Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 4, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-40Docta aliniangalia na baadaye akamwangalia mume wangu, akahisi kuna kutokuelewana kati ya ngu na mume wangu, akageuka kumwangalia mume wangu akamuona insi alivyokuwa, mimi sikujali, kama ingelikuwa ni kipindi kile cha nyuma ningeliingiwa na wasiwasi kuwa nimechokoza matatizo ya mume wangu, lakini kwa hivi sasa moyo wangu ulishainingiwa na kutu, na kuona kuwa huenda mume wangu anaigiza kuumwa,...

Lakini sikuwa na uhakika na dhana yangu hiyo, huenda kweli mume wangu anaumwa, lakini sijui kitu gani kilikuwa kimeniingia akilini, nilikuwa nimefikia hatua ya kuwaza hivyo, kuwa huenda anaigiza kuumwa, alishapona ...lakini kwa mipango yake huenda kaamua kufanya hivyo,...naliona kama ubinadamu umenitoka dhidi ya mume wangu.chuki ilishanitawala na sikuwa na muda wa kuipooza, ....

‘Kuna tatizo lolote...?’ akauliza docta, akiniangalia, halafu akamwangalia mume wangu.

‘Muuulize mgonjwa wako, mimi sina tatizo ...’nikasema na kugeuka kama nataka kuondoka

‘Hakuna tatizo docta, ni mambo ya kifamilia...’akasema mume wangu.

‘Lakini tulishakuambia kuwa mambo ya kifamilia uyaweke pembeni, hapa ni afya yako tu, je ukifa ni nani ataangalia hayo ya kifamilia...?’ akauliza

‘Nimekuelewa docta, hakuna tatizo...’akasema mume wangu na mimi nikageuka mara moja kumwangalia mume wangu ambaye na yeye aliniangalia, na uso wake ulionyesha hasira, mimi sikujali, nikageuka kumwangalia docta;

‘Docta mgonjwa anaendeleaje maana nimeongea naye tu?’ nikauliza

‘Kwa ujumla anaendelea vyema, na wiki hii tutaangalia, kama hali ni hii hii, ni bora tu arudi nyumbani, na cha muhimu na yeye kutimiza yale tuliyomuagiza, apunguze hasira, asiwe na mawazo, yaani ajiepusha nayale yote yanayoleta mashinikizo ya damu,....yeye mwenyewe keshaelewa...’akasema docta.

‘Lakini kumbukumbu na kila kitu sasa kipo kama kawaida?’ nikauliza

‘Kipo kama kawaida, ....haijatokea tatizo kuhusu hilo, na tutaangalai wiki hii, ‘akasema

‘Sawa nitakuja ofisini kwako tuongee kidogo...’nikasema

‘Karibu sana,...’akasema huku akimwangalia mgonjwa wake, ili kuhakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, na alipomaliza, akaondoka, na mimi nikabakai na mume wangu, nikasema;

‘Sasa mimi naona niondoke, kuna zaidi , kuna kitu unahitaji?’ nikamuuliza

‘Hakuna zaidi, ....nitafurahi kama utampata mdogo wangu, na ukimuona mwambia aje tuonane’akasema

‘Nitafanmya hivyo,...na nasikia rafiki yangu, anarudi karibuni’nikasema.

‘Keshamaliza kusoma, mbona mapema hivyo...’akasema akionyesha furaha usoni.

‘Mapema, kwa kitu ambacho hukuwa makini nacho, lakini kiratiba ni muda sasa,..’nikasema.

‘Kwahiyo anarudi lini?’ akauliza

‘Natumai wiki ijayo..’nikasema

‘Muda huo nitakuwa nyumbani,...hakuna shida...’akasema
‘Na mtoto wake atakuwa mkubwa sasa...’nikaanza kuchokoza

‘Ni kweli watoto hawakawii kukua,..’akasema huku akionyesha kuwaza jambo.

‘Sijui baba yake atakuwa  nani maana rafiki yangu kanificha kabisa..’nikasema.

‘Mzazi hafichwi,baba yake yupo na atajulikana tu, ...’akasema.

‘Yeye kasema mtoto wake hana baba, hata jina kaandika la kwake, yaani jina la mtoto na kwa baba yake, kaandika jina la babu yake’akasema.

‘Thubutu, huyo anajidanganya, baba yake yupo, hata akificha vipi, ..’akasema akionyesha kukerwa.

‘Wewe unamfahamu baba yake?’ nikamuuliza

‘Kama wewe humfahamu, mimi nitamfahamu vipi, hiyo ni siri yake, lakini nafahamu kuwa kila mtoto ana baba yake’akasema.

‘Lakini yeye kasema mtoto wake hana baba, kwani hakutaka baba yake ajulikane, na alifanya hivyo makusudi, apate mtoto, na sio kuwa na mtu mwingine anayeitwa baba, ni maamuzi yake, huwezi kumuingilia’nikasema.

‘Hilo anasema tu kwa watu wengine, lakini yule mtoto ana baba, na hilo yeye anafahamu, ni kuwahadaa watu wengine, labda kutokana na mipangilio yake, lakini ipo siku baba yake utamuona...’akasema

‘Mbona unasema kwa uhakika hivyo, kama vile unamfahamu baba yake?’ nikamuuliza

‘Uhakika ndio, kwasababu mtoto hawezi kuzaliwa bila baba, mimi napinga hiyo kauli yako ya kusema huyo mtoto hana baba..’akasema.

‘Mimi nimeongea naye, na amesema hakuna mtu wa kudai kuwa yule mtoto ni wake, na kila kitu keshakiweka sawa, hataki mwanaume yoyote kuja na kudai kuwa yule mtoto ni wake...’nikasema.

‘Mliongea naye lini?’ akaniuliza

‘Jana...anasema hilo keshaliweka kisheria, ...’nikasema.

‘Hana akili, anajidanganya, kama kasema hivyo, basi ujue anakuficha tu,..lakini nina uhakika anafahamu fika ni nani baba wa mtoto wake, na wameshakubaliana, jinsi gani mtoto huyo ataishi, na haki zote keshazijua, sizani atakuwa mjinga kukataa haki za mtoto wake..’akasema na kushituka kidogo, kwani alishaanza kujieleza.

‘Haki gani, kama yeye keshasema mtoto hana baba, haki hizo zitatoka wapi, kama baba wa mtoto huyo hajui, kuna maandishi gani ya kukubaliana,..yote hayo nimeongea naye, na kasema kwasasa hajui lolote kuhusu makubaliano, kama kuna mtu anajidanganya kuwa ni baba wa mtoto wake basi alie tu...’nikasema huku nikijishika shingoni kwa mikono miwili na tabasamu la dharau likiwa limetenda usoni.

‘Mke wangu usicheze na wanaume, ..mmh, unafahamu pamoja na kuwa mke na mume wanaishi pamoja, lakini kuna mambo mengine yanaweza kutendeka nje, hata mke asijue, ni makosa, alkini wakati mwingine inatokea, inakuwa ni bahati mbaya, au kutokana na kutaka jambo fulani....’akasema

‘Kutaka jambo fulani kama lipi?’ nikamuuliza

‘Yapo mengi , kuna watu wanataka mtoto, labda wa kike, hajabahatia kumpata yeye na mke wake, au mke wake, anakwua hamtimizii, sasa inatokea mwanaume anashindwa kuvumilia, na akatekwa na tamaa, ikatokea bahati mbaya, wakakutana na mwanamke mwingine..eeh, wakajikuta kwenye mapenzi, ..hiyo inatokea, tu, sasa wakipata mtoto, unafikiri hapo itakuwaje...’akawa anajiuma uma.

‘Kwa mfano kama wewe unavyotaka mtoto wa kiume, tuchukulie hivyo, na ikawa umetekwa na ulevi, bila kujijua, ukakutana na mwanamke, mkazaa naye, si ndio hivyo?’ nikamchokoza na yeye akatoa tabasamu la mwaka, sikujua kwanini anatabasamu hivyo.

‘Mke wangu bwana, tuyaache hayo, ila mimi nina uhakika kuwa huyo rafiki yako anafahamu ni nini anachokifanya, mtoto wake ana baba, na huenda wameshakubakubaliana, ila hataki kusema ni nani..’akasema.

‘Na huenda baba yake ni wewe?’ nikamuuliza

‘Mke wangu bwana, kwanini unasema hivyo?’ akaniuliza huku akiniangalai kwa uso uliotahayari.

‘Kwasababu mtoto anafanana na wewe...’nikasema

‘Kweli anafanana na mimi, hahaha, hata yeye, aliwahi kusema hivyo...mmmh, lakini mimi sijapata muda wa kumwangalia vyema, unafahamu rafiki yako amemficha sana....kama anafanana na mimi duuh, hiyo kali...’akasema huku akiendelea kutabasamu, na mimi moyoni nikasema `nimekunasa, .....’.

‘Kama anafanana na wewe hapo ina maana gani?’ nikamuuliza

‘Ina maana gani,...itakuwa na maana gani, mbona watu wanafanana tu,...inatokea tu, mimi sina uhakika na hilo,na tuliache kama ilivyo, kama anarudi, tutamuona, na mimi kama mume wako, kama mkataba unavyosema, nitaona ni nini cha kufanya kwa masillahi ya familia....’akasema

‘Yah, wewe kama mume, unaweza kufanya unavyooona ni vyema kwa amsilahi ya familia, unaweza kuzini nje, ukapata mtoto,na kwa vile wewe ni mwanaume, utafanya lile uonavyo ni jema, au sio?’ nikamuuliza

‘Tuyaache kama yalivyo, naona huko unakwenda mbali...’akasema

‘Kama ni wa kwako nakushauri ufuata taratibu za kisheria, umchukue kabisa, mshauri mwezako, ili awe ni wako kisheria, vinginevyo, utamkosa mtoto wako, kwani mwenzako keshakataa kuwa mtoto yule hana baba...’nikasema

‘Thubutu..anajidanganya tu...wewe utaona...’akasema halafu akajibaragua na kusema;

‘Mke wangu tuyaache hayo,....niache nipumzike...’akasema.

‘Mume wangu hayo yote ilikuwa ni mazunguzmo tu, ila nataka kukuelezea kuwa ndoa ni makubaliano kati ya mke na mume, kuna masharti ya ndoa, na moja ya masharti hayo ni kutokuzini, ukitembea nje ya ndoa ni kosa kubwa sana, ndio maana hata vitabu vya dini vimetoa adhabu kubwa sana, kwa mwanandoa  aliyekiuka hilo...nilishawahi kukuomba useme ukweli, hukutaka kufanya hivyo, na huenda kama binadamu ningekubaliana na hilo,...lakini ukaendelea kunificha, sasa hatua iliyofikia, sijui kama mimi nitaweza kulivumilia hilo tena....’nikasema.

‘Mke wangu nimeshakuambia kuwa hilo tuliache kama lilivyo, na sijakuambia kuwa huyo ni mtoto wangu, hayo unayasema wewe....na ni kweli, inaweza ikatokea hivyo, mume ukateleza, kwa bahati mbaya, na huenda kosa likatokana na wanandoa wenyewe...hilo hatulioni, tunasubiri matokea ya makosa ya wanandoa ndio tuje tulalamike, ....mke wangu haya tutakuja kuyaongea, na tutayamaliza, mimi kama mume, nina hekima ya kuyamaliza usijali....’akasema

‘Hakuna utetezi hapo,...sitaki kukuweka kwenye mawazo mengi, ila ninachotaka kusema ni kuwa tukumbuke misingi ya ndoa, na pia ukumbuke ule mkataba wetu unasema nini, nafahamu unaukumbuka vyema huo mkataba wetu, haujabadilika, upo pale pale...’nikasema

‘Nakumbuka sana, wewe mwenyewe ulikataa kuusoma, lakini kila kitu kipo wazi, mimi naukubali huo mkataba, na nikitoka hapa nataka tuupitie tena, kama kuna mapungufu tuyaangalie, kwani kama binadamu kuna kuteleza, ...kwahiyo nahisi kuwa kuna mabadiliko ya hapa na pale, hayo yote ni muhimu tuyaangalia, nilimtegemea sana, Marehemu, lakini...mmmh,.’hapoa katulia.

‘Lakini vipi, .....lakini mumesha-muua...’nikasema

Tume-muua, unasema nini mke wangu!?’ akauliza

‘Siku anapigwa risasi ulikuwepo, ...unabisha?’ nikamuuliza na yeye akanitolea macho, na baadaye akasema;

‘Mke wangu achana na mambo hayo,umeyapatia wapi hayo,....nishakuambia hilo ni swala la wanaume, liache kama lilivyo, utaona mwisho wake, utakuwaje, hilo lisikuumize kichwa ...wewe huoni hata polisi wenyewe wanajiuma-uma, kuna mambo yamejificha hapo,...tuyaache kama yalivyo...’akasema.

‘Vyovyote iwavyo, nakuomba ujitahidi upone haraka, ili tuweze kuyamaliza hayo mambo, na ili kama kuna lolote la kisheria, ujue jinsi gani ya kulitatua, kama ulivyosema kuwa hayo ni mambo ya wanaume, sawa, tutaona jinsi gani wanaume mtakavyolitatua hilo, maana nijuavyo mimi polisi wapo mbioni sasa hivi wanamtafuta huyo muuaji kwa nguvu zote,.....na sijui kwanini mdogo wako akaamua kukimbia, kwasababu yeye ni mwanaume, eti kwanini mdogo wako kaamua kukimbia, kwanini asisubiri kupambana kiume?’ nikamuuliza.

‘Mdogo wangu hajakimbia,... sizani kama kakimbia kwasabbu ya hilo, ukimuona mwambie aje, na nilishakukanya,inaonekana kuna jambo mumemfanya huyo mdogo wangu, akaingiwa na wasiwasi, kama kuna lolote umemfanya na ndio ikawa sababu ya yeye kukimbia ,ohoooh, mke wangu sijui kama utanielewa, ....yule ni mdogo wangu, na lolote baya dhidi yake, ni kama umenifanyia mimi, sitavumilia,...kamwe, vyovyote iwavyo, nitapambana na huyo mtu kwa hali yoyote ile...’akasema.

‘Unanitisha au unaniambia, ukumbuke unayeongea naye ni nani,...mimi ni nani kwako, mimi ni mke wako...au sio, au unafikiri unaongea na nani?’nikasema huku nikimwangalia na tabasamu mdomoni.

‘Kama unalielewa hivyo, basi fuata masharti ya mke ....kwani mkeanayefahamu taratibu za ndoa hawezi kumchezea mume wake, na mume wake akae kimiya, na mimi kama mume wako siwezi kukubali hilo,siwezi kamwe kuchezewa na mwanamke, niliyemuoa, hilo ujue, ...’akasema huku akiniangalia kwa hasira.

‘Sawa nimekuelewa mume -wangu, ugua pole, na pona haraka ili upate nguvu, unahitajika sana, ..na hayo unayoyasema yanahitaji nguvu , na sio nguvu tu, bali akili, busara na hekima ni muhimu sana, sio maneno matupu, mkataba upo wazi, na utafanya kazi yake, na nitahakikisha hilo linafanyika kisheria, kama mkataba unavyosema, kama ndoa inavyosema....hapo mimi sirudi nyuma tena, nimeamua, na unanifahamu nikiamua jambo sirudi nyuma, ugua pole...’nikasema na kugeuka kuondoka.

‘Hahahaha, mke wangu bwana, nakuamiania sana mke wangu, nashukuru kama umeukubali huo mkataba, natamani nipone haraka..hahaha kweli wewe ni kiboko, tutapambana , usijali mke wangu, mimi ni mume wako, hakitaharibika kitu,....’akasema na mimi sikugeuka nyumba, nikaelekea ofisi kwa docta.

***********

‘Hivi bado mume wangu anaumwa kweli,....sio kuwa alipona muda akawa anajiigiza kuwa abdo anaumwa?’ nikamuuliza docta moja kwa moja nikiwa bado ma mawingu ya hasira kichwani.

‘Kwanini unaniuliza hivyo, ?!’ docta naye akauliza kwa mshangao

‘Sio kwamba nasema haumwi, ila nahisi alishapona muda mrefu,... kwasababu wakati mwingine anaonekana kufanya mambo kama haumwi...alishafanya mambo ambayo hayawezi kufanywa an mtu anayeumwa kihivyo’nikasema

‘Ni kawaida maana matatizo yake ni ya kuja na kuondoka sio ugonjwa ambao unakuwa nao wakati wote, anaweza akawa yupo na hali nzuri kwa wakati fulani lakini baadaye hali ikabadilika, kutokana na matukio,..’akasema

‘Na anaweza akafanya mambo bila kujua kuwa alifanya?’ nikamuuliza

‘Ndio, ....nilishakuambia kuwa hata usiku anaweza akaamuka akafanya kazi, na asiweze kujitambua kuwa alifanya hivyo,...nikuulize kwanini umefikia kuniuliza hivyo?’ akauliza

‘Nahisi kuwa mume wangu alishapona muda mrefu, lakni anaigiza kuumwa..mimi nimeshaingiwa na mashaka hayo’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka na kusema;

‘Kwhiyo hata sisi wataalamu hutuamini, maana ukisema hivyo, unatufanya hata sisi tuonekane hatujui kazi zetu...’akasema akiniangalia kwa mshangao

‘Samahani docta, sina nia mbaya, ila ninataka kuhakiki mambo fulani fulani, nikuulize kwahiyo hayo matatizo aliyo nayo mume wangu, kama kwa mfano mtu akaamua kuigiza tu, mnaweza kumtambua kuwa anaigiza, huenda kwasababu zake akajifanya bado anaumwa, je mtaweza kumtambua kuwa anaumwa kweli, au anaigiza?’ nikamuuliza

‘Kwa hilo tatizo, huwezi kutudanganya sisi, tuna vipimo vya kuligundua hilo...ila sio muda wote mtu anaweza akawa anaumwa, kuna muda anaweza akawa na akili zake vizuri tu, lakini kuna muda anakuwa kama kachanganyikiwa, au akawa katulia tu....kwa watu wa kawaida wanaweza hata wasimuelewe, niamini mume wako alikuwa anaumwa kiukweli, sio kuigiza..’akasema

‘Sawa, docta, samahanai kwa kusema hivyo, maana kuna mambo mume wangu aliyafanya, na kwa akili za kawaida asingeliweza kufanya hivyo, ....nilikuwa nimeshamshuku kuwa anaigiza kuumwa...’nikasema

‘Ni kawaida kwa matatizo kama hayo, wengi wanaweza wasioone mtu kuwa anaumwa,matatizo aliyo nayo ni ya akili, ni kukosekana kati ya uwiano wa kili na mwili, hilo kwasasa limeshaimarika, ...usitie hilo kwasasa tunaweza kusema limekwisha, kabisa, usiwe na papara, na tunakuomba baada ya hapa,usimpe mume wako wakati mgumu,..bado atahitajia hali ya utulivu,atahitajia kujiweka sawa, japokuwa kwa kiasi kikubwa anaweza kuendelea na mambo yake kama kawaida..’akasema

‘Naomba akipona kabisa mniambie, ila nauliza, je wakati yupo hapa, aliwahi kutoka nje ya eneo lenu, nilisikia kitu kama hicho nikiwa jela?’ nikamuuliza

‘Mhh, hata mimi nilisikia hivyo, lakini sikuamini, maana kipindi kile, alikuwa hana uwezi huo, wa kwenda  mahali na kurudi bila kujulikana, niliwauliza wasaidizi wangu, wakasema hawana uhakika,...ni tetesi zilzagaa, lakini mimi siamini kabisa...’akasema.

‘Kwa jibu lako hilo, unanipa mashaka, je polisi waliwahi kuja kukuulizia swali kama hilo?’ nikamuuliza

‘Hapana kwanini waniulize?’ akasema

‘Kuna uhakika kuwa alitoka kweli na kwenda nje...kwa muda wa saa nusu saa,au zaidi kidogo, na akaenda huko alipokwenda, yakafanyika yaliyofanyika, akarudi, na hakuna aliyemuona, huoni kuwa hilo linatendwa na mtu aliye mzima,...?’ nikamuuliza

‘Siwezi kuamini kabisa,..hali ya mume wako kipindi hicho haikuwa nzuri, ukumbuke, matatizo aliyo nayo ni ya uti wa mgongo, hilo sio tatizo dogo kama mnavyofikiria nyie...ndio anaweza kufanya hivyo kwa msaada wa mtu.....lakini siwezi kuamini kabisa..na kwanini afanye hivyo,maana hiyo ni hatari....’akasema

‘Docta je akija polisi akakuuliza hivyo wewe utamjibu nini?’ nikamuuliza

‘Akaniuliza vipi, sijakuelewa?’ akauliza

‘Je mume wangu aliwahi kutoka hapa hospitalini siku fulani, na kurudi bila ya watu kufahamu?’ nikamuuliza

‘Jibu lipo lipo wazi,....’akasema

‘Ni muhimu sana, ukajiandaa kwa hilo, wewe kama docta,...’nikasema na kuinuka kuondoka, na docta akasema;

‘Hebu subiri kidogo.....

NB:Mambio ndio hivyo, tunajitahidi kihivyo, je tunafikisha ujumbe, je kisa kinafundisha, kinaeleweka, kinapendeza...sijui, hilo nawaachia nyie,

WAZO LA LEO:Kuna malalamiko kuwa wanandoa wengi hawajui ni nini maana ya ndoa, wanaingia kwenye ndoa kama fasheni tu, kwa vile inatakiwa iwe hivyo. Ni muhimu kama mzazi, ni muhimu kwa viongozi wa dini kuliangalia hili kwa mapana, hapa ndio chimbuko la kizazi, na kizazi bora hujenga jamii bora, yenye amani na upendo


Kwanini kabla ya ndoa, hawa watu wasipate shule ya ndoa, na hata ikibidi kuwe na shule kama hizi, ili kuziokoa ndoa nyingi zinazharibika,ili kuijenga jamii yanye upendo na amani ..wanandoa wengi wanaishi kwa taabu, kumbe tatizo ni dogo tu, elimu ya ndoa hakuna...ni ombi tu.


Ni mimi: emu-three

No comments :