Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 20, 2013

WEMA HAUOZI-51


Mwanadada aliendelea kumsimulia mama yangu , mama ambaye ndiye aliyekuwa akimsimulia mwanae, jinsi maisha yake yalivyokuwa, na jinsi gani alivyoweza kupambana kuitetea haki yake ambayo kama angekaa kimiya, angekosa kila kitu kutokana na dhuluma ya watu wachache. Hata hivyo mama yake alisema yote hayo yalitokana na wema, wema uliotokana na mtendo mema ambayo ndiyo ylioyomuwezesha  hadi kuweza kuwashinda waovu na  dhuluma zao…

Tuendelee na kisa chetu, tukiwa bado tupo msituni, na mwanadada na mwanadada akiwa na kundi lake, na ukumbuke kuwa yule muongozaji anayeufahamu huo msitu na miiko yake, alishasema kuwa yeye anaondoka, kwani kazi aliyotumwa kuifanya alishaikamilisha, je waliobakia wataweza kuikamilisha hiyo kazi,………
‘Hatukuweza kumshawishi yule muongozaji wetu msafara, na ikabidi yeye aondoke…japokuwa bado tulikua tukimuhitajia sana…..’akasema mwanadada.

‘Mimi ningelifurahia niendelee nanyi hadi mwisho, lakini kutokana na masharti niliyopewa, mimi siruhusiwi tena kuendelea zaidi ya hapo, kwahiyo endeleeni wenyewe na kama mtanihitajia  kutoa ushahidi mahakamani nipo tayari wakati wowote….’akasema huku akiondoka.

‘Jamani tusipoteze muda, kazi iliyopo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha huyu mtu anakamatwa, akiwa hai, ….na kama mlivyosikia, huku haturuhusiwi kutumia silaha, milio ya risasi hairuhusiwi huku msituni, sijui ndani ya hilo….’akasema mwanadada.

‘Lakini hakusema ndani ya handaki, kasema huku nje…tukimfuta huko ndani ikibidi tunaweza kutumia , lakini sio muhimu….’akasema mwanasheria, na mwanadada akamtizama kwa mashaka, na yule mkuu akatikisha kichwa kama kusikitika.

Kwa vile ule waya wa Antenna ulishakatwa, ambao tulikuwa na wasiwasi kuwa ndio unaopeleka mawasiliano huko, ndani tulikuwa hatuna wasiwasi tena, na kwa muda huo tulikuw tukisubiria kikosi kingine cha mkuu ambacho walitengana nacho katika kugawana majukumu, na haikupita muda kikosi hicho kikafika na hapo tukawa na uhakika kuwa hata kama jamaa ana kikosi huko ndani hatatuweza.

 ‘Mikakati ikaanza ya jinsi ya kuingia ndani ya hilo shimo kwa nia ya kumvamia mtaalamu, na sasa hatukuwa na lile lengo la awali la kuonana naye kwa ajili ya kuthibitisha zile sumu, sasa tulikuwa tunamuhitajia kama mshukiwa muhimu wa kesi yetu iliyokuwa bado mahakamani, ambayo kesho yake inahitajika kuendelea….

‘Mkuu, utaongoza kikosi chetu na mimi nitakuwa msaidizi wako..’akasema mwanadada.

‘Hamna shida, …’akasema huyo mkuu, na hakuacha kumwngalia mwanasheria wa familia, na uvumilivu wake ukafika kikomo, akamshika mwanadada mkono na kusogea naye mbali kidogo na kuanza kuteta naye, akauliza;

‘Na huyu mtu naye kafuata nini?’ akauliza akimuashiria mwanasheria wa familia ya marehemu mume wangu, na mwanadada hakutaka kuuliza kuwa anamuulizia nani alishajua anachoulizia akasema

‘Huyu mwanasheria ehe….yeye kasema ameamua kujiunga na sisi baada ya kugundua ukweli,….’akasema mwanadada.

‘Mimi bado simwamini, angalia hali ilivyo, kila unayemwamini unakuja kugundua kuwa ni mmoja wao, na anaongea kwa nia ya kujisafisha tu…sasa mimi nashangaa kweli baada ya yote bado unamwaini huyu mtu….!’akasema mkuu huyo akimwangalia mwanasheria kwa macho ya uficho.

‘Mimi naona tusiwe na mashaka naye, ….’akasema mwanadada.

‘Mwanadada, ninakuambia ukweli  hawa watu hawaaminiki, wanaweza kujigeuza kama kinyonga, ilimradi wapate wanachokitaka, na kwa vile sasa maji yameshawafika shingoni, …..ndio maana wanaamua kufanya hivyo, ….kuwa makini, walichokifanya kwa binti yangu sizani kama nitakuwa na amani na watu kama hawa, unafahamu kuwa binti yangu katoweka tena….’akasema akionyesha uso wa huzuni.

‘Unasema kweli…!?’ akauliza mwanadada kwa mshangao.

‘Katoweka kiajabu na hatujui tutamtafutia wapi, na yule kijana aliyekuwa ni rafiki yake, hali yake ilizidi kuwa mbaya sana, na wakati tupo huku, nikasikia binti yangu katoweka kijabu na mara wakasema hali ya huyo kijana rafiki yake imebadilika ghafla na kuwa krejea kwenye hali yake ya kawaida, wanasema hajambo kabisa, …..sasa sijui, kuna nini , na je kuna uhusiano wowote wa kupotea kwa binti yangu na hiyo hali yake…’akasema.

‘Unafikiri kuumwa kwa huyo kijana na kurejea kwa hali hiyo na hatimaye kupotea kwa huyo kijana kunatokana na hawa watu?’ akauliza.

‘Ndivyo walivyosema hawo watu wanaomshughulikia huyo kijana, na wanadai kuwa tusipohangaika kumshughulikia huyo binti, kesho ndio siku ya mwisho, hatutaweza kumpata tena, na baada ya hapo kunaweza kutokea makubwa zaidi….’ Akasema huyo mkuu kwa masikitiko.

‘Sasa wewe unasemaje?’ akauliza mwanadada akiwa kapagawa.

‘Mimi nina imani kuwa hawataweza kumzuru binti yangu, na kama ndio hawo, …na kama ni mambo yao ya kishirikina, mimi nitapambana nao kwa silaha….na nitahakikisha wote wanaohusika wanakwenda jela au nawamaliza kabisa….’akasema akikunja uso kwa hasira na kumshika mwanadada warejee kwa wenzao.

‘Ila nasema hivi huyu mtu usimwamini, asishirikishwe kwenye kazi zetu…’akasema huyo mkuu.

‘Sijamuamini moja kwa moja, ila kwa vile ninamfahamu, sizani kama anaweza kutusaliti, mimi namfahamu sana, mara nyingi ni mbishi, lakini ukweli ukidhihiri, akagundua kuwa kweli ana makosa, hachelewi kukiri,….ninakuhakikishia hilo, hataweza kutusaliti, lakini sio kwamba nimemkubalia moja kwa moja kuwa nasi….’akasema mwanadada.

‘Usije ukarubuniwa kwa vile alikuwa mchumba wako, tunapokuwa kwenye kazi kama hizi, mapenzi unayasahau kabisa…kama ningekuwa mdhaifi kiasi hicho mimi nisingelwieza kuja kuendelea na haya mambo, fikiria binti yangu kipenzi, ……hapana, nakuomba sana usije ukafanya makosa….’akasema huyo mkuu.

‘Usijali mkuu…..’akasema mwanadada huku akimtizama mwanasheria ambaye alikuwa akiongea na watu wa usalama kama vile ni mmoja wa kundi lao la kumkamata huyo mtaalamu.

‘Wasiwasi wangu ni kuwa nyie akina mama ni wepesi sana kutekwa na mapenzi mkajisahau, unajua mwanadad mapenzi yanaweza kuwa sumu, na kujikuta kazi yote tuliyofanya inakuwa ni kazi bure, hawa watu ni wajanja sana…sijawahi kukutana na watu wajanja kama hawa….’akasema huyo mkuu huku akimwangalia mwansheria ambaye alikuwa katulia upande wa pili, akisubiri na wenzake ni nini kitafuata baada ya hapo.

Mwanadada akapiga makofi, kuwaashiria watu waliopo hapo wakusanyike mahali pamoja, ili waweze kupanga jinsi gani ya kufanya, na walipokusanyika, mwanadada akasema;

‘Mimi sio mtaalamu sana wa kuongoza mapigano haya ya moja kwa moja, sisi utaalamu wetu ni kwenye ulingo wa mahakama,….japokuwa sio kwamba siwezi kazi hii, ila kwa vile yupo mkuu, mtaalamu wa mambo haya, siwezi kujifanya naweza, zaidi yake,… kwahiyo , inabidi mimi nikae pembeni tuongozwe na mtaalamu wetu huyu, mkuu wa kituo chetu katika idara ya upelelezi, natumai tutamtii ili tuweze kukamilisha kazi iliyopo mbele yetui, karibu mkuu…’akasema mwanadada.

Mkuu hakupoteza muda, akaanza kuelekeza jinis gani ya kufanya, na kila mmoja akampa kazi yake ya kufanya, na ilipofika kwa mwanasheria, akasita na kusema;

‘Mhh, nashindwa kukupa jukumu, …mwanasheria maana wewe haupo uapnde wetu, sina uhakika na ujio wako, ila nakuonya kama una lolote dhidi yetu, bora urejee huko kwenu, maana sitakusamehe , na nitahakikisha nachukua sheria mkononi mwangu kwani kundi lenu ni baya sana…’akasema

‘Kama huniamini mkuu, mimi nitalinda huku nje, msiwe na shaka na mimi nafahamu unajisikiaje,..hata mimi ningelikuwa upande wenu huenda ningejisikia hivyo hivyo, …..ila kama mtanihitajia niingie huko ndani nipo tayari, lakini naomba sana mtu huyu asitoroke, na akitoka nje, nitakula naye sahani moja,…’akasema huku akikunja uso kwa hasira.

‘Tuna watu wa kutosha, wewe tusubirie huku nje, na tunakukanya  kama ulivyosikia eneo hili halihitajii kutumia risasi, sasa usije ukatumia mbinu za kumuua huyu mtu, kama atatuponyoka ili asiweze kutoa ushahidi, utabeba hilo jukumu, utakuwa wewe ndiye mshukuwa mkuu …..’akasema huyo mkuu.

‘Msiwe na shaka na hilo, nalielewa sana….’akasema huku akionyesha kukerwa  na alipoona kuwa hataweza kuruhusiwa kuingia ndani akasema;

‘Na mkuu ninaomba sana muhakikishe mwanadada hadhuriki…..akidhurika na lolote na mimi sitakusamehe kwa hilo….’akasema na kumwangalia mwanadada kwa macho ya upendo.

‘Hahaha..leo hii unayasema hayo….umeshachelewa mpendwa....’akasema mwanadada akigeuka kuelekea pale walipoona jamaa akifungua ule mlango, na wanzake akiwemo huyo mkuu wakamfuata na kushirikiana kwa pamoja kuyasogeza yale majani yaliyokuwa yametambaa na kutengeneza kitu kama mkeka,  na kumbe kwa chini, kulikuwa na huo mfuniko, wakasogeza yale majani na kukuta ule mfuniko.

‘Haya jamani kazi imeanza akasema mkuu, …na yeye akawa wa kwanza kuingia baada ya kufunua ule mfuniko, na akafuataiwa na mwanadada….na maskari wengine wa usalama wakaingia, alibakia askari mmoja wa usalama, ..

‘Wewe kwanini umebakia nje..?’ mwanasheria akamuuliza akimwangalia kwa mashaka.

‘Mimi nahitajika kulinda huku nje…kwanza kwanini unaniuliza wakati wewe umeshaambiwa kuwa huhusiki….?’akasema huyo askari kwa hasira, na mwanasheria akatabasamu na hakupenda kuendelea kubishana naye, akasogea kichakani na kujificha huku macho yake hayabanduki kwenye ule mlango wa lile pango.

Yule askari wa usalama, naye akasogea upande mwingine, na alipoona yupo peke yake, akatoa simu na kuanza kuwasiliana …..

**********

‘Tulipoingia ndani ya hilo pango,….ambalo linaelekea chini kidogo kama shimo,…na kwa pale juu, kulitengenezwa vyema kabisa, kiasi kwamba hata mvua ikinyesha maji hayaendi chini,ule mfuniko hauruhusu maji kuingia na kwa pembeni kuna mzunguko wa kuwezesha maji yasituame hapo na kuleta madhara…na shimo hilo lilichimwa sio kwa kwenda chini moka kwa moja,  lilikuwa likienda upande upande, huku linaelekea chini kwa mahesabu ya aina yake…

Kwa pembeni mwa hilo shimo, kulikuwa na sehemu kubwa , kama kichemba, ambapo pikipiki na baiskeli vilikuwa vimewekwa na kufungwa na minyororo, na kushikanishwa na waya ambao inaonekana ni kwa ajili ya tahadhari, kama mtu akigusa tu,kunatokea ishara kwa ndani au mtu huyo hurushwa na umeme.

‘Mtu asiguse huyo mnyororo au hiyo baskeli na pikipiki, inaonekana imetegeshewa….’akasema huyo mkuu,
Ilivyotenegenezwa ilikuwa kama ngazi, kuwa unashuka kidogo kwenda chini, halafu unatembea kidogo kwenda mbele, ni kama ngazi, ilikuwa imejengwa vizuri, kama vile imesakafiwa, lakini ni kwa udongo wa mfinyazi….kila mmoja alishangaa ustadi uliotumika humo ndani, hata hivyo kila mmoja alikuwa akitembea kwa tahadhari akijua ni hatari gani iliyopo mbele yao….

‘Tuliifuata ile ngazi kwa uangalifu, na kwa vile sio mtereremko, hatukuweza kupata shida, na tulipofika mbele kidogo kwa pembeni kulikuwa na mlango, uliotengenezwa kwa mbao, na kuzungushiwa nondo, ni mlango uliotengenezwa kama suara kwa ufundi wa aina yake, na kupambwa kwa maua, na haukuwa umefungwa kwa ndani, kwani tulipojaribu kuusukuma ulifunguka kwa kwenda juu, nakuacha nafasi na baada ya muda kidogo hujifunga tena,

‘Hakikisheni hamuachi alama za vidole,….’akasema yule mkuu wa upelelezi, na kila mmoja alihakikisha kuwa amevaa soksi za mikononi kwa ajili ya kuzuia alama zao za vidole, na kila mmoja alikuwa na silaha tayari mkonono kama ni lazima kuitumia

‘Japokuwa tumeambiwa huku hakutakiwi  kutumia silaha, lakini tupo ndani ya shimo, kama itakuwa ni lazima, hatusita kuitumia silaha , kisichotakiwa ni nje, maana hawo mizimu hawapendi milipuko…milio ya bunduki ndiyo iliyowafukuza uraiani, historia inasema watu hawa walikimbia vita, walikimbia milio ya bunduki,…...’akasema huyo mkuu, na wamadada akawa anachunguza kwa macho huku na kule hakuwa akisema neno, aliitikia kwa kichwa tu.

‘Nilikuwa na mawazo mengi kichwani kwa muda huo, na ungeniuliza unawaza nini kwa wakati ule nisingeliweza kukuambia,…..ilikuwa kama kichwa kimelindukana vitu vingi na vyote vinatakiwa kufanyika na muda hautoshi…..’akasema mwanadada.

Wakafungua tena ule mlango na kwa haraka wakaingia ndani na kujikuta kwenye chumba kama cha mapokezi, sehemu zote kulikuwa na mwanga, kwani kulikuwa na taa zimewekeza ukutani, huwezi kuziona kwa jinsi zilivyowekwa kwa ustadi, na mwanga wakekufanya chumba hicho kiwe kama mchana,….wakaangaza huku na kule, na kwa chini, kulikuwa na busati,…

‘Mbona hakuna mlango?’ akauliza mmoja wa maaskari akiangalia huku na kule

‘Tumia akili bwana…’akasema huyu mkuu na kuinua lile busati, na hapo wakaona mlango wa chini huu haukuwa wa duara, ulikuwa wa mapana na marefu yanayolingana, na kulikuwa na kitasa kilichowea na kuchimbiwa ndani kulingana na ule mlango, na juu yake kuna kimbao, kiasi kwamba usingeliweza kuwa kuna kitsa kama hicho, ni mpaka ukibenua kile kimlango,…. Wakafungua kile kitasa kwa taratibu na ule mlango ukajisogeza bila kutoa sauti na kukaonekana ngazi za kwenda chini, wakashuka kwa taratibu..

Na hapo wakajikuta kwenye chumba kipana kama ukumbi, kukiwa na meza na viti, na viti vilikuwa vimekwa juu ya meza kuashiria kuwa kumefungwa, kama wafanyavyo kwenye maukumbi na kulikuwa na mlango moja tu wa ulioonekana mbele yao

Kote kuikuwa na taa za umeme, zilizowekwa ukutani kiufundi, kiasi kwamba, huwezi kujua kuwa kuna taa zipo ukutani,na ilionekana kama vile upo nje….kwakweli ujenzi huo utakuwa umegharimu pesa nyingi sana na utaalamu wa aina yake.

‘Kuweni makini,huenda huyo jamaa yupo tayari anatusubiri kwa silaha,na inaonekana hayupo peke yake…’akasema mkuu, na wote wakawa makini na silaha zao zikiwa tayari mikononi, kama zitahitajika kutumiwa, na mkuu akafungua ule mlango na ulipokuwa wazi, yeye akapenya kwa haraka na kuangaza huku na kule, na alipoona kuna usalama akawaashiria waingie waingie, hapo kulilikuwa na taa zilizofifia mwanga, ..ni za rangi, isiyojulikana kuwa ni rangi.

Chumba hicho hakikuwa kipana sana, lakini kilikuwa ni ofisi, ikiwa na kila kitu cha kiofisini komputa, mafaili,na simu ya mkononi na mashine iliyoonekana ndiyo inayoongoza kila kitu hapo ndani, kwani kulikuwa na screen kubwa ikiwa ukutani na kwa muda huo ilikuwa haionyeshi kitu, huenda ni kutokana na vile tuslihakata ule waya wa kusaidia kuona nje. Kwa pembeni yake kulikuwa na milango, ilikuwa milango miwili inayoashiria kuwa ni vyumba vingine ..

Mkuu akamuashiria mwanadada kuwa yeye na watu wawili waingie chumba kimojawapo nay eye na watu wawili wafungue mlango mwingine, mwanadada akakubali kwa kichwa, akiwa na silaha yake tayari mkononi, akashika kitasa cha ule mlango, na kwa taratibu akakinyonga kile kitasa, na mlango ukafunguka, kilikuwa chumba cha kulala, kitanda na kila kitu kama ilivyo chumba cha kawaida, na pale kitandani kulikuwa na watu wawili wamelala mwanamke na mwanamume..

Yule mwanaume alikuwa kalala kifudifudi, tumbo chini, huku mkono mmoja umeshikilia chupa ya kilevi, na mkono huo ulikuwa umening’inia pembeni mwa kitanda, na chupa ile ilikuwa kwenye stuli, japokuwa mkono ulikuwa umeshukilia ile chupa, kama vile hataki mtu kuichukua,…..

Pembeni yake, kwa ukutani alikuwa kalala mwanadada, ni binti mdogo tu,akiwa kalala huku kaangalia juu huku mikono imeweka kichwani kama mto, na alionekana kama analia….kwa kutoa machozi sio kwa sauti…

Yule msichana alikuwa ndiye wa kwanza  kushituka kuwa kuna watu wamefungua mlango,  na alipowaona hawo watu, kwanza litaka kupanua mdomo kupiga kelele, lakini mwanadada akamuashiria anyamaze, na yule mwanadada akatulia kimiya japokuwa alikuwa kainua kichwa, na ywele zake nyingi, alizokuwa kaziachia zilikuwa zimemfunika uso,na kubakisa sehemu za macho….na isingelikuwa rahisi kumgundua huyo binti ni naki kwa muda ule, na wote pale mawazo yao yalikuwa kwa huyo mtu aliyelala hapo kitandani.

Yule mwanaume alionekana alikuwa kalewa, au kalala kweli, maana kilichokuwa kikisikika ni mihemo ya ya mtu aliyelala, na kama kitu kinamkaba, kwahiyo mara kwa mara akawa kama anakohoa, na ilionekana dhahiri ni kutokana na jinsi alivyoalala …,na kwa jinsi alivyoshikilia ile chupa ya ya pombe  inaonyesha kuwa ni muhimu sana kwake, kuliko kitu kingine.

Mwanadada na watu wake wakaingia wakiwa na tahadhari na mmoja alikwa tayari ana pingu mkononi, taayri kwa kumfunga, na bastola zao mkononi,  wakamsogelea huyo jamaa pale alipolala…

Yule mtu kwanza alitikisika na kuwa kama anakoroma kuashiria kuwa alikuwa kalala, na akatulia kimiya, na mwanadada akamuashiria yule msichana kuinuka na wakati huyo msicahan anainuka pale kitandani, yule mtu kama mshale alijibinua na aliposimama alikuwa kashikilia bastola mbili mkononi, na kujibanza kwenye ukuta, akiwa tayari kwa mapambano.

‘Upo chini ya ulinzi…mtaalamu, usijaribu kufanya lolote..’akasema mwanadada.

‘Ni nani unamuita mtaalamu, mimi sio mtaalamu, mtaalamu wa kitu gani….na kwanini nipo chini ya ulinzi,…na kwanini mnaingilia maisha ya watu….?’ akauliza huyu jamaa akiwa kashikilia bastola akiieleekeza huku na kule, na kwa mbele yake alikuwepo yule msichana akitetemeka kwa uwoga na yule askari usalama naye akiwa kashikilia bastola yake, akiwa anamwangalia kwa makini huyo  mtu.

‘Kila jambo lina mwisho wake, yote uliyoyafanya sasa yamefika mwisho wake, weka silaha yako chini na jisalimishe ili tuyamalize haya mambo kwa amani, hakustahili kumwaga damu tena na hasa eneo hili, kama unavyofahamu kuwa huku hakutakiwi kutumiwa silaha… mtaalamu…’akasema mwanadada.

Yule jamaa kwanza alishikwa na butwaa, lakini kwa haraka akajibadili na kuondoa hiyo hali ya kushangaa machoni mwake, na kusema;

‘Ohoo, kumbe, mnataka sharieeh, ok, kwangu mimi haina tofauti, …nipo tayari kufa, …’akasema huku akiniangalia kwa mchao yaliyojaa hasira. Na kwa haraka akapiga hatua moja mbele kumkaribia yule msichana.

‘Tatizo lako hunijui mimi, wewe mwanamke mimi sio huyo unayemuita mtaalamu….kwanza kwa  usalama wenu tokeni kama mlivyokuja, ….sitasita kuitumia hii silaha, maana mumeniingilia nyumbani kwangu….’akasema huku akiwa keshakiweka kidole sehemu ya kufyatulia risasi.

‘Sikiliza….’akasema mwanadada na yule mtu akaelekeza hiyo bastola kwa mwanadada kama anataka kuifyatua, na yule askari wa usalama akawa anataka kujibu mashambulizi lakini mwanadada akamuasiria asifanye hivyo.

‘Kwanini mnanivamia kama mhalafu, mbona mnaingilia maisha ya watu, nina kosa gani mimi, au kwa vile mnaona ninaishi huku …mapangoni, haya ni maisha yangu niliyojichagulia mwenyewe,…..?’ akasema huyo mtu huku akimwangalia yule mtu wa usalama kwa jicho la kujiiba, na ghafla akamdaka yule msichana aliyekuwa karibu yake na kumshikilia huku akiwa kamlenga bastola kichwani.

‘Usijifanye hamnazo, sisi tumeshagundua janja yako….ulipokuwa mahakamani ukitoa ushahidi kuna sehemu uliteleze mimi nikafuatilia, na kugundua mengi kukuhusu wewe….kujibadili kwako, sio tatizo, kuna mambo mengi yameshafichukuliwa , kama kweli huna hatia, una haki ya kujitetea mahakamani, na haki itakulinda….’akasema mwanadada

‘Kama hamtatoka hapa au kuniruhusu mimi kutoka hapa ninammaliza huyu binti…mimi sihitaji kwenda mahakamani, sheria ninayo mwenyewe, ndio maana naishi huku, sitaki shida na watu, …lakini kama mnanitaka shari, sitasita kufanya lolote kujihami….’akasema na kumvuta yule msichana , na yule msichana akawa mbele yake, huku akiwa kamzungushia mikono yenye bastola na kuelekeza moja kwa mwanadada na nyingine kwa yule askari usalama.

‘Sikiliza ndugu yetu, mimi kuja kwangu hapa sio kwa shari, na ulionyesha moja wa kushirikiana na mimi, na nahitajika kulipa fadhila nitajitahidi kukutetea kadri niwezavyo…’akasema mwanadada na huyo mtu akacheka kwa dharau.

‘Tatizo wewe mwanamke huelewei unaongea na nani, …nimeshakuambia kuwa mimi ninasihi kwa sheri zangu, sihitaji huruma ya mtu, sihitaji kusaidiwa, …ninajua ni nini ninachokifanya, na ni nini mwisho wa yote, siogopi kufa, kufa nilishaandikiwa mapema….’akasema na kumsogeza huyo msicha kifuani kwake, na huyo msichana akawa analalamika kwa maumivu.

‘Muachie huyo msichana aende zake, kama kweli unajiamini, kama kweli huogopi kufa, kwanini uwahukumu wengine wasio na hatia…..’akasema mwanadada.

‘Sikilizeni msinipoteza muda, akafyatua risasi iliyopiga ukutani , na hapo mwanadada akafahamu kuwa huyo jamaa hatanii, na mawazoni mwake, alitaka kufanya lolote, na yule jamaa, akaiweka bastola moja mfukono kwa haraka na akawa an mkono mmoja upo hutu, akamshika yule msichna vizuri na kusema mnamfahamu vyema huyu binti ni nani?’ akauliza huyu mtu.

Na mwanadada akamwangalia yule binti kwa makini, kwani nywele zilizokuwa zimetimuliwa zilikuwa zimemfuniko usoni, na aliposema hivyo yule mtu, akamfunua zile nywele yule binti eneo la usoni na hapo mwanadada akaweza kumuona vyema yule binti.

‘Wewe binti umefuata nini huku?’ akauliza mwanadada kwa mshangao.

‘Sijui nimefikaje huku….’akasema huyo binti akiangalia huku na kule, na mara mkuu wa kituo katika kitengo cha upelelezi akaingia na kikundi chake na kusimama katikati ya mlango, na kumfanya yule mtu kuonekana kupagawa kwa wasiwasi, hakutarajia hilo tukio, alijua kuwa anapambana na hawo watu waliopo ndani, ….lakini kuna cha zaidi kilichomfanya hadi aonekane kuwa na wasiwasi kuliko kawaida ahasa alipomuona huyu mkuu

Hata hivyo, hakumuachikia yule binti, na wakati huo yule binti nywele zilikuwa zimemfunika kama mwanzo, sasa akawa anamsukuma yule binti asogee mbele, na yeye akatembe hatua chache kukaribia kwenye mlango, nahisi alishafahamu kuwa watu hawo hawawezi kutumia silaha zao, kwahiyo hakujali tena, akamsukuma yule binti  atembee kuelekea kule kule aliposimama huyo mkuu.

Mkuu alipoingia alikuwa kashikilia bastola yake mkononi, na macho yake yalikuwa kwa huyo mtu, tayari kwa lolote lile na alipomkuta huyo mtu kashikilia bastola akiwa kaikandamiza shingoni kwa huyo msichana, akasita lakini hakuacha kuuilekeze bastola yake kwa huyo mtu, na kwa muda huo akili yake ilikuwa kwa huyo mtu, hakuwa na haja ya kumwangalia huyo msichana ni nani,
Ni pale macho yake, yalipotua kwa huyo msichana,kwanza alimtizama kwa mashaka, halafu akawa kama kaduwaa, na baadaye akasema kwa mshangao

‘Binti yangu ….’akasema mkuu huku akiwa kaduwaa, hakuamini macho yake.

Na hiyo ndiyo nafasi aliyokuwa akiihitajia huyo mtu, kwani kwa haraka,alimsukuma yule binti, na yule binti kwa vile hakutajia hilo tendo, alikwenda moja kwa moja na kugongana na baba yake, na wote wakaserereka chini, na wakati huyo mkuu ana jizoa zoa, yule mtu akawapita na kuwasukuma wote wawii kwa pamoja na kuwafanya wawe wamelaliana, na hapo akawapita kwa haraka, na mkuu alishindwa kufanya lolote kwani binti yake alikuwa kamlalia,

Mwanadada na maaskari wengine, walikuwa wakijaribu kumwahi huyo jamaa, lakini huyo jamaa alikuwa mwepesi ajabu, kwani hayo yote aliyafanya kwa muda mfupi, na keshatoka mle ndani. Na mwanadada akawa anatoa amri kwa watu waliopo nje wahakikisha wanamshika huyo mtu, asitoroke, na mara wakasikia milio ya bastola na vilio vya watu vikasikika kuashiria maumivu .

‘Oh, mambo yameshaharibika….’akasema mwanadada, na yule mkuu akasema kwa suati

‘Msimuua, tunamuhitaji akiwa hai…..’alisema huku akiinuka na kuelekea huko nje, na wote wakajikuta wapo mlangoni, na mlango ulikuwa ni mdogo, inahitajika atoke mtu mmoja mmoja.

Mwanadada na mkuu, na maaskari wengine,wakatoka kwa haraka kuelekea sehemu hiyo ambapo milio ya risasi ilisikika, wakiwa na bastola zao mkononi, lakini walikuwa wamechelewa, kwani eneo la nje ya la hapo ofisini,  waliwakuta askari wao wawili wakiwa wamelala chini, huku wakivuja, damu, na wengine walikuwa wakifukuzana  na huyu jamaa huku wakijibizana kwa bastola…

NB: Je miiko itavumilika, kuwa silaha zisitumike, hasa kwa mtu kama huyo, ….Je kumdhibiti muhalafu wa namna hiyo inahitajika nini, zaidi ya kutumia nguvu, ….


WAZO LA LEO: Matendo mabaya yakikithiri, mioyo huota sugu, na ubinadamu hutoweka kabisa. Wanadamu huwa kama wanyama, huruma na upendo hutoweka, chuki visasi na husuda inauwa na hulka…amani hakuna tena.Swali la kujiuliza ni nini faida yake, wakati kila mmoja njia ni hiyo hiyo ya umauti, kwanini tusiwe wema, na dunia ikawa ni kisiwa cha amani.

***********

Maombi: Pendekeza blog hii kuingia kwenye mashindano ya best blog awards kwa kuandika email na kutuma kwa ``tanzanianblogawards@gmail.com’’

Kwenye subject unaandika diary yangu (http://miram3.blogspot.com/)  na kwenye maelezo unaandika hivi;
Naipendekeza blog hii ya diary yangu (http://miram3.blogspot.com/ kwenye kipengele cha;

Best Creative Writing Blog

Best Educational Blog

Best General Blog

Ni mimi: emu-three

No comments :