Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 12, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-46


Una ushahidi kuwa hiyo ndio katiba halali ambayo wewe na mke wako mlikubaliana na kuandika na mkisaidiwa na mwanasheria mkaenda kuisajili,?’ akauliza mwenyekiti, na mume wangu akatulia kidogo, halafu akasema;

‘Ndugu mwenyekii mimi hapa ni mkweo, ni mume wa binti yako, ndiye ninayefahamu ukweli wa mambo ndani ya familia yangu, na kwahiyo hicho ninachokuambia ndio ukweli wenyewe,....’akasema

‘Hujajibu swali langu, je hii ndio katiba halali mliyokubaliana wewe na mkeo,?’ akauliza tena mwenyekiti, na mume wangu akasema

‘Ndio, hiyo ndio katiba halali tuliyokubaliana mimi na mke wangu, na ukiangalia humo utaona sahihi zetu wote ikiwemo ya wakili wetu,...’akasema.

‘Sawa nilitaka kusikia kauli yako tena ili wajumbe wote waisikie, na sasa nataka kuthibitisha ukweli wa kauli yako, maana nimesikia malalamiko kuwa katiba iliyokuwa halali imebadilishwa , imegushiwa kiujanja ujanja na kutengenezwa katiba nyingine kwa minajili ya kujitwalia mali, na kuhalalisha mambo kwa manufaa ya mtu, au watu wake, bila ya mmoja kuhusishwa, na bila wakili wa familia hiyo kuhusishwa, .....’akasema mwenyekiti

‘Hiyo sio kweli mwenyekiti, muulize mke wangu, kama kweli hii sio katiba halali, na wakili yupo hapo, apinge kuwa hiyo sio sahihi yake....’akasema mume wangu kwa kujiamini.

‘Hiyo sio kazi yako, mimi kama mwenyekiti nafahamu jinsi gani ya kuhakiki hiyo kauli yako, na kama kweli ndiyo katiba yenu, ambayo mlikubaliana, tutathibitisha hilo,..mimi sikutaka sana kuingilia kwenye mambo ya katiba yenu, lakini kwa vile wewe mwenyewe kwenye kauli zako za awali, ulianza kwa kusema kuwa nyie mna taratibu zenu za kiutendaji na mna mipangilio yenu ambayo inalindwa an aktiba yenu halali, na kila kitu chenu kimeainisha kwenye hiyo katiba yenu, kwahiyo mambo yenu yanaongozwa kikatiba, na hamtaki watu wengine wawaingilie , kwasababu mna muongoz wenu, sio ndio hivyo mume wa familia?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio hivyo mwenyekiti, kila kitu kipo kwenye hiyo katiba..naona ajabu watu kutuingilia kwenye mambo yetu ya ndani,’akasema huku akitabasamu kwa dharau.

‘Kuna malalamiko,kuwa hiyo katiba uliyonipa , hii hapa...’akaiinua juu mwenyekiti,

‘Mimi sijui, maana hii hayo mliyatengeneza nyie wawili, na kilichomo humu, mnakifahamu nyie wawili, lakini katiba hiyo imesajiliwa kisheria, kwahiyo yaliyomo humo ni sheria yenu wawili,....na kila mmoja ana haki nayo, na kama mmoja atafanya ujanja na kuyabadili, kavunja sheria,...sasa kuna kauli kuwa katiba mliyotengeneza awali imegushiwa, imekarabatiwa kiujanja ujanaja,je wewe kama mume wa familia, unasemaje kuhusu hilo, ?’ akauliza.

‘Mimi nalipinga kabisa, hakuna kitu kama hicho, na huyo aliyesema, hivyo hafahamu ukweli wa mambo yetu ndani ya familia,...mimi kama mume wa familia, nina majukumu ya kulinda familia yangu, na ni pamoja na kuilinda aktiba hii, kwani imebeba mambo yetu yote,....sitakubali mtu aibadili, bila kumshirikisha mwenzagu, na haijabadilishwa,....’akasema

‘Ina maana hakuna katiba mbili, hii ya sasa na nyingine ya awali?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, hakuna katiba nyingine, kama ipo tofauti na hii ambayo kweli imesajiliwa watuonyeshe hawo watu wanasema hivyo, kwasababu kila kitu kipo kisheria, hata ukienda kwa msajili, utaiona nakala kama hii ipo,..’akasema

‘Na je kama itathibitishwa kuwa hii sio katiba halali, na y a kuwa hii imetengezwa kwa kugushiwa kwa malengo maalumu, utasemaje?’ akauliza

‘Nitasema nini, ..ni kwamba hakuna katiba nyingine, katiba ndio hii, kwanini mwenyekiti huniamini..kwanini 
unang’ang’ania kuwa kuna katiba nyingine, mimi ndiye mume wa familia na unatakiw auniamini mimi, kwani nasema hili kwa masilahi ya familia yangu’akasema kwa kupaza sauti kidogo.

Mwenyekiti akageuka kidogo kuniangalia mimi pale nilipokaa, na kutikisa kichwa akionyesha kusikitika, akasema;

‘Hakuna kitu muhimu katika ndoa kama uaminifu, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama kutii yale mliyokubalina nyie wawili kama wanandoa, na zaidi ya hayo,kama wanandoa mtakuwa na ajenda za siri kwa nia ya kuumizana, basi ndoa hiyo haina usalama tena, ndoa hiyo sio ndoa tena bali ni ndoana. Mimi nilishatoa angalizo kuwa kuna mambo yanayosamehewa kama watu watatenda kwa bahati mbaya...

‘Lakini kuna mambo ambayo unayaona kuwa kweli ni makusudi, na yana nia mbaya, na ukiyaachia yanaweza kukiharibu kizazi, uwongo, utapeli, kugushi, ni dhambi, unajenga taifa la watu wasio waaminifu..sasa mimi sitaki kuwa mchochezi, nimeletewa mashitaka hayo, kuwa kuna ukiukwaji wa sheria, tena wa hali ya juu, kwani kama mtu anaweza kubadilisha kitu kilichosajiliwa kisheria, akatengeneza kingine, kikiwa na sahihi za wahusika, basi huyo ni mkiukaji wa sheria wa hali ya juu..

‘Hii hapa ni katiba, ambayo inawahusu watu wawili, na sijui kama ndio yenyewe au la, wanahusika wataithibitisha, sasa mume wa familia anasema hii ndio katiba halali, kabla sijamuuliza mke,amabye ni kiuongo muhimu, ambaye walikaa pamoja yeye na mume wake, wakaitengeneza,  naona ni bora nimuulize mtengenezaji wa hii katiba mwenyewe , maana nikikimbilia kumuuliza mke, nitaionekana nimeweka shinikizo kwa vile ni binti yangu,...’akasema mwenyekiti.

‘Mume wa familia,  nakuomba wewe mwenyewe, uchukue hii katiba ukamuonyeshe wakili wenu ili athibitishe kwenye kikao hiki kuwa hiyo ndio katiba halali mliyoiandika wewe na mke wako, kwa msaada wa huyo wakili wenu.akithibitisha yeye, mimi sitakuwa na haja ya kumuuliza binti yangu, ..nitamuuliza tu kwa vile yeye ni kiuongo muhimu, na kama itakuwa imethibitishwa, basi sisi tutakuwa hatuna kazi kubwa, san a sana tutaangalia makosa yaliyotokea, na kuhukumu kutokana na katiba yenu, kama alivyo dai mume wa familia kuwa tusiingilie mambo yenu , basi katiba yenu itaongea....’akasema mwenyekiti.

‘Sawa kabisa mwenyekiti....’akasema mume wangu, huku akisogea mbele, na kuelekea pale alipokaa mwenyekiti, wakati anapita akapita pale alipokaa mdogo wake, akamnong’oneza kitu, na mdogo wake, akamwangalia kaka yake, kwa macho ya kushangaa, lakini huyo mdogo mtu hakusema neno.

Mume wangu akaichukua ile katiba kwaa mwenyekiti , akaikagua kwa kiufungua, akatikisa kichwa kama kukubali kuw andio yenyewe,huku akiwa anatabasamu akatembea hadi pale alipokaa wakili wetu na kumuonyesha wakili ile katiba huku akisema;

‘Ndugu muheshimiwa wakili, hii ndio Katiba ambayo tuliitengeneza tukishirikiana na wewe, na kama unavyoona kuna sahihi yako ...na hii hapa ni sahihi yangu na hii hapa ni ya mke wangu, nataka wewe uthibitishe kwenye kikao hiki kuwa hii ndio katiba halali, ili tuondoe hiki kiwingu cha kutoakuaminiana ...ukumbuek wewe ni wakili wa familia, na mimi ni mume wa familia, mwenye mamlaka yote a familia....’akasema

Kwanza wakili alisita kuipokea ile katiba, akamwangalia mwenyekiti, na mwenyekiti akasema;

‘Labda tufanye hivi, mimi nina wakili wangu, kabla wakili wenu hajathibitisha hilo hebu muonyeshe wakili wangu, ili yeye aione hiyo katiba, ili awe ni mmoja wa mashahidi walioyoiona hiyo katiba, ili baadaye tusije tukarukana, kuwa haikuwa hiyo, pia wajumbe wengine, kuna docta pale, kisheria anatambulikana anaweza naye kuthibitisha hilo, sio mbaya na wajumbe wengine wakaiona maana kwasasa haina siri tena,...’akasema

Mume wangu akatembea hadi pale alipokaa wakili wa wazee wangu akamuonyesha ile katiba, wakili wa mzee, akaichukua na kuifungua, akasoma kidogo, halafu kwa haraka akapitia ukurasa mmoja baada ya mwingine, akachukua simu yake, akawa anaipiga picha sehemu muhimu, halafu akasema

‘Je una nakala nyingine ya hii katiba yenu?’ akauliza wakili huyo

‘Ndio ninayo, nina nakala tatu, unaweza kubakia na nakala hii, kama unahitaji, zipo nyingine, hakuna shida,....’akasema na kwenda kwenye mkoba wake, akatoa nakala nyingine, na kusema;

‘Hiizi hapa nakala nyingine,zote ni sawa sawa,....’akasema

‘Haya kamuonyeshe wakili wenu, ili athibitishe kuwa Katiba hiyo ndio Katiba sahihi ambayo yeye aliitengeneza, na kuipeleka kuisajili kwa msajili wa katiba,...yeye ndiye mtu wenu wa sheria, kwani kwa jinsi ilivyo, hatua itakayofuatia, kama kweli kuna uvunjaji wa sheria kiasi hicho, basi yeye ndiye muwajibikaji mkubwa’akasema mwenyekiti.

Wakili wetu, aliichukua ile katiba, akafungua ukurasa wa kwanza, akawa anangaliai kwenye ganda la juu, kwa ndani, akawa kama anashangaa, hakusem neno, akafungua ukurasa wa kwanza na kuangalia kwa ndani, akainua ukurasa wa kwanza ni kufanya kama vile ananinginiza, kama vile mtu anayeangalia pesa kuwa ni halali,.....’akatikisa kichwa na kusema;

‘Hii sio katiba halali,siyo katiba niliyoipeleka mimi kwa msajili wa katiba..’akasema, na mume wangu aakichukua kutoka mikononi mwake na kusema;

‘Hii ni katiba halali, unaona sahihi yako hii hapa, na hii hapa ni ya mke wangu, unataka kusema nini, mbona unatupinga sisi wateja wako...’akasema akimuonyesha huyo wakili, lakini huyo wakili hakutaka hata kuiangalia,akasema

‘Ndugu mwenyekiti, kila fani ina watendaji wake, na wanao jinsi gani ya kulinda mambo yao, sisi, kama mawakili tunafahamu haya yote kuwa yanaweza kutokea, kwa hiyo kila mmoja ana namna yake ya kuweka mambo yake katika usalama, ili mtu mwingine asije akabatilisha kazi yake..hii kazi ni ya hatari na ina dhamana kubwa, ukizingatia kuwa unacheza na maisha ya familia za watu....’akasema.

‘Mimi na wengine tuna mihuri ya siri, ni wachache sana wasio na mihuri hiyo ya siri, inayothibitisha kuwa hii kazi ni ya mtu fulani, hii kazi ni yangu, hasa kwenye kazi kama hizi ambazo zina usiri wa kifamilia. Sikutarajia kuwa katiba hii aliyoitoa mume wa familia, ingeliweza kuwa sio yenyewe ambayo niliitengeneza mimi..maana ukiiangalia juu juu, utaona haina tofauti na ile katiba niliotengeneza mimi lakini kuna kitu kinakosekana, hakuna hiyo alama yangu, muhuri wangu, sasa uniambie ni kwanini huo muhusri wangu haupo, je ulitoa nakala nyingine, na kama ulitoa, bado ule muhuri wangu ungelionekana, ningelitambua kuwa ni nakala....’akatulia.

‘Umesahau tu....huo muhuri, sijui unakaa wapi,lakini mimi ninachojua ni kuwa hii ndio katiba halali, na wewe unachotakiwa ni kusimama kwa ajili yetu, kama unanipinga mimi basi wewe sio wakili wetu...’akasema

‘Mimi ni wakili wenu, lakini nasimamia sheria, siwezi kusema uwongo, hii sio katiba niliyoitengeneza mimi, ...na nilishapitia huko ndani kabla, kuna mambo yamebadilishwa...’akasema huyo wakili

‘Ndugu mwenyekiti, Wakati mume wa familia anaongea kwa kujiamini, nilijua kabisa huenda huyo aliyewatengeneza atakuwa anafahamu muhuri wangu, kwani kama aliweza kugushi sahihi, zetu, asingelishindwa kugushi muhuri wangu wa kificho, unaowakilisha kazi zangu...ndugu mwenyekiti, hii sio katiba niliyotengeneza mimi....’akasem wakili.

Mwenyekiti, akakunja uso, akamwangalia mume wangu, na kusema;

‘Mkwe,...nimeamua kukuita hivyo mkwe, ili nikupe heshima, yako, nataka unijibu hayo, ninayokuuliza kama mkwe, mkwe wa kweli hasemi uwongo, useme ukweli wako, kama mkwe, mkwe ana heshima yake, hawezi kumdanganya baba mkwe wake,...eti jamani uliona wapi mkwe anamdanganya baba mkwe wake, ...kwahiyo nakuomba, unjibu haya maswali kwa ukweli wako,, nakuuliza tena;

‘Hiyo katiba ni katiba halali mliyotengeneza wewe na binti yangu?’ akauliza baba.

‘Baba mkwe, mimi ninamshangaa wakili wetu, yeye ndiye anayewakilisha mawazo yetu na kutuwakilisha sisi, nashangaa, leo anapina kazi yake mwenyewe, mimi sijali huo muhuri wake anaosema, ninachojali ni hiyo sahihi, yake, je akiri mbele ya kikao hki kuwa hiyo sio sahihi yake, je hii sio sahihi ya mke wangu...?’ akauliza

‘Inaweza ikawa ni sahihi yangu,..lakini sahihi hii imechukuliwa kitaalamu na mihuri, kuna mihuri siku hizi, inabandikwa kwenye maandishi, na yale maandishi yanabakia kwenye ule muhuri, na unaweza kwenda kuyabandika sehemu nyingine, kama vile unavyoweza kufanya kwenye komputa kukopi na kupesti, ..’akasema wakili

‘Una ushahidi  kuwa ilifanyika hivyo?’ akauliza mwenyekiti

‘Ukiangalia kwa makini, utaona sahihi hizi ni kama zina kivuli, angalia kwa makini, kuna kivuli, na hii kwa wataalamu wa maandishi wanaweza kulithibitisha hili....mimi nilikuwa nashauri kwa vile jambo hilo limefanyika kitaalamu zaidi, ni bora tukawahusisha wataalamu wa  maandishi, na kwa vile tendo hili limefanyika likisaidiwa na wakili, nina uhakika, kuna wakili kashiriki kulifanya hili, kwani sehemu zilizobadilishwa zimebadilishwa kwa utaalamu wa hali ya juu  wa kisheria.....basi hili swala naona liende kisheria, lichunguzwe kisheria, ..’akasema

‘Nikuulize tena kuna kitu gani kingine unachokiona ni tofauti na mkataba halali ulioutengeneza wewe?’ akaulizwa

‘Kuna maandishi yamebananishwa, nahisi ni ili kusije kukaongezeka ukurasa, na kuleta tofauti kati ya mkataba ule halali wa mwanzo na huu wa kugushi...’akasema

‘Kabla hatujaingia ndani tukaona ni nini kilmebadilishwa na kwanini,  narudi kwako mume wa familia, je bado unashikilia msimamo wako huo kuwa hiyo ndio katiba halali ya familia, ambyo uliitengeneza wewe na mke wako?’ akaulizwa

‘Kauli yangu ni ile ile mwenyekiti, mimi nawashangaa, maana mimi ndiye ninayefahamu katiba ipi ni halali, kwani mimi ndiye ninayewakilisha familia yangu, nashangaa watu wa nje, mnakuja kuipnga katiba yetu, kwani mlikuwepo wakati tunaitengeneza,...hii hapa ndio katiba halali, kama ipo nyingine, nataka niione, ili hii ionekane hii sio yenyewe...’akasema

‘Kabla hatujathibitisha hilo,kabla hatujafanya unavyotaka wewe, nataka sasa nimgeukie mke wa familia, nataka na yeye, atuthibitishie kuwa hiyo katiba aliyo nayo mume wake, ndio katiba halali mliyokubaliana kati yenu wawili, ..’akasema

Kwa haraka mume wangu akaichukua ile katiba kutoka kwenye mikono ya wakili wetu akaniletea na kunikabidhi mimi,  huku akifungua sehemu zile tulizoweka sahihi zetu, ....kiukweli huwezi kuona tofauti kati ya katiba hiyo na ile ya kwetu ya awali, kwani kila kitu kilionekana sawasawa kwa juu-juu, ukiangalia kwa haraka haraka inafanana kabisa na katiba ile ya awali,,  kwa mtu asiyejua, hutaweza kugudua utofauti wowote mpaka usome ndani,na usome kwa makini kweli, kwani kuna lugha ya kisheria, ukibadili neno moja unaleta maana nyingine na kuna mambo yameongozeka, na mengine kupungua..nilihakikisha kuwa ni ile ya kugushi,...

Niliingalia kwa makini, na huku mume wangu akinitizama kwa macho yaliyojaa shauku, na aliponiona nasita kutoa majibu, akasema;

‘Mke wangu hii ndio katiba yetu, kila kitu kipo kwa ajili ya masilahi yetu, hakuna kilichobadilika, ukiangalia hapo kuna sahihi zetu, na sahihi ya wakili, mimi sioni kama ni katiba tofauti, ....hii ni kwa ajili yetu na watoto, ....’akasema akionyesha sauti ya huzuni, mimi nikamwangalia na kusema;

‘Una uhakika na hayo maneno yako, una uhakika kuwa unalolisema ndio ukweli, kuwa hii ndio katiba yetu tuliyoitengeneza mimi na wewe siku ile...naomba mume wangu uwe mkweli, na huu ndio mtihani wako, ukweli wako ndio utakaodhirisha kuwa kweli upo na mimi...’nikasema na mume wangu akageuka kumwangalia mwenyekiti.

‘Nimekuuliza swali mke wa familia, je hiyo katiba ndiyo mliyoitengeneza nyie wawili, ...jibu swali, sitaki umuulize swali mume wako, nataka kauli yako wewe, kwasababu wewe unaifahamu vyema,...?’ akauliza baba, na mimi nikamwangalia mume wangu ambaye alikuwa akiniangalia kwa macho ya huruma, na machoni, nikawa nawaona watoto wangu wawili, na sijui kwanini, lakini kwenye akili , ndani ya macho niliwaona watoto wetu wakilia, na kuita baba,baba yupo wapi....,

Nikageuka kumwangalia mwenyekiti, nikasema,;

‘Ndugu mwenyekiti, katiba hii, inafanana sana na katiba ya awali...ni vigumu sana kuitofautisha na katiba..ya....’nikaanza kuongea na mume wangu akatabasamu na kunikatisha akasema;

‘Unaona mwenyekiti, mim na mke wangu ndio tuliotengeneza hii katiba kwahiyo tunaifahamu sana, namshangaa sana wakili wetu kutegeuka, sijui ana masilahi gani...’akasema mume wangu, na alipomaliza nikaendelea kuongea

‘Lakini ndugu mwenyekiti, wakati katiba hii inatengenezwa, sijui ni hisia au sijui ni kwanini nilijiwa na kitu kama hicho kuwa huenda ikatokea kubadilishwa badilishwa hii tatiba, basi nikajiwa na wazo, kwa vile, sheemji yangu, yaani mdogo wa mume wanguni mtaalamu wa komputa, na mambo yake, nilimuomba anisaidie kutengeneza maneno ya siri ambayo ninaweza kuyaweka kwenye kumbukumbu zangu, kiasi kwamba mtu mwingine asiweze kugundua....’nikasema

Na sikuwahi kumwambia wakili wetu kuwa kwenye hiyo katiba kuna maneno nimeyaweka ya siri, kwahiyo hata yeye hajui hilo, niliyaweka wakati wakili wetu aliponiletea katiba hii kwenye mtandao ili mimi niupitie, ndipo hapo nikayaweka hayo maneno, na kila ukitoa nakala,halisi utayaona hayo maneno, yanakuwa huku pembeni, na ukitoa nakala, isiyo halisi maneno hayo hugeuka, yakawa kinyume chake....’nikasema na kumwangalia shemeji yangu ambaye alikuwa kabakia mdomo wazi.

‘Je shemeji hayo ninayozungumza ni kweli ...hukunitengenezea hayo maneno,...’ na akilini nikajiuliza kwanini shemeji yangu hakuweza kuwaambia wenzake kuhusu hayo maneno, wakati wanatengeneza hii katiba mpya, ili wayaweke hayo maneno, huenda hakuwepo, na huenda hakushirikishwa. Mume wangu aliposikia nikimtaja mdogo wangu akasema.

‘Mdogo wangu hahusiki na haya mambo, hii katiba ni kati yangu mimi na wewe, sema ukweli wako kama alivyokuuliza mwenyekiti, mimi ni mume wako,unahitajika kuwa na mimi, nah ii katiba ni kwa ajili yangu mimi na wewe, na watoto wetu, wengine hawana masilahi nayo, usikatae ukweli....’akasema kwa huruma, na mdogo wake, akanyosha mkono, akitaka apewe nafasi aongee, mwenyekiti akasema;

‘Unataka kusema nini, ....wewe ni mualikwa tu, ....na muda wako ukifika utaongea, au hebu niambia wewe ulitaka kusema nini?’akasema mwenyekiti, na shemeji yangu huyo akasema;

‘Nakubali kuwa kweli nilimtengenezea shemeji hayo maneno, lakini sikujua kuwa alikuwa na nia ya kuyaweka kwenye hiyo katiba,...na pia mimi sijui lolote kuhusu hiyo katiba, kuwa ilibadilishwa, na kuna ya zamani na mpya,naomba kwa hilo mnisamehe...’akasema

‘Nimewaambia mdogo wangu hajui lolote, haya mambo ni kati yangu na mke wangu, hii katiba tuliitengeneza tukiwa wawili, naomba msimuhusishe na hii katiba, ...’akasema kaka yake.

‘Lakini wewe unafahamu kuwa kuna katiba mbili,au nikuulize hivi je wewe uliwahi kuziona katiba mbili tofauti?’ mimi nikamuuliza

‘Siwezi kujibu hilo swali kwasasa, kwa hali niliyo nayo, ila ninachweza kusema ni kuwa niliwahi kuona katiba sasa sijui utofauti wake maana zote zinafanana, ...’akasema.

‘Mke wa familia, hujajibu swali langu, naona unaniingilia, je hiyo katiba ndiyo katiba mliyoitengeneza wewe 
na mume wako, jibu swali ili tuendelee,..?’ akauliza mwenyekiti, na mimi nikamwangalia mume wangu, na nilimuona sasa akionyesha uso wa kukata tamaa, na mimi kawaida yangu sipendi kusema uwongo, hasa mbele ya wazazi wangu, lakini kuna kitu kilikuwa kikiniuma, ufahamu huyu ni mume wangu nimezaa naye watoto,....hili limekuwa likinipa wakati mgumu, kwani hiyo katiba ndiyo hitimishona la kila kitu, na kila kitu kipo wazi, lakini hata hivyo, mimi nilitaka mume wangu awe mkweli, akiri kosa, na mimi ningelijua jinsi gani ya kufanya,...

Kwa hali ya mume wangu kutokutaka kusema ukweli, ilinipa shida sana, nilijiuliza ni kwanini, au kweli kumbukumbu hazipo, hakumbuki kuhusu katiba ile ya awali,...na nilijua kabisa kauli yangu itasababisha mimi na mume wangu tuwe maadui, na sijui kama kikao kitakuwa na amani tena, kama nitasema kinyume na anavyotaka mume wangu,...,..

Nikasema;

‘Ndugu mwenyekiti, naomba jibu langu lisubiri kidogo kwani kwanza, kwa sababu kuna mambo nahitajia yakamlike, kuhusu uaminifu na ukweli wa mume wangu, nilitaka mume wangu atoe kauli yake ukweli,kwangu, ....’nikasema.

‘Mwanangu, mimi ndiye mwenyekiti wa hiki kikao, na ukweli, ni kwa wote, ninachohitajia ni ukweli wako wewe, usizunguke, ukweli ni ukweli, usije ukaharibu ukweli wako kwa kungalia sura ya mtu, ukigeuza ukweli, ukawa uwongo, kwasababu ya dhamira fulani, hata kama wewe uaniona ni kwa masilahi ya huyo mlengwa, lakini ukasema uwongo, ukweli, ukaugeuza ukawa uwongo, wewe sio mkweli tena, wewe sio mwaminifu tena.

‘Mtu mkweli na mwaminifu husema, ukweli bila kujali huyu ni mume wangu au huyu ni mtoto wangu, au huyu ni mzazi wangu, ukweli utasimama kama ukweli, kwahiyo ninachotaka hapo ni ukweli wako wewe,...je hiyo katiba, kama ulivyoiona ndio katiba halali mliyoitengeneza wewe na mume wako....?’akaniuliza mwenyekiti

Na mimi nikamwangalia wakili wetu, nikaiangalia ile katiba, na sijui kwanini nilikuwa nasita kutoa kauli yangu,kuna hali fulani ilivunja ujasiri niliokuwa nao, kuna hali ya huruma iliniingia, sijui ni kwanini,na hali hiyo ilinijia pale tu nilipomuangalia mume wangu machoni, nikageuka kumwangalia rafiki wa mume wangu, ambaye muda mwingi alikuwa kimiya, alikuwa kakunja uso kama anatafakari jambo, na macho yetu yalipokutana, nilihisi akiniambia, msaidie mume wako, japo kwa hilo tu, unaweza ukampoteza mume wako, na alipoona namtizama akatabasamu, na mimi kwa haraka nikageuka kumwangalia mwenyekiti tayari kutoa jibu........

NB: Haya sehemu hii inaishia hapo kwasababu maalumu...tukutane sehemu ijayo.


WAZO LA  LEO: Ukweli utabakia kuwa ukweli, huwezi ukahalalisha ukweli kwa kusema uwongo , kwa ajili ya kumsaidia mtu, hata kama ni mtu wako wa karibu, ukisema uwongo, ukaukana ukweli, basi unavunja uaminifu wako, tujifunze kuwa wa kweli popote pale, ili tuwe waaminifu.

Ni mimi: emu-three


1 comment :

Pam said...

huruma huponza wanawake walio wengi na kusahau kutenda yanayostahili hata kama wanaumizwa na uhusiano uliopo ili kulinda mwonekano mbele ya jamii na mwisho huwa kupata kilema au kuuwawa..