Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 20, 2013

Mkuki ni wa Nguruwe-52


Mtoto akaletwa na mama hadi kwenye kiti kilichowekwa maalumu kwa kukaa shahidi anapitwa, mama akakaa akiwa kambeba yule mtoto, hakutaka kumpa yule binti, mama wa huyo mtoto, akamweka wazi ili kila mtu aweze kumuona, na wa kwanza kusema alikuwa rafiki yake mume wangu, akasema;

‘Bro, wewe kweli damu yako ni kali,  huwezi kukataa hapo, utafikiri ni pacha mwenzako...’akasema na mume wangu alikuwa katulia kimiya, hakuinuka, wala kusema neno, aliyeinuka alikuwa wakili wake, ambaye alikwenda hadi pale alipokaa mama, na kumwangalia yule mtu, akatabasamu, na kugeuka, akarudi pale alipokaa, mteja wake, akamnong’oneza kitu.

Mume wangu akamwangalia kwa macho ya kuonyesha mshangao, lakini hakusema kitu, akabakia kimiya, na mwenyekiti alipohakikisha kila mtu kafika kumuona yule mtoto, na ambaye hakuweza kufika alikuwa mume wangu, mume wangu hakuinuka, alibakia pale pale akiwa kainamisha kichwa chini, na mwenyekiti akasema;

‘Mume wa familia ni zamu yako kumuona mtoto, usikatae, maana hilo tumelifanya kutokana na ombi lako, ulifahamu kuwa una mtoto, lakini ukajifanya hujui, ukifikiria kuwa huyo binti kaja peke yake, hana ushahidi, sasa mtoto ndiye huyo hapo, nenda kamuona, je ni wa kwako,...’akasema mwenyekiti, lakini mume wangu hakuinuka, mimi nikainuka na kwenda kumchukua yule mtoto kutoka kwa mama, nikaenda naye hadi alipokaa mume wangu nikamuonyesha mume wangu.

Mtoto alikuwa akifanana na watoto wangu, na ukimwangalia huyo mtoto ni kama unamwangalia mume wangu, amefanana na mume wangu kwa kila hali...nikamsogeza huyo mtoto kwa mume wangu na kusema;

‘Unamuona mtoto anavyofanana sana na watoto wangu, utafikiri mapacha, muone anavyokuangalia, katambua kabisa kuwa wewe ni baba yake..humdanganyi mtu hapa, sura yake haijifichi, anafanana kabisa na wewe...kwa kila kitu, haya niambie, ..’nikamwambia,

Mume wangu badala ya kumwangalia mtoto akawa ananiangalia mimi usoni, na macho ya kutahayari, nilipoona hamuangalii mtoto, ananiangalai mimi tu, nikamuweka yule mtoto mapajani kwake, hakusogeza mikono yake, wala kusem a neno, moyoni nikasema ;ujumbe umefika. Nikamchukua na kumrudisha kwa mama, ambaye alimwangalia mwenyekiti kujua ni nini kinachofuata

‘Haya naona zoezi hilo limekamilika,...’akasema mwenyekiti na mama akamchukua yule mtoto na kwenda kukaa sehemu yake, pale alipokuwa amekaa awali.

‘Bado mwenyekiti, mimi nataka mume wa familia akubali kuwa huyu ni mtoto wake au sio mtoto wake, na kauli yake, ichukuliwe rasmi ndani ya kikao hiki, kama akimkana, basi kwa vile wapo wanasheria hapa, wataandika, mkataba rasmi wa huyo mtoto kuchukuliwa na mtu mwingine, maana hatakuwa na baba...’nikasema.

‘Sawa, ni wazo zuri, na sisi tupo tayari kumchukua huyo mtoto kama baba yake atamkana kuwa sio mtoto wake,..’akasema mwenyekiti.

Wakili wa mume wangu akawa anaongea na mume wangu, na niliona mume wangu akisita kusema neno, na baadaye akasema neno kwa wakili, na wakili akasema;

‘Mteja wangu  kasema hilo ni jambo lake binafsi, asingelipenda mtu kumuingilia, kwasababu kila kitu kipo wazi, anaona hilo la mtoto liachwe kama lilivyo, ataongea na mimi na ni jinsi gani ya kufanya..’akasema wakili wake.

‘Swali hapo ni je huyo ni mtoto wake, au sio mtoto wake, kikao kinataka majibu?’ akaulizwa

‘Ni mtoto wake kwa mtizamo wa haraka, lakini kuna maswala ya kuthibistiha, kufanana sio tija, tutahitajia kuhaikiki kitaalamu zaidi...’akasema wakili na watu wakaguna, maana hapo hakuna cha kuhakiki, kila kitu kipo wazi.

'Huo ushahidi umakamilika, iliyobakia ni je katiba inasema nini, naje ni ni kama familia itaamua kuhusu huyo mtoto, maana hata kama baba yake kakubali kwa shingo upande,lakini sisi kama familia ni lazima tujue hatima ya huyu mtoto kifamilia, kwani kazaliwa ndani ya familia,na hatuwezi kuliachia hivi hivi ...’akasema mwenyekiti.

‘Ni lazima huyo mtoto ahakikishiwe anapewa haki zake zote ikiwemo mama yake,..na hii inadhihirisha sasa tabia ya mume wa familia, na inavyoonekana ni kama vile bado ana watoto mwingine, mimi sijui,, labda hilo tumuachie mke wa familia,...lakini kwa huyu mtoto, kwa vile imeshathibitika hivyo, tunataka kikao kiliweke kisheria zaidi, na mtoto huyu atambulike rasmi kuwa ni wa mume wa familia,, au sio jamani?' akauliza mwenyekiti, na kabla watu hawajajibu akasema;

'Kama wao wanahitaji kuthibitisha kitaalamu, sisi hatupingi, lakini akumbuke kuwa kuna matendo alimfanyia huyo binti, ...hayo ni dhamira, ni kama unapokwenda kupanda mbegi shambani unategemea nini, kwahiyo sheria nayo ni lazima ichukue mkondo wake, hilo nawaachia wanasheria, sis hapa tumekamilika, hakiharibiki kitu hapa..’akasema mwenyekiti,na kuniangalia mimi, na mimi nikasema;

‘Huo ulikuwa ushahidi mmoja katika madhambi yake mengi, kuna mtoto mwingine ambaye hajajulikana, naona sasa ni zamu ya mume wangu kuongea mwenyewe, kwasababu anafahamu hilo, na anafahamu huyo mwingine kazaa na nani, mimi naona ni muda wa yeye kujirudi, ili tusipoteze muda....’nikasema

‘Haya mume wa familia, nasikia wewe ni kidume, unaacha watoto kila unapopita, nasikia una mtoto mwingine, ni nani, kikao hiki kinataka kumfahamu, ..funguka baba’akasema mwenyekiti, na wakili akawa anaongea na mteja wake, na wakawa kama wanasigishana, na baadaye wakili akasema;

‘Mteja wangu anasema hayo ni mambo yake binafsi hataki kuyaongea, hapa,..na hata hivyo, yeye hana mtoto yoyote mwingine kama mnavyo dai nyie, hawo wote wanaoletwa hapa ni shinikizo, na inakbidi akubali tu,...lakini huo sio utaratibu mzuri, ....kwahiyo kwa swala la watoto, analiomba lisitishwe, tuongee mengine, yeye anahitaji muda wa kulifanyia kazi...’akasema wakili.

‘Kikao hiki kinatoa madhambi ya mume wa familia, ambayo yeye aliyakana toka awali, kama yeye angekubali kuwa kuna madhambi yakafanya, akayasema japo kwa muhutsari tu sisi tungemuelewa, tukatafuta jinsi ya kumsafisha, lakini kwa ujeri wake, akaona sisi hatujui, anaweza kutuvunga akafanya apendavyo, sasa hatutayaacha madambi yake yapite hivi hivi, yatatajwa yote, ...’nikasema.

‘Hivi wewe unaposema nina madhambi, wewe ni mungu, unafahamuje kuwa nina madhambi, huwezi kunihukumu kihivyo, hayo ni makosa tu, yoyote anaweza kuyafanya, na kwanini unasema kuwa na mtoto ni dhambi..?.’akasema mume wangu kama ananiuliza huku kakunja uso kwa hasira.

‘Swala hapo ni je huyo mtoto umempataje,mtoto hana kosa, ila taratibu za kumpata huyo mtoto ni zipi,....hebu tuambie, huyo aliyeletwa hapo umempata kwa njia gani, sio kwa njia ya kumbaka, hiyo sio dhambi, ..nakuuliza hiyo sio dhambi, au wewe dhambi unaielewaje, kuna  huyo mwingine, hatujui umempataje huenda ni kwa kubaka hivyo hivyo, huenda hiyo ndio tabia yako ya kubaka, na ujue, uliyafanya hayo ukiwa wewe ni mume wa mtu, ukaikana ndoa yako kivitendo, ukanisaliti, je hiyo sio zambi?’ nikamuuliza.

‘Sema unavyoweza wewe, ..mimi kwa sasa sijali amueni mtakavyo, ila nasema ndoa haivunjiki, na haki zangu zipo pale pale...kama wewe umakuwa mungu wa kuhukumu watu, sawa, lakini kila mtu ana makosa yake, ...’akasema kwa sauti ya kukerwa.

‘Hayo yatafuata baadaye kama unavyodai kuwa ndoa haivunjiki, na haki zako zipo, sawa tutaliona hilo, hapa tumekamilika, sheria itasema, na hatutako hapa mpaka kieleweke, ... sisi tulitaka tushirikiane na wewe kama ndugu, tuakuomba na kukubembeleza, ili hili tatizo tulimalize kindugu, lakini wewe ukalipinga, na ukajitoa mapema, kwahiyo wakili wako ana kazi kubwa ya kufanya, kama ana ubavu wa kugeuza hayo makubaliano yenu, sisi hatuna shaka,.....’akasema mwenyekiti.

‘Makubaliano gani mnayoyasema, mimi hayo makubaliano siyatambui, nilishasema toka awali kuwa ninachokitambua mimi ni huo mkataba niliokuwa nao mimi, huo mwingine sijui umetoka wapi...’akasema kwa hasira

‘Naona wewe hujui sheria, kwa kukusaidia tu, wewe kaa uongee na wakili wako vizuri, atakushauri vyema kuhusu sheria, maana hapo unavyoongea, unaongea kama mtu asiyesoma, mkwe, usiniangushe...’akasema mwenyekiti, na kumfanya mume wangu amuangalie mkwe wake kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Tunaendelea na jingine, mke wa familia ulisema dhambi alizokufanyia mume wako ni nyingi, na tunaona kuwa yeye sio mtu wa kukubali na kukiri kosa, sasa ili tusipoteze muda, labda tukuulize, kuna dhambi gani nyingine, ambazo, amekiuka, na anahitajika kuwajiba nazo, au tumuulize mwenyewe muhusika, kuwa yupo tayari kukiri makosa yaliyobakia, ili tusipoteze muda?’ akauliza mwenyekiti.

‘Mimi sipendi kuyaongelea machafu yake,lakini yeye ananilazimsiha nifanye hivyo, kama nilivyosema, awali mume wangu ni mzinzi, ana tabia chafu, ambayo haivumiliki, inasadikiwa kuwa ana mtoto mwingine nje ya ndoa zaidi ya huyo aliyempata kwa kubaka, sasa ningelipenda akiri mwenyewe hilo, ili nimuone kuwa kweli sasa kawa ni muungwana, na yupo tayari kuwa raia mwema, kwa jamii, kwani yote tuliyomshukutumu nayo yamethibitika kuwa ni kweli,  je na hili la kuwa na mtoto mwingine nje, atalikataa...nataka nisikie kauli yake mwenyewe?’ nikauliza, na mwenyekiti akamwangalia mume wangu.

Mume wangu alipoona watu wapo kimya wanamuangalia yeye, kwanza akamuangalia wakili wake, na wakali wake akamuonyesha ishara kuwa aongee, na hapo mume wangu kwa hasira akasema;

‘Sina mtoto mwingine,...nyie lengo lenu ni kunizalilisha, sasa mimi nasema sina mtoto mwingine, na fanyeni mnalotaka....’akasema mume wangu kwa hasira

‘Una uhakika na hilo, maana sasa tukianza kutoa ushahidi mwingine, hakuna kurudi nyuma sisi tutachukulia kuwa wewe ni jeuri, hututhamini, na kwahiyo kama wanafamilia, tutahukumu, bila msamaha...’akasema mwenyekiti.

‘Nimeshawaaambia kuwa sina mtoto mwingine, kama yupo Malaya anayedai hivyo aje kama livyofanya huyo,wote hawo ni malaya tu, wenye shida ya pesa, hakuna kingine ...’akasema na kila mtu akawa kimiya kwa kauli yake hiyo chafu.

‘Kwanini unazungumza hivyo?’ mwenyekiti akamuuliza

‘Nimechukia sana, kwani kinachoendelea hapa ni kunizalilisha, ili nionekane mbaya, na mwisho wa siku mfanye mnavyotaka, mimi nimechoka, na amueni mnalotaka, lakini kauli yangu ni ile ile, mimi sikubali kuvunja ndoa yangu,na wala sikubali kuachia chochote, kwa ajili ya hawo ma-malaya, waliojielta kwangu...’akasema na kauli yake ilikatishwa, kwani kuna mtu aligonga mlangoni, na sote tukageuka kuangalia.

Mlango uligongwa tena, na ukafunguka, akaingia rafiki yangu, akiwa kambeba mtoto wake, akasimama kati kati ya mlango na kusema;

‘Hiyo kauli chafu imenikera, ...unafikiaje kutuita sisi Malaya, wewe ambaye uliyetembea na wanawake wengi tutakuitaje, au unataka tuseme kila kitu, sasa mimi nimefika, nasema hivi huyu hapa ni mtoto niliyezaa nawe,....’akasema rafiki yangu, ...na watu wakaguna.

‘Hebu kidogo, naona umetuingilia huo sio ustaraabu, naomba utulie tufuate utaratibu...’akasema mwenyekiti.

‘Hapana mwenyekiti, mimi naona mnapotez a muda wenu na huyu mtu , hatutaweza kukaa kimiya tukisubiri huyu mtu aseme ukweli, ambao hatausema, ni mwongo,mzalilishaji mbakali na pia anahusika na uuwaji, tunapoteza muda wetu bure, tuna mambo mengi ya kufanya, na kama ulivyosikia, amefikia hatua ya kuanza kututukana...’akasema rafiki yangu.

‘Mimi nataka anijibu swali langu kuwa ni nani Malaya, yeye aliyetembea na wanawake wengi huku ana ndoa yake halali na sisi ambao kwa hadaa zake alituzalilisha, ..ni nani Malaya?’ akauliza rafiki ynagu kwa hasira.

‘Kwani nilikuja nikakushika kwa nguvu,....wewe ulijileta mwenyewe kwangu, ukidai unataka mtoto, au umesahau, usitake nikakuumbua bure hapa...’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Wewe mwanaume, mimi nilikuja kwako nikakuambia nataka mtoto, sio kwamba mipombe yako ilikutuma na kunitilia dawa ya kulevya kwenye kinywaji kwa siri, nikazidiwa, ukanifanya ulichonifanya huko sio kubaka, wewe ni mbakaji, na sio mara moja, kama wewe ni mwanaume kweli kwanini utumie mbinu hiyo, ulishindwa kuongea.....na ole wako, chunga sana kauli yako, na ninakuambia yale yote uliyoyaandikisha kwa ajili ya huyo mtoto ninayataka yote, nimeshayawakilisha kwa wakili wangu...’akasema rafiki yangu kwa hasira.

‘Kama una wakili wako na mimi nina wakili wangu, usinibabaishe, ...hukutaka kukubali matakwa yangu toka awali, sasa unakuja kwa nyodo, hupati kiti hapa, nimeshakuambia,na mtoto...’akasema na wakili wake akamkatisha na kumtuliza.

‘Ndugu mwenyekiti samahani sana, sikutaka kuyasema haya, lakini itanibidi niseme kila kitu, ili mumuone huyu mtu alivyo mbaya, nakiri kuwa kweli nilimkosea rafiki yangu, lakini ni lazima mwisho wa siku tumtambue mbaya wetu ni nani...niwaambia ukweli, huyu mwanaume hapa alikuwa ni nyoka mliyekuwa mkimfuga wenyewe, sasa ni muda wake kumtoa shimoni, apewe kinachomstahiki, mimi nitawaambia kila kitu ...bila kuficha, nilishaahidi kuwa nitasema kila kitu siku ikifika, naona sasa muda umefika...’akasema rafiki yangu akiwa kasimama kati kati, huku kamshikilia mtoto wake..

‘Muongo mkubwa wewe, huna jipya, umemsaliti rafiki yako,sasa unataka kujikosha, hupati kitu kwangu na kwa rafiki yako umeharibu,umalaya wako umekuponza ....’akasema na mwenyekiti akasema

‘Hebu tutulieni kwanza, na rekebisheni hizo kauli zenu, kwani mwisho wa siku tutahitaji uhalali wa kuyatamka hayo maneno, huwezi kutamka neno la kashifa kwa mwenzako kama vile unatamka neno la kawaida, tutakuhitaji kulithibitisha hilo,kwasababu umeshamuhukumu mtu kuwa yupo hivyo , wakati huna ushaidi.... kwanza nataka tutulie, maana naona mambo yanajileta yenyewe, tunakuomba ndugu uliyeingia, utulie kwanza, ili tufuate utaratibu...’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, naomba mnipe hii nafasi , niongee, nafahamu mna utaratibu wenu, lakini naona kuna mengi yalitokea, na mimi imefikia kuonekana mbaya, hata kwa rafiki yangu, na ubaya zaidi uakpandikizwa juu, yangu, kuna marehemu Makabrasha kauwawa, na nashangaa, naambiwa mimi nilihusika, wakati huyo mnayemuita mume wa familai siku hiyo alikuwepo, hebu muulizeni vizuri siku hiyo alifuata nini kwa Makabrasha...’akasema na watu wakawa wametulia kimiya.

‘Sasa nataka nitobe kila kitu, ili ajue kuwa kachokoza kule kusipochokozwa, ...nimefika hapa na kukamatishwa watoto wa kihuni wanifanyie unyama, eti kwa vile nimetembea na mume wa mtu, huyu mtamuita mume wa mtu, mtu ambaye alishavunja ndoa yake, siku nyingi,...sasa naona nikae hapo, nianze kusema kila kitu, na mwisho wake, tutaona ukweli upo wapi, kuwa mimi ni Malaya au ni yeye...’akasema na kwenda kukaa kwenye kiti cha mashahidi.

‘Mke wa familai unasemaje, tuendee naye au una shahidi mwingine?’ akaniuliza na wakati huo nilikuwa nimeshikwa na hasira, sijui kwanini nikimuona huyo rafiki yangu, ninakuwa hivyo, nilitamani wale wahuni waje, wamfanyie ubaya mbele ya watu wote hawo, nikamwangalai huyo rafiki yangu kwa macho ya hasira, nikamwambia mwenyekiti.

‘Nataka huyu mtu asema ukweli wote, na haki itendeke, kwani wote lao ni moja, huyu na mume wangu, wote ni wasaliti, sina msamaha nao, ....’nikasema

‘Hata wewe usijitete, na kujiona msafi, una mapungufu, kwani isingelikuwa wewe nisingeliingia kwanye ubaya wa mume wako,..lakini hayo kwangu nimeyasahau, mtu wangu ni huyu, uneyemuita mume wako, nataka leo akitoka hapa, anaelekea jela, kwani hastahili kuishi kwenye maeneo ya raia wema, nina ushahidi wa kutosha, wa kumweka, ndani...’akasema rafiki yangu.

‘Usinitishe wewe, ....toa huo ushaidi wako, wewe ni Malaya tu...’akasema na rafiki yangu akatabasamu na kusema,

‘Utaona....’

NB: Haya mambo yamekwenda haraka, lakini ndivyo ilivyotokea, tuwepo kwenye sehemu ijayo,


WAZO LA LEO: Tuchunge sana kauli zetu tunapoongea, kuna maneno yakitamkwa mbele za watu, yanakuwa na picha mbaya, lakini kuna watu ni wepesi  kuyamtamka hayo maneno kama vile ni maneno ya kawaida, kwa lugha sahihi, yanaitwa ‘lugha za matusi’ . Kuna baadhi ya watu wanayatuma haya maneno bila kujali anayamtaka wapi, na kwa nani, na anamlenga nani, baya zaidi, wengi wanaozalilishwa kwa maneno hayo ni akina mama, ...iweje ugombane na mtu, ukimbilie, kumtusi mama yake, je  huyo mama kakukosea nini, ...tuchunge sana ndimi zetu, kwani tunajilaani wenyewe.

Ni mimi: emu-three

No comments :