Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 25, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-35



Kuotakana na afya ya mume wangu kubadilika, ilinibidi nia nze kufikiria upya yale niliyoyapanga, kwanza kiubinadamu, halafu kimkataba, na zaidi huyo anayeumwa ni mume wangu. Lakini hata hivyo, ilinibidi nifikirie zaidi jinsi gani ya kulimaliza hili tatizo, kwani kama nitaamua kusubiria mpaka mume wangu apone, mambo mengi yataharibika,...

Hapo nikakumbuka kuwa wanafamilia wa mareheme Makabrasha walishapanga tukutane, kujadili mustakabali wa mkataba aliouacha marehemu japokuwa mimi niliwakatalia kuwa siutambui, lakini kisheria ulikuwa na mantiki, na kuna ndugu yao mwingine ambaye alishatishia kulipeleke hilo swala mahakamani kuwa marehemu aliacha mkataba ulidai kuwa yeye alikuwa na hisa kwenye makampuni yangu.

Hili lililozuka sasa hivi linaweza likawa ni sababu ya kuchelewesha mambo ili mipango iliyopangwa ifanikiwe, lakini pia inaweza ikawa ni moja ya majaribu tu, kuwa litokee hivyo na muda kama huo ili lifanyike jamb....na mimi nina msimamo wangu kuwa likitokea tatizo ni bora kupambana nalo , ni bora kusimama kidete, na kuhakikisha unakabiliana na hilo tatizo, ...sikukubali kubweteka,au kukimbia tatizo, sio tabia yangu.

‘Nitapambana na kila anayejaribu kuingilia maisha yangu...’nikajipa moyo.

Baada ya mume wangu kufikishwa hospitalini nikarejea nyumbani na kwanza kabisa nilihakikisha kila kitu kipo kama kawaida, na ule mto na shuka lililotobolewa na risasi nilivikunja vizuri, na kuvihifadhi mahaal salama, kama vitahistajika kiushahidi. Hata ile bastola, mimi nilihakikisha siugusi bila soksi ya mkononi, vyote hivyo nikavihifadhi sehemu salama.

Nilijua kabisa sauti ya mlio huo wa bastola itakiwa imesikika kwa majirani, na nilishapanga jinsi gani ya kuwajibu, niliwaambia hakuna tatizo,....sikutaka kuwaambia lolote, kwani kila kauli utakayotoa, inaweza ikaja kukushitaji baadaye, japokuwa wengi walipoona mume wangu akitoka na kuelekea hospitali walijua huenda yeye ndio kaumizwa ...

Dunia haina dogo, hata mwandishi mmoja wa habari alifika kutaka kujua zaidi nikamwambia hakuna cha zaidi, hakuna tatizo, na ole wake akiandika mambo ya kizushi...na wananifahamu hakuna lolote lililoandkwa kwenye magazeti.

Tuendelee na kisa chetu....

*********

Baada ya mume wangu kukubali kwenda huko hospitalini, japokuwa hakupendezewa sana, kwani yeye aliona ni tatizo la muda tu, na alihisi kuwa limekwisha, kwani alivyoamuka alijiskia sio kama alivyokuwa akijiskia jana yake, na hapo kwa kumjaribu nikamuuliza maswali kama anakumbuka kuna kitu gani kilitokea usiku yeye alisema hakumbuki lolote, ina anahisi aliota ndoto ambayo haikumbuki vyema ilikuwaje,

‘Kuna ndoto niliota, lakini sikumbuki ni ndoto gani,...sikumbuki kabisa, lakini ilikuwa kama ya sio nzuri....’akasema huku akijaribu kukumbuka

‘Jana hukuwahi kuingia maktaba usiku ukachukua kitu?’ nikamuuliza

‘Hapana, mimi sijaingia huko kabisa, hilo usinidanganye, nakumbuka nilipotoka matembezi na mdogo wangu, .....wewe mwenyewe ulikuwepo, niliwahi kwenda kulala,....na sikuamuka tena hadi asubuhi,’akasema akijaribu  kukumbuka.

‘Na ulipolala hukuwahi kuamuka kwenda kujisaidia hata mara moja?’ nikamuuliza

‘Nilala kama gogo, ....sikugeuza hata ubavu, hadi asubuhi....’akasema.

‘Basi kuna tatizo...’nikasema

‘Kwani kuna nini kimetokea?’ akaniuliza

‘Nakumbuka kama ulitoka nje, ukaenda maktaba...ukachukua kitu’nikasema

‘Sikuamuka hata mara moja, labda kama uliota, mimi nililala fofofo...na nilipoamuka nilihisi kama nilikuwa nimeota ndoto ndeefu, lakini sikumbuki kabisa nilota nini...’akasema

‘Hakuna shida, wewe jitahidi sana kutuliza kichwa....lakini leo inabidi twend hospitalini wakafanye uchunguzi zaidi’nikasema.

‘Mimi siumwi mke wangu hali kama hiyo walisema inaweza kutokea , na itapita, usiwe na wasiwasi...’akajitetea.

‘Ulitakiwa mara kwa mara uwe unakwenda kiliniki, hujaenda, na ukumbuke kuwa uliambia kukitokea jambo lisilo la kawaida pia uende haraka ukamuona dakitari, na unaona hali uliyo nayo, unapoteza kumbukumbu, unafanya mambo usiku na hukumbuki kuwa ulifanya, ....ni muhimu tukamuone dakitari, hilo halina mjadala...’nikasema.

‘Haya mke wangu, kama unaona hivyo ni vyema, tutakwenda,.....’akasema.

‘Na utakwenda huko ukafanyiwe uchunguzi wa kina, ili tuone tatizo ni nini, kwahiyo unajiandaa kwenda kukaa huko kwa muda...’nikamwambi na hapo akashituka na kusema;

‘Hapana, ...siwezi kupoteza muda wangu huko, hakuna tatizo kubwa kiasi hicho...’akasema.

‘Wewe unasema hivyo, lakini mimi niliyeshuhudia mambo ya usiku, siwezi kukubali, ni lazima ukafanyiwe uchunguzi wa kina, kwa hiari , au...’nikataka kusema neno lakini yeye akakatiza na kusema

‘Sawa mke wangu nimekuelewa, nitakwenda,...nitafanya yote wanayotaka wao, sitaki mke wangu uishe kwa mashaka, nakupenda sana mke wangu ...’akasema huku akionyesha kutokufurahishwa na uamuzi huo....

‘Ujitahidi sana, kufuata msharti ya dakitari...’nikamwambia

‘Sawa mke wangu, usijali, nitajitahidi sana,....maana nataka kuondokana na hii hali,...unajua mke wangu niliacha kwenda kiliniki nikijua kuwa sina tatizo tena,...najua docta atanilaumu sana, lakini ...aah, hata hivyo najiona nimepona. Mke wangu nataka nipone kabisa tuchape kazi kama zamani. Tukae tufanya kazi, sitaki nije kuonakana sijui kulea familia yangu...’akasema.

‘Hamna shida, siku ukikumbuka yote yaliyopita ukaniambia ukweli moja baada ya jingine, ndio nitafahamu kuwa umepona...’nikasema.

‘Kwani sijakuambia kila kitu mke wangu, sizani kama kuna jambo sijakuambia, eti mke wangu kuna kitu sijakuambia, ...?’akauliza akiniangalia kwa mshangao

‘Hivyo unaonyesha kuwa hujapona, ukipona utakumbuka kuwa hujaniambia ukweli wote, na ni muhimu sana kwangu, ni muhimu sana kwa ajili ya familia hii...’nikasema.

‘Mhh, kweli , hakuna shida...’akasema na tukaondoka kuelekea hospitalini.

*********

Mume wangu alipofikishwa hospitalini, na kuanzwa kuulizwa maswali mengi nikiwepo , lakini alionekana kutokukumbuka mambo mengi ya nyuma, na hata kilichotokea usiku hakuwa anakifahamu, na baadaye nikakaa mimi na docta tu, muda huo mume wangu alishachukuliwa kwenye chumba cha uchunguzi, tukawa tunaongea na huyo docta.

‘Hebu niambie kuna kitu gani kigeni kimetokea kwa mume wako?’ akaniuliza

‘Kwanza namuona kabadilika kabisa sio yule mume wangu ninayemfahamu, sasa sijui ni kwasababu ya hayo matatizo au anaiigiza, maana simuelewi,..., kitabia, na hata matendo yake ni tofauti na zamani, na zaidi anakuwa msahaulivu,...’nikasema

‘Hiyo ni kawaida...nionavyo mimi ni kwasababu ya hilo tatizo,...na ushukuru kuwa yeye haikumuathiri sana, ....na hali yake sio mbaya,....yanayotokea ni matatizo ya kawaida tu. Nina uhakika kuwa akitoka hapa safari hii hali itakuwa njema kabisa,...Je kuna jingine lolote uliloligudua ambalo hakuwa nalo kabla?’ akaniuliza na mimi nikatulia kidogo akili ikiogopa kusema tukio la jana, sikutaka lijulikane na watu wengi, nikasema;

‘Eti docta kuna mtu anaweza kuamuka usiku akafanya kitu na akiamuka asubuhi hakumbuki kabisa?’ nikamuuliza

‘Kwa vipi, anaamuka akiwa na fahamu zake, au anakuwa amelala, ....maana kuna ugonjwa wa namna hiyo, lakini mtu wa namna hiyo anakuwa amelala, anaamuka akiwa usingizinini, na kutenda matendo ukiwa usingizini,..hajijui hapo, ....’akasema.

‘Kwahiyo anakuwa kwnye ndoto, lakini tofauti ya ndoto yake na ndoto za kawaida ni kuwa, yeye anatenda yale matendo kivitendo, ....’akasema.

‘Na hili linatokea kutokana na hiyo ajali yake?’ nikauliza

 ‘Ndio inaweza ikawa hiyo ni sababu, maana ubongo ni kitu, makini sana, kikipata mtikisiko wa namna kama hiyo ya ajali, unaweza ukaharibu mfumo mzima wa mwili, akili, ikawa sio yako tena, ndio maana unakuta watu wanapooza viuongo, wanapoteza kumbukumbu na wengine wanaharibikiwa kabisa...’akasema.

‘Lakini pia tatizo kama hilo linaweza kuwa ni la kurithi, huenda familia hiyo kuna mtu mwenye tatizo kama hilo, baba,mama, au wazee wao, lakini hili la mume wako, litakwisha tu maana kwa silimia kubwa tunaona ni kutokana na hiyo ajali iliyomkuta, na kama ni la kizalia ndio limejitokeza sasa, tutajua jinsi gani ya kulidhibiti..’akasema

‘Kwahiyo anaweza hata kufanya mambo mabaya bila kukusudia?’ nikamuuliza

‘Ndio... wengine wanafiki hata kuua, ukisoma visa vingu, huko Ulaya imetokea, hata hapa kwetu, tatizo huku kwetu hatuna kumbukumbu, lakini mambo kama hayo hutokea ...’akasema

‘Oh, sasa utawezaje kuishi na mtu kama huyo?’ nikauliza

‘Cha muhimu ni kufahamu chanzo cha matatizo hayo, je ni ya kuzaliwa nayo, kwenye ukoo wao kulikuwa na kitu kama hicho, au ni kutokana na majanga kama haya ya ajali,...baada ya hapo kuna utaratibu wa matibabu,....je mume wako amekuwa na tabia kama hizo?’ akauliza

‘Nahisi ndio hivyo..jana alitoka kitandani akaenda sehemu nyingine, akafanya matendo , na akarudi na bahati mimi nilikuwa sijui , nikamshitua, akadondoka akapoteza fahamu...sio kupoteza fahamu , ila alionekana kama kalala tena,...pale alipodondoka...’nikamwambia.

‘Mtu wa namna hiyo haitakiwi kumshitua,ukimuona anafanya hivyo, unatakiwa umfuatilie tu kimiya kimiya, ili kuhakikisha usalama wake, kwani atafanya kila kitu anachotaka kufanya na baadaye anarudi kulala kama kawaida, ukimshitua, unaweza ukamsababishai madhara mengine...’akasema.

‘Oh, ...sasa kama ni hivyo, mbona inanitisha docta....’nikasema

‘Usiwe na wasiwasi, mimi matatizo hayo nayafahamu sana, ndio ujuzi wangu, hilo tutaliangalia kwa makini, kuna jinsi ya kumpima, na tutagundua ukweli zaidi, usiwe na hofu, ..kama ni kutokana na ajali litakwisha lakini kama ni kutokana na kizalia, tutaweza kuliangalai kwa namna nyingine zaidi...mara nyingi tatizo hilo linahitajia muda sana kulitatua, hasa kama ni la kizalia, na wewe mke utakuwa na kazi ya kutusaidia, ili tujue hatua kwa hatua maendeleo yake, kwa hivi sasa tunahitajia tukae naye, tumchunguze, tuone tatizo lipo wapi zaidi...’akasema

‘Mhh, sijui kama ni kizalia,....maana haijawahi kutokea hivyo kabla, labda kwa vile sikuwa makini na hali kama hiyo..’nikasema.

‘Basi hiyo kazi tuachie sisi, tunafahamu jinsi gani ya kugundua,lakini hata hivyo ningelihitajia niongee na watu wake wa asili, kuna ndugu yake yoyote wa kuzaliwa naye, baba au mama ninaweza kuongea nao kidogo, kwani hilo linaweza kutupunguzia muda, kama hakuna tutajua jinsi gani ya kuligundua kitaalamu zaidi?’ akaniuliza

‘Yupo mdogo wake lakini sizani kama anafahamu lolote kuhusu historia zao, mimi nahisi kuwa tatizo hilo limetokana na ajali....’nikasema.

‘Kama limetokana na ajali lingejitokeza mapema,tungeliligundua siku za mwanzoni kwenye uchunguzi wetu...hata hivyo, kwa vile yupo kwenye mikono yetu, tutaliangalia kwa mapana yake, usijali....’akasema

‘Sawa docta nitafurahi kama nitapata taarifa zake, na ni kitu gani mumekigundua, kama ikiwezekana mapema zaidi, kama itawezekana, vinginevyo, mimi nawategemea nyie ...’nikasema.

‘Hamna shida tutawasiliana...karibu sana..’akasema na mimi nikaondoka kurudi nyumbani baada ya mume wangu kuingizwa kwenye wodi maalumu ya watu kama yeye, na tuliagana, na akaniambia;

‘Mke wangu usijali, sina tatizo, na usiwe na haja ya kuja mara kwa mara kuniangalia, mdogo wangu anatosha, yeye nitakuwa nikimtumia kama nitahitaji kitu, wewe hangaika na familia na kazi zetu, ili mambo yasisimame...’akasema

‘Hamna shida...wewe angalia afya yako, hakikisha unafuata masharti ya dakitari, usije ukatoroka..’nikasema

‘Kwanini nitoroke,...sijawahi kutoroka hospitalini, mimi sio kichaa, au mfungwa,...nimekuja hapa kwa hiari yangu mwenyewe, na nitafuata kial kitu, usiwe na wasiwasi na mimi...’akasema

‘Sawa kila-laheri...’nikasema na kuagana naye, nikaondoka hapo hospitalini.

********

Niliondoka hapo hospitalini nikiwa sijui nifanye nini, niliona mambo yanazidi kuongezeka badala ya kupungua, sikutarajia kabisa kuwa hali kama hiyo itakuja kujitokeza , na kwa hali kama hiyo inabidi nishindwe kuchukua uamuzi mwingine ,nikakumbuka mkataba wetu wa awali kuwa mmoja akiumwa hata kama kuna kosa au tatizo kubwa, taizo hilo, au kosa hilo linasahaulika kwa muda mpaka mmoja apone ....

Nikarudi nyumbani, na kumuita fundi ambaye nilimuagiza abadili vitasa vyote vya makabati, ....nikasimamia hilo zoezi mpaka likamalizika, halafu nikahakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, sikutaka kuangalia ndani ya makabati, japokuwa nilikuwa nataka kupitia pitia kabati la mume wangu, lakini nikaona huo sio wakati muafaka, kwani nilijua hakuna kitu cha zaidi ndani ya kabati hilo.

Wakati nataka kuelekea bustanini , kwani napenda sana kupumzika kwenye bustani yangu, mara akafika, mdogo wa mume wangu, alionekana kuwa na haraka, alisema kaja kuchukua baadhi ya vitu vyake alivyokuwa akivifanyia kazi usiku, huwa ana kazi zake anazozifanya, hata kama hayupo ofisini,  nikamwambia hakuna shida mimi nipo bustanini, akitaka kuondoka  aniambie.

‘Sawa, na kuna vitu kaka kaniagiza,nija kuvichukua ....’akasema

‘Sawa wewe mchukulia,mimi nipo bustanini, ukimaliza uje, nataka tuongee kidogo kabla hujaondoka....’nikasema.

‘Sawa lakini nina haraka kwani kaka anahitaji hivyo vitu vyake haraka, kaniambia nisichelewe...’akasema na mimi sikumjibu kitu nikijua ananikwepa tu, lakini nilishajua wapi pa kumpatia, na nilipanga kuwa akitoka tu nitambana kwa maswali muhimu,...nikaelekea bustanini na kumsubiria.
Baadaye alikuja bustanini, na kuniambia anataka kuondoka, na alionekana kama ana wasi wasi fulani, nikamuuliza keshachukua hivyo vitu alivyomuagiza kaka yake;

‘Ndio, lakini kuna kitu kaniagiza kaka, ...sasa kabati lake halifunguki..’akasema.

‘Kabati gani hilo?’ nikamuuliza

‘Basi hakuna shida, ....labda ufungua sio wa kwake, lakini...’akasema akiangalia ufungua aliokuwa nao mkononi.

‘Hivyo vitu vipo wapi, kwenye kabati lipi?’ nikamuuliza

‘Kwenye kabati lake ....la ...la ndani kule maktaba kwenu...’akasema huku akiwa na wasiwasi

‘Ina maana umeingia chumbani kwangu bila kuniambia kwanini usingelianiambia nikaenda kukuchukulia, ni kitu gani unakihitajia ?’ nikamuuliza

‘Mhh, niliona nisikusumbue, niliingia mara moja, kwenye kabati la kaka, kanipa ufungua wake, kaniagiza yeye mwenyewe nikamchukulia baadhi ya makaratasi yake ya kazini.... ’akasema

‘Makaratasi gani ya kazini, wakati dakitari kasema hahitajiki kujishughulisha na jambo lolote la kumfikisrisha, hebu niambia ni kitu gani alichokutuma,....kwanini hakuniambia mimi, wewe unamua kuingia kweye chumba change hadi mkaitaba bila ya mimi kujua, ...ni taratibu gani hizo, na hiyo tabia umeanza lini, ina maana kaka yako alikutuma hivyo, kuwa usiniambie?’ nikamuuliza nikaona anasita sita, halafu akasema.

‘Lakini kaka ndiye kaniagiza nikamchukulie...’akasema

‘Akakuambia kuwa uingie bila kuniambia mimi, ?’ nikamuuliza

‘Lakini nilikuambia kuwa kuna vitu vya kaka anavihitajia ukaniambie nikachukue tu...’akasema, na mimi nikaona nisiendelee na hayo malumbano, nikaona nimuingie kwa njia nyingine.

‘Hebu niambie jana mlipoondoka na kaka yako mliongea nini?’ nikamuuliza

‘Mambo ya kawaida tu ya kimaisha’akasema huku akionyesha kutaka kuondoka, na mimi sikujali nikaendelea kumuuliza

‘Kama yapi....nakuuliza hivyo, kwani unakumbuka jana ulisikia mlio..’nikasema nay eye kusikia hivyo akageuka kuniangalia mara moja, na kutulia kidogo halafu akasema;

‘Ndio hivi ilikuwa ni nini, maana nilisikia kama mlio wa bunduki, au bastola, kuna muda nimemuliza kaka, yeye anasema hajui kama kuna kitu kama hicho kilitokea’akasema

‘Yote hayo alifanya kaka yako, ..ndio maana nataka kufahamu jana mliongea nini’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka, na kusema;

‘Tulichongea ni mambo ya kawaida, aakitaka kujua maendeleo yangu, na akawa anaelezea mipangilio yake kuwa yeye anataka kufanya bidii zaidi katika kampuni zake  na kuhakikisha kuwa uzalishaji unakwenda juu, na kuhakikisha familia yake inakuwa vyema...’akasema

‘Kakuambia kampuni zake, kwani yeye ana kampuni ngapi, na kwanini akuambie hivyo ina maana huko nyuma mambo yalikuwa hayaendi vyema?’ nikauuliza

‘Anasema huko nyuma, alikuwa hajajitambua kuwa ana majukumu makubwa, kiasi hicho, sasa hivi kajitambua kuwa ana majukumu makubwa kama baba wa familia, kama mtendaji mkubwa wa makampuni yake, kwahiyo ianbidi abadilike, hataki kuja kulaumiwa...’akasema

‘Je mliongea kuhusu mkataba?’ nikauliza na hapo akashituka na kugeuka kuangalia sehemu nyingine, nikahisi hapo kuna jambo, kwanini nilipotaka mkataba ameonekana kama kutahayari.
‘Umenisikia swali langu, nililokuuliza...?’ nikasema.

‘Sijui unazungumzia mkataba gani, maana sielewi mambo yenu na kaka’akasema

‘Una uhakika na hilo, ...kuwa huelewi lolote kuhusu mkataba, wakati jana niliongea na kaka yako akaniambia yote, kuwa wewe unafahamu ...’nikasema

‘Kaka alisema hivyo?’ akauliza kwa mshangao

‘Ndio, ...sasa niambi ukweli, jana mlipokwenda na kaka yako hamkuongea lolote kuhusu mkataba, maana kama kakuambia kuhusi makampuni yake, huenda kafungua kampuni nyingine mimi siijui, huenda hayo yapo kwenye mkataba uliotengenezwa kimagendo,?’ nikamuuliza

‘Lakini shemeji umesema, kuwa mliongea na kaka kama mliongea naye kwanini unaniuliza mimi tena, na shemeji ni vyema hayo mambo ukasubiri kaka apone ili muongee naye vyema, ukiniuliza mimi unaniingiza kwenye mambo yenu ya ndani, ambayo sistahili kuwepo,....’akajitetea

‘Kama ni mambo ya kifamilia, kama ni mambo yetu ya ndani kwanini kaka yako anakutuma wewe mambo ambayo unajua ni kifamilia na unakubali, wewe unayafanya tena kwa siri bila ya mimi kufahamu, na kwanini wewe uwepo kwenye huo mkataba usifahamu kuhusu huo mkataba,halafu  kwanini kaka yako akakuambia mkaongee naye huko mlipokwenda , na kwanini anakuita Jembe?’ nikamuuliza na y eye hapo akawa kama hataki kusema lolote,akaniangalia mara moja na kusema;

‘Shemeji naomba unielewe, nafanya hayo kwa vile kaka ananituma, na mimi kama mdogo wake, ninawajibika kumtii, lakini ...sina  haja ya kuingilia mambo yenu ya ndani, sitaki kabisa kufanya jambo ambalo wewe litakuumiza, lakini pia sitaki kufanya jambo ambalo litamuumiza kaka yangu, wakati mwingine nafanya ili kaka asije akaathirika kutokana na kuumwa kwake,,..na yeye kama kaka anafahamu mipaak yake, nay a kwangu, akinituma na kuniambia jambp la lifamilia anafahamu ni nini anachokifanya, zaidi muulize yeye....’akasema

‘Hebu niambie ni jambo  gani ulilofanya kwa vile kaka kakuambia, lakini wewe hukulitaka kulifanya umelifanya ili kaka yako asije akaathirika?’ nikamuuliza na hapo akatulia kimiya, nikaona nisimpotezee muda .
‘Kuna kitu nataka nikuonyeshe na kama usiponiambia kile ninachokuuliza inabidi niwaite polisi, maana naona wewe unashirikiana na watu nje kuja kunifisdi...’nikasema

‘Shemeji , mimi sikuelewi, toka lini nikafanya hivyo....’akasema

Nikachukua ile mashine ya kuchukua kanda ya video nikaweka sehemu ambayo anaweza kuona, akaona jinsi kaka yake alivyofanya jana usiku...

‘Oh shemeji....mbona, ...oh, inaonyesha anampiga mtu, ...mbona ....’akawa hamalizii

‘Kwahiyo mlipanga kuwa mje mniue usiku,....ndio maana uliponiona asubuhi ulionyesha kushangaa, au unajifanay hujui alichokifanya kaka yako...?’ nikamuuliza

‘Shemeji hapana, hatujapanga hivyo, na wala sielewi kwanini kaka alifanya hivyo....kwanini tupange kuku-ua, ’akalalamika huku akishika kichwa akionyesha masikitiko.

‘Sasa mimi nimeamua, kwa vile kaka yako ni mgonjwa, lakini wewe ni mzima, unaweza kuisaidia polisi kupata ukweli wa haya, kwahiyo mimi nimeonelea niwaite polisi, wakija utawaelezea vyema, kwanini kaka yako alitaka kuniua, kama ni ugonjwa, wao watakuwa na kmbukumbu, na ninachojiuliza ni kwanini yeye akutaje wakati anafanya hicho kitendo, inaonyesha kuwa mliliongelea, na huenda wewe ulikuwa karibu ukisikilizia hayo aliyokuwa akiyatenda...’nikasema

‘Shemeji sio kweli, ..mimi jana nilikuwa nimelala , nilichelewa kulala kidogo kwani kulikuwa na kazi nazifanya, na hata usingizi ukanishika kwa haraka, nilikuja kuamushwa na mlio wa bunduki, sikujua kabisa ni nini kimetokea, na nilipoamuka ndio nikakimbilia kuja kuwaona, mimi nahisi kaka aliyafanya hayo bila kujijua,.....’akasema

‘Bila kujijua ehe,? ...., huoni anafanya waziwazi anaongea, anakutaja wewe,wewe unasema anafanya bila kukusudia...na huyo mwanamke aliyezaa naye ni nani, umesikia akisema kuna mwanamke wake, anampenda, ni nani huyo mwanamke?’nikamuuliza.

‘Mimi simjui huyo mwanamke,  ...naona alikuwa anaongea tu kama mtu aliyechanganyikiwa...huoni hata sauti yake inasikika kama mtu aliyelewa, kama teja, kama mtu yupo usingizini....’akasema.

‘Kila kitu nikikuuliza mimi unasema hujui, unasahau kabisa mimi ni nani kwako, na ni jinsi gani nilivyojitahidi kuhakikisha umefika ahpo ulipofika, ...sasa huenda na mimi natakiwa kufanya jambo ili niheshimike, uniheshimu kama mke wa akka yako, ..au unaiona kuwa mimi ni mjinga wenu, fadhila zangu ndio malipo yake haya, na sasa mnataka kuchukua kila kitu, kuniua eeh, kabla sijafa, mtakufa nyie, na hamtachukua chochote, mtarudi kama mlivyokuja, ...lakini kama utaniambai ukweli, mimi ni biandamu nitaangalai jinsi gani ya kufanya...’nikasema

‘Hapana shemeji sio hivyo , kaka anakupenda sana asingeliweza kufanya kitu kama hicho akiwa sawasawa, mimi nahisi kafanya hivyo, kutokana na kuchanganyikiwa...na unataka nikuambia kitu gani..mimi sijui zaidi ya hayo, msubiri kaka utamuuliza’akasema

‘Ngoja niwaite polisi, wakija utaongea nao hivyo, kwasababu sasa mimi siiwaelewi, kuna kitu mnataka kunifanyia, na nisipojihami mapema mtanimaliza......wewe utaweleza  yote jinsi gani unavyofahamu wewe, kwa ajil ya kumbukumbu, unasikia....’nikasema.

‘Shemeji, acha usiwapigie, subiri nikuambie, ...usifanye hivyo..’ akasema na mimi nikawa tayari nimeshampigia simu ofisa mmoja wa upelelezi ninayemfahamu..

NB: Je ndio imekuwa hayo.


WAZO LA LEO: Matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, kila mtu ana matatizo yake, na huenda wewe kutokana na matatizo uliyo nayo unaweza kufikia kusema yako ni zaidi ya wengine, sio kweli, kuna watu wa matatizo zaidi na zaidi,..kuna matajiri na utajiri wao, lakini ukiingia kwenye nafsi zao hawana raha. 

Hebu mwangalie jirani yako, maisha yale yalivyo, huenda ni duni na ana shida zaidi yako, ana matatizo makubwa kuliko yako kwako,hebu mwangalie yule ambaye ana mapungufu fulani mwilini, wengine hawana miguu, mikono, wamepooza...lakini bado mungu anawalia waanishi, sembuse wewe uliye mkamilifu, .Cha muhimu usikate tamaa, jitahidi, ukijua kuwa yote ni maisha.

Ni mimi: emu-three

No comments :