Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 5, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-41Nilipokuwa nyumbani, nilijikuta nikiwazia mazungumzo yangu na docta, na nilishindwa kuhakiki mawazo yangu ambayo yalinituma kuwa huenda ameshapona na mengi aliyoyafanya alikuwa na akili timamu, lakini kila nikiwaza zaidi najikuta nikiamini kuwa huenda mume wangu ana ajenda ya siri, na huenda yote aliyoyafanya alifahamu ni kitu gani amekifanya.

Docta alithibitisha kuwa mume wangu anaumwa, na kama alitoroka siku hiyo, basi huenda ni wakati akiwa katika hali yake, na hilo halitaweza kuthibitishwa kitaalamu kuwa alikuwa haumwi, wakati yeye kama docta alimuona abdo anaumwa.

‘Lakini alionekana nje ya hospitali yako, akiwa mzima’nikasema

‘Mimi sina ushahidi wa hilo, na wote niliowauliza hawana ushahidi wa hilo,...huenda alitoroka sawa, lakini tutathibitishaje...’akasema

‘Docta unafahamu kuwa hilo ni kosa, na limetendeka kwenye hospitali yako, kumbe wagonjwa wanaweza kutoroka na kwenda kufanya uhalifu na nyie msifahamu ...’nikasema

‘Ni nani kakuambia kuwa mume wako alitoroka, ...?’ akaniuliza

‘Polisi wana taarifa hizo, na kuna vielelezo, vinavyoonyesha kuwa siku hiyo alitoroka ...’nikasema

‘Itakuwa ajabu kweli kweli, na inabidi linifanyie uchunguzi, maana mwanzoni sikulichukulia maanani maana sikuamini kuwa kweli ilitokea hivyo,....nilimuuliza akanikatilia kata kata, na mimi nikamwamini...’akasema.

‘Docta unakumbuka kuna kesi ya kuwawa Makabrasha..’nikasema

‘Ndio niliisikia, yule jamaa alikuwa na maadui wengi sana,...nimesikia watu wakimuongelea, kumbe ule uwakili wake alikuwa akiutumia vibaya...’akasema

‘Ndivyo watu wanavyosema, kama marehemu sina cha kumuelezea, ila aliuwawa, na polisi wanafutilia kujua ni nani aliyemuua,..’nikasema

‘Sasa mume wako anahusika vipi?’ akaniuliza

‘Polisi,wanahisi kuwa mume wangu alikuwepo kwa Makabrasha siku hiyo, na wanasita kuja kumuhoji kwa vile bado mgonjwa,...na ili kuthibitisha hilo, watakuja kukuhoji na wewe mwenyewe,...’nikasema.

‘Mimi sina cha kuwaambia, maana hakuna ushahidi kuwa alitoroka...watu wangu wamesema muda wote walimuona akiwa hapa hospitalini, na yeye mwenyewe kasema hivyo,...sasa siwezi kusema lolote mpaka nifanye uchunguzi wa kina..’akasema

‘Mimi nimekutonya tu, kuwa kuna kitu kama hicho, ....usije ukashitukiziwa, na hao wasaidizi wako wawe na uhakika na hilo, kwani kama itagundulikana kuwa mume wangu kweli alitoroka,kwanza ni kosa kwa ofisi yako kuwa hakuna ulinzi wa kutosha, lakini pia mtajikuta kwenye matatizo, kuwa mnahusika kwa namna moja au nyingine kwenye mauaji ya Makabrasha...’nikasema.

‘Hilo haliniingii akilini, hata hivyo, sisi hatuna mkataba wa kumlinda mgonjwa kiasi hicho, kwani wagonjwa wanaoletwa hapa sio kwamba wamechanganyikiwa kiasi cha kulindwa, wanafahamu sheria na taratibu, mume wako hakuchanganyikiwa kiasi cha kulindwa...na kipindi kile, alikuwa hawezi kupanda vitu kama pikipiki...’akasema.

‘Mimi sina zaidi, kama nyie mnalithibitisha hivyo, basi ...jiandaeni kwa hayo majibu, na sina uhakika wa hilo wa moja kwa moja, ila kuna uwezekano wa polisi kuja kukuhoji,...’nikasema na kuinuka kuondoka zangu.

**********

Wakati naendelea kusoma diary ya shemeji yangu, nilifika sehemu inyoelezea tukio la usiku wa ajabu, yeye alindika hivyo, tukio la usiku wa maajabu, anasema siku hiyo hataweza kuisahau maana ni siku ambayo alionja asali....hakuelezea zaidi,...

‘Alionja asali...ni asali gani, na usiku huo ni usiku gani, kwanini akauita ni usiku wa maajabu, nikaendelea kusoma, niliangalia tarehe ya huo usiku wa ,maajabu, nikaona ni siku nyingi kidogo, sikutilia maanani sehemu hiyo,kwani huyo ni kijana ana mambo mengi, nikafika sehemu nyingine anasema;

‘Hivi kijana kama mimi ninaweza kumpenda mwanamke aliyenizidi umri, ...mbona nimetokea kuwapenda wanawake wakubwa, tena..wengine wake za watu...’aliandika akaachia hivyo, sikuelewa ana maana gani, inavyoonyesha ni kuwa alikuwa akiandika kwa kifupi, anachoelewa yeye mwenyewe....

Nikafika sehemu nyingine kaandika hivi,; mpendwa alinipigia simu, akaniambia kuwa ana mazungumzo muhimu na mimi,...sikupenda mambo yake, nahisi yatanipeleka kubaya, japokuwa namuonea huruma sana...mambo aliyofanyiwa na kaka mkubwa sio mazuri, ...’akaandika hivyo

‘Mpendwa hana raha, anasema kuna siri zimegundulikana zinamuweka pabaya, zikivuja yupo matatani, na kaka mkubwa anazifahamu, na kamtishia kuziweka hadharani, anaogopa, ananiomba ushauri...’akamalizia hivyo

Nikajiuliza kimoyo moyo, huyu mpendwa ni nani naona sehemu nyingi katajwa kwa neno hilo mpendwa, na majina hayakuandikwa, je ni rafiki yangu,....au ni ..mmmh, sina uhakika ngoja niendelee kusoma;

‘Mpendwa kasema hawezi kuvumilia, inabidi afanye anavyotaka kaka mkubwa, lakini inamuuma sana, hana jinsi anakuwa kama mtumwa wa kuzalilika, na anaogopa kuwa itakuaj kujulikana, na ndoa yake itavunjika, na huenda ikaathiri na watu wengine....’akamaliza hivyo

‘Huyu mpendwa ni nani,....kumbe ni mke wa mtu....’nikasema kimoyomoyo huku nikisoma maelezo mengine, ambayo aliendelea kuandika kifupi kifupi, nikafika sehemu anaelezea, alivyokutana na mpendwa, aliandika hivi;

‘Mpendwa anataka kuniingiza majaribuni,....anataka kufanya jambo ambalo mimi siliwezi, na anachotaka kutoka kwangu ni kikubwa sana, naogopa na sijui kama nitaweza kumtimizia malengo yake, sijui ana kusudia kufanya nini...mimi siwezi,...lakini sipendi kumkatalia...nampenda sana japo ni mke wa mtu...’akaweka alama za kuuliza

‘Mpendwa kanituma...sijui kama nitaweza, na kama nikiweza sijui kama nitashirikiana naye, na je ni nini lengo lake, na kwanini....’akaachia hivyo

‘Mpendwa kanitosa, ...sijui kafanya nini, sijui anashirikiana na nani,...je anahusika, na kwanini hataki kuniambia ukweli...nitajitahidi nifahamu kulikoni...namuonea huruma sana,’akaachia hivyo.

‘Kaka kaniita na kunitaka nimpeleke mahali,...mimi naogopa, maana hali yake bado ni tete, je anataka nini, ..nitafanya hivyo ili kutokumsababishia mambo mengina.’akaacha hivyo na hapo nikaangalia tarehe, ni siku ile ile aliyouwawa Makabrasha...ni kweli , kumbe ni kweli, mume wangu alitoka na mdogo wake.

‘Nikiwa njiani kaniambia anafuatilia maswala ya mkataba, na anasema mkataba ni mzuri wenye malengo mazuri, lakini mimi niliona ni dhuluma, hata hivyo kaka mkubwa, kasema atatusaidia, na kwa vile anajua sheria, tumtegemee yeye...ila gharama zake ni kubwa sana, ..mimi sikubaliani na hilo,lakini kaka anasema hana jinsi ni lazima tukubaliane naye kwani kashika mpini, swali la kujiuliza ni kwanini kaka anakubali kirahisi hivyo, mimi ninahisi kuna jambo, ni lazima nilijue...’akachia hapo.

‘Wakati tunafika, nilimuona mpendwa akitoka, alikuwa akisafiri, sikuwa na haja naye,mawazo yalikuwa kwa kaka, kwanini kataka nimlete hapo,..na nilikumbuka maagizo ya mpendwa, na mzigo wake nilikuwa nao, alisema atasaidia kuzuia hayo kaka anayotaka kuyafanya....

‘Kaka yupo kwenye hali ngumu, anaonekana kabanwa na kaka mkubwa, inabidi akubali kusaini mkataba wenye mamlaka makubwa kwa kaka mkubwa...ina maana mwisho wa siku kile kitu kitachukuliwa na kaka mkubwa, sasa ina maana gani, na kwanini kaka anakubali kirahisi hivyo, mimi sikubali, ni lazima nimsaidie kaka...’

‘Yote sasa yanategemea juhudi za mpendwa,..’nikawa najiuliza mbona nyuma kaandika kuwa mpendwa anasafiri, kamuona akitoka na mizigo, ...sasa vipi tena, hapo sikuelewa, huenda nitapata hayo majibu huko mbele, na wakati nataka kusoma zaidi mara simu yangu ikaita...

Simu ilipolia, nilizima lap top yangu haraka nikiwa na lengo la kuendelea kusoma baadaye, sikutaka nisome kwa haraka, nilitaka nisome kwa makini, kwani vilivyoandikwa hapo vinaweza kunisaidia, japokuwa vimeandikwa kwa kifupi kifupi. Nilihakikisha nimezima laptop yangu kwanza kabla sijaipokea hiyo simu,...

Niliangalia jina la mpigaji, lakini kulikuwa hakuna jina, wala namba, ya mpigaji ina maana huyo mpigaji hakutaka ajulikane ni nani,nikaiweka hewani na kutulia kidogo ili mpigaji aanze yeye kuongea, nay eye akakaa kimiya, nikauliza;

‘Wewe ni nani?’ nikauliza

‘Mwambie kaka mimi nipo salama, nitakuja mambo yakiwa shwari,nafahamu umeshafahamu kuwa nipo kwenye matatizo, na kuhusu mengi uliyoniuliza, nafahamu hadi sasa umeshapata majibu yake, japokuwa nilivyoandika naelewa mimi mwenyewe, sina zaidi ya hayo, ninachokuomba ni kumlinda kaka yangu....hana hatia, ...’akasema

‘Upo wapi?’ nikauliza

‘Usitake kujua nipo wapi nipo popote, pale, nafahamu huenda simu zangu zikawa zinafuatiliwa, lakini nakuhakikishia kuwa nipo salama, hawo watu hawawezi kufahamu mahali nilipo, na nikitoka hapa, sitapatikana tena, ..’akasema.

‘Usijidanganye, kwanini unakimbia, una kosa gani, rudi mimi nitakusaidia...’nikasema

‘Umeshindwa kumsaidia kaka, ndio utaweza kunisaidia mimi, ...ninachokuomba ni wewe umsaidie kaka yangu, yeye hajui lolote kuhusu hayo hao watu wanayoyatafuta. Na hajui kabisa aliyefanya hivyo ni nani,..hata mimi sina uhakika ni nani aliyefanya hivyo, ...japokuwa silaha iliyotumika niliichukua mimi, mengine utayaona, humo humo, sijui kama yatakusaidia lolote, nayafahamu mwenyewe...tafadhali, usije ukawapa hao watu hayo mambo yangu kwani kuna mambo yangu binafsi, ...’akakata simu.

*******

Niliangalia saa yangu huku nikiangalia ratiba ya wageni, wanaofika kwa ndege, na mimi nilikuwa nimekuja rasimi kumpokea mgeni wangu, japokuwa mgeni mwenyewe hakuwahi kuniambia nije kumpokea, na wala hafahamu kuwa mimi ndiye nimekuja kumpokea, lakini nina uhakika anafika leo.

Kufahamu siku ya kufika huyo mgeni ilitokea kama nadra tu, maana siku hiyo nilikwenda nyumbani anapoishi rafiki yangu, nikiwa na malengo ya kuhakiki uchunguzi wangu, kutokana na maelezo niliyoyasoma kwenye diary ya shemeji yangu.

 Nilifika hapo alipokuwa akiishi rafiki yangu kabla hajaondoka, kusoma, yeye kabla ya kuondoka alikuwa akiishi na mwanadada mmoja, ambaye wana udugu naye, japokuwa hawakuazaliwa tumbo moja, niliongea naye kidogo, kwa vile alikuwa kwenye duka lake , mara kwa mara alikuwa akitoka kuongea na wateja wake, na kuna muda alitoka na simu yake ikaonyesha kuwa kuna ujumbe umeingia,,...sio kawaida yangu, lakini hamasa ikanijia kwani pale simu ilipowekwa niliweza kuona maelezo ya kwanza kuwa ni ujumbe, unatoka kwenye namba...

‘Mbona hii namba ni ya nje, na ni namba ya rafiki yangu..ooh, samhani itabidi nifanye hivi.’nikasema kimoyo moyo, nikajikuta nikiichukua ile simu na kusoma ule ujumbe..

‘Ndugu yangu ninakuja kesho, nipokee uwanja wa usiku saa mbili, usimwambie mtu yoyote...’mwisho wa ujumbe

Nilipohakikisha kuwa ni huyo rafiki yangu, nikaufuta ule ujumbe, nikahakikisha haupo kwenye sehemu yoyote kwenye ile simu, halafu nikairudiha ile simu pale pale, na mara akaingia huyo mwenyeji wangu.

‘Nilisikia kama mlio wa simu, mlio wa kuingia ujumbe kwenye simu...’ akasema huku akiangalia simu yake, na alipoona hakuna ujumbe akaniangalia na kuniuliza.

‘Simu yako ina mlio kama wa kwangu nini, maana nina uhakika kuna mlio wa simu nimeusikia, na hapa kwanu hakuna ujumbe ulioingia?’ akauliza huku akiiweka simu yake pale alipoiweka awali.

‘Ndio kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu, huenda ndio uliousikia, naona una kazi nyingi, ngoja mimi niondoke, nitakuja wakati mwingine,...’nikasema

‘Hapana usiondoke, mimi siku zote ni hivi hivi, hata akija mgeni tunaongea hivi hivi,hebu niambie ni kitu gani ulikuja kuniuliza umesema unataka kuniuliza kitu...’akasema

‘Nilitaka kufahamu ni lini rafiki yangu anakuja, shoga yako...’nikasema

‘Alisema atanifahamisha leo, ni lini anakuja, hajanipigia au kunitumia ujumbe, ....sina uhakika ni lini hasa, unamfahamu zake, yule ni shushu wa kimataifa umemjenga wewe mwenyewe, hasemi lini anakuja, ....anasubiria akiwa tayari kupanda ndege, ndio anakuambia,au kama kuna kituo njiani, anaongia kwenye intarnet cafĂ©, ndio anatuma ujumbe...’akasema.

‘Hamna shida,...kama ningelifahamu ni lini anakuja ningeenda mwenyewe kumpokea, ..’nikasema

‘Mhh, mara nyingi hapendi mtu mwingine kumpokea, ni mimi tu...sijui kwanini, nashangaa hata wewe hakuambii, wakati wewe ni rafiki yake mkubwa..’akasema

‘Kila mtu ana hulka zake....labda ana maana yake...’nikasema

‘Nina hamu sana ya kumuona mtoto wake, maana alivyo mzuri,...na hakutaka kabisa watu wamuone, mimi nilibahatika tu kwa vile alikuwa yupo hapa kwangu, tena nilimuona kwa kujiiba, hakutaka hata mimi nimuone...’akasema.

‘Kwanini alikuwa akifanya hivyo, hata wewe hakutaka umuone, naona ajabu sana...?’ nikauliza.

‘Nahisi haniamini, ...lakini utamficha mtoto mpaka lini, maana sura haibadiliki, ....’akasema

‘Mhh, kwani ulivyomuona mtoto wake anafanana na nani?’ nikajikuta nikimuuliza hivyo

‘Mhh, watotow adogo wote hufanana, mimi nilimuona kama anafanana na watoto wako...yaani kabisa, utafikiri baba yao ni mmoja, ...’akasema

‘Labda baba yao ni mmoja, huwezi jua...’nikasema

‘Hapana, hawezi kufanya hivyo, japokuwa mmmh,....mume wako naye, mambo yake ya chini kwa chini,....’akabenua mdomo nikajua kuna umbea hapo unataka kutembea, nikauliza

‘Kwanini unasema hivyo?’ nikauliza

‘Hata mimi ipo siku alinijia, akaanza zake, sikuamini, nikamtolea nje, baadaye akajirudi na kusema alikuwa ananitania tu, lakini mtu akikutania unamfahamu,...hata hivyo alikuwa kalewa nikamsamehe, na kama angeliingia anga zangu, angekoma ubishi...’akasema

‘Kwahiyo alikutongoza?’ nikamuuliza

‘Sio mara moja,....ana bahati sana, ni kwa vile nakuheshimu sana wewe, na kumuheshimu rafiki yako, vinginevyo, ....utajiri wake tungegawana, ....’akasema.

‘Ungefanya nini, kwani kutembea na mtu ni lazima magawane utajiri? Nikaanza kumdadisi

‘Sisi ambao hatuna waume, tunafahamu sana mambo mengi, kuliko nyie mliopo kwenye ndoa, hasa mimi ambaye nilionja ndoa nikaachika, nafahamu jinsi gani ya kumchuna mwanaume,...hasa akiwa an pesa, na hawezi mume wa mtu aje kwangu nimkaribishe bure, hasa akiwa tajiri, nitahakikisha anakung’uta mfuko, anafunga akaunti yake ya benki, wananiogopa hawo watu....’akasema.

‘Kwahiyo wewe na shoga yako ndio tabia yenu, ndio maana kaamua kuniingilia kwa mume wangu?’ nikamuuliza

‘Hayo anayajua yeye mwenyewe, na kama kafanya hivyo, nitamshangaa sana, maana yule ni sawa na mdogo wako,...lakini dunia hii ina mengi, huenda walipokuwa huko wakilewa, yaliwashinda, na kwa vile mume wako anaonekana ana njaa ya .....hahaha, nisikuumize bure’akaanza kucheka, na mimi nikamuuliza.

‘Ulijuaje kuwa ana njaa?’ nikamuuliza

‘Mwanaume mwenye njaa, ...tamaa utamfahamu tu...mimi niliachana na mume wangu kwa mambo hayo hayo...na sitaki kuolewa tena, maana kuna wanaume hawashibi,...hata uwafanyie nini....sasa niliona nimpe nafasi hiyo, atembee kila nyumba ale weeeh, akishiba ndio atatulia, ataoa, lakini sio aje kunioa mimi tena, maana hata mimi sasa sishibi, bado nadai...’akasema.

‘Je mume wangu aliwahi kukuambia hivyo, kuwa hashibi?’ nikamuuliza

‘Sijawahi kumpa nafsi ya kuongea namimi kihivyo, maana simuhitaji, nakuheshimu, nawaheshimu watu wake...sikutaka tu, lakini kama ningelitaka ningeshampata na kama angeliingia anga zangu, nina uhakika angening’ang’ania kama ruba ....nakuheshimu wewe tu....siwezi kukuvunjia heshima yako, unafahamu mimi nakujali sana, umenisaidia mambo mengi, na siwezi hata siku moja kukuvunjia heshima yako...’akasema.

‘Nashukuru kusikia hivyo, angalau wewe umeniambia ukweli...na je ulishawahi kumuona shemeji yangu hivi karibuni?’ nikamuuliza

‘Unasema mdogo wa mume wako?’ akauliza

‘Ndio....’nikasema

‘Jana tu nilikuwa naye hapa nyumbani...’akasema

‘Oh, ina maana yupo hapa Dar,...?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Angeenda wapi yule, yule ni mtoto wa mjini bwana,...ni mjanja hutaamini, namtumia sana kwenye biashara zangu, ananitafutia wateja wa hapa na pale, ninachomsifia ni mwaminifu, akipata pesa zangu ananiletea, sina wasiwasi naye...’akasema

‘Lina anatarajia kuja hapa kwako?’ nikamuuliza

‘Hilo sina uhakika, .....huwa kama kuna mteja wangu anamfahamu, na nikamtuma kuniletea pesa  zangi ndio anafika, na wakati mwingine alikuwa akifika kama katumwa na kaka yake kukutana na mwenzake hapa.....’akatabasamu kwa kebehi.

‘Mwenzake ndio nani huyo?’ nikamuuliza

‘Utaajza mwenyewe, ndivyo maisha yalivyo, tatizo nyie mlioolewa mnataka kushiba wenyewe, sasa sisi tutakula wapi, hamtuonei huruma, mjini hapa , tutabanana kiaina ....heheheeee’akasema huku akicheka kile kicheko cha akina dada

‘Ina maana , kumbe walikuwa wakikutania hapa, yeye na mume wangu eeh...’nikasema

‘Hayo sijakuambia mimi, usije ukaniletea kesi, aaah, mimi hayo siyajui,....ngoja nisije kuitwa mbeya,akija wewe umuulize mwenyewe, hivi wewe fisi nambuzi watakuwa wakitembea na kukaa pamoja muda wote, wasitafunane, nani kakudanganya...., ni rafiki yako ndio , na ni rafiki wa kweli kweli au sio, basi kama ni rafiki wa kweli kweli, ukubali mchangie kile kitu, na mimi sioni ajabu, ndivyo maisha yalivyo, tupendane kiukweli-kweli, au sio,  ...hahahaha...utajiju’akasema na kutoa kicheko cha dharau, sikupendezewa , hasira zilinipanda, na sikutaka kuongea naye sana

‘Niambie ukweli, maana wewe ni mtu wangu, je ni kweli ndugu yako alikuwa na mafungamano ya ukaribu na mume wangu,..na walikuwa wakikutana hapa kwako?’ nikamuuliza nikionyesha hasira

‘Hahahaha...acha wivu bwana, nikuambie ukweli shoga yangu, usihangaike na wanaume, wanaume ni kama kuku wa kienyeji, kila anayekutana naye, ni wake...ukiwachunguza sana, utakufa kabla muda sio wako...akiwa kwako ni wako, akitoka nje ni wakila mtu,..’akajishika kiunoni kama ananiringishia, halafu akasema;

‘Nikuambie shoga, ...hiyo iweke moyoni, mume hana mke akiwa nje, ...na wewe ukiweza fanya hivyo, lakini chunga sana.....maana sisi wanawake tuna kamba mguuni, unasikia sana, sio sawa na wanaume..hahaha, utajibeba, ..utanyidoa....na toto lake sawa sawa na watoto wako, hapo unataka nikuambie nini tena...mimi usinihusishe...kwaheri.’akasema kama ananinong’oneza.

Niliumia sana, hasira chuki vilitawala moyoni mwangu, nikaapa kufanya jamb ambalo halijawahi kufanyika,

*******

‘Ndege inayotoka Ulaya inaingia.....’sauti  ya mtu aliyekuwa jirani yangu ilisikika na kunikatiza mawazo yangu nikainuka kwa haraka na kuelekea sehemu ya kupokelea wageni, nikiwa na hamu sana ya kumpokea aliyekuwa rafiki yangu yangu..sikupenda sana kumuita rafiki tena, kwani hastahili kupewa cheo kama hicho. Niliamua kuja kumpokea nikiwa na yangu moyoni, sikuwa na utani tena na hawa watu, kwani ushahidi nilioupata unatosha, ..

Nilikumbuka nilipoongea na wale mabaunsa ambao nilishapanga nao, nia ni kumesha mtu kama huyo, ambaye anaishi kwa kuiba waume za watu, na wao wakaniambia wapo tayari, nikiwa tayari nitawaambia huyo mtu ni nani na anapatikana wapi,...

‘Ninaweza kumpeka ile sehemu niliyowaelekeza awali, kana itawezekana, ikishindikana, nitawaachia nyie mfanye mnavyoweza.....ila sitaku ile ya kumharibu kabisa, ni kiasi cha kumpa fundisho tu....’ niliwaambia.

‘Sisi tunakusikiliza wewe, kama vipi wewe tuambie ni nani , sisi tutajua jinsi gani ya kumpata, cha muhimu ni pesa,....’ wakasema.

‘Pesa sio tatizo, muhimu hiyo kazi ifanyike kwanza..’nikasema

‘Dada wewe mwenyewe utasikia kwenye bomba, sisi hiyo kazi  sio mara ya kwanza kuifanya, watu kama hawo ni lazima tuwafundishe adabu, ...tuna jinsi zetu za kuwawezea, hata awe mjanja vipi, ...hiyo kazi tuachie sisi, tukimalizana naye, atakimbia huu mji kama ataweza kuhimili mambo yetu na wengi tuliowafanyia hivyo, walikimbilia kunywa sumu...’akasema huyo kiongozi wao

‘Mimi sitaki mumuue, mumesikia, nataka atie adabu, akione cha moto,..’nikasema.

‘Hatumui, kama ni kujiua atajiua mwenyewe, maana kasheshe yake sio mchezo, anaweza asiweze kutembea wiki, wewe ulishawahi kusikia mambo tuyayofanya, polisi ni jamaa zetu, kwani wanafahamu tunalolifanya, ni kuwatia adabu watu kama hao, tukimaliza hiyo kazi, tunapotea kwa muda, tukitumia pesa zetu.....’wakasema.

‘Mkimaliza kazi, pesa yenu mtapata, anatarajia kufika leo toka Ulaya, nitawaelekeza wapi pa kukutana naye, mengine mnajua nyie,....’nikasema.

‘Sawa tunasubiri kutoka kwako....usituvunge tena kama kipindi kile, ulituambia tukasubiria lakini hukutuambia ni nani’akasema huyo kiongozi wao.

Mara abiria kutoka ulaya wakaanza kuingia, na mmoja mmoja akawa anachukua mizigo yake, na kutoka, na ilikuwa kama rafiki yangu hakuwepo kwenye hiyo ndege, lakini mwishoni nikamuona alikuwa kihangaika na mtoto, naona mtoto wake alikuwa akimsumbua, akafika sehemu ya kuchukulia mizigo, akachukua mabegi yake, yalikuwa mawili makubwa, na wakawa wanazozana na mkaguzi , huyo mkaguzi alikuwa akidai pesa, kwani ile mizigo ilikuwa imezidi uzito...

Mimi nikasogea karibu kiasi cha kuweza kuongea, japokuwa tulikuwa kwa nje na wao wako kwa ndani, isingeliruhusiwa mimi kama mpokeaji kuingia sehemu ile ya ndani, nikauliza;

‘Kiasi gani unadai kwa huo uzito ulizidi?’ nikauliza na yule mkaguzi akataja, nikampa pesa yake, na rafiki yangu akaruhusiwa kutoka, na mizigo yake, alionekana kushangaa sana kuniona , na hakusema kitu hadi mizigo yake ilipotolewa nje, na mimi nikamwambia.

‘Karibu bongo..’nikasema na yeye akatabasamu kidogo, halafu akauliza

‘Umekuja kumpokea nani?’ akauliza

‘Nimekuja kukupokea wewe, ....’nikasema

‘Ulijuaje kuwa nakuja leo?’ akauliza kwa mshangao

‘Wewe ni mfanyakazi kazi kwenye kampuni yangu, umeenda kusoma kwa kibali changu, isitoshe wewe ni rafiki yangu, nimeishi na wewe na kujitolea kukusaidia kama mdogo wangu, na zaidi ya hayo nasikia kuwa weweni mke mwenza, kwanini nisihindwe kufahamu lini unafika,....’nikasema na yeye akaguna na kusema;

‘Mhh, imekuwa hayo, mbona unanitisha, hata hivyo nashukuru kwa kuja kunipokea, lakini kuna ndugu yangu anakuja  kunipokea...’akasema

‘Ndugu yako hatafika, nimefika mimi badili yake, yeye  ana kazi zake za kumalizia, hakuna shida, nipo hapa kwa ajili yako, na nitahakikisha unafika kunapohusika, unakumbuka ahadi yangu?’ nikamuuliza

‘Ahadi gani?’ akauliza na mimi nikatabasamu, huku nikiwaonyesha wabeba mizigo wapi gari langu lipo, nikasema;

‘Gari langu lipo tayari, mimi nimeona ni muhimu nikuwahi mapema, maana ahadi ni deni, au sio..., ....’nikasema

‘Ahadi gani mbona sikuelewi, ...’akasema huku akiwa kasimama,

‘Twende bwana,...unaifahamu sana hiyo ahadi, unaijua sana,’nikasema na yeye akawa hasogei pale aliposimama,  halafu akasema ;

‘Mimi siondoki na wewe, nitaondoka kwa taksi, naona una lako jambo,...kauli yako inanitisha’akasema

‘Usipoondoka na mimi , utaondoka na polisi, ukumbuke siku Makabrasha anauwawa, ulikuwepo, umesahau eeh,..’nikasema na aliposikia hivyo akashituka, na kuniangalia kwa mshangao, akasema

‘Mhh, hayo sasa makubwa, ni nani kanivumishia huo uwongo,mimi niliondoka akiwa hai, taarifa za kifo chake nimezipata wakati nimeshafika Ulaya...’akasema

‘Tutaongea ndani ya gari, twende zetu...’akaanza kutembea kuelekea kwenye gari langu, na mizigo yake ikawekwa nyuma kwenye buti la gari yangu, na yeye akaingia kwenye gari moyoni nikasema;

‘Bado mmoja....wewe sasa umeshaingia kwenye mitego yangu,  ...’nikasema kimoyo moyo. Kabla sijaingia kwenye gari nikainua simu na kuwapigia watu;

‘Muwe tayari, ....keshafika, nitawaambia ni nani, tukifika kwao, fuatilieni gari langu, nitapitia ile njia niliyowaelekeza, mengine mtajua nyie....’nikasema.
‘Sisi tupo tayari bosi....’wakasema

Nikaingia kwenye gari na kuanza kuondoka

NB: Je hayo yatafanyika, itakuwaje, tuzidi kuwemo, 


WAZO LA LEO: Tuweni makini sana, kwenye maswala ya kulipiza kisasi, tunapofanyiwa mabaya, kwanza tuwe na subira, tuhakiki huo ubaya,tukimtegemea mungu, kwani huenda ubaya huo ukawa na ujumbe kwako, ukikimbilia kulipa kisasi unaweza ukajiingiza kwenye matatizo makubwa ambayo hukutegemea, na majuto huja baadaye, majuto ni mjukuu.
Ni mimi: emu-three

No comments :