Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, November 13, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-27Nilizindukana na kujikuta nipo hospitalini, na pembeni yangu alikuwa kakaa mume wangu, huku kajiinamia, nikajaribu kuinuka, lakini nikahisi maumivu ya kichwa, nikashikilia kichwa, na mume wangu akanisogelea na kujaribu kunisaidia, nikainuka na kukaa vizuri,

‘Pole sana mke wangu unajisikiaje...’akasema kwa unyenyekevu.

‘Kumetokea nini?’ nikauliza

‘Inaonekana kuna watu walitaka kukuumiza huko jela...’akasema

‘Kuniumiza kwasababu gani, nimewafanyia nini kibaya, na hawo watu ni akina nani?’ nikawa nauliza maswali kwa mfululizo.

‘Hayo maswali kwasasa hayana msingi, cha muhimu ni kuwa upo salama, na hilo limesaidia kupatikana kwa dhamana yako haraka, kwani kuna watu walishaiwekea pingamizi...’akasema.

‘Oh, kumbe....’nikasema huku nikishika kichwa, sehemu ambayo nilifungwa bandejii na mume wangu akaniangalia kwa mashaka na kuuliza

‘Kwani unajisikiaje?’ akaniuliza huku akiweka mkono sehemu ile iliyowekwa bandeji na mimi nikawa najihami asije akanitonesha, na akaondoa mkono wake, na kuniangalia machoni.

‘Maumivu ya kichwa kwa mbali, lakini sio sana, haya niambie na wewe unaendeleaje, maana mgonjwa anamuuguza mgonjwa...?’ nikamuuliza

‘Mimi kwasasa sijambo, sina wasiwasi kabisa, nipo tayari kupambana na yaliyopo mbele yangu, ...’akasema huku akijiweka vyema, kama vile anajiandaa kuongea.

‘Una maana gani kusema kuwa unajiandaa na kupambana na yaliyopo mbele yako, ...?’ nikamuuliza

‘Dunia hii ilivyo, maisha yetu wanadamu yalivyo, kila siku ni mapambano, au sio, huwezi kulala tu, ukafanikiwa, ni lazima upambane, na mimi nimejifunza jambo ..’akatulia kidogo, nikawa na wasiwasi nisije nikamkwaza, nikaona nibadili maongezi, nikasema , kama kuuliza.

‘Hivi huyu wakili wangu yupo wapi...maana nataka kujua mambo yanaendeleaje...’ nikawa kama nauliza huku nikitafuta simu yangu, sikujua ipo wapi.

‘Wameondoka muda mfupi uliopita, watarudi, kuna mambo wanafuatulia....unatafuta simu yako, nahisi ipo kwenye mkoba wako, nikuletee?’akaniuliza huku akiinuka na kuchukua mkoba wangu uliokuwa umewekwa kwenye meza, sijui ni nani alinichukulia, sikutaka hata kuuliza. Akanipa simu yangu, nikaiwasha kwani ilikuwa imezimika, nikawa nimeishikilia mkononi.

‘Oh, hamna shida, ..hivi leo tarehe ngapi, ...’nikasema huku nikiangalia simu, akaniambia tarehe na saa, nikasema;

‘Ahsante sana mume wangu,..nikamtaaj jina lake, na yeye akatabasau na kusema

‘Ahsante mke wangu, na kunitaja jina langu...’nikatabasamu, halafu nikasema;

‘Kama dhamana imepatikana basi iliyobakia ni kuangalia kesi hiyo itakwenda vipi, na huyo muuaji ajulikane ni nani, ili niwe huru....’nikasema na kutulia, nikamwangalia mume wangu, nilimuona kabadilika, kakonda, na inaonyesha kuwa ana mawazo sana, nikawa naogopa kumuuliza maswali, lakini yeye akaanza kuongea;

‘Mke wangu, kuuwawa kwa Makabrasha kumenishitua sana,sikutegemea kabisa, ni kama namuona , yaani jana tu mtu mlikuwa naye, leo hayupo, keshatoweka duniani, hatutamuona tena,  hii inaonyesha kuwa sisi wanadamu si chochote...na wengine wanajiona wana nguvu wana kila kitu wanaweza kufanya wapendavyo, kuua kwako ni rahisi tu, kama wao hawatakufa’akasema.

‘Ni kweli, ndio maana umri wetu mdogo tuliopewa tunatakiwa kuutumie vyema, ukikosea na kuutumia vibaya, unaweza hata usipate muda wa kujitetea, utarudi kwa udongo, na siku ya mwisho unaamukia kwenye hukumu ya mungu...’nikasema.

‘Ni kweli,..hilo nimeliona na nimekuwa nikiliwazia sana, ...’akasema

‘Unawaza nini cha zaidi?’ nikamuuliza huku nikimwangalia usoni.

‘Hasa haya yaliyotokea kwetu, yananipa shida kweli kweli, ndio maana hata nilipokuwa hospitalini, nilikuwa nikihangaika kuweka mambo sawa, na nikitafuta njia ya kuyasawazisha, lakini mwili ulikuwa haukubali,..nilikuwa kwenye mtihani mkubwa sana...lakini sasa naona kila kitu kipo sahihi , ni swala tu la kukubaliana...’akasema.

‘Mhh, usijali, hayo yatakwisha, na maisha yataendelea, cha muhimu ni kama ulivyosema, kukubaliana, na kingine cha muhimu, ni kuwa kuna makosa yamefanyika, na kama yapo, mkosaji anahitajika kukubali kosa na kulikiri kosa lake...ili tujua jinsi gani ya kuliweka sawa, kama kuna mengine, ...basi tutakaa na kuyajadili, ..ila mimi ninachotaka, na ni muhimu sana kuambiwa ukweli...’nikasema.

‘Unataka kuambiwa ukweli, ukweli upi tena,..mmh, sawa hilo halina shida, ila ukweli mara nyingi unauma....’akasema

‘Mhh, kwanini ukweli uume, ..labda kama una mashaka, ...lakini kama una nia thabiti,ya kujua na kukubali kwa nia njema sizani kama utaumiza,...tatizo ni kuwa watu wengi hawataki kusema ukweli, wakichelea yatakayotokea baada ya ukweli . Lakini ni vyema tukajifunza kuwa wakweli, bila hivyo , hatutafika,...’nikasema nikimwangalia, na yeye akawa akiangalia pembeni, nikamuuliza

‘Vipi hali yako kwa ujumla, umepona vyema, maana tusije kuongea hapa likazuka jingine,..?’ nikamuuliza.

‘Mimi nimepona, nilifuata masharti yao,kama walivyotaka, japokuwa ilikuwa kazi nzito, maana nilikuwa kama mfungwa, lakini kiukweli ilinisaidia sana, na waliponipima kwa mara ya mwisho waliniambia nimepona kabisa, walisema kila kitu kipo safi, hakuna matatizo tena, usiwe na wasiwasi na mimi mke wangu....’akasema.

‘Kwahiyo upo tayari kusema yote yaliyotokea, , ....?’nikamuuliza.

‘Hilo ndilo nataka tuliongelee, lakini wewe unaumwa, tusubiri, kwanza, japokuwa nilikuwa na mambo muhimu, ya kujadili, na wewe...ni kweli kuna mengi yametokea, na kuna yetu wenyewe, na kuna ambayo nilisaidiwa na marehemu kidogo, kiushauri, ....hayo nayo yana nafasi yake, japokuwa yapo kwenye maandishi,....’akatulia kidogo.

‘Yapi hayo yaliyopo kwenye maandishi?’ nikamuuliza

‘Ninaongea kuhusu mkataba...’akasema

‘Unaongea kuhusu mkataba upi, maana mkataba wetu wa hiari umetoweka, na sasa upo mkataba wa kugushi, wewe hapa unazungumzia mkataba upi?’ nikauliza.

‘Mkataba wa kugushi!?’ akawa kama anauliza na kushangaa.

‘Kwani hujui, na wakati wewe na Makabrsaha ndio mliofanya hayo!’nikamwambia huku nikimwangalia nikiwa na mashaka nisija nikazua balaa, lakini sikuona mabadiliko,, yeye kwanza akainamisha kichwa chini, na baadaye akasema;

‘Mke wangu nakupenda sana, ..na nisingeliweza kukubali tuachane...mimi kama mume wako niliona ni heri nifanye jambo, kuilinda ndoa yetu, ... nilifahamu fika kama mkataba ule ungelifika kwa wazazi wako, basi mimi na wewe ingelikuwa ndio mwisho wetu ...wangeliuchukua ule kama kigezo, cha kuvunja ndoa yetu, kutokana na hayo yaliyotokea, ...nikaona nifaye yaliyo sahihi kama mume, ..nikamuona mwansheria, yeye akasema hilo kwake ni kazi ndogo tu...’akaanza kuongea.

‘Kwahiyo kumbe wewe ndiye uliyeonana na marehemu ukamwambia wazo hilo, kuwa mgushi mkataab wetu, na mtengeneze mambi yenu mtakavyo,na yeye akakubali na kulifanyia kazi?’ nikamuuliza

‘Mke wangu kuna mengi yametokea kabla ya hilo, hilo lilikuwa ni kama hitimisho la mambo mengi yaliyokuwa yamejificha, huenda hata mimi sikuwa na mawazo hayo kabla,...sipendi kumuongelea vibaya marehemu, ..kwa vile hayupo na hakuna wa kumtetea, lakini yule alikuwa rafiki yangu mkubwa sana, na mengi alikuwa kanishauri kabla, na sikuwa na mtilia maanani, na ilipotokea tatizo, nikaanza kumkumbuka yeye....’akatulia

‘Tatizo gani lililotokea hadi kukimbilia kwake?’ nikamuuliza.

‘Hilo nitakuja kukuambia kwa wakati muafaka,....’akasema

‘Kwahiyo sasa hivi unataka tuongelee nini?’ nikamuuliza

‘Kuna mambo kidogo, tunahitajika kukubaliana...tuyaongee, ili ukibali, na tukakubaliana basi kinachofuata ni utekelezaji tu...’akasema, na mimi  kwa vile sikujua anataka kuongelea jambo gani, nikasema;

‘Mhh, kama upo tayari kuyaongea hayo uliyoyaoanga kuyaongea sasa hivi, mimi nakusikiliza...’nikasema

‘Nipo tayari, labda wewe mgonjwa, kama haupo tayari, tusubiri, ..kwani muda upo, na mimi nimeahidi kuwa nitakuambia kila kitu, ..ila kwa masharti kwamba, tuyaongee kwanza wawili, na tukubaliana wawili, kama hakuna tatizo, basi,tusiwahusishe wengine, ...kwani hapa yalipofikia nahisi haya mambo yanatupeleka pabaya, kama imefikia sehemu ya kuuana, ..mimi naanza kuogopa...’akasema.

‘Unaposema ku-uana, una maana gani,?’ nikamuuliza

‘Kwanini Makabrasha ameuwawa,..?’ akaniuliza

‘Mimi sijui, ....na nimejikuta katikati ya mambo haya, na hata kushutumiwa kuwa mimi ndiye niliyemuua, wakati sijui kabisa mambo haya, na ninaona mambo mengi yanatokea bila hata kujua ni kwanini, siambiwi ukweli,...inanipa mashaka sana ...na inafikia mahali nashindwa haat kuwaamini watu, hasa marafiki wangu wa akribu, naona kama wananizunguka....’nikasema.

‘Kwahiyo kama huwaamini, hata wakikuambia ukweli, nahisi hutaweza kuwasamehe, ....?’ akaniuliza.
‘Ukweli ndio utaoamua,...maana sijaambiwa ukweli, ...’nikasema.
‘Mimi ni mume wako, niakuambai ukweli...’akasema.

‘Ni bora fanye hivyo, maana nilishaahidi kuutafuta ukweli mwenyewe, na kama ikifikia hapo, nikautafuta mwenyewe, huo ukweli nikaugundua , nikaona una nia mbaya na mimi, sitavumilia tena...’nikasema.

‘Ni kweli,...inahitajika kufikia hapo, na mimi nimeliona hilo, kuwa kinachotakiwa hapa ni ukweli, mimi sina wasiwasi na hilo maana nimeshajiandaa kwa upande wangu, mwanzoni nilikuwa naogopa sana, lakini sasa,...hata kama nitauwawa, ..kuna nini kimebakia, kama mtu aliyekuwa akijiamini kupita kiasi kauwawa, sembese mimi...’akasema.

‘Kwahiyo wewe unataka kusema nini?’ nikamuuliza.

‘Mimi nakusikiliza wewe kwanza...’akasema kwa kujiamini.

‘Sikiliza mume wangu, usije ukajidanganya na huo mkataba wa kugushi, ukajiona kuwa upo salama, huo mkataba wa kugushi, ni ukiukwaji wa sheria, na hilo tunaweza kulithibistiha  kisheria, kuwa huo mkataab wa sasa ni wa kugushi...hata kama kila mbinu zimetumika, kuubadili, lakini kila kosa lina udhaifu wake, ..’nikasema.

‘Hakuna kosa kwenye huo mkataba wetu, na sijui kwanini unauita wa kugushi...’akasema.

‘Huo mkataba mpya mimi siukubali, maana sikushirikishwa,..kwanza ni mkataba wa nani na nani, ...nasema hivi na unielewa kuwa mimi sitakubaliana na ujinga huo, nahitaji ule mkataba wa mwanzo kwanza, na kama una marekebisho ni juu yangu mimi na wewe kuyafanyia kazi, na sio mtu mwingine...’nikasema.

‘Na mimi narudia tena kukuambia mke wangu, mimi sijui kama kuna mkataba uliogushiwa, upi huo uliogushiwa....!’akasema.

‘Mume wangu acha hayo maneno...kwa kauli yako ulisema uliona kuwa kuna vipengele ambavyo vingebakia wakaona wazazi wetu, ndoa ingelivunjika, je hivyo vipengele vipo au havipo...na sasa unakuaj na kauli nyingine, ambayo nahisi inanionyesha kuwa kweli una malengo yasiyofaa, ambayo mimi sitayakubali....’nikasema.

‘Mke wangu, mimi sijui mambo ya kugushi mkataba,...mimi sio mwanasheria, nitagushi vipi kataba, na mkataba huandikwa na wanasheria, mimi ninachofahamu ni kuwa upo mkataba wetu wa hiari, na huo ndio utakaoweka mambo yetu bayana,...’akasema.

‘Una uhakika na hayo unayoyasema?’ nikamuuliza na yey e kwanza akaniangalia, halafu akaangalia chini na kusema;

‘Mke wangu, kwanini niswe na uhakika na hilo, nimeshakuambia kuwa mimi nakupenda sana, na hayo yaliyofanyika, yalifanyika kwa nia njema tu, ya kulinda ndoa yetu,  na nakuhakikishia kuwa mkataba wetu upo, na una ammbo mazuri tu, ya kuwezesha mimi na wewe tuendelee kuishi kwa amani na upendo , na mimi nitakuwa mume mwenye mamlaka kama mwanaume, sio mwanaume jina...’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo?’ nikamuuliza.

‘Mkataba ndio unasema hivyo...kuwa mimi kama mume nitakuwa na mamlaka ya uongozi wa familia, nitaweza kupitisha maamuzi, kama ninaona ni sahihi kwa masilahi ya familia....wewe utakuwa msaidizi wangu, na hiyo ndio kawaida,..mume unakuwa na nguvu ya kuongea, kwa vile una mamlaka,  kwani hapo kuna makosa...’akasema.

‘Haya unayoyaongea yapo kwenye huo mkataba, na yalipitishwa na kukubaliawa na nani?’ nikamuuliza

‘Mimi na wewe..na wakili wetu..’akasema.

‘Tatizo lako, Makabrasha alikuingiza kwenye anga zake za ulaghai, na umesahau kuwa wewe sio mwanasheria, huyo mtetezi wako hayupo tena duniani, kuna mambo ya kisheria huyafahamu,...na hayo yatakupeleka pabaya,...mkataba  uliokubalika kisheria ni ule tuliokaa mimi na wewe tukakubalina sio huo uliokaa wewe na mwanasheria wako, ....’nikasema.

‘Ndio huo huo, hakuna mkataba mwingine...kila kitu kipo sawa, kuna sahihi yako, kuna sahihi ya mwanasheria...’akasema.

‘Mwanasheria gani?’ nikamuuliza.

‘Mwanasheria wetu wa familia, ..ngoja nikuonyeshe mkataba wetu..hakuna kitu kilichobadilika, ni mambo madogo madogo tu ulikuwa huyajui, ....na yote ni kwa masilahi yetu...’akasema huku akiutoa huo mkataba, na mlangoni, niliona mtu kasimama kwa nje, nahisi alikuwa akisikiliza tunachoongea, sikuweza kumtambua ni nani,...nikataka kumpa ishara mume wangu, lakini hakuwa makini na yeye akawa ananionyesha sehemu zile za sahihi akasema;

‘Huu ndio mkataba wetu,..unaona hii hapa ni sahihi yangu, hii ni ya kwako, hii ni sahihi ya mwanasheria wetu wa familia,...hakuna kilichobadilika, ...unaonaeeh...’akasema huku akifungua fungua huo mkataba, na mimi nikamwangalia kwa makini na kusema;

‘Mume wangu usitake tufikishane huko..huko unapokwenda ni kubaya, usikubali hayo mambo aliyokudanganya Makabrasha, ..huyo jamaa anajulikana sana kwa hadaa an ulaghai, hata watu wana usalama wanalitambua hilo..sasa na wewe usiwe mshirika wake, tunachotakiwa kwasasa ni kusahihisha yale makosa yaliyotokea, ili tuanze pale tulipoishia, ...tusilazimishe migogoro isiyo na msingi, na tusitake kulazimisha chuki na uhasama, wakati kuna njia nzuri ya haki, yenye kuleta mariziano na maafikiano,...hebu nikuulize hivi wewe unachotaka hasa ni nini?’ nikamuuliza mwishoni.

‘Nakupenda sana mke wangu , sitaki mimi na wewe tuachane...’akasema

‘Ni nani kasema hatutapendana na tunataka kuachana?’ nikamuuliza.

‘Hayo yaliyotokea yangeliweza kufanya tuka....kosana, huoni ilishaanza fitina, na tulikuwa tunakwenda kubaya, nilikuwa sina kauli, ni kama mume bwege,...na hayo yalitokana na vipengele visivyo na msingi kwenye mkataba wetu, nilikuwa naogopa kuwa vipo, kumba hakuna,kumbe kuna mambo mazuri tu, ....ndio maana sasa najiamini, napigania upendo wangu kwako, na pigania ndoa yangu....’akasema.

‘Unapigania ndoa yako au unapigania mali?’ nikamuuliza na hapo akashituka na kuniangalia machoni.

‘Mke wangu nimesema kuwa nakupenda sana....sipiganii mali, kwanza kwanini  niipiganie mali wakati ipo , mali ninayo,....huwezi kupigania kitu chako, eti mke wangu, mbona sikuelewi...’akasema.

Hapo akaanza kunichefua, nikaona mwenzangu kadhamiria kweli, na ile subira ya kumuonea huruma kuwa ni mgonjwa, ikaniishia, nikaona sasa nipambane na mtu ambaye hataki kuelewa, nikasema ;

‘Kwahiyo umedhamiria hayo mliyokuwa mumepanga na marehemu?’ nikamuuliza

‘Sijapanga kitu na marehemu, yeye alinishauri tu kama mwanasheria wangu, alipitia mkataba wetu, akausoma, na kuniambia upo safi kabisa, akanionyesha hivyo vipengele muhimu kuwa nisiogope maana mimi kama mume nina mamlaka ya kufanya yale ninayoona ni sahihi kwa masilahi ya familia...’akasema.

‘Kwahiyo ndio ukafanya ulivyoona kuwa ni sahihi,..hata kama mimi sijaurizia, ?’ nikamuuliza

‘Nimefuata mkataba unavyosema, ...sijakiuka kitu, kama ilitokea kwa bahati mbaya, basi Katina inanipa nafasi ya kujirudi, ndio maana nipo haap mbele yako kukuomba msamaha kwa hayo yaliyotokea, ili tusonge mbele..katiba inasema hivyo, sisi kama wana ndoa wakati mwingine tunakosea kama wanadamu, kosa likishagundulika, na sote tukalikubali ni kosa, basi mkosaji anatakiwa kutubu, na kuomba msamaha, na sote tunakubaliana na kushikana mkono, ndio ndoa ilivyo ...’akasema

‘Basi nashukuru, nakuomba uondoke, nataka kupumzika, naona hatutaelewana kwa sasa....’nikasema

‘Lakini mke wangu kuna mambo nataka tuyaongee, ...kuna mtu anasubiri, maamuzi yangu mimi na wewe’akasema

Nani anasubiri hayo maamuzi yangu mimi na wewe, na hapa tulikuwa tunaongea tu, hakuna maamuzi yoyote yamepita hapa, ..hatujakubaliana lolote hapa.mimi siutambui huko mkataba wenu, .’nikasema.

‘Mtoto wa marehemu, anahitajia maamuzi yetu, ...’akasema

‘Nimeshakuambia hakuna maamuzi yoyote yaliyopitishwa hapa, kama una lako jambo endelea kivyako, na kama umezamiria hayo uliyokusudia, basi tutapambana,sheria ipo, haki ipo ..maana nakuona hutaki kunielewa, tukakubaliana, na nakuasa,uwe makini, usihadaike na tamaa za watu wengine, kumbuka ulipotoka,...kumbuka kuwa ndoa hujengwa na mume na mke, na wengine wote ni wapambe tu, ...ukiwafuta wapambe, mkafarakana wanandoa, hawo hawo wapembe, waliokuhadaa, watakuja kukucheka.

‘Nimekuelewa mke wangu...usijali, mimi kama mume wako sitakubali hilo litokee...’akasema huku akiinuka kuondoka, nilishangaa sana, ni kitu gani kimempata mume wangu awe hivyo..kabadilika, kawa sio yule mume ninayemfahamu...

‘Umenielewa vipi?’ nikamuuliza kabala hajatoka

‘Umesema niondoke,unataka kupumzika, au?’ akaniuliza huku akigeuka kuniangalia.

‘Sawa ...tukikutana tena nataka uwe umejiandaa, ...kusema ukweli, wa kwako, na sio wa shinikizo, nataka ule mkataba wa awali uwepo, ili tulinganisha na huo mkataba wenu mpya,  vinginevyo hatutaelewana...’nikasema.

‘Hamna shida mke wangu, ...mimi nipo, tutaongea tu, na tutayamaliza bila wasiwasi, mimi ni mume wako, na nina haki zote kisheria, na nafanya hayo kama tulivyoainisha kwenye mkataba wetu..’akasema kwa kujiamini.

Na mara mlango ukafunguliwa,kwa nje, niliona watu wawili, na mmoja, anafanana sana na marehemu nahisi ndio mtoto wake, alikuwa akitaka kuingia ndani, na mume wangu akawa anamzuia,nikasikia wakisema;

‘Huyu ndiye yule wakili wangu niliyekuambia, atachukua nafasi ya baba...

‘Tutaongea huko mbele,...’akasema mume wangu mlango ukafungwa, na mimi nikampigia simu wakili wangu, nikijua sasa ni mapambano, hakuna kulala.

‘Sikiliza hayo ndiyo mazungumzo yangu na mume wangu...’nikasema nikiiweka simu hewani

NB: Doa la tamaa limeshagusa mtima, ibilisi hachezi mbali hapo,...je itakuwaje, Kwa leo inatosha.


WAZO LA LEO: Maisha ya kiujanja ujanja, dhuluma ,kugushi, hayana amani,...kwa vyovyote utakavyofanya ili kufanikisha dhuluma, ili kupata kipato kisicho halali, ili kuhalalisha uwongo wako, ujue hilo ni deni kwako, na aina hiyo ya maisha,inaondoa baraka, inaondoa amani, na upendo. Hata kama utafanikiiwa na kupata hiyo dhuluma na hata kuwa tajiri, lakini utajiri wako utakuwa hauna heri, hauna amani hauna baraka, na mwisho wake ni dhiki, kujuta na kuzalilika. Wangapi wangapi walifanya hivyo, na sasa  hawapo dunia tena, tukumbuke dunia hii ni mapito tu, chuma chumo la halali, ili maisha ayko yawe na amani, baraka na furaha..

Ni mimi: emu-three

No comments :