Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, December 16, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-48Mwenyekiti, akauliza tena;

‘Huyu mtu wenu ameenda wapi, mnakumbuka nyie ndio mliotaka awepo hapa kwenye hiki kikao mkifahamu kuwa anatafutwa kwa uhalifu, na mimi nikamthibitishia mkuu wa kituo, wa upelelezo kuwa, huyo kijana atakuwepo hapa hadi mwisho wa kikao, na mimi nitamkabidhi kwake, sasa kaondoka, mnataka mimi nieleweke vipi, kuwa namlinda kwasababu ni mkwe wangu, mdogo wa mkwe wangu, niambieni huyu mtu kaenda wapi...?’ akauliza mwenyekiti

‘Mwenyekiti, huyu mtu alitoka kipindi tunaangalia hiyo lap-top yako, na hakuna aliyefikiria kuwa huyu mtu ataondoka, kwa vile alifika hapa kwa hiari yake mwenyewe, mimi sikumuona wakati anatoka, lakini hata mtu angemuona angelifikiria labda anakwenda kujisaidia...’akasema rafiki wa mume wangu.

‘Haiwezekani mtu atoke humu ndani bila ya mtu yoyote humu, kumuona,  docta , wewe na mke wako mlikuwa huku nyuma, wakati tunaendelea na hilo zoezi, hususani mke wako ambaye kwa muda mwingi alikuwa amekaa huku nyuma, alikuwa wa mwisho kuja kuangalia tunachokifanya, kwahiyo nina uhakika, kuwa atakuwa alimuona huyo kijana akitoka, kwanini tusiwe wakweli, ...’akasema mwenyekiti.

‘Hapana mimi sijamuona akitoka, kiukweli mimi muda mwingi nilikuwa nimegubikwa na mawazo yangu, sikuwa nikimtizama mtu, na hata ningelimuona akitoka ningelijuaje kuwa anatoroka, sikumuona kabisa...sikuwa na haja ya kumuangalia yeye, nina mambo yangu mengi kichwani ya kuangalia, kwanini nihangaike kumchunga yeye, ....’akasema huyo mke wa rafiki ya mume wangu, na mwenyekiti akamwangalia kwa mashaka, na kumuuliza

‘Unavyozungumza hivyo hueleweki, ina maana haupo pamoja na sisi hapa kwenye kikao, sasa umefuata nini, ni kweli unaonekana kabisa kama vile haupo ndani ya kikao, upo kimwili lakini kiakili unaonekana haupo kabisa, kuna tatizo gani linalokukabili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Haya ni ya kwangu, niachieni mwenyewe, kama ikibidi Itafika muda wake, mtayafahamu, ....naona tuendelee na kikao....’akasema huyo mke, na mimi nikaona niingilie kati nikasema;

‘Baba , hilo la kutoroka kwa shemeji yangu, tuwaachie polisi wakiuliza tutawaambia ukweli, sisi sio walinzi wa huyo mtu na sisi hatutawaficha ukweli,ni kuwa huyu mtu alikuja kwenye hiki kikao  na baadaye akatoroka,sisi tungelifanyaje...’nikasema

‘Hilo unalitamka tu kirahisi kama mtu siyekwenda shule, hivi kweli kuna mtu atakuamini ukisema hivyo, wakati mimi nilishachukua dhamana juu yake, hivi nyie taifa la leo mna nini akilini mwenu, msipende kuchukulia mambo kirahisi tu, kitendo kama hiki kinatutia dosari, uamanifu wetu unapungua,..'akafoka mzee

'Kiukweli mimi sipendi kabisa tabia ya namna hiyo...unapoahidi kitu, unatakiwa ukitimize, ...mimi sio tabia yangu ya kukubali dhamana halafu ninakuja kuihini,mnaniharibia mwenendo na tabia yangu..’akasema mwenyekiti na kuanza kumpigia simu huyo mkuu, sikutaka kumzuia tena, yeye akaongea na huyo mkuu akamweleza ilivyokuwa na alipomaliza kuongea naye akasema

‘Sawa tuendelee, wanamfuatilia wenyewe, keshajiharibia kabisa, ...’akasema

‘Kwanini mnamfanya hivyo mdogo wangu,kwani ungekaa kimiya unafikiri wangekuja kukuuliza, nyie mnajipendekeza kwa hao watu, lakini hawatawasaidia lolote, siku yako ikifika wanakusweka ndani kama hawakujui’ akasema  mume wangu, na hapo nikakumbuka jinsi alivyomnong'oneza kitu muda uliopita

‘Hiyo ndio tabia ambayo siitaki, na hilo nimekuwa nikiwakanya, ....kama umezoea tabia hiyo ya uwongo, mimi kwangu haipo, na kwanini unasema tumemfanya nini mdogo wako, hakuna aliyemfanya kitu mdogo wako, sisi tunatimiza wajibu wetu kama raia wema, ukiishi kwa kufuata sheria, muda wote unakuwa na amani, lakini kama unaishi kiujanjajaja,ukawa mkiukaji wa sheria, ukawalinda wahalfu muda wote utaishi kwa mashakamashaka....’akasema mwenyekiti.

‘Mdogo wangu hana hatia,yeye sio mhalafu...polisi wanamshuku bure,wamshindwa kazi yao sasa wanapapatika...na huenda kaondoka hapa kutokana na vitisho vyenu, kama litamkuta baya nyie ndio mtawajibika...’akasema mume wangu.

‘Tuendelee na kikao chetu, atawajibika mwenyewe, yeye anajiona ni mtoto wa mjini, haya ngoja tuone ujanja wake utaishia wapi. Na wewe, nakuonya, sasa sitaki utani,tuambie, imekuwaje, ukawa na mkataba tofauti na ule mliokubaliana na mke wako, na ukijua kuwa huo ni ukiukwaji wa sheria,umekiuka kiapo chako ulichokiweka kisheria wewe na mke wako, ndivyo unavyoishi hivyo,...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Mimi sijui kama huo mkataba ni tofauti na ule tuliokubalina na mke wangu, kwangu mimi nauona ni ule ule,na kama nilivyowataka, japokuwa msajili kasema hivyo, nahisi nay eye kaongea tu bila ya kuuangalia mkataba huu nilio nao, angeliona angeligundua kuwa hata wao wamefanya makosa, kwanini hawa watu wakubali jambo, bila kunihusisha mimi, mimi ndiye mume, niye ninayefahamu ukweli wa huo mkataba, kwani ni wao waliubuni,....kama nyie mnadai kuwa uligushiwa mimi sijui...na ninani kaugushi?’ akauliza mume wangu.

‘Unauliza ni nani, hilo swali tunakuuliza wewe, kama sio wewe, na kama hujui wakati wewe umekiri hapa kuwa wewe ni mume na wewe ndiye unayebeba dhamana za familia, haya tuambie ni nani aliyeugushi huo mkataba, kwanini kunapatikana mikataba miwili, huu mkataba ulio nao unatoka wapi, hayo ni maswali yako ya kujibu...’akasema mwenyekiti.

‘Hayo nimeshawajibu, sijui...ninachojua ni kuwa huu mkataba ndio halali.....na kama sio halali mimi sijui, kwangu mimi hadi sasa bado sijaamini...’akasema na watu wakamwangalia kwa mashaka, na alipoona watu wanamwangalia yeye, akasema;

‘Kama ni hivyo, ili niwaamini, mnao huo mkataba mnaosema ni halali?’ akauliza

‘Umeshaonyeshwa na msajili wataka upi tena, eeh, usitusumbue  .....’akasema mwenyekiti

‘Ili niwaamini naomba utolewe hiyo nakala nyingine mliyo nayo, nyie,..., ili tuone kweli kuwa upo tofauti na huu....’akasema

‘Mimi naona lengo lako ni kutupotezea muda, hebu mke wa familia mtolee huo mkataba, anaoutaka yeye, na kwa amri ya kikao hiki, halali, tunataka ujibue maswali yetu, kwani kila ulichokitaka umekipata, kwahiyo timiza wajibu wako, sisi tumeshatimiza wajibu wetu....’akasema mwenyekiti.
Mume wangu akanigeukia, huku akionyesha kushangaa, pale aliponiona nikitoa mkataba kwenye mkoba wangu, nikauinua juu, na kusema;

‘Mkataba halali ndio huu hapa, mkataba uambao umeuulizia ndio huu hapa...’nikasema na yeye akabakia mdomo wazi, akiwa katoa macho ya kutokuamini.

‘Mpe wakili wenu wa familia authibitishe kuwa ndio wenyewe,..’akasema mwenyekiti, na mimi nikainuka na kwenda kumkabidhi wakili wa familia ambaye aliufunua akaanza kuukagua na kufanya kama alivyofanya kwenye mkataba aliokuwa na mume wangu, halafu akatabasamu na kuuliza;

‘Umeipatia wapi hi nakala, ndio wenyewe kabisa, sasa mambo yamekwisha, tumemaliza kazi...’akasema kwa furaha.

‘Siamini ina maana mke wangu umeamua kunifanyia hivyo, ...ina maana ..haiwezekani, kumbe,..hapana,....umaupata wapi huo mkataba, uli...uli...oh, huyu mdogo wangu yupo wapi’akasema huku akiwa kashika kichwa.

‘Haya mume wa familia, sasa kazi inaanza, natumai sasa upo tayari, hatuna muda wa poteza,kama wenzako wamekusaliti, utakwenda kuwauliza baadaye, sasa hivi ni kazi ...jibu swali letu, kama ningelikuwa mimi ndio wewe ningekiri makosa na kukubali yaishe, maana mwisho wa hadaa ni fedheha, kwanini unataka ufedheheke’akasema mwenyekiti.

‘Swali gani,...sikumbuki kama uliniuliza swali...’akasema

‘Nilikuuliza kuwa kwanini huo mkataba uliokuwa nao ni tofauti na mkataba halali, tunahitaji kulitambua hilo, kama wanafamilia, kama wajumbe wa kikao hiki, na ikibidi pia sheria inatakuhitajia uilezee kwani wao bado wanatafuta kiini cha hilo tatizo, ilikuwaje kuwepo na mikataba miwili,..’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi muda mwingi nilikuwa naumwa, na siwezi kujua jinsi gani huo mkataba ulivyobadilika, mimi hadi sasa sioni tofauti yake, sijaona hayo mabadiliko ni yapi...’akajitetea hivyo.

‘Kwahiyo bado hutaki kukiri kuwa kuna hujuma mlipanga, kuwa mlifanya kosa, kwahiyo kama wanafamilia, kama kikao tukufikirieje, unaonekana unatujaribu, unatuona sisi hatuna akili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Sijasema hamna akili, lakini siwezi kusema mimi nimefanya hujuma, nikiri kosa ambalo sijalifanya, hilo halipo,kwani kama ni  hujuma iliyofanywa mimi siijui, huenda kuna watu walifanya hivyo, bila ya mimi kujua, hasa kipindi kile nilichokuwa naumwa, nilipopata ajali, ndio maana nimekuwa niking’ang’ania kuwa hiyo katiba ndiyo ile katiba niliyo kuwa awali na ndiyo iliyokuwa sahihi, mimi sikumbuki kuwa na katiba nyingine tofauti..mnakumbuka kuwa ajali hiyo ilinifanya niwe nasahau...’akajitetea

‘Lakini kama sikosei, katiba hiyo iligundulika kuwa imebadilishwa kabla hujapata ajali, ina maana mipango hiyo mliipanga mapema, na mlikuwa mkiifanyia kazi hatua kwa hatua,, na ajali hiyo ilipotokea mkapata sababu nyingine, na hiyo ajali ilitokea mkiwa kwenye michakato yenu ya kukamilisha hiyo hujuma....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi hayo siyajui, nayasikia kutoka kwenu, na kwa jinsi inavyokwena hapa, mimi naona nitafute wakili wangu, kwanini naona mnataka kunitia hatiani, na mimi sitaweza kujitetea kwa hali kama hii...’akasema

‘Kwahiyo unarudi kule kule, kuwa hili swala kwa vile ni la kisheria zaidi, na linaonekana ni kuvunjwa kwa sheria ilitambulikana kisheria, twende ngazi za juu, tulipeleke hili swala mahakamani...’akaulizwa

‘Sijasema twende mahakamani, ...sio lazima twende mhakamani, hapa tuna mawakili, lakini hatupo mahakamani, wakili atanisaidia kunitetea na mimi, ...mimi hapa sina mtetezi wote mnanisakama mimi, na inafika mahali siwezi kujitetea kisheria.....’akasema.

‘Hakuna anayekusakama wewe, wewe ndiye uneyeweka mazingira ya kuonekana, hivyo, kama ungelikubali kusema ukweli, haya yote yasingelitokea, kwanini usikubali kuwa kuna shetani aliwapitia, mkaamua kupanga hayo mliyoyafanya, lakini kwa vile dhamira mbaya haijengi, basi imefika kikomo,kubali, tuangalie jinsi gani tutalimaliza hili tatizo...’nikasema.

‘Wewe mke wangu hujui tu, mimi hapa nafanya kila iwezavyo kuulinda ndoa yangu, wenzako wanataka ivunjike, hili lipo siku nyingi, kama kweli unanipenda, ulitakiwa uwe pamoja na mimi....huoni kuwa wamenitega,...kama hupo na mimi bado wewe ni mke wangu,...’akasema.

‘Sikuelewei ukitaja neno kupenda,....’nikasema.

‘Unaona, nilijua kabisa mnanitega, wewe na familai yenu, mumelipanga hili makusudi,na kwa vile umeshaona mumefanikiwa mipango yako, sasa unatafuta njia za kuniharibu kabisa maisha yangu, mimi sikubali....na kwa hilo la kukubali kuwa nimefanya kosa, mimi hadi hapo sioni kosa langu kabisa, mimi kauli yangu ni hiyo kuwa sijui kama hiyo katiba iligushiwa, na hiyo mipango mnayosema nyie siijui, ni nani walifanya mnajua nyie, mimi sijui,....kwanini nikubali jambo ambalo silijui...mnataka niseme uwongo.’akasema.

‘Kwahiyo unataka tulitolee ushahidi kama hilo la hiyo katiba kuwa sio katiba halali, ujue kila tutakavyofanya hivyo ndivyo na sisi tunashindwa kukuamini tena, na hapo ina maana kuwa wewe haupo nasi..unajiweka mbali na sisi, unaikimbia ndoa yako kiujanja, huku unajifanya upo nayo’akasema mwenyekiti.

‘Tangu hapo naona mumeshaniweka pembeni, sizani kwenye nafsi zenu kuwa mimi nipo na nyie, mumeshaniweka kwenye kundi la wahalaifu, unaona mdogo wangu ambaye hana kosa mumeshamuitia polisi, na nahisi hata mimi mtanifanyia hivyo hivyo,niwaulize kama angelikuwa ndugu yenu wa damu awe anatafutwa na polisi, mngelimfanyia hivyo mnavyomfanyia ndugu yangu,au kwa vile sio ndugu yenu?’ akauliza

‘Huo ni unyonge unaojitakia, nimeshakuambia, wewe kama mume wa familia unatakiwa upambane kiume, lakini katika misingi ya ukweli na haki, hiyo kauli yako uliyoongea sasa hivi kuwa tunakuonea wewe na ndugu yako, ni kauli ya kujizalilisha, kujishusha, ...ongea ukweli, toa hoja zenye mshiko, tuoni ukweli upo wapi,...’akasema mwenyekiti.

‘Ukwelii gani nitakaouongea sasa hivi mniamini, mimi sijajizalilisha, ndio maana ninaendelea kukataa hayo mnayonishinikiza nayo, haya nipeni huo ushahidi kuwa mimi nilikuwepo kwenye huo mpango wa kufanya hayo yaliyotokea...maana ndivyo mnavyotaka nyie, mimi nimeshawambia ukweli wangu, hamunikubalii, sasa kwa vile mnaona nasema uwongo, nikosoeni uwongo wangu...’akasema kwa kujiamini.

‘Kwa hali hiyo ni kuwa hutaki kusema ukweli, unataka sisi tuutafute kwa nguvu za ushahidi, ..kama unataka iwe hivyo, sisi tutafanya, lakini kwa mtaji huo ni kuwa wewe hutaki kushirikiana nasi, hutaki kuwa mwenzetu, ukatusaidia tukalimaliza hili tatizo kama wanandugu....na kwa hali hiyo ikibainika na ndivyo ilivyo, tukatoa ushahidi, basi hatuna jinsi nyingine, hukumu itafuatia kitanzi chenu wenyewe kitakuhukumu.’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo nyie mnataka mimi niseme nini?’ akauliza

‘Sema yote yaliyotokea, jinsi gani mlivyoibadili hiyo katiba, na kwanini ,lifanya hivyo. Na mlikuwa na nani na nani, haafu unaomba msamaha yamekwisha,...sisi kama kikao tutakaa na kuangalia jinsi gani ya kulimaliza... huo ndio uadilifu na utawala bora, kwanini mnataka msutane kwanza, mshikane mashati, hata ifikie damu kumwagika, ...hiyo ni tabia ya watu wasio waungwana’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sio mtoto mdogo, wa kudanganywa kihivyo, nawafahamu sana, hapo mnataka kunitega tena, kama mlivyonitega hapo mwanzo, ...ukweli niliouongea ni huo huo, kama kuna ukweli mwingine niambieni nyie, na mnithibitishie na mimi kama nitaona kuna ukwel ambao niliusahau ,au nilikuwa siujui, maana mengi yametokea nikiwa mgonjwa, sikumbuki, nikumbusheni nyie,....’akasema

‘Na ikiwa ni hivyo, tukakuthibitishia kuwa ni mpango ilipangwa na wewe ukiwemo ukiwa na akili zako timamu, ukishirikiana na wenzako, kwa ajili ya masilahi fulani, ..  upo tayari kuwajibika?’ akaulizwa

‘Hiyo ni juu yenu...lakini mimi sijui kama kulikuwa na mipango huyo, mimi sikumbuki....’akasema.

‘Unakumbuka sana, unalifahmu sana, ndugu mwenyekiti naona tunapoteza muda, huyo mtu nimeshamuelewa, ...anachotaka ni kuona je tunafaamu hiyo mipango yao, je tunafahamu hayo aliyoyafanya yanajulikana,...hataweza kukubali na kusema ukweli...mimi naona tuendelee na kikao, na hatima ijulikane, mkataba upo utafanya kazi yake...’nikasema.

‘Kutokana na uchungzi uliofanyika, inabainisha wazi kuwa mipango hiyo ilikuwepo kabla yaw ewe hujapata ajali, ...wao waligundua kuwa kuna mikataba miwili, mapema kabisa, wakawa wanafanya uchunguzi na walipombana mtu wao, mtu wao kwa vile ni muadilifu akakubali kusema ukweli, kuwa kuna shinikizo lililomfanya abadili mkataba ule halali na mkataba huo mpya alioletewa, na
mtandao....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi hayo sijui....sikumbuki, kama nilivyowaambia ninachojua mimi , hii ndio katiba, niliwahi kuwekeana na mke wangu,kama kulitokea kubadilishwa, basi labda kuna mtu alifanya hivyo, akanitumia mimi kama chambo, kwa vila anafahamu kuwa kumbukumbu zangu hazikiwa sawa...’akasema

‘Alikutumia kwa msilahi ya nani, yake au ya kwako, hebu tuangalia hiyo katiba, inamgusa nani, na kwa masilahi ya nani, ...usitudanganye, na kama unahisi hivyo kuwa labda kulikuwa na mtu kafanya hivyo kukutumia wewe, basi tuambie ni nani...’nikasema.

‘Ni kwa masilahi ya familia yangu, mimi na wewe, ukiangalia, katiba inatuhusu mimi na wewe, na ya kwamba hakuna mtu mwingine wa kuingilia masilahi yetu, zaidi ni mimi na wewe....’akasema

‘Ni ile ya mwanzoni ilikuwa haifanyi hivyo?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui hiyo katiba ya mwanzoni ilikuwa inasemaje, sikumbuki, kwani ninachofahamu mimi ni haya kwenye katiba hii, labda nyie mnikumbushe ..’akasema.
Mwenyekiti akamtizama binti yake, na kutikisa kichwa, na wajumbe wengine kwenye kikao wakaonekana kuchoka, na hapo mwenyekiti akasema;

‘Naona tupate mapumziko kidogo, tukirudi tunaingia ajenda nyingine, tukitumia katiba halali, mliyojiwekea wenyewe, huu ujanja wanaoendelea hapa, tumeshaufahamu,tunafahamu kuwa baada ya ajli ulipoteza kumbkumbu, na mengi yalifanyika kipindi hicho, ...huenda ilichukuliwa hivyo kama mwanya wa kukamlisha huo mpango, ...’akasema mwenyekiti

‘Kwahiyo unamaanisha kuwa kwenye huo mpango tulipanga mimi nipate ajali, ili baadaye nisingizie kupotewa na fahamu,yafanyike kama yalivyotokea ...hivi kweli kuna mtu mwenye akili zake  anaweza kufanya jambo kama hilo la hatari, ina maana hata hawo madakitari walionihudumia  wanahusika na huo mnaouita mpango, maana wao wanajua fika kuwa nilipotewa na fahamu , na kupoteza kumbukumbu kwasababu ya hiyo ajali.....?’akasema mume wangu.

‘Hatukatai kuwa kutokana na hiyo ajali ulipoteza kumbukumbu na hali hiyo akasabbisha wewe kutokukumbuka mambo ya nyuma, lakini hiyo kwa mtizamo wenu,na uchunguzi wetu hali hiyo ilikuwa imetokea  kwa muda fulani tu, ambao kitalamu inajulikana, ...wewe ukauendeelza ule muda, na kuendelea kujifanya kuwa bado unaumwa, ili kutimiliza malengo yenu....’nikasema.

‘Hivi kweli mke wangu unaweza kusema maneno kama hayo, naona kweli umenichoka, sikujua kama utafiki hatua hiyo, ....kuna nini kibaya nilichokufanyia ambacho kimeweza kukugeuza na kunichukia kiasi hicho, mke wangu, mimi sio kama wanavyonifikiria hwazazi wako,kwanini nikudanganye mke wangu, kuwa naumwa na uzidi kuteseka, ili iweje, hapana, siwezi kukufanyia hivyo, hizo ni hisia umepandikiziwa, usiwasikilize watu wasioitakia ndoa yetu mema....’akasema.

‘Dunia ya sasa imejaa hadaa, mkwe wangu mimi nakufahamu sana, usijifanye kuwa hayo yaliyotokea huyafahamu, nakufahamu na washirika wako wote,mimi niltaka kuona kuwa kweli labda umebadilika kama alivyokuwa akidai mke wako, lakini kwa haya uliyoyaonyesha leo, sioni ajabu ....kuna watu siku hizi, wameamua kutumia udhaifu wa wenzao kwa jili ya kufanikisha malengo yao, ..kauli yako utakayoitoa mbele za watu , wao wanaitumia kwa malengo yao....tukio dogo, ambalo nyie mtaliona ni la kawaida tu, wenzenu wanalifanyia kazi kwa masilahi yao...’akasema mwenyekiti.

‘Ajali iliyokupata, ilichukuliwa kama nafasi nzuri ya kufanikisha malengo yenu, na huenda kulikuwa na hujuma kwenye gari lako,...ilipangwa makusudi, ili itokee, ....lakini hilo halikuweza kuthibitishwa, nia ilikuwa nife , kwani siku hiyo nilipanga kulitumia hilo gari lako,....lakini kwa bahati , ukalichukua mwenyewe, sijui ni kwa kusahahu au....’nikasema

‘Huo uwongo wa hali ya juu...’akasema mume wangu.

‘Hiyo ajali ilipotokea, ikawa imefanikisha baaadhi ya mambo yenu,hata kama utakataa kuwa hiyo ajali ilipangwa, kwa nia ya kumuua binti yangu, lakini ilichukuliwa kama sehemu ya kuwezesha mambo mengi,mengi yalifanyofanyika yalifanyika  baada ya hiyo ajali, ili usiwepo nyumbani, li isionekane kuwa wewe unahusika, ...’akasema mwenyekiti na mume wangu akatikisa kichwa kukataa.

‘Kwa vile tumeongea sana na huu ni muda wa kupumzika, ...hiki kikao kinakupa nafasi ya mwisho, ya kufikiria kwa makini..., tukirudi uje na ukweli, kama utaendelea kutuficha huo ukweli ambao sisi tumeshaujua, kikao, kitakuchukulia wewe kama mhalifu ambaye kafanya kosa, lakini hataki kukiri kosa, na hivyo, unatuweka katika nafasi ya kutengeneza kesi, ya kifamilia,na hukumu tutaitoa wenyewe, kama inatosha kuishia kifamilia, tutaimaliza kifamilia, kama itabidi, na kwa mujibu wa sheria, kuna mambo ambayo hatuyawezi kuyahukumu, hayo tutawaachia wenyewe, lakini cha muhimu, ni ukweli....’akasema mwenyekiti.

‘Sasa tukapumzike kidogo, nafahamu bado kuna ajenda nyingi, zenye maswali mengi yanayohitajai majibu, na yote ni dhidi yako, na moja wapo,ni kutuambia kwanini ulimuacha wakili wenu wa kawaida ukaamua kumtumia Makabrasha, hivi wewe kweli ulikosa mawakili, mpaka uamue kumchukua Marehemu...hilo nakufungua akili tu, kuwa sisi tunafahamu mengi zaidi ya unavyofikiria!’ Akasema mwenyekiti na kumfanya mume wangu amuangalie mwenyekiti kwa mshangao.

‘Makabrasha ndiye aliyekuwa kichwa chenu, mbinufu wa hayo yote, ni nani asiyemfahamu Marehemu kwa mambo yake, yeye anatambulikana kwa mbinu zake, za kugeuza sheria, kwa masilahi yake binafsi,haat wewe mwenyewe,unamfahamu hivyo,  hii ni kuonyesha kuwa ulimchukua kwa lengo  maalumu ili mfanikiwe kwa kile mlichokipanga, na mliona kuwa mkataba ndio njia sahihi ya kuyafanikisha hayo malengo yenu...mkaona muutumie huo huo,..’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo hatua ya kwanza ni kuubadili huo mkataba, kwa masilahi yako, ambayo baadaye wewe bila kujua kuwa mwenzako alikutega, ni kuwa masilahi hayo yanakuja kuhamie kwake, ndio maana akakushawishi tena kutengeneza mkataba mwingine wa makabidhiani, kati yako wewe na yeye, maana huo mkataba wako na mke wako mlioutengeenza ulishakupa amdaraak ya kufanay upendavyo...yote hayo tunayafahamu...’akasema mwenyekiti na mume wangu akawa kainama chini.

‘Marehemu anatambulikana kwa uhalifu wake wa milungula, wenzetu huko majuu, wanaita blackmail. Yeye kwasababu lisoma soma huko, akaona kwa wabongo, hawana ufahamu sana na mambo hayo, basia anaweza kuutumia njia hiyo kujitajirisha,...baba, mkwe wangu, ilikuwaje wewe umtumie Makabrasha kwa jambo la kifamilia kama hilo ambalo ni very sensitive,...usitudanganye, inaonyesha kabisa yeye alishakuingiza kwenye mitego yake, ukawa huna jinsi, sasa kwanini suituambie ukweli,ili tuweze kuliweka hili jambo sawa,...tutahitajai majibu yako, ...tukirudi,...’akasema mwenyekiti, na mume wangu akasema;

‘Makabrasha ni rafiki yangu wa siku nyingi, kumtumia mimi sio jambo la ajabu sana, na mengi anasingiziwa, tu, mimi sipendi kumuongelea marehemu, lakini nitajitetea kwa nafasi yangu, na kumtetea yeye ikibidi,lakini mimi sitapenda kumuongelea yeye sana, maana hayupo duniani, kama kuna lolote dhidi yangu,nitajitetea mimi kama mimi kadri ya uwezo wangu, kwasababu sina hatia, nilikuwa natimiza majukumu yangu kama mume wa familia, na kuyafanya yale niliyoona ni sahihi, kama kuna niliyotelekeza ni katika kuhakikisha naweka mambo sawa, mengi mnayonisakama nayo hapa ni ya kupangwa tu, ili ndoa yangu ivunjike..mimi nitaipigania ndoa yangu na sitakubali ivunjike.........’akasema

‘Tutaona tukirudi, kama nikuivunja ndoa yako utakuwa umeivunja ndoa yako wewe mwenyewe, kwani wanasema mume au mke mjinga huivunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe,...na wewe huna tofauti na watu hawo,..kama sivyo, thibitisha kwa kusema ukweli, vinginevyo baba, ...lakin tusipoteze muda tukapumzike, tusiwachoshe watu, au mnasemaje.?’akasema mwenyekiti, na kabla watu hawajajibu mume wangu akasema;.

‘Mimi sijaivunja ndoa yangu, niliyokuwa nayafanya ni katika kuijenga ndoa yangu kwa njia iliyosahihi,ili na mimi nionekane mume, kwa hivyo, mimi nasema hivi ndoa haivunjiki, hilo nawahakikishia kwasababu hakuna  kosa la ajabu hapo la kuvunja ndoa yangu, katiba niliyokuwa naitambua mimi ilinipa mamlaka kama mume, kama muoaji, nifanye yale niliyoona ni sahihi kwa masilahi ya familia yangu,....’akasema halafu akageuka kuniangalia mimi na kusema;

‘Mimi sijakwenda kuingilia ndoa za watu, mbona nyie mnakuja kuingilia ndoa yangu...mimi nimeoa, sijaolewa, kwanini hamnipi uhuru ndani ya ndoa yangu, nilikuja kuoa, sikusema kuwa niwe na watu wa kunisaidia,...baba na mama yangu wapo kijijini, hata siku moja hawajawahi kuja kuniingilia kwenye ndoa yangu , nawashangaa nyie, ...ni kwa vile mlikuwa hamtaki nimuoe binti yenu au....niacheni niijenge ndoa yangu mwenyewe, mimi sitakubali mtu aniingilie, mimi ni mume wa familia na nitabakia kuwa hivyo,  ...’akasema na mimi nikacheka na kusema;

‘Unasema nini, eti kuwa ndoa bado ipo, wewe kwa vitendo ulivyovifanya, bado unashikilia kuwa ndoa bado ipo, ..vitendo vyako vimeshaivunja ndoa yako tayari, ina maana gani kung’ang’ania kuwa ndoa ipo na nani,...hujisuti moyoni, hujuti moyoni, ukakiri kuwa umefanya kosa...nimeshakutambua unachokitaka nini,, unachotaka kwangu ni kufanikisha malengo yako tu, yenye mlengo wa kutwaa mali, na ili uje kunizalilisha baaaye, hapana, hilo skubali, leo tutajua moja...’nikasema na yeye akaniangalia kwa jicho baya, akisema;

‘Na wewe mke wangu, usiseme neno, mengo umeyasababisha wewe mwenyewe, ...ukitaka niyasema nitayasema, ndio maana nasema ndoa ipo, na haitavunjika..na kama umeamua wewe kuwa ndoa haipo mimi sikubali, nitaisimamia kwa nguvu zangu zote...’akasema huku akipiga meza kwa ngumi , na watu ambao walishaanza kutoka nje, kwa ajili ya mapumziko  wakawa wanamuangalia na mwenyekiti akarudi na kuuliza

‘Jamani kuna tatizo lolote...?’ akauliza mwenyekiti na mume wangu akasema

‘Hakuna tatizo tunaongea tu na mke wangu...’akasema huku akijaribu kukunjua uso wake.

‘Mimi, nimesema huu ni muda wa mapumziko, tutakutana baada ya nusu saa, mimi natoka, nimeitwa na mkuu wa polisi wa kituo chenu, nitarudi, kabla ya muda huo, nikirudi nataka tuyamalize yote, na haki itendeke,....’akasema na m ume wangu akamwangalia kwa mashaka, na kusema;

‘Unaona, baba yako anakwenda wapi,....ndio zenu hizo, anakwenda kuwaweka sawa hao watu wake, nakuambia ukweli mimi siogopi, najua anachotaka ni kumfunga mdogo wangu, akija na mimi ananitafutia sababu za kunifunga, kwa hali hiyo, mimi napinga kuendelea na hiki kikao, mpaka aje wakili wangu...tukiahirishe hiki kikao’akasema  huku akiwa kashika kichwa, baadya akalivaa koti lake huku akiendela kushika kichwa, kama vile kinamuuma, akaanza kuondoka.

‘Eti nini...unakwenda wapi wewe...?’ nikamuuliza.

NB : Haya tutaona tukirudi mapumziko kama kikao kitaendelea.


WAZO LA LEO: Kuna matendo tunayotenda kila siku hasa kwa wanandoa,  matendo ambayo kiimani, kimila, na kiutaratibu yanakuwa moja kwa moja yameshavunja miiko, na  mikataba ya yale tuliyokubalina, hata kabla hautajoa kauli zetu. Kila kitu kina makubaliano na masharti yake, ndoa ina masharti na makubaliano yake, ndio maana ikaitwa ndoa. Je tunafahamu nini maana ya ndoa! Je kama ndoa ni kuhalalisha mahusioano kati ya wawili hao, iweje mtu umsaliti mwenzako. Mtu anayeisaliti ndoa yake ni sawa na yule mtu  anayeacha nyama yake safi nyumbani na kwenda kula nyuma iliyooza maporini, huyo keshavunja ndoa yake kivitendo,...Tuweni makini  na ndoa zetu.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Lizbeth said...

Story imefika patamu kweli, ngoja tuone jinsi mume wa familia anavyoumbuka