Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, November 15, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-29


Mtoto wa marehemu alionekana mtu mwema, na alikuwa tayari kuniambia mengi ambayo huenda yangelifanikisha malengo yangu, ya kutaka kujua ni kitu gani kinachoendelea, kitu gani kilichoweza kumbadilisha mume kiasi hicho,lakini yeye akatoa ombi , kabla hajasema yale mambo muhimu ninayoyataka;

‘Nataka umsikilize mume wako..mkubaliane naye..mkisha kubaliana naye , mkawa kitu kimoja,basi sisi tutajitoa kabisa kwenye huo mkataba ulioandaliwa, mkataba huo ulionyesha kuwa baba ana hisa kwenye kampuni zako, ...’ Nilijiuliza huyu mtu kawekeza lini kwenye kampuni yangu.
Nikaendelea kumsikiliza huyu jamaa, akisema;

‘Pia baba ana zaidi ya nusu ya hisa kwenye kampuni ya mume wako, ina maana yenye ndiye mwenye usemi kwenye kampuni hiyo...’ hili lilinifanya nimuone mume wangu hana maana, utakubali vipi kumpa mtu mamlaka kwenye kampuni yako mwenyewe, kuna tatizo gani, kampuni inajiendesha haina amdni, iweje umpe mtu hivi hivi, hapo nikahisi kuna tatizo.

‘Yule jamaa aliendelea kuesema kuwa, yeye kachelewa kuondoka kwasababu ya kuhakikisha kuwa maagizo aliyoyaacha baba  yake yanatekelezwa, inaonekana baba yake alishajua yupo kwenye hatari, na ndio maana aliacah hu usia.

‘Wao kama familia walisema hawataki kujihusisha na mambo aliyokuwa akiyafanya bba yao, na hata yale aliyoyaacha kwao waliyaona ni machafu, sio halali,...ila wanachotaka wao , baba yao mdogo, kama walivyomtambua, yaani mume wangu, asije akapata taabu kutokana na hayo yaliyotokea nyuma,kwani kwao ni mtu aliyewatendea wema, na wao ni nafasi kwako kulipa fadhila, wakisisitiza kuwa, wema wake aliowatendea kwao ni mkubwa sana...’

Mimi niliposikia hivyo, nikahisi kuna kitu kimejificha hapo, au kuna jambo linapikwa, na nisipokuwa makini, ninaweza kukubali matakwa yao, nikajikuta kwenye matatizo mengine, lakini hata hivyo, sikuwa tayari kukubaliana na ombo lao kama walivyotaka, ila nilitaka kupata mengo zaidi, ambayo huenda yakafichua hayo yaliyojificha, ndio nikamuomba huyo jamaa amlete mama yake niongee naye..

Nikamwambia;

‘Naweza kuonana na mama yako.....?’

Endelea na kisa chetu.......

‘Unataka kuongea na mama, nashukuru sana, kama unataka kuongea naye, kwani hata yeye alikuwa na hamu sana ya kuonana na wewe, ...’akasema.

‘Na yeye alikuwa na haja gani na mimi?’ nikamuuliza

‘Pamoja na hayo yaliyotokea, yeye alishasikia sifa zako, za uchapa kazi, na kwa vile yeye ni mjasiriamali, alikuwa na hamu akuone, ajifunze mengi kutoka kwako...’akasema.

‘Kwani mama yako huko kijijini anafanya nini?’ nikamuuliza

‘Amejiajiri, ana miradi yake, ni mmoja wa viongozi wa akina mama, na tunataka awekeze hapa Dar, lakini hiyo ni mipango ya baadaye...’akasema.

‘Mnataka kufanya hivyo kwa urithi wa baba yenu, maana nasikia ana nyumba zaidi ya tano, .....?’nikauliza.

‘Nyumba zote tumepiga mnada, kwa ajili ya kulipa watu, waliopata madhara kutokana na mambo yake, ...hutaki chochote kutoka kwake,ila tulitaka kulisafisha jina lake ili mungu amsamehe, na hilo tumajitahidi kwa kuhakikisha kile alichokichuma, ndicho kinachofuta madhambi yake...’akasema.

‘Mnaonekana hamtaki ubaya wa baba yenu uwangilie na nyie?’ nikauliza

‘Ndivyo tunavyotaka, lakini watu wengine wanaonekana kutokutuamini, hata hivyo, hata kama hawatatuamini sisi tutafanya yale tunayoona ni sahihi, tukimaliza hayo, basi wale wenye nia njema na sisi watatuamini....’akasema

‘Mimi sina ubaya na nyie, kama kweli mna nia hiyo njema, ila sitaki mtu kuniingilia kwenye mambo yangu, ....baba yenu alianza hivyo, akajitahidi, na nilimkanay sana, bado hakuchoka, akatafuta mbinu mpaka akaweza kuingia kwenye mambo yangu hata bila ya mimi kufahamu..’nikamwambia.

‘Kwahiyo, ili kweli niwaone kuwa hampo nyuma yake, na hamna nia njema, nawataka kwanza, nipate mkataba wangu, ambao yeye aliubadili....’nikasema na yeye akanikatiza na kusema;

‘Sisi hatujui lolote kuhusu mkataba wenu, sisi mkataba tulioupata ambao hata wakili wetu anaufanyia akzi ndio huo, unaoonyesha  kuwepo kwa hisa za baba kwenye kampuni zenu, na ndio maana kwanza tulitaka kulithibitisha hilo, na mume wako, amethibitisha hilo...ila alisema kuwa hiyo ya umiliki wa hisa zaidi ya nusu, ya hisa, hakuwa na hiari, ..ilikuwa kama shinikizo kwake, alikubali tu ili mambo yaishe..’akasema.

‘Aliwaambia ni kutokana na shinikizo gani?’ nikamuuliza

‘Hakutaka kusema ni shinikizo gani, lakini kwa vile tunamfahamu baba, kuwa akiwa anatafuta kitu, hasa mali, hajali aliyepo mbele yake, hatukutegemea kuwa watafikia hatua ya kushinikizana kiasi hicho, kwani haiingii akilini, mume wako akubali kumpa nusu ya hisa baba..ni lazima kuna kitu kipo nyuma yake...’akasema.

‘Wewe hukugundua ni kitu gani?’ nikamuuliza.

‘Naona niliyotaka kukuambia kwa sasa yanatosha, na kwa vile unataka kuongea na mama, ngoja nikamuite, muongee naye, nitamsubiria kwenye gari...’akasema

‘Ina maana mumekuja naye!?’ nikamuuliza kwa mshangao.

‘Tulikuwa naye, alikuwa na mambo yake, nikamwambia napitia kwako kwanza kujaribu kama utakubali kuongea na mimi, ...yupo nje kwenye gari....’akasema

‘Sawa nitafurahi nikiongea naye, na samahani sana, kwa kutokukubali ombi lenu mapema, unafahamu hali halisi, mambo yametokea mengi kiasi kwamba huwezi kumwamini mtu tena...’nikasema.

‘Hamna shaka, ..nimefurahi sana kuongea na wewe nah ii iwe ni mwanzo tu wa mazunguzmo yetu, na nina imani tutashirikiana kulimaliza hili jambo..’akasema na kusimama, tukashikana mkono, na akaondoka na kuniacha nikiwa nimesimama nikimwangalia anavyoondoka.

**********

Mke wa marehemu alikuwa wale akina mama wahangaikaji, wake wa shoka, hata jinsi alivyokuwa akitembea kuja pale nilipokaa alionekana ,mama mchapakazi,...hajibaragui, au kutembea kimikogo, anatembea kama mwanajeshi, alifika pale niliposimama, kwanza akaniangalia kama ananikagua, halafu akanisogelea tukakumbatiana, na kusalimiana.

‘Siamini kama ni wewe..’akasema

‘Kwa vipi dada...?’ nikamuuliza

‘Unafahamu, nimeziona  picha zako kwenye magazeti tu, kwenye majirida mbali mbali, ..lakini unavyoonekana kwenye picha, sio sawa na nilivyokuona leo, ukiwa katika hali yako halisi...’akasema

‘Kwani leo nipo vipi na huko kwenye magazeti naonekana vipi?’ nikamuuliza.

‘Tuyaache hayo, maana sisi akina mama tukikutana mengi tutakayoanza kuzungumzia,ni  mavazi, muonekano , sura, hata tutasahau jambo muhimu, na majukumu ya kila siku, mimi siku hizi sitaki kupoteza muda tena, na tangu nije hapa Dar, naona napoteza muda wangu bure...’akasema huku akikaa kwenye kiti.

‘Haya niambie kulikonI, mna matatizo gani na mume wako?’ akakimbilia kuniuliza hilo swali.

‘Kwanza nikupe pole za msiba wa mumeo, japokuwa siku ile nilifika kukupa pole,lakini hatukuweza kuongea vizuri, nahisi bado kulikuwa na hisia kuwa huenda mimi ndiye niliyemuua mume wako..’nikasema.

‘Ni kweli kibinadamu,ni lazima iwe hivyo, japokuwa mimi na mume wangu tulikuwa mbali sana, lakini ni mume wangu,sikuwezi kumkataa, japokuwa yeye, kwa kauli yake, alishanifanya kama sio mke wake....na huoni sasa naitwa mjane, maana nilikuwa mke wake, akubali asikubali.. ..sina budi kulikubali hilo, na yote ni mapenzi ya mungu..’akasema akionyesha huzuni.

‘Je wewe ulikuwa ukimpenda mume wako?’ nikamuuliza.

‘Sana tu...huwezi amini, mimi nilikuwa nampenda sana mume wangu, na nikuambie ukweli, mimi ndiye niliyemtaka mume wangu..awe mpenzi wangu, japokuwa ndoa ilikuwa kama ay kulazimishana...’akasema na kunifanya niingiwe na hamu ya kuyafahamu maisha yao.

‘Hebu niambie ina maana wewe ndiye uliyemtongoza mume wako? ‘nikamuuliza kiutani

‘Haswaa, mimi ndiye niliyemtongoza mume wangu, sio kwamba alikuwa hanipendi, kihivyo, hapana, kipindi hicho tulikuwa kwenye ushindani wa kumpata yeye, ..tulikuwa wanawake watatu,,kila mmoja anataka yeye ndiye ampate huyo mwanaume, kipindi hicho yeye ni kijana, sisi ni mabinti wadogo sana,...ilikuwa hapatoshi, lakini mwisho wa siku nikasimama mimi kidedea, ..tukawa wapenzi, japokuwa upenzi wa kijijini ulikuja kulete matatizo tu...’akasema.

‘Hongera, ...’nikasema

‘Unafahamu, mimi tangu nikiwa mtoto, nililelewa kwa shida, sikuwahi kupata raha, ...wazazi wangu hawakunidekeza, hawakuwa na kitu, kwahiyo ilikuwa ni maisha ya suluba, ..kula na kulala kwa shida, ..unajua maisha tena ya kijijini..basi ikatokea nikamfahamu mume wangu, kiajabu ajabu tu,yeye alikuwa msomi, na tena msoni kweli, ....kila mara humuoni hivi hivi, anakitabu, ana karatasi, anaandika..’akasema huku akitabsamu.

‘Yeye nakumbuka tangu nimfahamu, alikuwa ni mtu wa kusoma vitabu tu...hata alipokimbilia mjini, na baaadaye akawa anafika fika, alikuwa muda mwingi ukimuona  kashikilia kitabu, hivi vitabu vya hadithi, alikuwa anapenda sana kusoma vitabu vya kizungu, nakumbuka kuna vitabu vyake, aliwahi kunionyesha, hata mimi baadaye nilipojiendeleza nimekuwa nikivisoma, hivi vinaitwa, eeh, Jemsi Hadley Chase, na Peri 
Masoni, nahisi ndio maana akajikita kwenye uanasheria...’akasema.

‘Siku ya kwanza kukutana kwetu, ilikuwa kama vile wanavyoonyesha kwenye sinema, maana ilikuwa ni kwenye shughuli, mimi nilikuwa kasichana, na bahati mbaya mwili wangu ulikuwa haraka, ni baadhi ya wasichana kijijini kwetu tuliokuwa kimwili haraka, ...ilikuwa siku hiyo nafanya usafi kuwaandalia wageni, mara wakati nawapelekea watu maji ya kunywa, nikagongana naye, ..akadondosha kitabu chake, kikalowana maji...maana kulikuwa na maji maji sakafuni, mimi nikakiokota na kukifuta kwa kitambaa change cha kichwani.

Nilipomaliza nikamkabidhi kitabu chake, kumbe mwenzangu wakati wote huo nahangaika kukifuta kile kitabu, alikuwa akinitizama, na hata namkabidhi hicho kitabu, bado alikuwa akinitizama tu machoni....hapo bado mbichi nasoma...urafiki ukaanza, ooh, sijui ilikuwaje, nikabebeshwa mimba,....balaa likazuka...siunajua tena enzi hizo...nikafukuzwa nyumbani...’akasema.

‘Nilikwenda kuishi kwa bibi, mpaka nikajifungua...hebu fikiria, darasa la sita enzi hizo, unabebeshwa mimba,hata darasa la saba sikumaliza, ingawaje baadaye nikijisomesha, usinione hivi , nilijisomesha hadi sekondari, kiaina aina.

‘Basi aliponipa mimba, wazazi wangu wakafahamu, palikuwa hapatoshi jamaa huyo akakimbilia mjini,....’akasema

‘Lakini umesema wewe ndiye uliyemtongoza, naona hapo inaonyesha yeye alikupenda pendo la awali,...au sio, lile pendo watu mnaonana hapo hapo, kunajengeka hisia za kupenda...’nikasema.

‘Baada ya pale, siunajau tena mambo ya shule, nikawahadithia wenzangu, basi, marafiki zangu kila mmoja akataka amjue, na walipomfahamu ikawa ndio kila mmoja anajinadi kuwa huyo ni rafiki yake, mimi ikaniuma sana, ina maana kuwaelezea wenzangu ndio imekuwa nongwa..basi nikaona nisilaze damu, ...’akasema.

‘Nilipoona wenzangu wanambana sana huyo kijana, kila mara wapo naye, nikaamua kumwambia ukweli, ilikuwa ni kazi nzito, lakini mwisho wa siku alikubali kuwa hata yeye ananipenda sana tangu siku ile kwenye shughuli, basi...mambo yakaanzia hapo, ikawa mimi na yeye, nikawa nachapwa nyumbani kwa ajili yake, sikusikia,...haniambii  mtu...na asiyesikia la mkuu huvunjika mguu...ikatokea kama mchezo tu, ...’akatulia.

‘Pamoja na urafiki wetu huo, hatukuwa na mambo ya kisasa, haya ya kimjini mjini, hapana...ilikuwa ni kukaa pamoja kuongea, kutaniana, kukimbizana,...ila siku hiyo sikumbuki ni kitu gani kilitokea, na tukajikuta tumefanya jambo ambalo ndilo lilimleta huyu mtoto wangu duniani....’akatulia kidogo.

‘Nilitenda hilo mara moja, na ikawa nio tiketi ya shida, ...shida kweli...na nikuambie ukweli, mtoto huyo niliteseka kwenye mimba yake, nikamlea kwa shida sana, huwezi amini. Siwezi hata kukusimulia, ....na mungu hakunitupa, pamoja na kumlea kwa shida, sikupenda awe mtoto wa ovyo ovyo, nilijitahidi kumlea kihali niliyoona ni njema kwake..’akasema.

‘Ina maana ulipomzaa huyo mtoto, hukupata msaada kutoka kwa mume wako?’ nikamuuliza.

‘Msaada gani, angelipata wapi pesa za kunisaidia wakati yeye mwenyewe alikuwa kula kulala..hana mbele wala nyuma, na aliponipa mimba akakimbilia mjini kujificha, hakuonekana, hadi nilipojifungua na alifika kwa mara ya kwanza mtoto anatembea,hamjui ,.....na sikutaka hata kuongea naye..’akasema.

‘Ikawaje sasa mpaka mkafunga ndoa?’ nikamuuliza

‘Wazazi wangu waliweka shinikizo..kuwa ni lazima anioe...huoni , hata nikiwa naye naonekana mimi ni mkubwa kuliko yeye, lakini ni kwasababu ya maisha, na mwanamke mara nyingi anaonekana mkubwa, kama mkiwa umri sawa..sisi wanawake tunakuwa haraka haraka, na ukizaa ndio basi tena...’akasema.

‘Basi ikabidi kweli anioe, japokuwa hakutaka, alishaniona sifai tena..japokuwa mimi nilikuwa nampenda kweli kweli,...hata tulipoona hatukuwa sawa, ilionekana kama ndoa ya lazima, akawa ananinyanyasa, ...yaani sikuwa na raha na yeye, na hakutaka hata kutembea na mimi, yaani tutembee kama mke na mume, haikuwahi kutokea....aliniona simfai, mwanamke wa kijijini, mshamba,  asiyejua kujiremba...na yeye keshakulia mjini, anawafahamu warembo wa mjini, eeh..’akasema akibenua mdomo kwa dharau.

‘Basi bwana, ..mimi nikawa mama wa kijijini, sikujali, bado nilimtambua yeye kama mume wangu, yeye akawa anishi mjini , mimi kijijini, sikujali, nikawa napigika kijijini, maisha ya shida, ..hanitumii pesa, akibahatisha ni mara moja kwa miezi mitatu, ni pesa yenyewe pesa basi, nikawa nahangaika kivyangu kumlea mwanangu, sikujali na wala sikukata tamaa, na wala sikuwahi kumsaliti mume wangu...’akasema.

‘Nikawa naletewa taarifa za ajabu ajabu kutoka huko mjini, kuwa mume wangu ana wanawake, sio mwanamke, ana wanawake, anawabadili kama nguo...ikafika mahali nikamuuliza, na kumshitaki kwa wazee, nilivyosikia, hutaamini kibao kiligeukia kwangu, kuwa nasikiliza majungu, ni wapi nilimuona na hawo wanawake,...iliniuma sana, kwani mmoja wa wanawake zake, namfahamu, alikuja kuniambia yeye mwenyewe, kuwa mimi nitabakia hukukijijini yeye atakuwa akistarehe na mume wangu mjini...’akasema.

Mwanzoni nilipata shida sana, na ikafikia hatua nikaamua kumwenda huko mjini, ili nikapate huo ushahidi wanaoutaka wazee, najuta kwanini nilifanya hivyo, maana nilizalilika,....sitasahau, kwani siku hiyo nikiwa nimevalia zile nguo zetu, kwetu kijijini niliziona za maana , gauni refu...mikono mirefu, kitambaa kichwani,...nikaingia dar, ilikuwa ni mara ya tatu, nilishawahi kufika kabla.

‘Nilikuwa nafahamu wapi mume wangu huyo anaishi, nikafika bila hata ya yeye kufahamu, ilikuwa saa kumi kumi hivi, nikafika nyumbani kwake, ...kulikuwa na mvua mvua inaanza kunyesha, nikafike eneo alikopanga chumba, alikuwa na chumba kimoja, maisha muda huo hayajamnyookea,nikagonga mlango , mara akatokea mwanamke na khanga moja kiunoni, akafungua mlango, huku akisema kwa nyodo.

‘Hivi nani hawa wanaharibuu starehe za wenzao, ni Malaya gani wewe...’akasema huku akinifungulia mlango, na kuniona mimi, akashikwa na butwaa, maana ananifahamu, alikuwa mmoja wa mabinti ninaowafahamu kutoka huko huko kijijini,, binti huyo alikuwa mdogo sana kwangu .

‘Ni wewe....?’ akauliza kwanza kwa aibu lakini baadaye akabadilika na kugeuka kuangalia ndani, na kusema kwa sauti iliyojaa dharau;

‘Haya wewe bwana, kuna mgeni wako nje..’akasema na kuingia ndani, na mimi nikaingia na kumkuta mume wangu akiwa na kichupi, kakaa kwenye sofa, akageuka na kuniona, hakuonyesha ile dalili ya kushituka akasema;

‘Wewe mwanamke ni nani kakuambia uje bila taarifa, bila ya kibali changu, nataka nikiinuka hapa haupo ..rudi huko ulipotoka..’akasema huku haniangalii machoni...’

‘Mume wangu niende wapi, ..wakati nimekuja kwako, ..nitapata wapi basi muda kama huu?’ nikamuuliza

‘Utajua mwenyewe....kwani ni nani alikuambia uje, nilishakuambia kuwa sikutaki...unang’ang’ania tu kuwa wewe ni mke wangu, hebu jiangalie, hivi wewe ni shepu ya kuwa mke wangu, ...huoni aibu, eti kusema `mume wangu’, sikiliza rudi huko huko ulipotoka,unasikia...’akasema na kusimama, bila kujali kuwa kavaa kichupi tu, akanisukumia nje, huku yule mwanamke wake, akiniangalia kwa nyodo kashikilia kiuno...sikuona taabu, nikatoka nje..nilikaa pale nje, kibarazani hadi walipomaliza mambo yao, ...’akasema huku akitabasamu tu.

‘Ina maana hawakujali, na bado walikuwa wakiendelea na starehe zao?’ nikamuuliza.

‘Yaani tena kwa karaha, maana walijua nipo hapo nje, na mvua inanyesha..lakini kila kilichokuwa kikifanyiak ndani, nilikuwa nakisikia, kwa dharau..ili kunionyesha kuwa mimi sina maana..’nililowana, maana kibaraza kilikuwa hakina sehemu nzuri ya kujificha, na walipomaliza starehe zako, wakatoka wakaenda bafuni kuoga, wakavalia, wakaondoka, sijui walipokwenda, nikabakia hapo nje,sijui niende wapi.

‘Bahati nzuri jirani yao, akanikaribisha ndani, akanipa nguo nikabadili, akanipikia tukala, japokuwa chakula hakishuki, huyo huyo akanisaidia nauli, kesho yake asubuhi nikaondoka nikarudi nilikotoka,...hebu ona huo unyama, hata nauli hakunipa...nimesaidiwa na majirani ambao waliniambia mume wangu kila siku anakuja ni mke mwingine...na sijui kwa vipi hakupata ukimwi...’akasema huku akikunja uso.

‘Niliporudi kijijini, nikamsimulia mama yangu hayo nailiyoyaona, akasema, hayo ndio yo niliyoyataka, waliniambia sikusikia, ni kweli , walinisema sana, kipindi hicho, wakanichapa, lakini sikuwasikia, na niliona kweli ni dhambi zangu ndizo zinaniandama ngoja nipatilizwe, ...

‘Niliishi kijijini kwa shida, hadi nilipokutana na huyo mume wako....’akasema

‘Mlikutana na mume wangu eeh?’ nikauliza

‘Ndio mume wako, namuona kama mdogo kwangu, lakini alinionea huruma sana, kwani alikuwa akiniona ninavyoteseka, yeye alikuwa akihangaika na shughuli zake anapita kwetu ananiachia chochote,, huwa alikuwa akiniita shemeji....basi ndivyo tulivyozoeana. Hakuwahi kupita hapo bila kuniacha kitu.

‘Kuna kipindi niliumwa sana...karibu ya kufa, hatukuwa na hata senti nyumbani, sina pesa ya kununua dawa, kwani nikwenda hospitalini na kuandikiwa dawa za kununua, ...hatuna pesa, na tatizo hilo lilikuwa kubwa, hadi nikaambiwa nikafanyiwe upasuaji, ..nipelekwe mjini, hakuna pesa , na mume wangu alipoambiwa hakujali..alitaka nife tu...’akatulia.

‘Namshukuru sana mume wako, nafahamu kipindi hicho, alikuwa hajaku-oa...kama sikosei, akauza mbuzi wake, akapata pesa, na kuzileta nyumbani, hatukuamini, akasema amekuja kunisaidia ili nikatibiwe...na kweli nikapelekwa mjini nikafanyiwa upasuaji, nikatibiwa nikapona..sitamsahau mume wako...’akasema.

‘Je alifanya hivyo kwa sababu gani hasa?’ nikamuuliza

‘Yeye, alisema alifanya hivyo, kwa vile mume wangu ni rafiki yake ,mume wangu  alikuwa akimfundisha fundisha ufundi wa magari, ..udereva,..unafahamu mambo ya kijijini, basi wakaivana, sijui zaidi ya hapo ilitokeaje wakaivana kiasi hicho, kwahiyo yeye alinitambua kama shemeji , mke wa rafiki yake, akanijali kihivyo.....na ujirani mwema tu...’akasema.

‘Kwahiyo kwetu sisi , kama familia, tunamthamini sana mume wako, ni mtu mwema sana, na alipenda kuwasaidia sana watu,..sio mimi tu, ..yeye alikuwa na tabia yake ya kupenda kusaidia watu, japokuwa familia yao ina tabia ambayo wengi wanaiona sio nzuri, baba yale ni mlevi kupindukia, na mama yake akawa hivyo hivyo....basi ni familia ya shida, lakini yeye akawa anajibidisha na maisha yake, kuhangaika kivyake..hadi hapo mlipokutana naye...’akasema.

‘Mhh, kweli umenifungua masikio, hayo yaliyokukuta ni makubwa, mimi niliona nipo kwenye mitihani, lakini wewe ilikuwa zaidi, sasa ikawaje?’ nikamuuliza.

....NB: Ikawaje kwa mama huyu, tutaona sehemu ijayo, ili tujifunze kutoka kwa mama huyu, je ilikuwaje mapaka akaweza kuishi maisha ya kujitegemea, je yeye na mume wake, walikuja kuafikiana baada ya yote hayo?


WAZO LA LEO: Maisha yana mitihani yake, ukiona kwako ni kugumu, ujue kuwa kuna wenzako kwao ni kugumu mara mbili yako, ukipatwa na mitihani ka hiyo...usikate tamaa, pambana, ukijua kuwa wewe sio wa kwanza kupata mitihani kama hiyo, wapo waliopata mitihani hiyo na wakaishinda, kwanini wewe usiweze...kumbuka baada ya dhiki, mara nyingi ni faraja.
Ni mimi: emu-three

3 comments :

Yasinta Ngonyani said...

kazi nzuri ndugu yangu ..kumbuka tupo pamoja ila tu majukumu mengiiii,,Nimependa wazo la leo....mno.

EDNA said...

Jirani mimi nilipita kuomba maji ya kunywa tuu na kuacha zangu salaamu, maana ni kitambo kweli.Jumamosi yako na iwe njema jirani yangu wa ukweli.

emuthree said...

Nakushukuru sana ndugu wangu,@Yasinta Tupo pamoja, na jirani yangu, kweli ni muda kweli, hatujatembeleana, lakini yote maisha, tupo pamoja.