Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, December 31, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-56Niliyoyakuta Dar, yalinikatisha tamaa, kwani sikutegemea kuwa kuna watu wamefikia kiwango cha hali cha uhalifu wa kimataifa na wanafanya blla kuogopa, niliyotendewa ni makubwa, ni kama yale niliyokuwa nikisoma kwenye visa au kuangalia kwenye picha, sikuamini, maana nilipofika tu, nikiwa natoka chumba cha kukaguliwa mizigo, wakati najiandaa kutafuta usafiri, mtu mmoja alikuja nyuma yangu na kunishikisha kitu kwa nyuma, nilihisi maumivu, kilikuwa ni kisu kikali, akaniambia

‘Fuata tutakavyokuelekeza, kuna taksi ile pale mbele yako, mlango wake upo wazi, ingia, na mizigo yako tutakuchukulia, hatutaki kukuumiza...’akaniambia, na baadaye akanipa bahasha, akaniambia

‘Fungua hiyo bahasha...’kwa mikono ya kutetemeka, nikafungua, nikaona picha zile zile nilizozoea kutumia, akaniambia

‘Siku hizi hapa bongo kuna magazeti mengi yanazitafuta picha kama hizo, hatutaki kukuharibia jina lako, na kukuharibia maisha yako ya baadaye, sisi tunataka kulijenga jina lako uwe karibu na wenye pesa, kwahiyo timiza masharti yetu madogo tu, tutakuwa sambamba...’wakasema na mimi sikutaka kubishana nao, nikafuata kama wanavyonielekeza, tukaondoka hapo hadi sehemu nyingine, sio mbali sana na hapo uwanja wa ndege.

‘Tumefika mpendwa, tunachokuomba ni kuwa sisi ndio tumekuita uje, hatutaki wewe uonane na mtu mwingine yoyote bila idhini yetu, kwahiyo tutakupeleka mahali maalumu utakaa hapo, na kila unachokitaka utakipata, ...’akasema na tukaingie kwenye jengo moja, jengo hilo nilikuja kugundua kuwa ndio ofisi anayotumia Makabrasha, kwenye lile jengo kuna sehemu ya chini ya ardhi, lakini hakuna mtu anayefahamu .

Nilipelekwa sehemu hiyo, na kuingizwa kwenye chumba chenye kila kitu, ...ni chumba cha kifahari, nikaambiwa hapo nitakaa mimi hadi nitakapopewa maagizo mengine...’wakasema na wakaondoka.

Kitu cha kwanza nilitaka kujua ni nani yupo nyuma ya haya yote, sikujua ni nani kwa muda ule,.japokuwa kwa mtizamo wa haraka, toka awali, nilijua kuwa anayefanya haya yote ni Makabrasha, kutokana na maaelezo ya watendaji wangu, lakini sikuwa nimeamini kuwa huyu mtu anaweza kufikia kufanya jambo la namna hiyo, ...nikatulia na mwanangu, maana mtoto wangu alikuwa kila kitu. Sikutaka kabisa kuanzisha harakatai zangu, ningeliweza kufanya hivyo, lakini sio kwa hali kama hiyo na mtoto mdogo.

Ilipofika muda fulani, nikasikia mlango ukifnguliwa, na akaingia dada mmoja akiwa kabeba vifaa, alikuwa kafunga uso wote, haonekani sura, kaacha  sehemu ya macho tu, inaonekana ni muhudumu, alibadili vifaa, vilivyotumika, na kuweka vingine, hakuniangalia, alifanya hiyo kazi, na alipomaliza, akanijia, na kuniuliza

‘Una shida yoyote?’ akaniuliza

‘Ndio , nataka kutoka nje...’nikasema

‘Mhh, fuata maagizo , kama ulivyoambiwa, mpe mtoto hiki hapa achezee...’akanipa kitoi, na mimi nikakichukua kwanza kukikagua, na yule dada akaondoka, na mimi nikawa nimeshikilia kile kitoi, nikawa nakitingisha tingisha, mara kikaachia na kubomoka, na ndani yake kukadondoka kikaratasi, sikufanya haraka kukiangalia, nikawa nafakirekebisha, had kilipokuwa sawa, nikampa mtoto akawa anachezea, mimi nikachukua gazeti kusoma, na baadaye lile gazeti nikaliweka kwenye kile kikaratasi, nikaliinua pamoja na kile kikaratasi na kukifungua, kilikuwa na maneno machache tu;

‘Tupo pamoja..’ nikakigeuza nyumba nikaona namba ya simu, nikaikariri halafu nikakitafuna kile kikaratasi, nikaona nipate usingizi kidogo, maana nilikuwa sijapata muda wa kupumzika, na sikuwa nafahamu ni jambo gani litafuta baadaye, sikutaka kuhangaika kupiga simu, maana nilivyolikagua kwa haraka, kwa juu niliona kifaa cha kuchukulia matukio, kwahiyo kila ninachokifanya humo ndani kinaonekana, nikawa makini kwa hilo.

Nililala kwa muda wa nusu saa hivi, nikahisi sipo peke yangu, sikufahamu huyo mtu aliingia muda gani, lakini nilijua kabisa kuna mtu mwingine, sikuwasha taa, nikasubiri, mara nikahisi kitanda kikiguswa, nikajiandaa tayari kwa mapambano, nikahisi mkono ukinipapasa sehemu ya tumboni, nikatulia nione lengo la huyu mtu,..

Aliposogeza mkono chini, kwa haraka, nikaudaka mkono wake, na kuupinda kitaalamu, na mimi kwa haraka nikaruka kitandani huku mtoto wangu akiwa tayari mikononi mwangu, nikasimama, na wakati huo huyo mtu yupo chini sakafuni, analalamika kwa amumivu.

‘Aaah, umeniumiza, ...nini unafanya wewe...’sauti ikaniuliza

‘Kwani wewe nani na lengo lako ni nini?’ nikamuuliza

‘Usijali sikuja hapa kwa nia mbaya, kwanza sina muda wa kufanya lolote na wewe, nimeshachoka, nilikuja kukusalimia tu, nikawa napendezewa kushika mwili wako uliojengeka kimazoezi, una mwili mzuri sana...’akasema

‘Nataka kupumzika, huoni nimemsumbua mtoto wangu, ni nani wewe, washa taa, nikuone...’nikasema

‘Wala usisumbuke kuwasah taa, nimekuja kukusalimia, tu, kesho asubuhi nina kikao na wewe, ajenda ni moja, kukubaliana na hayo tuliyoyapanga, wewe utatusaidia kutupa taarifa chache, na huenda tukakutuma mahali, ukimaliza kai yetu, keshokutwa unarudi kuendelea na masomo yako....’akasema.

‘Hujanijibu swali langu, wewe ni nani/’ nikamuuliza

‘Utanifahamu kesho, samahani kwa usumbufu, nashukuru kwa kuwa mvumilivu, ukifanya hivyo, na kufuata masharti, ukatii yote tunayohitajia, hutapata taabu, na haya tunayafanya kwa ajili yako, na familia yako,...mwenyewe utaona, kwa hivi sasa lala,..usijali..’akasema na kuondoka, sikutaka kujishughulisha zaidi, nikarudi, na kulala na mtoto wangu, hadi asubuhi.

Asubuhi na mapema, nikaingia bafuni, na kuoga, na kubadili nguo, niliporudi pale nilipomuacha mtoto, nikakuta mtoto wangu hayupo,, nilimuacha akiwa amelala, ..hapo wakawa wamenichokoza, nikavaa nguo haraka na kuanza kutoka, na kabla sijafikia mlango, sauti ikasema;

‘Mtoto wako yupo salama, atapata kila kitu anachohitaji, cha muhimu ni kufuata masharti yetu, vinginevyo, mtoto huyu anaweza akawa historia kwako....’sauti ikasema,hapo, nikasimama kwa muda, nkijilaumu kwanini niliwaamini, na kumuacha mtoto wangu pale kitandani, ilikuwa muda wa majozi kwangu maana sikutaka mtoto wangu apate shida, awe mbali na mimi, nikatulia huku nikimuomba mungu, ili mtoto wangu awe katika mikono salama.

Muda niliuona ukienda pole pole, ilipofika saa mbili, nikaja kuchukuliwa hadi juu, kwenye chumba kama ofisi, nikaambiwa nikae hapo nisubiri, mara akaingia mtu,akiwa kashika faili, ni kabrasha lenye karatasi nyingi, akasogea pale nilipokaa, akasema;

‘Nimeleta huu mkatana, ninakupa nusu saa uusome, halafu unatakiwa kuweka sahihi yako kwenye sehemu stahiki, natumai, unaelewa wajibu wako, ...’akasema na kuniwekea hilo faili mbele yangu, nikalichukua na kuanza kufungua ukurasa mmoja mmoja, nikawa nasoma;

Ulikuwa mkataba wa hiari, ambao mimi nakubali kuwa nitafanya kazi, chini ya kampuni iliyotajjwa jina, na nitakuwa nikimtii kiongozi wake, hapo kwenye kiongozi wakaacha nafasi , hakukuweka jina la huyo kiongozi. Sehemu nyingine, inataka mimi nikubali kuwa mtoto huyo ana baba yake, jina , sehem u ya jina hakuna kitu, mbele yake, ikasema,baba huyo ndiye mwenye mamlaka na huyo mtoto, na mtoto atapata haki zake zote kutoka kwa baba huyo...

Kukawa na maelezo mengine mengi, ya hisa, na mimi nikapewa sehemu ya hisa, kama nitakubali yote, na kutimiza maagizo yote, na sitamtambua mtu mwingine yoyote kama bosi wangu zaidi ya huyo aliyetajwa hapo,....

Nikamaliza, kusoma, nikainua kichwa kumuangalia huyo mtu aliyeleta hayo makabrasha, nikamuuliza

‘Mtoto wangu yupo wapi?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui maswala ya mtoto, kazi yangu ni kukuleta hiki nilichokuletea kama umemaliza kusoma, weka sahihi yako, tumemaliza kazi...’akasema

‘Mimi siwezi kuweka sahihi yangu mpaka nimuone mtoto wangu...’nikasema na kabla sijatulia mara ukutani kukatokea maandishi, kama vile unaangalia runinga, na mara mtoto wangu akatokea, akiwa kabebwa na mwanamke,a kimpa maziwa ya mpira, na mtoto wangu alikuwa katulia

‘Natumai umemuona mtoto wako..yupo salama,...’akasema na mimi nikachukua peni, na kuweka sahihi yangu, hiyo ni sahihi maalumu, ambayo, naitumia kwa nafasi kama hizo, huwezi kuona tofauti, lakini mimi mwenyewe nafahamu wapi nimebadili,...nilipomaliza kuweka sahihi, nikaweka peni chini, na yule mtu akanishika kidole gumba, na kukiweka kwenye wino, akaweka kidole changu kwenye karatasi, hakufahamu kuwa mimi nilishajiandaa kwa hilo, hiyo alama itakayoonekana hapo,siyo yangu.

‘Nafikiri tumemaliza, subiri kuna sehemu unatakiwa kwenda...’nikaambiwa, nikasubiri kidogo mara akaja mtu na kuniambia nijiandae, kwani tunatoka nje ya jengo, na ninatakiwa kufuata masharti kama namjali mtoto wangu.

‘Hivi nyie kweli mna ubinadamu, kuna mtu anaweza kukaa masaa yote hayo bila kuonana na mtoto wake, mimi sitaweza kufanay lolote mpaka nimuone mtoto wangu, nimguse...’nikasema na mara kwenye ukuta nikaonyweshwa mtoto wangu, akiwa kashikiwa kisu kooni...

‘Shsssiti...’nikasema, sikutaka kusema jambo, nikaondoka na hawo watu nikiwa njiani nikaambiwa nakwenda kumsalimia mgonjwa,

‘Mgonjwa gani..?’ nikauliza

‘Mzazi mwenzako...’nikaambiwa na sikutaka kusema zaidi, na hapo nikapelekwa hadi alipokuwa kalazwa, mume wa familia, nikaongea naye, na sikutaka kumuuliza mengi, japokuwa yeye alikuwa akiniuliza maswali mengi, na mwisho wake nikamuuliza

‘Wewe upo kundi moja na hawo watu waliomteka nyara mtoto wangu?’ nikamuuliza

‘Eti nini, wamamteka nyara mtoto wetu, haiwezekani, ngoja niongee nao...’akasema akichukua simu, na mimi nikamzuia na kusema;

‘Haina haja, ila nakutahadharisha, kama upo kundi moja na hawo watu, ujue, kitakachotokea baadaye hutaweza kuamini kuwa mimi ndiye huyu unayeniona hapa...hili lililotokea jana na leo, sitalisahau maishani, na litakuja kulipwa kwa gharama kubwa sana, ...’nikasema

‘Mimi sikuelewi unasema nini, mimi nimesikia umekuja mara moja, kwa ajili ya makubaliano, na umekuja ili ujue hatima na mtoto, na mimi nimekubali kuwa nipo tayari kuwajibika kwa ajili ya mtoto, nimeona umekubali na kuweka sahihi yako, sasa tatizo lipo wapi...’akasema

‘Tatizo ni kuwa nyie hamnifahamu kuwa mimi ni nani...sawa mimi sina zaidi, nashukuru kuwa nimekuona, na naona umepona, tofauti na nilivyoambiwa ...’nikamwambia na yeye akawa kama kakumbuka jambo, na kujiweka kitandani kama mgonjwa aliyezidiwa.

‘Mhh, kumbe ndio janga yako eeh...’nikasema

‘Janja gani....mmh, ulisema nini umeshajifungua eeh...’akawa anaongea kama mtu asiye kuwa na kumbukumbu, au aliyechanganyikiwa, nikatabasamu na kugeuka kuondoka, na yeye akasema;

‘Chunga ulimi, macho na masikio yako, ...kwa ajili ya mtoto wetu,...usiondoke bila kuniaga...’akasema na mimi sikugeuka kumwangalia nikatoka nje, na kusubiri maelekezo mengine. Nikaona nifanye kila wanachokitaka wao , ilimradi mtoto wangu awe salama, kwahiyo nilifuata kila wanachokitaka, bila kupinga, hadi siku ya kuondoka ilipofika.

Siku ambayo kesho yake naondoka, nikaona nisiwe mjinga, nikaona nifanya jambo, alipokuja yule muhudumu, nikamuuliza;

Hili jengo linamilikiwa na nani?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui...’akasema na akamaliza shughuli zake akaondoka, nikachukua bakuli iliyokuwa na mboga, ile mboga nikaimimina sehemu nyingine, niliona uzito wake, unaweza kufanya hicho ninachotaka kukifanya, nigaukwa kwa haraka sana nikairusha ile bakuli hadi kwenye kile kitufe nilichojua ni cha kuangalia matukio, kwa shabaha ile kikavunjia ...

Nilitarajia mlio wa tahadhari, lakini sikuusikia, nikaona nimefanikiwa jambo muhimu, kwa haraka nikapanda juu, na kuvuta nyanya zake, kuhakikisha hakuna mawasiliiano kwenye hicho chumba, nikatoka nje, na kuanza kutembea bila kujua nielekee wapi, nikaiachia hisia yangu iniongoze, nilipanda hadi juu, nikaanza msako, wa kutafuta wapi mtoto wangu amewekwa.

Wakati napita kwenye chumba kimoja, nikasikia watu wakiongea, nikatega masikio, na hapo ndio nikasikia sauti ya kiume na ya kike wakibishana jambo, mwanzoni ilikuwa kama ugomvi na baaaye wakatulia na kuongea sauti ya masikilizano.

‘Nimeshakufanyia kila kitu unachokitaka kwangu ni nini mbona unanifanya kama mtumwa wako, ...’sauti ya kike ikalalamika.

‘Ndio wewe ni mtmwa wangu ulielewe hilo, japokuwa nafahamu kuwa nakuonea, lakini ni kwa vile wakati mwingine hutaki kutiii amri yangu, ninachotaka kutoka kwako ni utii, nikitaka hiki au ufanye hivi, ni mari moja, ...hata hivyo nisamehe, leo akili yangu haijawa sawa,...nisamehe mtumwa wangu eeh,..pindi hivi utakuwa huru, ..ngoja mambo yakamilike, usiwe na wasiwasi, tutayamaliza haya kwa amani kabisa, kwani unataka nini kutoka kwangu...’sauti ya kiume ikauliza.

‘Nipe hizo kumbukuzi zote za mapicha machafu uliyochukua kwangu na kwa watu wengine, niyaharibu, ili watu wawe na amani na ndoa zao...’ ikasema sauti ya kike.

‘Hilo lisikutie wasiwasi, ndoa zenu zitakuwa na amani kama nyie wenyewe mtajituliza na waume zenu, tatizo nyie mumekimbilia kuolewa kwa kutaka mali, na sio upendo, kwahiyo hilo sio kosa langu , ama kwa hizo picha, video, nitaviharibu, mbele yako, wewe nipe mud animalize kazi yangu, sitaki tena kukaa na hivyo vitu, kazi kubwa nimeshaimaliza...’ikasema sauti ya kiume

‘Ila badi kitu kimoja, cha muhumu sana, mimi kazi zote nimezifanya mimi, hamjanilipa chochote cha maana, ..nataka malipo yangu kama tulivyokubaliana...’akasema

‘Malipo gani zaidi, ..pesa umelipwa tena nyingi sana na ukadai upewe hisa, ukapewa vyote hivyo unaona havitoshi, ama kweli mchoyo hatosheki, shetani hashibi madhambi, hata siku moja,lakini ukumbuke mwisho wa mabaya ni kuumbuka tu,na wewe naona mwisho wako unahesabiwa,...’sauti ya kike ikawa inaongea kwa kulalamika.

‘Naelewa hayo sana, ndio maana njiandaa kuachana na tabia hiyo, nikikamilisha hili, natulia, ....nitakuwa na haja gani ya kuhangaika, wakati kuna kampuni, zainazalisha, ....tatizo anayenichelewesha ni huyo mpenzi wako, akija kesho, kama hanielewi, ataniona mbaya...’akasema na kukawa na ukimiya kidogo.

‘Naona kama kule kwa bosi wako hakuonyeshi kitu, au ...nitaangalia baadaye huyo hana ujanja, mtoto yupo kwenye himaya, yangu, ....’akasema.

‘Huyo mnamsumbua bure, yeye ni mzazi, na sioni umuhimu wake, kwenye mambo yenu, muachieni akasome, na mpeni mtoto wake, hana tatizo na nyie...’sauti ya kike ikasema.

‘Wewe utakuja kuona umuhimu wako, ila kumbuka, akija mpenzi wako...., unajua hajasaini ule mkataba wa makubaliano kati yangu mimi na yeye, nilimwambia akakubali, na hajui kuwa mimi ndiye namsaidia,hebu angalia, pale alipo haumwi, lakini nimeshaongea na docta, ili ionekane anaumwa,kwa manufaa yake..., ...‘akasema.

‘Utahangaika sana, lakini hawo hawo unawasumbua, ..hasa huyp docta, na wengineo, watakuja kuwa mashahidi siku ukiwa umesimama kizimbani...’ikasema sauti ya kike.

‘Thubutu, labda kizimba cha kaburini, lakini nikiwa hai hivi hivi, hanipati mtu, ni nani atayemfunga paka kengele, wakati hao hao wanausalama wana madhambi kibao, wote nimewaweka hapa, kwenye mkono wangu, akijaribu kunishika mtu, naweka madhambi yake mbele,....wacheza na mimi, ...sasa hivi dunia ni yangu...’sauti ya kiume ikasema.

‘Haya we jidanganye, ....na huyo docta naye ulimpatajemadhambi yake, maana namuona ni mtu mtulivu sana,...?’ sauti ya kike ikauliza.

‘Hawo unaowaona watulivu, ndio balaa, wana mambo yao ya chi ni kwa chini, na wakati mwingine ni uwoga tu, nilimkamatisha kabinti kamoja karembo, ...huyo binti akafika kwake, kwa matibabu, akamrembulia mara mbili, docta, akaswajika, ...vyombo vikanasa tukio, wacheza na mimi, akaingi akwenye anga zangu, nikamweka kwenye anga zangu, alipoona uchafu wake,akasalimu amri, unacheza na mimi...kwahiyo mpenzi wako, anaweza kufanya apendavyo, kila kitu kipo shwari, niamini mimi...’sauti ya kiume ikasema.

‘Huo ni uchafu wako, mimi siwezi kusema lolote kuhusu hilo, ipo siku utaumbuka, na ...’akatulia kidogo, hapo nikaingiwa na wasiwasi, nikifikiria huenda wamenishitukia.

‘Mbona unasita kuongea, umemkumbuka bwana wako nini, ...yule hana lolote tena, na siku akijua kuwa unamhadaa, ndio atakufukuza kama Malaya, ..wewe tulia hapa kwangu...’sauti ikasema

‘Kwahiyo ni kitu gani zaidi unahitajia kutoka kwangu?’ sauti ya kike ikauliza

‘Kwanza wewe unahitajika kuwa mfanyakazi wangu,na bosi wako, pili, nataka huyo kidume wako, akubali kila kitu, keshi akija aweke sahihi yake, ya kukabidhi hisa zake kwangu, nataka kampni yake niimiliki mimi, na hiyo ya mke wake, nitakuwa namiliki nusu, ....hilo linawezekana kwake, kwa vile mkataab unamruhusu yeye kwa mume wa familia, ...ninataka mimi ndiye niwe mumiliki wa hayo makumpuni kwa hisa, sitaki utani, nataka nipumzike kuhangaisha kichwa changu...’akasema

‘Kwahiyo wewe unataka mimi nifanye nini?’ ikauliza sauti ya kike

‘Kama kweli unampenda mpenzi wako, mshawishi mpaka akubali, akikubali mimi nikawa mumiliki, nitaharibu ushahidi wangu wote, na nyie mtakuwa huru,...ila wewe bado nakuhitajia sana, ...nakutamani sana uwe nami kila siku...’ akatulia na bbadaye akasema;

‘Ila nakuhakikishia kuwa  nitaharibu kila jambo lenu nililokuwa nalo, hata hivyo, kwanini msishirikiane na mimi, kwanza mtapungukiwa na kitu gani, mimi nimfanya kila kitu, nimeshabadili ule mkataba mgumu wa hiyo familia...na pia nimewatengenezea mikataba ya kuwahakikishia maisha yenu yanakuwa mazuri, sasa mnataka nini, mlitakiwa mnishukuru kwa juhudi zangu hizo, na hayo mengine ya kuchukua mapicha yenu, ni juhudi tu za kuwasaidia, sasa mlitaka niyafanye hayo bure,..’ akatulia.

‘Usifikiri niliyafanya hayo kwa kutaka mwili wako, mimi sitaki mwili wako tu, wapo wazuri zaidi yako,na kila siku wanazaliwa warembo, ... wewe nimekutaka ili kufanikisha lengo langu,na sasa naona kila kitu kinakwenda vyema,  mwisho wa siku wewe mwenyewe utanisifu, na kuniimbia kuwa mimi ni jembe...’sauti ya kiumeikasema.

‘Huyo bosi wako kesho akiondoka, ana uhakika wa maisha yake ya baadaye, na akirudi baada ya masomo yake, anakuwa chini yangu, yule ni jembe mwenza, kwa kazi zangu, namtamani sana awe chini yangu, ...sina haja naye kwa sasa, kesho ataondoka na mtoto wake,...usijali kuhusu huyo mtoto, na wewe utamzalia mpenzi wako mtoto mwingine, achana na huyo msomi wako, pesa zake za manati,...’akasema.

‘Ila hata kama utakuwa na mpenzi wako, au huyo unayemuita mume wako, hakikisha kuwa kila nikikutaka unakuja haraka,...maana wewe ndiye maalumu kwangu, wewe utakuwa wangu milele,wewe ni mtumwa wangu wa kudumu,  japokuwa utakuwa na mume, sijui mpenzi, lakini mimi ni bwana wako, ...unasikia wewe kijakazi wangu...’sauti ya kiume ikasema na kukawa kama kupigana hivi, huku mwanamke akilalamika na kusema;

‘Wewe ni jambazi mwizi, mnyama, hustahili kuishi, mchawi mkubwa wewe, nitahakikisha siku ya leo hulioni jua likizama, kama mimi sio mwanamke wa shoka, utaona...’sauti ikasema na kicheko cha dharau cha mwanaume kikasikika, na kusema;

‘Hayo nimeyasikia sana, ..sijali, hata nikifa leo, sijali, kwani nimeshatumia vya kutosha na familia yangu haitanilaumu, nimewawezeka kila mtu na mali yake ay kutosha, angalau watanikumbuka kwa hilo, hata watu wakisema nilikuwa mbaya, lakini wao kimoyo moyo watakuwa wakifurahia...’sauti ikasema.

Sikutaka kupoteza muda, kwa haraka nikarudi chini, na kwenda kujifanya nimelala, kwani nilishakuwa na uhakika kuwa mtoto wangu yupo salama na kesho ninaondoka, ...na kesho asubuhi, nikajiandaa, na sikupewa mtoto wangu hadi ninafika uwanja wa ndege, kwani walihakikisha sipati muda wa kuonana na mtu mwingine yoyote au kufanya chochote ....

‘Je mume wa familia hayo yaliyoongelewa hapa na huyu askari kanzu wenu au rafiki wa mke wako ni kweli, natumai sasa kama ni muungwana, utaungama, na kukiri makosa yako, sasa hivi tunatarajia utasema ukweli, na kukiri makosa yako kwani, hatuoni haja ya wewe kuendelea kukataa, ukweli upo wazi, na muongeji aliyepita ni mtu wako wa karibu, na zaidi ya hayo ni mtaalamu wa upelelezi, unasemaje mume wa familia...?’ akauliza mwenyekiti, na mume wangu akatulia kimiya kama sio yeye aliyeulizwa na baadaye akasema;

‘Huyo ni mnafiki mkubwa, msaliti, na hayo aliyoyasema sio kweli, muongo mkubwa huyo, yote hayo kayatunga, kwa vile keshajua kuwa rafiki yake kamshitukia, na akaona njia ya kujikosha na kutunga huo uwongo,, ...na kwa uwongo wake huo, nitahakikisha, kuwa unawajibika,..’ akasema huku akiwa kamwangalia mwenyekiti, na baadaye akamgeukia rafiki yangu na kusema;

‘Wewe, unafikiri kwa kuongea hivyo, umesalimika, unajidanganya, hata siku moja tajiri hamuangalii masikini mara mbili, ukikosea ujue huna maana kwake, umechezea shilingi kwenye shimo la choo, umenisaliti, na kwahiyo wewe......ninakuambia ukweli  nitakuonyesha kuwa mimi ni nani, utaona...’akasema huku akisimama, akaanza kutembea kuelekea mlngoni, na watu wakabakia wanamshanga

‘Unakwenda wapi, kikao hakijaisha, ...’akasema mwenyekiti,

‘Siwezi kukaa hapa kuzalilika, kila mmoja akosimama ananisimanga mimi, ...siwezi kuvumilia tena, uwongo wenu, ...’akasema, na mara sauti ya mumbe mmoja ikasikika ikisema;

‘Kabla hujaondoka ni bora ukasubiri nikathibitisha hayo aliyoongea shahidi aliyepita...’
Mwenyekiti akamwangalia muongeaji, na kumuuliza;

‘Unaweza kuyathibitisha hayo....?’ mwenyekiti akamuuliza aliyeongea hivyo, na huyo aliyenga akageuka kumwangalia mume wangu, ambaye alisimama ghafla pale aliposikia sauti hiyo, na pole pole akageuza kichwa kumwangalia muongeaji, na muongeaji, akatikisa kichwa...


WAZO LA LEO: Ni kawaida kwa binadamu, kulalamika, pale anapotendewa ubaya, lakini binadamu huyo huyo, akimtendea mwenzake anaona ni jambo la kawaida tu,...ni bahati mbaya, ni ibilisi, nk ,  sio vizuri tukijenga tabia hiyo, kwani sote ni binadamu hakuna mwenye moyo wa sugu, usiohisi maumivu, ndio maana wahenga wakasema  mkuki ni kwa nguruwe,...
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Yaani hiki kisa kinamvuto kila kukicha