Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, October 29, 2013

Mkuki ni kwa Nguruwe-18


Nilipomaliza kuongea na mdogo wa mume wangu, akili yangu ilikuwa kama imepandikizwa hasira fulani, nilitaka niongee , nifoke, kama vile nipo ofisini na wafanyakazi wangu, lakini haikuwa rahisi , kwani nilikuwa kwenye kifungo maalumu,..kifungo cha kuwajibika kwa mume. 

Kutokana na hiyo hali, ya hasira, iliyotokana nay ale maelezo ya mdogo wa mume wangu, sikuwa na akili ya kuangalai kushoto au kulia, kwani kama ningeliangalia sehemu zote hizo, huenda ningelimuona mume wangu akiwa na yule msaidizi wangu,...Mimi nilipotoka pale bustanini, niliharakisha kuingia ndani, na kujipweteka kwenye sofa.

Wakati nipo kwenye sofa, nikijaribu kupotezea, japokuwa haikuwezekana, maana yale maeno ya shemeji yangu yalikuwa yakijirudia rudia kichwani, hadi ikafikia hatua ya kujiuliza ni wapi nilipokosea, ina maana wema wangu wote niliofanya kwa wenzangu kwa nia njema, haukuwa na maana, kilichokuwa na maana ni hayo wanayoyataka wao....

Ni wakati huo nikiwa kwenye lindi la mawazo, ndipo, nikasikia sauti nje, ilikuwa sauti ya watu waliokuwa wakiongea, na walikuwa wanakaribia mlangoni. Wazo la kwanza lilikuwa kwenda kuhakikisha kama mue wangu amelala, au ameshaamuka, ....lakini kitu kikaniambia nichungulie kwanza nje, na nilipochungulia nje kwa kupitia kwenye dirisha ndipo nikagundua kuwa kumbe mume wangu alikuwa nje, kumbe alikuwa ameshaamuka, na alikuwa na msaidizi wangu,na kama ilivyo kawaida yake, alipoamuka alitaka kwenda nje, azungshwe zungushwe na kigari chake huku na kule.

Nilipoona hivyo, wazo likanijia kuwa huenda walitoka muda mrefu, na wakafika hadi kule bustanini, wakatuona tukiongea na shemeji yangu, ...na hapo nikakumbuka kuwa kuna kipindi nilipokuwa nikiongea na shemeji yangu, nilimuona shemeji yangu huyo akiangalia nyuma yangu, kwa macho yaliyokuwa yakiashiria kuna kitu alikuwa akiangalia kwa nyuma yangu, lakini mimi nilizarau na kuzania ni ile tabia ya shemeji yangu ya kunionea aibu..huenda muda huo, ndio aliwaona mume wangu na mfanyakazi wangu wakitembea.

‘Kwanini shemeji yangu hakunishitua...?’ nikajiuliza.

‘Au hakuwaona, au aliwaona wakiwa wameshasikia kile tulichokuwa tukiongea...?’ nikaona nisiumize kichwa, nikafungua mlango na hapo nikakutana na mume wangu, akiwa kabadilika usoni, kwanza akaonyesha uso wa huzuni, akihuzunika kuhusu mdogo wake, na pili akakunja uso, akijua kuwa huenda tulikuwa tukisigishana na mdogo wake hasa pale aliponiuliza;

‘Mdogo wangu kakukosea nini..’

Tuendelee na kisa chetu.

Kauli hiyo ilinifanya nishikwe na butwaa,na kuduwaa kidogo, na mume wangu akauliza tena.

‘Mdogo wangu kakukosea nini..’

Aliporudia hilo swali, kwa sauti ya hasira mimi nikamuashiria yule msaidizi wangu aondoke, nikasoegea mbele ya kile kigari-kiti na kuchuchumaa mbele ya mume wangu, nikaweka mikono yangu kwenye mapaja ya mume wangu na kusema.

 ‘Oh mume wangu sikujua kuwa umeamuka, kwanini hukumwambia msaidizi wangu aniite nije nikutoe mwenyewe nje, unafahamu nipo likizo kwa ajili yako...’nikasema.

‘Nimekuuliza swali na unakwepa kunijibu, hufahamu jinsi gani nilivyojisikia nilivyoona mdogo wangu kapiga magoti mbele yako...’akasema na hapo nikshituka na haraka haraka akili yangu ikajiweka sawa na kumwambia

‘Oh,kumbe mume wangu ulituona, nilikuwa nataniana na shemeji yangu, nilikuwa namtishia kwa kumtania kuwa kuja kwake hapa nyumbani nikiwa kazini, kuna ajenda ya siri, ...’nikasema

‘Ajenda gani ya siri...?’ akaniuliza akiwa ananiangalia kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Nilimtania kuwa huenda alikuwa akija kumsumbua mfanyakazi wetu wa ndani...na kwambia kama ni hivyo nitakuambia halafu itakuwa mwisho wake...nilimwambia kwa utani tu,..ndio akanipigia mgoti kusema hajafanya, na nisije kukuambia lolote, maana anaogopa usije ukaumiza moyo wako kwa kitu ambacho hajakifanya....’nikasema na hapo nikaona uso wa mume wangu ukibadilika, kutoka kwenye hasira, hadi kwenye kutabasamu;

‘Na wewe bwana, mimi nilishapaniki, maana nimjuavyo bwana mdogo, sio mwepesi kiasi hicho, cha kumpigia mtu magoti na kumuomba msamaha, nikajua kuna jambo kubwa sana, ambalo mdogo wangu aliona bila kufanya hivyo hatasamehewa....ni hivyo tu mke wangu au unanivunga?’akaniuliza.

‘Ndio hivyo tu mume wangu, kwani huniamini...?’ nikamuuliza na kabla hajajibu nikasema;

‘Au wewe ulikuwa unahisi ni jambo gani, ambalo ningelimfanyia shemeji yangu hadi anipigie magoti?’ nikamuuliza na kabla hajasema neno nikaendelea kuongea;

‘Mume wangu, ukumbuke yeye namuona kama mdogo wangu, kama ulivyooona tumekuwa tukijitahidi kwa pamoja kumjenga katika njia njema,ya kumbadili kutoka kwenye tabia ya utegemezi kwenda kwenye tabia ya kuweza kuishi mwenyewe, na hilo tumefanikiwa...’nikasema.

‘Ni kweli mke wangu, na inabidi nikushukuru sana kwa wema wako huo, kama ingelikuwa ni mimi mwenyewe ningelishakata tamaa, maana bwana mdogo alikuwa keshadekezwa na mama,maana yeye ni kipenzi cha mama, na wao walifikiria kwa kmfanyia hivyo ndio wanampenda,wakawa wanamdekeza, kumbe wanamharibu tusingelimwahi mapema, angeshajiunga na hayo makundi ya kuuza madawa ya kulevya....’akasema.

‘Ni kweli mume wangu, hilo ni kosa wanalofanya wazazi wengi, ambao kwa kuwadekeza watoto wao ndio wanafikiria kuwa ndio mapenzi kwa mtoto, kumbe ni kinyume chake, wanawaharibia maisha watoto wao bila kujitambua, huko sio kupenda, ....hakikisha mtoto unamlea katika hali ambayo ukiondoka leo ataweza kusimama peke yake, unahakikisha anawajibika ipasavyo, kuanzia asubuhi mpaka jioni, na wao wanafnaya kazi...fanya hivyo hata kama mtoto ataona humpendi, lakini baadaye atakukumbuka...’nikasema.

‘Ndio maana naona hawa mabinti unavyowafanyiza kazi , utafikiria wazazi wao hawana uwezo, ina maana gani sasa kuweka wafanyakazi wa ndani, kama kila kazi unataka na wao wafanye, mimi wakati mwingine naona kama umezidi kuwatumikisha watoto wetu, huoni kama unawatesa?’ akaniuliza.

‘Hivyo ndivyo watoto wanatakiwa kuwa,hata kama kuna wafanyakazi, wafanyakazi pia na wao ni sehemu ya familia, sio watumwa, wanasaidiana, na niliwaambia wawe wanawaelekeza watoto wetu kazi, ili na wao wafanye, hii itawasaidia kuwajenga kiakili, wanajua kuwa na wao wanawajibika, ili kesho na kesho kuwa, kama hatupo....wanaweza kufanya kila kitu wenyewe. Kumbuke haya yote ni ya kupita,leo tumatajiri kesho tunaweza kuamuka masikini, kwa maisha haya tuliowajengea watoto wetu, wanaweza kuishi bila shida....na ndivyo nilivyojitahidi kumfanyia shemeji yangu, alivyokuja hapa, kama tungemlegezea, angejiunga na wavuta unga....nilishamuona ndio maana nikawa mkali sana kwake....’nikasema.

‘Ni kweli ulijitahidi sana, mpaka akawa anakuogopa, na hata kufikiria unamtesa, kumbe ulikuwa na malengo maalumu, nakuaminia sana mke wangu, kwani kweli kama usingelifanya hivyo, alikuwa kwenye muelekeo wa kuingia kwenye makundi mabaya..hasa ya madawa ya kulevya, ndipo alipokuwa akielekea,....’akasema.

‘Na bora hakuwa ameanza kuyatumia hayo madawa huko alipotoka, kwani kama angelianza, ingelikuwa ni vigumu sana kumdhibiti, ....elimu aliyoipata japo likuwa bado, haiwezi kumsiamia kimaisha, lakini ilimsaidia kumfanya aweze kupambanua mema na mabaya, na ndio maana ya elimu, japokuwa ilikuwa haitoshi kwa maisha ya sasa, ... na tulimuwahi mapema kabla hajapotoka, na ikasaidia kwani alituliza kichwa, na kujipanga upya, akatulia, na kufuatilia yale yote tuliyomuelekeza, na tumefanikia, ni jambo la kmshukuru sana mungu,..hivyo ndivyo wazazi tunatakiwa tuwe, tusaidie, hata kama sio mtoto wako, ilimradi uanishi naye, mfanye kama vile unavyowafanyia watoto wako,utaona matunda yake baadaye....’nikasema.

‘Nikisikia hivyo mke wangu najihisi kama nimepona, maana, nina jembe pembeni, najisikia raha sana, nashukuru sana mke wangu sijiu hata  nikupe nini..mungu mwenyewe ndiye anajua, ndio maana najuta sana kwa hayo yaliyotokea...na kama usingelinisamehe, nilitamani nife tu...’akasema na mimi hapo nilitakiwa kuiondoa hiyo hali kwa haraka nikamwambia;

‘Mume wangu usijali,..nimeshakusamehe, cha muhimu ni wewe kupona, hlo ndilo unatakiwa uliwazie jinsi gani unatakiwa kufanya mazoezi na kuondoa mawazo....’nikamwambia

‘Nikipona mke wangu, nitakuwa na wewe bega kwa bega, sitatetereka tena, na nimegundua kosa langu ni nini, ma kumbe ulikuwa na malengi mazuri tu, ...hata hivyo, wakati mwingine kama binadamu, tunajisahau, na kutokujua undani wa mwenzako, na hili nimegundua kuwa ni tatizo, ...nitajitahidi sana tuwe pamoja tuiondoe hiyo hali, au unasemaje mke wangu..?’akasema kama ananiuliza. Sikutakiwa nimweke katika hiyo hali ya kusononeka, kwahiyo nikajitahidi kureejsha yale mazungumzo ya mdogo wake.

‘Usijali mume wangu, cha muhimu kwa sasa, ni kuhakikisha yale tuliyo anza nayo yanafankiwa, na hasa hili la huyo mdogo wetu na watoto wetu pia..’nikasema.

‘Huyu mdogo wangu kwa sasa hana tatizo, keshajiweka mahali ambapo hatuna haja ya kuhangaika naye tena,..akiharibu hatuna lawama...na kwa watoto wetu bado wadogo, hatuna shaka nao, tutawajenga kimaadili, na umeshafanikiwa kwa hilo, kama wanaweza kuamuka asubuhi na kuwajibika hata bila kuelekezwa, tunataka nini tena mke wangu.’akasema.

‘Hapana bado,...bado wanahitaji kuelekezwa, ama kwa huyu mdogo wetu naye pia bado anatuhitajia sana, ndio kwa kiasi kikubwa kakamilika, lakini bado hajafikia ile hatua ya kuweza kuwekeza, japokuwa amekataa, lakini ni vyema tukamsaidia akawa ana ajira yake mwenyewe, mimi sipendelei sana ajira ya kuajiriwa, nataka ajiajiri mwenyewe,...’nikatulia kidogo na yeye akaniangalia akitaka kusema neno, nikamuwahi kwa kusema.

‘Ajira za kuajiriwa zinalemaza sana, ukiajiriwa, kwa hali ilivyo sasa, utapata mshahara mdogo, na siku zitakwenda, umri utakwisha, utanyonywa wee, huku wajanja wanafaidi jasho lako, na mwisho wa siku utajikuta huna lolote la maana,.....kwasasa tumuache kidogo, ajifunze maisha halafu na sisi kidogo kidogo tutatumbukiza nguvu zetu, ili aanzishe jambo lake mwenyewe....’nikasema.

‘Oh, hiyo ni kweli.....sasa umenipa matumaini, kumbe nilikuwa nimefikiria vibaya, nilipoona mdogo wangu kakupigia magoti mbele yako, niliumia sana, nilihisi kama mimi ndio nipo pale nakuomba msamaha, nilitamani nisimame nije nifanye jambo ....lakini kumbe hasira hasara,  nilihisi kuna tatizo limetokea, kafanya jambo baya,au kuna jambo baya kalisikia na hataki kutokee madhara, ,..’akasema.

‘Hilo halitatokea, ilimradi tu awe mkweli kwangu, na ndivyo maisha yangu ninavyotaka yawe, kuaminiana ndio tabia yangu, tuwe wakweli, tuambizane ukweli, kama nimekosea, niambie, na mimi ukikosea nitakuambia, unanifahamu silazi jambo, papo kwa papo ninakupasha. Na kazi ndio msingi wa maendeleo, ni lazima tujitume, hakuna lele mama katika maisha,...., hakuna kulala katika maisha kama una afya huumwi, chapakazi,..., ukilala wenzako wapo macho, wapo kwenye maabara, wanagundua, wanasonge mbele, ukiamuka huwakuti tena, ....ndivyo napenda maisha yetu yawe hivyo, tuchape kazi....’nikasema na yeye akaniangalia, halafu akawa kama anajikagua, nilihisi kuwa anajisikia unyonge katika hali aliyi nayo, kuwa yeye sio mtu tena.

‘Utapona tu mume wangu, tutashirikiana na kuhakikisha kuwa malengo yetu yanatimia, ..na malengo yetu yaendane na umri wetu, haitakiwi unafikia umri wa kukaribu kustaafu bado unahangaika, ..unatakiwa muda huo, unakuwa na muda wa kupumzika, hapo ndio nafasi ya hata kustarehe, unafaidi matunda yako, ujana, ni kuhangaika uzee ni kustarehe, na nashangaa watu wanafanya kinyume chake...mimi sijui maisha yangu yapoje..ndivyo nionavyo mimi...’nikasema na yeye akawa kama ananishanga.

‘Wenzako starehe ni ujanani, wewe unasema starehe ni uzeeni...’akasema akitabasamu.

‘Ukiwa kijana ndio uan nguvu za kuzalisha, mwili unahitajika kuchapa kazi, usipoteze muda, ndio kuna starehe, lakini ziwe kwenye kuujenga mwili, na sio kwenye kuumiza mwili,...watu tuwajibike....tutumie kila dakika katika kuzalisha jambo,...sio kuharibu, mwili una thamani sana, kama utautendea haki yake, uzeeni utastarehe sana...’sijui kama ninaeleweka.

‘Nakuelewa mke wangu...lakini sizani kama jamii itakuelewa...’akasema.

‘Jamii itatuelewa tu,...jambo lolote linaanzia kwa mtu mmoja mmoja, na baadaye wengine wanafuatia...’ nikamwambia.

‘ Ndio maana uliniona silali, sikutaka muda upite bure...’nikasema

‘Ama kwa mdogo wetu huyu, tutakuwa naye bega kwa bega, hakitaharibika kitu cha mhumi tuwe karibu naye...labda afanye kisiri siri, tusigundue ni kitu gani anakifanya, ...hata hivyo, kwa hatua aliyofikia, hawezi tena kufanya jambo baya, pale alipo anawaza maendeleo tu, anawazia maisha yake ya baadaye ...’nikasema.

‘Tuombee iwe hivyo..nashakuru sana mke wangu , umeniondoa wasiwasi, maana nilihisi kuna tatizo, hasa pale niliposikia, ukisema eeeh,  japokuwa sikusikia vyema, maana masikio yangu sijui na yenyewe yameathirika kwasababu ya hiyo ajali, nilisikia kitu kama ukisema ; `.... msione ajabu tukitengana, nasema ukweli kama hamtaniambia ukweli sasa tutatengana..kama asiposema ukweli, unaweza kuchukua hatua ambayo, .....’sijui ulisema neno gani...sikusikia vyema..niliogopa sana kauli hiyo’akasema.

‘Ni maongezi yangu na yeye, nilikuwa najaribu kumkanya....kiutani, kuwa aniambie ukweli, kama anataka kumuoa mfanyakazi wetu asema kweli, na aliposikia hivyo, akahisi nimekasirika , ndio akakimbilia kupiga mgoti, ....’nikasema na mume wangu akatabasamu, na niliona mazungumzo hayo yalimfurahisha sana, nikaamua kumuuliza;

‘Naona tukiongelea mambo ya ndoa, mapenzi, kusaidia,....mara nyingi nakuona unafurahi sana, kwanini?’ nikamuuliza.

‘Maana hayo ndiyo maisha ya mwanadamu, ndio yanayompa mwanadamu raha na faraja, ,..hasa kwa mke na mume, ..hata kama hamna kitu, lakini mkawa mnapendana, mnashauriana, manapeana moyo, mtajikuta nyi ni matajiri tu, lakini hata kama mna utajiri wa kupindukia, lakini hakuna mapenzi, hakuna mashikamano kila mtu anawaza lake, nyi ni masikini tu...maana mioyo yenu haina raha,.....’akasema huku kionyesha uso wa huzuni.

‘Kwahiyo unafurahi sana tukiongelea hayo mambo kuliko mambo ya kikazi?’ nikamuuliza.

‘Kazi ina mahali pake mke wangu, na mahali pake ni ofisini, ...ofisini kazi, na nyumbani pia kazi, tutazeeka akbla umri sio wetu, ha huenda hata tusipate muda wa kufaidi jasho letu,  nina furaha sana tukiwa hivi nyumbani tunaongea, tupo bustanini, tunasahau kabisa mambo ya kazini, tunatimiza wajibu wetu wa ndoa, ndoa ina raha yake, na moja ya raha yake ni kupendana, kuwa karibu, na kufurahia kile mungu alichowakutanisha... ndoa ni raha bwana asikuambia mtu, kama mkiijulia, ndoa yenye mapenzi ya kweli, inaleta faraja, vingievyo, unafikiri mtu utafanya nini, ili kichwa kipoe na mihangaiko ya dunia,..’akasema kama ananiuliza.

‘Kwahiyo kumbe mume wangu ulikuwa hupendi kwa jinsi nilivyokuwa nikifanya, mbona hata wewe ulikuwa ukifanya hivyo?’ nikamuuliza.

‘Ilibidi nifanye kama unavyofanya wewe, ili twende sambamba, nikijua ni kwa muda maalumu, huenda itafika muda tutakuwa pamoja kama mke na mume, tufaidi matunda yetu, na tukione tupo na raha, sasa utajiri wetu una maana gani, sikukuelewa, nilipoona kwa ndio mtindo wako wa maisha, hakuna kualala, hakuna starehe, hakuna kuburudika kama mke na mume, ...nikaona nitafute njia mabadala, kumbe nilikuwa naharibu...mara nyingi, nilitaka kukuambia, lakini sikupenda kukuuzi mke wangu’akasema

‘Mume wangu, mimi ni mke wako, na una haki ya kunishauri pale ninapoteleza, na ni makosa ukiona mimi nafanya yale usiyopendezewa nayo, ukanyamaza kimiya, ungeliniambia tu, ningeliskusikiliza’nikasema.

‘Kuna muda nilijarubu kufanya hivyo kimatendo, lakini nilishindwa, kwani kila nilipokuwa nikijaribu kukusogelea nilikuona ukiwa na kazi zako, na kuna wakati mwingine uliniambia una kazi nyingi, huna muda wa kuchezea, unakumbuka uliwahi kuniambia hivyo, wakati huo nilikuwa nakuhitajia sana, uwe karibu nami, kwani nilihisi ibilisi anataka kunichezea....lakini nikashindwa, je ningekulazimisha, hapana nisingeliweza kukufanyia hivyo mke wangu...niliona nikuache tu...nahisi nilikosea, lakini ningelifanya nini kwa wakati huo..?’ akawa kama ananiuliza.

Nikajaribu kukumbuka kama kuna muda aliwahi kunijia nikamwambia hivyo, inawezekana, maana nikiwa kwenye kazi, sitaki utani,  ni kweli kuna muda nilikuwa na kazi nyingi sana, na sikutaka zilale, na hapo niliweza kusema lolote, bila hata kukusudia hivyo, sikutaka kupteza muda, ..lakini yote hayo niliyafanya kwa ajili ya familia, kumbe mwenzangu alikuwa akipata taabu...oh, kweli nimeanza kujitambua...

‘Oh, mume wangu ndio maana ukakimbilia kulewa..nasikitika sana, japokuwa nitakulaumu kwa kutokuaniambia ukweli, ungeliniambia ningekusikiliza, ungelitafuta muda muafaka ukaniambia, mimi ni binadamu tu....kwanini hukusema?’ nikamuuliza.

‘Kulewa, nilianza kama masihara tu, nilipokuwa kwenye starehe, kupoteza mawazo, kuna jamaa huwa tunakutana naye, sio huyo rafiki yangu, hapana ni jamaa tu ambaye huenda naye ana matatizo yake, huwa anapenda kusema;

‘Unafahamu mke wa kukupotezea muda, ukiwa na mawazo....unafamhamu ndio huyu...’akawa anaigiza sauti ya kilevi mpaka nikasikia kucheka.

‘Ukiwa nyumbani na mke wako hana habari na wewe, basi kuna mke mwingine, japokuwa yeye anahitaji gharama, lakini hana hiyana, huyu ndiye mke wa gharama,lakini hana hiyana pombeee....’akawa anaendelea kuigisa zauti ya kilevi na mimi nikawa nacheka.

‘Ukiwa na pombe, basi umepata mke wa kukuliwaza, yeye anakufanyausahau yote, hata kumsahau mke wako wa ndoa, si hakutaki bwana, basi huyu anakutaka ila tu anahitaji pesa,.....ukiwa na pesa aah, unapata mke mpya asiye na majigambo, kazi yako ni kunywa, ni kunywa....’akawa anaigiza hiyo sauti na mimi nikawa nacheka sana.

‘Umenichekesha kweli leo, unaigiza kama mlevi kweli, au ni kwa vile na wewe ulikuwa ukiongea hivyo wakati umelewa....?’ nikauliza.

‘Lakini hayo yote sikufanya kwa kujitakia, ...ndio ni uzembe wangu, nakubali, na kweli nimekosa, lakini wakati mwingine naweza kukulaum kidogo, lakini sio sana..kidogoo tu, kuwa wewe ndiye uliyenisukuma hadi nikaingia huko kusikofaa...’akasema na mimi nikamwangalia huku nikijaribu kuzuia maneni yangu makali, nikasema kwa unyenyekevu

‘Mume wangu Ina maana haya yote yametokea kutokana na mimi, kutokana na ....ndoa yetu, kwani kuna nini nimekosea, ...maana nionavyo mimi ilikuwa ni swala la kuambizana tu...mimi nina imani kuwa kama ungelianiambia ukweli, ningelikusikia sijui kama ningelikukaidi, lakini kwa wakati muafaka....na je kutokana na kulewa huko huoni ndio kumekusukuma, hadi kufanya mambo yasiyofaa...?’nikamuuliza na niliuliza nikiwa na tahadhari.

‘Ndio maana najuta sana mke wangu unisamehe sana, maana kweli pombe ni ibilisi, kila siku iliyokuwa ikienda kwa mungu,  ndivyo nilivyojikuta nikitamani mengine mabaya, sikuwa na tabia hiyo kabla, ...maana ukinywa, raha yake muwe kikundi, uwe na  wenzako, na mwisho wake, wanakuja hata wale uliokuwa ukiwakwepa, na na...nashindwa hata kuongea,...’akatulia,kama anawaza jambo, haikutakiwa iwe hivyo, nikauliza

‘Kwa hawo wengine walikuwa wakijileta wenyewe, si unawaita, au,?’ nikauliza.

‘Kwenye majumba ya starehe, sio wote wanakuja kwa lengo moja, wengine wanakuja kwa malengo mengine kabisa, nimejifunza hilo, na hata wale unaozania kuwa ni marafiki, wanaweza kutumiwa mwanya huo kukughilibu..ukiwa umelewa, huwezi kutathimini mambo kihekima, unajikuta umetenda hata yale ambayo hukukusuidia..ni pombe, sio wewe.....’akasema.

‘Ina maana pombe ndio ilikutuma utende hayo uliyoyatenda...?’ nikamuuliza.

‘Ndio maana nilikuomba msamaha, ni kweli ni pomben, kama isingelikuwa ni pombe, nisingeliweza kufanya hayo niliyoyafanya, na kwanini nilikunywa pombe, jiulize hilo swali, kwanini nilikuwa nakunywa hadi kupitiliza, ukipata jibu utafahamu useme nini, na ni kweli mimi nakbali upande wangu kuwa nimekosa, kwani mimi sio mtoto mdogo, wa kufanya hayo,...hayo  niliyokuomba msamaha...’ akasema huku akikwepa kuniangalia machoni.

‘Mhh, mume wangu hay ohayo, hayana jina, ...ok, siwezi kukulazimisha kuniambia kwa sasa, lakini tutakuja kuayaongea, usijichoshe na mambo mengi...’nikasema.

‘Ina maana sijakuambi makosa yangu , unataka nikuambie kila kitu, hutakasirika mke wangu, mimi ninaweza kukuambia kila kitu, ilimradi tu, nisikukwaze, tena kuna mtu muhimu nasikia anakuja, na akija nafikiri mambo yatakuwa safi, unataka nikuambia mke wangu?’ akaniuliza huku akiniangalia machoni, na mimi nikawa nimeshika shingo kwa mkono mmoja huku nikitabsamu, na kusema;

‘Nitafurahi sana, lakini....’nikasema na mara nikasikia sauti za nyayo za mtu akitukaribia nikageuza kichwa kimwangalia huyo mtu, alikuwa rafiki wa mume wangu.

‘Oh, naona leo mpo na raha, maana nimesikia kicheko, ..kicheko cha raha, ...’akasema huku akituangalia, na mimi moyoni nikasema huyu mtu ana nini , maana kila nikiwa na kwenye nafasi nzuri ya kuongea na mume wangu hujitokeza.

‘Kwanini nisiwe na raha na mimi nipo na mume wangu..’nikasema.

‘Ni kweli hayo ndio maisha,...inatakiwa  mfanye hivyo kila siku,, au mara kwa mara, au sio rafiki yangu?’ akamuuliza mume wangu huku akimsogelea na kushikilia kile kigari,..na mume akasema;

‘Na wewe bwana, unakuwa dakitari wa kila kitu....’akasema

‘Ni kweli natamani iwe hivyo, na nimekuja na mtu wa mazoezi, leo tunataka kumfanyisha mume mazoezi maalumu, na kama hutajali naomba nimchukue mume wako’akasema

‘Unataka kumpeleka wapi?’ nikauliza nikimwangalia kwa uso uliotahayari.

‘Ndani ofcourse, tunahitajia tuyafanyie ndani, kuna vifaa maalumu kaja navyo docta...’akasema, na sikuwa na jinsi nikakubali, na wakati wanaondoka kuingia ndani yeye aligeuza kichwa na kuniangalia kwa nyuma, akasema;

‘Uwe makini....’akaniambia.

Nikamwangalia kwa macho ya mshangao, na nikataka kumuuliza niwe makini kwa kitu gani , japokuwa nilifahamu ana maana gani,  na yeye akasema kwa sauti ili kumuondoa mume wangu wasiwasi,kwani alihisi kuwa umesikia hayo maneno aliyoniambia, akasema;

‘Shemeji uwe makini, usimchekeshe sana mgonjwa, maana akicheka sana, ..anaweza kudondoak kwenye kiti chake,...’ na mume wangu akasema;

‘Ukiona nimedondoka kwenye hiki kiti ujue kuwa nimeshapona..maana bado nahisi sehemu yote ya chini kama sio yangu....’akasema na mimi nikawa nawafuatilia kwa nyuma hadi tulipoingia ndani, na wakati wanahangaika kumtayarishia, nikatoka nje kidogo, na baadaye akaja huyo rafiki wa mume wangu, akaniambia.

‘Nimekuona ukimuhoji sana mume wako, ...huu sio wakati muafaka, wa hayo maongezi yako...nilishakukunya ukimhamasisha kuongea, atafikia sehemu ataongea ukweli na hivyo itamzididhia huzuni, na wewe ukiusikia huo ukweli, ninavyokufahamu hutaweza kuvumilia, utakasirika, utasema ovyo, unafikiria baada ya hapo kutatokea nini.....kwanini una haraka na hayo mambo, uwe na subira  na hicho unachotaka kukijua, utakifahamu, lakini usije ukafanya jambo ambalo utakuja kujijutia.’ Akasema na mimi nikawa namsikiliza tu.

‘Kwani mimi nimemuuliza nini kibaya,..tulikuwa tunaongea tu na mume wangu, na kwanini wewe unayejua ukweli hutaki kuniambia, ..wewe unajifanya kuwa unanijali, kumbe kuna mengi makubwa unanificha, hutaki kuniambia ukweli, na huenda haya yote yasingelitokea kama ungelikuja mapema ukaniambia...’nikasema.

‘Ina maana unanilaumu mimi, ...unanichekesha, kweli, ushindwe mwenyewe kuihudumia ndoa yako halafu uje kuwalaumu watu wengine, umesahau mara ngapi ninakuja kuongea na wewe na kuajribu kukuelekeza halafu wewe uannitolea nje, kuwa nimetumwa na wazazi wako kuja kukuharibia ndoa yako, umeshahau eeh, sasa unaona yamekukuta, unataka kunilaumu....’akasema.

‘Huna maana wewe, na ole wako nikifahamu ukweli, ...ukweli ambao ulitakiwa wewe uniambia ukanificha, ..sitakusamehe kamwe...’nikasema.

‘Unakumbuka nilishaanza kukuelezea ukweli ukasema hutaki kugombanishwa na marafiki zako, hususanai mume wako, umeshasahau eeh, usinione kuwa mimi ni mjinga, nafanya haya kihekima, ni bora ukawaachia wenyewe wanandoa wakajibadili wao wenyewe, maana kijiingiza kwenye ugomvi wa wanandugu unaweza ukaonekena wewe ni mbaya...’akasema.

‘Kwahiyo umesahau ile ahadi yako,?’ nikamuuliza

‘Ahadi gani?’ akaniuliza

‘Kuwa kamwe hutakubali mtu aniumize...’nikasema.

‘Na ndicho ninachokifanya...wewe mwenyewe utaona, si unajifanya mpelelezi, endelea,...lakini mimi nitajitahidi kuhakikisha kuwa hakuna mt anayekuumiza,ahadi yangu ipo pale pale, hata kama hunitaki niwe karibu na wewe....ila nakukanya uwe mwangalifu, usichukulie mambo kwa pupa..’akasema huku akitabasamu na kushika kidevu

‘Halafu kuna ujumbe, nimeupata, kutoka eeh, kwa rafiki yako, yupo karibu kurejea...anasema anakuja kumaliza mambo fulani fulani, halafu atarejea kusoma, ...sijui ni mambo gani, kwani hamjawasiliana naye ?’nikamuuliza

‘Rafiki yangu yupo?’ nikamuuliza nikionyesha mshangao.

‘Una marafiki mangapi bwana, huyo huyo,..unayemwamini kupidukia,...nahisi ukweli sasa utagundulikana, ila bado nakukuanya, uwe makini, hasa akija huyo rafiki yako,...huenda yatakuja kutokea mambo ambayo, yatakufanya usiwaamini tena wale unaowaona ni marafiki zako, lakini huenda yote umajitakia mwenyewe.....’akakatizwa, kwani alikuwa akiitwa ndani.

‘Eti nini....?’ nikamuuliza nikiwa nimeshakunja uso.

‘Tutakuja kuongea siku nyingine....lakini hebu kunjua huo uso wako please’.

NB: Tabasamu na wewe mpenzi wa blog, kisa kinaendelea, wasemaje?



WAZO LA LEO: Ndoa nyingi zina matatizo yake, na huenda yakawa ni matatizo madogo tu, lakini kwa wanandoa wakashindwa kuyatatua, kwa vile, hakuna anayekubali kushuka chini, kila mmoja anajiona anafahamu zaidi ya mwingine...au mmoja anaogopa kumuelezea mwenzake ukweli.....wewe kama rafikji tumia hekima kuwashauri, usitumie mwanya huo kuharibu badala ya kujenga. Hekima ya ushauri ni muhimu sana kwa watu kama hawo.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Unknown said...

Mmh, naingawa huyu dada ndie aliemshauri rafki yke lkn pia marafiki sio wa kuwaamini kbs wanaweza wakakufanyia kitu kby ndio haya sasa yaliyomkuta mdada hembu tusubiri italavyokuwa.

Unknown said...

Hebu tusubiri rafki yake aje tuone itakavyokuwa ila marafiki sio watu wa kuwaamini kihivyo.