Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, December 17, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-49

  
 Baada ya mapumziko mwenyekiti alirudi, na kutuambia tuingie ndani, ili yuendelee na kikao chetu, na wakati huo mume wangu alikuwa keshaondoka na haijulikani kama atarudi tena,au ndio keshakimbia kikao, nikataka kwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti, lakini kabla sijainuka kwenye kiti , mara mume wangu akaingia akiongozana, na jamaa mmoja na moja kwa moja wote wawili wakaenda kuonana na mwenyekiti.

‘Mwenyekiti nimeona nimchukue wakili wangu, ili aweze kunijibia maswali, kwani naona nimelemewa, ...’akamwambia mwenyekiti.

‘Kwani tulikubaliana vipi, na kwanini umtafute wakili, kuna kosa gani kubwa umeliona ambalo linahitajia wakili?’ akamuuliza mwenyekiti.

‘Lakini nyie mna mawakili wenu, ..mbona mimi sijalalamika hilo..’akasema

‘Hawa wapo kwasababu ni watendaji wetu wa kila siku wakili wangu ni mtendaji wangu wa kila siku, huyo wakili wenu, ni mtendaji wenu, anahitajika kutoa ushahidi wa huo mkataba,..haya ni mambo yetu hayahitaji mtu mwingine ambaye sie mtendaji wetu wa kila siku, na kama umeamua kuleta wakili, basi tulipeke hilo swala mahakamani...’akasema mwenyekiti.
‘Hapana nia ya kumleta huyu wakili ni kunisaidia tu, kwa saabbu kuna mambo mengine yanahitajia sheria, na natambua kabisa tukimaliza hapa, watakuja maaskari, kama sio mimi ni kwa ajili ya mdogo wangu, ndio maana nimeamua kumleta huyu wakili...’akasema

‘Ili afanye nini....?’ akauliza mwenyekiti.

‘Ili aone kuwa ninatendewa haki,..’akasema

Mwenyekiti akatugeukia na kusema; Mnaona jamani mwenzenu kaamua kwenda kuleta wakili akidai hatendewi haki, kwahiyo anataka mtu wa kumsaidia, je nyie mnaliunga mkono hilo swala, maana sisi tulikuwa tumelifanya kifamilia zaidi, lakini mwenzetu kaona hatendewi haki,...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Kama kaamua hivyo, inadhihirisha wazi kuwa hayupo nasi, sisi tutaendelea tu kama kawaida, ila tunachotaka kumwamba huyo wakili  ni kuwa sisi tuna mkataba ulisajiliwa kisheria, na huo ndio utatumika, kama amekuja na mengine ambayo hayafahamu ni wajibu wake, kuuliza kwanza..’nikasema

‘Mimi nimeletwa hapa na huyu mteja wangu, alishanisimulai yote siku nyingi, na nilichukua nafasi ya marehemu, kwahiyo yote nayafahamu, sio mtu mgeni kwa hili linaloendelea hapa...’akasema.

‘Sawa haya ndugu yetu tuambie maana sasa una wakili, ni kwanini, uliamua na wenzako kubadili hiyo katiba?’ akaulizwa

‘Mimi sijabadili hiyo katiba na wala sijui kama hiyo katiba ilibadilishwa...’akasema na mwenyekiti akamwangalai huyo wakili wake, na kuuliza

‘Labda tumuulize wakili wako, maana ameshasema kuwa analifahamu hili jambo kwa undani wake, je unafaahmu kuwa kulikuwa na makataba kati ya wanandoa hawa, ambo ilikuwa ikiongoza familia na taratibu zao za kila siku ikiwemo makampuni yake?’ akaulizwa

‘Nafahamu,..’akajibu

‘Kuna uhakika kuwa mkataba huo wa awali uligushiwa, na mteja, wako anashukiwa kwa kuwa mmoja wa kulikamilisha hilo, je unalifahamu hilo?’ akaulizwa

‘Hilo ndilo limanifanay nifike hapa, kwani mteja wangu anashukiwa kufanya jambo ambalo, halitambui, yeye anatambua mkataab wake, kama alivyokabidhiwa na wakili wake ambaye ni marehemu, na hakufahamu kuwa kuna mabadliko, yoyote, ukumbuke kuwa mteja wangu alipatwa na ajali na kipindi kingi alikuwa kwenye matibabu, na huo mkataba inaonekana ulibadilishwa kipindi hicho akiwa mgonjwa,...’akasema wakili.

‘Una uhakika na hilo muheshimiwa wakili?’ akauliza mwenyekiti

‘Kwa taaifa za kutoka kwa mteja, wangu ndio nina uhakika..muheshimiwa mwenyekiti.’akasema huyo wakili
Mwenyekiti akachukua simu na kumpigia msajili wa mikataba,na akaweka sauti a kusikika watu weote, na kumuuliza msajili,  ni lini iliogundulikana kuwa mkataba wa kifamilia wa hiyo familia ulibadilishwa, na huyo msajili akataja tarehe ambayo ilionekana ni kipindi cha nyuma kabla hata mume wangu alikuwa hajapata ajali,...

‘Umesikia tarehe iliyotajwa, ilikuwa hata kabla mteja wako hajapatwa na hiyo ajali,  mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa,je unawezaje kusema hiyo michakato ilifanyika akiwa yeye hajui, kwahiyo yeye alikuwa na ufahamu wake, na alishiriki, ...’akasema mwenyekiti.

‘Mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa, kipindi mteja wangu akiwa hajapata ajali, inaweaekana ikawa hivyo, hatukatai, lakini yeye alikuwa hajui kuwa mabadiliko hayo yameshaffanyika,,...na kama waligundua hivyo, hawakumfahamisha mteja wangu,   walimfahamisha wakili wake, ambaye na yeye kipindi hicho pengina alitingwa na shughli nyingi, na alikuwa akisubiri muda muafaka wa kumfahamisha mteja wake,, na wakati anajiandaa kuja kuonana naye ndipo ikatokea hiyo ajali, ni ajal haina kinga, haina taarifa....’akasema wakili huyo

‘Uwongo una mwisho wake, sisi tunataka kuwaonyesha kuwa hayo yalifanyika kipindi ambacho mume wa familia hii akiwa mzima na fahamu zake na alipanga yeye na wezake hiyo katiba ibadilishwe, namsimamisha wakili wa familia anayetambulikana kisheria,atuelezee ilivokuwa;

Wakili wetu wa familia akasimama na kuanza kuelezea mchakatao mzima wa katiba ulivyoanza, hadi kukamilika, na mangapi yemeshafanyika na kumalizwa kikatiba, na mafanikio yake, na alipofika kwenye changamoto zake, akasema,;

‘Pamoja na nia njema ya katiba hiyo, bado kulikuwa na changamoto zake, lakini zaidi ni hizo zilizofanywa makusudi kwa nia ya kuharibu lile lengo jema la kuanzisha hiyo katiba. Kiukweli katiba au makubaliano kama hayo yangelitumika kwenye ndoa zetu, nahisi ndoa nyingi zingaliimarika, na hakuna ambaye angelidiriki kuvunja ndoa yake kwa matendo yake.

'Ilikuwa tarehe mmh,....’akaangalia kwenye mkabrasha yake na kutaja tarehe,’

'Siku hiyo alinijia mume wa familia ofisini kwangu, akaniambia anataka kubadili baadhi ya vipengele kwenye mkataba wa kifamilia, nikamuuliza kwa vipi maana huo mkataba upo kisheria, na ukitaka kubadili chochote kwenye huo mkataba kuna taartibu zake,kwanza inabidi wakae yeye na mke wake wakubaliane, halafu inabidi tuandike maelezo kwanini tunataka kufanya hivyo, tukaombe kwa msajili, kun mlolongo wake kisheria, ...?’nikamwambia.

‘Mimi nafahamu jinsi ya kuubadili, hata bila kupitia hiyo milolongo isiyo na maana, kwani mkaaba ni wetu wenyewe, kwanini niwahusishe tena watu wengine, kama nataka kubadili sihitaji kumuomba mtu, wewe sema kama hauwezi nimtafute mtu mwingine atakayefanya hiyo kazi...’akaniambia.

‘Sio swala la kuweza, ni swala la utaratibu, yoyote anayefahamu sheria, ni lazima azifuate taratibu hizo,mimi nakushauri kwanza nenda mkaongee na mke wako, muone kama kuna sehemu za kubadili,mkubaliane,ili tukienda kuomba, tufanye kazi ya kujitosheleza, sio leo hiki kesho kile,...mkashakuwa tayari nitakuja tuongee, ili tufuate taratibu zote..’nikamwambia.

‘Sikiliza wewe nimeshakuona hutufai, nimeshatafuta wakili mwingine ambaye atashughulikia maswala hayo yote, kwani kama jambo dogo kama hili linakushinda huoni utatukwaza, kuna mambo mengi yanahitajika, na hili dogo ni mojawapo, wewe umeshindwa, mimi kuanzia leo nakufuta awakili wa familia, nimeshapata wakili mwingine....’akasema

‘Mambo hayaendi hivyo bro, kuna taratibu zake bosi, hata kama mimi mnaona sifai, ujue tumeshaandikishana mkataba , na kama mnataka kuukatisha huo mkataba wangu na nyie pia kuna taratibu zake, huwezi kuamua mara moja kuwa wewe sio wakili tena,....ngoja niongee na mke wako tukutane, tuone jinsi gani ya kufanya...’nikamwambia.

‘Nimekuambia mimi kama mume wa familia, sijakuambia umwambia mke wangu, mke wangu ana shughuli nyingi za kampuni, hili la uwakili kaniachia mimi, kwahiyo haina haja ya kuongea na mke wangu na hata ukiongea naye haitasaidia maana nimeshapata wakili wangu...anayejua kazi...’akasema.

Mimi niliwasiliana na mke wa familia naye akaonekana kushangaa, kwa tukio hilo akasema nimpe aongee na mume wake, na baada ya siku mbili, akanijia Makabrasha...akiwa na ajenda ile ile kuwa amekuja kuchukua nafasi yangu, kwahiyo nimkabidhi shughuli zote, ...nikamwambai hilo halipo, na ili ahakikishe nikampigia mke wa familia, na mke wa familia akaniambia hakuna kitu kama hicho, na nisitoe chchote kwa huyu mtu, yaani Makabrasha...’

Makabrasha akaniambaia kuwa hilo lipo na litafanyika, kwani hayo ni mambo ya kifamilia, mume anaweza kuamau kubadili chochote kwenye mkataba, kama anaona kuna ulazima, kwa masilahi ya familia, ..akaongeza kusema kuwa mke kwa sasa katingwa na majukumu mengi, na mambo mengine yanaweza kusimama, kwahiyo hiyo katiba ainaitajika marekebisho, akaniomba tushirikiane angalau kwa hilo.

‘Wewe ni mwanasheria, unafahamu taratibu, haiwezekani hayo mambo kufanyika kwa haraak hivyo, kwasabbu huo mkataba umeshasajiliwa, kuna michakato inatakiw akupitia, kwahiyo ni bora hilo swala tukawauliza wahusika wakiwa wote wawili, hata hivyo, mke wa familia anasema hakutambui wewe...’nikamwambia.

‘Na mume wa familia hakutambui wewe...’akaniambia huyo makabrasha.

Sikutaka kubishana na yeye, niliwasiliana na mke wa afmilia, na mke wa familia akazidi kunisisitiza kuwa huyo mtu hanitambui na kama akizidi kunisumbua ashitakiwe, na sijui ikawake, sikumuona tena akifika kwangu, ila siku moja nilikwenda kwa msajili kwa nia ya kufuatilia mambo aliyonituma mke wa familia, nikiwa pale, nikajiwa na wazo la kupitia mkataba wa familia, nikaenda kuonana na huyo anayesimamia hiyo mikataba,

‘Cha ajabu kabisa huyo jamaa wa masijala ya mikataba akaniambia kwasasa hanitambui mimi,...anamtambua wakili mwingine, alieletwa na wahusika, kwahiyo sistahili kuchukua chochote, ikabidi nimpigie simu mke wa familia, na mke wa familia, akaniambia nifuatilie kwa msajili mkuu, na nilipokwenda huko, wenyewe waliona ajabu, wakaniambia niwape muda watalifuatilia hilo swala..

Wakati wao wanalifuatilia huko, mimi nikaona kuwa hilo sasa ni tatizo, hata kama ni ajira,unatafuta kipato, lakini kama kuna sintofahamu ya namna hiyo ni bora uwaachie wenyewe, lakini kwanza nikaona, nionane na wahusika wote wawili. Nikaongea na mke wa familia dhumuni langu hilo, yeye alinikatali na kuniomba nisiachane naye na hayo mambo atayasawazisha, basi nikamshauri kuwa ni bora tukae kikao yeye na mume wake, na ikibidi tumkaribishe huyo Makabrasha tuliongee kwa mapana, ili tupate muafaka, lakini mke wa familia alipinga kabisa kumkaribisha huyo Makabrasha akisema anamfahamu sana huyo mtu yeye hawezi kumruhusu mtu kama  huyo kuingiza kwenye shughuli zake.

‘Basi tukkubaliana kuwa tukae yeye na mume wake, akakubali  na tukakubaliana tufanye hicho kikao mwisho wa wiki hiyo, lakini kabla hicho kikao hakijafanyika ndio hiyo ajali ikatokea...’akasema huyo wakili.
Mwenyekiti akamuangalia wakili wa mume wangu na kumuuliza;

‘Je una swali lolote kwa wakili mwenzako, maana huo ndio ukweli wenyewe,sasa kama ulidanganywa, basi ujue umeingia choo cha kike...’akasema mwenyekiti na watu wakacheka.

‘Mimi hapo sioni tatizo, ..katiba sio msahafu, kuwa hauwezi kubadilishwa, wazo kama hilo la kufanya amrekebisho alikuwa nalo mteja wangu, kipindi hicho hajapatwa na ajali, na alikuwa katika harakati za kulifuatilia kisheria kwa kupitia kwa huyo marehemu...hilo hatulipingi, ni jambo la kawaida...’akasema huyo wakili na akainama kunong’onezana na mteja wake, halafu akasema;

‘Ni kweli mteja wangu akiwa na nia hiyo alimtumia wakili Makabrasha, ambaye ndiye aliyeanza mcahakato wa kufuatilia jinsi gani ya kufanya hayo marekebisho ya hiyo katiba, na wakati anaendelea na mchakato huo, bahati mbaya mteja wangu akapatwa na ajali, ya nyuma yakafutika kwenye ubongo wake, na alipopata nafuu, akaikumbuka katiba yake, na aliyoiona ndio hiyo aliyokuwa akiwaonyesha nyie, hakuwa na kumbkumbu zingine za nyuma, hata mkienda hospitali mtapata taarifa zake...kwahiyo michakato mingine ilifanyika yeye akiwa mgonjwa...’akasema wakili.

‘Nikuulize swali, hayo mabadiliko yaliyofanyika kwenye hiyo katiba mpya ndivyo alivyopendekeza mteja wako kabla hajapatwa na hiyo ajali au kuna mengine yaliongezwa yeye hakuwa na ufaham nayo?’ akaulizwa

‘Hilo yeye hakumbuki, kwasababu hana kumbukumbu sana za nini kilitakiwa kibadilishwe, na mlipomshinikiza zaidi, ndio kumbukumbu ikaanza kumrejea kuwa hilo jambo lilikuewepo akilini mwake, kipindi cha nyuma, na bahati mbaya akapaat ajali, sasa huenda kweli hayo yaliyopo humo kwenye katiba ndiyo aliyokuwa amependekeza au kuna mengine yaliongezwa kwa ushauri wa wakili wake..yote yawezekana, tatizo lililopo hapa ni Makarasha hayupo, ndiye angetupa jibu lenye uhakika, na mbaya zaidi kazi zake zilikuja kuibiwa zote na watu, sasa sikuweza kujua wapi aliishia...’akasema huyo wakili.

‘Naona tusipoteze muda kwa hio, hapa tumeshaona kuwa kweli, kulikuwa na mbinu za kuibadili hiyo katiba bila ya mke wa familia kuhusishwa, lakini hazikufanikiwa,..vyovyote tutakavyoliweka, litasomeka kuwa kulikuwa na hujuma za hadaa,a, baada ya kukataliwa na mke wa familia, na wakati mke wa familia anajitahidi waliongee  yeye na mume wake, akitafuta ni kwanini mwenzake anataka kuwe na mabadiliko katika hiyo katiba, mwenzake akawa anajaribu kupoteza muda ili wafanikiwe katika mbinu yao hiyo, na kwa haraka wakakimbilia kufanya hicho walichokifanya...’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo basi katiba hiyo aliyokuwa nayo mteja wako ni batili, haipo, na haitambulikani kisheria, sisi  tunaendelea kutumia katiba halali, na hiyo ndiyo tunayotaka ifanye kazi yake hii leo,...sawa muheshimiwa wakili?’ akaulizwa, na kabla huyo muheshimiwa wakili hajajibu, mume wangu akamnong’oneza kitu wakili wake, na wakili wake akawa kama anasita kuongea, na kukawa na kama ubishi , na wakili wake, akasikika akisema;

‘Hayo ni mambo ya kisheria huwezi kuyakwepa, acha iwe kama ilivyo, nitajua jinsi gani ya kupambana nao hawaniwezi hawa...’akasema na mume wangu akaonekana kutokurizika na maamuzi ya huyo wakili, na baadaye kidogo baada ya wao kuongea kidogo huyo wakili akamgeukia mwenyekiti na kusema;

‘Samahani kwa kuwapotezea muda, unafahamu mteja wangu anakuwa na wakati mgumu, kwani hiyo katiba inayotambulikana kisheria, yeye, haikumbuki sana, ...sasa inamuwia vigumu kwake kukubali moja kwa moja...naomba hilo mliweke akilini, ila anahisi hadi kufikia hatua ya yeye kuomba kuwe na mabadiliko, marekebisho, anahisi kulikuwa na vipengele vilivokuwa vikimkandamiza na kutokumpa nafasi ya kutumiza wajibu wake kama mume wa familia...’akasema huyo wakili.

‘Kwahiyo..?’ akawa kama anauliza mwenyekiti.

‘Kwahiyo mteja wangu anasema, tukiendelea kuitumia katiba hiyo ya zamani, yeye anaweza akadhulumia na kutendewa isivyo haki, na ndio maana aliamua hiyo katiba ifanyiwe ukarabati,..anaomba itumike katiba hiyo mpya kwa masilahi ya familia, kwani yeye ameipitia na kuiona ina faa sana kwenye familia yake..’akasema wakili.

‘Wewe kama wakili unaifahamu vyema sheria, hilo kweli ni sahihi, maana ukumbuke hiyo katiba, ilishatumika huko nyuma, na hakukuwa na matatizo, matatizo yamejitokeza baada ay mteja wako kufanya mambo kinyume na makubaliano,....’akasema mwenyekiti, na kabla wakili hajasema neno mwenyekiti akaendelea kusema;

‘Hoja kama hiyo alitakiwa aisema kabla,hajafanya hayo aliyoyafanya, kama tutakuwa tunabadili katiba kila tukiivunja, unafikiri hiyo itakuwa ni katiba tena, mkataba gani wa namna hiyo wa kuangalia masilahi ya mtu mmoja mmoja, na kwanini alipoona hivyo, hakuongea na mke wake kwanza, ..hizo ni njama za makusudi, hayo yanajulikana , hija yake haina mshiko, hata wewe wakili unaliona hilo, kama unafahamu akzi yako vyema, naona tusipoteze muda tuendelee au sio muheshimiwa wakili,...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naomba tuendelee na ajenda nyingine,...katiba yetu ni hiyo hiyo, tumashaona kuwa kulikuwa na njama za kuibadili, kwa vile mume wangu alishaona kuwa kafanya madhambi, tena madhambi makubwa, na akafahamu kuwa kutokana na hiyo katiba, ataingia matatani, akaamua kumshiriksiha makabrasha ,akimfahamu fika kuwa ni mtaalamu wa hadaa, wa kucheza an sheria kibatili, ....’nikasema.

‘Madhambi gani niliyafanya wewe mke, usitie mafuta kwenye moto, ..sisi tunataka kulimaliza hili kwa masilahi a familia, wewe unaleta mambo mengine,mimi ninaangalia mbali kwa ajili ya vizazi vyetu, na sio kwa ajili ya kuwafurahisha watu wengine, wewe hujui kuwa wenzako wana malengo mengine kabisa, ambayo sio kwa ajili ya ndoa yetu...’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Kulimaliza hili kwa vipi ukumbuke hizo ajenda nyingine zinahusiana na huo mkataba, na tumeshindwa kuingia kwenye ajenda hizo kwasababu ya huo mkataba wenu wa bandia..., ajenda nyingine ni madhambi yako uliyoyafanya ambayo ni kinyume cha katiba hiyo. Tumepoteza muda kwasababu ya uwongo wako, na sasa uwongo wako umebainika, na madhambi yako yanakusuta, kama unajiamini kuwa hujafanya madhambi, tuendelee na kikao...’nikasema.

‘Sijafanya madhambi yoyote mimi, na wala siogopi, ninachotaka ni kuitetea ndoa yangu ambayo naona wenzako wanataka kuivunja kwa nguvu,...’akasema mume wangu, na mwenyekiti akaingilia na kusema;

‘Kwa vile tumeshaona kuwa katiba ya kugushi haina mamlaka tena hapa, sasa tunaingia kwenye kipengeel cha pili, ambacho kinahusu ukiukwaji wa makusudi wa katiba,  na mienendo mibaya siyokubalika kwenye ndoa,ndivyo ajenda yetu inavyosema ...’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu muheshimiwa wakili, mteja wako anashitakiwa kwa makosa mbalimbali aliyoyafanya akiwa na akili zake timamu, makosa ambayo kikatiba yanatambulikana kama makosa makubwa, ambayo ukiyafanya, kama katiba inayooelezea, adhabu yake ni kubwa pia, ...kuna mambo yameanishwa hapo,na mojawapo ni kuwa ndoa itakuwa imebatilishwa, imeharibiwa na mke au mume, akitenda hayo yaliyoanishwa hapo...’akainua ile katiba kama anamuonyeshea huyo wakili.

‘Kuna makosa makubwa, kama zinaa, uzinzi, kuua, kuiba, ushirikina ....hayo ni baadhi ya makosa makubwa, na mke au mume  ana haki ya kupewa talaka, na haki zote, zitachukuliwa na mwenzake...na ni haki gani hizo, zote zimeelezewa kwenye kipengele kinachofuata,..’mwenyekiti akawa anasoma kwa taratibu huku akimwangalia wakili wa mume wangu.

‘Mimi sitaki kuingia undani wa hiyo katiba kwani wakili wao yupo, yeye ndiye mtaalamu wa hiyo katiba, kwani yeye ndiye aliyeikamilisha kisheria, kama ni muhimu  atasimama na kubainisha au kufafanua kila kipengele, lakini kwa sasa tunataka kuyafahamu hayo madhambi makubwa aliyoyafanya mume wa familia....’akasema mwenyekiti na mara mume wa familia akamgeukia wakili wake na kuanza kulalamika

‘Unaona mimi nilikuambia hawa watu walinitega, na nilikuambia uhakikisha hiyo katiba haikubaliki, sasa wewe umekubali kirahisi hivyo, unafikiri nilikuita hapa uje kufanya nini, uje kusikiliza huo utumbo wao na mbinu zao za kunichimbia kaburi, kama huwezi kazi sema, nikatafute mtu mwingine....’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Ina maana huu tunaoongea hapa ni utumbo?’ akauliza mwenyekiti aliposikia mume wa familia akilalamika.

‘Samahani ndugu mwenyekiti, hayo yamemtoka mteja wangu, akionyesha wasiwasi tu, ninamuhakikishia mteja wangu kuwa  hilo la hiyo katiba lisimtie shaka, cha muhimu ni kuangalia hayo mashitaka yanasemaje, kwani kama yalivyoanza kuelezewa, hayajafafanuliwa na ushahidi ulio dhahiri , kwahiyo hayana msingi, mimi kama wakili nitakutetea kisheria, na haki yako italindwa, una wasiwasi gani, usijali...’akasema huyo wakili kwa kujiamini.

‘Wewe umeharibu kila kitu..’akasema mume wangu akiwa kainama chini na mwenyekiti akaona asipoteze muda, akaendelea na kikao akisema;

‘Kwanza kabisa kama kawaida ya mambo ya kifamilia huwa tunampa nafasi mtetezi, atoe kauli ya kukiri kosa, kwani jambo hili ni la kifamilia, mtetezi, anaweza akakiri kosa na kuelezea udhaifu wako, kwanini alifanya hivyo, kwa kupitiwa, au kwa makusidi, na sisi kama familia tutamsikiliza, cha muhimu ni yeye kuongea ukweli, ukweli ni silaha kubwa kwa mtu yoyote, ukikiri kosa ukatubu, watu wanakusikiliza, kwasababu kila mtu ni mkosaji, sasa tunakupa nafasi hiyo mume wa familia, hapo hatuhitaji wakili wako, tunahitaji kauli yako kwanza, ....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sijafanya hayo madhambi makubwa mnayonisingizia, yote ni uwongo na ni mbinu za kuniharibia ndoa yangu...’akasema mume wangu kabla hajaruhusiwa.

‘Je uliposema madhambi makubwa, ina maana unayafahamu hayo madhambi makubwa ni yapi, kikatiba?’ akaulizwa na akakaa kimiya na wakili wake akasema;

‘Mteja wangu anasema kuwa hayo madhamb mnayomshutumu nayo hajawahi kuyafanya, kibinadamu kuna kuteleza, yeye kama aliteleza hakupewa muda wa kujitetea, kama kuna jambo lilitokea akalifanya ni yale ya kibinadamu tu, yoyote anaweza kupitiwa, ndio maana alitaka katiba hiyo ifanyiwe marekebisho, maana inahukumu moja kwa moja bila kujali ubinadamu...’akasema wakili.

‘Sisi tutatoa ushahidi kuwa hayo aliyoyafanya sio kwa bahati mbaya, kama ni kwa bahati mbaya mbona hataki kuyakiri hayo makosa, kukataa kwake, kuwa hajafanya kunaonyesha usugu, na uthubutu wa mteja wako, na tusipoteze muda, .kama hataki kukiri makosa basi sisi kama wanafamilia tunataka kuyaweka makosa yake hadharani, na wanafamilia watayaangalia, kwa mizania, je alifanya hayo madhambi kwa bahati mbaya au alikusudia,...’akasema mwenyekiti.

‘Leteni huo ushahidi bwana...mimi siogopi kabisa, nafahamu mumenitega tu hapo, lakini mimi nitapigania haki yangu mpaka mwisho..ndoa haivunjiki kirahisi hivyo, nimeshasema, na ndio kauli yangu mpaka mwisho...’akasema na wakili wake, akamnong’oneza jambo, na mume wangu akasema;

‘Sawa fanya unavyoweza wewe, umeshanikatisha tamaa,...endeleeni...’akasema kwa hasira

‘Mke wa familia elezea hayo aliyokufanyia mume wako, ambayo ni kinyume cha ndoa , ni kinyume cha makubaliano yenu, na kinyume cha aktiba yenu, ili kikao, kihukumu, kikiongozwa na katiba yenu wenyewe, sisi hatuna kazi hapo, kazi yetu ni kupima uzito wa hilo kosa,..’akasema mwenyekiti, na mimi nikasimama, na safari hii, nikiwa sitaki kabisa kumwangalia mume wangu, nikasema;

‘Mume wangu ni mzinzi, na mnafiki....’nikasema na mume wangu akasimama na kuniangalia kwa hasira

‘Unaleta matusi hapa...’wakili wake akamkalisha chini na kumnong’oneza kitu, na mimi sikumjali nikaendelea na maelezo yangu.

‘Kwanini nasema kuwa mume wangu ni mzinzi na mnafiki, angalia katika katiba yetu, kosa linalotambulikana kama uzinzi na unafiki , ni kufanya nini, sijakutukana kama unavyodai wewe, ila umejitukana wewe mwenyewe kwa matendo yako, kauli yangu inashuhudia tu, hayo uliyokwisha kuyafanya kwa vitendo vyako mwenyewe, ashakumsi matusi, kuwa wewe ni mzinzi kwa jina jingine wewe ni muhuni na sitasita kukuita malaya....’nikasema na watu wakaniangalia kwa mshangao.

‘Sitamki haya meneno kwa nia mbaya, hapa wapo wazazi wangu nawaheshimu, naomba wakili wetu atusomee kwenye katiba yetu; mzinzi ni mtu gani, au Malaya ni mtu gani:..nikasema na mwenyekiti akatabasamu huku akitikisa kichwa kama kunikubali, na mwenyekiti akanyosha mkono kumruhusu wakili asome maana ya maneno hayo, wakili akasema;

‘Mzinzi ni tabia ya mwandoa ambaye katenda tendo la ndoa kwa asiyekuwa mke wake au mume wake..’akasema wakili.

`Na mnafiki ni yule asiyetunza ahadi, mwongo mdanganyifu, mzandiki, ...’akasema wakili.

‘Na Malaya...’kabla hajaendelea nikasema

‘Inatosha....’ nikatulai kidogo

‘Mume wangu nimegundua kuwa wewe ni mzinzi, na tabia hiyo ipo kwenye damu,...na wewe ni mnafiki wa hali ya juu, kwa vile umehini ndoa yetu, umezini na wanawake zaidi ya mmoja, ukijua kabisa kuwa hilo ni kosa, na mungu akatoa ushahidi usipokwepeka, ...

‘Mume wangu wewe ni mnafiki, kwa vile umeyakana makubaliaono yetu, ukadanganya, ukashindwa kutimiza yale uliyoyaahidi, na ukatafuta njia ya kuhadaa ...’nikasema kwa huzuni.

‘Hayo yote ni makosa makubwa, kifamilia, na uliyafanya hayo ukiwa na akili zako timamu na sio mara moja, ingelikuwa mara moja tungelisema,..ooh, ni bahati mbaya, uliteleza, lakini imekuwa ni tabia yako, hadi ukaumbuliwa ....na mungu hakukufichia madhambi yako, ....’mara mume wangu akasimama na kusema;

‘Sio kweli, wewe umeamua kunitukana tu na kuniumbua, hayo unayoyasema yote ni uwongo, wewe nakuona sasa umeungana na wazazi wako, ili mnisaliti, hayo uliyosema nimeyafanya wapi, ni nani shahidi yako, ..nimeshutikia,lengo lenu, nia yenu ni kunizalilisha tu, wakili wangu yanukuu hayo matusi, kwasababu ninaweza kumchukula hatua huyu mwanamke, hanijui mimi..’akasema mume wangu.

‘Hujatukanwa, Katiba yenu inaelezea hivyo, ila wewe ulitakiwa umwambia mke wako athibitishe kauli yake, kama ni ya uwngo basi tutayachukulia kama ni matusi na wewe una hiari ya kumuadibu mkeo, na hata kumshitaki kikatiba,lakini kama ni kweli, wewe una tabia hiyo, basi usikasirike kuitwa kwa sifa hiyo..’akasema mwenyekiti.

‘Sio kweli , mimi sina hiyo tabia, yeye ni mtaalamu wa kuongea tu, anaona sifa kumharibia mume wake sifa, na hajui hilo kindoa ni makosa, unatakiwa ufiche siri za mwanandoa mwenzako, wewe unazianiak hadharani, hiyo ni tabia gani, na wazazi wako wanakuunga mkono, siwaelewi...’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Ndugu mwenyekiti, sio kwamba napenda kutaja siri za mume wangu hadharani, lakini kwa hali kama hii alitegemea mimi nifanye nini, inabidi tufanye hivyo, kwasababu hukutaka kukiri mwenyewe tukiwa wawili, hukutaka kusema ukweli, uliendelea kufanya jinsi ulivyotaka wewe kwa masilahi yako binafasi, na hawo waliokudanganya, ...na mbele ya hiki kikao hukutaka kukiri ukweli, japokuwa kusema tu, kweli nilifanya nisameheni, hutukutaka utaje kila kitu, ...kukiri kosa unashindwa, ulitaka mimi nikaie kimiya huku ukiendelea kuvunja amari za ndoa, hapana, hilo halipo...’nikasema na kutilia.

‘Sijakusingizia,kama  itaonekana ni uwongo, mimi nipo tayari kuwajibika,..naona umenielewe, kama upo tayari kukiri kosa yaishie hapa, tuone kikao kitasemaje, nipo tayari, je unakiri kosa,?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukataa, na baadae akasema.

‘Usinifanye mimi mjinga, kama una uashidi utoe, na uwe ushahii kweli kwani vinginevyo, kibao kitakugeukia wewe, ...nitahakikisha naitumia hiyo hiyo katiba kukufunza adabu...’akasema kwa hasira.

‘Haya bwana, sasa ili kuthibitisha kauli yangu nitamuhitaji shahiidi yangu mmojawapo,  wapo wengi wa kuthibitisha hilo, ila kwa sasa namuomba....’nikageuka kuwaangalia washiriki,nikamwangalia rafiki yake, na yeye alikaa kimiya tu, nikamwangalia mke wake, alikuwa kama hayupo, alionekana ana mawazo mengi, na kabla sijatamka neno ...’ mama ambaye muda mwingi alikuwa kimiya akasema;

‘Mimi naomba aje Binti yangu wa kufikia, ..aje yeye kwanza maana anahitajika kwenda kujianaa kesho anasafiri....’akasema mama na mwenyekiti akauliza

‘Je unamuafiki huyo shahidi...?’ akaniuliza na mim kwa vile sikujua huyo binti ni nani, japokuwa nilishahidi moyoni, sawa hata yeye anafaa, akimaliza nitamsimamisha mwingine, na mwenyekiti akasema huyo binti akaitwe , na  watu wote wakawa na hamu ya kumfahamu huyo binti ni nani,  ambaye ataweza kutoa huo ushahidi .

Watu wote mle ndani wakakageuza kichwa kuangalia mlangoni, waliposikia mlango ukigongwa, na mara ukafunguliwa, na mwenyekiti akasema;

‘Sogea huku mbele,....’

NB, Ni binti wa kufikia huyo anakuja kutoa ushahidi , je atasema nini


WAZO LA LEO:Kukosa ni kawaida ya binadamu, hakuna anayeweza kujithibitishia kuwa hatendi kosa, yapo ya bahati mbaya na yapo makosa ya kudhamiria, vyovyote iwavyo, unapokosea unastahiki kukiri na kutubu kosa lako, na kumuomba msamaha yule uliyemkosea, unapokosa ukabainika, au hata kama hujabainika, wewe ukalikana lile kosa, lakini kweli umekosea, umlitenda lile kosa, utakuwa ukizidisha uzito wa lile kosa ina maana unatenda kosa jingine la kukana kosa. Tujifunze kuwa wa kweli, na tukikosea tujute, tutubu na tudhamirie kuwa hatutatenda tena hayo makosa. 

Ni mimi: emu-three

No comments :