Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, January 23, 2014

Baada ya Dhiki Faraja-Kisa kipya Utangulizi


                                              BAADA YA DHIKI FARAJA
                                                     Utangulizi
Nikiwa na barua yangu mkononi, nilifika kwenye ofisi niliyoelekezwa, muda hu nilishachoka kutokana na jua kali na kutembea kwa miguu, ajira siku hizi ngumu kweli, unaweza ukamaliza kiatu kwa kutembea kila ukifika kwenye ofisi unachona na kiratasi za kupunguzwa wafanyakazi, hata hivyo sikukata tamaa nikajua kazi nitapata tu.

Leo hii nikaamukia kwenye ofisi mojawapo, ambayo kwa taarifa za haraka inamilikiwa na mzawa, ni mtu aliyejiwekeza, hadi akafanikiwa, na alikuwa akitafuta mhasibu. Niliamuka asubuhi sana, nikijua usafiri ni wa shida, nikaingia kwenye dala dala hadi kwenye hizo ofisi, nilipofika zikutaka kuulizia, maana ofisi yenyewe ilikuwa ikionekana,  jina la ile kampuni lilionekana wazi, kwenye jengo hilo,  ilikuwa sio kubwa sana, na kama nilivyoelekezwa, ni kampuni ya mtu binafsi.

Nikagonga geti, na mlinzi akanifungulia, akaniuliza wewe ni nani na umekuja kufanya nini, nikamweleza, akanionyesha wapi nielekee, nikakatembea hadi kwenye jengo lenyewe la ofisi, nikafungua mlango na kuingia kwenye hiyo ofisi, cha kwanza kukutana nacho ilikuwa kelele za..

‘Piga, ua,...kata mtama, oooh, ..., nitakuua, huna adabu wewe...huniwezi...’

Mbele yangu kulikuwa na baadhi ya wafanyakazi, niliona wakiwa kwenye heka heka za kuamua ugomvi, kulikuwa na jamaa wawili walikuwa wakipigana, kwa nguvu zote, hadi makoti yao ya suti, yakawa yamechanika, hawakuwa wakijali, nikashikwa  na mshangao, hakuna aliyejali kuniuliza wewe ni nani na unataka nini, maana kila mmoja alikuwa akitafuta upenyo wa kuangalia pambano la majamaa wawili ambao walivalia suti za ofisi, japokuwa sasa mashati ya ndani yalikuwa yamelowa majasho.

Hata ,mimi nikaingiwa na hamasa ya kuona lile pambano, nikatembea hadi pale, jamaa walikuwa wamepigana miereka, wapo chini, na moja damu zilishaanza kumvuja puani, huyu wa juu,akawa ana msindilia mwenzake magumi ya nguvu kama anataka kuua, na mwenzake akawa akijaribu kujizuia,kwa muda ule hakuna aliyeweza kuwaamulia, watu walishachoka kuwaamua, wakaona wawaachie watwangane hadi hamu zai ziishe.

‘Jamani hawa watu si watauwana?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Waache wauwane, tumewaamulia lakini hakuna anayetujali,kisa kidogo tu kimewafanya wapigane hivyo,mapenzi, yamegukia siasa, mara imani zao za dini...’akasema mmoja wapo akiwa haniangalii, ila anaangalia hilo pambano.

‘Yule atashinda tu kwa jina la Yesu,...’akasema mmoja wapo na mwingine akadakia

‘Na yule atashinda kwa nguvu za Allah...’akadakia mwingine aliyekuwa pembeni yake
Nikashikwa na butwaa, dini hapa zimeingiaje tena, nikatulia, na mara kukazuka mabishano ya wale waliotaja imani za dini zao kuwa hawo wanaopigana watashinda kwa nguvu za imani zao, kwani haw wanaopigana walikuwa na imani tofauti, kwahiyo hata washabiki wakawa wanamtetea kila mmja kutokana na imani ya dini yake...

Hutaamini hawa wenzao, wakaanza kubishana kwa maneno makali,kila mmoja akitetea nguvu za imani yake, ikawa kama vurugu tena, ..mzozo ukazidi na watu wakaanza kushikana mashati, na wale waliokuwa wakipigana awali walikuwa wamechoka, wakiwa kama majogoo, waliopigana muda mrefu.

Lakini pambano lao lilikuwa halina nguvu tena, kilichokuwa na nguvu ni huu mvutano uliotokea kwa watazamaji, ambao walikuwa wakitupiana maneno makali kukashifiana, kila mmoja akiongea yake, na ilionyesha wazi, hawa wanaopingana kwa maneno makali ya chuki na kashifa wakieleza kwenye imani za dini za mwenzake, hawakuwa wakizielewa dini zao vyema, kutokana na hoja walizokuwa wakizitoa, lakini jaziba, zilikuwa zimewapanda, na mara fujo ikaanza....

‘Nyie kuna nini hapa....’sauti kali ya kike ikasikika, na mara watu wakatawanyika, mbio mbio kila mmoja akikimbilia sehemu yake ya kazi, kumbe alikuwa ndio bosi mwenyewe kaingia, nikageuka taratibu kumwangalia huyo bosi, ....nilishangaa, maana nilipokuwa nikiwasiliana naye nilijua ni mswahili, kutokana na Kiswahili chake kizuri, lakini hapa namuona kama ni asili ya nje, lakini nilivyomchunguza vyema, nikaona ni damu mchanganyiko, inaweza ikawa wazazi wao walikuwa na asili mbili, sikujali sana.

Na mimi kwa haraka nikaenda kuonana na mpokea wageni, ambaye wakati huo alikuwa akihangaika kuweka meza yake sawa, inaonekana alikuwa nje, maana niliona kaweka bahasha yanye kitu kama vitafunio pembeni, na alikuwa keshajisahau, hadi bosi wao alipoingia, na sasa anajiweka sawa kuonekana kiofisi zaidi.

‘Samahani dada, mimi naomba kumuona meneja uajiri...’nikajitambulisha.

‘Hakuna meneja uajiri hapa, huyo aliyeingia ndiye mwenye kampuni, na ndiye bosi wa kila kitu...’akasema huyo mwanadada akijiangalia kwenye kiyoo, hakutaka hata kuniangalia.

‘Nimeleta barua yangu , niliwasiliana naye kwa barua pepe, akasema nije nionane naye...’nikasema

‘Subiri, kaa hapo kwenye kiti, huoni ndio kaingia, na mambo yenyewe leo yamekuwa ni vurugu vurugu, watu wanataka kuuana, kisa ni mapenzi, ....’akasema

‘Mapenzi ina maana haw watu walikuwa wakigombana kwasababu ya mapenzi, wanamgombea nani!...?’ nikamuuliza

‘Eti mimi, ...mimi nimewaambia mwenye kisu kikali ndiye mla nyama, ...wakaanza kuzozana, mara wakashikana mashati, mara ngumi, mimi taratibu nikatoka zangu nje kutafuta vitafunio, nasikia huku nyuma wamepigana hadi kuuana...shauri lao’akasema

‘Mbona nimekuta watu wakibishana na maswala ya dini na siasa...?’ nikauliza

‘Hawa watu ndivyo walivyo, kitu kidogo, kikitokea badala ya kukizungumzia hicho kitu, na kuangalia chanzo chake wanakimbilia kukiingiza kwenye kubishana kuhusu imani zao,...mimi nawashangaa sana, maana hata dini zao wenyewe hawazijui vyema, kuswali hawaswali, kutwa ulevini, kamarii, na vijiweni, kazini kwenyewe ndio hivyo, wanasubiri bosi aje ndio wanakimbilia kujifanya wanafanya kazi, kweli imani za dini zinasema hivyo...’akawa kama anaiuliza na mimi nikataka kumuuliza wewe je hujioni....

‘Kwahiyo aliyeshinda ndiye atakuwa mpenzi wako?’ nikamuuliza

‘Thubutu, ni nani awe na mpenzi njaa, kali kama hawa, mawazo yao ya kufikiri finyu kabisa ...mimi nina mchumba wangu kila siku ananileta na gari, sema tu mkiwa ofisini kuna ile hali ya kupitisha muda, unapata mpenzi wa muda, unakuwa na rafiki wa hapa na pale, ili mambo yaende sawa, lakini sina shida ya mtu....’akasema na mara mlango wa bosi ukafunguliwa

‘Unaongea na nani wewe badala ya kufanya kazi..’sauti kali ya kike ikatanda hewani, hutaamini, yule dada alikaa kwenye meza yake na kuangalia kwenye komputa yake na kujifanya anaandika kitu, huku akifunua funua makaratasi, utafikiri kweli alikuwa akiandika jambo kwa kuangalia ile karatasi anayoifunua, ...nilimwangalia kwa mshangao mkubwa, anavyoigiza kufanya kazi.

‘Wewe ni nani mbona umesimama hapo, unahitaji nini...’sauti ya huyo mwanadada ikaniuliza.

‘Mimi nimekuja kuleta barua yangu ya maombi ya kazi,...nilikuwa nawasiliana na wewe...’kabla sijamaliza akaja pale niliposimama na kuichukua ile barua yangu na kuniambia

‘Njoo ofisini kwangu, ....’akasema na mimi nikamfuata huko fisini kwake, na alipofungua mlango, tukajikuta kwenye ofisi nyingine kubwa, ambapo kulikuwa na wafanyakazi kama watano, kila mmoja alikuwa kimiya kwenye kazi zake na wawili wao walikuwa wale waliokuwa wakipigana, walikuwa wameinamisha vichwa chini, nahisi ni kuficha uvimbe kwenye nyuso zao, ...na mbele yao ndio kulikuwa na mlango mwingine wa kuingia kwenye hiy ofisi ya huyo bosi.

‘Karibu nikusaidie nini.....’akaniuliza huy mwanadada, baada ya kukaa kwenye meza yake, huku akiifungua ile barua.

‘Mimi ndiye niliyekuwa nikiwasiliana nawe kwa barua pepe kuhusu kuomba ajira hapa, katika idara ya uhasibu, na mara ya mwisho tuliongea na simu ukasema nije leo....’nikamwambia

‘Ohoo, ndio wewe...ok, sasa niambie una jua nini katika uhasibu?’ akaniuliza

‘Karibu kila kitu, kuanzia ukarani hadi kutoa taarifa kuu za kimahesabu...’nikamwambia.

‘Safi kabisa, nataka watu wa namna yako, watu wanajua kazi, kuanzia chini, sio mtu anakuja katoka shule au chuo anataka kuwa meneja, anataka kuwa bosi hataki kwanza kujifunza mambo ya chini, hajui kazi za chini zipoje, huyu mtu atawezaje kuwasimamia watu wa chini kama hajui wanafanya nini...mimi nikuambie ukweli, nimetoka mbali sana....hutaweza kuamini, hapa nilipo ni mmumiliki ya hii kampuni, lakini huwezi amini kuwa nimefanya kazi hata ndani, ...’ akaniangalia kwa macho makali.

Nilimuona kama ananitania, nikatulia kumsikiliza na yeye alipoona namwangalia huku natabasamu, akahisi simuamini, akarudia kwa kusema;

‘Nimefanyakazi kama mfanyakazi wa ndani, nimezalilika,  ...nimetaabika, hadi kufikia kutaka kujiua, ...kwa kusingiziwa machafu ambayo sijawahi kuyafanya, na anayekusingizia, ni baba yako mzazi,...leo hii namiliki kampuni hii na nina wafanyakazi ambao wanataka niwalipe pesa nyingi tu huku hawafanyi kazi...muda mwingi hawafanyi kazi...’akageuka kuangalia wafanyakazi wake kwa kupitia kwenye dirisha la viyoo.

‘Lakini watu hawa hawajui jinsi gani nilivyotaabika, hadi kufikia kiwango hiki, wanafikiri hali hii imetoka mawinguni, ukiondoka kidogo tu, wapo kwenye magumzo, ubishani wa mipira, mara siasa, mara dini, umbea mtupu,  mabishano yao yasiyo na maana yoyote, angalia mfano, leo nimefika nakuta watu wanapigana, sasa kweli tufika kwa mtindo huu, nataka kuisafisha hii ofisi na kuajiri watendaji kazi wazuri, sitaki ujinga...’akawa kama ananiuliza.

‘Mhh, bosi ina maana wewe uliwahi kufanya kazi za ndani, house girl?’ nikamuuliza

‘Ndio maana yake, huwezi amini, lakini ndio ukweli wenyewe,  maisha yangu yamepitia hali ngumu, ambayo naweza kusema ni wachache sana waliowahi kupitia maisha niliyowahi kupitia mimi,...nimeitwa malaya na baba yangu mwenyewe mzazi, wakati huo simfahamu hata mume...nikapigiwa nikisingiziwa kuwa ninafanya umalaya, na huenda nina mimba, wakati hu sijawahi kutembea na mwanamume yoyote, nikakatizwa masomo, nimefungwa,...ikafikia muda nikachoka, nikaamua kujiua.....’nikaona machoni yakimlenga lenga machoni,.

‘Usinikumbushe, maana watu hawajui tulipotoka, na wengi nikiwasimulia wanaona ni uwongo ....mwenyewe nikikumbuka maisha yangu yaliyopita nataka hata kulia,.....lakini leo hii unaona,nina kampuni, ninaajiri watu, na kunifanya niamini kwa vitendo kuwa, baada ya dhiki kweli ni faraja, ...’akachukua leso yake na kufuta usoni, nahisi ni kufuta yale machozi yaliyoanza kumtoka.

‘Karibu kwenye ofisi yangu, nitakusimulia kisa changu, mwenyewe utashangaa, kwani yote ni maisha,lakini mimi ninaamini kuwa ukivumilia, ukajitahidi, ukafanya kazi kwa bidii,utafanikiwa....ni kweli kabisa utafanikiwa, lakini ukikaa na kulia, na kulaani, huku hufanyi jitihada, utashia kubaya,...kama methali hiyo inayosema, baada ya dhiki, huja faraja, na mimi sasa nimefarijika,....

********

NB: Ndugu wapenzi wa blog hii, nimediriki kukileta kisa hiki kwani wengi sasa hivi wanapitia katika mitihani ya kimaisha, maisha kweli ni magumu sana, hali za uchumi zinazidi kuwa tete, watu wanafikia hatua ya kukata tamaa, na baya zaidi, hakuna anayetaka kufanya utafiti wa kisayansi akaona tatizo hasa ni nini...

Kinachofuata ni kutafutana uchawi, kila mmoja anamtafatia ubaya mwenzake , kwa kutupiana lawama, chuki za ndani kwa ndani zinaanza kujiejenga na kutafuta visingizio hata kusipofaa, wengine tunawalaumu viongozi , tunailaumu serikali, tulioiajiri wenyewe, kama ulimuajiri kiongozi mbovu, ni nani wa kulaumiwa, ni wewe uliyemuajiri na kumpa kura yako, sasa tujiulize kihekima,...ni kwanini hali kama hizi zinafikia hapa..

Swali la kujiuliza kama umemuajiri mfanyakazi mbovu unatakiwa ufanye nini....?

Kisa hiki kipya pamoja na kuangalia maisha magumu aliyopambana nayo huyu mwanadada, tutajaribu pia kuangalia jinsi gani tunaweza kujikwamua, japokuwa ni kwa shida,...badala ya kukaa na kumlaumu huyu au yule, kutokana na madhila ya kimaisha,...ni kweli, maisha ni magumu, mtu unaamuka hujui atakula nini,...anashindia kitumbua na kipande cha muhogo....

‘Lakini je ni sahihi kukaa na kubishana, na baya zaidi tunageuza ubishani wetu hata kule kusipostahili. kwenye imani zetu  za dini,..nafikiri kama tungelitumia vyema imani zetu za dini, kusingelikuwa na ugomvi, na maisha yangelikuwa ni ya amani,...

‘Tatizo, tunageuza hisia za hulka zetu za asili za ubinafsi, chuki za umimi, husada za kwanini, imani za kishirikiana, na kuzipandikiza kusikofaa, maana dini zote zinafundisha amani na upendo, kama wewe unaingiza chuki, ushirikiana husuda, na uhasama kwenye imani yako ya dini, huo ni ubinafsi , basi hiyo sio imani sahihi ya dini, hizo ni tabia zetu za asili.

WAZO LA LEO: Tusipende kuingiza mambo yetu binafsi, chuki zetu za asili, utofauti wetu wa kimaisha , utofauti wetu wa kisiasa kwa kutumia mgongo wa dini. Dini zipo kwa ajili ya kuzisafisha nyoyo zetu ili zijae upendo, amani na kuvumiliana, hazipo kwa ajili ya kujenga chuki, ...


Tukitumia dini ili tupate wafuasi, ili tufanikiwe jambo fulani, kwa njia ya chuki, propaganda potofu, tunafanya makosa hiyo ni dhambi kubwa sana, kwani fitina ni mbaya kuliko hata uchawi, kwani matokea yake ni mabaya sana, watu watauana, na wakiuana ujue wewe ndiye unayebeba hizo dhambi.

Ni mimi: emu-three

No comments :