Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, January 6, 2014

Mkuki ni kwa Nguruwe-58


Watu wote walikuwa kimiya wakitaka kusikia kauli ya shahidi huyo mpya, hasa pale alipotoa ombi,kwa mwenyekiti, la kuomba jambo ambalo hakuliweka wazi,  na mwenyekiti akiwa na mashaka na huyo shahidi akamuuliza ni ombi gani hilo,

Tuendelee na kisa chetu..........

 ‘Kifo cha Makabrasha ni tukio ambalo halikutarajiwa na wengi, hata mimi sikutarajia kuwa huyo mtu angeliuliwa kirahisi hivyo,...nitalielezea hili kwa undani zaidi ili kila mtu apate kuelewa, ila kabla ya kulielezea hili, nina ombi moja kwako mwenyekiti na washiriki wa kikao hiki...’akasema shahidi.

‘Kitu gani unachotuomba, ..?’ akauliza mwenyekiti na shahidi huyo akatoka pale alipokuwa amekaa akatembea hadi alipokaa mwenyekiti na kuanza kumnongoneza jambo, waliongea kwa muda, kwa kunong’onezana, na mwenyekiti akawa kama anakataa, kwa kutikisa kichwa na alionekana kabisa hataki hayo anayoambiwa na huyo shahidi,...

Baadaye mwenyekiti akasema , kwa sauti ambayo tulimsikia ;

‘Nitampigia yeye mwenyewe, atajua ni nini la kufanya lakini mimi sitaki kabisa ...’akasema na akashisha sauti, kwani shahidi alionekana kutokutaka hayo anayoongea naye yaisisikike, na alipoona mwenyekiti hakubaliani naye, akasogea kinyume nyume akiwa kama katahayari, hata hivyo, akageuka na kurudi sehemu yake, na kuanza kuongea;

‘Nafahamu kabisa wote humu ndani nii watu wenye hekima, akili na utashi wa kufikiri, haya nitakayowaelezea hapa ni mambo ambayo sikustahili kuwaelezea, ni mambo ambayo nilitakiwa niwaelezee polisi, lakini kwa ajili ya kuliweka hli jambo sawa, nimeamua kuwalezea,  kwani nikiacha kuelezea ilivyokuwa mkitoka hapa, kila mmoja atatoka na yake, na mwisho wake, nitakamatwa kabla sijamaliza kile nilichokianza.

Mwenyekiti aliposikia hivyo, akainua simu yake na kumpigia mtu, na kumfanya shahidi atulie kwanza, na mwenyekiti akawa anaongea na simu huku akiwa kainama na alikuwa akiongea kwa sauti ndogo, kama vile hataki watu waliopo humo ndani kusikia anachoongea, na alipomaliza akasema;

‘Samahani kidogo, nilikuwa naweka mambo sawa, ...haya shahidi unaweza kuendelea na maelezo yako....’akasema mwenyekiti akionyesha kukerwa na kitu, na shahidi akatulia kwanza akimuangalia mwenyekiti na baadaye akasema;

‘Ni hivi...Makabrasha hayupo peke yake, japokuwa wenzake, wameamua kujifanya hawahusiki, na hata mimi sikuwahi kuwa na hawo wenzake kwa karibu,ila niliwahi kusikia wakiongea na Makabrasha wakipanga mipango yao, na kuna watu wakubwa tu, lakini kwa nafasi yangu siwezi kusema lolote hapa, ila kuna mtu mmoja ambaye alikuwa akifika mara kwa mara kuonana na Makabrasha, nitakuja kumuelezea mwishoni kama mambo yakienda sawa  ....’akaelezea huyu shahidi.

‘Kwahiyo sio swala dogo kama mnavyolifikiria nyie, ...mimi nitajitahidi kuelezea upande wa mtu wetu tu, ambaye anatuhusu sana,...huko kwingine hakuwahusu,...kwa manufaa yenu, na kwa manufaa yangu pia,...kwa wenye kuelewa wataelewa, na hata mkisikia leo nimekamatwa, au ku-uwawa, mjue jinsi gani ya kulieleza hili kwa jamii...’akasema kwa sauti ndogo.

‘Mwenyekiti nafahamu toka awali umekuwa makini na swala hili, nafahamu ni kwanini, na nafahamu kuwa wewe na polisi mnaaminiana sana, lakini nakupa angalizo, kuwa kumbukumbu nyingine walizokupa wewe, ni za uwongo, kuna mambo wameyaficha, makusudi, huenda ni katika mbinu zao kwa ajili ya kufanikisha kazi zao, au ni kwa ajili tu ya kuficha ukweli...mimi huko sitaongelea sana kuthibitisha hayo....’akasema na mwenyekiti akamwangalia kwa mashaka, lakini hakusema kitu.

‘Nafahamu kabisa kuwa mwenyekiti hunifahamu undani wangu,ninaishije hapa Dar,  zaidi ya kufahamu kuwa nimeolewa na docta, na wewe ulikuwa mstari wa mbele kuipinga ndoa yangu, siwezi kukulaumu sana, ...kwa vile unafahamu sana asili ya huko nilipotoka, na kwa hekima zenu, haya yanayotokea kama wangeliwasikiliza nyie huenda haya yasingelitokea. Lakini yote ni maisha....’akasema shahidi.

‘Maisha yangu ya kawaida, licha ya ndoa, wengi wananifahamu kama mama shughuli, leo nipo hapa kesho nipo kule, hata mshirika wangu hajui zaidi ya kunitumia kwa manufaa yake...hata mume wangu hajui zaidi ya kunifahamu kama mama shughuli..’akasema akimgeukia mume wangu na baadaye mume wake.

‘Anayenifahamu vyema, ni  rafiki wa mke wa familia, kwani yeye ndiye aliyekuwa bosi wangu, hata mke wa familia hanifahamu vyema, zaidi ya kuwa ni jirani yake, na zaidi ya kuniona nikimsaidia rafiki yake kwenye mambo fulani fulani...nawaambia hivyo, maana kama mambo haya yatakwisha kwa amani, basi sitaki tena kazi hizi za hatari, mimi nimejipanga kivyangu, maisha ni popote, hata kijijini inawezekana....

Mimi ninachotaka kuwaelezea ni jinsi gani ilivyotokea, siku Makabrasha alipouwawa, ...ni kweli nilikuwepo kwenye hilo jengo, ....’akatulia kidogo akimwangalia mwenyekiti, kama anachelea kuongea jambo, lakini mwenyekiti akamuashiria aendelee kuongea;

‘Makabrasha alikuwa na maadui wengi, na wengi wao, walifikia hata kumlaani,na inapofikia hatua wanadamu wenzako wanakulaani, wanatamani hata ufe, ujue wewe huna thamani tena katika hii dunia, hata kama ni tajiri, lakini ndani ya mioyo ya watu, wewe ni mfu, ...’akatulia kama anasubiria jambo, akamwangalia mwenyekiti.

Mwenyekiti alikuwa katulia kama anawaza jambo, lakini baadaye akachukua simu yake na kumpigia mtu akawa anasikiliza na kuwafanya watu watulie wakisubiria hata shahidi huyo alionekana mwingi wa wasiwasi , hadi mwenyekiti alipomaliza kuongea na simu, halafu akaonyeshea kidole guma, kuashiria mambo yapo shwari..

‘Endelea shahidi uwanja ni wako, nimeshafikisha ujumbe wako.....’akasema mwenyekiti na shahidi bado akiwa na wasiwasi akasema;.

‘Katika maisha yetu haya, watu wana matatizo yao, wengine hawajui wataishi vipi, wanahangaika usiku na mchana, ili wapate angalau riziki zao...lakini maisha ni magumu, usiombe..., watu hawa hawana utulivu wa moyo, wana amani ya kiwiliwili tu, lakini hawana amani ya moyoni,...ndivyo maisha ya walio wengi yalivyo, watu kama hawa wanatafuta upenyo litokee jambo watoe hasira zao...’akasema na kugeuka kumwangalia mume wa familia.

‘Watu wana matatizo yao makazini mwao, wananyonywa, wanachokifanya hakiliangani kabisa na kile wanachokipata, nguvu kazi yao inatumika vibaya, ...hakuna anayewajali, wanahangaika, kupata, agalau huduma muhimu, angalau mahitajio muhimu, lakini kipato chao hakikidhi hata hizo huduma muhimu. 

Wanachokipata ni kama vile wenzetu wanavyosema tonge mdomoni, hata mdomoni kwenyewe ni kama onja –onja, unategemea huyu mtu atakuwa na amani kweli...huyu akipata nafasi ya kufanya unyama ataufanya unyama kweli

Watu wana matatizo sana huko kijijini , usione watu wapo kimiya, mtu analima mvua hakuna, pembejeo hakuna, anatumia jembe la mkono, mtu huyu kila siku anakatwa kodi, kila anachonunua, ni kodi, akigeuka huku kodi, mtoto wake wanadaiwa ada, yeye anaumwa magonjwa yasiyohesabika, akienda hospitalini, hakuna dawa...akanunue, akanunue, na kodi yake imeenda wapi, mtu kama huyu utasema ana amani , ni kweli ana amani ya kiwiliwili, atavumilia, lakini moyoni hana amani..na akipata kisingizio cha kufanya ubaya ataufanya kweli kweli..

Siku tulipoongea na mwenzangu tuliyajadili haya, na Makabrasha alituambia hayo niliyoyaongea mwanzoni, akasema alipoiona system,...ilivyo, jinsi watu wanavyokula, wanavyohujumu, wanavyowatesa wenzao, akaona hakuna jingine na yeye ni lazima atafute njia  ya kutumbukiza mrija wake, ..na yeye aweza kufanya awezavyo, ili naye apate maisha mazuri.

Hizo ndio ndoto zake, kuwa katika hii dunia, ni kila mtu na hamsini zake, kama una uwezo wa kufanya hivi, na ukapata, basi fanya, kama kuna sehemu unaweza kuitumia kama ngazi ili na wewe ulipate tunda fanya hivyo, na yeye akasema atatumia kisomo chake, akili yake, kuhakikisha, anapata kutoka kwa matajiri, kwani anasema matajiri wengi hawajapata hicho walichokipata kwa njia za halali, kwa hiyo hata yeye akiwaibia ni halali yake....hizo ndio sera zake.

Alipotuona tumebahatika kuolewa na kuoa kwa watu wenye uwezo, akasema kama hatutaungana naye, basi na sisi ni wamoja wa watu wanaohujumu raia, kwahiyo tutakuwa maadui zake...hizo ndio sera zake, na alichofanya yeye, ni kutumia elimu yake, katika nyanja yake, akachanganya na ujanja wake wa vitabuni, akabuni njia zinazojulikana kama blackmail.Sijui tafsiri yake ni nini kwa Kiswahili, ....’akasema na kumwangalia mwenyekiti.

Wakati tupo kijijini tunahangaika na maisha, Makabrasha alikuwa akifika, anatuweka chini, anatueelzea mambo mengi, aliyoyagundua, na yanayotendeka, mambo ya kidunia, na utajiri wao, kwakweli hata mimi nilivutika sana, nikatamani niolewe na mtu mwenye uwezo, ndio maana tuliona na sisi tutatafute sehemu ya kuuona ubinadamu wetu, na sisi angalau tujue kula wali kwa uma, angalau na sisi tuweze kuiona dunia, ni kweli mimi nikaolewa na mume ambaye ana uwezo wake, na mwenzangu akamuoa, binti wa watu, tukajisahau.

Ndipo akatokea huyu jamaa, na ndoto zake, na sera zake, kwake yeye hilo lilimuuma sana, kwani alishapanga mipango yake, mingi....hutaamini kutoka na mbinu za huyu mtu, kutokana na kazi yake hiyo aliweza kupata pesa nyingi tu, na akaanza kujenga nyumba, na sio nyumba, ni gorofa, hadi anaingia kwenye noa zetu, yeye alishakuwa na mipango ya kumalizia gorofa lake lilitoka ardhini, kwenda mbinguni.

Watu kama hawa wapo wengi, wanaishi kiujanja ujanja, wanakuja kwako, wanakupima udhaifu wako, wanakuona una njaa kali, wanaanza kupenyeza sera zao, na nyie bila kujua, kwa vile mumesahaumia, mumeshteseka, ....mna visasi ndani ya moyo, mnakubali, mnaingia kichwa kichwa, na kufuata yale anayowaelezea, hamjui mwenzenu kajiapanga vipi, ....

Nimebahatika nikapata ndoa yangu, sawa, ilikuwa ni ndoa yenye ajenda ya siri, lakini ni ndoa yangu, sawa, ilikuwa nampenda mtu mwingine, lakini ni ndoa yangu, ambayo huenda asingelikuja huyu mtu ningeliweza kujifunza nikayasahau ya kale,tukaendelea kuishi hivyo hivyo, kwa kudanganyana, wengi wanaishi hivyo mpaka umauti unawakuta,  ni mke na mume kimwli, lakini kindani mioyo yao inatamani kwingine...huwezi amini, mume wangu alikuwa kila siku akinifundisha jinsi gani ya kuishi kwa raha, kama mume na mke, nilikuwa nikimuitikia kwa kichwa, lakini moyoni nilikuwa na jereha, ..

Haya na mengine mengii yalijenga chuki kwenye moyo wangu, nakutamani kufanya lolote, kwa yule ambaye namuona ni kikwazo kwangu, lakini sikufikia hatua ya kutaka kuua, naogopa sana kumwaga damu ya mtu asiye na hatia, na ikizingatia kuwa mimi nimejifunza uaskari, na moja ya nidhamu ya uaskari, ni kuua adui, aliyeanishwa kisheria kuwa kweli huyu ni adui yako na anastahili kufanyiwa hivyo, ....

Nafahamu wengi watanishangaa, nikisema nimejifunza uaskari, naomba mlielewe hivyo, na mlichukulie hivyo hivyo, ndio maana nikatoa ombii kwenu, kuwa haya niakayoyaongea hapa, yaishie hapa hapa,, tukitoka hapa, kila mtu na hamsini zake, hayo mengine waachieni wahusika, wanajua ni nini wanachokifanya, lakini kama mtu atajitia kidomo domo, ....sawa nitakamatwa, kama mshukiwa, wa mauaji, lakini je ni kweli nilifanya hivyo...?’ akageuka kuwaangalia watu.

Nafahamu mpaka hapo nimewachanganya, ...mtaelewa tu...’akawa kama anatabasamu.

‘Sasa naomba nianze maelezo yangu kwa jinsi ilivyokuwa ....akageuka kumwangalia mume wangu ambaye naye alikuwa akimwangalia kwa hamasa, kama vile haamini kitu gani kinachotokea; kama vile hamuamini huyo mwanamke kuwa ni yule yule aliyekuwa akimfahamu siku nyingi.

Mume wa familia alikuwa ameshapona muda mrefu  tu, lakini kutokana na alivyopanga Makabrasha , akatakiwa kuendelea kuigiza kuumwa hadi hapo mipango ya mtu huyo ikamilike, aliambiwa hilo ni kwa manufaa yake mwenyewe ili asije akaonekana kuwa yupo kwenye mipango fulani, ili mke wake aendelaa kumpa nafasi , kwani kwa hayo aliyoyafanya kikatiba yao ya kifamilia, ndoa haipo tena,..sasa asingelweza kuondoka hivi hivi...ile ndoto yetu ya kijijini isingelikamilika..

Mimi nikawa nimepewa kazi ndani ya ofisi ya Makabrasha, nikiwa kama muhudumu wake maalumu, lakini nia na lengo lake niwe karibu naye, nisije nikaharibu mipanglio yake, kwahiyo nikawa napangiwa kazi hata za usiku, na mume wangu kwa vile alikuwa hajui kinachoendelea yeye alifahamu kuwa nipo kazini. Aniniruhusu , ananiamini ....

Nilimuandikia na hata kuongea na rafiki wa mke wa familia kuwa mimi sifanyi kazi naye tena, ikiwa ni moja ya mikakati ya Makabrasha ili aweze kuniajiri yeye, na hata rafiki wa mke wa familia alipofika, mimi nilikuwa ndani ya jengo, jengo ambalo analimiliki Makabrasha, na humo kuna mambo mengi ambayo hayajulikani. 

Hadi hapo Makabrasha alikuwa hajanifahamu vyema, zaidi ya binti wa kimasikini, wa kule kijijini..na alikuwa akifahamu kidogo kuwa nilikuwa natumiwa na rafiki wa mke wa familia,...

Mipango ikiwa inakamilishwa, mikataba imeshabadilishwa, na mikataba mipya imetayarishwa, na kuwekwa inapostahili, sasa Makabrasha akaanza kutoa makucha yake, akatayarisha mikataba mipya ambayo itampa yeye nafasi ya kumiliki makampuni, na mali nyingi, ambazo kwa muda mrefu alikuwa akizimezea mate, lakini alifanya hivyo kwa mgongo wa mume wa familia. Na mume wa familia, alikuwa hana nguvu tena, kwani alishawekwa kwenye mikono ya Makabrasha. Akili yake ya kuwaza mbali ilikuwa imefika kikomo.

‘Nitafanya nini kwa sasa, huyu jamaa ana siri zangu nyingi, ana mambo yangu mengi, ambayo akimuonyesha mke wangu au wakwe zangu, nitafukuzwa kama mwizi, kwahiyo inabidi nimkubalie kila kitu...’akaniambia na mimi nikawa sina njia ya kumsaidia, nikamwambia, kwa usalama wake, akubali tu, hadi hapo nitakapogundua njia ya kulimaliza hilo.

Mimi nilishaamua kuwa nilimalize hilo, kwani kama nisipofanya jambo, hali hiyo itaendelea kututesa katika maisha yetu yote, tutakuwa watumwa wa mtu mmoja, na hata kama tutaendelea kuishi kwenye ndoa zetu, itakuwa ni ndoa jina tu,..kwa mfano mimi nilitakiwa kumtii huyu mtu kama mtumwa wake, kila anachokitaka nimfanyie, hata kuzalilika, sasa kulikuwa na manufaa gani hapo, nikaona nijitolee muhanga, nifanye kazi yangu...sote sisi ni maaskari kwenye jamii, inapofikia mahali kama hapo, unastahili kuonyesha uaskari wako...tumia mbinu za medani...shauri lenu..’akasema na kutabasamu.

‘Usijali, mshirika, mimi nitajitolea kwa ajili yako....kama utanikumbuka sawa, nafanya haya kwa vile nakupenda, japokuwa penzi kwako kwangu silioni..nimeshakuona kuwa wewe unanitumia ili upate unachokitaka, huna tofauto na Makabrasha...’nikamwambia.

‘Kwanini unasema hivyo, mimi mbona  nakupenda sana, umeshahu tulivyoahidiana kule kijijini...kwa hali iniliyo nayo, nashindwa kutimiza ahadi zetu, kwani nimewekwa sehemu ambayo siwezi kukuonyesha kuwa nakupenda, lakini moyoni tupo pamoja,....huoni sasa naumwa, ugonjwa wa kuigiza, nikipona tu na yeye akifanikiwa anvyotaka, nitatafuta njia ya kumkomoa, tutarudisha mali yetu yote...’akaniambia

‘Umeshachelewa wewe hupati kitu tena, ...kama huyu jamaa ataendelea kuwepo duniani, ujue wewe utakuwa mtumwa wake wa kudumu, na hutakuwa na ndoa yenye furaha tena, ..na sizani kama ndoa yako ipo hai tena, kama itakuwepo ni kwa  huruma tu...’nikamwambia.

‘Sasa tufanye nini?’ akaniuliza

‘Sasa hivi unaniuliza eeh, sasa tufanye nini, kamuulize Makabrasha,ninachoweza kusema niliyo nayo niachie mwenyewe, wewe endelea na Makabrasha wako...’nikamwambia.

‘Hivi wewe unajiamini nini , wewe unafahamu vyema huyu mtu, ...nakuonya kama una jambo dhidi yake, unajitakia matatizo,achana naye huyo mtu....’akasema.

‘Mimi ni askari, ninafahamu ni kitu gani ninachokifanya, ninachohitajia kwasasa ni silaha tu,...sina silaha,na sitaki kuazima silaha kwa aliyekuwa bosi wangu, nimeshaacha kazi ...’nikamwambia, na yeye abakia kimya akiniangalia kwa macho yaliyojaa mshangao, maana alikuwa hanifahamu kuwa mwenzake katika kuhangaika na maisha, nilishapitia kozi za kijeshi,...’akatabasamu.

‘Wewe mwanamke, usije ukajidanganya, ukaangalia sinema ukaigiza, ukafikiri hayo mambo ni rahisi hivyo kwanza nikuulize lini umejifunza kutumia silaha?’ akaniuliza.

‘Mimi nafaham kutumia silaha kama unvyofahamu wewe kutumia kijiko wakati wa kula,...’nikasema kwa mbwembwe , na yeye akaniangalia kwa macho ya mshangao, nikamwambia;

‘Nipe hiyo silaha uone nitakavyoitumia, hilo kwangu ni dogo sana, na cha muhimu kwa sasa ni mimi kuipta hiyo silaha, sio jinsi gani ya kuitumia au kutaka kujua nilijifunza wapi kutumia silaha, mjini hapa, ...cha muhimu kwa sasa ni muda, tunakimbizana na muda...’nikamwambia.

‘Mhh, haya,... ndio maana kila mara upo na rafiki ya mke wangu, najua ni yeye kakufundisha, lakini  uwe makini na silaha, mimi sipendi sana kushika shika silaha,...’akasema.

‘Nahitaji sana silaha kipindi kama hiki, lakini sitaki mtu afahamu kuwa nina silaha,..hasa rafiki wa mke wako, au aliyekuwa bosi wangu, sitaki ajue nina mipango gani ....Nahitaji sana silaha, na tatizo ni muda, ningeenda kuazima kwa watu wangu ninaowafahamu, japokuwa sipendi iwe hivyo, lakini muda....sina muda kabisa nikitoka hapa kama unavyoona nina watu wananilinda..wapo hapo nje wananisubiria.’nikamwambia.

‘Kama ni silaha, na ...mimi ninaweza kukupatia silaha, lakini silaha ya nini, unataka kumuua nani, usiniambia umefikia hatua ya kutaka kumuua Makabrasha?’ akaniuliza kwa mashaka.

‘Sitaki kumuua mtu yoyote, na sina mpango huo, ila ikibidi...’nikasema nikiwaza jinsi gani ya kumfamisha mtu kama huyo.

‘Lakini siwezi kufaya kosa kama hilo,la kuua, hapana, kama ningelitaka kufanya hivyo ningelishafanya mapema sana, ...ila silaha itanisaidia sana mimi kwa kujihami, muda wake ukifika, nikiwa na silaha, ninakuwa kama nina wasaidizi watano nyuma yangu, ..’nikamwambia na nikweli nikiwa an silaha, hunibabaishi.

‘Kuna jambo nataak kulifanya usiku wa leo, na asubuhi yake, ni muhimu sana niwe na wasaidizi wangu, na wasaidizi wangu ni silaha..kama nitakuwa sina silaha, sitawezi kufany a kitu, jamaa kajizatiti sana, ana walinzi, ana mitandao ya ulinzi, kwahiyo hata nikiwa na silaha, itakuwa ni kwa muda maalumu tu....’nikamwambia.

‘Naona wewe unajitakia matatizo makubwa kwa Makabrasha, na je huyo mtoto wake, ambaye ni mkorofi utawezaje kumdhibiti vipi maana yule ni kichaa, eti kasomea sheria, mbona haviendani! ...Mimi kwa ushauri wangu,achana nao, mimi nimeamua tuwape kila wanachokitaka, ili tu ...wasije wakanichafulia jina alngu, nikafukuzwa, hata hivyo, ...mbona mambo yapo safi, mikataba ile inanipa mamlaka ya kufanya kila jambo, kama mume wa familia....’akaniambia.

‘Halafu mwisho wake itakuwaje,..hujaliangalia hilo kwa mapana yake, hapo ulipo kwa lolote utakalolifanya kwa sasa, bado upo kwenye matatizo, hasa ya ndoa yako. Ile mikataba mnayojidanganya nayo si chochote silolote,...'akasema.

'Hivi wewe unamfahamu Makabrasha ...?' akaniuliza.

'Namfaahmu sana, ila wewe huifahamu familia uliyo nayo, familia ya mke wako, sio ya kuchezea, kwanini hamniulizi mimi ambaye nimeifanyia kazi za siri familia hiyo, kwanini mnakuwa wakaidi, wewe unamfuata Makabrasha, yeye ni jambazi, mwisho wa siku anakuruka, wewe utaenda jela, yeye kwa vile ni wakili anafahamu jinsi gani ya kujitetea,....’nikamwambia.

‘Sasa wewe ulitaka mimi nifanye nini kwa hatua kama hii?’ akaniuliza

‘Ni kweli kwa akili zako fupi hukuwa na jinsi nyingine, maana wewe ni kidume,...ni kweli hata hivyo umeshachelewa, kama ungelinisikia toka mwanzo, yote haya yaasingelifika hapa, tamaa zako za kimwili, na akili fupi ya kufikiri ndio imekufikisha hapo,...sijui kama kweli haya yataisha kwa amani, na hata yakiisha kwa amani, sijui kama ndoa yako itakuwepo tena, na baya zaidi unaweza ukaishia jela, wakikuhurumia sana, watakutupa kijijini ukawe omba omba...’nikamwambia.

‘Thubutu, hilo halitatokea, na likitokea, nitafanya jambo ambalo halitasahaulika katika familia yao...’akasema

‘Utafanya nini....?’ nikamuuliza

‘Wewe niambie silaha unahitaji ya nini..?’ akaniuliza.

‘Kuna mtoto wake, yeye ndiye namuogoap sana, anataka kunifanya mimi kama anavyonifanya baba yake, siwezi kuzalilika kiasi hicho, silaha itanifanya nimdhibiti...’nikamwambia bila kumfafanulia mambo mengine ambayo niliyapanga kichwani mwangu,sikuwa namuamini sana kwenye mambo hayo ya kivita..

‘Kama kweli unahitaji silaha, na kama kweli itaweza kusaidia jambo, mimi nitafanya kila mbinu hadi niipate hiyo silaha,..hiloniachie mimi , nitachukua silaha ya mke wangu,nitamtumia mdogo wangu, maana siwezi kutoka hapa kwa sasa..ila tukubaliane, kuwa silaha hiyo itakuwa inaletwa kwako usiku kama ukiwa na kazi za usiku, asubhi tunairudisha...au unasemaje?’ akaniuliza.

‘Kama unaweza kuipata hiyo silaha,  itasaidia sana, nahitaji kuwa nayo sanasana usiku wa leo, na asubuhi utakapokwenda kukutana na Makabrasha, baada ya hapo inaweza isiwe na kazi tena, ...’nikamwambia nay eye akaniangalia kwa mshangao, hakuamini kuwa mimi ninaweza kutumia silaha.

‘Sikiliza kwa makini, kesho ukifika kuonana na Makabrasha, ujaribu sana kumchelewesha ili nipate muda wa kusimamisha mitandao yake ya ulinzi, na ...kwa vile mtoto wake, atakuwa hayupo, ...kama alivyodai, japokuwa simuamini, ...nitaweza kufanya mengine bila kujulikana, yote inategemeana na muda, muda ni kitu muhimu kwenye mapambano kama hayo...’nikamwambia.

‘Kwani unataka kufanya nini kitakachosaidia, maana mengi yameshafanyika, mikataba karibu yote nimeshaisaini kukubali, umebakia huo mmoja tu,.....na wewe mwenyewe umeshasaini mkataba wako, kilichobakia ni mume wake, ambaye hatakuwa na kauli ya kubisha,...hivi mume wako umeshaongea naye...?’ akaniuliza.

‘Siwezi kufanya ujinga kama huo, unafikiri mimi ni mjinga kama wewe...kanisainisha huo mkataba, nimekubali kufanya hivyo, lakini siwezi kuongea na mume wangu, nafahamu kabisa mume wangu hawezi kukubali, san a sana, ni kunitafutia njia ya kupewa talaka haraka..ndio maana nahitaji hiyo silaha...’nikamwambia.

‘Kumbe...ni kwa ajili yako, ..kwahiyo mimi haitanisaidia sana, kwasababu nimeshakubali kila kitu...’akasema kwa shingo upande. Na wakati huo ujumbe ukaingia kwenye simu kuwa muda wa kuongea na huyo mtu umekwisha ninasubiriwa nje tuondoke, nililetwa na mlinzi wa Makabrasha, ambaye baadaye huhakikisha kuwa nimerudi ofisini kwake, au nyumbani kwangu, nilikuwa nikifuatiliwa kila hatua, ili nisije nikafanya kinyume na makubaliano.

Ujumbe huo ulipoingie kwenye simu yangu niliuosoma, pamoja na mengine, niliambiwa nisisahau kuwa usiku wa leo kuna kazi, kwahiyo nimuombe mume wangu. Nilifahamu hilo, na nilishamuaomba mume wangu, lakini moyoni nilijua usiku huyo utakuwa usiku maalumu, huenda wa mapambano au wa kumaliza kazi niliyokwisha kuianza, cha muhimu niipate hiyo silaha, ...

‘Je hiyo silaha inaweza kupatikana  kwa usiku wa leo, ...?’nikamuuliza nikiwa na mashaka ya kupatikana hiyo silaha. Na mume wa familia aliniangalia kwa makini, na wakati ananiangalia mimi akilini nilikuwa  nikijiuliza, hata kama ikipatikana hiyo silaha, ni jinsi gani ya kuiingiza kwenye lile jengo maana jumba lile lina mitambo ya kunasa matukio na hiyo mitambo ikihisi kuwa mtu ana silaha, kuna ving’ora vya vya hatari vinalia, na kuna askari wa Makabrasha wasio na akili nzuri, wakitokea hapo, ni kupiga hata kuua.

‘Hilo niachie mimi, ...silaha itapatikana, na natumai hutaifanyia jambo la kijinga...’akasema na mimi nikaingiwa na wazo na kusema;

‘Usiku wa leo kuna tafrija kwenye lile jengo, itakuwa ni nafasi nzuri ya mimi kuweza kuipenyeza hiyo silaha bila kujulikana,..unaonaje?, kama kweli itapatikana usiku wa leo muda wa saa tano hivi, itakuwa vyema, je mke wako hawezi kuhisi kuwa silaha haipo?’ nikamuuliza.

‘Mara nyingi haitumii, ipo kwenye kabati lake siku zote, sijawahi kumuona akiichukua, hata kama kuna tukio la hatari, huwa haichukui, ipo tu..sizani kama atakuwa na wasiwasi nayo...’akaniambia.

‘Basi wewe jitahidi, mtume mdogo wako,akaichukue ...mimi nitawasiliana na yeye, nione jinsi gani nitakavyoichukua hiyo silaha, lakini asifike sehemu ya mapokezi, ..asionekane kabisa kwenye hilo jengo,nitamwelekeza jinsi gani ya kufanya ...’nikamwambia, na tukakubaliana hivyo...na tulikuwa tukiongea nje kwenye eneo analochukulia mazoezi ya viungo kwasababu ya matatizo yake ya ajali.

‘Na kweli usiku ule nikaipata hiyo silaha, silaha iliyokuja kumuua Makabrasha,...swali ni je niilipata pata vipi hiyo silaha, na ilitumikaje, nitawaelezea yote hayo...’akasema na kutulia kidogo, akamwangalia mwenyekiti.

Mwenyekiti alikuwa akiangalia saa, na mara shahidi huyu akaenda pale alipokaa mwenyekiti wakawa wananong’ona, sikujua wanaongea kitu gani, lakini walipomaliza kuongea, mwenyekiti alichukua simu na kumpigia mtu, huku akiwa kamuangalia huyo shahidi kama vile anaogopa jambo kutoka kwa huyo shahidi.. ...
NB: Je silaha hiyo ilifikaje kwa shahidi, na je ilitumikaje kumuua Makabrasha na je kwanini shahidi huyu anaongea sana na mwenyekiti, tukutane sehemu ya tatu ya hitimisho la kisa hiki.

WAZO LA LEO: Kila hila mbaya, ina walakini wake, na mwisho wa hila mbaya, ni kuumbuana tu. 

No comments :