Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, December 2, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-38‘Sawa kama hutaki kuniambai huo ukweli, mimi bado nalifuatilia hilo, kama nitagundua kuwa unafahamu au unahusika kwa hilo, kwa namna yoyote ile, basi, mimi na wewe hatutakuwa marafiki tena,tutakuwa kinyume chake,...’ nakumbuka nilimwambia shemeji yangu hivyo, niliwaza sana kauli hii niliyomwambia shemeji yangu, na moyoni nikifahamu kuwa sio yeye peke yake, ambaye, alikuwa rafiki  yangu nikimwamini, nikajitoa kwa hali na mali juu yao, nikijua nafanya hivyo kwa rafiki kumbe najidanganya mwenyewe, ...sio yeye peke yake, kumbe wapo wengi, lakini mmoja baada ya mwingine, nitamuonyesha kuwa unafiki hauna mwisho mwema.

‘Huo unafiki wao, wa kujionyesha kuwa ni marafiki zangu, sasa utawaumbua kwani utakuwa sio urafiki bali ni uadui...’nikasema kimoyo moyo.

Niliichukua ile laptop yangu, na kuhakikisha nimeificha mahali ambapo hakuna anayeweza kuiona, na ni baada ya kuiweka hiyo kumbukumbu yangu muhimu, hewani kwenye mtandao wenye kifungo, kuwa ninaweza kuifungua popote mwenyewe kwa ufunguo wangu,  na kwa hiyo hata kama hiyo laptop yangu ikatokea kuibiwa au kuharibika, bado nitaweza kuwa na huo ushahidi, kwani upo kwenye mtandao wa kudumu.

‘Ahsante sana shemeji....japokuwa ulijitahidi kunificha, kwa kuwajali wale uliowaona ni muhimu kwako, sasa tuone kama wataweza kukusaidia...’nikasema kimoyo moyo.

Kwakweli baada ya kupata ushahidi huo, moyo wangu uliingiwa na kiwingu kizito, nikajawa na ujasiri, nikijua kuwa hilo ninalokwenda kulifanya nalifanya kwa nikiwa sahihi, kwani sio mimi niliyeanza, kwani mimi nilitimiza wajibu wangu, nikajitolea kadri ya uwezo wangu, wao, ndio walionisaliti, hata pale nilipowapenda na kuwasaidia kama ndugu zangu, ..yaani,hata mume wangu...siamini.

Sikutarajia kuwa mambo mengi yaliyotendeka, yalikuwa yamepangwa, na ilisubiriwa tu, kutokee tukio kama kichochezi, ...sikutarajia kuwa wanadamu wanaweza kuwa na hali hiyo, wawe ni marafiki kwa upande mmoja na huku upande wa pili wanatafuta njia ya kuhakikisha unaharibikiwa, unapoteza kil kitu,...wanakuchuna, kwa nia tu ya kukufanya wewe uwe ni ngazi yao ya kufika huko wanakotaka, na kukipata hicho wanachokitaka huku wakikubeza, na kukudharau....

Kumbe ndivyo watu walivyo eeh, unaweza ukamwamini mtu, hata kumweka kwenye nafasi ya ndugu, mpenzi, mume au mke, ukamsaidia, mkaishi pamoja, kumbe moyoni mwa mwenzako haupo kabisa, kumbe mwenzako  ana malengo mengine kabisa...anasubiria tu kupatikane kisingizio....
Nilipowaza hivyo nikaona nihakikishe kwa mara ya mwisho,...na kuhakikisha kuwa kile nilichokigundua ni kweli, hapo nikainua simu na kumpigia rafiki yangu,....

Endelea na kisa chetu.........

***************
Nilimpigia rafiki yangu simu, na akawa hapokei, nikaona nisipoteze muda naye, kwani kwa vyovyote iwavyo atarudi tu, na kutokana na taarifa niliyoipta yupo karibuni kurudi, na akirudi kitaeleweka, ushahidi ninao, na kwa hiyo kilichobakia ni kuwaandaa vijana, ni lazima adhima yangu itimie, ni lazima watu kama hawa wakomeshwe....

Siku hiyo sikutaka hata kufanya kazi, nikaona na mimi nifanye yale waliyokuwa wakifanya wenzangu,japokuwa kwa mdomo tu, nikaona na mimi nikapoteza mawazo, ...nikaona na mimi niende kupiga umbea, japokuwa sio tabia yangu, lakini niliona na mimi nionje tamu yake, kwahiyo nikaamua kumtembelea jirani yangu,  rafiki wa mume wangu, nilijua yupo, kwani niliona gari lake likiwa nje.

Nilitoka kwenye eneo la nyumba yangu na kuingia eneo la nyumba ya dakitari, rafiki wa mume wangu, tupo jirani tu, nikafika, nilijua nitamkuta na mkewe, na ndivyo nilitaka iwe kwani hayo ninayoenda kuyaongea yanawahusu wote wawili, sikujali matokea yake....kama hawakujali yangu kwanini nijali yao.

Nilipofika malngoni nilisita kidogo, nilihisi kuna upweke, nyumbani kwa docta, kulikuwa kama hakuishi watu, kulikuwa kimiya kabisa, utafikiri hakuna mtu, nikagonga hodi, na rafiki wa mume wangu akafungua mlango na aliponiona kwanza alishangaa, pili akatabasamu, na ilionekana kama alikuwa na safari, kwani alikuwa na mkoba wa safari, usoni alionekana hana raha, nikamuuliza;

‘Vipi docta unasafiri bila kuaga, na mbona usoni unaonekana kama huna raha..,sasa kama docta ukiondoka, bila kuaga, ni nani atatutibu, wagonjwa watatibiwa na nani’nikasema kwa dhihaka.

‘Ni bora ningeumwa,ni bora ningekuwa naheshimika kihivyo, kama dakitari,...lakini ...nahisi maisha yangu yamekuwa kama nyumba ya kupanga isiyo na wapangaji,najua jinsi gani ya kuishi maisha ya raha, lakini ninaishi na mtu asiyetambua hilo, kila unalolipanga , ukitarajia liwe hivyo, unajikuta kwenye vikwazao,....sikutegemea kabisa kuwa maisha yangu yatakuja kuwa hivi,...nimejitahidi kutumia ujuzi wangu lakini inakuwa kama ule usemi usemao, penye miti hakuna wajenzi,....’akasema

‘Pole sana.. sikujua hilo, mimi nilitambua kuwa docta hawezi kuumwa,tena anaumwa ugonjwa ule ule ambao ni yeye ni dakitari bingwa wa ugonjwa huo....ajabu kabisa.’nikasema na sikutaka kujua ana matatizo gani na yeye akaniangalia kwa makini na kuuliza

‘Kwanini unanipa pole wakati hujajua nina matatizo gani....?’ akaniuliza

‘Nafahamu.... na hata hivyo sipendi kuingilia mambo ya ndani ya watu wengine...lakini nahisi matatizo uliyo nayo wewe hayapo mbali na ya kwangu , hata hivyo, wewe ni dakitari na moja ya mambo yako ndani ya fani yako ni hiyo, ya kusaidia watu wenye mifadhaiko ya ubongo,hata kama wewe ni muhanga wa hilo ...’nikasema.

‘Ungelijua...nimejitahidi kadri niwezavyo, ...lakini mmmh, hata hivyo sijakata tamaa, tatizo ni mgonjwa mwenyewe, ....akiwa tayari kusema ukweli, akawa huru kufuata hayo ninayomshauri basi....’akasema na kuniangalia.

‘Sawa nakutakia kila-laheri, hata hivyo sikufika hapa, kwa ajili ya kukuchunguza mambo yako ya ndani, ila nimefika kukuambia kuwa ule mkatana wangu niliokuwa nikiutafuta nimeshaupata...’nikasema

‘Oh,hongera sana, ...ulikuwa wapi, ni mume wako amekupa, au?’ akaniuliza

‘Hapana, nimetumia mbinu zangu tu mwenyewe,..si nyie wote mumeamua kunificha, mkajifanya hamjui, lakini mwisho wa siku mtakuja kuumbuka...hilo ninawaahidi, wanafiki wote mtaumbuka.’nikasema

‘Ohh shemeji mbona unatoa kauli nzito za vitisho, hebu niambie kwanza kuhusu taarifa hiyo njema,...’akasema

‘Ndio hivyo kama ulivyosikia..’nikasema.

‘Kwahiyo mambo yako sasa ni safi, maana uliniambia ukiupata huo mkataba umemaliza mambo yako, na mume wako, natumai ni kwa amani, heri yenu kama ni hivyo, natamani na mimi niyamalize mambo yangu kwa haraka iwezekanavyo, lakini nahisi kuna safari ndefu mbele yangu, kuna tatizo naliona limejificha, lakini ..hata hivyo nitakuja kuliigundua tu, unafikiri...utaona,...’akasema

‘Mhh, kumbe, mambo yanaanza kuwafika shingoni, au sio, hebu niambie mipango yenu imefika wapi, maana nakuona hata wewe hauna raha, kwanza, kwani mke wako yupo wapi?’ nikamuuliza, maana hali aliyokuwa nayo ilionyesha yupo kwenye mawazo mazito.

‘Mke wangu hajarudi, ....aliondoka muda, hajarudi, sijawa na uhakika tatizo nini,nipo peke yangu kama unavyoniona, aliondoka bado nikiwa namfanyia uchunguzi, ...’akasema.

‘Uchunguzi gani, kwani alikuwa anaumwa?’ nikamuuliza

‘Ana matatizo ...sio kuumwa hasa, lakini kuna hali ilijitokeza, akawa hayupo sawa, alianza kuonekana mwingi wa mawazao, ...unafahamu binadamu ukitingwa na mawazo mengi, huo ni ugonjwa, tena ugonjwa mbaya sana,sasa mke wangu kuna kipindi alikuwa hivyo, nikawa najaribu kumuuliza na kutafuta tatizo ni nini ....’akasema.

‘Ulishaligundua tatizo lenyewe?’ nikamuuliza

‘Mhh, hapana, ...na angekuwa muwazo kwangu akaniambi tatizo ni nini , ningelishajua jinsi gani ya kulitatua, lakini inaonekana ni jambo asilotala kumshirikisha mtu, ...hapo naingiwa na wasiwasi sana...’akasema

‘Wasiwasi gani tena, huyo ni mkeo, na mara nyingi umekuwa ukinisisitizia hayo, kuwa mimi na mume wangu tuwe kitu kimoja, je iweje kwako,....nashindwa kukuelewa, au ndio mambo yanazidi kuwashinda, nilijua tu mtakuja kuumbuana wenyewe....’nikasema

‘Shemeji mpaka hapo sijakuelewa, ....’akasema

‘Utakuja kunielewa siku ikifika...’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka, na kusema;

‘Kwahiyo umekuja kunisuta, ...au kuna nini kilichokuleta?’ akaniuliza

‘Nilikuja kuonana na mkeo,..sasa kaam hayupo basi tena...’nikasema

‘Ndio hivyo hayupo lakini mimi nipo, nieleze kuna tatizo gani’akasema

‘Ina maana mke wako hajarudi kutoka kipindi kile alipofariki Makabrasha,....mimi nilijua alisindikiza msiba tu, atarudi,kweli ujirani wetu huu hauna maana, muda wote huo umenificha, nikiuliza mkeo hajambo wewe unasema hajambo, au ndio katika mipango yenu, jirani mwenye mipango ya siri, ...’nikasema

‘Yeye hakuondoka kwa ajili ya kusindikiza  msiba, aliondoka kwenda kusalimia kwao,na akatumia mwanya huo, ili ashiriki kwenye huo msiba, lakini lengo la safari yake, lilikuwepo kabla, ...sasa tangu aondoke, alirudi mara moja, akaondoka tena, na hapo ikwa ndio kimoja,hajarudi mpaka leo,  nikimpigia simu anasema kuna mambo ya kifamilia bado anayafuatilia, inafikia sasa ukimpigia simu hapokei, mpaka nimeamua niende huko huko nikajue moja..’akasema

‘Basi ni vyema, ni bora uende,maana ukiona mwenzako ananyolewa, wewe tia, maji, ulipoona mimi nahangaika na ndoa yangu ukafikiria labda tunafanya makusudi, ....mambo ya ndoa yana mitihani yake...na baya zaidi mkawa na mipango ya hujuma kwa wenzenu, sijui kwanini watu wanataka kufisidi maisha ya wenzao,..watu unawaamini, lakini kumbe wana lao jambo.’nikasema

‘Mbona waongea kwa mafumbo,..!’ akasema.

‘Sio mafumbo, kama yako yamekushinda, sijui kwanini ulijifanya kunisaidia mimi, au kwa vile ni fani yako?’ nikamuuliza.

‘Ni kweli hiyo ni fani yangu, na siwezi kusema yamenishinda,..kwani nimejitahidi sana kumuonyesha mwenzangu jinsi gani ndoa inatakiwa iwe, na alikuwa akinisikiliza, utazani kweli anaelewa, lakini mwisho wa siku anakuwa kama sio yeye, ..na akawa hana raha, ukiongea naye, anakuwa kama hayupo, nikajua ana tatizo kubwa sana, nikajaribu kulitafuta lakini sikufanikiwa, hakuniambia kabisa, ndio maana kipindi fulani uliniona sifikifiki kwenu..’akasema

‘Mhh,Ndio kipindi kile ndio ukawa unakwenda kulewa na mume wangu, mkijidanganya kuwa mnapoteza mawazo, kumbe ulikuwa na yako ndani hutaki kusema...na kumbe kuna mdudu mtu, usijifanye huhusiki, nyie lenu moja, siwezi kuamini, lakini ipo siku, nitawaanika hewani, sitakubali kamwe....’nikasema nikizidi kumrusha roho.

‘Mhh, naona usiponiambia kuna nini sitakuelewa,..hebu niambie kuna nini kinakufanya uongee hivyo?’ akaniuliza na mimi sikuwa tayari kumwambia lolote nikasema;

‘Kipindi kile mlichokuwa mnalewa na mume wangu, ndio kipindi ambacho mlipanga mambo yenu kwa siri, su sio..ukajifanya wewe huna tatizo, kumbe una tatizo, kumbe mlitumiwa mwanya huo kufanya mambo yenu kwa siri....’nikasema.

‘Mambo gani...?’ akaniuliza

‘Mhh, unajifanya huyafahamu, hebu niambie wewe na mke wako mna matatizo gani kwanza, na kwanini kama mlikuwa na matatizo kwanini hukuwahi kuniambia?’ nikamuuliza kupoteza lengo.

‘Ndio ni kweli nilikuwa na yangu, lakini mimi kama docta, akija mgonjwa anaumwa siwezi kumwambia huyo mgonjwa kuwa hata mimi nina ugonjwa kama huo, nitajitahidi kuficha matatizo yangu ili niweze kumsaidia huyo mgonjwa, ndivyo ilivyo ndio maana wanasema mganga hajigangi,...lakini shemeji mbona unaongea hivyo kuna jambo gani umeligundua, hebu niambie maana ni siku sasa hatujaweza kukaa tukaongea kama ilivyokuwa zamani....’akasema

‘Kwahiyo ukawa unakufa na tai shingoni,...mmh, hayo ni mambo yako na ndoa yako, hata kama nimegundua kitu, siwezi kukuambia kwa sasa, maana inaweza ikawa ni fitina, ila kuna siku tutakaa tuongee, mkiwa wawili, na mimi kwa mpangilio wangu nilitaka tukae wote , mke wako, mume wangu, na wazazi wangu ikibidi, na wale wote wanaoitwa marafiki, hilo nimelipanga,....nakupa tu kama utanguzi...’nikasema.

‘Kwani kuna nini kikubwa kimetokea, ni kuhusu mkataba wenu, au kuna jingine ?’ akauliza huku akiniangalia kwa mshangao

‘Kune mengi sana, na huenda hayo yakapasua jipu, nimevumilia vya kutosha, na hali iliyofikia ni bira lawala kuliko fedheha, sijali kuwa mlikuwa marafiki zangu, sijali tena hilo nataka ulielewe mjiandai vyema, mjue siri imeshafichuka, ...’nikasema

‘Mbona unaniacha hewani, hebu niambie shosti wangu, maana wewe ndiye uliyekuwa rafiki yangu wa karibu, japokuwa hayo matatizo yako yalifanya tuanze kuwa mbali, lakini mimi sijakata tamaa, wewe utaendelea kuwa rafiki yangu tu, ...’akasema

‘Shosti, rafiki mpenzi, mnayatamka kwa uzuri, lakini moyoni mna jambo, sawa hakuna shida,....’nikasema

‘Kwani kuna nini mpenzi wangu....’akasema

‘Mpenzi!, hiyo kauli sitaki kuisikia, mimi nilijua umeshajirejebisha, ...jaribu kujifunza kuwa wewe ni mume wa mtu, na mimi ni mke wa mtu, tuwe na mipaka ya uhalali ili kusije kukaingia fitina, mimi najaribu sana kuchunga hiyo mipaka, kwani akili za wanadamu ni nyepesi sana, kutizama yale mabaya kuliko yale mazuri,..chunga sana hilo..na kama ningelikuwa nafahamu kuwa mke wako hayupo nisingelifika hapa leo.’nikamwambia.

‘Ni kweli, nimejitahidi kufanya hivyo, nimejirekebisha sana, japokuwa ni kwa shida,.. lakini tatizo kubwa ni mwenzangu, sijamuelewa, ...huenda ipo siku nitakuambia unisaidie muongee naye, huenda ukaweza  kukuambia ana tatizo gani...’akasema.

‘Mmm, una maana mke wako,....?’ nikamuuliza

‘Ndio mke wangu, ....’akasema

‘Maajabu , wewe ni docta, tena wa fani hizo, umeshindwa kumsaidia mke wako, wakati unawasaidia watu wengine, halafu kazi hiyo unamtupia mtu asiye na hiyo fani na zaidi ya hayo na yeye ni mgonjwa wa matatizo hayo, unanishangaza kweli...’nikasema.

‘Ugonjwa mwingine unatibika kwa uzoefu, mtu anaweza akaumwa sana na tatizo fulani, na kwa ajili ya kulihangaikia lile tatizo,hadi kuliponyesha, akawa kajenga ufahamu wa jinsi gani ya kulitibu hilo tatizo, zaidi ya hata docta anayelifahamu kinadharia, wewe kama umeweza kulitatua tatizo lako basi umeshakuwa mtaalamu...’ akasema.

‘Lakini sijakuelewa, samahani kidogo, maana haya mambo mimi siyajui, lakini inabidi nikuulize tu, hebu nikuulize kwani wewe na mke wako kuna tatizo gani? Nikamuuliza tena hilo swali

‘Hakuna tatizo, ...kati yangu mimi na yeye,  siwezi kusema tuna tatizo, kama yapo ni ya kawaida, ila nahisi yeye mwenyewe ana tatizo, lakini hataki kuniambia ana tatizo gani, kuna kipindi alionekana hana raha kabisa, nakumbuka hata wewe ulikuja kuniuliza hilo, nikakuambia ndivyo alivyo...mimi ni dakitari, lakini huwezi amini, mke wangu ananiona kama watu wengine, nikijaribu kutumia utaalamu wangu kwake, anakuwa kama haniamini, basi nikaona nimtumie mwenzangu aje asikilize kuna tatizo gani,...’akatulia

‘Mwenzako alisaidia, au hata yeye alishindwa?’ nikauliza

‘Alishindwa..mke wangu ana siri kubwa moyoni, na ni siri kweli...unafahamu mke wangu ni jasiri, ni kama askari, lakini kuna tatizo limemshinda,....’akasema.

‘Anaonekana hata mwili wake kaujenga kimazoezi, sijui ni kutokana na kazi yake...’nikasema.

‘Huo ujasiri kwa hilo tatizo, naona umemtoka, hata mimi nilimwambia kuwa yeye mbona anaonekana ni jasiri, kuna kitu gani kimemshinda, hadi awe hivyo....lakini anasema hana tatizo, ni mawazo yangu tu, anasema hana tatizo ...ndio kauli yake hiyo...’akasema.

‘Mhh, labda hataki wewe ujihusishe na hayo aliyo nayo, au ndio mbinu yenu wote lenu maoja, sasa unaona mambo yamewafika shingoni unajifanya wewe huhusiki, au ndio mbinu ya kumkimbiza kijijini ili mfute madhambi yenu,...’nikasema na yeye akaniangalia huku akionyesha uso wa kuwaza.

‘Sikuelewi kabisa...’akasema

‘Basi kama hunielewi kwa sasa utakuja kunilewa baadaye, au kamuulize mke wako akuambie, huenda yeye anasubiria muda muafaka wa kukuambia ukweli, kama kweli hujui, ila ninachoweza kukuambia ni kuwa mke wako ana tatizo...’nikasema.

‘Mhh,, sijui kama ni hayo ambayo hata mimi nilikuwa nayawaza, maana huniambii ukweli, hata mimi nilifikia hatua ya kuwaza sana,..., unafahamu kuwa mke wangu na mume wako walikuwa marafiki kabla, hujaolewa na mume wako, hawa watu wawili walikuwa wapenzi lakini sio wa ndani sana, kama ilivyokuwa mimi na wewe...’akasema

‘Unaanza kufunguka eeh, ....utasema sana, maana hayo ulinificha, sikuwa nayafahamu kabla, sijawahi hata kulisikia hayo kabla, mlikuwa mumenificha wewe na rafiki yako,....’nikasema nikionyesha mshangao.

‘Kwasababu mume wako ni rafiki yangu, hayo tunayafahamu wenyewe, na kwa vile kila mmoja alikuwa kama kamuibia mwenzake, ikawa imekwisha hivyo, lakini kipindi mume wako analewa sana, kuna muda mume wako alikuwa anakuja hapa kwangu, anashinda hapa, na mimi naondoka, sina wasi wasi naye, na sikuwahi kulifikiria hivyo...ila nikahisi kuna jambo ...siwezi kuliweka akilini kuwa lipo, maana sijawahi kulithibitisha, hivyo, na siwezi kumshuku rafiki yangu....’akasema.

‘Kwahiyo unahisi kuwa kulikuwa na mahusiano ya siri?’ nikamuuliza

‘Hapana sijasema hivyo, japokuwa kuongea kwao ilikuwa kama mimi na wewe tunavyoongea, kwa ukaribu zaidi, kwa vile walikuwa hivyo, nilimuomba mume wako ajaribu kumuuliza mke wangu kama kuna tatizo...lakini hata mume wako hakuweza kuambiwa,...unaona , jinsi gani mke wangu alivyoliweka hilo kama siri yake..’akasema.

‘Mhhh, hayo mambo, kwanza hukuwahi kuniambia hivyo, kuwa hawa watu wawili walikuwa marafki, ilikuwa siri yenu, ...lakini nikuambie ukweli, hakuna siri ya mambo machafu, utafanya ukijidai huonekani, lakini ipo siku utaumbuka,hayo machafu yenyewe yatawaumbua..., wewe subiri tu....’nikasema

‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza akiniangalia na uso uliojaa kutafakari.

‘Mimi sitaki kukufitisha na mke wako, wewe ni docta, jaribu kutumia ujuzi wako wa kidakitari, huenda ukamsaidia mke wako, nakumbuka hata wewe ulinishauri hivyo hivyo, nijitahidi sana, ili niweze kumsaidia mume wangu, japokuwa mengine yanazidi mpaka, .....sijui kama mimi na mume wangu kuna dawa itakayoweza kuponyesha hilo jeraha, ..ni kubwa sana, namuomba mungu anisaidie, lakini ....ni lazima jambo lifanyike...’nikasema.

‘Aaaah, hebu tumalize moja , kabla ya jingine, niambie ukweli, umegundua nini kuhusu mke wangu na mume wako,?’ akaniuliza.

‘Siwezi kukuambia lolote kwasasa, ..hayo ni yako na mke wako...wewe ni rafiki yangu na mimi kuja kwangu hapa nilitaka nikutane na mke wako tuongee, mke na mke..sikutarajia kuwa nitakukuta hapa, na hayo niliyoyagundua mimi, hayataweza kukusaidia, ni mambo yangu na mume wangu,...tatizo ni kuwa kuna watu wataumia kwasaabbu ya tamaa za watu wachache...akili za watu zimeganda, wanahadaiwa, wanakubali kirahisi, wanatumia kauli, na kufanya yale walioyokuwa wameyapanga...sasa sijui kama hili linaweza kuisha kirahisi hivyo,..sizani, wewe unajifanya hufahamu, lakini nahisi wote nyie ni kundi moja.’nikasema

‘Shemji kwani kuna tatizo gani, mbona unanitisha...?’ akaniuliza

‘Utalikuja kulijua kwa wakati muafaka, ila nakushauri, ....sana, umsaidie mke wako, yupo kwenye hali mbaya,...kiakili , na ndio maana nilitaka nikutane naye, ..sasa unaniambia kuwa mume wangu na mke wako waliwahi kuwa marafiki,hili linanifanya nihitimishe yale niliyokuwa sijayafahamu...kumbe ni kweli...haya tutaona mwisho wake’nikasema.

‘Yapi hayo uliyoyagundua,...hebu niambie ili usiniweke hewani?’ akaniuliza.

‘Mhh, unajua mimi kama mke, nilikuwa namuamini sana mume wangu,...na hata ule mkataba nilishauri tuwe nao tu, sikuwa namshuku mume wangu kwa lolote lile,ndio maana wakati unaniambia mengi kipindi kile kuhusu mume wangu na rafiki yangu sikuwahi kuhisi vibaya, ...sasa kulisikia hili tena kuwa mke wako na mume wangu waliwahi kuwa marafiki..hapo sasa naanza kuhitimisha uchunguzi wangu,...’nikasema.

‘Ehe, umegunua nini, hebu niambie....’akasema

‘Mimi , ninahisi kuna jambo linalowahusisha nyie nyote hata wewe ukijifanya kuwa huhusiki, tatizo ni kuwa , kwa hivi sasa siwezi kumwamini mtu yoyote maana nyie wote mna mambo yenu ya chini kwa chini,,...nimeshaanza kufunguka akili, ...kwa mtaji huo,hapo hatoki, hakuna ujanja tena, ......wewe subiria uone vumbi lake, mjue kuwa mumekutana na mwanamke wa shoka....’nikasema.

‘Sijakuelewa bado, kuna kitu gani umekigundua, kuna nini kimetokea, hebu niambie tafadhali?’ akaniuliza

‘Usiwe na wasiwasi, utakuja kulijua hilo, mimi kama ni ukweli, sitaweza kuwaficha, ila nahitajia niutoe wakati mufaka,, hasa akiwemo mke wako, ...unasema mke wako anarudi lini, au wewe unakwenda lini kuonana na yeye huko kijijini?’ nikamuuliza

‘Leo hii naondoka kwenda huko, sitarajii kukaa sana, nakwenda leo ikiwezekana kesho tutakuaj naye, ila sijui huko alipo kuna tatizo gani hasa..lakini nitaligundua huko huko....’akasema.

‘Sawa mimi namuhitaji yeye mwenyewe, kuna mambo nataka kuongea na yeye kwanza, na kwenye hukumu, anatakiwa kuwepo, asikie , aone, na ikibidi athibitishe, ...mimi sikupenda iwe hivyo, lakini sina jinsi, na kama nitaongea naye uso kwa uso, huenda nikayamaliza mimi na yeye kama akiwa mkweli, lakini nahisi kuna mambo makubwa dhidi yake..ambayo yapo nje ya uwezo wangu, sitaweza kumsaidia....’nikasema.

‘Mambo gani hayo?’ akaniuliza akikunja uso kwa mashaka.

‘Kwa hivi sasa siwezi kuyasema, ndio maana nataka niongee naye uso kwa uso..kama itabidi uhusike hakuna shida, hayo ni mambo yangu mimi na yeye kwanza, nataka aniambie ukweli, vinginevyo, ujirani utakufa, sitajali tena kuwa ni mke wako, sitajali kuwa wewe ulikuwa eksi...’nikasema.

‘Ina maana huenda hayo unayoyafahamu au liyoyagundua yanaweza kuwa chanzo cha kuharibikiwa, ndio maana alikuwa katika hiyo hali,.....?’ akauliza

‘Mimi sina uhakika na hilo, kwakweli mimi sitaki hata kufikiria zaidi, maana hata ,mume wangu sitaki hata kumuona kwa hivi sasa, .....lakini nitajitahidi kutimiza wajibu wangu mpaka hatua ya mwisho, nafahamu wengi watakuja kunilaumu, lakini ni bora nusu shari kuliko shari kamili, ni bora kuzuia kuliko kuponya, su sio?’ nikamuuliza

‘Unaniuliza kitu ambacho sikujui, kwanini huaniambii ukweli?’ akauliza

‘Nenda kaongee na mke wako, msikiliza, na huenda anaweza kukuambia ukweli..kwa hivi sasa sio wakati muafaka wa kuyaongea hayo, yatafika muda tutayaongea, na kila mmoja atakuwa na maamuzi yake, lakini kwangu mimi maamuzi yako kwenye mkataba wangu..vinginevyo, ni kusaidia tu, ni ubinadamu tu, lakini je unaweza kujitolea kwa mtu ambaye anataka kuku-ua, ..hivi kweli unaweza kufanya hivyo, haiwezekani...’nikasema.

‘Kwahiyo hutaki kuniambia ukweli?’ akaniuliza

‘Hivi nyie watu mpoje, ..wewe kuna mambo mengi ulikuwa ukiyafahamu, ulinificha, na huenda ungeliniambia haya yote yasingelifika hapa,..sasa wewe yule yule unataka nikuambia ukweli, kwa vile yamewafika shingoni,....nikuambia ukweli, boti limeshatoboka, sasa hivi ni kila mtu na ujuzi wake, kama hujui kuogelea, ..basi tena,...mimi nimeshamaliza...’nikasema na kuinuka kuondoka.

‘Unafahamu wewe ni rafiki yangu mkubwa, na kama isingelikuwa huyo mume wako kukuwahi, wewe ndiye ulikuwa chaguo langu,....mimi sijakuficha ukweli, nilifanya yale ninayohisi kitaalamu ndivyo yanatakiwa yawe hivyo, kuna mambo hata mimi sikuwa na uhakika nayo,kame ningelikuambia na baadaye iakwa kinyume chake, ningeumbuka, na hata utaalamu wangu ungelikuwa hauna maana...’akasema

‘Nimekuelewa, hakuna shida...’nikasema.

‘Kwahiyo kama umenielewa, kuna nini umekigundua mbona hutaki kuniambia ukweli...’akasema

‘Kwasababu ukweli huo ndio hitimisho ya haya yote, ukweli huo utahitimisha kila kitu, na kila mmoja atabakia na lake, ...wewe nenda kaongea na mke wako kabla jamaa hawajamuwahi..’nikasema

‘Una maana gani kusema hivyo...’akaniuliza kwa mashaka.

‘Nimesema hivi mke wako anakuhitajia sana, ...ana matatizo, lakini hayo matatizo anahitajika yeye akuambie 
wewe mwenyewe, nilitaka mimi niongee naye mwenyewe, ili nithibitishe kutoka kwa mdomo wake mwenyewe, lakini kwa vile yupo mbali na muda haupo, ni bora wewe ufike mkaongee naye kwanza, kwani huenda sio kweli...huenda ..kuna kitu kingine, hata mimi bado sijaamini, sina uhakika,...kwasababu bado watu hawataki kusema ukweli....’nikasema

‘Na wewe pia hutaki kusema ukweli, ....’akasema

‘Mimi sijakataa kusema ukweli, lakini ukweli wangu unategemea ukweli kutoka kwa wahusika, kama wahusika wameficha ukweli, na unachokisikia ni kutoka kwa watu wengine, nusu nusu, unaweza ukawa ni ukweli uliotengenezwa,  uonekane ni ukweli, kumbe ni hujuma za watu, ndio maana naogopa, ndio maana nataka niongee na mke wako uso kwa uso....’nikasema.

‘Sasa unaonaje, tukiongozana kwenye hii safari, mkaongee huko huko...?’ akauliza

‘Haiwezekani,...hilo siwezi kulifanya, njooo naye, kama hataki kuja, basi ...lakini nina imani kuwa atakuja, kwa hiari yake mwenyewe, ..au vinginevyo,...sijui, hilo nkuachia wewe mwenyewe na mke wako, ipo siku litakuwa letu sote, lakini kwa sasa ni lako na mke wako, lilikuwa langu na mume wangu, sasa limegukia kwako, yale yale....’nikasema na kuinuka kuondoka, na kumuacha docta akiwa kaduwaa, ...moyoni nikasema;

`Bado mmoja....’

NB: Nafahamu sehemu hii itawachnganya watu, lakini mwisho wa yote utaelewa tu, hapo ndio tunaitafuta hitimisho.


WAZO LA LEO: Mara nyingi ni rahisi kuona mambo ya wenzetu, kuliko mambo yetu,ni mara nyingi tunaweza kuona dhambi za wengine kuliko za kwetu, hata tukafikia kunyosha kidole, na kulaumu, kusuta hata kukejeli, tukasahau kuwa makosa yetu , dhambi zetu ni zaidi ya hizo za unayemnyoshea kidole. 

Matatizo ya mke na mume yanatatutuliwa na mke na mume, matatizo ya familia yanatatuliwa na wanafamilia wenyewe, nk, ni vyema,tukajaribu kutumie hekima, katika kuingilia maswala hayo, ni tufanye hivyo kama wenyewe wanataka tufenye hivyo,...

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Nimependa sehemu hii imenikumbusha na imenigusa kwa namna fulani ...pamoja daima.

emu-three said...

Nashkuru sana kusikia hivyo ndugu wangu @Yasinta, kisa chetu kinagusa maisha yetu ya kila siku,TUPO PAMOJA