kuoana...hakuna kizuizi hapo,...’nikasema na kumwangalia aliyekuwa mke wa docta.

‘Lile swala la kuwa eti kwasasa kajifunza, hatarudia tena, mimi bado linanitia mashaka, na ninaona nistumie mwanya huo kuwaharibia upendo wao na mpenzi wake wa asili, nilishangea na mpenzi wake huyo na tumekubaliana mambo fulani fulani, ....

'Kwa ujumla mimi sioni kwanini wasioane, wanahitaji nini tena, sioni kwanini mpenzi wake huyo aende akaanza maisha ya kipeke yake huko kijijini, akae hapa, wafanye kazi, tumeshaliongea hilo na yeye japokuwa hakukubali moja kwa moja, lakini natumai wakikaa na mwenzake, watakubaliana..’nikasema na kugeuka kumwangalia mume wa familia halafu aliyekuwa mke wa docta. Daocta alikuwa kashika shavu utafikiri hayupo kwenye kikao, naona alikuwa kiumia sana moyoni.

‘Sasa kazi ni kwenu wapendwa..ila cha muhimu, kazi kwanza, hayo mengine baadaye, ni muhimu sana hilo, muhangaike, ili muweze kuuendeleza huo utajiri kwani haukuja kirahisi hivyo, unahitajika kuwajibika, msilale, fanyeni kazi kwa bidii, nina imani mtafanikiwa, na kama mkihitaji ushauri wangu mimi nipo, tutasaidiana pale mtakaponihitajia, lakini kwa nia ya kutoa ushauri tu.

‘Ama kwa yule aliyeitwa rafiki yangu, mimi sina kazi tena na yeye, nilichofanya  kwake ni kumsaidia, na kwa vile keshakuwa na anaweza kujichukulia maamuzi yake mwenyewe, basi, ....naona nimuache, kama watakubalia na mpenzi wake wa siri,wanaweza kujiunga kwa pamoja wakajenga kampuni yao ikawa yenye nguvu...yeye sasa ana uwezo huo , hata wa kujiajiri...sina wasiwasi na yeye, ...

‘Hayo ndio maamuzi yangu, na sina zaidi naomba mawakili wetu wayaweke hayo sawa, na taratibu zote za kutalikiana zifanyike kwa amani, nataka hili zoezi lifanyike kwa amani ili baadaye tukikutana tukutane kama marafiki, hakuna chuki wala kununiana, hayo ndio maamuzi yangu na hakuna kurudi nyuma, nawaomba wazazi wangu walipokee hilo , wakijua kuwa mimi sasa sio mtoto mdogo tena....’nikasema nikiwaangalia mawakili wetu na wazazi wangu, nilimuona mama akipitisha mikon usoni na kujifuta....

‘Na kwa hivyo basi, ili kuweka mambo sawa, na kumhakikishia mume wa familia kuwa mimi sina kinyongo na yeye tema, nawaomba mawakili, wafanye taratibu za kisheria kuziondoa hisa zangu kwa kampuni ya mume wangu na kumumilikisha yeye, ...na pia waziondoe hisa za mume wangu kwenye kampuni yangu, na kwahiyo mimi nitamiliki kampuni yangu peke yangu, na yeye na wasaidizi kama watakubaliana wataangalia ni nani apate kipi ...nafahamu mume wa familia atakuwa na hisa kubwa kama mumiliki, ..wengine watakuwa na hisa zao ndogo ndogo, lakini sitawasaidia sana,...kama watatulizana.

‘Na kwa vile mume wangu ndiye mkosaji, mali nyingine alizozikuta zitabakia kama zilivyokuwa, kama alivyozikuta, ni mali yangu na watoto wangu ...ama kwa nyumba, nyumba aliyokuwa akikaa kwa sasa baada ya kutoka kuumwa na kifungoni , ile ni mali ya kampuni yake, basi itakuwa ni mali yake, sina haja nayo...’niliposema hivyo, mume wa familia akainua uso na niliona ukikunjuka na zile hasira alizokuwa nazo usoni zikayeyuka..

‘Mnaona wenyewe, ni nini kilichokuwa kikitafutwa, natumai keshakipata, mimi namtakia maisha mema, na hili liwe fundisho kwake, na kwa wenzake,....mwenyekiti mimi naona nimemaliza....’nikasema huku machozi yakinilenga lenga. Mume wa familia alikuwa kavaa miwani, naona ni kwa ajili ya aibu ya hayo yaliyotokea.

‘Basi  sisi kama wazazi, kama mumeriziana hivyo, natumai tumemaliza au mume wa familia una la kuongea....maana bado wewe ni mume wa familia hadi hapo sheria itakapochukua mkondo wake...au nimekosea?’ akauliza mwenyekiti na mume wa familia akawa kimiya kwa muda, lakini baadaye akasema;

‘Sina la kuongea, nitaongea nini wakati maamuzi yameshapita....’akasema na kukaa kimiya huku akiwa kainama na ile miwani aliyovaa huwezi hata kufahamu anafikiria nini, leo hakuvaa kikazi, kwani mara nyingi kwenye vikao kama hivi huvaa suti safi, kuonyesha yeye ni bosi, leo alivaa kinyumbani zaidi.

‘Ni vyema tukasikia kauli yako kama mume wa familia, hata kama mwenzako ameshaamua hivyo, je umerizika, ...upo tayari kuendesha hiyo kampuni mwenyewe. Swala la talaka, mliongea, na hapa ni kama taarifa tu, ....sasa hebu tuambie na wewe una kauli gani...’akasema mwenyekiti.

‘Labda niongee tu, kwa vile mnataka kusikia kauli yangu, nasema hivi kama binadamu nina mapungufu yangu, haya yaliyotokea ni kweli niliyafanya, lakini kipindi nayafanya nilijua natimiza wajibu wangu,...na wakati mwingine, nilizidiwa na kuyafanya hayo yasiyofaa...lakini nimejifunza, na nilikuwa tayari kujirudi, lakini mwenzangu hataki,....

‘Sikuweza kujibishana naye, maana utasema nini, wakati mwenzako kashika mpini,..ni haki yake aamue hivyo, huenda tangu mwanzo alitaka iwe hivyo, lakini hakukuwa na mwanya huo, sasa umepatikana,...mimi nasema hivi kwa vile kaamua hivyo, na iwe hivyo, kama ningekuwa na njia nyingine ya kumshawishi kuwa sitarudia tena ningelifanya hivyo, lakini sina,...

‘Ni kweli, ...nilikuwa na hasira sana, nikiona nasota jela, ...mimi sijaua, ...na ...sawa sitaki kulalamiak sana na kwa vile yeye keshahitimisha,  basi sina jinsi, mimi nimekubaliana na maamuzi yake, nitajitahidi kufanya yale yote yanayostahili niyafanye, na kwa vile tuna mafungamano na yeye ya watoto, ..natumai hatanifukuza nikifika kuwaona watoto wetu...

‘Nimekubaliana na yeye juu ya watoto kuwa waendelee kuwa kwenye mamlaka yake, kwa vile kaona kuwa yeye anaweza kuwalea katika malezi bora, yeye kaona wakikaa na mimi nitawaharibu,...sio kweli kuwa mimi ni mbaya kiasi hicho, inapofikia kwenye malezi, mzazi yoyote atajitahidi kuwalea watoto wake katika maadili mema, lakini sikutaka kupingana sana juu ya hilo, kwa vile kwa kufanya hivyo tunaweza kuwaathiri watoto kisaikolojia,...

‘Sawa,mimi  nimekubali, kwa vile nawapenda sana watoto wetu, na nia yangu ni wao waishi maisha mema, yasiyokuwa na tabia mbaya kama za kwangu..nimekubali kwa kauli yake kuwa hajui huyo mke nitakaye muoa,kweli anaweza kuwa na mpenzi ya dhati kwa watoto wetu, ...mimi kama mzazi nawapenda sana watoto, nisingelikubali mtu awatese, lakini kwanini tugombane kwa hilo, basi nimewaacha watoto wakae naye, sina kinyongo kwa hilo.

‘Ama kwa kampuni, mimi nitajitahidi kuiendesha kwa juhudi kubwa sana, na nitakaa na wenzangu, kama alivyopendekeza mke wa familia, kuwa nishirikiane na aliyekuwa,rafiki yake, inabidi nifanye hivyo kwa vile pia ana damu yangu,  napia eeh, nitamshirikisha,na,.. ..na....’hapo akasita huku akimgeukia mpenzi wake wa asili kwa aibu, na mimi nikasema;

‘Mpenzi wako wa asili....mke mtarajiwa’nikasema na watu wakacheka, na yeye akainama chini kwa kutahayari, lakini akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Na yeye pia ataingizwa kwenye kampuni, kwani anaweza, na tutasaidiana na wote, natumai, hata wao wamejifunza mengi, na kwahiyo hatutafanya makosa ..kampuni hiyo itaimarika na kuendelea kama kawaida...nimejifunza mengi , ni kweli namshukuru mke wa familia kanisaidia sana,...tena sana,...na kwa hivi sasa ninaweza kuiendesha hiyo kampuni bila ya kusaidiana na yeye, lakini kwa vile na wenzangu wana uzoefu wa kikazi, na wana haki, ...sitawatupa, nitakuwa nao bega kwa bega...’akasema huku akiinua kichwa na kumwangalia mwenyekiti.

‘Na pia nawashukuruni sana wazazi wangu kwa kunipigania na kunijali,..nafahamu kama ingelifuatwa sheria basi ningelikuwa sina changu tena...sikutegemea kabisa kuwa mngelinifikiria na kunitetea hadi hatua hii ya mwisho..kweli nimeamini kuwa nyie ni wazazi wenye hekima, sitawatupa, na sitawasahahu katika maisha yangu yote, nyie moyoni kwangu ni wazazi wa kweli...’akasema akimwangalia mama na baba yangu.

‘Hata hivyo sina  budi kukiri kuwa nimekosa, nimesikia kila mmoja akitaka mimi nikiri hivyo, ni kweli moyoni nakubali hivyo, lakini mara nyingi kutoa kauli inakiwua ni nzito, sasa naona nitoe ya moyoni kuwa nimewakosea sana, na samahani kwa yote..ni hayo, sitaweza kuongea zaidi, ahasanteni...’akasema mume wa familia huku akionyesha huzuni fulani.

‘Mwenyekiti samahani kidogo naomba nifanye tendo hili kabla hatujafunga kikao...’nikasema na nikatoka pale nilipokuwa nimekaa na kumsogelea mume wa familia, na yeye akawa kama kashikwa na butwaa, nikamuashiria aliyekuwa mke wa docta aje, na yeye bila kinyongo akasogea pale nilipokuwa, kwanza nilichofanya ni kumkumbatia mume wa familia, na nikawambia;

‘Ahsante kwa yote, nimekusamehe, na nakutakia maisha mengine mema, ..’na yeye kwanza alisita kunishika na mikono yake, lakini baadaye akanishika tukakumbatia kwa muda, halafu tukaachana, nikamsogelea aliyekuwa mke wa docta, na kumshika mkono, nikasema;

‘Nakuomba, mume wangu, utimize ile ahadi yenu, mliyowekeana kule kijijini, mkae na mwenzako huyu, mpange siku gani mtafunga harusi, ....sina shaka, na uchumba, maana moyoni huo siku zote ulikuwepo, sasa wadhihirishieni uma kuwa kweli mnapendana, kwa kukumbatiana...’nikasema na wao kwanza waliangaliana, na baadaye, wakasgeleana na kukumbatiana,...vigelegele na shangwe vikatanda.

‘Baadaye na mimi nikamkumbatia aliyekuwa mke wa docta, na tukachekeana, na  nikamgeukia mume wa familia,...nikamsogelea tena na kunyosha mikono kumkaribisha kifuani kwangu, tukakumbatiana, kumbatio la mwisho,  kwa amani na kuagana, huku machozi yakinitka, ilikuwa kumbatioa la kwaheri. Ni heri kwa hayo yote...

Kulikuwa hakuna njia nyingine, ilibidi hayo yafanyike kwa masilahi ya wote, na namshukuru mungu, kuwa tulifikia muafaka, kwani baada ya kikao hicho, na kumbatia hilo la mwisho kama mume na mke wa familia, mawakili walifanya kazi yao vyema, ndoa ikavunjwa, talaka ikatayarishwa, na ikawa mwisho wa ndoa yangu na mume wa familia, yeye akaanza maisha yake na mimi maisha yangu.


MWISHO


NB: Mume wa familia kama ilivyotarajiwa baada ya miezi mitatu walifunga ndoa na mpenzi wake wa asili, ndoa tuliyoisimamia mimi na docta na wazazi wangu, na ilifana kwa kweli, ...mimi nikawa best woman wa mke wake, na docta akawa best man wake...

 Sio siri, yaliyopangwa na mungu hayapingiki, baada ya mvutano, na ushawishi mwingi wa docta, nilikubali turejeane urafiki wetu, na sisi mapenzi yetu ya asili yakarejea, nikakubali ombi lake kuwa tufunge ndoa, ahadi ikatimia tukawa mke na mume.

 Na aliyekuwa rafiki yangu, yeye aliendelea kumlea mtoto wake, na alisema hataki kuolewa tena, sijui  kwanini, ....pengine hajapata anayemtaka, yote maisha,..yeye anadai alichokitaka keshakipata, yaani mtoto, na mdogo wake aliyekuwa mume wa familia yangu, alihamia Kenya na kuanzisha maisha yake huko
Hicho ndicho kisa changu mpendwa...


WAZO LA LEO: Mkioana na bahati mbaya ikafikia hatua ya kutalikiana na juhudi zote za kusuluhishwa zikashiniakana, basi achaneni kwa amani, kuliko kuishi huku mkiumia,fanyeni hivyo kwa amani na upendo, kwa masilahi ya watoto wenu, na mahusiano mema, ili mje kutembeleana kama marafiki wa zamani kwa upendo na furaha

Natoa wazo hili sio kwamba napenda mawaza ya talaka, ila wakati mwingine inabidi iwe hivyo, kwani kuna mengine hayavumiliki, na hatuwezi kujidanganya kuwa tutaishi hivyo hivyo tu, ya mungu mengi, huwezi kujua ni nini kakupangia badili yake,hatuwezi kulazimisha kitu ambacho hakitakuwa na amani kwetu, tukaishi kwa maumivu na masononeko, Japokuwa kiukweli,kuachana si kuzuri, hasa mnapokuwa na watoto, mkifikia kuachana basi peaneni mikono na muombeni mungu wenu, mtafanikiwa.

NAWASHUKURU WOTE WALIKUWA NAMI TOKA MWANZO WA KISA HIKI, MUNGU AWABARIKI SANA, NA MAONI YENU MAOMBI YENU, MUNGU AYAKUBALI, HUENDA SIKU MOJA NA MIMI NITAWEZA.....kutengeneza kitabu, au hivi visa kuweza kuigizwa kwenye runinga, halikadhalika kupata wadhamini, maana haya yote nayafanya kwa gharama na muda,..lakini msijali ipo siko...TUPO PAMOJA, mwisho wa kisa hiki ndio mwanzo wa kisa kingine.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Liz said...

STORY NZURI SANA NA MKE WA FAMILIA KATOA UAMUZI MZURI. TUNASUBIRIA STORY NYINGINE KWA HAMU, MUNGU AKUPATIE AFYA NJEMA

Pam said...

nzuri sana though inaumiza sana, ni maisha na tunajifunza kutokana na matukio kama haya

mama brenda said...

Bravooo