Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, January 30, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-5



Ilikuwa usiku wa maneno, sikumbuki ni saa ngapi, simu yangu ikawa inaita, sikutaka kuipokea, maana nilikuwa nimechoka sana, kwani nilipotoka kazini, ili kumkwepa yule mdada, nilipitiliza hadi uwanja wa mpira nikajiunga na wenzangu wengine kwenye mazoezi, na nilipotoka hapo nikapitia sehemu nyingine, kuangalia mpira ligi za Ulaya,hadi saa tano, nikarudi nyumbani na kulala.

Niliiwasha simu yangu ambayo nilikuwa nimeizima makudi, ili huyo mdada asinisumbue, na ilipowaka tu, milio ya kuingia ujumbe wa maneno, ikaanza kuingia kwa mfululizo, sikutaka kusoma huo ujumbe kwani nilifahamu ni kitu gani anataka, nikaiweka simu pembeni, na mra simu ikaanza kuita. Nikaangalia mpigani ni nani nikaona ni namba ngeni

Nikaacha ikalia mpaka ikakatika, baadaye kwa kupoteza muda, nikaanza kusoma ujumbe alionitumia huyo binti, zilikuwa nyingi, nikawa nasoma kwa haraka haraka, hadi nikafikia ujumbe ambao ulinitia wasiwasi

‘Nimekusubiri sana, bahati kaja huyu muhuni, tumesihia kugombana, naomba uje unisaidie niondoke hapa...’

‘Oh, njoo haraka kuna tatizo kubwa, nakuomba ufike haraka, ...la sivyo naituma ile picha kwa bosi wako.

‘Njoo, uniokoe, kama kweli unanipenda njoo, ....kuna tatizo kubwa sana na wewe peke yako ndiye utaweza kunisaidia, usipofika, utakuja kujijutia...’ na ikawa mwisho wa ujumbe.

Mara simu ikaanza kuita, nilipoangalia nikaona ni namba nyingine ngeni, safari hii nikaamua kuipokea, na sauti ya mwanaume ikasema;

‘Wewe ndiye Mosi?’ akauliza.

‘Kwani wewe ni nani?’ nikauliza kwa sauti kali.

‘Ni muhimu, kuna dada mmoja yupo hapa, amekunywa kupitiliza, hawezi hata kutembea, na amesema anakusubiria wewe, hatuwezi kumuacha aendelee kukaa hapa, kasema tukupigie wewe uje kumchukua vinginevyo, sisi tutamtoa na kumtupia kwenye mtaro wa maji machafu, hatulazi walevi humu ndani....’akasema na kukata simu.

 Mimi niliwaza sana, huenda huo ni mtego, wamefanya hivyo makusudi ili nifike kwa huyo mwanamke. Lakini kama ni kweli, kuwa huyo binti kalewa sana, na alitarajia kuwa mimi ndiye nitaenda kumchukua, na balaa likimtokea, huoni kuwa nitakuja kulaumiwa mimi na jamii, hapana, huu sasa sio ubinadamu

Kwa vile sio mbali sana, ngoja niende nihakikishe mwenyewe....’nikasema

Tatizo kwenye nyumba hii ninayokaa mwenye nyumba ni matata, kwani hufuatilia sana wapangaji wake, na hasa akikuona ukitoka usiku, lakini sikujali, nikijua kuwa hiyo ni dharura.

 Basi nikawaza saana mwisho nikasema ngoja tu niende, kwani kutaharibika nini, mimi nitakwenda, kama ni kweli kalewa mimi nitambeba hadi kwake na kwa vile anaishi na mdogo wake, itakuwa rahisi, huyo mdogo wake, atamsaidia kumlaza kitandani, na mimi nitarudi kwangu, sitataka kuongea naye
.
Nikatoka nje, na kuifuata pikipiki yangu na wakati natoka mwenye nyumba akatokeza na kuniuliza;

‘Saa hizi unakwenda wapi?’ akaniuliza nikishangaa, nikijiuliza huyu mtu huwa halali , ina maana muda wote yupo macho kuangalia usalama wa nyumba yake.

‘Kuna mtu kanipigia simu ananihitajia anaumwa’nikasema
‘Hiyo miito ya muda kama hii sio mizuri, kama ingelikuwa mimi nisingelikwenda huko, nakushauri achana naye, puuzia huo muito, kwa manufaa yako, rudi kalale, huyo mtu utamuona kesho.’akaniambia.

‘Hapana hiyo ni dharura, atakuwa mgonjwa, ni muhumi niende tu’nikasema nay eye akaguna na kusema.

‘Haya utakuja kukumbuka ushauri wangu, ukirudi hakikisha kufunga mlango wa nje...’akasema na mimi sikumsikiliza kwani akili yangu ilikuwa ikimuwazia huyo mdada, huenda keshatupwa nje , na wahuni wanaweza kumfanya vibaya.

‘Utakuwa ni uonevu, kwanini binti mrembo kama huyu anajizalilisha hivyo...’nikawa najiuliza huku nikiendesha pikipiki langu kwa mwendo kasi, kwani muda kama huo barabara ilikuwa nyeupe, sikuwa na wasiwasi wa kukutana na magari.

Kwa vile kulikuwa sio mbali sana, nikawa nimefika kwenye hilo jengo, nasikia mwanzoni ilikuwa ni nyumba ndogo tu ya wageni,lakini baadaye imeboreshwa na kujengwa kuwa hoteli kubwa, lakini bado watu wanapaita `nyumba ya wageni.

Nilifika hapo, sikupitia mlango wa kawaida, nikapitia kwa nyuma,kwenye jengo hilo kuna mlango wa nyuma, mimi naufahamu sana, unaweza kupenya, na kuingia ndani bila kupitia mlango mkuu.Sikutaka watu wanione, maana huenda kuna watu bado wanasterehe zao, nikaingia kwenye mlango wa nyuma hadi ndani sehemu ninayofahamu watu maalumu hukaa.

Nilishawahi kukaa kwenye hiyo nyumba ya wageni, ni hoteli kubwa tu, ina sehemu za kulaza wageni, na mimi nilipofika hapa kwa mara ya kwanza, nilipanga hapo, kabla sijapata chumba, kwahiyo kuna sehemu za kupenya kama hutaki mtu akuone, na unachotakiwa ni kumpa yule mlinzi kitu kidogo, kama akikuona.

Nashukuru sikuonekana, nikatembea hadi sehemu ambayo nafahamu atakuwepo huyo mdada, lakini kulikuwa hakuna mtu, nikageuka kutaka kwenda kumuona mmoja wa wahudumu wa hapo, kabla sijafanya hivyo, nikaona ujumbe wa maneno.

‘Kama ukifika, nipo chumba 233, nimeamua kulala hapa hapa....’
 Nikajiuliza nifanye nini, maana huo sasa ni mtego, nikageuka kutaka kuondoka na mara jamaa mmoja anayefanya kazi hum ndani akaniona, ananifahamu akanijia na kusema;

‘Mimi ndiye niliyekupigia simu, huyu Mdada, amefanya vurugu na jamaa yake, kumbe hawaelewani siku hizi, mimi nikaona kwa vile kalewa sana, nimpele juu, kwenye chumba cha wageni, ...kwani hawezi kabisa kutembea,...’akasema.

‘Oh, huyo jamaa yake yupo wapi?’ nikamuuliza.

‘Alitolewa na walinzi, kakasirika kwelikweli ...na kama angelikuwa na silaha angeliua mtu, ...’akasema.

‘Sasa kama huyo dada kalala, mimi naondoka, ...maana nikionana naye kwa sasa sitaelewana naye.’ Nikasema.

‘Kwanza nifahamu ni nani atalipia hicho chumba, maana mimi nimetoa msaada tu...tumehangaika kumbeba hadi huko, na bosi akifahamu tumefanya hivyo, bila malipo ya awali, tunaweza kufukuzwa kazi, kwahiyo nakuomba kesho ufike na pesa....mimi nitakudhamini...?’ akasema baada ya kuuliza.

‘Tutaongea kesho, anaweza kulipa mwenyewe,.... , hata mimi nitalipa lakini sasa hivi sikuja na pesa, tufanye kesho, ...’nikasema.

‘Ok, lakini ni vyema ukaenda kumuona,maana alikuwa akikutaja sana kuwa tukuitie...’akasema huku akiniangalia na tabasamu mdomoni, kuonyesha mzaha.

‘Hapana....’nikasema lakini kimoyo moyo, nikaona ni vyema nifike nimuone huyo binti kama yupo salama, lakini sikutaka huyo jamaa afahamu. Kwahiyo yule jamaa alipoondoka kuendelea na shughuli zake mimi kwanza nikaangalia huku na kule kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeniona, na kwa haraka nikapanda juu, hadi kwenye hicho chumba nikagonga, kimiya, nikagonga tena kimiya, nikazungusha kitasa cha mlango mlango ukafunguka....

**********

Mpendwa aliendelea kunisimulia kisa chake,

‘Lakini leo nakuona haupo sawa, kama mtu ambaye hajapata usingizi....’Bosi akaniuliza

‘Aaah, nimechoka tu...’nikasema, huku akilini nikiwazia yaliyotokea jana, sikutaka hata kuyakumbuka.

‘Nikuambie kitu, katika maisha yako penda kujenga ratiba na mpangilia wa nyendo zako, na katika ratiba yako hakikisha unakuwa na sehemu ya kutosha ya kulala, kulala ni muhimu sana kwa afya ya mwanadamu, usipolala, unaweza kujiathiri afya yako, na hata utendaji wako wa kazi ukawa mbovu.

‘Siku hizi nawashangaa watu badala ya kulala, wanakalia kuchat. Wanatumia muda muhimu wa kulala kwa kuongea na wenzao kwenye simu, na wanachoongea hakina tija, kwanza unatumia gharama ya simu kwa hasara, kwanini mtu hujiulize gharama hiyo niliyotumia kwa kuchat, ina marejesho gani yenye faida...’akatulia na kuniangalia.

‘Kama mtu mwenye hekima, jenga tabia yenye manufaa, kuwa kila gharama ina marejesho yake yenye faida, usikubali kupoteza muda wak bure, ambayo ni gharama, muda ni gharama, kama usipoutumia vyema, ukazalisha jambo basi ni hasara, na muda kamwe harudi nyuma, ni kama maji ukiyamwaga aridhini yanapotea, ..muda haurudi nyuma, umri unakwenda mbele, usija ukajutia muda wako ukiwa mzee, hautasaidia kitu...’akaniambia.

‘Kwahiyo muda wa kulala, hakikisha unalala, ili kuuweka mwili wako sawa, gharama ya kulala, inalipwa kwa kuboresha afya yako, usipolala, unaifanya ile gharama isiwe na marejesho kwahiyo ni hasara kwako...sijui unanielewa...?’ akaniuliza pale aliponiona nimeduwaa.

‘Nimekuelewa bosi.....’nikasema huku nikiwa kama mtu aliyezindukana kutoka kwenye usingizi, kwakeli nilikuwa nimechoka, kimwili na kiakili, na moyoni nilikuwa ninajijutia kwa yale yaliyotokea jana, ....


‘Haya, leo kwa vile nina kikao baadaye,ngoja nikuhadithie sehemu ya kisa cahangu, kwani hata hivyo, nakuona akili yako haipo sawa, lakini kazi niliykupa jana umemaliza...?’akaniuliza.

‘Nimeshamaliza bosi, nimeshakutumia kwa barua pepe....’nikasema.

‘Ok, sawa, ...nakumbuka kwenye kisa chetu, tuliishia pale nilipoingia kidato cha pili, kidato hicho nakikumbuka sana, kutokana na machungu yake...’akasema

‘Haya tuendelee na kisa chetu....’akasema

‘Kidato cha pili kilifungua ukurasa mwingine wa maisha yangu, kama nilivyokuambia, mdogo wangu ambaye tulikuwa tunasoma naye, alishajenga chuki dhidi yangu, kwahiyo akishirikiana na mama yake wakawa wananifitinisha mimi kwa baba, na kwa vile baba alikuwa haniamini tena, akawa anaamini kila analoambiwa.

 Siki hiyo niliporudi nyumbani, nikawakuta mama na baba wanaongea, kumbe walikuwa wakinijadili mimi, hawakunipa hata muda wa kupumzika, wakaanza;

‘Haya tuambie huyo mwalimu unayetembea naye ni nani, ...?’ akauliza mama

‘Mwalimu gani ninatembea naye?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Ina maana na wewe unatuuliza swali, unafikiri hatufahamu yote yanayotokea huko shuleni, kumbe kufaulu kwako kote huko ni maksi za hongo,..’akasema baba.

‘Baba mbona mimi sielewi hicho mnachongea, ni mwalimu gani huyo ambaye atakubali kunipa maksi, na mimi sina mazoea na mwalimu yoyote,.....zaidi ya kimasomi darasani...’nikasema

‘Ndio tunafahamu kuwa mahusiano yenu yameanzia kimasomo, na baadaye yamekwenda kimapenzi, unafikiri sisi hatujui ni kitu gani kinachoendelea huko shuleni..’akasema baba.

‘Sio kweli, mimi sina mahusiano na walimu, ....kama ni kuonana nao ni kwenye masomo tu...’nikasema

‘Juzi ulikwenda kwa mwalimu wako wa hisabati ulifuata nini?’ akauliza baba, ni kweli nilikwenda kwake, kwasababu yeye aliniagiza nikachukue madaftari, na wakati huo yeye alibakia shuleni, nikayafikisha, sasa sijui taarifa hizo zilikujaje nyumbani tena kwa kupotoshwa.

‘Ni kweli nilikwenda kwa huyo mwalimu, alinituma madaftari yetu, nikamkuta mke wake..yeye alibakia shuleni...’nikajitetea.

‘Unaonaeeh, ulikwenda nyumbani kwake, na sio mara ya kwanza, na somo hilo unafaulu sana, na mwalimu huyo nasikia yupo karibu sana na wewe. ...’akasema baba.

‘Mwalimu huyo ananifahamu na kunituma kwa vile nafaulu sana somo lake....’nikajitetea.

‘Unaanza kusema mwenyewe, sasa sikiliza, nimeyachunguza haya yote na wewe mwenyewe umenithibitishia hivyo kuwa unafahamiana na huyo mwalimu, adhabu yako utabakai hapa nyumbani hakuna kwenda shule...’akasema baba.

‘Lakini baba mitihani inakaribia na mimi sina kosa lolote, kwanini msiwaulize walimu kama kweli mnayosema ni sahihi...’nikawaambia.

‘Siwezi kupeleka kesi ya tumbili kwa ngedere, hawo hawo ndio mnaofanya nao umalaya, halafu nikawaulize, nimeshasema utabakia hapa nyumbani, hakuna kwenda shule, tuone huo umalaya wako utapeleka wapi..’akasema baba, na mama akasema;

‘Na humu nyumbani hakuna kutoka, utakuwa ukifanya kazi za hapa nyumbani, kutoka kwako ni mpaka mimi nikutume, na utakwenda na mtu...’akasema mama.

Mimi nikaona nitumie mbinu, kwani mitihani inakaribia, na wao nia yao labda ni kunikomoa ili nisifaulu mitihani, na nilifahamu hizo ni mbinu za huyo mdogo wangu, ili nisifaulu mitihani, nilichofanya ni kuwaomba majirani zangu ambao nasoma nao, wanipatie madaftari yao, nikawa naandika nikiwa nyumbani na kujisomea.

Majirani na watu wakaanza kumsema baba kuwa anachofanya si sahihi, ni kumnyima mtoto haki yake, na hata serikali ikijua atachukuliwa hatua za kisheria, hapo akalegeza kamba, na kuniruhusu niende shuleni. Nilipofika shuleni, nikaamua kutulia, na kusoma yale yote waliyofundishwa wenzangu, na mtihani wa taifa ulipokuja nikaweza kuufanya na mungu akanijalia nikafaulu kuingia kidato cha tatu.

Mdogo wangu kwa tabia yake mbaya , hata walimu wakamfahamu, na alishapewa onyo, lakini hakusikia, hata mtihani huo akawa hakufaulu, kwahiyo hakuweza kuingia kidato cha tatu, na kwa utukutu wake, walimu wakaamua kumfukuza, mimi nikaendelea na masomo yangu nikiwa kidato cha tatu, nikijiuliza je wazazi watasemaje maana huyo ndiye waliyemtegemea kama mlinzi wangu.

Maisha ya shule kama unavyoyafahamu, kuna ile hali ya wanafunzi kuwa marafiki, wakike na wa kiume, na mimi nikawa naandamwa na wanaume, kila mmoja akitaka urafiki na mimi, nilijitahidi sana kutokujishughulisha na mambo hayo, lakini kama binadamu inafikia mahali unasema ngoja na mimi niwe na rafiki tu, japo tu wa kuongea naye, kama walivyo wenzangu , sikuwa na nia ya kuwa na urafiki wa mapenzi ya ndani.

Ushawishi huo ukaniteka akili yangu, na marafiki zangu wakawa wananishawishi kuwa ukiwa na rafiki wa kiume, ataweza pia kukulinda na mabaya mengine, kwani wakati mwingine uantembea sehemu yenye hatari, lakini ukiwa na rafiki wa kiume karibu yako, unakuwa na usalama zadi, na mimi hilo nikaliona lina umuhimu wake, japokuwa kwa umri wangu, nilikwa siogpi sana.

Kazi ikawa kumpata rafiki wa kweli, ambaye atanielewa, walikuwepo wengi wanaofaa, lakini sikuwa na mazoea nao ya karibu sana, lakini siku moja, nikakutana na kijana moja ambaye alinionyesha upendo dhati, ilitokea tu, hata siwezi kueleza ilikuwaje, akawa karibu na mimi sana, kila nikiwa mnyonge anakuwa karibu kuniliwaza, na kunipa moyo, nikiwa na shida ya kimsomo, anakuwa karibu name, tunasaidiana.

Kwakeli kijana huyo akaiteka nafsi yangu, na akili yangu ikatokea kumpenda, nikaona huyo anafaa kuwa rafiki yangu wa karibu, kwanza alikuwa sio muhuni, hakuwa kwenye yale makundi mabaya, na katika maongezi yetu,alikuwa akiweka mkazo sana swala la masomo, nikaona huyu atanifaa, kwani hataniharibia maisha yangu. Kwa ujumla nikapmenda sana na niliendelea na masomo yangu vizuri tu huku nikiwa na uhusiano na huyo kijana, wa maongezi tu.

Kumbe mdogo wangu alikuwa anatumwa kuja kunichunguza, na alipogundua kuwa nina rafiki wa kiume, ambaye mara kwa mara nipo naye, akaenda kutoa taarifa huko nyumbani, na kuwaambia wazazi wangu kuwa nina mwanaume, na ameshanifuma nikifanya mapenzi na huyo mwanaume, kitu ambacho sio kweli.

‘Baba mimi nina uhakika nimewaona kwa macho yangu...’akasema huyo mdogo wangu akiwaambia baba na mama.Na niliporudi shuleni, kabla sijaweka vifaa vyangu nikaitwa na kuanza kuhojiwa.

‘Haya tuambie huyo mwanaume wako ni nani?’ akauliza baba.

‘Mwanaume gani baba?!’ nikauliza kwa mshangao.

‘Huyo uliyekuwa ukifanya umalaya naye,..kila siku upo naye, haya bisha kuwa huna mwanaume shuleni ambaye kila siku mnaonekana naye’akasema mama.

‘Hao ni wanafunzi wenzangu, tunakuwa na vikundi vya kujisomea, hakuna lolote baya nimelifanya..’nikajitetea

‘Hivyo vikundi ni vya kwako wewe mwenyewe, na huyo mwanaume, na hizo kazi mlizopewa ni za kufanya mapenzi, mnafundishwa hivyo...’akasema mama kutilia chumvi

‘Mapenzi!!?’...nikauliza kwa mshangao.

‘Unajifanya hujui,..hujui maana ya mapenzi, wakati wewe ni mwalimu wao, nasikia unaongoza kwa umalaya hpo shuleni...’akasema mama

‘Jamani hayo yametoka wapi, kwanini mnawasikiliza watu, kwanini hamfiki shuleni mkawauliza walimu, watawaambia tabia yangu ilivyo, huo ni uwongo...’nikasema.

‘Tatizo lako wewe ni mbishi, muhuni, na unatufanay sisi ni watoto wadogo, huko ulipofika sisi tulipitia, tunafahamu sana ..lakini sisi hatukuwa Malaya kama wewe, tulivumilia hadi tukaolewa, sasa wewe unaona umefika,....’akasema mama, na wakati huo baba alikuwa anasikiliza, macho yalionyesha chuki, hasira, na kama angelikuwa na kitu kibaya angeniumiza kabisa,...baadaye baba akasema;

‘Mnaona wenyewe sasa...mimi nilipoamua huyu mtu asisome mkanina mimi ni mbaya, mkaniatangazia kwa majirani kuwa sipendi maendelea ya watoto wa kike, sasa mumeyaona wenyewe,... sasa haya yamethibitika waziwazi umeonekana ukifanya umalaya wako na huyo mwanaume wako, ...’akasema baba kwa hasira huku akitafuta fimbo.

‘Baba sio kweli, sijawahi kufanya mapenzi na mtu yoyote, huyu ni muongo tu..’nikasema lakini baba hakusikiliza, alichukua fimbo na kuanza kuniadhibu kwa viboko huku nikiwa nimefungwa kamba, kichwa chini miguu juu.

Na hiyo haikutosha chini, kwa pale waliponining’iniza, kichwa chini , miguu juu, wakaweka jiko la mkaa, likiwa karibu sana, joto likawa linanipandia usoni, na hapo nikaachwa nikae hapo hapo, usiku kucha, na ni baada ya kupigwa na fimbo hadi fimbo kukatika katika na kuishia mwilini.

Nililia na kuomba msamaha, japo sikufanya kosa, lakini hakuna aliyenisikiliza, na baba alipochoka kuniadhibu akasema;

‘Sasa nakusimamisha shule kabisa, wewe si unataka kufanya uhuni kunidhalilisha mimi huko shuleni,nasikia umeamua kufanya hivyo, ili unizalilishe mimi, nionekane sijui baba asiyejua kulea watoto, .... sasa mimi nakusimamisha kabisa shule, sahau kabisa kuhusu shule, maana wewe shule ilikuwa sehemu ya kujifundishia uhuni, huko hutaenda tena...’akasema baba kwa hasira.

Iliniuma sana kwa vile ilikuwa imebakia muda mchache sana, wa kufanya mitihani ya kuingia kidato cha nne, na kwa hali ilivyo, ilionekana dhahiri kuwa kweli baba kadhamiria nisiendelee na shule,hata sikujua nifanye nini...

NB: Je niliruhusiwa kufanya mtihani, au ndio ilikuwa mwisho wa masomo yangu,...tukutane sehemu ijayo


WAZO LA LEO:.Unapoletewa taarifa zenye dalili ya fitina na uwongo, usizichukulie kama zilivyo , kwanza zichunguze kabla hujaamua lolote, kwani sio watu wote wanaokutakia mema.

Ni mimi: emu-three

No comments :