Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, January 10, 2014

Mkuki ni kwa Nguruwe-61


Shahidi alipoona mwenyekiti anapiga simu, kwa minajili ya kuwaambia kuwa yeye anafahamu yaliyotokea humo, na huenda anamfahamu muuaji wa Makabrasha, shahidi akasema;

‘Mwenyekiti tafadhali nakuomba usiwaambie polisi kuwa mimi nafahamu kilichotokea siku hiyo, nay a kuwa nimesema kuwa namfahamu huyo muuaji wa Makabrasha. Elewa nafasi yangu kwa sasa,kwani nikiwaelezea hayo, kuna watakaokimbilia kunikamata na kuniweka ndani, lakini utambue kuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine, na hawataki ukweli ugundulikane.

‘Nakuahidi mwenyekiti, wakati ukifika, mimi mwenyewe kwa wakati wangu nitakwenda kuonana nao, bado kuna mambo nayafuatilia, na kama wangelitaka kunikamata, wangeshamikamata , hujiulizi kwanini hawajanikamata, ina maana wao ni wajinga muda wote huu wasifahamu kuwa nilikuwemo kwenye hilo jengo wakati Makabrasha anauliwa, wanafahamu, lakini wana mbinu zao, kuna jambo wanalifuatilia, a wanafahami ni kitu gani ninachokifanya....’akasema.

‘Kwahiyo unavyosema hivyo, wewe na polisi mnashirikiana?’ akauliza

‘Sijsema hivyo mwenyekiti, naomba usininakili vibaya, mimi sina maingiliano na polisi, na kama ni uchunguzi wa kazi zangu, naufanya kwa manufaa yangu,au kwa mtu aliyenituma, mimi ni mwekezaji tu...’akasema.

‘Kwa mimi nilivyoona,  ninahisi umeifanya hiyo kazi hasa hasa kwa manufaa ya mpenzi wako wa zamani, na ulikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili yake, nimeyafuatilia maelezo yako yote, na hasa pale ulipofikia kuacha kazi kwa mtu wako wa kwanza kwa ajili ya kwenda kupambana na wale walioingilia maisha yenu na mipango yenu,

‘Ni sawa kila mtu ana ndoto zake, lakini tuwe makini katika kujitolea muhanga kwa nafsi nyingine, kwani hatuna uhakika kuwa kweli huyo tunayejitolea muhanga kwake, yupo nawe moja kwa moja, huenda mwenzako anakutumia tu, kwa masilahi yake, hali kama hiyo ni hatari. Kwa uhakika zaidi, hebu mwangalie mwenzako, alivyokufanyia, wewe naona humfahamu vyema huyo mpenzi wako wako, kama unavyodai unamfahamu kihivyo, yeye kwa tabia yake, imeonyesha dhahiri kuwa ni mbinafsi, yupo tayari akutumie wewe kwa manufaa yake, na mwisho wa siku anaweza asiwe nawe tena....’akasema mwenyekiti.

Mume wa familia, akainua kichwa na kumwangalia mwenyekiti, akiwa kakunja uso,wa kutafari, nahisi kuna kitu alitaka kukizungumza, lakini akawa anasita kukiongea, hakusema neno, alimwangalia mwenyekiti kwa muda, halafu akageuka kumwangalia huyo shahidi, wakaangalia, na baadaye akatikisa kichwa kama kusikitika,  halafu akainamisha kichwa chini na kutulia, hakusema neno, na mwenyekiti ambaye alikuwa akimwangalia, akitaraji kauli kutoka kwa mume wangu, lakini alipomuona huyo mtu katulia tu, akaendelea kusema kwa kumchokoza huyo mtu;

‘Kama ni uwongo kwa hitimisho langu, kama nimemzulia uwongo, huyo hapo muulize, ...kama kweli yupo na wewe mia kwa mia, kama kweli, yupo na wewe au kama kweli yupo na mke wake aliyemuo kwa ajali ya kujinufaisha, aseme tusikie, uwanja ni wake, ...’akasema mwenyekiti.

Walipoona mume wa familia kakaa kimiya, shahidi aliyepita, akasema;

‘Ndugu mwenyekiti, mimi nafahamu ni kitu gani ninachokifanya, na sikufanya hayo kwa ajili yake tu, nilifanya hayo kwa vile nawajibika kufanya hivyo, kama yeye ataona kuwa mimi ni mjinga, sikuwa na maana njema kwake, hilo ni yeye na kichwa chake, na haliniumizi sana kichwa changu,ingeniumiza sana, kama ningelikaa kimiya baada ya kuona hayo yalitokea, yanapita bila kutafutiwa ufumbuzi, ndio maana nikaamua kuusema huo ukweli kwenu, kwani nafahamu nyie ndio waathirika wakubwa wa kadhia hii yote...’akasema huyo shahidi.

‘Sasa kama unakubali kusema ukweli na kufichua maovu kwanini usishirikiane na wale walipewa dhamana hiyo na serikali, ambao ni polisi, kwanini ufanye hayo kimiya kimiya, peke yako, huoni kuwa kwa kufanya hivyo ni makosa?’ akauliza mwenyekiti.

‘Muheshimiwa Mwenyekiti , nafahamu fika wewe unafahamu vyema hilo ninalolifanya, na sio geni kwako, kuwa kuna mambo mengine hutakiwi kukimbilia kuwaambia polisi, inabidi ujirizishe mwenyewe kwanza, kwani ukikimbilia huko, wao watakachokifanya ni kukushika, wakisema unakamatwa kwa ajili ya kuisaidia polisi, na hata kama hawatakukamata kwa bahati mbay, wao watakuzuia usifanye uchunguzi wako,...’akatulia kidogo, halafu akasema.

‘Ndio ni utaratibu wao, kwa nia njema wakakushika au kukuzuia, ila wao wafanye wajuavyo wao, kiutalaamu wako, huenda wakafanikiwa au wasifanikiwe kwa kile ulichokianza au kukigundua. Lakini kwa vile wao wanaona ni kazi yao, hata kama itwashinda hata kama watafanya yale unayoona wao, ni uzuia haki, au yale uliyoyaona kuwa yapo, na yalitakiwa kufuatiliwa kivingine, wao hawatakusikiliza watakuzuia, na watafuata wanavyotaka wao, na matokea yale yale uliyotegemea kuyapata usiyapate tena, na wao pia wasiyapate, na unafikiri kwako wewe uliyezuiliwa, itakuwaje, watakushika wee, huenda ukasota jela, mpaka ukaathirika kiafya.

‘Mimi kutokana na utendaji wangu wa hii kazi,nimejifunza mengi, kwahiyo sioni kama nafanya kosa, kutokuwaambia yale niliyoyaona, nafahamu wengi mtaona hivyo,...ila mimi nafahamu nafasi yangu kama raia mwema, ni wakati gani niwakilishe hayo niliyoyaona kwao, na muda huo ukifika, utaona matunda yake, sio mara ya kwanza kufanya kazi kama hiyo, mwenyewe utakuja kuoona, labda hawo wahusika waniwahi na kuniua...’akasema.

‘Na wakiniua ni ajali kazini, ni kama askari kufa vitani, sioni ajabu...’akasema  hivyo baada ya kutulia kidogo, na mwenyekiti akatabsamu na kusema;

‘Ndio hapo unapokosea,...maana wao ni kazi yao kulinda raia, na kuhakikisha haki inatendeka, na kwa jinsi unavyoongea ni kuwa una wasiwasi kuwa hao jamaa wanaweza kukudhuru, ni vyema ukajisalimisha kwa usalama, na wao watawajibika kwa hilo, kwani wao wana mamlaka na uwezo wa kukulinda...’akasema mwenyekiti.

‘Una uhakika na hilo ndugu mwenyekiti, kuwa wanaweza kunilinda, hahaha....wangapi wangapi waliambiwa hivyo, na sasa tumewasahau, kukulinda kwako ni kukuweka jela, wanasema kwa manufaa yako, au manufaa ya jamii, au sio..huko jela kweli ni kuzuri kukaa, ulishawahi kukaa jela ndugu mwenyekiti, hebu muulize binti yako, akuambia, jela sio mahali pema kuishi, kuna hatari zake hasa za kiafya, achilia mbali kuathirika kisaikolojia,....sawa ikibidi nitaenda huko, lakini kuna jambo bado nalifuatiliaa, nisingependa kuongea na  kwa hivi sasa, tafadhali mwenyekiti nakuomba unielewe hivyo...’akasema.

Mwenyekiti akamgeukia mume wa familia na kumwangalia, akageuka kuniangalia mimi, halafu akasema,;

‘Kama alivyosema shahidi, hayo ya nani muuaji wa Makabrasha ni mambo ya polisi, na hatutakiwi kuyaongea hapa, kilichotuweka hapa na mambo yetu ya kifamilia, tufanye yale yaliyopo kwenye mipaka yetu, tusipende kujifanya tunajua sana, na kuingilia kazi za watu, aheri mwenzetu anajua jua mambo hayo, sasa sisi tukiulizwa kwanini, tutasema nini....’akasema mwenyekiti na kuwaangalia mawakili.

‘Ninashukuru tuna watu wetu wa sheria, na wameona juhudi zetu katika kuliweka hilo sawa, kama tunakosea wao watatusahihisha, ila cha muhimu kutokana na ajenda yetu tumeshakipata, na kabla hatujaingia kwenye kipengele cha mwisho, ambacho ni makubalian au hukumu, ningelipenda tumpe nafasi mume wa familia aongee, ajitetee, kwa nafasi yake, na hili hatutaki wakili wake aliingilie kati, kwani kwa hivi sasa kila kitu kipo wazi, ...ukweli umedhihiri, na uwongo umejitenga...’akasema mwenyekiti, na kumwangalia mume wa familia.

Mume wa familia, akainua kichwa na kumwangalia mwenyekiti, akatikisa kichwa kama kukataa, haikueleweka, kwanini anatikisa kichwa vile,  akabakia kimiya hakuongea, baadaye akainmisha kichwa chake kama ilivyokuwa awali, akatulia kimiya.

‘Je mume wa familia hayo yaliyoongewa na mpenzi wako wa zamani ni kweli au na yeye kajitungia uzushi wake?’ akaulizwa mwenyekiti, na kumwangalia mume wa familia, ambaye alikuwa bado katulia kimiya, na mwenyekiti akaongeza kuongea kwa kusema;

‘Huyo ni mtu wako, yupo kwenye moyo wako, kipenzi chako cha asili, ...singeliweza kusema hayo aliyoyasema, kama anglijua kuwa anakuumiza, kajitosa kwa ajili yako, sasa je hayo aliyoyaongea yana ukweli, unayakubali, au ni kama yale yale ya rafiki wa mke wa familia, maana yanathibitisha yale aliyoongea huyo rafiki wa mke wa familia, na uliyapinga kwa nguvu zote, sasa je na haya unayapinga, ni uzushi, hayana ukweli, toa kauli yako kama mwanaume...’akasema mwenyekiti, na mume wa familia akaendelea kukaa kimiya.

‘Kukaa kwako kimiya inaonyesha nini, ama ni kutuzarau, au ama ni kiburi, au tusemeje?’ akauliza mwenyekiti, na mume wa familia akaendelea kukaa kimiya, na mimi nilipoona hivyo, nikaona niingilie kati, nikasema;

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tusipoteze muda, kuna mengi yamesemwa na yote ni ukweli mtupu, kwa mwenye hekima, ataelewa, na kukiri kosa, lakini kwa mtu mwenye tabia yake, ataona ni yale yale,tu,...lakini tuyaangalia hayo kwa mapana yake, ni nani hasa alilengwa, utaona ni mimi, utaona ni mali za familia ya mke, mali zilizotoka kwenu wazazi wangu,...ni kweli mimi, nilifanya juhudi tukafika hapo tulipofika, na nilijaibu kumshirikisha mwenzangu, ili ajifunze, na ilikuwa ni kazi kubwa, kumjenga mtu awa hulka yake...’nikasema.

‘Wakati mwingine, ilibid mimi nigeuka kuwa kama mume wa familia, kufoka, na hakupendeza, alkini nilifanya hivyo, kwa vile mimi nafahamu, kwa vile mimi nimekulia katika familia ya hali hiyo, kazi kwetu ni kipimo cha utu, kazi kwetu  ni jadi, hayo mnayoyaona, hizo mali, na utaji, na ukiangalia, mwenye I wetu, haukuja hivi hivi...nayasema haya ili watu waelewe....’nikamwangalia mume wa familia aliyekuwa bado kainama.

‘Naafhamu kabisa kusudio lao hawa wenzetu, ni kuwa kila tajiri, kila mwenye uwezo, kaupata kwa njia za kubumashi, kutepeli, kuiba,..sio kweli, ...wapo wengine, kama sisi, ..najivunia hilo, kwani mimi nimeishi na wazazi wangu, nimeona jinsi gani walivyokuwa wakijituma, wakajinyima, ...wakahangaia usiku na mchana, ..huku na kule, na matunda yake ndio hayo...sasa mlitaka mimi nilale, nibweteke, na kusema mali zipo, mali za baba na mama zipo, nitumie tu, hilo haliwezekani...’nikatulia kidogo.

‘Ndio maana ilifika mahali, nikasahau kila kitu, nikasema sasa ni kazi, starehe baadaye, huenda kwa kufanya hivyo, nilimkwaza mwenzangu, akaona nazarau majukumu muhimu ya ndoa,...lakini je huko mwanzo ilikuwa vipi, kama ningelifanya hivyo, hawo watoto wangelipatikana,...ilifika mahali nikaona kuna umuhimu wa kujitosa ili kukiokoa kile tulichokianza, hakuna kulala, hakuna staeeh kwanza, mpaka uone kuna faida..ndilo lilikuwa lengo langu, sikueleweka kivitendo, walitaka, au alitaka nitamke kwa ulimi.

‘Nimejifunza mengi kwa hili, na kwa akuli ya haraka haraka , ninaweza kusema, imekuwa kama mtoto akililia, wembe muache, ukimkata atajifunda, lakini pia imekuwa changamoto kwangu, kwani yote haya yaliyotokea muathirika mkubwa ni nani, ni mimi na watoto wangu..., ni kama vile wote walikuwa na lengo moja la kuniadhibu mimi , kwa kosa nisilo lijua, ...naona wengine wamefikia kusema ni kutokana na mimi kujisahau katika majukumu yangu ya ndoa, nk...

‘Lakini hebu angalia huo mlolongo mzima, kumbe haya yalikuwa yamepangwa kutoka huko kijijini hata kabla ya ndoa yangu, na ndoa yangu ikawa kama kisingizio, na udhaifu wangu wa kibinadamu ukatumiwa kama ngazi ya kutekeleza hayo yaliyokwisha pangwa, nashukuruni sana kwa hayo,nawashukuruni sana, wote, mliokuja kwangu na kuwapa kial kitu changu, ikiwemo nafsi yangu katika moyo, nikawaona kama ndugu, kama marafiki wema, kama mume mpenzi,...lakini hii ndio faida yake, mtoto akililia wembe muache, ukimkata atajifunza.

Kwa hivi sasa nina machungu moyoni, huenda nikitoa uamuzi wangu, naweza kuharibu, nahitajai muda wa kulitafakari hili kwa undani, ...yaliyotokea yamenifungua macho, masikio, nimejua ni nini nahitajika kukifanya, huenda kabla sijasema yale ya moyoni, ambayo nitakuja kuyasema kesho au siku itakayopangwa na mwenyekiti,  ningelipenda kumuuliza mume wa familia, maswali machache, mbele yenu, na nataka ayajibu mwenyewe kwa kinywa chake, ...bila kuficha..'nikasema na kumgeukia mume wa familia,

'Mimi ninayekuuliza haya ni mke wa familia nakuuliza wewe kama mume wa familia, nategemea wewe kama mume wa familia, utayajibu hayo bila kuniogopa, kama utaniogopa itakuwa ni ajabu, ...uume wako utatiliwa mashaka...’nikasema na watu wakacheka.

Na mume wangu akaniangalia kwa macho yaliyojaa hasira, ni mimi sikujali macho yake, nikasema;

‘Swali langu la kwanza, ni lile lile swali la mwenyekiti, ni swali la msingi na lenye hekima,  je hayo yaliyosemwa na wote hasa shahidi wa mwisho aliyekuja kuthibitisha, je hayo aliyoyathibitisha ni ya kweli au kajitungia mwenyewe...nataka unijibu hilo swali, kwani majibu yake, yataweza kunipa mimi mwanga,ili nisije nikahukumu kwa dhuluma, na sio mimi nitakayehukumu, muelewe hivyo, ni sote mimi na yeye, kwani tulipoandika huu mkataba, hatukusema mimi, tulisema sisi, yoyote atakyekiuka, atawajibika, sasa isiwe mkuki ni kwa nini....’nikamwangalia mume wa familia na yeye akaniangalia kwa macho yale yale yaliyojaa hasira, na akasema;

‘Nilijua kuwa itafika hapo, nilifahamu kuwa ni  mtego wa panya, sawa, nimekubali, na sina haja ya kung’ang’ania maliz zenu,...ninachoweza kusema kwa sasa na huenda ndiyo kauli wengi wanaisubiria, ni kuwa nisamehe mke wangu,.....japokuwa yana ukweli, ni kweli,....ila ukweli mwingine unafutika, chanzo , kwanini, hakitaanagliwa tena,..sijali, nakubali kushindwa, nimekiri nimekosa,...lakini mke wangu, katika maisha kuna kukosa, kuna kupanda an kushuka,..hayo ni majaiibu na kama binadamu unaweza kuyapitia, na mimi sio wa kwanza....’akasema na sasa akabadili uso wa hasira na kuwa uso wa huzuni.

‘Mke wangu, nakupenda sana...nilijitahidi kufanya hivyo, kukupenda, na kumbuka watoto wetu wapo wananihitajia mimi, baba yao, wanakuhitajia wewe mama yao, ndio maana nilifanya kila niliwezalo nionekane na mimi ni baba wa familia, niwe mkali, niwe na mamlaka, lakini ikaja kuvurugwa na watu wengine, ....sitaki kuwatupia wao lawama, nafahamu hakitaeleweka tena..hata hivyo kauli yangu ni kuwa, mimi ndiye baba wa familia, na hayo niliyoyafanya, nilitaka nieleweke hivyo, kama nimekosea nakubali na nakiri kosa...’akasema.

‘Hahaha hatimaye mume wa afmilia amekiri kosa, japokuwa kwa shingo upande, lakini sio kutoka moyoni, akisema anakubali kwa vile ametegwa kama panya, jamani, hebu angalieni huo mlolongo wote, kuna kutegwa hapa...au ni huo mfumo dume, mnaotaka kutuonyesha jamani...wewe uwe kama jogoo, leo huyu kesho yule..hivi kweli ni ubinadamu huo, ni utu huo...sikubali, na nilihitajia kauli iliyonyooka, na kauli thabiti, kuwa hayo yaliyosema ni kweli au ni uzushi..sijaiona hiyo kauli....’nikasema, na mwenyekiti aakingilia kati na kusema;

‘Kwahiyo kwake yeye hayo aliyoyaongea ni kukubali kuwa yote yaliyosemwa ni ya ukweli, ....labda tungelihitajia kauli ya kujiamini, ili tupate jibu la uhakika, unafahamu mimi ni mwanaume, na inaniuam sana nikisikia, hiyo kauli ya mfumo dume, kwanini mfumo dume, kwanini tusikubali ukweli, na kuwa wawazi, kama tumekosea basi tukubali, kama wanaume, sasa mume wa familia, tunataka jibu la kimwanaume kweli, usijifanye legelege, wewe ni mwanaume bwana...jitetee, tetea uume wako’akasema mwenyekiti.

‘Nimeshajibu mwenyekiti, naona kama mnanizalilisha sasa, hizo kauli zeni sizipendi, nafahamu kuwa nimekosea, na nimeshatoa kauli yangu, lakina hizo kauli zenu ni za kunifanya mimi mtoto , si chochote, nafikiri ni zarau, kutokana na asili yetu, kuwa labda sisi tumekulia, na kulelewa kitabia mbaya, hatupendi kazi, tuna tamaa,na kitu kama hicho, lakini mkumbuke yoyote anaweza kupitiwa, na shetani, akaghibilka na ni ibilisi, na .....ni nimeshawaambia kuwa sikuwa na nia mbaya, kwa hayo niliyoyatenda, na hamtaki kukubali ukweli kuwa  nilifanya hayo yoate kwa ajili ya kuilinda familia yangu, kwani kama nisingelifanya hivyo, hamjui ni kitu gani Makabrasha alinitishia nacho...’akasema

‘Tunataka tusikie hicho kitisho alichokutishia Makabrasha, maana kukutishia wewe ni kama alitishia familia yote hapa, je alikuambia nini, sisi tunavyojua ni kuwa Makabrasha alikutishia kuwa usipofanya anavyotaka yeye, atakuumbua kwa machafu yako uliyoyafanya, atakwenda kumwambia mke wako, na mkwe wako, au sio?’ akauliza mwenyekiti.

‘Pamoja na hayo, ...’akatulia na kutikisa kichwa kama kusikitika,

‘Hamkumjua Makabrasha nyie, hamkuwahi kuishi naye kwa karibu, yeye alisema, anaweza kuiumiza familia yangu, hasa watoto, atawateka nyara na kuwafanya wasionekane tena, ..hata wakionekana watakuwa mazezeta...hivi wewe kama mzazi ukisikia hivyo, utachukua hatua gani...’akasema

‘Hivi wewe kwa akili zako uliamini kuwa Makabrasha angeliweza kufanya hayo aliyokutishia, au alishakufahamu udhaifu wako kuwa wewe ni mwoga, ...au hebu tupe mifano hai, ambayo yeye aliwahi kuwafanyia watu wengine, ili tuamini kuwa vitisho vyake vilikuwa ni kweli...’akasema mwenyekiti.

‘Mimi nawapenda watoto wangu, iwe ni kweli au si kweli, iwe ni vitisho tu au ni kweli, mimi nilichotakiwa kufanya ni kile nilichoona ni sahihi, kwa ajili ya kuilinda familia yangu...’akasema

‘Ina maana hata kutembea na wake za watu, mfanyakazi wako wa ndani inatokana na vitisho vya Makabrasha?’ akaulizwa na hapo akakaa kimiya.

‘Au labda tukuulize hili swali huenda nalo linaweza kuwa ni sababu ya Makabrasha, je ni kitu gani kilichokufanya uwe mnzizi na kuisaiti ndoa yako?’ akaulizwa

‘Ni hali iliyokuwa imenizunguka, nilikuwa nimechanganyikiwa na mambo mengi yalikuwa yakiniandama, ikiwemo hilo la mipango aliyoibuni Makabrasha, na hata hivyo, mke wangu alikuwa na kazi nyingi sana, na yeye alitakiwa awe karibu na mimi ili niweze kuyasahau yote hayo, lakini hata nilipojaribu kumvuta ili aniliwaze, niliona kama yeye ananisukuma...’akajitetea.

Mimi nikamwangalia kwa hasira na kusema; ‘Huo ndio utetezi wako, kuwa mimi sikuwa karibu nawewe, je uliwahi kuniambia hilo, kwa kinywa chako nikakukatalia au kukusukuma, ...?’ nikamuuliza

‘Kwa vitendo visivyo dhahiri, unaweza ukamkatalia mtu, kwa vitendo visivyo vya moja kwa moja, na mimi 
kama mtu mzima nililiona hilo, kuwa hukuwa karibu na mimi na niliposema kusukuma sio kwa kusukuma kwa mikono, ni kwa vitendo, visivyo moja kwa moja...’akasema

‘Kwa matendo hayo ina maana nilionyesha hivyo kwa vile sikupendi,au ni kwa vile nilikuwa nawajibika kwa ajili ya kujiendeleza, kwa ajili ya maisha yetu ya baadaye na familia?’ nikamuuliza

‘Hapana sijasema hivyo, kuwa hunipendi, na hujawahi kunitamkia hivyo, kiukweli ulikuwa unanipenda na ulikuwa ukifanya hivyo kwa ajili ya kuinua kipato chetu zaidi na zaidi, lakini hukufanya yale yanayostahili kuonyesha upendo wa mke, ulijali sana kazi hata muda usio wake...’akasema.

‘Ina maana wakati mke wako anahangaika na kazi hadi kusahau majukumu yake ya ndoa wewe ulikuwa huna kazi , au sema ukweli huenda  mke wako hakuwa na kazi kweli, alikuwa akijifanya ana kazi kwa mbinu za kukwepa majukumu yake ya ndoa, sema ukweli, jitetee?’ akaulizwa.

‘Hayo yapo wazi, kazi ni kazi, na majukumu ya ndoa yapo pale pale...siwezi kusema alifanya hivyo kwa ajili ya kukwepa majukumu yake ya ndoa, hapana, ni kweli alikuwa akifanya kazi kiukweli, niliona kwa macho yangu, na siwezi kumlaumu sana kwa hilo..’akasema

‘Kama huwezi kumlaumu kwanini ukamsaliti, kwani  ukafikia hadi kutembea na mfanyakazi wako wa ndani, kwanini ukafikia hadi kutembea na mke wa mtu,...tunataka kujua ukweli, jitetee kwa hayo, huenda ulikuwa na sababu ya msingi, ambayo ukituambia tutakuelewa, ?’ akaulizwa tena na mwenyekiti.

‘Nimeshasema ni .....ni ibilisi tu, tamaa zilinizidi, nikashindwa kuvumilia, kama binadamu inaweza kufikia hatua hiyo,..., nilipitiwa,......’akainama chini.

Mimi nikamwangalia na nikasema ;’ ‘Mwenyekiti, mimi nimesharizika na jibu la swali hilo, ngoja nimuulize swali la pili...’nikasema na mwenyekiti akatabasamu na akamwangalia mume wa familia, halafu akasema;

‘Haya muulize maana ni mume wako unamfahamu sana kuliko sisi, ...’akasema mwenyekiti

Swali langu la pili, ni hili, ni muhimu sana , tena sana unijibu kutoka moyoni mwako, ...maana ukinidanganya tutajua,...ni kwa ajili yangu na wake wenzangu.’nikasema na kumwangalia na yeye akaniangalia kwa mashaka, akisubiri hilo swali.

‘Je unampenda mpenzi wako wa asili?’ nikamuuliza na yeye akawa kama anatabsamu, kama vile nimemzihaki, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo mpenzi wake wa asili na baadaye akamwangalia rafiki yake, yaani docta, halafu akasema;

‘Kwanini mnaniuliza swali kama hilo, ...sioni umuhimu wake kwa sasa, hapa naona mnaendelea kunitega tu, hilo swali leni lina ajenda ya siri, na mimi kama binadamu, siwezi kudanganyika, niliyoyafanya niliyafanya nikijua mimi ni mume wa familia, nilikuwa na mimi nawajibika, kwa manufaa ya familia yangu, mlitaka nikae tu,...’akawa katoa macho ya hasira akimwangalia mke wake.

‘Mzee, samahani sana baba yangu kama nitakosea, ni hivi kweli kuna mtu anaweza kuja pale kwako baba akakupangia jinsi gani ya kuishi,wewe umeshaoa , una mke wako,halafu watu wengine waje na sera zao...au ni kwa vile mimi...hebu nikuulize baba ulipomuoa mama, familia ya mama waliwahi kuja kwako na kuwapangia  jinsi gani bora ya kuishi na familia yako...mbona hayo hamyafikirii....’akasema huku akigeuka kumwangalia mama yangu.Na mama akawa anamwangalia tu.

‘Kiukweli sio swali la kuniuliza hapa mbele ya kadamnasi, ni kunizalilisha tu,ni kunitega tu ,sitaki maswali ya namna hiyo, nooh, now its too much...naona sasa mnataka kunakila puani, mumeshanizalilisha vya kutosha, sasa ansema basi, amueni mnalolitaka....’akasema kwa hasira huku akisimama na huku anamwangalia mwenyekiti akiwa ametoa macho.

‘Huna haja ya kukasirika hivyo, na hoja uliyotoa, au kama ni swali uliloniuliza, halina msingi, ni kuonyesha jinsi gani usivyokuwa makini na ndoa yako,...kwanini tumefikia hapa, ni kwasababu umekiuka sheria za ndoa...hatukuja kuingilia ndoa yako, tumekuja kusikiliza mashitaka ....usitake kuturudisha nyuma....'akasema mwenyekiti.

'Na hilo swali kauliza mke wako, anataka majibu, na ana maana yake kukuuliza hilo swali,kwa wenye hekima wanaelewa ni kwanini kakuuliza hivyo, hatumtetei, bali mimi kama mwenyekiti nimeona hekina ya hilo swali, kwahiyo, jibu swali baba, usikwepe mada kwa jaziba, jaziba hapa hazitakusaidia kitu,hilo swali  hata mimi naona lina umhimu wake, ili kubainisha ukweli wako ndani ya moyo wako....jibu kama ulivyoulizwa.’akasema mwenyekiti, na mume wa familia akainama kidogo, na watu walifikiria hatajibu, lakini baadaye akainu akichwa na kusema;

 ‘Kwa hali iliyofikia naona kama mnanilazimisha niseme hata yale yasiyostahili, sawa mimi nitasema ili muweze kufanya mnayotaka, sitajali tena..nitajibu  kama ifuatavyo...., hakuna asiye-elewa jibu la swali hilo, japokuwa nafsi itatamani kusema vinginevyo, nakubali nimeshakubali kosa, nakubali kuwa na sisi kutokana na umasikini wetu, tulikuwa katika harakati za kutafuta maisha bora, na njia tuliyoona ni sahihi ni hiyo, kwa vile tulikuwa na mwalimu wetu na yeye kwa kipindi hicho tulimuamini, ..hatukuwa na njia nyingine...’akageuka kumwangalia docta.

‘Docta ataweza kunisaidia hilo, kuwa moyo wa binadamu unakuwa na kitu kikishanasa kwenye moyo, inakuwa vigumu kukiondoa, kutegemeana na mazingira,...tunaweza kujidanganya, tunaweza kujitahidi, lakini kama kitu hicho kipo, kinaonekana kila siku, ..hutaweza kukisahau, huenda hilo ndilo kosa lililotokea,...kama mwenzangu angeliolewa mbali kabisa, tukawa hatuonani, huenda tungalisahauliana, lakini ukumbuke kuwa nyuma yetu alikuwepo Makabrasha, anataka tutimize ahadi zake, mitihani ikawa mingi,..shauku na kutamani kukanitawala....ni vitu ambavyo kama hujakutana navyo huwezi kuelewa...’akasema.

‘Swali bado lipo pale pale...hujalijibu kama linavyotakiwa kujibiwa, je unampenda mpenzi wako wa asili, au tuulize hivi bado unampenda mpenzi wako wa asili au ulikuwa ukimtumia tu, ili upate yale uliyokuwa ukiyataka,....?’ akaulizwa na mwenyekiti.

‘Umeshasema mpenzi  au penzi la asili,...hilo kwa wengi, wanaolifahamu halifutikia,kuna watu walikuwa na wapenzi wao wa asili, lakini hawakuoana, wakaenda kuoa wengine, lakini moyoni bado ule upendo upo, ...siwezi kudanganya, nampenda, ...na ilikuwa ni pendo la ujana, na la asili kama unavyosema, lakini sasa nimeoa, nina mke, kwahiyo nafasi ya upendo wake kama mpenzi wa asili inafichika, unabakia upendo kwa mume wangu..siwezi kusema haupo, upo,..na utaendelea kuwepo,kwa nafasi yake na nafsi kubwa ni kwa mke wangu, nampenda sana mke wangu ...ndio maana nikamuoa,...’akasema.

‘Hujaulizwa kuhusu mke wako, kuwa unampenda au la, vitendo vyako vimeshajielezea,swali uliloulizwa ambalo ni muhimu kwako kulijibu ni je bado unampenda mpenzi wako wa asili, ...au hayupo tena moyoni kwako, ikiwa na maana ulikuwa unamyumia tu kukamilisha mambo yako....?’ akaulizwa swali hilo tena.

‘Nampenda, sijasema kuwa simpendi, sio kweli kuwa nilikuwa namtumia tu,upendo wetu haujafutika, ila ni kwa upendo huo wa kiasili, kwa hivi sasa nina mke, kwahiyo mpenzi huyo wa zamani hana nafasi sawa kama ilivyokuwa ....ninaweza kusema hivyo, sina zaidi....’akasema na kuinama chini.

Mwenyekiti, mimi nimeshapata jibu la swali hilo, naomba nieleweka hivyo,...’nikamwambia mwenyekiti na kumgeukia mume wa familia, nikasema;

‘Nashukuru kwa jibu lako hilo, nimekuelewa, kama binadamu hayo yapo...siwezi kuyapinga, lakini mlolongo mzima unajieleza, dhamira yenu, ipo wazi, ....hayo maswali nimekuuliza kama nyongeza ili kusikia kauli yako kutoka kwenye kinywa chako mwenyewe, kwani wenzako walishatamka yao kutoka moyoni, wewe hukupenda kufanya hivyo kwa hiari yako mwenyewe, mpaka shinikizo la ushahidi, sawa, hiyo ndio hulka yako hatuwezi kuigeuza..., sio shida, nimeshakuelewa, ....’nikasema an kumgeukia mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tufunge kikao, ili kila mtu aweza kuyafikiria haya yote yaliyoongelewa hapa, na wanasheria, wayafanye kazi kisheria, tufanye la msingi na kwa hekima, ile tuweze kujenga jamii yenye kufuata haki na ukweli,...nafikiri tukiyafanya haya kwa familia moja moja, jamii itabadilika,...na samahani sana kuwasumbua wazee wetu, nafahamu mlihitajika kupumzika, lakini hili pia ni jukumu lenu, kama wazazi, naowaombeni tena mkae mtumie hekima zenu, ili muone tutalitatuaje hili tatizo,na kwa upande wangu na wa mwenzangu halikadhalika, tunahitajia muda wa kuliwazia hilo kwa mapana zaidi.

‘Ila kiukweli, mimi napenda kusimamia kwenye haki, na haki ya makubaliano ipo wazi,tulishakuabaliana na kurizia kuwa mkataba wetu uwe ndio dira ya maisha yetu ya ndoa, na tulikuwa tunakwenda vyema tu, sasa limetokea hili kubwa lao, kwanini tusahau yale tuliyokubaliana, kwa vile limemgusa mtungaji, hapana, ni lazima tufike mahali tuseme sheria ni msumeno...kwahiyo kitabu hiki,...mkataba huu, utasimamia kila kitu,...narudia tena, mkataba huu ndio utasimamia kila kitu tulichokubaliana....’nikageuka kumwangalia mume wangu, nilimuona akiniangalia kwa chuki, sikumjali tena.

Nikageuka kuwaangalia wanasheria wetu, huku nikiwa nimekiinua kile kitabu cha mkataba wetu juu, na wao wakawa wanatikisa kichwa kukubaliana name, halafu nikageuka kumwangalia mwenyekiti, na kuendelea kusema;

‘Lakini kwa sasa siwezi kusema zaidi naomba iwe hivyo kwa sasa, labda ndugu mwenyekiti, kwa rizaa yako unaonaje tukikiahirisha hiki kikao, akili yangu hapa haifanyi kazi tena,sijui tukuatane lini, kesho au kesho kutwa, tatizo ni kuwa kuna wale wa kusafiri,..na kama ulivyosema kuna watu wa usalama wapo nyuma yetu, sasa sijui.... tunaomba kama inawezekana wale wa safari waahirishe safari zao, ni muhimu sana wakasikia kauli yangu ya mwisho kuhusu jambo hili,na wakaona hukumu itakavyokuwa, kwani kila aliyeguswa na hili, atahitaji, haki yake, au kuwajibika...

‘Sawa mke wa familia, lakini nakuonya, usiniingilie uenyekiti wangu,...’akasema na kuangalia saa yake, halafu akageuka kuwangalia watu, akasema;

‘Ni kweli,  nikiaangalia saa muda umekwenda sana, na kuna watu wapo hapa, japokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine, lakini wanakazi zai, kuendelea kuwachosha hapa ni kuwatesa, yupo docta hapo, japokuwa kaniambia yupo mapumziko, lakini anahitajia kupumzika, wapo mawakili wetu, na kulikuwa na watu wa kusafiri kesho, tunaomba, ...kama ilivyoombwa, waahirishe safari zao...’akasema na kumwangalia mke wa docta, na mke wa docta akasema;

‘Kwangu haina shida, nitaangalia, na muelekeo ulivyo, kama nilivyokudokezea..’akasema na mwenyekiti 
akamwangalia kwa mashaka, halafu akageuka kuangalia wajumbe huku akisema;

‘Kwa upande wa binti yetu wa kufikia..oooh, hilo nitaongea na mwenzangu, tutangalia kama inawezekana kuahirisha hiyo safari yake, maana alishajiandaa kuondoka, hata hivyo kwa vile ni muhimu sana na inagusa hatima yake na mtoto wake, tutaliangalia hilo, na nitawajulisha kesho asubuhi na mapema kama kikao kipo au tupange siku nyingine

‘Hata hivyo wasi wasi wangu ni kwa watu wa usalama, nahitajia kupata kibali chao, hili tatizo sio la ndani ya familia tu, tatizo letu limegusa na maswala ya kijinai, ni muhimu sana mkalielewa hilo, kwahiyo kila tunalolifanya kama familia, tunahitajika kuwajulisha wenzetu wa usalama, ili tuweze kusaidiana nao, ndio jukumu letu kama raia wema,...

‘Kwa hivi sasa tunavyoongea hapa, wao , watu wa usalama wapo kazini, wanahangaika kumtafuta muuaji wa Makabrasha, msifikiri kifo chake kimefukiwa na mchanga, hapana, wanawajibika, usifikiri umesalamika kama unahusika, kifo cha mtu kinamuandama mtendaji hadi siku anaingia kaburini, ...na kwa taarifa tu, wapo katika kumnasa muuaji. Anaweza akawa miongoni mwetu, hatujui, kwani kafanya hilo tendo kwa ujanja wa hali ya juu....’akakatiza mazungumzo, kwani simu yake ilikuwa inalia, akaangalia mpigaji, akawaangalia wajumbe, halafu akasema;

‘Samahani subirini kidogo niongee na watu wa usalama, naona ndio hao wananipigia huenda kuna amri nyingine,...subirini kidogo msiondoke....’akasema  huku akipokea hiyo simu...

NB: Haya tunasubiri hukumu..


WAZO LE LEO:Jehivi kweli kuna kisingizio cha kuisaliti ndoa yako? Je unaposalitiwa au kusaliti ndoa yako kama mwanandoa unahitajika kufanya nini?. Ni maswali madogo lakini yenye mambo makubwa, wewe kama mwanandoa kabla hujafanya kosa la kukiuka sheria za ndoa,fikiria mara mbili, ni athari gani zitakazotokea baada ya tendo hilo,kwani matokea ya dhambi hiyo ni kubwa sana, kitendo cha muda mfupi, lakini mazara yake yanaweza kugharim maisha yako na athari kwenya familia yako. Tuweni makini.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Pam said...

habari M3, plz post sehemu zinazoendelea hata weekend and public holidays niliomba wakati fulani ukaweka kama weekend moja halafu baaasi..