Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, January 8, 2014

Mkuki ni kwa Nguruwe-60



Binadamu tulivyo, hata ujitahidi vipi, hata uwe mjanja wa kuvumilia usingizi, kuna muda kwenye usiku, inafika unashindwa kuvumilia na ni lazima utapitiwa na usingizi tu, na ndivyo ilivyotokea kwangu, ...’ Shahidi akaendelea kuongea.

‘Japokuwa nilitaka usiku huo nikeshe, ili kuhakikisha mambo yangu yanakwenda kama nilivyopanga. Lakini usingizi ukanipitia, kwani baada ya shughuli za usafi, kupanga mambo aliyokuwa akihitajia Makabrasha, kuweka taratibu za vikao vyake vya kesho, nikajikuta nimechoka sana.

Niliongea kidogo na Makabrasha kuhakikisha kuwa kila kitu chake kipo sawa, na akaniambia hatanihitajia tena kwa usiku huo, na  yeye akatoka kwenda chini kwenye sehemu ya hoteli kujiburudisha na watu wake, mimi nikaingia chumbani kwangu kubadili nguo, kabla ya kufanya hivyo, nikajilaza kidogo kitandani, nikiwa na mawazo yangu, nilijiegemeza kidogo kwenye mto, nikiwa nimeweka mikono nyumba na kichwa changu kulalia viganja vya mikono, hapo hapo usingizi ukanipitia.

Nilishituka ni asubuhi, na kilichoniamusha ni simu yangu , iliyokuwa ikilia, nilikuwa nimeweka mlio wa kutikisika tu, ...bila kuangalia mpigaji , nikaipokea hiyo simu kwa haraka, ilikuwa ni sauti ya mdogo wa mume wa familia, nikamuuliza kuna nini asubuhi hiyo, akaniambia yupo karibu na eneo la hilo jengo alimleta kaka yake.

‘Oh, kumbe kumekucha...kwahiyo, mpo na kaka yako? ’nikamuuliza nikipiga miayo, nikainuka pale nilipokuwa nimejiegemeza, na mdogo wa mume wa familia, akasema wapo naye, na yeye ataondoka, na kurudi baadaye kumchukua, kwani sio vyema kwa yeye kuonekana hapo nje. Nikamwambia sawa, hakuna shida.

Kwa haraka nikainua godoro, pale nilipoficha silaha yangu, nikaiona ipo, nikarudishia godoro kwa haraka, kwani nilihisi kuna mtu anakuja kwa nje, nilisikia mlio wa yayo za mtu, nikajiweka sawa, nilijua nitakuwa nahitajika kuweka mambo sawa, kwa ajili ya wageni, ...hakuna mtu aliyeingia, nikafungua mlango kuchungulia kwenye korido, sikumuona mtu, lakini nina uhakika kulikuwa na mtu anakuja muelekeo wa chumba changu.

Nikarudishia mlango na kutulia kidogo, nikamigia mdowa wa mume wa familia, nikamuuliza kama kaka yake ameshaingia ndani, na kama anahitaji nimpe ile silaha, na yeye akasema;

‘Kwa hali ilivyo hapa nje, huwezi kunipa hiyo silaha, ..lakini ulisema utaihitajia hiyo silaha leo kama kaka akifika, kwanini unataka kuirudisha tena?’ akaniuliza.

‘Kazi muhimu nimeshaimaliza, ila kuna kitu nataka kukufanya, kama itawezekana, lakini sio muhimu kwa sasa nilishaongea na kaka yako, kama akiwa mjinga na kusaini huo mkataba atakuwa kaharibu kila kitu, yote inategemea yeye, vinginevyo, kwa vile ni mchana siweze kufanya lolote na hiyo silaha, kwahiyo sio muhimu kwa mchana wa leo, lakini kama unaona hakuna usalama huko nje, basi ngoja ikae kae huku, huenda nikaihitajia...’nikamwambia.

‘Sawa hamna shida, kama alisema atafanya kama mlivyokubaliana, sijui mume kubaliana ninini,...’akasema na mimi nikamwambia.

‘Tutaongea baadaye, je unavyoona kwa kaka yako,yupo safi, anaweza kufanya niliyomuagiza ayafanye...?’ nikamuuliza, akasema;

‘Yupo safi, skuona tatizo lolote kwake...’akasema na mimi nikakata simu,i nikainuka kitandani na kwenda kuoga na kujiweka sawa, kiofisi zaidi, nilimpigia simu mume wangu, kumtakia hali;

‘Mume wangu haujambo, samahani sikuweza kukupigia simu usiku nilibanwa sana na kazi...’nikamwambia.

‘Hamna shida hata mimi nilikesha hospitalini, kulikuwa na wagonjwa wa dharura, ndio nimefika nyumbani mara moja, kuangalia usalama,na sasa hivi naondoka, huenda nisirudi mpaka jioni au usiku....’akasema.

‘Sawa ukiwa na nafasi, tutaonana,jioni au  ...’nikamwambia.

‘Tutawasiliana kama nitakuwa na nafasi, vinginevyo, nakutakia kazi njema,...’akaniambia na mimi moyoni nikawa naumia sana, niliumia kwa hayo ninayoyatenda, kwa mume mwema kama huyo. Kiukweli, sijawahi kuishi na mtu ambaye anakujali, na kukuonyeshea mapenzi ya dhati kama mume wangu, lakini maumbile yalivyo, hisia na ...sijui niseme vipi, hakuna angaliweza kushika nafasi ya mpenzi wangu wa asili...’akasema na kumwangalia mume wa familia ambaye alikuwa kainamisha kichwa chini.

‘Hata hivyo, kama isingelikuwa Makabrasha, na huyo mpenzi wangu wa asili kuja kuniharibia mipango yangu, mimi ilishafikia hatua, nikaamua kuwa huyu ndiye mume wangu nitajitahidi kumpenda hasi mwisho, lakini ghafla ndio akaja mume wa familia na matatizo yake, ikabidi niwe mtu wa kumliwaza, na unafahamu damu zetu zinaendana, kuliwazana, kunaturudisha nyuma, na mnajikuta mumevunja ahadi za ndoa.

Ilianza kama mchezo, ikawa sasa ni kawaida, akija amelewa, au kuchanganyikiwa mimi namfarisi na akinihadithia mambo yake na mke wake, namuonea huruma sana, nahisi kipindi hicho ndicho Makabrasha aipata mwanya wa kuchukua picha ambazo ni moja ya kumbukumbu za picha za video alizokuwa kazihifadhi, sikuweza kupata muda wa kuziangalia, niliziharibu bila ya kuzianalai vyema.

Na alipokuja mume wa familia na kashifa aliyoitengeneza Makabrsaha kuwa ataitumia kuharibu ndoa zetu, kama hatutakubali matakwa yake, ndio ikaharibu kila kitu, hata yale mawazo yangu ya kuendelea na ndoa yangu hiyo ikaanza kuingiwa na doa,

Kuna kipindi mume wangu alishuku, mabadiliko niliyokuwa nayo, lakini nilimficha kabisa, japokuwa moyoni nilikuwa naumia sana, na sikuweza kumwambia mume wa familia kuwa mimi naumia sana kuendelea kumdanganay mume wangu...

Wakati nawaza hayo, nikasikia tena mtu akitembea kwenye korido, na mimi nikafungua chumba haraka na kutizama nje, nikaona mtu akiongia kwenye moja ya chumba kilichokuwepo mbele, sikuweza kumuona vyema, alikuwa ni mwanaume,ilikuwa ni kitendo cha haraka,....aliingia kwenye chumba kilichokuwa bado kwenye matengenezo, kilikuwa hakijamalizwa, nikahisi huenda ni mmoja wa mafundi, kaamua kuwahi, lakini kwa uhakika, nikaona niende niangalie.

Nikarudi ndani kidogo na kuvaa nguo za kikazo, nilifanya haraka haraka, nikatoka na kwenda hadi kwenye kile chumba, sikuona mtu, nahisi huyo mtu alishatoka, lakini atakuwa kafanya haraka sana, na atakuwa ni mwepesi sana, ila kulikuwa na dalili zote kuwa huyo mtu aliingia hapo, na kutoka. Nikatoka kwenye kile chumba na kuangalia sehemu zote hakukuwa na mtu maeneo ya karibu, nikajaribu kuangalia kila pande, lakini sikumuona huyo mtu.

Ili kuwa na uhakika zaidi nikawapigia walinzi kuwauliza kama kuna wafanyakazi wa ujenzi wameshawahi asubuhi, wakasema hawajafika. Hapo nikaingiwa na wasiwasi, na afadhali kama mitambo ingelikuwa ON, ningeliweza kujua ni nani, kwa kwenda kuangalia huko.

Mimi nikaondoa wasiwasi, nikajiandaa na kuelekea ofisini kwangu. Kabla sijafika huko, nikapitia chumba cha mitambo ya usalama, nikaingia na kuweka ile mitambo ON, halafu kwa haraka nikarudi ofisini kwangu....
Nilikuwa na ofisi yangu na humo nilikuwa kama mhasibu, mtunza masijala, na pia ni katibu muhutasi wa Makabrasha, kwahiyo utaona jinsi nilivyokuwa na kazi nyingi. Na hapo ndipo mara nyingi nakaa kama hakuna kazi nyingine. ni ofisi iliyokamilika kila kitu, komputa simu, mafile..nk.

Ofisi yangu hiyo ipo mbali kidogo na ofisi ya Makabrasha, ile ni kwenye korido moja. hiyo ni ofisi wakati nafanya kazi za kuweka kumbukumbu, ila nikiwa nafanya kazi za ukatibu muhutasi, huwa ninakuwa kwenye ofisi kubwa karibu na Makabrasha. Katika maswala ya usafi yupo mtu anafika kufanya hiyo kazi lakini kipindi hicho alikuwa likizo, kwahiyo nilikuwa na kazi kubwa ya usafi,na kazi nyingine....

 Hata hivyo kazi kubwa nilishaifaya usiku, nikapitia pitia sehemu muhimu na kuhakikisha kuwa zipo safi, baadaye nikataka kwenda  chumba cha Makabrasha, nilifahamu wakati kama huo yeye na rafiki yake yaani mume wa familia watakuwepo kwenye chumba cha maongezi, wakipata vinywaji, kabla hawajaingia ofisini kuzungumza mambo yao ya mikataba, nawafahamu sana taratibu zao kila wanapokuja kuonana, na ndipo nafasi ya mume wa familia ya kupata kinywaji, kwani akitoka hapo anatakiwa kuigiza kuumwa...

Nilifika ofisi ya Makabrasha nikaona kafunga na ufunguo, kama nilivyotarajia,...huwa hataki kufanya makosa, chumba chake kama hayupo huwa kimefungwa, na hakuna mtu anaruhisiwi kuingia kama mwenye hayupo, hamuamini mtu, hata mtoto wake mwenyewe haruhusiwi kuingia hapo kwenye ofisi yake kama hayupo, hata mimi sina ufungua wa chumba hicho wa akiba. Sikuwa na kazi kubwa kwenye chumba hicho, kwani usiku nilishakifanyia usafi, haikuwa na haja ya mimi kufanya usafi mwingine. Na hata yeye alishaniambia hanihitajii ofisini kwake mpaka aniite,kwahiyo haikuwa na haja ya kuingia tena humo, nikarudi ofisini kwangu

Nikiwa pale, nikapigiwa simu, na mtu ambaye hakujitaja jina, akaniambia;

‘Acha hayo unayokusudia kuyafanya, kwani tumeshakujua njama zako, kama utaendelea na mambo yako,utakuja kujuta, ...’halafu akakata simu, sikumuelewa ni nani, ni sauti ngeni kabisa, na ilikuwa ya kukwaruza kwaruza, nahisi aliweka kitambaa mdomoni, ...sikusema neno, maana mimi kutokana na akzi yangu vitisho kama hivyo nimeshavipata sana, na mara nyingi nina hulka yangu kuwa mtu mwoga hutanguliza vitisho, na mtu kama huyo hana lolote, mtu jasiri ni yule, anayetanguliza vitendo.

Na wakati nimetulia nikiwaza cha kufanya, mara simu nyingine ikalia, hii ilikuwa ya aliyekuwa bosi wangu, akaniambia yeye anaondoka,..

‘Sawa. Samahani nimeshindwa kuonana na wewe, lakini natumai mambo yanakwenda vyema, na mtoto wako umeshampata...’nikasema.

‘Mtoto sijampata, licha ya kuwa nimewatimizia mambo yao yote, wameniambia nitakutana naye uwanja wa ndege, kwahiyo hapa nilipo sina amani kabisa...’akasema.

‘Mimi nina uhakika mtoto utampata na yupo salama, huyo anayekaa naye, ni dada mwema sana anafahamu jinsi ya kulea watoto, nilimtafuta mwenyewe, niliambiwa nimtafute...’nikasema.

‘Kwahiyo wewe upo wapi?’ akaniuliza.

‘Usijali, nakutakia safari njema, ukirudi natumai mambo yatakuwa yamebadilika,...’nikasema na kukata simu.
Baadaye nilitwa na Makabrasha, nikaenda ofisini kwake, alikuwa peke yake, sikumuona huyo mgeni mwingine, ...sikuuliza, yeye akasema;

‘Jamaa yako ameshafika, yupo wash-room, nimekuita mara moja, kuna kumbukumbu zangu sizioni kwenye mtandao wetu, nimeongea na mtoto wangu anasema anakushuku huenda ni wewe umeweza kuingia kwenye komputa ya kuhifadhi kumbukumbu na kuziharibu, hebu niambie ukweli,mimi ninakuamini sana ...’akasema na mara simu yake ikalia, akaniangalia na kusema;

‘Ondoka tutakuja kuongea badaye, na kama ni wewe unahuska na hayo, kama anavyodai mtoto wangu, tutakosana, na nitakufanyia jambo ambalo hutaweza kulisahau, nitasahau urafiki wetu wote, na kukuharibia maisha yako,...uombe mungu kumbukumbu hizo zipatikane, la sivyo na wewe utapotea kama hizo kumbukumbu...’akasema akiniangalia kwa hasira.

‘Mimi sijui unachokiongea, nitawezaje kuingia kwenye komputa na kuharibu hizo kumbukumbu, mimi sina ujuzi huo, na hapo huoni ...anayeweza kufanya hivyo, ni mtoto wako, kwanini umuamini  mtoto wako, huoni ni unjana wake, kaamua kukugeuka,baada ya nyie kukorofishana jana...’nikamweleza nay eye akiwa na wasiwasi, kwani inaonekana hakutaka huyo mgeni wake anione hapo, akawa ananisahiria nitoke na mimi nikasema huku natembea kuelekea mlangoni;

‘Mimi nahisi aliyefanya hivyo ni mtoto wako huenda kazificha hizo kumbukumbu kukukomoa, kwa vile hutaki kukubaliana naye, sasa ananitupia mimi lawama, ili kutukosanishe, hebu fikiria hilo kwa makini...’nikasema na yeye akakunja uso kama anawaza, na kuniashiria nitoke humo ndani haraka.

Mimi nikatoka, na wakati natoka, hadi sehemu ya mapokezi ya ofisi hiyo, huwa mimi nakaa hapo kama kuna wateja maalumu, ila kwa leo sikutakiwa kukaa hapo, na mara mlango wa chooni ukafunguliwa akatokaa mume wa familia, hakuniona, kwani alitoka kwa haraka na kuelekea kwenye mlango wa ofisi ya Makabrasha na kuingia huko. 

Mimi nikatoka humo haraka, na kuelekea ofisini kwangu, ...sikuhitaji silaha kipindi kama hicho, ingenisaidia kama mume wa familia angesema hataweza kuifanya kazi niliyomuagiza, nilitaka akatae na kucheleweza kuweka saini kwenye hiyo mikataba, ili niweze kusafisha kila kitu kwenye kumbukumbu zao, nikawa nimepumzika nikifanya kazi zangu zingine.

Sikuonana na hawo watu, nikawa na kazi zangu zingine za kiofisi hadi mchana, na muda ukafika wa mimi kuondoka kurudi nyumbani hadi jioni, nikawasiliana na Makabrasha kwenye simu kuwa mimi natoka, na yeye akajibu kwa mkatao kwa kusema;

‘Sawa...’ na kabla hajakata simu akasema;

‘Nakuhitajia uwahi hapa jioni, nina mazungumzo na wewe...’akasema kwa sauti iliyonitia wasiwasi, nikafahamu labda ni kwa vile kakataliwa na mume wa familia kutii matakwa yake.

Nikaelekea chumbani kwangu ninachojipumzisha, ni chumba kabisa cha kulala, na kuhakikisha funguo ninazo, nikarudi kidogo nyumbani kwangu, sikuonana na mume wangu siku hiyo, kama alivyosema ana kazi zake, nilipumzika nyumbani hadi  jioni, na baadaye nikarudi ofisini kwangu, baada ya kumpigia simu mume wa familia akaniambia kuwa hawakuafikiana na Makabrasha,kumbe aliweza kufanya kama nilivyomwambia  hawakuelewana kabisa, kwani Makabrasha alitaka hilo zoezi liishe leo hii, wakapanga waje kukutana tena jioni, au usiku wa leo, nikaona tena mambo yapo pale pale, nikashukuru kuwa silaha bado ninayo.

Niliporudi kwenye hilo jengo, nilihisi mwili ukinisisimuka, sikuelewa ni kwanini, nikawauliza walinzi kama mtoto wa Makabrasha alifika, wakasema hajafika siku nzima ya leo, nikashukuru mungu, na nilipofika kwa Makabrasha akawa hayupo sawa, nahisi ni kwa vile mume wa familia alimkatalia kusaini huo mkataba, na hakutaka kuongea na mimi kama alivyotaka asubuhi. Mimi sikujali, nikaingia kwenye chumba changu, nikahakikisha ile silaha ipo.

Silaha ilikuwepo pale pale, sikuigusa, maana nilikuwa mikono mitupu, nilikuwa mwangalifu sana kuigusa ile silaha, nilihakikisha kuwa siigusi mpaka niwe nimevaa kinga kwenye mikono yangu. Nahisi hapo ndipo nilipofanya makosa, kwani ukumbuke, kuwa nilishaweka ile mitambo ya kuangalia matukio ya humo ndani, ON, kuruhusu kuonekana kwa matukio yote kwenye hilo jengo, na wakati naangalia hiyo silaha, sikujali kujificha, kama nilivyofanya jana.

Ilipofika jioni mambo yakaanza, nikawa napilika pilika za hapa na pale, na nilitaka nihakikishe kuwa mkataba huo hausainiwi, ...ndilo lengo langu kubwa kwani yale yaliyokuwa yakitushinikiza nilishayaharibu, labda wawe na kumbukumbu sehemu nyingine. Nilichokuwa naombea ni kuwa huyo mtoto wa Makabrasha asionekane leo kabisa, ili niweze kulizuia hilo tendo la kusaini huo mkataba kabisa. Nikajaribu kumpigia mtoto wa Makabrasha ili kuhakikisha kama kweli hatakuja, na simu yake ikawa haipatikani,...

Nilipata taarifa kuwa mume wa familia keshafika,ilikuwa jioni ya kuingia usiku, na nilijua kuwa wapo kwenye maongezi yao na Makabrasha, na hapo nikataka kuchukua silaha, nitoke nayo, lakini isingeliwezekana kwa vile mitambo ya kuonyesha matukio ipo ON,...ukitoka nayo tu, ving’ora vya hatari vitaanza kupiga ukelele,  kwahiyo nilichofanya ni kutoka pale na kwenda kuchukua ufungua za kile chumba cha mitambo hiyo. 

Nilikuwa na ufunguo wa kile chumba, sikuurudisha ofisini kwa Makabrasha, huo ufungu huo unakaa kwa Makabrasha, lakini niliuchukua siku kadhaa, nilipomweleza kuwa nataka kufanya usafi , na yeye hakuwa na wasiwasi na mimi, akanikabidhi.

Nilipofika kwenye hicho chumba, nikaingia na kuweka OFF kuzuia mitambo isione matukio, nikaingia kwenye komputa na kufuta matukio ya nyuma tangu pale nilipoweka ON, ,..

Halafu nikarudi ofisini kwangu ili niweke mambo safi kabla sijawaingilia Makabrasha na mume wa familia, ...hapo nilipanga kutumia nguvu, kuhakikisha kuwa mkataba huo hausainiwi, na kumlazimisha Makabrasha atoe mikataba yote aliyokuwa nayo, ...Nilishamwambia mume wa familia akiwa anaongea na Makabrasha ahakikishe simu yake inachukua maelezo yote, na nilitaka wakati nawavamia niwahi kuchukua ile simu ya Makabrasha anayohifadhi maongezi yake na watu, ili iwe ni ushahidi.

Yote hayo yataweza kufanyika kiurahisi kama mtoto wa Makabrasha hatakuja, lakini akifika, itakuwa kazi nzito kidogo, hata hivyo, nilishapanga nipambane nao, kwani nimeshafanya mengi ambayo yatanifanya mimi na Makabrasha tusielewane tena, hasa akija mtoto wake, na kumuonyesha kuwa ni mimi ndiye niliyefuta mambo yake kwenye kumputa ya kuhifadhi uchafu wake, kama atakuwa na ushahidi wa kufanya hivyo, sikuwa najali tena....

Nikiwa nimetulia ofisini kwangu nikimalizia kazi mbali mbali, na mara nyingi unapoanza kazi za mahesabu,kuweka kumbukumbu za mahesabu kwenye komputa, na kutayarisha  taarifa mbali mbali, masaa yanakwenda haraka bila kujua, nikawa nimesahau kabisa wajibu wangu mwingine. Nikaangalia saa, na kuona nimetumia saa moja na nusu,...nikaacha kila kitu, na kujiandaa kutoka mle ndani, niende chumbani kwangu ikibidi nikachukue silaha, ili nikaweza kuwavamia Makabrasha na mume wa familia.

Kwanza nilitaka kuhakikisha kuwa hawo jamaa bado wanaongea, au ameshaondoka, na kabla sijafanya hivyo kukasikika king’ora cha polisi kwa mbali, mwanzoni nilijua ni polisi wanapita, lakini kilipofika maeneo ya kwenye jengo kikasimama hapo, na  mimi nikashituka, kuna nini tena ...

Nilichofanya kwa haraka nikumpigia simu mlinzi kumuuliza kuna nini, na mlinzi akasema hana uhakika, askari wenzake ndio wamelekea huko juu. Mimi nikainua simu na kumpigia bosi , yaani Makabrsha, ikawa inalia bika kupokelewa, nikahisi kuna tatizo. Sikutaka kutoka humo kwa haraka, nikapiga simu kwa walinzi kama mtoto wa Makabrasha keshafika, huyo mlinzi akasema hana uhakika, kwani yeye alitoka, na kumuachia mwenzake ulinzi, na huyo mwenzake  ameshaondoka.

Baada ya dakika chache, nikapiga simu tena  kwa walinzi kuulizia kuna nini, wakaniambia kuna tatizo kubwa limetokea nani ya ofisi ya Makabrasha, na polisi wameshafika,..

‘Polisi!, tatizo gani la kuwahusisha polisi?, wamekuja kufanya nini?’ nikauliza maswali mengi kwa haraka bila kujua nauliza nini.

‘Makabrasha kapigwa risasi na hali yake ni mbaya sana, sijui kama atapona...’akasema huyo mlinzi na aliposema hivyo, kwa haraka nikajua ni mume wa familia kafanya hivyo, lakini kwa silaha gani, kwani sizani kama angeliweza kuingia na silaha pale mlangoni, japokuwa nilikuwa nimezima kiwambo cha kuhisi hatari.

‘Na nani, mbona muda mfupi uliopita nilikuwa nikiongea naye, haiwezekani..ngoja nikahakikishe....’nikasema na kutoka kwenye ofisi yangu, ili kama mume wa familia yupo hapo niweza kutoa msaada,lakini nilikuwa nimechelewa, kwani nilipotoa kichwa kuangalia kwenye korido, nikawaona maaskari.

Kumbe maaskari walishafika, nikarudi ofisini kwangu kwa haraka kabla hawajaniona,na kujifungia, sikutoka kabisa, na sikutaka kufanya lolote maana sikujua nikikutana na hao polisi nitasema nini, na cha ajabu, siku hiyo hakuna polisi aliyekuja kunihoji. Nilisikia wakisema wameshamshika muaaji,...yaani mke wa familia.

‘Mke wa familia, alikuja muda gani?’ nikauliza, na walinzi wakasema alifika hapo akitaka kuonana na Makabrasha, na polisi wameshamshika, yupo chini ya ulinzi.

‘Je yule mgeni wa Makabrasha wa mwanzo aliondoka muda gani?’ nikauliza.

‘Aliondoka, muda na baadaye ikagundulikana kuwa Makabrasha amepigwa risasi...’akasema.

‘Ni nani aligundua hilo?’ nikauliza.

‘Hatujui, hata sisi tuliona ajabu, maana hakuna mlio wowote wa hatari uliosikika, ina maana mitambo huko juu haifanyi kazi?’ akawa kama ananiuliza na mimi hapo nikaanza kuingiwa na wasiwasi, maana ni mimi niliyezima hiyo mitambo, ina maana moja kwa moja nitashikwa kwa kuhusika na mauaji hayo, hapo nikawa na wakati mgumu. 

Nikatafuta upenyo, hadi nikaupata nikatoka pale haraka na kwenda chumba cha mitambo kwa haraka nikaweka ON, japokuwa nilijua kuwa nimeshachelewa, na kwa haraka nikarudi ofisini kwangu, na kutulia kuwasubiri polisi wakija kunihoji, lakini hilo halikutokea kabisa siku hiyo.

Siku hiyo nikiwa nimejifungia humo ndani nilikuwa nikimuwazia Makabrasha, sikuamini kuwa atakufa, kwa jinsi nilivyomfahamu na tambo zake, hata hivyo, kuna muda nilijikuta nikimuwazia kuwa huenda atakuwa ameshakufa kama alipigwa risasi, na sijui ni sehemu gani....

Unafahamu mtu hata awe mbaya vipi, linapomfika jambo kama hilo, la ugonjwa au umauti, hata kama ni ugonjwa tu, ila unahisi hataweza kupona, unaingiwa na moyo wa huruma, ukizingatia kuwa mimi nilikuwa mtu wake wa karibu, japo sikupenda iwe hivyo, japokuwa nilikuwa na kisasi naye, na chuki iliyopitiliza kwa hayo aliyonifanyia, lakini sikuwa na dhamira ya kumuua.

Nilishangaa, kwani mambo yalikwenda harakaharaka, na Makabrasha akakimbizwa hospitalini, na baadaye tukapata taarifa kuwa Makabrasha hatunaye duniani. Kafariki kwa risasi, na ilikuja kugundulikana kuwa risasi na bunduki, bastola iliyotumika kumuua Makabrasha ni ile niliyoletewa, sikujua ni nani aliyeweza kuingia chumbani kwangu na kuiiba, na alijuaje kuwa nina bastola!

Hapo shahidi akatulia kidogo, na mwenyekiti akamwangalia shahidi kwa mashaka, na kumuuliza;

‘Hapo kwakweli sisi hatukuelewi, Ina maana unataka kutuambia kuwa  sio wewe uliyemuua Makabrasha, ukishirikiana na mpenzi wako wa zamani kutokana na maelezo yako uliyoyuambia?’ akaulizwa

‘Nakumbuka, tangu mwanzo, kabla sijaongea mimi, wewe ulikuwa ukiamini kuwa aliyefanya hivyo ni mume wa familia na mdogo wake, au sio , sasa iweje unishuku mimi, kwa vile nimeelezea huo ukweli, ndio maana nilikuwa nasita kusema huo kweli jinsi ilivyokuwa, ina maana kufanya hivyo nimefanya makosa?’ akauliza

‘Kutokana na maelezo yako toka mwanzo, inaonyesha ni wewe, kwasababu silaha iliyotumika kumuua Makabrasha ulikuwa nayo wewe hadi hatua ya mwisho, na wewe ndiye uliyafahamu wapi silaha hiyo ipo, sasa unaposema wewe haukuwepo kipindi Makabrasha anauwawa, tunaona kama unaficha ukweli...’akasema mwenyekiti.

‘Hivyo ndivyo ilivyokuwa, huo ndio ukweli, wa siku hiyo,...kama mliambiwa vinginevyo ni uwongo, maana mimi nilikuwepo humo ndani, tatizo, ni kuwa, kile kifaa cha kuchukulia kumbukumbu za matukio kilichokuwepo, nilikuwa nimekiweka  OFF, ni kweli ni mimi ndiye niliyekiweka hivyo, kwahiyo tukio zima, halikuonekana...’akasema.

‘Huoni kuwa polisi watajua kuwa wewe ulifanya hivyo makusudi ili ufanye mauaji na kusiwe an ushahidi au sio?’ akauliza mwenyekiti.

‘Baada ya kufikiri sana na kupata taabu ya kuwazia hilo tukio lilivyokuwa, nikaona ni bora niseme huo ukweli ulivyokuwa, lakini nikijua kabisa, nikielezea huo ukweli kwa yoyote vile , achilia mbali polisi,yoyote nitakayemuelezea jinsi ilivyokuwa hataamini kuwa sio mimi niliyemuua Makabrasha, ....lakini huo ndio ukweli, hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwa utata huo nikaamua kukaa kimiya na nilichofanya nikwenda kukaa huko kijijini.

‘Mhh, mimi sijui, lakini nionavyo mimi polisi wakisikia hayo maelezo yako , moja kwa moja wewe utakuwa mshukiwa namba moja, na sijui kwanini mpaka leo hawajakukamata, ina maana hukuwahi kuongea nao?’ akaniuliza.

‘Nimeshaongea nao, lakini nilijua jinsi gani ya kuwaambia, na hawakuwa na ujanja wa kunikamata, ila kiuhakika, itafika siku watanikamata , kama sio leo, ...siku yoyote watanikamata, lakini kwanini niendelee kujificha, ukweli ndio huo...’akasema.

Mwenyekiti akaangalia saa yake, na alionekana na maswali mengi ya kumuuliza huyo shahidi, lakini kabla hajamuuliza huyo shahidi, huyo shahidi akasema;

‘Mimi imenichukua muda  kuliwaza hilo, lakini moyo unanisuta, na kila nikiwaza sana naona sijatenda uadilifu, na watu wengine wanakamatwa ovyo, wakishukiwa kwa hayo mauaji, na imekwenda, nona kama inafifia, ukweli unaanza kubatilishwa, na kuna watu wengine, wanatarajiwa kukamatwa, hasa mume wa familia na mdogo wake, nikaona sasa inapokwenda ni kubaya, ni bora nijitokeze mimi mwenyewe niseme ukweli, hata hivyo ni nani nitamwambia huo ukweli aniamini, kwenda polisi ni kama kwenda kujifunga mwenyewe...'akasema.

'Kwahiyo umeamua kujitokeza kwa vile sasa inaelekea kumgusa mpenzi wako wa asili?' akauliza mwenye huku akitabsamu kwa utani.

'Hapana, ....mimi kama mpelelezi, hilo nilikuwa nalifanyia kazi, nilikuwa kwenye uchunguzi binafasi, kumjua ni nani hasa alifanya hayo mauaji, maana nashindwa kujua, mtoto wa Makabrasha, hakuonekana siku hiyo, na asingeliweza kumuua baba yake, ...unaona hilo...'akatulia kidogo, halafu akasema;

'Kiufupi, sikutaka kusema huo ukweli, kabla sijamaliza uchunguzi wangu, ila ninachotaka kuwaambia hapa ni hivi, ...mimi sijamuua Makabrasha...na sikuwa na mipango hiyo, mimi nilikuwa na mipango yangu mingine kabisa ya kumnasa huyo mtu na kumfikisha kwenye vyombo vya dola, na iwe mwisho wa mtandao wake....’akasema

‘Sasa kama sio wewe ni nani aliyemuua Makabrasha?’ akauliza mwenyekiti.

‘Kama mtaniruhusu ninaweza kuongea nionavyo mimi,kutokana  na uchunguzi wangu, lakini hamuoni kuwa hayo ni maswala ya polisi, ambayo hayahusu hiki kikao?’ akauliza na mwenyekiti akakaa kimiya kwa muda. Baadaye  akachukua simu yake akitaka kupiga , huku akimwangalia huyo shahidi, na shahidi akageuka nyuma kuangalia mlangoni, kama anataka kukimbia.

NB: Ni nini kitaendelea.


WAZO LA LEO: Sio vyema kuwa na silaha za moto kwenye majumba yetu, kama bastola na bunduki, na kama ni lazima, kutokana na maisha yetu, tujitahidi sana kuwa na tahadhari na silaha hizo, tuhakikishe kuwa sehemu tunaziweka silaha hizo ni sehemu za siri na iwe unaifahamu wewe mwenyewe kama neno lako la siri. Wakati mwingine, kuwa na silaha za moto ndani ni kama kufuga nyoka mwenye sumu. Tuwe makini.
Ni mimi: emu-three

No comments :