Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, January 17, 2014

Mkuki ni kwa nguruwe-63


‘Ndugu wajumbe hiki ni kikao cha hitimisho cha kikao kilichopita, kama mnakumbuka vyema, kikao kilichopita tulikikatisha kutokana na muda, na pia wajumbe walishachoka, na pia tukaomba wale wajumbe waliotarajia kusafiri waahirishe safari zao, lakini kutokana na mambo yaliyokuwa juu ya uwezo wetu, mengi hayakufanyika kwa wakati, kama mlivyoona wenyewe,...sintofahamu iliyotokea na baadhi ya wajumbe wa kikao hiki wakakamatwa.....’Mwenyekiti akaanza kuongea.

‘Poleni sana kwa mkasa huo, kama wanafamilia sote lilitugusa, ndio maana tulikuwa bega kwa bega kuwaombea dhamana wale waliokamatwa, lakini tulikataliwa kutokana na pingamizi za wanausalama, na mliona ni kitu gani walichokuwa wakikitafuta hadi kufanikiwa kile walichokitaka...’akaendelea mwenyekiti.

‘Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu polisi kwa jitihada zao, tukaona kuwa wanatusumbua, wanatumia mabavu nk, lakini wakati mwingine inakuwa haina jinsi, kwani  raia ambao walitakiwa kutoa ushirikiano, wanakuwa wagumu, wanaficha ukweli kwasababu zao binafsi, na hapo ndipo polisi wanapoamua kutumia nguvu...na wakati mwingine wanafanikiwa, kama mlivyoona kwenye tukio hilo.

‘Siwezi kuwalaumu sana wale mliofanya hivyo, lakini kuna mambo ambayo nataka kuyaweka wazi kama wanafamilia, huenda wengine hawatanielewa, lakini ni vyema nikaeleza sera na taratibu za familia hii, mimi bado ni mwenyekiti wake, na kama bado mnanitambua hivyo, ni lazima nisimamie yale mamlaka ya kifamilia...’akatulia.

‘Katika familia hii, tumejitahidi sana kuwa mbali na kashifa,...na hili nimekuwa nikilirudia mara kwa mara katika kila kikao, na kile anayekuja kuoa kwetu, au tukimleta muolewaji hapa, ninajaribu kuwaasa kuhusu hili, lakini hali inazidi kubadilika, ...kiukweli hili lililotokea limetutia doa kubwa, na sijui tutafanyaje ili tutaweza kujiisafisha, japokuwa tumesalimika lakini baada ya juhudi kubwa sana...sikufurahia kitendo hiki, nawaonya ten asana, hili lisijirudie tena.

‘Hebu niwauliza ni nani anayependa kukaa jela, hivi jela ni kuzuri,....hivi ni nani anapenda kukaa na wasiwasi, akakosa raha na amani akawa anaishi kwa mashaka-mashaka, hakuna anayependa kuwa hivyo, sasa kama hatupendi  kuwa hivyo, kwanini tujiingize kwenye yale ambayo tunayaona yanaleta kashfa, yanatuweka katika hali ya kukosa amani na usingizi, kwanini....?’ akawa kama anauliza.

‘Ndio maana katika familia hii tunalipinga sana, na wale wanao-olewa au kuoa ndani ya familia hii, nimewaonya na nitendelea kuwaonya tena na tena, hatutaki kashifa, na kama una dalili na mienendoo hiyo tutakusakama, mpaka ubadilike....mimi kwa hili nimeona kuna upuuzaji wa kimakusidi,na nilipojaribu kulikemea kwenye wanandoa, wengi wamekimbilia kusema tunaingia lia ndoa zao, ...hivi kweli kukutahadharisha, na kukuonya ili uishi maisha ya amani na upendo ni kuingilia ndoa zenu, hilo kwakweli mimi kama mwenyekiti wenu sitalivumilia, labda mniondoe ...uenyekiti...’akasema .

‘Sasa basi, tunaanza kikao chetu, na ajenda moja kubwa, ni hukumu,...lakini kabla ya hukumu, ningelipenda tuliweke wazi tukio zima lilivyokuwa, najua kila mmoja ana dukuduku la kufahamu ni nini kilitokea,hadi muuaji wa Makabrasha akapatikana, tunashukuru kuwa mwenzetu ambaye alishirikiana na polisi hadi kupatikana huyo mtu amekubali kuwepo tena kwenye kikao hiki.

‘Yeye tulimualika na mumewe, na mara nyingi kwenye vikao vyetu, hawa watu wanakuwepo kwasababu wao wenyewe wamekubali kuwa sehemu ya familia yetu ....sasa ningelipenda kumuomba  mmoja wa wahusika, ambaye kwa namna moja au nyingine, japokuwa mahakama pia imempa onyo, lakini alijitolea muhanga hadi mtu aliyekuwa akitafutwa akapatikana,....tunakuomba, mke wa docta uchukue nafasi hii utuliezee japokuwa kidogo, jinsi ilivyotokea hadi mkafanikiwa kumpata Muuaji...’akasema mwenyekiti,

Mke wa docta, akakohoa kidogo na kusema;

‘Mhh, naona hiyo mke wa docta, itaendelea kuwepo, ....’akasema huyo msemaji, na mwenyekiti akadakia na kusema;

‘Samahani, unafahamu hilo halijawa wazi kwenye hiki kikao ndio maana tunaendelea kukuita mke wa docta,....nimesikia juu juu kuwa wewe na mume wako mumeshapitisha shauri lenu, lakini kwa vile ulishaingia kwenye hi familia bado sisi tutaendelea kukutambua kama mwanafmilia hadi hapo mwenyewe utakapoamua kujiondoa...’akasema mwenyekiti na kumwangalia aliyekuwa mke wa docta.

‘Kwakweli mazoea yana taabu, hata mimi mwenyewe huwa ninajisahau na kujiita mke wa docta, lakini ukweli ndio huo, na kuanzia leo ningelifurahia mkisema, aliyekuwa mke wa docta,...nimeamua hivyo kwa hiari yangu mwenyewe, baada ya kuona kuwa sitakuwa nimemtendea mwenzangu haki , kwa yale yaliyotokea mimi nimeona niwajibike, hata hivyo kutokana na kazi zangu mwenywe nimeona kuwa nahitaji kukaa mwenyewe ...maana huwezi kulazimisha jambo kama moyo hautaki.

‘Ni ukweli usiopingika kuwa tumeshamaliza taratibu zote za talaka, kisheria, na hivi mnavyoniona nipo mbioni kuelekea kijijini, huko nimeshajipanga, nina miradi yangu na maisha yangu, na nitakaa kwa muda hadi hapo nitakapoamua ni nini kingine cha kufanya, maana ukiingia kwenye hii fani, muda wote unahitajika, ..ila kiukweli kutokana na haya yaliyotokea nisingelipena kufanya kazi za kutumwa-tumwa tena, inafikia sehemu unajizalilisha,...ndio kazi, lakini jamii haiwezi kukuelewa, sasa hivi nataka kujituma, na kujiajiri....’akasema aliyekuwa mke wa docta.

‘Kwanza kabisa nawaombe radhi kikao hiki na wanafamilia hii, kwa hayo yaliyotokea, mimi kama binadamu nimkosaji, na mkosaji anastahili kusamehewa, ...ni kweli nimekosa sana, hasa kwa mume wangu, nimeshamuomba sana masamaha, na japokuwa kanikubalia, lakini bado nahisi sijasamehewa, maana kosa nililolifanya ni kubwa sana,...’akasema huku akimgeukia docta.

Baadaye akainama kidogo, halafu akamwangalia mwenyekiti, naona nianze kutoka maelezo japokuwa ymeshapita, lakini kwa faida ya wanafamilia, nitaelezea ilivyokuwa;

‘Kwa ujumla aliyemua Makabrasha ni mtlaamu wa hali ya juu, aliyefanya hilo jambo kwa kuangalia nyakati, ..., na aliyapanga hayo maujai kwa utaalamu wa aina yake...ilikuwa vigumu sana kumnasa, kwanza alienda na muda na pili akawa antumia uzaifu wa watu, na kuyachanagnya matukio, kiasi kwamba polisi walifikai kuhisi huyu au yule, bila kupata ushaidi kamili.

Hata mimi mwenyewe sikuwa na uhakika na kile nilichokuwa nikikiwaza kwani hata yule niliyemuwaza kuwa ndiye, mwisho wa siku nilijikuta nakosa ushahidi kamili, na hata nilipotoa wazo kwa polisi, wao walishia kuniona ni muongo, najaribu kukwepa ukweli, kwani wao walishafikia kunishuku mimi kuwa ndiye niliyefanya hayo mauaji, kwani mimi ndiye niliyekuwepo kwenye hilo jengo, na silaha iliyotumika nilikuwa nayo mimi....

Lakini mwisho wa siku wakakosa ushahidi wa kunikamata mimi kama mshukiwa muhimu wa mauaji hayo, maana hata mimi nafahamu sheria na jinsi ya kujitetea, na kwahiyo ikabidi wanitumie mimi sasa ili tuweze kulifanikisha hilo, tukaanza mchakato wa pamoja..

Kwanza niliwaambia ili kumpata huyo muuaji, kwanza tumchambue huyo mtu, aliyefanya hivyo ana sifa gani, kwani mimi nilikuwepo humo ndani, na mazingira ya humo ndani na yafahamu, mtu hawezi akaingia na silaha bila kutokea mlio wa hatari,....nikawaambia ni lazima mtu huyo awe analifahamu hilo, pili awe,analifahamu hilo jengo vyema, maana mauaji hayo yalifanyika kwa muda mfupi, na kwa tahadhari ya hali ya juu, ...

Niliwaambia kuwa mtu huyo inaonekana kama alipita mlangoni ni mtu nayefahamika, na hata walianzi hawakuwa na wasiwasi naye, kama alipita mlangoni,hakupita mlangoni, atakuwa alipitia wapi, kwani hakuna njia nyingine zaidi ya hapo mlngoni, na mlngo wa kuingia , kwenda juu ni mmoja tu..

Jengo hilo lina juu na chini, kwahiyo mtu huyu anafahamu hata ramani ya jengo, wengi hawafahamu kuwa kuna sehemu ya chini ....

Nikawaambia huyo muuaji, alipomaliza hiyo kazi atakuwa alikimbilia vyumba vya chini na kukaa huko hadi hali ilipotulia, ...na ina maana huyu muuaji ana chumba maalumu cha kujificha huko chini, sasa ni nani anayelifahamu hilo jengo vyema, zaidi ya Makabrasha na mjenzi wake....hapo ikawa kazi kumtafuta mtu anayejulikana kuwa analifahamu hilo jengo vyema, ..

‘Lakini pia mtu huyo awe anafahamu mtandao wa ulinzi wa lile jengo, awe anaweza kuusimamia huo mtandao, bila watu kujua, na awe anaweza kuona ni kitu gani kinafanyika ndani ya hilo jengo, ina maana basi walishirikiana wawili, ili mtu aweza kufanya hilo jambo bila wasiwasi....hapo polisi wakasema hakuna, zaidi ya Makabrasha mwenyewe,..

'Mimi nikawaambia wapo watu wengine wawili,ninaowafahamu mimi ...moja ni mtu aliyaminika sana na Makabrasha, na huyo likuwa mlinzi wa siku nyingi wa marehemui, huwa hajulikani sana machine mwa watu, na anamlinda makabrasha akiwa hajionyeshi, anakuwa kwa mbali..

‘Ni nai huyo mtu..?’ wakaniuliza.

‘Ni mlinzi wake wa karibu, ...nilipowaambia hivyo, wakamtafuta huyu mtu na wakamkamata, wakamfanyia uchunguzi, ikaja kugundulikana kuwa ni kweli siku hiyo ya mauaji huyo mlinzi alikuwepo, na alifika hapo lakini akandoka, kwani aliitwa nyumbani mke wake alikuwa mgonjwa, sio mgonjwa mja mzito, akaruhusiwa na kuondoka, na walipolifuatilia hilo wakaona ni kweli, muda mwingi, alikuwa haospitalini, na alipotoka hapo akaelekea nyumbani, na mauaji hayo yalifanyika kipindi akiwa hospitalini., kwahiyo akawa hausiki.
‘Haya tuambie huyo wa pili ni nani,....?’ wakaniuliza

‘Ni mtoto wa Makabrasha,...’ nikawaambia na wao wakaguna na kuniambia hilo haliwezekani, mtoto hawezi kumuua baba yake, hata mimi sikumpa nafasi kubwa huyo mtu maana nijuavyo mimi, siku ile muda wote hakuonekana kwenye jengo, na kama angelionekana walinzi wangeliniambia,..hakuna hata mlinzi mmoja aliyemuona jamaa huyo akiingia kwenye jengo, sasa alipitia wapi, nahakuna njia nyingine ya kupitia zaidi ya hapo mlangoni, kwahiyo huwezi kumshuku yeye hata mara moja, ....hapo nikawa sina la kusema, ina maana aliyebakia ni mimi, ....’

‘Na wa tatu ni wewe....’wakasema polisi

‘Hapana mimi nisingeliweza kumuua Makabrasha, kama ningelitaka kufanya hivyo, ningelishamuua siku nyingi tu.....’nikajitetea.

‘Tuambie ukweli, maana wewe ulisema alikufanyia mambo mengi mabaya na ulikuwa na hasira naye.., kama sio wewe ni nani mwingine..?’ polisi wakaniuliza.

‘Mimi nataka tusaidiane kwa hili, nina uhakika muuaji yupo, na anatuchezea akili, ninachowaomba, mimi ijulikane kuwa bado nipo rumande, huku mkinipa nafasi ya kutoka kila ninapohitaji kutoka, ili niendelee na uchunguzi wangu, nina uhakika tutampata huyo muuaji, lakini kwa njia zangu, msiniingilie...’nikawaambia.

‘Hatuwezi kukuachia kwasababu sasa hivi wewe ni mshukiwa namba moja,na pili kuna tetesi kuwa kuna watu wanataka kukuua...’wakaniambia.

‘Kwanini watake kuniua, kama sio kwamba wao ndio wauwaji, na sasa wamoena  kuwa nilikuwa mbioni kuwafichua ndio maana wanataka kiniua, kwanini hamjiulizi hilo, nipeni hiyo nafasi, nina uhakika tutampata huyo muuaji,..’nikawaambia polisi.

‘Hebu tuambie mpango wako...?’ akaniuliza mpelelezi wao, nikamuambia hii kazi nataka kushirikiana na mmoja wa wapelelezi wao ninayemuamini, akaniambia sawa kwanini yeye, nikawaambia kwa vile namfahamu na nimeshawahi kufanya kazi na yeye...hata hivyo wakataka wafahamu mipangilioa yangu ipoje..’akaniambia.

‘Mimi nawaomba jambo moja, mimi nitaendelea kuwepo humu, ila muda fulani fulani nipeni ruhusa ya kutoka, na nyuma yangu awepo huyu mpelelezi, na mlinzi wa kificho, asijulikane kabisa, na pili  chombo cha kuvaa ambacho, nikikivaa mtaniona kila ninapokwenda...’ wakaitana na kukaa kikao chao, wakajadiliana na baadaye wakanikubalia, lakini ni baada ya mabishano ya marefu, kwani wao walitaka kila hatua niwe pamoja nao, nikawaambia kwa njia hiyo hatufanikiwa. ..

‘Siku ya kwanza sikufanikiwa, na ya pili, lakini ya tatu nikafanikiwa, na siku zote hizo nilikuwa nikienda kwenye hoteli moja ambayo jamaa hawo ninaowashuku hupenda kwenda kustarehe, hapo kuna kila starehe, na nilijua udhaifu wao, ni pombe na umalaya...

 ‘Mimi nikajiweka kinamna, nilipewa gari, la kifahari, na pesa kidogo, nikajifanya kama binti wa geti kali, nilijibadili kabisa, na ungeniona usingelinitambua kuwa ni mimi, huwa nikiwa kazini nabadilika kabisa,....

‘Wanaume kwa uroho wao, waliponiona ile siku ya kwanza, wakaanza kunimezea mate, maana nilitokelezea, hata ingelikuwa ni nani, angenitaka. Wakwanza nikamtolea nje, maana sikuwa na haja naye, akaja mwingine na mwingine, hadi siku ya tatiu alipokuja mtu wangu ninayemtaka....

‘Mtu niliyemlenga sana na huyu mlinzi wa karibu wa Marehemu, na sasa alikuwa akifanya kazi kwa mtoto wa Makabrasha, huyu nilikuwa bado sijakata tamaa naye, ..hisia zangu zilinituma kuwa atakuwa anahusika, na hata kumuua Makabrasha, na kwanini aendelee kuwa karibu na mtoto wa Makabrasha, wakati kipindi cha uhai wa marehemu, hawa watu wawili walikuwa hawapatani.

‘Siku hiyo huyu jamaa akanijia, na alionekana kuwa na pesa kweli, nikahisi wana jambo wamelifanya, nikajibaragua na baadaye tukaelewana, hakunitambua kabisa kuwa ni mimi, hata ingelikuwa nani, asingelitambua, ...tuakaanza kuongea kidogo, moja likazaa jingine, tukawa marafiki wa muda mfupi, mimi niafahamu sana hiyo kazi, nina uzoefu nayo...jamaa bila kujijua akanasa kwenye anga zangu....sikumchelewesaha, wakati anakwenda kujisaidia mimi nikaweka kitu kwenye kinywaji chake.

‘Kuna aina ya madawa ukimwekea mtu, analewa, anapagawa, akili inamchenguka, ...lakini hapotezi fahamu, wanaitumia sana majasusi wanapotaka kupata taarifa kwa mtu,...niliiomba kwa watu wa usalama, wakanigaia, na hiyo ndiyo ilikuwa silaha yangu, sikutaka bastola hapo...

Aliporudii kutoka kujisaidia, nikaendelea kumelegezea, akajisahau na kuanza kunywa kinywaji kile bila kufikiri mara mbili, akaanza kulegea, na akili ikaanza kumtoka, na mimi hapo hapo nikamwambia;

‘Mimi ni mchumba wa mtu, sitaki kuonekana onekana je, hakuna sehemu nyingine ya siri , tunaweza kustarehe, nay eye bila kujua huo mtego akaniambia;

‘Kuna sehemu naifahamu, twende.....mimi kwanza nilijifanya nina wasiwasi na mchumba wangu anaweza kuniona, yeye akasema jambo nzuri, gari langu tuliache hapo, atamwambia mlinzi, na tuondoke na gari lake, mimi nikaona huo ndio ushauri mnzuri...tukatoka hapo tukainga kwenye gari lake,  baada ya kuongea na mlinzi anayemfahamu na kumkabidhi gari langu.

‘Unajua nimekua nikikuona mara kwa mara, lakini nilikuwa sipati muda wa kuongea na wewe maana mara nyingi nakuja na mchumba wangu....’nikamdanganya.

‘Kweli siamini ina maana siku nyingi unafika hapa, mbona nilikuwa sikuoni?’ akaniuliza huku akiniangalia kilevi.

‘Nafika mara moja moja,lakini mara nyingi nakuwa na mchumba wangu,  siunafahamu tena,...sisi ni wachumba wa watu, tunatakiwa kuwa na tahadhari...’nikasema nikamuona ananikodolea macho, maana alikuwa akiyalazimisha, akasema;

‘Ni kweli sura yako kama niliwahi kuiona mahali...’akasema na kunishitua lakini nilikuwa na uhakika hawezi kunifahamu, maana kuna utaalamu wa kubadili nyusi, na rangi za macho, na nywele, sikuhitaji kuvaa ngozi bandia,...mimi katika kazi yangu hiii wanapenda kuniita kinyonga, ....naweza tukawa pamoja sasa hivi nikaingia chumbani nikitoka hunikumbuki tena....

Basi, yule jamaa akasema kwa vile naogopa, atanipelekea sehemu ambayo anaiona ni salama, tukaingia kwenye gari lake, na kuanza safari, kama nilivyotarajia nikaona tunelekea uwanja wa ndege, nikajua ni kule kule, na mtego umefanikiwa,...tulipofika karibu na jengo la Marehemu, jamaa huyo hakulipeleka moja kwa moja kwenye maegesho ya mgari, akalipitisha kwa nyuma, hadi sehemu nyingine, kunapohifadhiwa magari ya jengo la pili yake, akachukua ufungua na kufungua geti, kulikuwa na geti dogo la jengo hilo la pili..kulikuwa hakuna walinzi.

‘Huku ni wapi? Nikamuuliza

‘Huku ni kwa rafiki yangu, ila nataka tuingie kwenye hilo jengo hapo, ni la marehemu, kuna hoteli ya ndani kwa ndani, humo tutastarehe tupendavyo, huyo mchumba wako hatakuona kabisa..’akasema kwa sauti ya kuonyesha hayo dawa imemchukua na sikupenda hiyo dawa iishe nguvu kabla hatujaingia ndani.

Tulipoingia kwenye hilo geti dogo, nikaona akifungua mfuniko, kama ile mifuniko ya mashimo ya maji machafu, nikamuuliza;

‘Unafanya nini ...?’ nikamuuliza

‘Usijali hii ni njia muhimu ya kuingia ndani, hakuna anayeifahamu zaidi yangu mimi na marehemu na mtoto wa marehemu....’akasema.

‘Huyo marehemu unayemtaja ni nani?’ nikamuuliza

‘Mhh, alikuwa akiitwa Makabrasha ameshafariki....’akasema

‘Mhh, yaani kafariki na kuliacha jengo nzur I hivyo, na wewe ni mtoto wake?’ nikamuuliza

‘Hapaan yupo mtoto wake, ndiye analimiki kwa sasa..’akasema

‘Na huyo mtoto wake ni nani anaonekana ni tajiri sana....?’ nikamuuliza

‘Achana naye, akikuona wewe najua ataninyang’anya anapenda sana kuninyanganya mawindo yangu...sio mtu mzuri, ...hana huruma, akikuamba utakuwa chakula cha mchwa utakuwa kweli...haogopi, ...’akasema na moyoni nikasema mumekwisha, ...kumbe kuna njia hii ...nikatulia kwanza, sikutaka kumuuliza sana, asije akanitilia mashaka, akafungua kile kifuniko na kuninyoshea mkono kuwa nisogee pale, hakufahamu kuwa mimi ni mwanajeshi.

‘Sasa tunaingia, ni kusafi kabisa, kwa nje kunaonekana hivyo, lakini ukiaanza kuingai utakutana na ngazi, zinakwenda moja kwa moja hadi kwenye hilo jengo la marehemu, hii ni sehem yake maalumu ya usalama...’akasema.

‘Oh, kwanini awe na njia za namna hii, mnauza madawa ya kulevya nini?’ nikamuuliza

‘Matajiri wengi wana mbinu zao za kuishi, wanajihami kwa kila njia...’akasema.

‘Sasa kaam ni hivyo huyo marehemu alikufa kwa ugonjwa au aliuwawa?’ nikamuuliza

‘Walimua bwana,..alikuwa bosi wangu, nikiwa na shida, ananisaidia, sasa nimebakia na huyu mnyama, ananifanya kama mtumwa wake, ianbidi nitumie mbinu za kumuibia, sina ujanja...kama jana nimemchomoa mamilioni ya pesa..bila hata kufahamu, akabakia kusema kaibiwa na watu wa benki...’akasema.

‘Oh kumbe walimuua, jamaa wa watu, kwanini walimuua....?’ nikamuuliza

‘Mambo ya mali hayo, unafikiri, ukiwa na watoto waroho, wanawake waroho, na una mali, ujue upo hatarini, na ikizingatiwa hata hizo mali umezipata kwa dhuluma, umekwisha, .mke au mtoto wako mwenyewe anaweza kukumaliza.....’akasema na kutulia.

'Kwahiyo ina maana waliomuua ni mtoto wake, au mke wake, au walishirikiana kumuua....?' nikamuuliza
Akafungua mlango wa kuingia kwenye jengo, huku akiwa kimiya, halafu akaniangalia na kusema;

'Tumeshafika...karibu hoteli ya maraha ya Marehemu....'akasema na mimi nikamuuliza

'Kwanza nijibu swali langu....'nikasema

NB: Tuishie hapa kwa leo maana afya sio nzuri, na mitihani ya kimaisha inani kwaza, yote maisha..., nitajitahidi tutamalizia sehemu hii na hitimishi la kisa hiki kwenye sehemu ijayo.


WAZO LA LEO: Mali na watoto ni mtihani mkubwa kwa wazazi, ukiwa nazo ni nzuri lakini ina mitihani yake, kwa watoto ujue jinsi gani ya kuwalea, ili wote wakulie katika maadili mema,  ujue muhimu kwa watoto wako ni elimu. Elimu ndio urithi mkubwa kwa watoto na sio mali.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Pole na yanayokusibu, Can't wait for the mwisho wa story please kesho tuwekee.

Pam said...

Pole na kuumwa, pona haraka. Makwazo ya maisha ni sehemu ya mapito yetu hope ufumbuzi utapatina.