Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, January 20, 2014

Mkuki ni kwa Nguruwe-64


‘Ni mali zake mwenyewe ndizo chanzo cha kifo chake....’akasema

‘Kwa vipi, mbona sikuelewi,....mbona unapenda kuongea kimafumbo-mafumbo...maana mimi nijuavyo mali ni utajiri unaokufanya upate kile unachokitaka, sasa ilikuwaje mali zake mwenyewe zimuue huyo marehemu...?’ nikamuuliza.

‘Kutokana na mali zake kulitokea kutokuelewana yeye na familia yake ya pembeni, ufahamu huyu mtoto sio mtoto wa mke wake wa ndoa,...alizaa nje ya ndoa, sasa huyo aliyekuwa hawara yake, akawa anamfunda mtoto wake, kumfisidi baba yake...mwanzoni mtoto huyo alikuwa hataki, lakini aliposhindwana na baba yake kwenye mambo ya mirathi, akaona afuate yale anayotaka mama yake.

‘Ndio tatizo la uhuni, ukifanya haya mambo kwa siri, ipo siku siri hiyo itakuumbua, marehemu ana watoto wengine, lakini hawo wengine hawana matatizo, tatizo lipo kwa huyo mtoto wake aliyemuona ni kichwa chake...mtoto huyo ni mama yake, walikuwa na ajenda ya siri,....lakini walijipendeekza kwa mzee, na kuonekana wapenzi wake wa karibu....mimi hilo nalifahamu sana.

‘Haiwezekani ina maana mtoto ndiye aliyemuua mzazi wake, kwasababu ya mali, haiwezekani...ungelisema mke, hapo ningelikubaliana na wewe, maana sisi wanawake, tukiamua jambo, tunaweza, nimeona waume wengi wakiuliwa na wake zao, tena wa ndoa achilia wake wan je....’nikasema nikiwa na maana yangu

‘Mhh, unaonaeeh, lakini  tuyaache hayo maana jamaa ana msikio, na tukiongia kwenye hili jengo jamaa atakuwa anatuona, na kutusikia, kwahiyo, ngoja ....’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;

‘Kama anatuona na kutusikia, mimi siwezi kukaa hapa, wewe uliniambia hapa ni sehemu ya usalama, kumbe kuna watu wanatuona, hapana, wewe hunitakii mema,mimi naondoka...’nikajifanya kutoka kuondoka.

‘Mimi nafahamu jinisi ya kufanya tusionekanezima mitambo yake..usijali...nitaizima kwa muda, tukimaliza starehe zetu nitaiwasha.’akasema.

Basi tukaingia ndani ya hilo jengo, kumbe hilo jengo baada ya kufariki Makabrasha, mtoto wake, akalimiliki, na kulikodisha kwa mtu mwingine, ...hata hivyo sehemu ya chini alikuwa akiitumia mwenyewe,..Hata huyo aliyekodishwa alikuwa hana uelewi wa kutosha na sehemu hiyo ya chini, huko aliambiwa hahusiki. Kuna mlango wa kushuka chini, huo mlango upo ndani ya chumba kilichojengwa kama stoo, na muda wote chumba hicho kimefungwa...

Kutokana na maelezo ya huyo jamaa, mtoto wa marehemu alikuwa kila siku anafika hapo, akifanya kazi zake, na wakati mwingine anaingia na wanawake anaowaamini , lakini hata hao waliobahatika kuingia, hawakuweza kutamibua vyema  sehemu hiyo chini, maana wanafika hapo wakiwa wamelewa, na hutolewa mapema..., kuna vyumba vya siri huko chini, na huko ndipo alipohifadhia mambo yake.

Kwahiyo nia na lengo langu kwa huyo jamaa ni kufahamu wapi anapohifadhia kumbukumbu zake, ambazo nyingine ni mapicha ya kashafa aliyoyachukua kwa ajili ya kuwatishia watu wake na kupata pesa. Mimi kwa ufahamu wangu nilijua nimeshayamaliza hayo baada ya kufuta zile kumbukumbu kule juu, kumbe huku chini ndipo kwenye kila kitu.

‘Sasa hebu niambie ni nani aliyemuua huyo jamaa wa watu, maana naanza kuingiwa na hamasa ya kumtambua huyo marehemu na familia yake, wakati mwingine unaweza kujifunza kutoka kwa familia za wenzako, eti wewe unasemaje...?’ nikaanza kumchota.

‘Hiyo familia achana nayo, ni familia ya laana, walichokitenda hawataweza kuishi kwa amani, nikuambie ukweli, pamoja na utajiri wao wote, bado wanaishi kwa majuto, na wakati mwingine nasikia huyo jamaa analia na  hata kupiga makeleke usiku...’akasema

‘Ni nani analia, ....?’ nikamuuliza

‘Si huyo mtoto wa marehemu, wewe unacheza na damu ya mtu, na damu yenyewe ya mzazi wake...’akasema

‘Una uhakika gani kuwa yeye ndiye aliyemuua?’ nikamuuliza huku akiandaa meza na vinywaji, sikutaka kunywa, lakini nilijua hiyo ndio njia pekee ya kupoteza muda na kuzii kuongea...

‘Uhakika sikuwa nao mwanzoni, lakini nilikuja kuangalia mkanda wa matukio, niliouchukua pale ofisini kwa Makabrasha, yeye mwenyewe aliniambi siku nikisikia kafa, nifungue sehemu moja ya siri, iliyokuwa chumbani kwake, nitoe hicho kifaa cha kuhifadhi matukio ya hilo jengo, nimpe mtoto wake mkubwa..’akaniambia.

‘Kwanini alikuambia hivyo, ina maana alishafahamu kuwa atakufa?’ nikamuuliza

‘Watu kana hawo, hujihami tu, ...na sijui kwanini, nahisi kama alishatabiri kifo chake kwani siku ile ya mwisho aliniambia, niondoke, ila nikisikia lolote limetokea, nisisahau kufanya kama alivyoniagiza, na mimi nikamuitikia, na niliposikia kuwa amekufa cha kwanza kukifanya ni hicho, nikafungua sehemu hiyo ya siri ma kukichukua hicho chombo, na alipofika huyo mtoto wao mkubwa nikamkabidhi...

‘Ina maana huyo mtoto wao mkubwa anafahamu ni nani aliyemuua baba yao?’ nikamuuliza.

‘Kile chombo kilikuwa kinachukua matukio ya mle ndani ya ofisi na mazungumzo yake na watu mbali mbali, na muuaji, alijitokea mara moja akiwa kavaa nguo za kuficha sura, kwahiyo sizani kama huyo mtoto wake anamfahamu huyo muuaji...,mimi niliwahi kuchukua kile ambacho hakikuwa wazi, ambacho mitambo yake ndio ipo huku chini,

‘Sasa wewe ulifahamu vipi kuwa muuaji ni nani?

‘Wewe unauliza sana maswali, kama polisi, tunywe, tustarehe, tusahau machungu ya dunia, unasemaje...’akasema huku akinisogelea akitaka kunibusu, nikawa natumia mbinu za kumweka mbali, ili niaweze kupata taarifa muhimu, nikasema;

‘Kuongea pia ni sehemu ya starehe, niambie kwanza,una wasiwasi gani, umeshasema huku hakuna mtu anayeweza kutuingilia, tuongee, ili tujuane vyema, ...’nikamwambia.

‘Aaa, bwana, wewe umesema una mcumba, hata nikikufahamu vyema itasaidia nini, ...’akasema.

‘Unajua mimi nina tatizo moja, ukiniambia jambo likanivutia, natamani kulifahamu vyema, na mimi nimekupendea kwa jinsi unavyoweza kuchunguza mambo na ujanja mwingi, ..sasa wewe mwenyewe umenugusia maisha ya huyo marehemu yamenivutia sana, niambie wewe ulimgunduaje huyo muaji wa marehemu kwasababu mimi ulivyonieleza, naweza kukuhisi kuwa wewe huenda ndiye uliyemuaa huyo marehemu, ?’ nikamuuliza

‘Hapana mimi nisingemuua tajiri wangu, ili nipate nini, mimi siku ile niliondoka mapema niliposikia mke wangu kashikwa na uchungu, na nikapigiwa simu kuwa tajiri yangu kapigwa risasi, nikaja kwa haraka, na cha kwanza ni kufanya kama alibyoniagiza,

‘Kwahiyo kumbe hata wewe humfahamu vyema huyo muuaji wa marehemu , unafanya kukisia tu, na ujanaj wote huo, ulishindwa kumfahamu muuaji wa bosi wake, au unaogopa kuniambia...?’ nikamuuliza

‘Kwakweli mwanzoni nilikuwa nakanganyikiwa hata mimi , kwa asilimia kubwa nilikuwa nawatuhumu  watu wawili, ...kuna jamaa mmoja, alikuwa anafika fika sana na ni rafiki wa marehemu namfahamu sana, japokuwa alikuwa mgonjwa, lakini alikuwa anaweza kutoka huko hospitalini na kuja kukutana na marehemu,..., hata siku ile wakati naondoka, alikuwa ameshafika....yeye nikamtuhumu sana, polisi hawakufaamu kuwa mtu huyo aliwahi kufika...’akasema.

‘Mtu gani huyo wewe ulimgunduaje?’ nikauliza

‘Mimi na marehemu siri yetu ni moja, ....aah, achana nye huyo, ila kulikuwa pia na dada mwingine, ni mtu wa karibu na huyo marehemu , nilimshuku sana, nakumbuka hata wakati naondoka, niliongea na mtoto wa marehemu, huyo mtoto wa marehemu akaniambia niwe makini sana na huyo dada, kwani kamshuku anaweza kufanya jambo baya kwa baba yake....’akasema.

‘Mhh, kwahiyo....?’ nikataka kumuuliza swali, lakini akanikatiza na kusema.

‘Hawo wawili niliwatilia mashaka sana,....’akasema

‘Kwanini uwatilia hawo watu wawli mashaka?’ nikamuuliza.

‘Kuna mabishano ya mara kwa mara ya watu hawo, na kulikuwa na mambo ya mikataba yao ya siri, walikuwa hawajaelewana, nikajua ni yale mambo ya marehemu ya kuwabana watu ili apate pesa kutoka kwao, japokuwa nilikuwa nawafahamu hao watu, lakini mambo mengine kama siri za mikataba yao alikuwa haniambii, .....’akasema.

‘Kwahiyo ikawaj tena usiwashuku watu hawo?’ nikamuuliza.

‘Siku moja, nilifika nyumbani kwa huyo bosi, wakati nafika mlangoni,  nikawasikia,, ...mtoto alikuwa akiongea na mama yake,...hiyo sehemu nimeirekodi,  siunajua tena mitambo ipo wazi wakati wote,hawakufahamu kuwa mimi nipo hapo mlangoni,, na wakawa wanaongea jinsi gani wataweza kuisafisha damu ya marehemu, kwani mtoto alikuwa akisema alikuwa akimuota baba yake akimjia mara

‘Mimi nitakutafutia mtaalamu atakusaidia...lakini usije ukajiweka roho juu, kuwa marehemu anakujia, hizo ni ndoto tu....’akasema

‘Lakini naota ndoto za kutisha, najuta kwanini nilifuata ushauri wako...’akasema huyo jamaa kumwambia mama yake

‘Kama usingelifanya hivyo, ungeliwezaje kumiliki hilo jengo na mali za marehemu nishukuru sana mim kwa kukushauri hivyo, ...;akasema huyo mtoto.

‘Mama mimi sitaweza kulisahau hilo tukio,japokuwa tumelifanya kwa makini na hakuna anayeweza kutushuku sisi, labda huyu mlinzi wetu , nina wasiwasi kuwa atakuwa katuhisi, kwani nilipochelewa kumpa zile pesa zake, amesema anafahamu kuwa tunahusika katika kifo cha baba,.....’akasema.

‘Atafahamu vipi, kwani siulisema uliharibu kumbukumbu zote kwenye ule mtambo wa kunasia matukio,..’mama akasema.

‘Labda awe alifika kabla yangu akaangalia mtiririko wa matukio, ..kitu ambacho kinanitia wasiwasi...’akasema

‘Kama ni hivyo, kwanini asimfuate huyo marehemu ....kwasababu akibakia hai, hutakuwa na amani...’akasema mama.

‘Tukianza hivyo, tutaua wengi, kwasababu hata yule mwanadada aliyekuwa akifanya kazi na mzee, pia na yeye anadai ana ushahidi huo huo , na yule ni hatari zaidi ya huyu mlinzi wetu, huyu mlinzi wetu, ukimpa pesa atanyamaza lakini yule mwanamke, hawezi kufanya hivyo, na amekuwa akihangaika kumtafuta muaji, ...’akasema.

‘Kama ni hivyo unafikiri tutafanya nini, ....ni kuwamaliza mmoja mmoja,, sio alzima kwa kifo cha hapo hapo, tunaweza kutumia sumu,...na ajali za kawaida tu, hilo niachie mimi, wewe hakikisha huyo mlinzi, unamweka sawa...’akasema mama.

‘Basi niliposikia hivyo, sikuwa na amani....cha kwanza nilichofanya ni kwenda kuangalia kile kifaa nilichokichukua kwa marehemu, ....nilikuwa sijapata muda wa kukiangalia mwanzo hadi mwisho, ndipo nikagundua ukweli...kumbe...ndio yeye aliyefanya hivyo...’akasema an kutulia.

‘Nikagundua kuwa kumbe nian ushahii mzuri sana, nikawa nawaza nifanye nini, niwaambie polisi, nikaona hapana muda bado wa kufanya hivyo...

‘Nikahakikisha ule ushidi nimeuweka sehemu ambayo hawataweza kuupata, kwanza nilitaka niutumie kutajirika, baada ya hapo, kama watanizid nguvu, nawakamatisha kwa polisi,..ndio sasa wameanza kunijali, nafahamu wanatafuta mbinu kuupata huo ushahidi nilio nao, halafu waniue, lakini nilimwambia huyo jamaa akiniua na yeye ajue anakamatwa...’akasema.

‘Kwa vipi sasa....akikuua, polisi hawajui kuwa unafahamu siri zako..’nikamwambia.

‘Nimeziweka mahali ambapo, hawataziona, na nimeshatayarisha taarifa yangu, nikaiweka mahali ambapo, nikifia tu, itasambaa...kuwepo kwangu hai ndio naweza kuidhibiti isivuje..’akasema.

‘Sasa kwanini uishi maisha ya hatari kihivyo, waambie polisi, utakuwa umejiokoa, kwasababu kwa hivi sasa unafanya makosa, polisi walifahamu kuwa unamfahamu muuaji na una ushahidi umeuficha, utashikwa kama na wewe ulihusika, waambie polisi, uoshe mikono yako....’nikamwambia.

‘Mpaka nihakikishe nimekipata ninachokitaka, wana mali nyingi sana,na pia wameharibu, urithi wa baba yao, kwenye huo urithi, mimi nilitakiwa kupewa sehemu ya mali, kwani mimi mzee yule alinitahamini sana, sasa nimewaa,mbia ili hayo yaishe, wanijengee jumba la maana, na liwe na miradi, ili niweza kukaa hapo na kusahau kila kitu...’akasema

‘Wameshalitimiza hilo?’ nikamuuliza

‘Wameanza, nimepata kiwanja, na tayari ujenzi umeanza, sina wasiwasi, ndio unaniona na mimi nastarehe, kama vile mzee, yule, ..kwasababu mzee, alikuwa akinijali, wao wakajifanya wanaanza kunisahau...’akasema.

‘Kwenye huo mtambo, hakuna ushahidi unaoweza kuwakamata hawa watu kuachilia huo ulio nao wewe?’ nikamuuliza, nikamuona keshachoka na maswali, akasema ...

‘Wewe sasa unauliza maswali mengi, ...hebu njoo hapa nikuonyeshe..’akasema na tukatoka hapo akanipeleka kwenye hicho chumba chenye mitambo ya usalama, mimi sikuwahi kukisia kuwa chumba hicho nacho kina mitambo hiyo, kilikuwa chumba, kama stoo, lakini kwa ndani kuna chumba kingine, na humo kuna mitambo kama ile ile ninayoifahamu mimi, usingeliweza kuligudua hilo.

‘Unaona hapa, hapa kuna mitambo, ambayo haijawahi kuzimwa, ile ya juu, inazimwa mara kwa mara, lakini hii ipo wakati wote, na anayeusimamia huu mtambo, ni huyo mtoto wa marehemu, akifika, anahifadhi kumbukumbu zote za siku, na kusiweka, mahali pa usalama, kwahiyo hilo tukio analo yeye, na sizani kama atakuwa hajaharibu hiyo sehemu.

‘Sasa wewe uliwezaje kuipata hiyo sehemu?’ nikamuuliza.

‘Marehemu alikuwa anafahamu hayo yote, kwahiyo kule kwake, kuna mtambo mdogo, wenye mawasiliano na huku,..kila akifika, anaangalia, anawasiliana na huu mtambo mkubwa, anajua ni kitu gani kilitokea, hakuwa na haja ya kufika huku.

‘Kwahiyo wewe ulipofungua, kama alivyokuelekeza mzee, ukaona tukio zima..hukumwambia mtoto wake mkubwa?’ nikamuuliza.

‘Nilipokichukua, sikuwa na haraka ya ki haukiangalia, nilikuja kukiangalia baada ya kusikiliza hayo mazungumzo kati ya mtoto wa marehemu na mama yake,siku ile...ndipo baadaye nikaenda kukiangalia kwa makini, ndio nikaoana tukio lilivyokuwa...aliiingia kwa njia hiyo tuliyoingilia, akajibadili, akavaa kama mafunzi, akajifunika uso mzima, usingeliweza kumtambua...akaenda chumba cha yule mwanadada,akachukua bastola...

‘Wakati huo huyo mwanadada alikuwa kwenye ofisi yake, akafanya haraka na kwenda ofisi ya marehemu ambapo wakati huo, marehemu alikuwa akiongea na yule jamaa, yake, nilishangaa kwanini mlio wa hatari haukulia, kwani yeye alikuwa na silaha, nikagundua kuwa yeye kwa vile ni mtaalamu aliweza kuzima sehemu ya mlio wa hatari....

‘Basi akafika kwenye ile ofisi, ..nahisi baba yake alimuona, kwa pupa, akampiga risasi...na wakati anataka kummaliza huyo jamaa mwingine, ile bastola ikawa imeishiwa risasi, kwa ujinga wake, aliichukua ile bastola, bila kuhakikisha kuwa ina risasi za kutosha, kwa mshituko wa kile alichokifanya, akaibwaga ile bastola kwenye meza...nahisi alifanya hivyo makusudi ili watu wengine, hasa huyo jamaa aliyekuwepo humo ndani ashukiwe kama muuaji,...

‘Ila baadaye niliona mwanadada mwingine akiingia, huyo ndiye waliyekuja kum-kamata kama smhukiwa, wakazidi kuchelewa, na ushahidi mwingi ukawa umepotea...’akasema kwa haraka haraka, nilimpata kwa vile nilishajua mengine...

‘Sasa nikuulize kumbe wewe ulikuwa na ushahidi wote huo, kwanini hukuwafahamisha wanafamilia, yaani mtoto mkubwa wa marehemu?’ nikamuuliza

‘Sikufanya haraka hivyo, hata hivyo, wao yaani yeye na mama yake hawakutaka kuingilia yote hayo, japokuwa walihisi kuwa kuna mtu anahusika, walipopata taarifa ya polisi kuwa huenda ni watu wa ndani, wa usalama waliokuwa maadui zake, waliamua kulichukulia kihivyo, wakaamini, na cha ajabu hawakutaka mali ya marehemu, ....’akatulia kidogo.

‘Kuna mali kidogo ambayo, mwenzao alitengeneza mirathi ya kugushi, ili kupoteza lengo, basi mali hiyo kidogo ndiyo waliyoipata wakaigawa kwa mayatima, na watu waliodhulumiwa na marahemu, hicho kitendo kilimuuzi sana huyu mtoto wake mwingine, maana yeye ndiye alikuwa bega kwa began a marehemu kuzipata hizo mali, lakini hakuweza kufanya lolote akichelea mambo yake yanaweza kufichuka.

‘Unafikiri kwanini huyu mtoto mkubwa na mama yake hawakutaka kuchunguza kwa undani kifo cha baba yake?’ nikamuuliza

 ‘Hapo kwakeli, sijui,...sijui kwanini hawakutaka kufanya uchunguzi wao wa kina...ila mimi nilitaka kumwambia huyo mtoto wa mzee yale niliyokuwa nayafahamu kwa wakati huo, lakini huyo mtoto wake, aliniambia niachane kabisa na maisha ya baba yake, kwani yeye hataki kabisa kuyaingilia na wala hataki mali yake, alishajitoa kwake, yeye amefika kwasababu ni baba yake na niw ajibu wake, kumzika, mengine kama ninayo ni mwambie huyo mdogo wake...

‘Aliponiambia hivyo nikaona basi haina haja...nitautumia huo ushahidi nilionao nionavyo mimi,..siuona-ona sasa unanisaidia, japokuwa nahisi nipo kwenye hatari, hata hivyo, hatari imekuwa ndio maisha yangu,...huwezi jua, kifo changu kinaweza kuwa kama cha marehemu..’akasema.

‘Mimi nakushauri kitu, ongea na polisi, jisalimishe, ili uwe na maisha ya usalama, maana hujui wenzako wamejipanga vipi, kwanza kama ulivyosema kwenye mirathi ya marehemu alikutaja kama mmoja wa warithi wake, huoni utafaidika kihalali ukifanya hivyo....’nikamwambia.

‘Mhh, ni rahisi kusema hivyo, lakini huwajui hawa watu, ...mimi siwaamini, na wala siamini kuwa polisi watawaweza hawa watu, hebu angalia toka marehemu afariki hadi leo, wamefanya nini, ....mimi naona wengi wao, ni wale wale. ..nitafanya nionavyo mimi hapo nitakaposhindikwa basi nitajua la kufanya...’akasema.

‘Je na huyu mtoto wa marehemu akikugundua huoni utakuwa ndio mwisho wako?’ nikamuuliza.

‘Huyo na mama yake hawaniwezi ..mimi kila wanachokifanya ninakiona,...mzee wao alinifundisha mambo mengi, ndio maana aliniamini, ...unaona nilivyo mjanja,  pale nyumbani kwako, napaona kila siku, ...wakiongea , wakipanga, mimi napata taarifa...’akasema.

‘Kwahiyo wao kwa sasa, wanaofisi zao wapi, au hawapo hata nchini, ... wamekwenda wapi ?’ nikamuuliza, maana mama na mtoto wake, hawajaonekana hapa jijini kwa siku ya tatu sasa, nikaona niulize hilo swali ili watu wa usalama wasikie na wajue jinsi gani ya kufanya.

‘Wamekwenda Kenya, kuna miradi yao wanaifuatilia, ilikuwa miradi ya marehemu, ilikuwa haijakamlishwa kuhamisha umiliki kutoka kwa baba kwenda kwa huyo mtoto, .....wakilimaza hilo, basi tena, wao sio wenzetu..lakini kwanini wachukue kila kitu, kwanini mimi wasinipe haki yangu, ndio maana nimelifanya hili, kwa hivi sasa kila kitu wameniachia mimi mpaka wakirudi...’akasema

‘Kumbe sasa wewe ni bosi...’nikasema.

‘Nafahamu wakirudi wanaweza kuja na ajenda ya siri, lakini mimi nitaigundua tu, ..hawaniwezi...’akasema.

‘Inakuwaje mtu afahamu siri za watu wengine, hicho chombo alichokuachia marehemu kipoje...naona dunia ina mambo mengi, mimi mambo mengi siyajui, naona kama miujiza tu...?’ nikamuuliza

‘Unafikiri ni chombo kikubwa, ni sawa na simu tu, unatembea nayo, ukitaka kuangalia mahali fulani ulipoweka vitu vyako, unabonyeza namba, unawaona, ...kama unataka kukihamisha hicho kidude kwenye komputa unakiweka, ...hapo unaweza kuangalia, kama unavyoangalia picha za kawaida, wanawasanifu watu kweli kweli, lakini mpaka upandikize chombo fulani hapo unapotaka kupata taarifa ....mimi ni mtaalamu bwana..’akasema kwa sauti ya kilevi.

‘Sasa wewe una uhakika gani kuwa mwenzako huyo naye hakufanyii kama unavyo mfanyia yeye,huenda huko alipo anakuona..huenda hata nyumbani kwako unapoishi kapandikiza kitu kama hicho?’ nikamuuliza.

‘Kuna kifaa kingine cha kugundua hivyo vitu vya kupandakiza, mimi kama mlinzi ninacho, kama kuna kitu kimepandikizwa kwako kinakuashiria, lakini sijawahi kumuonyesha huyo mtoto wa marehemu, aliwahi kukipandikiza kwangu, nikakigundua, kwahiyo mimi nipo mbele zaidi yake....’akasema.

‘Wao wanarudi lini?’ nikamuuliza

‘Kesho, ila kila siku nawasiliana nao, wanaweza wakaja hata leo, kwa usalama mara nyingi hawasemi lini wanafika, ndio maisha ya watu kama hawo, kama alivyokuwa marehemu, ila mimi nafahamu ni kesho.....’akasema.

Mara simu yake ikalia, akaiangalia, na kusema, ...

‘Bosi,...naona keshafika, huenda wapo hapo uwanja wa ndege,...sasa mimi kwa hali niliyo nayo,sijui kama nitaweza kuwafuata, inabidi nimwambia mtu akawachukue, ngoja niongee naye kwanza, maana nahisi nimelewa sitaweza kuongea nao katika hali hii, au unasemaje mpenzi,....’akasema.

‘Kweli...’mimi nikasema huku nikijua sasa kazi imekwisha, nikahakikisha namsogelea ili kusikia anachoongea, sikuweza kusikia huyo bosi wao anaongea nini, lakini alivyokuwa akijibiwa nilisikia, jamaa akawa anajiuma uma,..mimi kwa haraka nikawasiliana na watu wangu kwa ujumbe wa simu, na wao wakanijibu kuwa wananifuatilia kwa karibu,nisiwe na wasiwasi.

‘Haloo bosi, mnasemaje?’ nikamuuliza huku akijaribu kunikwepa ili nisiwe karibu naye, lakini sikumpa nafasi hiyo nikamsogelea, akawa sasa anaongea na simu, akasema;

‘Unasema mumeshafika, mpo nyumbani, mbona hamkuniambia nije kuwapokea hapo uwanja wa ndege, nipo hapa karibu kabisa...!’akasema kwa akionyesha mshangao.

‘Ohoo, ndio nilizima kidogo, maana nina mtoto, nastarehe kidogo, siunajua leo ni mapumziko bosi...sasa sikutaka mambo yangu yaonekane huko, nitawasha,...nikimaliza..nipe nusu saa,...sasa hivi, kwanini bosi, mbona unaniharibia starehe zangu, unasema kuna nini..hapana bosi, mimi nina uhakika hakuna kitu kama hicho...una uhakika,...’akasema na nilimuona akiwa na wasiwasi.

Baadaye alinigeukia, na kusema;

‘Mhh, naona mambo yameharibika, kitumbua kimeingia mchanga....’akasema akionyesha wasiwasi.

‘Kuna nini kimetokea....? nikamuuliza

‘Jamaa anasema kafika tu ,polisi wamemvamia, ananihisi eti mimi ndiye nimemuuza, polisi wameshafika kwa bosi, haapo kajiiba ,kusogea pembeni, kunipa tahadhari, nihakikishe hawafiki huku,  sasa naona mambo yangu yameharibika, sijui nifanye nini, ..kwanini polisi wamefanya haraka kiasi hiki hata ujenzi haujakamilika...’akasema, na mimi nikamwambia.

‘Wewe usijali, ..cha muhimu ni kutoa ushirikiano na polisi, maana inavyoonekana polisi wameshafahamu ni nani muuaji, sasa ukijificha, na wewe utashikwa kama mshirika wao..mimi naona hapa hakuna usalama tena nataka kuondoka....’nikamwambia na yeye akawa kama anafikiria jambo.

‘Sasa bosi  kasema niharibu kila kitu, ....’akasema

‘Wewe, usije ukafanya hilo kosa, unaharibu vidhibiti vya polisi, huoni kuwa wewe utaonekana  mshirika wa hayo mauaji..’nikamwambia.

‘Ok, nimekuelewa, lakini kwanini huyu bosi anasema hata hivi nipo na watu wa usalama, mimi simuelewi kabisa... ngoja nikawashe hiyo mitambo niliyokuwa nimeizima, tuondoke zetu, wameniharibia starehe yangu,....nisubiri...’akasema na mimi nikamuuliza

‘Tutatokea wapi?’ nikamuuliza nikimchelewesha na yeye akaniangalia halafu akaingalia kule tulipoingilia, na kusema

‘Hukohuko tulipoingilia....’akasema, na kabla hajamaliza  mara tukasikia mlango ukigongwa, akaiangalia huku akionyesha wasiwasi, akaniashiria kwa mkono, nitoke, kwa kupitia ule mlango tulioingilia, huku yeye akaianza kuelekea kwenye kile chumba cha ile mitambo, lakini kabla hajaufikia huo mlango, mara mlango ukafunguliwa.

Wa kwanza kuingia alikuwa askari, mwenye sare, na baadaye wakaingia wengine, wakiwa wamevalia kiraia, wote hawo nawafahamu,...

‘Sisi ni askari usalama, mpo chini ya ulinzi, hakuna kusogea au kugusa kitu chochote..’akasema huyo mwenyesare, lakini hakuwa na silaha yoyote zaidi ya rungu, ...nikajua kwanini, wasingeliweza kuingia na silaha kwa kupitia upande wa juu, mlio wa hatari ungelitushitua, na huyu jamaa angelikimbia, ...lakini na mara tukasikia sauti kutoka kule tlipoingilia wakaingia askari wengine, hawa walikuwa na silaha, na hapo hapo mlio wa hatari ukaanza kulia...

‘Kwanini mnanivamia nimefanya kosa gani?’ akauliza na wao wakamshika na kumfunga pingu, na kumweka chini ya ulinzi, mimi taratibu nikatoka,nikijua nimetimiza wajibu wangu ...kazi nyingine yote waliimalizia wao, kila kitu kikawa wazi, muuaji akajulikana, na ushahidi wote ukapatikana,mtoto na mama yake, ndio waliomuua Makabrasha,...’akasema huku akimwangalia mwenyekiti.

‘Inatosha, tunakushukuru sana, mengine yote, tunayafahamu kwa wale waliokuwa wakifuatilia hiyo kesi na kuhudhuria mahakamani, kuwa wahalifu hawo, wanatumikia jela zao, haki imtendwa, iliyobakia ni sisi kama familia, tutimize yale yanatuhusu, na kusuluhisha tatizo la familia hii, kama wazazi ni lazima tutimize na sisi wajibu wetu,..’akasema mwenyekiti.

‘Sasa ni ajenda ya mwisho, ajenda hii ni hukumu, au mstakabali wa ndoa ya mke na mume wa familia ....na hapa mimi sitaingilia sana, maana wanandoa waliosababisha hiki kikao wapo hapa, na walishapata muda wa kukaa pamoja na kulijadili hili, nasikia bado kuna mvutano, ...sasa mimi kama mwenyekiti, nahitajika kutumia rungu langu la uenyekiti...kulimaliza hili tatizo,..., 

NB: Naona tutamalizia sehemu ijayo, kwa leo tuishie hapa, je ni nini maamuzi ya wanafamilia hawa, tutaona sehemu ijayo.

****** Nashukuru sana kwa dua zenu, hali ya afya imetengamaa..Tupo pamoja*******

WAZO LA LEO: Ubaya na matendo mabaya, sio sifa ya kujinadi mbele ya wenzako, kuwa mimi ni mjuzi wa ubaya fulani, watu hawaniwezi, nk....kwanini tusijisifu kwa matendo mema, tuangalie wenzetu waliobuni , na kugundua mambo ambayo mpaka leo yapo, yanatumika kwa manufaa ya jamii, ina maana watu hawo, ni kama vile bado wapo hai, ...hizo ndio sifa njema,..., 

Ni mimi: emu-three

1 comment :

mama brenda said...

Hongera sana m3 hakika hii simulizi inafundisha sana dah roho inauma inaiasha maana ni simulizi ukinikuta nasoma niko bize hadi mumewangu anatamani apasue cm coz hata ukiniita sisikiii big up emu3 but naamini mwisho wa mkuki kwa nguruwe ndio mwanzo wa simulizi nyingine