Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, November 9, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-24


‘Nahisi rafiki yangu atakuwa mikononi mwa huyo wakili, kwani aliniambia mtoto wake, alitekwa nyara na watu wasiojulikana, na baadaye akapigiwa simu, kuwa ili ampate mtoto wake inabidi kusaini mkataba walioandaa hawo watu...

‘Kwasababu ya mtoto wangu sikuwa na hiari, nilikubali kusaini huo mkataba..’ hata mimi kama mzazi ningefanya hivyo, nikajisemea kimoyo moyo.

Ina maana huyo rafiki yangu, akasaini huo mkataba, na huyo rafiki yangu alikuja kugundua kuwa mkataba huo hakuwa na madhara sana kwake, zaidi ni dhuluma kwa watu wengine, ...lakini hakuwa hiari, akakubali, akasaini, na alitarajia kumpata mtoto wake...hakusema kuwa alimpata au la,na nafikiri hawo watu wamemzunguka, au...’ndivyo nilivyomwambia rafiki wa mume wangu, na huku nikiwaza mengine,

Kama kwaida ya rafiki wa mume, wangu, kupinga kila kitu, akawa ananiuliza maswali mengi,ambayo sikuwa na majibu nayo....kwani wakiti huo akili yangu ilishakuwa na mawazo mengine.

Wakati huo akili yangu ilishaona kuwa rafiki yangu huko alipo yupo matatani,hasa baada ya huyu rafiki wa mume wangu kuniambia kuwa Makabrsha ana ofisi huko uwanja wa ndege, na pia rafiki yangu aliniambia kuwa yupo huko uwanja wa ndege, na wakati anataka kunielezea zaidi simu yake ilikatika, mkatiko ambao uliashiria kuwa huko hakuna mema.

Kwangu mimi moyoni, nilihisi hawo watu waliomteka mtoto wake, wamemgeuka, na lolote linaweza kutokea, na mimi kama rafiki yake, ilibidi niende nikamsaidie, hata kama kuna hizo tetesi ambazo zinanichanganya, na mpaka sasa akili yangu ilikuwa hajaamini...

‘Ni lazima nifanye lolote, japokuwa nilikuwa nimechelewa....

Endelea na kisa chetu.....

********

Usiku una mitihani yake, japokuwa nilikuwa na nia ya kumsaidia rafiki yangu, lakini moyoni, nilikuwa na mashaka ya usalama wangu, sio mtu wa kuogopa ovyo, lakini wakati mwingine unahitajika kuwa na tahadhari, kwani huwezi kujua wenzetu wamejiandaa vipi, ....kwa ubishi wangu sikuweza kumsikiliza rafiki wa mume wangu pale aliponisihi nisije nikaenda huko uwanja wa ndege, kwani aliona dalili hizo kuwa nataka kuelekea huko, japokuwa sikutaka kumwambia naenda wapi, na hata aliposisitiza kuwa tuondoke pamoja, mimi nilimkatalia,...

‘Nakufahamu sana unataka kwenda huko uwanja wa ndege, ...usije ukafanya hayo makosa, mimi kama mtu ninayekujali, nakukataza kabisa usiende huko....’akasema.

‘Usinifanye mimi kama mtoto mdogo. Ninafahamu ni kitu gani natakiwa kukifanya, na wewe huwezi kunizuia,...’nikasema na sikumsubiria , nikamuacha akiwa kaduwa, na nahisi nilimuona akipiga simu, lakini sikuwa na muda wa kumwangalia,...

Kawaida yangu na huyu mtu, tunakutana,huwa hatukubaliani kirahisi, yeye ananifahamu hivyo, na mimi namfahamu sana tabia yake, mimi na yeye ni kama mafahali wawili, ...na sikupenda aniona mimi sijui ni nini ninchokifanya hata hivyo, nilishamfahamu kuwa mengine anayafanya ili nimuone kuwa ananijali, au anafanya kuwarizisha wazazi wangu..sikupenda kufanyiwa hivyo.

Kwa jinsi nilivyoona mimi, nina wajibu wa kwenda huko, kUfanya lolote, maana rafiki yangu alikuwa kwenye mikono yangu, na isitoshe, yeye bado ni mfanyakazi wangu, sasa kanipigia na simu na nimehisi kuwa yupo kwenye hatari, ...kwanini nisifuatilie,...sawa ilibidi niwaambie polisi, lakini hawo polisi nitawaambia nini, ....sijagundua kuwa kweli yupo kwenye hatari, niwaambia nikifika huko, kama itakuwa ni lazima.

Japokuwa nilikuwa nimejipa moyo, kuwa hakuna litakaloweza kunitatiza, lakini nilitakiwa kuwa makini, maana naenda kukutana na watu wanao-onekana kuwa ni hatari. Mimi sijaona uhatari wao, lakini kutokana na kauli ya huyo rafiki wa mume wangu, inaonekana hivyo,..na huenda watu hao hawajali sheria kwa vile wapo na mtu ambaye, anajidanganya kuwa anaweza kucheza na vipengele vya sheria na kufanya apendavyo.....hilo mimi siamimi..

Wasiwasi wangu ni kuwa huenda watu hawo wana silaha, na mimi sina silaha,na nikifika huko wanaweza kufanya lolotelile,.... aheri na mimi ningelikuwa nimechukua ile bastola yangu, ili wakinitishia na silaha na mimi nawaonyesha kuwa nina silaha na ninaweza kuitumia,....kwahiyo sasa nifanye nini?’ nikajiuliza.
Niliona kuwa kama nitakwenda nyumbani kuifuata hiyo silaha yangu, nitakuchelewa zaidi.

‘Hamna shida ngoja niende huko huko, sio lazima upambena kwa silaha, hata hivyo sizani kama kutakuwa na haja ya kutumia silaha, ikibidi, nitatafuta njia nyingine...pale kuna kituo cha polisi karibu nitawaarifu kama kuna hatari....’nikasema, huku nikijaribu kupiga simu ya huyo rafiki yangu mara kwa mara kama atapatikana, lakini hakupatikana.

Tatizo la Darisalama, ni foleni, maana hadi kufika TAZARA ilinichukua muda mrefu ambao sikutegemea, utafikiri unatembea kwa miguu, ilifikia muda nikaona kama ninapoteza muda wangu bure, kwenda huko uwanja wa ndege, wakati sitaweza kufika kwa wakati muafaka, nilitaka nigeuze gari nirudi nilikotoka, lakini kila nilipotaka kufanya hivyo, nafsi ikawa inanisuta,nikazidi kusonga mbele, huku nikijipa matumaini kwa kusema kimoyo moyo

‘Huyo ni rafiki yangu, ni lazima nimsaidie, kama anavyonisaidia mimi, kama nisipomjali sasa hivi, nitaonekana nilikuwa namtumia tu kwa masilahi yangu..hata hivyo huyo ni zaidi ya rafiki yangu...japokuwa , watu wanamvumishia vibaya, ‘nikasema na akilini nikawa nasikia ile sauti wakati naongea na yeye kwenye simu:

‘Mtoto wangu alichukuliwa kama dhamana,....waliponiita, kwa ajili ya kuweka sahihi ya huo mkataba, sikufahamu kama itakuwa hivyo, na nilifahamu kuwa lengo lao ni jema tu, siku nilipofika nikiwa nyumbani kwangu, wakati nipo bafuni naoga, walifika watu nisiowafahamu, wakamchukua mtoto wangu..nilichanganyikiwa, maana kwa muda huo sikuwa na mfanyakazi wa ndani, ...mtoto nilimuacha kalala chumbani,lakini baadaye wakanipigia simu, kuwa kama namtaka mtoto wangu, akiwa hai basi nifanye wanavyotaka wao, nikawaulize nifanye nini...

Hawa watu wana nia mbaya, wanadiriki kumchkua mtoto mdogo kwa ajili ya pesa, ...mimi ni lazima niwashitaki...na hii inaonyesha kuwa kweli rafiki yangu yupo na kundi baya, kwanini asiseme toka awali, au kuifahamisha polisi...mmh, ndio mambo ya kuzarau vyombo vya dola...lakini hakijaharibika kitu. Ni lazima nifike huko tusaidiane naye,, ..japokuwa nahisi nimechelewa sana....’nikasema.

Nilifika eneo la TAZARA, na nilipoangalia saa, nikaona ni muda ambao kama ni msafiri wa ndege hiyo ya saa tatu, kwa muda huo alitakiwa awepo uwanja wa ndege, na kwahiyo kama rafiki yangu huyo anasafiri leo, basi kwa muda huu alitakiwa kuwa ndani ya uwanja wa ndege, na kama kashikiliwa na hawo watu anaweza kukosa safari yake hiyo,..

‘Ni lazima nifike nimuokoe ili aweze kusafiri, ....na akirudi tutaweza kufanay makubwa, ...kama kweli hajanisaliti,kama anavyodai rafiki yangu, sizani kama anaweza kufanya kitu kama hicho....’nikazidi kuingiwa na mori, huku nikizidi kukanyaga mafuta, lakini mbele kidogo, foleni,.’

‘HIzi foleni jamani hazijui kuwa nina haraka sana....’nikalalamika.

Tuliporuhusiwa hapo Tazara, kukawa hakuna foleni kunzia kuelekea uwanja wa ndege, nikaweza kuendesha gari langu kwa mwendo ninaoutaka, hadi nikafika maeneo ya uwanja wa ndege, hapo nikapunguza mwendo, na kujiuliza nifike kiwanjani moja kwa moja,  nione kama huyo rafiki yangu keshafika au nifike kwanza kwenye hilo jengo, ambalo ndilo nasikia ni ofisi wa huyu wakili wa mume wangu.

Kwa mtizamo wangu, nilihisi kuwa rafiki yangu atakuwa kashikiliwa kwenye hilo jengo, na kama nikimkosa hapo basi atakuwa sehemu nyingine, ambayo sikuwa na uwezo wa kuitambua kwa muda huo, na hata kama nitamkosa lakini juhudu zangu, ni dhamira ya kweli,....nikimkosa kabisa itabidi nimpigia huyo rafiki wa mume wangu anaweza kufahamu wapi alipofika kwa ajili ya kuwahi uwanja wa ndege..

‘Lakini nahisi huyu mtu, anayejiita wakili, ambaye sasa kaingilia anga zangu anaweza ndiye kamshikilia rafiki yangu....ni lazima ...hisia zangu zinanituma hivyo, ngoja nikapambane naye, mimi simuogopi kabisa.....’nikasema huku hisia zangu zikinituma hivyo, na hapo hapo, nikageuka huku na kule kulitafuta hilo jengo..

Nikakumbuka maelezo niliyoelekezwa kuwa jengo hilo lipo, ilikwua sio sehemu ya kupotea maana jengo hilo lilikuwa likionekana wazi wazi, unapofika maeneo hayo ya uwanja wa ndege. Baada ya kuliona hilo jengo, akili yangu ikanituma nifike kwanza kwenye jengo hilo.,.....

Nikaendesha hadi kwenye hilo jengo, na kama nilivyoambiwa sehemu kubwa ya chini imechukuliwa na waendesha biashara za vinywaji, kwahiyo kwa wakati huo watu walikuwa wamekaa kwenye viti vilivyopangwa kwenye miti iliyopandwa kwenye bustani ya eno hilo, wakinywa, na mziki ulikuwa ukipigwa....

Mimi nilipoingia eneo hilo na gari langu, wakaja wapokezi, wakinikaribisha kwa bashasha, huku wakinielekeza sehemu ya kuegesha gari langu, nami nikafanya hivyo, na kutoka nje ya gari, na wale wahudmu, wakaendelea kuonyesha ukarimu wao, inaonekana walisomea hiyo kazi, kwani walijua jinsi gani ya kumkaribisha mgeni, mpaka unavutiwa ..

‘Unakaribishwa mgeni, hapa kuna huduma mbalimbali, kuna vinywaji, kuna chakula, au kama unahitaji kumpumzika kuna sehemu ya kupumzika, vipo vyumba, na huduma nyingine ...’nikashangaa, maana sikujua kuwa jengo hilo lina mambo yote hayo, nab ado halikamilika, kweli watu wapo mbele kwa biashara, maana huduma hizo ni kama vile upo kwenye hoteli.

‘Kwani hapa kuna vyumba vya kulala wageni?’ nikauliza

‘Ndio vipo vingi tu, vina kila kitu, unahitaji chumba, kwa muda gani je upo peke yako?’ wakaniuliza.

‘Hapana sihitaji chumba, mimi nataka kumuona Makabrasha...’nikasema

‘Oh, unamuhitaji bosi,....mhh, nafikiri bado yupo ofisini kwake, na muda kama huu alitakiwa kuwa huku chini, anapenda sana kujichanganya, ....nafikiri bado yupo ofisini kwake, tangu jioni yupo huko huko, leo sijamuona akishuka huku chini, sio kawaida yake, nahisi ana kazi nyingi....kamuone mlinzi pale,utajiandikisha halafu atakuelekeza ofisini kwake, karibu sana...’akasema huyo mpokeaji wageni.

‘Nashukuru hamna shida, na gari langu....?’nikauliza

‘Kama unahitaji ulinzi, inabidi ulipie pale, kwa yule mlinzi, lakini kama unajiamini, basi liache hapo hapo, wengi wameacha magari yao hapo, ila kama unahitajia ulnzi wa ziada, zipo huduma hizo, wapo walinzi kwa kazi hizo,..hapa usalama ni mkubwa sana...usiwe na wasiwasi mama’akasema huyo mtu wa mapokezi

Mimi nikaona bora nipate hiyo huduma ya ulinzi wa ziada, nikaenda kwa yule mlinzi, nikaandikisha, na kulipia, halafu nikafika sehemu ya mlinzi wa kwenda juu, alikuwa kakaa na mbele yake kuna meza, na kitabu kikubwa, alikuwa anasinzia, na aliponiona akasimama na kunikaribisha, nikamuelezea shida yangu.

‘Oh, kwa muda kama huu, hataki wageni, ....lakini mmh, ngoja, ...’akachukua simu yake na kupiga, ikawa inaita tu, akaniangalia, na kusema;

‘Unaona hataki hata kupokea simu, tafadhali naona nikukague,...uende tu ukamuone...’akasema nana hapo nikawa huru, hata kama nitachukua muda mrefu huko ninapokwenda, lakini gari langu kipo kwenye usalama. 

Nikaelekea kwenye ngazi za kupanda, juu, ..

Nilipoanza kupanda ngazi ya kwanza simu yangu ikaita, nikaangalia ni nani mpigaji, nikaona ni rafiki wa mume wangu, sikutaka kupokea simu yake kwa muda huo, nikaikata, na kuanza safari ya kwenda juu, huku nikiwa na mawaza mengi.

‘Hivi haya aliyoniambia huyu rafiki wa mume wangu yanaweza kuwa ni kweli, kuwa huenda mume wangu ndiye baba wa mtoto wa rafiki yangu...haiwezekani, kwa jinsi ninavyomfahamu mume wangu, ambaye siku tunaandikisha ule mkataba, aliapa na kuapa kuwa hatanisaliti, ...inawezakana kweli mtu akaabdilika na kukana kiapo chake,....sio mume wangu, kwa jinsi ninavyomfahamu, sijui, .....haiwezekani.

‘Lakini kama ni kweli,....sijui kama nitaweza kumsamehe mume wangu, siwezi, kwanini anifanyie hivyo...siwezi, ni lazima mkataba ufanye kazi, yake, ...japokuwa nampenda, na ...’nikatulia pale nilipoona mtu akitokea juu, akishuka kwa kasi, alikuwa akikimbia. Alikuwa kavaa mawani muesi, na kofia kubwa, kiasi kwamba huwezi kuona sura yake, mpaka, ainue kichwa kidogo.

Yule mtu aliponiona, kwanza alinitupia jicho, na nafiki ananitambua maana aliponiangalia, kwa haraka, na ghafla, akasita, kama anataka kuongea na mimi, lakini akawa kama kashituka, akanipita kwa haraka na kukimbilia chini, mimi sikumjali nikaendelea na safari yangu ya kwenda juu.

‘Ina maana mume wangu alitenda hivyo, akiwa na maana gani, kama kweli kaamua kunisaliti, au ni kwasaabbu ya pombe, inawezekana wakati amelewa,alifikia kufanya hivyo bila kujitambua na alipobaini kosa lake ndio akazidi kuchanganyikiwa...aaah, hiyo sio sababu, siwezi kuvumilia huo utetezi, lazima mkataba ufanye kazi yake..

‘Lakini tatizo mkataba ndio huo umefanyiwa ufujaji,...ina maana hakuna kitakachoweza kumuwajibisha mume wangu, ...hata kama ni hivyo, lakini yale tuliyokubaliana sote wawili tunayafahamu sote wawili, mimi nitachukua uamuzi wangu kutokana na tulivyokubaliana, sasa kama yeye ataona nimemuonea,atakwenda mahakamani, huko ndio tutapambana..

Nilikumbuka hilo la mkataba, nikawa na hamu sana ya kuusoma vyema, huenda kuna vipengele wameongeza vya kumuwezesha kunibana kisheria,...ndio, kumbe ndio maana pale kwenye ule mkataba waliandika kuwa 
`....mume ndiye atakuwa na mamlaka ya mali yote, na maamuzi yote.....’ thubutu, mali yangu mwenyewe, mtu aje aniamulie..hilo halikubaliki, tutapambana hadi tone la mwisho, na ikibidi, nitachukua hatua ambayo watu hawataniamini....

‘Kama rafiki yangu...’nikasita, na kujilaumu, kwanini nimefika hapo, maana kama rafiki yangu ndio huyo kanisaliti na kuzini na mume wangu,....basia takuwa ni adui yangu mkubwa...ina maana kweli rafiki yako mwenyewe anaweza kukufanyia mambo hivi, siamini, hapana hizo ni hisia za huyu rafiki wa mume wangu ambaye kila mara anatafuta njia ya kunigombanisha naye...

‘Lakini....’hapo nikatulia kidogo..

‘Ina maana kweli, hivi kwanini akili yangu ilikuwa imefungwa kiasi hicho, mtoto wake, anafanana na watoto wangu, ina maana ...oh, inawezekana, ...inawezekana, hapana, haiwezekani,...kwanini wasiseme katembea na mdogo wa mume wangu, hilo pia linawezekana...mmh, nitayajua huko huko.

‘Kama ni kweli ...kama ni kweli rafiki yangu aliamua kunisaliti, basi hilo neno rafiki litafutika mara moja, na badala yake, neno adui litasimama badala yake..sitamsamehe, kwanza, nimekumbuka....’nikasema na kuitoa simu yangu.

Nilitafuta namba ..nikaanza kuipiga huku natembea mwendo wa kawaida, na huyo mtu alipoipokea nikasema;

‘Mimi ni yule dada niliyekuambia unitafutie wale mabaunsa wa ile kazi, ...nitakuarifu pindi, ..ndio, kuna dada mmoja, kama nikithibitisha kafanya hivyo, nataka tumfunze adabu, ...kabisa kabisa, waweke tayari tayari.....’nikakata simu.

Mara nikasikia king’ora cha polisi kikisikika kwa mbali sana, na hali kama hiyo ikanipa wasiwasi, nikasimama kidogo kusikilizia, kama king’ora hicho kilikuwa kikitokea mjini, au njia ya kutokea Gongolamboto, sikuweza kukisia vyema, maana kulikuwa na sauti kubwa ya mziki. Nikajipa moyo kuwa huenda hawo wana safari zao,...

Nikawa nimeshafika eneo la rosheni ya pili, nikatulia kidogo kuangalia upande gani ofisi hiyo ipo,na nilipotupa macho kushoto, nikaona kwenye mlango, maandishi, `WAKILI WA KUJITEGEMEA, MH. MAKABRASHA..

‘Mh. Mkabrasha...’nikasema kwa sauti ndogo, huku nikitabasamu.

Nikatulia kidogo, maana sasa huenda naingia kwenye matatizo, na nisipokuwa muangalifu ninaweza kuhatarisha maisha yangu, japokuwa watu wengi walioniona na watakuwa mashahidi wangu, kama likitokea lolote, lakini kama nimeuwawa, itasaidia nini,.....hata hivyo siwezi kujiaminisha sana, kuwa kuna watu wameniona nikipanda juu, kwani watu wote hawo wanaweza kuwa watu wake...wakamtetea yeye.

Kwanza nikavaa soksi za mikononi, maana ukiwa unakwenda sehemu zenye mashaka, ni vyema ujenga tabia ya kujihami, na mimi tabia hiyo nimekuwa nayo mara nyingi, hasa unapokwenda sehemuunazohisi ni hatari ni vyema pia ukajihami na alama za mikononi, lolote linaweza kutokea, ..nikazitoa kwenye mkoba wangu, na kuzivaa kwa haraka haraka, huku moyo wangu ukinienda mbio. Mara nayingi nakuwa na hizi soksi kwenye mkoba wangu.

Nikaufikia huo  mlango, ulioandikwa jina la huyo muheshimiwa, nikajaribu kusikiliza kama kuna sauti yoyote inatokea ndani, lakini kulikuwa kimiya, kimiya kabisa,unachoweza kusikilia kwa mbali ni hizo sauti za ving’ora na mziki toka chini,....nikaona nispoteze muda, nikaugonga huo mlango mara tatu...kimiya, mara nyingine tatu kimiya

Mwili ukaanza kujenga hisia nyingine, nywele zikaanza kunisisimuka,....nikakumbuka wale watu chini, waliniambia kuwa huyo muheshimiwa yupo juu, kwenye ofisi yake, kwanini nagonga mlango wake mara nyingi, bila ya yeye kutokea au hata mtu wmingine kuja kunifungulia mlango, nikagonga tena na tena kimiya..

Nikaona isiwe taabu nikashika kitasa cha mlango nikakizungusha taratibu, nikaona mlango unafunguka...nikausukuma polepole, ukafunguka kiasi cha mimi kupita, nikaona hapana, nikausukuma, ukafunguka kwa mapana, kiasi cha kuona ndani, nikaona kwe mbele sehemu ya mapokezi, ..kumbe ni ofisi kubwa tu, nikaangalia nje kama kuna mtu anakuja ...hakuna, nikaingia ndani.

Na wakati huo vile ving’ora vya polisi, vilikuwa vimeshafika eneo karibu na hilo jengo ni kama vile wanakuja eneo hili, nikaona afadhali, kama rafiki yangu yupo matatani, nitapata wasaidizi, nikapata nguvu, nikaingia ndani, na kuangalia huku na kule nikaona mlango mmoja umeandikwa:
OFISI YA WAKILI..., nikaangalia saa yangu ilikuwa saa mbili, nikausogelea ule mlango, nikagonga,...kimya nikagonga tena, kimiya....mara simu yangu ikaita, nikaizima bila kuangalia mpigaji, nikashika kitasa na kufungua mlango, mlango ukafunguka....

Kwanza nilisimama huku nikiangaza macho kukagua hicho chumba na kama kuna usalama,, ilikuwa ni ofisi nzuri tu, ikiwa na kila kitu kincahoweza kupatikana kwenye ofisi za mawakili,na macho yangu yakaenda moja kwa moja kwenye meza, niliona mtu kakaa huku kalala kwenye meza, yaani kichwa kakiweka mezani, , lakini ulalaji ule sio wa kawaida, ni kama mtu kalazimishwa, na macho yangu yakatua pembeni yake, nikaona mikataba, na mmoja kati ya hizo ni ule mikataba wangu ... nahisi ni hiyo waliyotengeneza wao, lakini jamaa anaonekana hajitabui, kalewa sana, au ni usingizi gani huo..

Hasira zikanipanda, nilitaka nifike kwa huyu mtu nimuinue nimsuke suke, nikifahamu kuwa kalewa, hatakuwa na ubavu wa kupambana na mimi,...na hapo inaonekana kanywa hadi kapitiliza maana pembeni kwake kulikuwa na chupa kubwa ya kinywaji cha pombe kali, na gilasi mbili,....kuonyesha kuwa hakuwa peke yake, nikaachia mlango, na kusogea kuingia ndani, huku king’ora cha polisi kikisikika kwa nguvu, kuashiria kuwa sasa askari wapo chini ya hili jengo.

Hata hivyo, akilini mwangu nilikuwa na mashaka, nikijiuliza hawo maaskari wamefuata nini hapo...kusije kuwa kuna matatizo.....nikaona nimalizane na kilichonileta, kwanza nimuamushe huyu mtu nimuulize rafiki yangu yupo wapi, na kwanini, kaingilia maswala ya familia yangu kwa kuharibu mkataba wangu na mume wangu,...nilipofikia hapo kimawazo sikujali mambo ya polisi, nikasogea upande ule aliokaa huyo jamaa ili kukabiliana naye....

Ni wakati huo huo, nasogea na mara macho yangu yakatua pale alipolala huyo jamaa, nikaona kitu kilichonishitua, nikaganda, nikarudi nyuma hatua mbili, nikashika mdomo,...kujizuia,..lakini haikuwezekana, nikajikuta nimepiga yowe, unafahamu yowe, sijawahi kupiga yowe kama hilo....na mara nikasikia mlango ukifunguliwa nyuma yangu.....

Tuendelee kidogo, mmh, kidole kinauma......wikiendi njema

NB: Kwa leo,..hapa hapa


WAO LA LEO:Kila kazi ina ujuzi wake na taratibu zake, ndio maana watu wanakwenda kuzisomea hizo kazi, tusijifanye kuwa tunafahamu kila kitu, eti kwa vile ulipitia pitia shuleni, kuna vitabu umesomasoma , hiyo peke yake haitoshi ...ndio maana kuna taaluma tofautitofauti, na kila taaluma, ina mabingwa, ina wataalamu wake, ina watu wanapewa madaraja na nyazifa mbalimbali, kuonyesha kuwa hizo ni fani zinazojitegemea, tusipende kujiingiza kwenye kazi za watu ambazo huenda ni za kitaalamu zaidi, na kujifanya tunaufahamu nazo, ilihali hatujazisomea, tujue kuwa  kuongea na kutenda ni vitu viwili tofauti,..tuweni makini na fani za watu.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Pam said...

Shukrani m3..

emu-three said...

Pam shukurani na ww pia kwa kuwa pamoja nami na wengine wote. TUPO PAMOJA