Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, November 28, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-37



Nilifika chumbani kwangu na kwa haraka nikaingia maktaba nikiwa na shauku ya kuuona huo mkataba, shauku niliyokuwa nayo ilikuwa haimithiliki, utafikiri nilikuwa nakwenda kugundua alimasi iliyofichwa, kwangu mimi huo mkataba ulikuwa na thamani kubwa, sio kwa ajili ya kulinda masilahi yangu tu, lakini pia kulinda utu wangu, kilichokuwemo humo, kilikuwa ni kwa ajli ya utu wangu, na kama utapotea basi mimi nitaonekana sina maana,, nitadhalilika,....

Nikawa natembea kwa haraka haraka,nikijua kuwa sasa ukweli utadhiri, na wale wote waliotaka kunidhulumu, na kuishia maisha ya hadaa nyuma ya mgongo wangu wataumbuka, ...na hilo nilishaliahidi kwa wazazi wangu kuwa nitahakikisha, nalifanyia kazi bila ya msaada wao, na wao waliniona kama mfa maji,....lakini sasa ukweli watauona, na kile nilichokuwa nimekiahidi mbele yao watakiona kwa macho yao. 
Sikutaka kubweteka, sikutaka kudeka,kwao kuwa kwa vile mimi ni mtoto wa kike, sitaweza kuishi bila ya msaada wao.

Nilitaka kuionyesha jamii, kuwa hata sisi wanawake tunaweza, tunaweza kutunza siri, tunaweza kutunaza dhamana, ...kwangu mimi kipao cha ndoa, nilikiona ni muhimu sana, ndio maana sikutaka kughilibiwa, kama nilijitahidi kufanya hivyo, japokuwa kulikuwa na mapungufu, kwanini mwenzangu afikie hatua hiyo kubwa ya kunisaliti, hapana, kama kafanya hivyo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake, lakini sheria ipi, maana huo mkataba ndio ulikuwa ni sheria yangu..sasa umepotea

‘Kama nitaupata huo mkataba, nitawaonyesha watu kuwa hili linawezekana, kama kutakuwa na mkataba wa ndoa na mkaufuatilia, mwenye makosa akahukumiwa kutokana na amkubaliano yenu, basi kila mwanandoa ataogopa kufanya maasi, ....’nikasema huku niendelea mbele kuelekea sehemu iliyopo sheria yangu, mkataba wangu, utakaonilinda kwa hilo...

‘Na wale wote walionisaliti, itabidi wawajibike, sitajali kama ni rafiki yangu, au ndugu yangu...’nikasema huku nikifungua mlango wa maktaba, ambao sasa nilikuwa na ufungua mwingine mpya,japokuwa nilipotoka sikuwa nimefunga na ufunguo, ila nikitoka nje , nitakuwa nafunga sehemu zote nyeti...

‘Nikimalizana na huyu shemeji yangu, nitaanza kupambana na rafiki yangu, sitajali urafiki tena, mapaka kieleweke, na mwishi namalizia na mume wangu,...nina uhakika kuwa mume wangu kasaliti ndoa yangu, na ninachotakiwa kupata ni ushahidi, na ....na mkataab wetu utahukumu....’nikasema.

Nikalifungua kabati la mume wangu, kwa ufungua ambao unafungua kwa namba maalumu, ...hata uchonge ufungua, usingeliweza kufungua, nilifanya hivyo, ili kila mmoja awe na namba zake za siri, kwahiyo mume wangu akija nitampa ufunguo wake, na namba zake za siri.

Nikafungia hilo kabati lake, kwa ndani kuna sehemu tatu, nikavuta kidroo cha sehemu ya kwanza, niliona makaratasi ya malipo, stakabadhi za malipo na vyeti vya biashara, hakuna huo mkataba...

Nikafungua sehemu ya pili, hakuna kitu, hapo hasira zikaanza kunipanda ina maana huyu kijana kanidanganya, nikasema na kufungua sehemu ya tatu, hakuna kitu...nguvu zote zikaisha, na sikujau nifanye nini tena, na wakati nimekata tamaa, kwa pembeni nikaona bahasha kubwa,iliwekwa kwa kusimama, isngelikuwa rahisi kuiona, nikaitoa ile bahasha, ilikuwa nzito, nikaitoa, na kuigeza juu chini kukitoa kilichopo, kikatoka kitabu....

Kumbe ilikuwa sio kitabu , ulikuwa mkataba, na mwanzoni nilifikiria ni ule mkataba wa kawaida, lakini pale nilipoona alama yangu nikagundua, ni ule ule mkataba niliokuwa nautafuta, nikauchukua na kuanza kuufungua, kuhakikisha kuwa ndio wenyewe, na nilipojirizisha nikafunga yale makabati na kuanza kutoka.

 Wakati nainua mguu, nikakanyaga kitu, nikainama kukiangalia, kilikuwa kidude kidogo,cha  kuhifadhia kumbukumbu, unaweza kukiweka kwenye simu au kwenye komputa, nikakiokota, nahisi kilidondoka kutoka kwenye hiyo bahasha, waakti nilipoiinamisha juu chini kuutoa huo mkataba,na hapo nikakumbuka kauli ya shemeji yangu;

‘Shemeji kama kuna kitu changu naomba uniletee, ...

`Huenda hiki kitu ndicho anachokitafuta....’nikasema huku nikikiangalia kwa makini, moyoni nikaingiwa na shauku ya kujua kuna nini humo ndani, lakini kwa namna nyingine niliona nafanya makosa, nitakuwa nachunguza vitu vya watu, na mimi sitaki tabia hiyio, hata hivyo kwa hali ilivyo kwasasa hamasa za kufahamu ni kitu gani kimo humo ndani ikanijia, nikatoka hadi chumbani hadi kwenye laptop yangu, nikakichomeka, na maandishi yakatokea;

Diary yangu, kumbukumbu za kila siku.....’

‘Oh, kumbe ni kumbukumbu zake, hakuna shida..na wakati nataak kukichomoa, nikaona maelezo yaliyonivutia, nikayasoma kwa haraka..

‘Kumbe...’nikasema

‘Sasa nimekupata, kama atakuwa anaweka kila kumbukumbu za kila siku, kumbe nitaweza mambo muhimu ninayoyatafuta, amekwisha, hana ujanaj tena, ...’nikasema na kwa haraka nikaweka sehemu ya kunakili hizo kumbukumbu kwenye komputa yangu, ilichukua muda kidogo, na kumbukumbu zote zikanakiliwa kwenye komputa yangu, halafu nikakitoa kile kitufe, na kukiweka kwenye ile bahasha nikatoka nacho hadi kule bustanini.

‘Shemeji kwenye hiyo bahasha uliona kitu changu?’ akaniuliza

‘Kitu gani?’ nikamuuliza kama vile sijui,

‘Naiomba hiyo bahasha, umeshautoa huo mkataba unaoutaka, natumai sasa tumemalizana, uliouona eeh....?’ akauliza huku akichungulia ile bahasha kwa ndani, na mara akakitoa kile kitufe na kwa haraka akakiweka mfukoni

‘Ni kitu gani hicho?’ akaulizwa na wale maofisa wa upelelezi

‘Ni kifaa cha kazi zangu za ofisini, ni muhimu sana, ningelipoteza kazi za watu...’akasema

Mimi nilikaa kimiya sikusema kitu na hapo yule ofisa akaniuliza kama nimeuona huo mkataba na kama ndio wenyewe niliokuwa nautafuta, nikamwambia ndio nimeuona ndio wenyewe.

‘Shemeji kwa hali ilivyo huyu mtu inabidi tuondoke naye...’akasema huyo jamaa wa usalama

‘Hapana, mimi nimewaambia kila kitu, kwanini sasa mnanigeuka, ...tulikubaliana nini?’ akalalamika huyo shemeji yangu na mimi hapo nikamuonea huruma na kusema;

‘Kwa vile kakubali kushirikiana na sisi mimi sioni kwanini muondoke naye, ...mimi nitamdhamini, siku mukimuhitaji atakuja, mnaonaje ombi langu hilo?’ nikawauliza

‘Kuna mambo mengi bado anayaficha, hajakuwa mkweli, ndio maana tunataka tuondoke naye..tunauhakika akifiak huko atasema kila kitu.’akasema

‘Nimewajibu kila kitu, sijaficha jambo, jambo gani nimelificha?’ akauliza shemeji yangu akiwa kakasirika.

‘Tunashindwa kurudia swali mara nyingi,...wewe usituone kuwa sisi ni watoto wadogo, hapa tulikuwa  tunakuuliza maswali ya kukupima tu, mengi tunayafahamu, kwa mfano tu, hilo la kusema ulikwenda kutupa hiyo silaha porini halafu ikaibiwa hiyo sio kweli,ukweli ni kwamba kuna mtu ulimpa hiyo silaha, hilo umetuficha,hukusema ukweli, kuna mengi tunayahitajia kutoka kwako,na usiposema huo ukweli, utaozea jela...’akasema huyo mtu wa usalama, na kumfanya shemeji yangu atulie kimia.

‘Mimi naomba nimdhamini, kwa vile bado mnafuatilia mambo mengine, huyu niachieni mimi, nawashukuru sana, kwa msaada wenu, mimi bado nina maongezi na shemeji yangu, mkiwa tayari kumuhoji, mtaniambia, ila kwa leo naombeni tuishie hapa , kwani kile kitu muhimu nilichokuwa nikikihitajia nimekipata...kama kuna zaidii tutafahamishana...’nikasema

‘Huyu ni mhalifu, ..huo aliofanya ni wizi, japokuwa anamtupia lawama kaka yake kuwa alimtuma, hilo sisi hatulikatai, lakini hakutaka kusema ukweli,toka awali, kwani hii sio mara ya kwanza kuhojiwa,..japokuwa waliomuhoji awali ni watu wengine, lakini alichowaambia nikifahamu...’akasema.

‘Yeye hajui kuwa kila siku anafuatailiwa, hajui kuwa bado uchunguzi unaendelea,na hatua iliyofikia, ni ya kuamalizia, tu, ...watafikishwa wote wamahakamni kujibu makosa mengi, ikiwemo hilo la kumuua Makabrasha....hata kama sio yeye aliyefanya hivyo, lakini alishiriki kwa namna moja au nyingine...’akasema huyo mtu wa usalama.

‘Sawa kama mumefikia huko, siwezi kuwapinga, ila kwa vile bado hamjakamilisha uchunguzi wenu, basi mimi naomba huyu mtu msimchukue, mimi namdhamini kwa kauli, tu, namfahamu sana shemeji yangu huyu, siku mukimuhitaji, nitahakikisha anafika huko kituoni,...’nikasema na wale watu wa usalama wakakubaliana na mimi wakaondoka, na mimi nikabakia na shemeji yangu.

‘Shemeji sasa umefanya nini?’ akaanza kunilaumu.

‘Ndivyo ulivyotaka wewe iwe hivyo,  na kuna mambo mengi bado nayahitaji kutoka kwako, usiponijibu leo, mimi nitawaambia hao watu waje wakuchukue, ila nataka tuyaongee mimi na wewe kwanza, ukiniambia ukweli, mimi nitajua jinsi gani ya kukulinda,...’nikasema

‘Mambo gani tena hayo shemeji hapa nilipo nimechanganyikiwa nafahamu kaka atakuwa ananisubiri na nimechelewa kwenda kumuona?’ akauliza kwa wasiwasi.

‘Nataka kumjua huyo mwanamke aliyezaa na kaka yako’nikamwambia

‘Shemeji mbona huyo mtu mimi simjui, na kaka hajazaa na mwanamke yoyote, hizo ni ndoto zake tu,....waakti wmingine anawaza, na kwa vile alikuwa akitarajia kupata mtoto wa kiume, basi nahisi mawazo yake hayo anayapeleka kwenye hali halisi, ...mimi simjui’akasema

‘Una uhakika na hilo jibu lako, maana nikigundua kuwa unanificha, basi sitakuamini tena, unanifahamu nilivyo, ninapokuahidi kitu, siachi kutekeleza, na ukinidanganya, siwezi kukuamini tena, na lile nililoahidi dhidi yako huwa sirudi nyuma.....’nikasema na yeye akaa kimiya, nikasema

‘Sawa kama hutaki kuniambai huo ukweli, mimi bado nalifuatilia hilo, kama nitagundua kuwa unafahamu au unahusika kwa hilo, kwa namna yoyote ile, basi, mimi na wewe hatutakuwa marafiki tena,tutakuwa kinyume chake,...sitakutambua kama ndugu yangu wa karibu tena, , japokuwa nimejitolea kadri ya uwezo wangu hadi ukafikia hapo ulipo, sitaajli hayo, kwani hata hivyo, nina maana gani kwenu, mumenichukulia kama ngazi yenu ya kupaat mlichokitaka...’nikasema

‘Shemeji kwanini unataka kuniweka mimi kama rehani, mume wako yupo, ndiye muhusika mkuu, kwanini usimsubiri apone uje umuulize yeye mwenyewe, ukiniuliza mimi maswali  kama hayo ya mtego unaniweka mimi mahali pabaya,...nakuomba unielewe hivyo,..mimi nafanya mengi kwa shinikizo, najikuta sina jinsi,...’akasema na mimi nikawa nimemuangalia tu, halafu akasema;

‘Hivi shemeji, hebu niambie haya niliyoyaongea leo hapa kwa hawa watu wa usalama, je akija kuyagundua haya niliyoyasema hapa itakuwaje, ...mimi najuta sana, nimeshindwa ...oh, nimemsaliti kaka yangu, kaka ambaye ananipenda sana, na ambaye kajitolea kwa hali na mali kwa ajili yangu...’akasema

‘Ina maana kaka yako ndiye aliyejitolea kwa hali na mali juu yako, unakumbuka mwanzoni kaka yako alikuwa akisemaje juu yako, alikuwa hakuamini, alishakuweka kwenye kundi la wavuta unga,mimi nikajitolea na kumhakikishia kuwa nitakusaidia hadi utabadilika, je ni nani aliyejitolea kwa hali na mali kati ya kaka yako na mimi..umesahau hayo eeh, kwasababu ya tamaa, kuwa mtamiliki kila kitu eeh?’ nikamuuliza

‘Wote mumejitolea kila mtu kwa nafasi yake, hilo nashukuru sana, ndio maana kuna mambo ambayo nimekuwa siyafurahiswi kuyafanya, au kuona unafanyiwa, na ndio maana nikajitolea na mimi kule kunapowezekana, ..wewe hujui tu ....lakini siwezi kusema zaidi, ninachoweza kusema kwa sasa ni ahsante kwa wema wako huo..hata kama unaona kwasasa namukuwa sio mtiifu kwako, lakini sio kwa nia mbaya, ni pale inapofikia hatu ya kuchagua kaka au wewe,hapo mimi mnaniweka kwenye njia panda....’akasema

‘Sasa sikiliza,shemeji yangu, wewe ni mtoto wa juzi, ulipolala ndipo nilipokuwa nimelala siku nyingi, nikaamuaka na kufanya kazi,...kwahiyo sasa ni juu yako, nimewabeba kiasi cha kutosha, nimewambembeleza kiasi cha kutosha, naona sasa ni muda wenu kufanya hivyo,..jua kabisa kwasasa wewe upo kubaya, kuwa umeshirikiana na muuaji wa Makabrasha, ...unalifahamu hilo’nikasema

‘Sijasema hivyo, ...sijashirikiana na muaji wa Makabrasha, hivi nyie hamuelewi, jinsi gani tulivyo na Makabrasha, yule ni ndugu yetu, hivi kuna mtu anaweza kumuua ndugu yake, na uone kaka alikwenda kuonana naye kwa ajili ya mambo ya kisheria, yeye alijitolea kumsaidia kaka, sasa tuje kumgeuka na kumuua, mbona haliji akilini...huo ni uzushi tu’akasema na kutulia

‘Hujasema hivyo ndio kuwa wewe ulisaidia kumuua Makabrasha, ila umesema wewe ndiye ulichukua bastola yangu, ukaipeleka huko ulipoipeleka,..hiyo bastola ndiyo iliyotumika kwenye mauaji,maeelzo yak ohayo yanakuponza, hapo huwezi kukwepa mkono wa sheria baba  maelezo yako uliyoyatoa hapa yanaonyesha hivyo,...’nikasema huku nikigeuka kwenye meza ndogo iliyokuwa pembeni yetu.

‘Unaona kile kifaa pale,  kinachukua kila kitu tulichoongea hapa, kwahiyo, kwangu mimi huna ujanja, pili nina ushahidi mwingine utakaokutia jela, ushahidi ambao, utaongea badala yako,nina imani ushahidi huo utaniambia kila kitu...’nikasema

‘Ushahidi gani huo shemeji...’akasema huku akiniangalia kwa mashaka.

‘Nikuulize kitu , hicho kitufe chako unahifadhia kazi za ofisini kama ulivyodai,  au kuna mambo mengine binafsi?’ nikamuuliza

Hapo akaduwaaa, akaniangalia , na macho yakamtoka pima, akainamana na kusema;

‘Ina maana shemeji umefikia hapo sikuhizi, mbona sio tabia yako, kuchukua vitu vyangu bila idhini yangu...!?’akasema

‘Ni nani aliyeanza kuchukua vitu vya mwenzake bila idhini ya mwingine, mimi sikuwa na tabia hiyo, nilikuwa nakuamini kupita kiasi, lakini wewe na kaka yako mukanigeuka, na nimeona hakuna njia nyingine ila ni kufanya hivyo, na nitafanya vikubwa zaidi ya hivyo, .....sikutaka kabisa kufanya hivyo..’nikasema

‘Kwahiyo shemeji unataka mimi nifanye, nini,..hebu jaribu kuniangalia na mimi,...huku kaka huku wewe, nifanye nini, mbona mnanionea bure,   ...’akawa analalamika.

‘Shemeji mimi nakuomba tafadhali, nipo chini yamiguu yako, kama umekiangalia hiki kitufe, naomba iwe siri yako..nakuomba tafadhali,.....’akasema na kutaka kunipigia magoti , na mimi nikageuka kuondoka, nikisema;

‘Nimeshakupa muda wa kutosha, ...na bado hutaki kuwa upande wangu, na nafanya haya kwa manufaa yenu, hebu fikiria jinsi kaka yako alivyofanya, nini ingekuwa mwisho wake, unafikiri nyie mngelifaidi nini, jasho letu lote lingeishia wapi, ....hivi nyie hamlioni hilo, au kwa vile hamna hasara nayo, hata kama mnaona hakuna hasara nayo, lakini angalieni muda tuliotumia, fikirieni kwa makini ..hamuaoni hiyo kuwa ni dhuluma.Mwisho wa siku mali yote ingeenda kwa, Makabrasha, angelichukua kila kitu, na kuwaacha nyie mikono mitupu,....’nikasema.

‘Oh shemeji,...mimi hayo nilimuonya kaka, hakunisikiliza, kaka akiamua jambo lake, haambiliki, mpaka aone mwisho wake,...oh shemeji kama umeangalia mambo yangu, umeniweka kubaya...’akasema huku akiangali huku na kule

‘Umejiweka mwenyewe kubaya, ..wewe na kaka yako mpo ukingoni mwa mto uliojaa mamba, mumejichimbia wenyewe kaburi, sitaki kuwatisha, ila nawaonya na kuwapa muda kidogo wa kusema kila kitu,bado muda mnao, jitokezeni mseme ukweli kabla mambo hayajaharibika, vinginevyo, sijui kama kutakuwa na suluhu juu ya hili, nenda kaongee na kaka yako, mjipange vyema...’nikasema na kuondoka.

‘Nitaongeaje na kaka wakati anaumwa?’ akaniuliza na mimi sikumjibu kitu, nikaondoka na kumuacha akiwa kasimama, kachanganyikiwa, na haukujua afanye nini....mimi sikumjali, nikaondoka kuelekea ndani.

Nikasubiri kama nusu saa, nikamuona akija , lakini baadaye akabadili mawazo, nikamuona akiondoka, huku kainama chini,alikuwa kama jogoo aliyeloweshwa maji, akachukua pikipiki lake na kuondoka, na mimi nikaichukua laptop yangu na kuanza kuangalia ni kitu gani kilikuwa kwenye kile kitufe, alichokuwa nacho shemeji yangu...


NB: Kisa ndio hicho kinafikia mteremko, ndio tukaingia kwenye hitimisho, tukiwa na maswali mengi;
‘Je ni nani aliyemuua Makabrasha, na je mdada atagundua ukweli wa msaliti wake wa ndoa, je atatimiza ahadi yake...tusubiri tuone.


WAZO LA LEO: Kuna watu inapofikia hatua ya kupata mali, wanapohisi kuwa kuna masilahi, wanapokuwa na uhakika wa kupata pesa, vyeo, ....hawaangalii tena ubinadamu, wema, unaondoka na kinachobakia moyoni ni ubinafsi,....watu kama hao wapo tayari hata kuwadhulumu, wazazi wao, au watoto wao, au marafiki zao, achilia mbali ya bosi kwa mfanyakazi wake. Mali , pesa , vyeo ni mtihani mkubwa kwetu, tuweni makini kwa hilo, tuangalie na kuchunga  haki ya mtu, tuangalie na kuchunga dhamana za watu, hayo ni madeni makubwa, kama tutahini.
Ni mimi: emu-three

No comments :