Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, August 14, 2013

WEMA HAUOZI-49


Wakili mwanadada akiwa nyuma ya pikipiki, aliendelea kuwasiliana na watu wake, na nyuma yake kulikuwa na pikipiki nyingine mbili, kila moja ikiwa na watu watatu yaani dereva na watu wengine wawili nyuma ya dereva huyo, na mmoja wa watu hawo alikuwepo mwanasheria wa familia ya marehemu mume wangu.

Mwanasheria huyo baada ya kesi ya siku hiyo, alikuja moja kwa moja kwa wakili mwanadada, na kumkuta wakili huyo akiwa anaongea na simu, hakujali,au  kusubiri, au kusikiliza ni nini mwenzake anaongea kwenye simu, yeye moja kwa moja alianza kuongea kwa kusema;

‘Nasikia Mtalaamu katoweka,…nina hamu sana ya kumhoji huyu mtu uso kwa uso….’akasema na huku akiangalia upande ule walipokuwa wamekaa mashahidi , ambao wengine walishaanza kuondoka ili kusubiria hiyo siku ya kesho.

‘Na kwakweli baada ya kusikia kuwa yeye kahusika na kifo cha kaka yangu, akishirikiana na kiongozi wa kijiji, siwezi kukubali atoke hapa bila kushitakiwa, na ilibidi ashikiliwe moja kwa moja, …sasa mnaona eti katoroka, huyu alitakiwa kushitakiwa,  kama alivyoshikiliwa kiongozi wa kijiji na wenzake….’akasema na safari hii akimgeukia wakili mwanadada na kumwangalia na kipindi hicho wakili mwanadada alikuwa kshikilia simu sikioni, akiwa kaangalia chini, akisikiliza jambo kwa makini.

Wakili mwanadada, akainua kichwa na kumwangalia mwanasheria huyo, akakunja sura na kuangalia pembeni huku akiwa bado kashikilia simu sikioni, na mwanasheria akawa bado anaendelea kuongea.

‘Wewe mtu atatorakaje mbele ya ulinzi wa watu wanaoaminika, …hii ni ajabu kabisa, na hili mimi sitalikubali…kama mna njama na yeye, ili eti awasaidie , ili eti aje asamehewe, mimi sitakubali …wale wote waliohusika ni lazima wawajibike…..’akasema huku akiendelea kumwangalia mwanadada.

Wakili mwanadada, akawa sasa haongei na ile simu, alikuwa akisiliza tu huyo aliyekuwa akimpigia simu anavyoongea na kuitikia neno moja moja, kama `mmmmmh’, `sawa,’ `kabisa’…`hakuna shida….’, na alipoona huyo mwanasheria anazidi kuongea na isingelikuwa rahisi kwake kusikilizana na huyo anayeongea naye kwenye simu, akasema;

‘Samahani kidogo tutaongea baadaye kidogo, kuna mtu hapa, baadaye…..’akakata simu na kumgeukia mwanasheria huyo, wakawa wanaangaliana uso kwa uso na mwanadada akauliza;

‘Vipi kuna tatizo?’ akauliza wakili mwanadada.

‘Eti kuna tatizo,…!?, wewe huoni kuwa hili ni tatizo,kwangu mimi sawa ninaweza kusema hakuna tatizo, ndio maana  nimekuja kwenu ili kuongeza nguvu kwa upande wenu…..kwa maana kama watu kama hawa wanatoweka kiajabu, mnafikiria haki kweli itatendeka’akasema.

‘Hatujasema kuwa tunahitajia nguvu mpya, tena zaidi kutoka kwa wapinzani…halafu ni nani kakumabia kuwa mtaalamu katoweka, na ukumbuke yule kaitwa kama shahidi, na yupo tayari kuwepo kama akihitajika, kuondoka kwake, sio maana katoweka moja kwa moja…’akasema mwanadada akimwangalia mwanasheria huyu, ambaye alionekana kukonda, …na kutokuwa na raha.

‘Una uhakika na hilo unalolisema , au unajipa tumaini….wewe unamfahamu vyema huyo mtu,…na unakumbuka alisema nini wakati anatoa ushahidi, kuwa huenda ikawa ndio mara ya mwisho kuonekana…’akasema mwanasheria na kumfanya wakaili mwanadada azidi kumwangalia kwa mashaka.

‘Kwahiyo unasemaje?’ akauliza wakili mwanadada, akiwa bado bado anamtizama moja kwa moja huyo mwanasheria machoni.

‘Mwanadada, nakuomba sana unielewe, kesi hii imenifungua masikio, na …kiukweli, sikujua kuwa nipo kwenye kichaka cha mbwa mwitu….na nilipogundua hilo, nisingeliweza kutoka tu, bila ya kuwa nauhakika wa njia ya kutokea,….ilibidi nitafiti njia ipi bora ya kutoka hapo kichakani, na pia angalau nitoke na kitoweo….’akasema kwa mafumbo mafumbo.

‘Kwahiyo unasemaje?’ akauliza mwanadada huku akiangalia saa, alijua hana muda wa kupoteza, kwa vile wameshamuahidi muheshimiwa hakimu, kuwa kila kitu kitakamilika leo hii hii, na kesho kesi inaendelea kama kawaida, sasa mtu muhimu aliyemtegemea kwa ajili ya kusaidia kukamilika kwa uchunguzi wa baadhi ya vielelezo ndio huyo hayupo.

‘Nataka huyo mtu akamatwe kama alivyokamatwa mwenzake….’akasema mwanasheria.

‘Haya mkamate…..’akasema mwanadada kwa sauti ya kejeli.

‘Sikiliza mwanadada, usinione kuwa nasema haya kwa kukupotezea muda, kama uliniona ndani ya mahakama, nilikuwa naingia na kutoka…nilikuwa nafuatilia mambo haya kwa karibu sana kuna jambo nimeligundua, nitakuja kukuelezea baadaye, ….baada ya kusikiliza ushahidi wa huyo mtaalamu nimegundua mengi, na bado nafuatilia…huyo mtu kweli katoka, lakini kuna watu wangu wanamfuatilia kwa karibu….hawezi kutupotea hii leo’akasema na hapo mwanadada akaingiwa na hamu ya kumsikiliza.

‘Kwanini mnamfuatilia shahidi wetu, anawahusu nini?’ akauliza.

‘Siamini maneno yake kuwa katekwa na mizimu…..’akasema na wakili mwanadada,akakunja uso kwa mshangao.

‘Ehe, kwa vipi?’ akauliza mwanadada sasa akiwa katulia kumsikiliza, aliona huenda jamaa huyo ana mambo ambayo yatamrahisishia kazi yake, japokuwa bado alikuwa hamuamini.

‘Huyu mtu ni mjanja sana….wewe huoni kwanza kaamua kuwasaliti wenzake, kiujanja-ujanja, ili aonekane yeye ni mtu safi, …kweli mtu huyu anastahili kuitwa mtu msafi….na eti yupo na mizimu inamlinda na ili kuhakikisha anasema ukweli, na sasa katumia mbinu kuwapotea ili mumuamini, hayo yoye ni ujanja wake, …..nyie hamlioni hili, au kwa vile ni shahidi wenu, mnayachukulia mengine kirahisirahisi tu..?’ akauliza huku akiwa kashika kiuno

‘Mhh, sasa unayaona haya, tulipokuwa tunakushauri uliziba masikio,na hata hivyo una gani na hayo unayoyasema au ni hasira za kutaka kulipiza kisasi…kwa vile kasema yeye ndiye aliyetoa maelekezo ya kutengenezwa sumu, ambayo ndiyo iliyomuua kaka yako?’ akauliza wakili mwanadada

‘Kama ningelichukulia hasira na kutaka kulipiza kisasi, ningelishachukua hatua mbaya zaidi, hebu fikiria, unasikia kuwa watu wamehusika kumuua ndugu yako, halafu wapo nje, unafiria utafanya nini…?’ akauliza.

‘Sasa sema tufanyeje, au umenijia kwa shauri gani, maana muda unakwenda mbio….’akasema wakili mwanadada.

‘Hapo sasa tupo pamoja, cha muhimu kwanza ni kuhakikisha kuwa huyu mtu anakamatwa, tukamtafute huyu mtu awepo rumande, nahisi atakuwa yupo mahali kajificha…’akasema

‘Kajificha wapi…na kwanini ajifiche?’ akauliza mwanadada kwa mshangao, halafu akasema

‘Sijui ni nani kakuambia,lakini ni kweli wanadai kuwa katoweka kiajabu ajabu….haijulikani wapi alipo na sikuweza kupata muda wa kuongea na yeye kuwa bado anahitajika’akaambiwa.

‘Mimi kama nilivyokuambia kuwa nina watu wangu, …watamfuatilia huyo mtu kwa karibu watampata tu..nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu tu, na ndani ya hawo watu wangu kuna mtu ambaye anafahamu mambo hayo ya mizimu ni mkali, na anayajua haswa, japokuwa siyaamini …, yeye kadai kuwa anaweza kutambua wapi alipokwenda….’akasema.

‘Sawa basi tusipoteze muda, lakini nakuonya, kama ni moja ya mbinu zenu, utakuja kuumbuka mwenyewe…sikutishii, ila ninakuambia, ….’akasema mwanadada, huku akitaka kupiga simu, na mwanasheria huyu akasema.

‘Niamini mwanadada,…kuanzia sasa tupo pamoja, nitahakikisha sheria inafuata mkondo wake, nimechoka na haya mambo, nahitaji mambo haya yaishe tuweze kuendelea na maisha mengine, na nimechoka na haya mambo ya kijiji chetu,….kinahitaji mageuzi, uchafu huu uondoke, ili tukiendeleze kijiji chetu,…mbona mambo haya ni kale, hayastahili kuwepo kwenye dunia hii ya sasa…’akasema huku akikunja uso, na mwanadada akawa anafauta namba kwenye simu yake na mwanasheria huyo akaendeela kusema.

‘Na hilo halitafanikiwa kama tukiwakumbatia watu kama hawo…watu wa namna hiyo wote,wasafaishwe, waonywe, wafungwe, wakitoka watakuwa wamejifunza jinsi gani ya kuishi na watu wengine kistaarabu, na sio kiujanja ujanja…’akasema huku akionyesha kidole kule walipokuwa wamesimama kambi ya utetezi.

‘Haya twendeni…lakini tunahitajika kujiandaa, …una silaha,?’  mwanadada akamuuliza huyo mwanasheria na huyo mwanasheria akatabsamu na kusema.

‘Sina silaha, unanitega nini, lakini watu wangu waliopo huko wanazo silaha, usiwe na shaka na mimi,…nisingeliweza kuja hapa mahakamani na silaha…’akasema mwanasheria huyo akionyesha hasira usoni.

‘Lakini ..ujue bado hatupo pamoja,wewe una kambi yako ….tunachohitajia ni wewe kutuonyesha huko alipoelekea huyo mtaalmu, na wewe ukae pembeni kabisa…usije ukajiingiza katika maswala yasiyokuhusu ukatuharibia utaratibu wetu…’akasema mwanadada na mwanasheria huyo akacheka na kusema.

‘Hauna haja ya kuniambia hilo, wewe mwenyewe utakuja kuniomba nisaidie,…mwenyewe utaona, wewe hujawahi kuuingia huo msitu….’akasema huyo mwanasheria.

‘Wewe uliwahi kuuingia huo msitu, kwani kuna nini cha kutisha, wanyama wakali, au kuna nini…?’ akauliza mwanadada akiwa na mashaka.

‘Mimi ni mzaliwa wa huku,…na nimewahi kufanya matembezi ndani ya huo msitu, hadi kwenye hayo mapango ya watu wa kale, …’akasema na kutulia, wakati simu ya mwanadada ilipolia, na mwanadada huyo akaipokea na kusikiliza, akasema;

‘Tunakuja,….hakikisha wote wamekamilika, na wasifanye lolote mpaka tufike…wasije waharibu bado tunamuhitaji huyo mtu …..’akasema huyo mwanadada na kabla hajaendelea kuongea mara mara akaja jamaa mmoja,akiwa kashikilia usinge, ni aina ya fimbo, lakini imefunikwa na ngozi ya mkia wa mnyama, na alikuwa akiizungusha zungusha hewani, na mwanasheria akasema;

‘Huyu ndiye mtu atakayetusaidia kufika huko, ni mtaalamu wa mambo ya mizumu…na mashetani’akasema na wakili mwanadada akamwangalia huyo mtu kwa mashaka, na hakutaka kusema kitu, maana macho ya yule mtu yalikuwa yanatisha, na shingo yake ilikuwa imekakamaa utafikiri anainua kitu kizito. Na uso wake ulikuwa umekunjamana kama mzee, alikuwa anatisha.

‘Sawa twendeni, ..lakini hatukuwa tunahitajia watu wengi ambao wanaweza kuharibu mpangilio wetu, nia na lengo letu ni kumpata huyo mtaalamu ili atusaidia katika kuviangalai hivyo vielelezo, na si vinginenvyo…huyo sio mhalafu, hatuna kibali hicho….’akasema mwanadada. Na yule mtu akacheka na kukatiza mara moja, kama vile kaambiwa nyamaza, akasema.

‘Sivyo hivyo unavyofikiria mwanadada, ndio jina lako kama sikosei, eheee, mimi nimeona mbali, kuna tatizo, ….lakini siwezi kulisema hilo tatizo hapa, mpaka hapo utakaposhuhudia mwenyewe…maana nyie watu mnahitajia ushahidi wa kuone, lakini ukumbuke kuna mengine hayawezi kuonekana kirahisi, bila ya msaada wetu….’akasema huyo mtu.

‘Tusipoteze muda, twendeni…’akasema mwanadada na kutaka kupanda pikipiki na nyuma yake alikuwa kijana mmoja shababi, alikuwa na silaha, akionyesha kuwa ni mwanausalama, huyu ni mlinzi wake, anayemuamini sana.

Yule mtu aliyeletwa na mwanasheria akamsogelea mwanadada, na huyo mlinzi akamwangalia kwa makini, ….na mwanadada naye akawa kama anashangaa kwanini huyo mtu anamsogogelea na huyo mtu akasema;

‘Huko tunapokwenda kunahitajia ujuzi wa ziada, ni vyema wote nikawapaka mafuta maalumu ya kuondoa harufu zetu za kibinadamu,..vinginevyo tukifika huko hatutaona kitu , au tutapoteana au lolote baya linaweza kutokea,….silaha zenu, hazitasaidia kitu, kama wenyewe wakigundua kuwa mpo huko kwa nia fulani…..mtajikuta wote mumelala, na mkizindukana mnaweza kujikuta wote mpo uchi, huku mumefungwa kama wafungwa….’akasema

Kabla mwanadada hajasema kitu, huyo mtu, akaanza kuwapaka mafuta, na alipomaliza zoezi hilo, akasema ;

‘Haya tunaweza kuondoka…lakini kila mmoja amuombe mungu wake kwa imani yake,maana huko tuendapo sivyo kama mnavyofikiria, mnakwenda vitani, na mnakwenda kupigana na watu wasioonekana….’akasema huyo mtu .

‘Tusianze kutishana hapa, kama mnaogopa kaeni,sisi tunajua ni nini tunakwenda kufanya, hatuna nia mbaya na lengo letu ni kuongea na shahidi wetu…mnanielewa…’akasema wakili mwanadada na kukaa vyema kwenye pikipiki yake akamgeukiwa mlinzi wake, kumuashiria kuwa yeye yupo tayari.

‘Tunaweza kuondoka….’akasema huyo mlinzi baada ya kuangalia saa yake na kuangalia huku na kule,

Msafara ukaanza.

**************

Wakati wanaelekea huko akili ya mwanadada ikawa inaunganisha matukio haya na yale aliyoyasikia ndani ya mahakama, akawa anajaribu kumuwaza huyo anayeitwa mtaalamu, japokuwa ni shahidi yake, lakini akili yake ilikuwa haikubali kumwamini moja kwa moja.

Na kabla hajamaliza kumuwazia huyo mtalaamu, mara akili yake ikakumbuja jambo, ikamkumbuka binti ya mkuu wa kitengo cha upelelezo kwenye kituo hicho cha usalama,Akakumbuka siku aliyomtembelea binti huyo, na akakumbuka maongezoi yao, na tukio la ajabu lililotokea siku hiyo.

Nia na lengo lake lilikuwa kutaka kujua, jinsi gani ilivyotokea  kwa huyo binti, ilikuwa katika kuhangaika hangaika kutafuta ushahidi, na akaona labda huyo binti anaweza kuwa na lolote, basi katika kuongea na binti huyo, akataka kujua jinsi ilivyotokea hadi binti huyo kutoweka hapo nyumbani.

Yule binti alionyesha kuogopa, alipoulizwa swali hilo na hapo mwanadada akahisi kuna jambo huyo binti analificha, na huenda analificha kwa kumuogopa baba yake.

‘Naomba uniambie ukweli, maana kama una jambo linakuogopesha au kukupa mawazo, au kukuumiza, njia rahisi ni kulitoa moyoni, na  ni bora ukamtafuta mtu unayemuamini ukajaribu kumwambia ili akupe ushauri, nakuona una jambo, ….niamini mimi, nina uhakika nikilisikia ninaweza kukusaidia…niaini, au huaniamini mimi?’akamuuliza

‘A-a-ah…sina tatizo ila tu nikisikia mambo ya huko,….ya tukio hilo nahisi kuogopa…mimi nakuamini kweli nimesikia sifa zako, unasaidia sana watu,….hata hivyo, mimi sina tatizo’akasema huyu binti akikwepa kumwangalia huyo mwanadada machoni.

‘Kwanini uogope, na wewe ulisema kuwa hujui ulipopelekwa na hujui kulitokea nini?’ akaulizwa.

‘Ndio hivyo, ndio maana naogopa,isije ikatokea tena….’akasema huyo binti na wakili mwanadada, akamwangalia huyo binti, na kuhisi kuna jambo.

‘Mimi ni mwanamke mwenzako, japokuwa ni mkubwa kuliko wewe, lakini ninaweza kukusaidia, je ulifanyiwa kitendo chochote kibaya?’ akaulizwa, na huyo binti akaguna na kusema

‘Nitajuaje na mimi nilikuwa sijijui…’akasema na kuangalia pembeni

‘Je uliporudishwa, baba yako alikupeleka kupimwa, kuhakikisha kuwa hakuna lolote baya ulilowahi kutendewa?’ akaulizwa na huyo binti, akaangalai chini, na alipoinua kichwa, machoni kulikuwa na dalili ya machozi.

‘Nakuomba usiendelee kuniuliza hayo …natamani nife, nikiyawaza hayo…tafadhali, usije….oh’akasema na hapo wakili mwanadada, akamsogelea na kumkumbatia na yule binti, akamshikilia mwanadada kwa nguvu, kama vile anaogopa jambo..na hapo akili ya mwanadada ikahisi kuna jambo lilitokea kwa huyo binti, lakini hakupenda kumshurutisha kuliongea, akaona ampe muda.

Ni wakati mwanadada akiwa anataka kuondoka na yule binti akiwa anamfuatilia kwa nyuma kama anamsindikiza, mara yule binti akadondoka, na kuanza kutikisika na akawa kama mtu aliyepagawa, na mwanadada, akawa anahangaika kumsaidia, na mara yule binti akaanza kuongea sauti ya mwanaume;

‘Ehe…umesahau eeh, nilikuambia nini…wewe sasa ni mke wangu, sitaki ukiuka masharti…’ile sauti ya kidume dume ikasema. Na mwanadada akawa anashindwa asema nini, lakini wazo likamjia, na akakumbuka hadithi za watu waliopandwa na mshetani kuwa unaweza ukawauliza, na wakakuambia jambo.

‘Je ulimwambia nini mke wako?’ akauliza mwanadada kwa mashaka maana hakujua anavyofanya ndivyo au sivyo.

‘Muulize mwenyewe,…alipokuja kwangu na kutambulishwa kwangu, alikubali kuwa mimi ni mume wake, na tukaozeshwa, na ghafla akanikimbia….na nilimwambai sitamuacha..kamwe….na hakutakiwa kuongea siri ya mume wake..’ila sauti ikasema.

‘Lakini huyu bado mdogo, ataolewaje…?’ akauliza mwanadada.

‘Hahahaha…huyu bado mdogo!?, wewe wasema hivyo, …alipokuja kwangu, alikuwa keshajua mambo ya kikubwa,…nyie wanadamu mnajifanya na siri kubwa, huyo sio mtoto, alishajua tayari mambo ya kikubwa….alikuwa na mtu wake wanadanganyana, wanakutana naye mara kwa mara, wakijifanya wanasoma,..kwahiyo huyo sio mtoto kama unavyofikiria wewe, na mimi nikaona ili kumuokoa ni bora tu ni muoe….sijafanya makosa, …’ile sauti ikasema.

‘Huyo kijana anayesoma naye yupo wapi?’ akauliza mwanadada, akitaka kuhakikisha

‘Huyo kijana, keshahama hapa, baada ya kupata vitisho kutoka kwangu, lakini jana alikuwepo hapa, eti kaja kusalimia,anadanganya kaja kwa ajili ya mke wangu, na huyu mke wangu akaanza kumsimulia mambo yangu, nimekasirika sana, na huyo kijana nimempa adhabu kali sana, hatanisahau na hataweza kuongea na binti huyu tena..na kuokoka kwake ni kwa huyu mke wangu kunrejea, na akichelewa baada ya siku mbili atakufa…’ila sauti ikasema.

‘Je sasa wewe unaishi wapi?’ akauliza mwanadada.

‘Nyumbani kwangu ni mapangoni, nyumba ya mizimu, ambapo ndipo tulifunga ndoa na huyu binti, kama huyu binti angetulia, angekula raha zote za dunia , lakini akawa mjanja, eti anajifanya mtu wa dini, …nimempa siku tatu tu, kunirejea  akiwa hai, ….asipofanya hivyo, atarejea kwangu akiwa mfu,..na hapo atakuwa wangu wa kudumu…’ile sauti ikasema, na mara huyo binti akatulia kimiya.

Baadaye huyo binti alizindukana, na akawa kama anashangaa, na kuuliza

‘Nipo wapi hapa…kwani kumetokea nini?’ akamuuliza mwanadada

‘Upo nyumbani kwenu, kwani vipi?’ mwanadada akamuuliza.

‘Naona kama nilikuwa mapangoni..kwenye nyumba nzuri…..kuna kila aina ya vitu vizuri na nikaambiwa nichague moja, niishi huko, na rafiki yangu apone, au nikatae rafiki yangu afe, na mimi nitakwenda kuishi huko, nikiwa maiti..nikaogopa kujibu, …na ndipo nikazindukana…’akasema.

‘We binti hebu niambie ukweli, ulipokuwa huko mapangoni kilitokea nini na huyo rafiki yako ni nani?’ akamuuliza na huyo binti akawa kama kashituka na kuuliza

‘Eti nini mapangoni…nani kakumbia nilikuwa mapangoni…..’na akageuka na kukimbilia ndani, na mwanadada hakuweza kumuona tena, na huyo binti hakutaka kuongea na yeye tena, hata alipojaribu kumbembeleza,basi akaondoka kwenda kuulizia nyumbani kwa huyo kijana anayesoma naye

Alipofika nyumbani kwa huyo kijana, aliwakuta watu wakiwa na majonzi,na alipoulizia kuhusu huyo kijana akaambiwa huyo kijana kapatwa na matatizo, alianguka ghafala, na kuanza kupatatapa, na amekuwa kama kapagawa, ..

‘Ni kama mashetani, lakini sio ya kawaida…’akasema ndugu wa karibu wa huyo kijana

‘Sasa yupo wapi?’ akauliza mwanadada.

‘Imebidi asafirishwe haraka, maana ikipita siku mbili anaweza kupotea moja kwa moja…’jamaa huyo akasema.

‘Kwanini?’ akauliza

‘Hatujui, wanajua wazazi wake…ni mambo ya mapepo, na wasipohangaika, wanaweza kumkosa kijana, huenda kaingilia nyumba za watu….’akasema huyo jamaa na mwanadada akamwangalia kwa mashaka, na kujiuliza kajuaje yote hayo.

‘Kwao ni wapi?’ akauliza

‘Kwani wewe ni nani na kwanini uanmuulizia ….ooh, nimekukumbuka wewe ni wakili mwanadada, …achana na mambo hayo, hayatakusaidia kwenye kesi yenu’akasema.

‘Kwanini unasema hivyo hivyo?’ akamuuliza.

‘Nimekuona tu,….huko unapokwenda ni kubaya, chunga sana….’akasema huyo mtu na kuondoka.
Mwanadada hakuweza kupata taarifa zaidi, za huyo kijana au huyo binti, na alitaka ajue ni nini hatima ya hayo yote.

‘Tumeshafika msituni, sasa mnifuate mimi…tuache hizi pikipiki hapa….’yule mtu wa mwanasheria akasema na zile pikipiki zikawekwa na mmoja akachagulia kuzilinda…

‘Haya twendeni…..’safari ya miguu ikaanza, na kabla hawajafika mbali, kukaanza kusikika kitu kama upepo, ukivuma kwa kasi kuelekea hapo walipokuwa na ukawa unafika na kupotea , unafika na kupotea, na yule mtu akawa anachezesha ile fimbo yake, kama kuufukuza….

NB: Dunia hii ina mambo

WAZO LA LEO: Kuna ammbo mengi sana ya ajabu yapo hapa duniani, na mengi yanasababishwa na sisi wanadamu, kuna wanadamu wanaamini mambo yasiyotufaa, ya viumbe vingine, vyenye maisha yao, na hatukuwa na mamlaka navyo, na hata kujiingiza kwenye mambo ambayo mwisho wa siku yanakuja kuwaathiri, na sio kuwaathiri wao tu, na watu wengine wasiohusika,….

Kwanini tujiingize kwenye mambo hayo, kwanini tujiingize kwenye matatizo, wakati maisha yetu yenyewe ni ya matatizo matupu, …ni kwasababu ya kutafuta utajiri, kutafuta umaarufu au ni kwasababu gani, kwanini tusifanya mambo ya ugunduzi wa kisayansi, yenye tija kwetu….jamani wangapi walifanya hivyo na sasa hawapo hapa duniani, utajiri, mali, watoto, vyote hivyo havikuwasaidia kitu, tukumbuke kuwa vyote hivyo ni mitihani, vilikuwepo, vipo, na utaviacha,…cha muhimu, ni kuwa mtu mwema tenda mema , kwani kamwe wema hauozi.Ni mimi: emu-three

No comments :