Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, December 10, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-44


Nilifika sehemu ambayo huwa tunafanyia vikao vyetu, ni kazini kwangu , lakini kuna sehemu maalumu imejengwa kwa ajili ya vikao, na siku hiyo ilipangwa kabisa kuwa kutakuwepo na kikao changu na familia yangu, ndio maana msaidizi wangu alikuja nyumbani kunikumbusha.

Nilipofika kwenye chumba cha mkutano nilimkuta baba keshafika, kama kawaida yake, huwa ni mtu wa kujali muda, alikuwa tayari kakaa kwenye kiti huku akifungua makabrasha yake, na lapotop yake ikiwa pembeni, na wakati nafika, alikuwa akiongea na simu. Alionyesha kuwa kafika muda mrefu, na aliponiona naingia akafunga makabrasha yake na kuhakikisha kayaweka vyema, halafu akasimama kunisamilia, halafu akaangalia saa yake na kusema;

‘Nilitarajia watu watafika kwa muda, lakini naona dakika tano zimepita, siwaoni watu, ..’akaanza kulalamika

‘Foleni na hulka zetu baba, lakini nina uhakika wote watafika,....’nikasema

‘Sawa  hebu kaa kwenye kiti tuanze kuongea yetu, ya baba na binti yake, unaona hata mama  yako hajafika, nay eye ni muhimu sana kwenye kikao hiki, alisema anapita dukani kununulia vifaa vyake na binti yake...’akasema

‘Na binti yake, binti gani huyu?’ nikamuuliza.

‘Utamuona tu , na yeye atakuwepo kwenye kikao, ....’akasema na sikutaka kumuuliza zaidi, maana inawezekana ndio mtindo wa wanaume kuwa na watoto nje, lakini siwezi kuamini kuwa baba yangu ana mtoto nje, ni mtu anayejali sana sheria, na itikadi na ni mcha mungu wa aina yake, yeye kila mara anasema uongozi bora, kiongozi bora huanzia nyumbani kwake.
Nilipotulia kwenye kiti, aliniangalia kwa makini kama anaitizama ndani ya ubongo wangu kuna nini, halafu akasema;

‘Nilitaka kufahamu maamuzi yako, nataka nijue ni nini msimamo wako baada ya haya yote, nataka nikushauri kama baba yako, kama mzazi wako, japokuwa mimi na mama yako tumeshaongea na kufikia uamuzi wetu, ambao sio tofauti na ule wa mwanzoni,....’akasema

‘Baba maamuzi yangu yatatolewa mbele ya wahusika, ninawahitajia wenyewe waje wathibitishe waliyoyafanya, nina kuwa kama watakuwa wakweli wakajitakasa , yote yaliyotokea tutayamaliza kwa amani na saama, vinginevyo, kama ndivyo walivyo, na watang’ang’ania kuwa waongo, ......basi sheria itachukua mkono wake, mimi nina imani kuwa kwenye wengi hapataharibika jambo,....’nikasema na baba akaniangalia kwa makini bila kusema neno kwa muda, na nilipotaka kufungua mdomo wangu akasema;

‘Hayo unayozungumza kuwa kwenye wengi hapaharibi neno, ni kama vile upo kwenye kikao cha wazee wenye busara na hekima zao, ambao wanaweza kususluhisha mambo kihekima, lakini ukumbuke kuwa kikao hiki, ni cha sisi wazazi wako, ambao ndio wazee, wengine ni mume wako, rafiki zako na wahusika wa kazia nzima, ambao wengi wao ni wahasimu wako, wanaojali masilahi yao , unatarajia wao watakushauri jambo jema?’ akaniuliza

‘Lakini nyie si mpo, nyie mnawakilisha wazee, mtaongea mawazo yenu nitawasikiliza, na wahusika watawasikia, watajitetea, wewe ni mwenyekiti wa kikao hiki, unatakiwa uwe kati na kati, usionyeshe upendeelo, ukawakandamiza watu, tuwape nafasi wajitetea, huenda kuna ukosaji wa bahati mbaya, huenda hata sisi tuna makosa....’nikasema nikitabasamu huku nikionyesha adabu, maana mbele ya baba unatakiwa ujiheshimu kweli.

‘Huwezi kunifundisha nini cha kufanya, naifahamu sana kazi hiyo kama mwenyekiti, nimeifanya kazi hiyo karibu nusu ya umri wangu, kwahiyo hilo nalifahamu sana, ndio maana nataka nikuweke sawa, ili nisije nikajikuta nakusuta mbele za watu, nisije nikawa naegemea upande wangu, na sitakubali uniangushe....’akasema na kuinama kama vile ananikaribia, na isingeikuwa meza, angefikisha kichwa chake karibu yangu, akasema;

‘Hebu niambie wewe ulishafikia wapi, maana uliniambia kuwa unafanya uchunguzi, na utakuja kutoa maamuzi yako mbele ya kikao, ..nataka kuona mtoto wangu anaongea kama mimi, au zaidi ya mimi, unanielewa, nataka niione kazi yangu kwako, kama huwezi uniambie, nitajua ni nini cha kufanya...’akasema

‘Hivi baba hujaniamini, baada ya yote hayo niliyoyafanya, baba mimi sio mtoto tena, ni mtu mzima nafahamu ni nini ninachokifanya, nimeweza kuisimamia kampuni yangu bia kutetereka, na ikawa kubwa, kama unavvyoiona, nimetulia kidogo baada ya matatizo na mume wangu, lakini kuna msaidizi wangu ambaye anaifanya hiyo kazi vizuri tu, japokuwa sasa naona mume wangu kaamua kuingilia kote, akini ni kwa muda tu, kwanza anaumwa hawezi kupigika itakiwavyo, baada ya hiki kikao nitarejea tena kwenye ulingo wangu..’nikasema

‘Binti yangu, sio kwamba nakushusha chini katika utendaji wako wa kazi, hapana, kiukweli unajitahidi sana, hata mimi najisifia mbele ya wenzangu, lakini hili lililotokea, ....mmh, limekushusa, haya yaliyotokea kati yako na mumeo wako, imeharibu kila kitu. Unafahamu kupanda juu, kunachukua muda, akini kushuka, ni mara moja tu...’akarudisha kichwa na kuegemea kiti, haafu akasema;

‘Mimi sitaki ushuke kihivyo, nataka uendelee kuwa juu, hilo lililotokea, nataka lisafishwe, maana watu wameshakushusha sana, wewe huwezi jua, kwani kuna usemi kuwa kama mzazi, kama baba na mama unashindwa kuihudumia familia yako, ukashindwa kuiongoza basi hutaweza kabisa kuongoza jamii, kuongoza kampuni,..na hili linaonekana wazi kwa jamii, sasa kama wewe na mume wako mumeshindwa kukaa pamoja, na hili tulilijua ndio maana tukakushauri kuwa huyo sio mume mwema....’akasema

‘Baba mimi sijashindwa kabisa kuiongoza familia yangu, na unapozungumza hivyo, unasahahu kuwa mimi ni mke wa mtu, ambaye nina mipaka yangu, ...lakini hata hivyo, sio kwamba nimeshindwa kuiongoza familia yangu kama mke...nimejitahidi kufanya yale ya mpaka wangu, kwa kadri ya uwezo wangu, yaliyotokea yamekuwa changamoto kwangu..na sizani kwamba nitafanya hayo makosa tena,..kamwe, baba niamini, ....’nikasema

‘Kama unayosema ni kweli, kama ni hivyo, nataka nimuone binti yangu, akionyesha ukomavu wake, nataak nijione mimi, japokuwa watu wanasema nimezaa binti, akini nina imani kuwa wewe ni binti, lakini umewajihi umimi, kia nikikuangalia usoni, najiona mimi, naomba, na sio naomba, nataka ufanye kweli, nataka uwaonyeshe watu kuwa familia yetu haiyumbushwi na watu wasio jua maadili,...’akasema

‘Baba usiseme hivyo, ukazizarau familia nyingine, ukachukua azaifu wa mtu mmoja, ukauchanganya na familia zao, mimi nina uhakika kuwa tabia kweli zinaweza kujengwa kutokana na familia husika, kurithiana nk, lakini ukumbuke sasa jamii zimechanganyikana, tabia za kifamilia zinajichanganya na kuleta tabia nyingine tofauti,  mtu akishapevuka akachanganyika na jamii nyingine, anajichuja, anakuwa na tabia yake nyingine, kwahiyo baba ngoja tuone kama kwei kuna mabadiliko tutayachukuliwa kihekima zaidi, kitaalamu zaidi, ...’nikasema

‘Binti yangu, Usije ukaharibu, maana mimi nilijua utafanya maamuzi ya msingi kwa masilahi ya familia, lakini unavyoongea inaonyesha kuwa upo tayari kukubali yote yaishe hivi hivi..mimi hilo sitakubali, kwasababu tabia ya kizalia haina dawa, hayo waliyokufanyia ni mwanzo tu, ujue chini kwa chini kuna dhambi za damu ya mtu, unafikiri hiyo damu itafukiwa kwa mchanga tu hivi hivi, hata kama tutayamaliza kienyeji, lakini sio sahihi, kuna mtu kauwawa, hakuna haki iliyotendeka, hata kama alikuwa na madhambi yake, watu wanasema aheri kafa, lakini ni wapi sheria ilisema auiwe,hilo uliangalie kwa makini..’akasema

‘Baba mimi naomba unipe nafasi hiyo, kama nitakuwa nimekosea mtanisahihisha, lakini nina imani kila mmoja atajihukumu mwenyewe muda ukifika, uwongo na hadaa una mwisho wake, ...wewe subiria, tu, tusichukue maamuzi kabla wenyewe hawajajitetea tukaona ukweli upo wapi..’nikasema

‘Ukweli wote ninao hapa, unayaona hayo makabrasha , huo ndio ukweli wa kila mtu, vijana wangu wamefanya uchunguzi wa kina, na mimi kutokana na uzoefu wangu, nimeyakinisha kuwa ni kweli. Sio kwamba wameniletea hiyo taarifa nikapokea kama ilivyo na kuikubali tu, la hasha, ....nilifuatilia kwa namna yangu nikagundua kuwa ni kweli,.....’akasema na mimi nilipotaka kuongea akanikatisha na kusema;

‘Na muda mfupi uliopita nilikuwa nawasiliana na mkuu wa upelelezi wa kituo chenu, na yule aliyefuatilia kesi ya mauaji ya Makabrasha, wameniambia mengi ambayo wameyagundua wao kama wao, japokuwa yana uwalakini,ukilinganisha na uchunguzi wangu lakini ukweli upo pale pale, kuwa mume wako sio mwaminifu, mume wako ana ajena za siri dhidi yako, na akilenga sana mali zako, hafanyi hivyo kwa upendo kutoka moyoni, na hayo ukitaak nitakuonyesha,...mimi imeniuam sana, lakini sio ajabu, kwani asili yao ninaifahamu fika...’akasema huku akifungua makabrasha yake, lakini baadaye akayafunga na kusema;

‘Mume wako hajui , hakumbuki wapi alipotoka, yeye anafikiria kuwa mali aliyo nayo, ilipatika kwa dhuluma, anashindwa kufahamu chimbuko za hizo mali zimetoka wapi, sisi tulihangaika, tukifuata sheria, babu , baba, walikwua wachakazi, na mimi nikarithi hivyo, na kiichotusaidia ni ukweli, uwazi, sheria, na itikadi,...kwanini usifanikiwe, kama unajituma kwa uadiifu, tatizo watu wanataka kupata kwa kupitia kwenye migongo ya wenzao, dhuluma, ndiyo sera yao, unapata kutoka kwa mlalahoi, ambaye kula kwake ni kwa shida, wewe unalimbikiza, unajiona ni mjanja, hatuendi namna hiyo...’akasema

‘Baba mimi nimekuelewa, ndio maana nataka mume wangu aje aongea mwenyewe ukweli wake,muda ukifika,kama kweli ana itikado hiyo ya dhuluma, kama kweli nia yake ni kuchuma kutoka kwenye migongo ya wenzake, tutamsikia, ...’nikasema

‘Hivi wewe unawafahamu hawo watu, aje aongee ukweli, ili akafungwe, aongee ili akose kila kitu, ina maana gani kufanya mipango yote hiyo, unafahamu mipango hiyo ilianzia wapi, ina maana walikuwa wakiigiza, ii baadaye waseme mchezo umekwisha, sasa basi, ..nikuambia mwanangu watu kama hawo hawakubali kirahisi...mwanangu binadamu sivyo walivyo, inapofikia kwenye masilahi ukweli unasahaulika...’akasema baba.

‘Baba hayo tutayaona, akishindwa kusema ukweli, ushahidi utaongea, ...wahusika wote watakuwepo, watasema na vielelezo tunavyo vitaoonyesha kila kitu....’nikasema

‘Halafu unatarajia wao wakubali,...mwanangu, hatua iliyofikia ni ya uamuzi,....kwasababu wao wanataka kuishi kwa dhuluma, basi, tuwaachie waende wakaishi kwenye uwanja wao ambao sio hapa kwenye hii familia yetu,, familia yetu sio sehemu yao,...unasikia, hayo ndio maisha yangu, ndivyo baba , babu na kizazi chetu kilivyoishi, haki na ukweli. Na ili kuhakikisha kuwa hayo yanafanyika, inabidi wakati mwingine uchukue maamuzi magumu, hata kama ni ndugu yako kafanya hivyo, anatengwa, anawajibishwa, bia hivyo hatutafika, ...’akasema

‘Nimekuelewa baba, nikuulize kitu, huyo mkuu wa upelelezi kaamua kufanya nini, baada ya ugunduzi wao huo?’ nikamuuliza baba ii kupoteza lengo, kwani sikutaka kutumia sera za baba, nilikuwa na njia zangu mwenyewe, na baba akaniangalia akatabasamu, na kusema;

‘Nimemuaomba anipe muda, baada ya kikao hiki, nitajua ni nini cha kufanya, na kwa vile bado sijafahamu uamuzi wako ni nini, ningelishamuamuru afanye kazi yake, afuate sheria, awakamate wahusika, na watajua wenyewe a kufanya, lakini kama ningeliachia iende hivyo, ina maana inakugusa na wewe, na hatima yake ni nini, na sisi tutaingia, na hapo ni kashifa inajijenga...’akasema.

‘Ni kweli baba ndio maana hata mimi nikalichukulia kisiasa zaidi, kwasababu mume wangu yupo ndani ya familia, maamuzi yoyote tutakayotoa yataweza kuathiri familia yangu, kuna watoto, ....unahisi watajisikiaje, na huenda na nyie mkaingilia kati, kitu ambacho sikukitaka, nilitaka haya niyatatue wmenyewe, lakini kila nilivyojitahidi, naona nyie mnaingilia kati, ndio maana nikaona leo niwahusishe rasmi,...sasa kwangu mimi  sitaki kusema lolote mpaka wote waseme ukweli wao, ...’nikasema.

‘Niwajuavyo hawo watu, sizani kama ukwel utasemwa,...na hata kama hautasemwa, mimi nimeshaufahamu ukweli wote na umauzi nimeshaupitisha....’akasema baba na mara mlango ukagongwa, wajumbe wa kikao wakaanza kuingia:

***********

Mjumbe wa kwanza: alikuwa ni mama, akiwa kavalia kitaifa zaidi, muda wote utamkuta hivyo, akiwa na nywele zake za asili, hajawahi kuziweka dawa, ngozi ya asili hajawai kuichubua, san asana ni machoni kaweka kanta, akatabasamu, kama kawaida yake, huwa hataki kukunja uso, yeye ana kauli yake kuwa mwanamke hatakiwi kukunja uso, akikunja uso anaharibu ngozi ya sura yake, mwanamke muda wote unatakiwa kutabsamu,kujenga uzuri wa uso, kama uwa inavyojichanua ...

Kwanza alipoingia alisimama, nilijuwa kwanini kafanya hivyo, mimi nikasimama na kumkimbilia, tukakumbatiana, na akanishikilia kwa muda, hadi nikaona nijtoe maana ilizidi, baadaye mama akasema;

‘Mwanangu, pole sana na majanga, hiyo ndio mitihani ya ndoa, tulijua, hayo yatatokea, wakati mwingine mnatuzarau sie wazee, mnatuona sisi tumepitwa na wakati, na wakati wenu hamkanyiki, mnasema mna haki zenu, sasa ndio hayo yanayowakuta, lakini sasa umejifunza, na umejionea mwenyewe, ...’akasema na mimi nikakaa kimiya, na mama akaendelea kusema;

‘Nimeona sehemu mbambali wazee wakishukiwa eti ni wachawi, chuki za watu , matatizo yao binafsi yanaelekezwa kwa wazee, badaa ya kuangalia kiini cha tatizo, ambacho ni hai ngumu, ambayo haisababishwi na wazee,...watu wanafikia  kuwasingiziwa wazee uchawi, hivi watu kama hawo wanatarajia nini mbele ya mungu, tuchukulie kama sio kweli, halafu wanakwenda kumuua huyo mzee, halafu mnatarajia neema katika hii dunia,hakuna neema tena....ni laana tu’akasema

‘Mimi namshukuru mungu nimebahatika, kwetu tunajiweza, nimeolewa kwenye familia inayojiweza yenye tabia sawa na familia yetu,... sijaweza kuishi maisha ya shida,lakini wazee wengi wa kijijini, wamepitia maisha ya shida, kula yao ya shida, mazingira wanayoishi ni ya shida,...ndio maana ngozi, miili yao macho yao yanakuwa hivyo,nyie vijana mnasema hizo ni dalili za mchawi, hebu elimikeni , mumuona adui yenu ni nani,..adui yenu ni ujinga,kwanini watu hawalifahamu hilo ....’akasema mama.

Mimi ni kiongozi wa akina mama, na ni mmoja anayetetea haki za akina mama na haki za wazee, kwahiyo akiongea hivyo sikuona ni ajabu, anajisahau na kujiona yupo kwenye uwanja wake,..nikampa nafasi, aongee.

‘Mwanangu, wakati mwingine mtu unaogopa kuwa mzee, maana uzee imekuwa ni balaa,uzee umekuwa ni mtihani, ukikaribia uzee, unaanza kuwaza, huna mbele wala nyuma, matajiri wameshakunyonya vya kutosha, sasa wanakutupa, ukafe, nyumbani watoto ndio hawo tena, walikuwa wakikuangalia, sasa wanakuona ni mzigo,...majirani wanaanza kukuzushia majanga,.... wazee hawapendwi, angalia nchi za wenzetu, wazee wanatunzwa, wanaheshimika, huku kwetu Afrika ni kinyume chake,jamani tunataka nini katika hii dunia,...’akasema mama.

‘Mama lakini mimi sijawatupa wazazi wangu....’nikasema

‘Unaweza usitutupe kwa kauli lakini kwa matendo ukafanya hivyo, kama hutusikii yale tunayokuambia ina maana gani, unatuzarau,unatuona tumepitwa na wakati,...maana tunafahamu umechanganya damu na watu gani, ....ambao mwisho wa siku, watatuona hatuna maana,....sisi tunahangaika usiku na mchana kuona unaishi kwa amani, upat familia bora yenye maadili mema, tunakushauri yale tunayofahamu yatakusaidia katika maisha yako hutusikii, hiyo ni moja ya sababu kuwa hatuna maana kwako, unatuona sisi ni kikwazo kwa mambo yako, lakini sisi tuichokuwa tukikiangaia ni matunda yenu, kizazi chenu,kitakuwa vipi, sio hapo tu, kwenye starehe zenu, upendo wenu, lakini ni nini matunda ya hayo yote....’akasema mama, na baba katikisa kichwa kumkubalia mama yangu, nikajua wao walishajipanga na ajenda yao, nikakaa kimiya.

Kwa ufahamu wangu, mama hajawahi kumpinga baba waziwazi, hilo kama lilifanyika ni basi kalifanya kipindi nimeshaolewa, lakini nilipokuwa mdogo, kama kuna jambo mama haliafiki, atatafauta njia ya kumuita baba pembeni, wataongea mpaka wakubaliane, ...na wakianzisha mazungumzo hayo, wanaongea jambo walilokubaliana. Kuna wakati nilikuwa najiuliza iweje baba na mama wawe na kauli moja, ina maana wote wanafikiria jambo moja, kwakweli nilipenda sana maisha yao, na nikatamani niwe kama wao, lakini naona hiyo kwa sasa imeshindikana.

Watu wanasema mimi nimerithi sana tabia ya baba yangu, baba pamoja na kuwa kila anachokiongea mama anakiunga mkono kama vile wamefikiria pamoja, lakini kwa namna nyingine, baba alikuwa na mkali, na akitaka jambo lake lifanyike, litafanyika, lakini sio kwa nia mbayam ni kwa ushawishi, wanaweza wakakaa na mama, wakilijadili hadi wanafikia muafaka.

Tabia ambayo nimeijenga hadi leo ni tabia ya kukunja sura, baba alipenda sana kukunja sura kama hakupenda jambo, na tabia hiyo ndiyo niliyo nayo mimi, tofauti na mama, mama muda wote anatabasamu, kwake yeye anasema tabasamu ni asili ya mwanamke, ukikunja uso unaharibu sura ya uso wako, na unaulazimisha uzee kabla ya muda wako. Tabia hiyo ya kukunja sura, ilikuwa inamkera sana mama, na alipenda kusema, kwanini nakunja uso kama mwanaume...kama baba yako.

Nilimwangaia mama, mama haonyeshi kuzeeka sana, watu wanasema sura yake haifanani kabisa na umri wake, ukimuona utafikiri ni msichana, kinachomfanya aonekane ni mtu mzima ni uvaaji wake, anavaa nguo za kiutu uzima, vitenge, na sana sana anapenda kuvaa mabera, na nguo pana pana,....na kichwani huwezi kumuona kajiachia, yeye na kilemba, au kitambaa.

 Tuliachaiana na mama, huku akiendelea kuniangalia usoni, kama vile ananikagua kama nina kovu, au nin tatizo lolote, akatikisa kichwa, kama kunisikitikia, na aliporizika akageuka, kuangalia kule aliposimama baba, baba alikuwa keshasimama alipomuona mama kaingia, ni tabia ya baba, kumuheshimu yoyote. Yeye kama kaja mtu,na aikuwa kakaa, atasimama, bia kujali kuwa ni mdogo au mkubwa, atasimama, kabla hajasalimiana naye.

Nilijaribu kuangalia nje, maana nilimuona mama wakati anakuja alikuwa kaongozana na mtu, lakini wakati anaingia ukumbini, aliingia peke yake, huyo aliyekuja naye, kamuacha nje,nikataka kumuuliza huyo aliyekuwa naye ni nani, lakini nikaona nisubiri, huenda huyo aliyekuja naye ataingia baadaye, nikamwangalia mama, ambaye kwa muda huo, alikuwa kamgeukia baba , baba naye alikuwa akituangalia kwa makini, huku akijaribu kutabasamu na alipomuona mama anamwangalia akasema;

‘Maisha jamani, sikujua kuwa itafika muda, utakaa mbali na watoto wako, natamani sana siku zirudi nyuma, kipindi kile nipo pamoja na familia nzima, upo karibu na watoto na mama yao kama hivyo...lakini ndio basi tena, kila siku zinavyokwenda ndio unazidi kukimbiwa,...na naona kama ndio safari ya kuwaacha ..’akasema baba akitusogelea, tukawa tumeshikana, na mara mlango ukagongwa ,akaingia mjumbe mwingine.

     ************

Huyu alikuwa wakili wa familia ya baba, mimi niliamua kuwa na wakili wangu, kwahiyo huyo wakii wao akawa anawashughulikia wazazi wangu, mimi nilitafuta wakili wangu, amabye pia natarajia kuwa atafika, nikasalimiana na wakili huyo baada ya kusaliamiana na wazazi wangu, alipomaliza kusalimiana na mimi akasogea kukaa na baba wakawa wanaongea mambo yao, na mimi nikapata muda wa kukaa pembeni na mama, tukawa tunaongea yetu.

‘Vipi wajukuu wangu wanaendeleaje?’ akaniuliza

‘Hawajambo, wanaendelea na masomo yao...’nikasema

‘Na nyie mnapenda kuwapeleka watoto shule wakiwa wadogo, ...mtoto akimaliza shule anakuwa hajapevuka kiutu uzima, wakati wetu ukimaliza shule, unakuwa unajitambua, akili imeshapevuka, hata ikitokea bahati ukaolewa, unafahamu majukumu yako ni nini....siku hizi wanamaliza shule wadogo, lakini cha ajabu wanafahamu mambo makubwa kuliko umri wao, lakini zaidi ni yale mabaya...’akasema huku akicheka.

‘Ndio maendeleo mama, ili tupate muda wa kusoma zaidi, ili mtoto afike elimu ya juu, sio kuishia sekondari tu...’nikasema.

‘Ni kweli kama kweli watafanya hivyo, tatizo ni kuwa wanajifunza mambo ya kuwaharbu, kuliko mambo ya kuwajenga, muda mwingi wapo kwenye mitandao, na wanachoongea ni mambo yaliyo juu ya umri wao, na ni wepesi kuhadaiwa, ninawasikitikia sana, kwa vile mambo ya mitandao kwetu hayana vizuizi, wenzetu wameweka vizuizi, huwezi kuingia sehemu zote, wenztu huko ukiingia kwenye aina fuani ya mitandao, unaulizwa umri wako, na kwa vile wanavitambulisho, wana stakabadhi za kusafiria, ambazo zinathibitisha umri wao, zinawasaidia..’akasema

‘Ni kweli,...huenda na sisi wakianzisha vitambulisho vya taifa wakakuja kuvitumia kwa njia hizo, kuwa huwezi kuingia mitandao ya kikubwa, kama umri hakuruhusu, ukitaka kuingia mpaka utaje namba ya kitambulisho chako,.....’nikasema

‘Mhh, lakini kwa Wabongo, itawezekana hiyo kweli, tatizo linaanzia kwenye hawo wanaodhibiti, watakaosimamia hayo mambo, uadilifu wao una walakini,haya ikishafikia kwa watumiaji ooh,....wataiba hizo namba na kuzitumia wapendavyo, labda kuwe na namna nyingine ya zaida....tuombe mungu maana kizazi chenu kina changamoto sana, tena sana, elimu, imekuwa ghali,lakini sio elimu ya kuelimika ni elimu ya kusoma tu, ili upate kazi ....na hata hivyo,bado vichwa vyenu ni vigumu sana, kwa vile mambo yamekuwa mengi sana, .....haya niambie maisha yako na mume wako yakoje, maana yanayotokea kwako yananitoa doa, umeniabisha mwanangu?’ akaniuliza

‘Mama maisha yangu na mume wangu ni kama ulivyosikia, na nimeona kikao hiki kiwe ni muhimu ya kuliongelea hilo,nawashukuru sana kwa yote, na wakati mwingine najilaumu kuwa huenda ningelifuata maneno yenu haya yaliyotokea yasingelitokea, lakini yote ni sehemu ya maisha, hayo yalitakiwa yatokee ili iwe ni changamoto, kwangu mimi na kwa wengine, utajifunzaje bila kupitia changamoto kama hizo....’nikasema.

‘Kwahiyo wewe uwe ni sehemu ya kujifunzia, upate shida, uumie, ili wengine wajifunze, au wewe ujifunze, huoni kuwa nu kuumizana, kupoteza muda, na ni hatari, ...watu wanauana, watu wanateseka, ndivyo mnavyotaka hivyo....mimi hilo siliafiki,..kwasababu kulikuwa na njia ya kuepukana nalo,ukakaidi umekuponza uking’ang’ania kitu mpaka ukipate, ndivyo alivyo baba yako...’akasema.

‘Mama, usijali leo yote tutayaweka sawa, wewe subiria tu,....’nikasema, na tuikatishwa, kwani mlango uligongwa.

Wakaanza kuingia wajumbe wengine, akaingia wakili wangu, akafika rafiki ya mume wangu akiwa na mkewe, na baaaye akaingia mume wangu, alipofika akajibaragua, kama ujuavyo, waliokuwepo wapo hapo ni wazazi wangu, ni wakwe zake, kwahiyo alionyesha ile adabu ya ukwe...hata hivyo nilipomuangalai usoni, nilimuona hana raha, japokuwa alijitahidi kujionyesha kuwa yupo sawa, na akaanza kuwajibika kwani yeye ndiye mwenyeji wa kikao, japokuwa mimi ndiye niliyekiitisha, baadaye ainisogelea na kuniambia;

‘Ni lazime niwajibike, japokuwa wewe ndiye umeitisha hiki kikao, kama mume wako ninawajibika  hivyo, unakumbuka kwenye mkataba wetu unasemaje, mume anatakiwa kuwajibika kwa ajili ya familia, au sio?’ akawa naniuliza, mimi nikatabsamu, na kusema;

‘Mkataba upi unaouzungumzia, wa zamani au mpya?’ nikamuuliza huku nikitabasamu,hapo akasita na baadaye akasema;

‘Hakuna mkataba mpya na wa zamani, hiyo kauli unaiotoa...’akasema na hapo nikajua hajafahamu kuwa nimeshaupata ule mkataba wenu wa asili.

‘Tutaona..muda ukifika hilo litasahihishwa, ...nenda kafungue kikao,’nikasema nay eye bila kusita akaenda mbele na kusalimia watu akafungua kikao, na kumkaribisha mwenyekiti wa kikao, ambaye ni baba, kikawaida kwenye familia yetu, kukiwepo na kikao kama hicho mwenyekiti ni baba, japokuwa mara kwa mara, anasema hilo jukumu sasa litakuwa ni letu.

Baba hakuenda mbele , alikaa pale pale, kwanza alianza kufungua makabrsha yake, na kabla hajasema neno, mlango ukagongwa, na kwa vile wote tulijua kuwa tumekamilika, hatukutarajia mtu mpya, kujitokeza tena, kwahiyo hiyo hali ikatufanya, sote tugeuke na kuangalia mlangoni, kuona ni nani huyo anayeingilia, na kikao hiki hakimuhusu, mlango ukafungulia, akaingia mtu akiwa amevalia kofia la waendesha pikipiki, na alipoingia akalivua kofia lake....

NB: Haya mambo yanaendelea tuwe pamoja.


WAZO LA LEO: Nakumbuka babu yangu alisema; ‘Uongozi ni wito, uongozi ni kubeba dhamana za watu, na ukiwa kiongozi mwadilifu, watu wako ni kwanza, na wewe unakuja baadaye, kwahiyo kimasilahi, utahakikisha kuwa watu wako wametosheka kwanza, kabla ya kujali tumbo lako, huo ndio uongozi bora. Je kiongozi kama huyo yupo katika hii dunia ya sasa,...Ndio maana tunasema Mandela alikuwa kiongozi wa kweli, kwani yeye alijaribu kulifanya hilo.

Ni mimi: emu-three

No comments :