Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 13, 2013

WEMA HAUOZI-48


Mlango wa mashahidi ulipofunguliwa  akaingia shahidi mwingine akiwa kafunga bandeji kubwa  upande wa mkono wa kushoto, toka begani  hadi ubavuni, japokuwa alikuwa kavaa koti, lakini koti hiloo lilikuwa kama limeegeshwa tu, nafikiri alikuwa na kaliegesha hilo koti hivyo makusudi, ili ionekane ile sehemu aliyopigwa risasi, …alitembea polepole huku  mkono wa kulia umeshikilia mkono ule wa sehemu yenye jeraha, akasogea hadi sehemu ya kuapishwa na baada ya kukamila zoezi hilo akasogea sehemu aliyotakiwa kukaa.

Mwanadada alitulia akisubiri amri ya kuanza, na hakimu alikasema mwanadada anaweza kuendelea na shahidi wake…mwanadada akainama kidogo kama kutoa heshima na kumsogelea shahidi wake huku akitabasamu kumpa faraja huyo shahidi aone ni jambo la kawaida;

‘Hebu taumbie wewe ni nani na shughuli zako ni zipi, na jitahidi kusimamia kwenye kesi yetu, maana muda haututoshi,….’akasema wakili mwanadada, huku akigeuka kidogo kichwa kuangalia upande ule wa watetezi, na alimuona mshitakiwa mkuu, akiwa kama ndio katoka kwenye mshituko mwingine, na kwa muda huo alikuwa akijaribu kujiweka sawa, ..

Shahidi huyu alitaja jina lake halisi halafu akendelea kusema;

‘Mimi ni mlinzi na mtekelezaji wa maswala ya ujasusi ya kiongozi wetu wa kijiji,…..’akasema na mwanadada akawa kama anatabsamu, anageuka na kuwa kama anataka kutembea, lakini akiwa vile vile akauliza;

‘Hebu tufafanulie vyema, maana hivyo vyeo, ni vyeo vikubwa sana, tunavyovisikia kwenye vyombo va habari na hatukutazamia kuwa kwenye kijiji kama hicho kuna watu wenye vyeo kama hivyo’ akaambiwa.

‘Ni kweli, na hakuna anayejua cheo hicho zaidi ya watu wa kundi letu na sio watu wetu wote wanaonifahamu kwa cheo hicho, wao wananiona kama mlinzi tu wa mzee, na ndivyo wanavyojua kuwa kazi yangu kubwa ni usalama wa mzee wetu,…’akatulia kidogo na kabla mwanadada hajamuuliza swali akasema kwa haraka haraka.

‘Lakini hilo la usalama ilikuwa ni kwa mara chache sana,kama imetokea mzee kunihitajia , akiwa kwenye safari ambazo anahisi kunaweza kusiwe na usalama,….ila mimi nilikuwa na maalumu, hiyo ni kazi ya siri, kazi yangu hiyo ya siri, ndio inatokana na cheo hicho, cha ujasusi, huwa nilikuwa nikitumwa kwenda kufanya jambo, sehemu ambayo haiendeki ovyo….’akatulia kidogo.

‘Una maana gani kusema sehemu ambayo haiendeki ovyo na ni kazi gani hizi ulikuwa ukitumwa ?’ akaulizwa

‘Kwa mfano mimi ndiye niliyetumwa kwenda hospitalini, kumpelekea Jemedari juice yenye sumu, na hebu angalia ulinzi wake ulivyokuwa, ni nani angeliweza kupenya hadi kuingia humo ndani, …lakini mimi kwa uzoefu wangu niliweza kuingia humo ndani, na kumpa Jemedari juice hiyo, na yeye bila kujua kuwa kuna kitu ndani yake, akainywa….’akatulia.

‘Hebu tuambia ulipenya penya vipi, na wakati kulikuwa na ulinzi mkubwa kiasi hicho?’ akaulizwam na huyo jamaa akacheka kwa dharau.

‘Ule sio ulinzi wa kunifanya mimi nishindwe kuingia….niliingia wakijua kuwa mimi ni mmoja wa wakuu wa usalama, waliokuja kukagua, …na ukumbuke kuwa tuna mtu wetu ndani ya kituo ….hakuna aliyenitilia mashaka….’akasema

‘Ulipoingia ukampa juisi na yeye akapokea na kunywa, bila kukuuliza wewe ni nani na …nakumbuka alikuwa hataki kula?’ akaulizwa.

‘Kwa muda ule alishaanza kukubali kula, na mimi nilipofika nilimwambai kuwa kuna mtu kamletea kinywaji, na nimethibitisha kuwa hakina tatizo…..na yeye akanywa hata bila ya kuingiwa na wasiwasi….’akasema

‘Kwanini alikunywa bila kufikiria, au bila ya kuogopa?’akaulizwa.

‘Hata mimi nilishangaa, maana aliponiona tu….kwanza hakujua ni mimi, lakini nilipotoa kofia yangu, akanigundua akasema ;

‘Afadhali umefika, najua ni nini kusudio lako, hata mimi nilikuwa nasubiria iwe hivyo, maana nimechoka, ….ni bora nikapumzike, maana watu hawanielewi,….., ‘..akatulia na kuonekana kukerwa na maelezo hayo, au kujisikitia kwa kitendo hicho alichokifanya.

‘Kwakweli, nilitamani nimwambia kuwa asinywe, na tusingizie kuwa amekunywa, lakini wakati huo Jemedari alishaipokea ile juisi na kuanza kuinywa kwa fujo,na hapo sikutaka kumhoji zaidi nikachukua chupa ile kuondoka zangu…..’akasema

‘Uliondoka na chupa yako, hukuiacha hapoo hapo?’ akaulizwa

‘Niliondoka nayo…nisingeliweza kuiacha hapo, …najua vyema kazi yangu’akasema na wakili mwanadada, akawa kama anashangaa, halafu akauliza swali jingine;

‘Je uliwahi kutumwa kufanya hivyo kwa watu wangapi, katika kumbukumbu zako?’ akaulizwa

‘Aaah, sio wengi sana, kazi ya kupeleka juizi iliyochanganywa na sumu sio kazi yangu sana, hiyo ni kacha ndogo, angeliweza kuipeleka mtu yoyote tunayemwamini, lakini kwa hali kama ile, hakuna angelwieza kuingia kwa kujiamini, kama mimi…. ‘ akashika kichwa kama anawaza jambo, halafu akasema;

‘Hata hivyo mambo kama hayo yamekuja kutokea muda wa karibuni, kulikuwa hakuna tatizo kipindi cha nyuma, mambo yalikuwa yanakwenda bila matatizo, wengi walikuwa watiifu tu, lakini baada ya kuchomwa moto mama mkunga, ikaonekana kuna mgawanyiko ndani ya kundi, na hapo nikaanza kutumwatumwa kwenye mambo kama hayo, hasa kwa wale watu wakorofi waliojaribu kuwa wasalati….’akasema

‘Na ulitumwa kuwapa sumu,au kuwafanya nini ….?’ akaulizwa

‘Kuna njia nyingi za kuwanyamazisha watu wa namna hiyo, inategemea na mtu huyo yupoje, wengine hutumii hata nguvu, unatumia mkono mtupu, wengine inahitajia silaha, na wengine sumu….na wengine vitisho…..wengine kuteka nyara na kupelekwa kwenye mateso kidogo tu….ni mambo ya kitaalamu kidogo, siwezi kuyaelezea kwa maneno ….’akasema huku akiangalia bandeji alilokuwa kalifunga .

‘Nakuona umefungwa mkono, ulifanya nini mpaka ukafungwa hilo bandeji?’ akaulizwa

‘Ilifikia sehemu nikaona, hii kazi hainifai tena, …..unajua ubinadamu, upo, hata uwe mkatili kiasi gani, kuna muda unajishuku, unajiona kuwa sasa imezidi, ….unaogopa na kuogopa, na ndivyo ilivyonitokea mimi, nikawa najiuliza kwanini mimi nitumike kuwauwa watu, na wengine hawana hatia kabisa, wakati mwingine damu za watu zinaniandama, …silali mpaka nilewe sana, sasa maisha gani hayo, hata kama ninalipwa pesa nyingi kiasi gani, lakini sina raha…..nikaamua ni bora niachane na maisha hayo, …lakini uamuzi wangu huo ulikuwa ni wa siri, hakuna aliyefahamu….’akatulia kidogo.

‘Hata hivyo nilikuwa sijafahamu nifanyeje, maana kuacha kazi kweny ekundi hili ina maana nikubali kuuwawa…hasa kwa mtu kama mimi, ndio ningetoroka na kwenda mbali,….au nchi za nje, lakini niliona nikifanya hivyo, bado moyo, nafsi ya kibinadamu itakuwa ikinisuta kila siku,….sasa nifanyeje…’akatulia kidogo.

‘Mimi nikaona ni bora nifanye jambo la wema,….kwani niliwahi kumsikia mtu wa imani za dini , akisema ukifanya makosa, fanya wema, huenda wema huo ukafuta hayo madhambi yako, na kawaida wema huwa hauozi, …hata kama watakuja kuniuwa hawa watu, lakini angalai nitakuwa nimefanya wema mdogo katika maisha yangu…..’akatulia kidogo.

‘Niliazimia moyoni nikijua tendo hilo, litanipeleka ahera, na ilivyo, muuaji atakufa kwa kuuwawa, hilo nilikuwa siku zote nalijau, ….basi , nikasema kabla sijauliwa ni bora nitoe siri zote kwa watu wa usalama, …’hapo akabetua mdomo kama anatabasamu.

‘Hapo napo nikajikiuta kwenye kikwazo, niende kwa watu wa usalama wepi…..maana nijuavyo mimi, mkuu mwenyewe yupo kwenye kundi…..’akatuli  huku akicheka kwa dharau.

‘Jamani kuna mambo humu…..ni wa vile mnasema kuwa muda ni mdogo, ningewaambia mengi yaliyojificha, hasa kwenye kundi hilo, lakini kwa vile mumesema kuwa nahitajika kuongelea yale tu yanayohusiana na hii kesi basi nisipoteze muda…’akasema huku akiwa kainama chini, kama mtu anayetubu dhambi.

‘Ndio nikafikia uamuzi wa kumpigia simu Mwanadada, na ndio nikakuita wewe nikukabidhi ushahidi wote, …na huo ni cha mtoto,…maana nisingeliweza kubeba kila kitu, lakini huo unahusiana nah ii kesi, cha ajabu kabisa, ilikuwa siri yangu na wewe niliyekupigia simu, sasa sijui ilikuwaje,…na nilikuonya kuwa usimwambia mtu mwingine, maana nakifahamu kituo chetu….wengi wapo mikononi mwa baosi wao…..’akatulia kidogo.

‘Ohh, nahisi uliwapigia watu wa usalama ukiogoap kuwa labda mimi nilikuwa na dhamira mbaya, ukaharibu, na mengine unayafahamu kuwa nilipokuwa nakukabidhi huo ushahidi ndipo, wakanipiga risasi,…..’akasema huku akijiangalia

‘Kwa bahati nzuri risasi hiyo haikuniathiri ndani, nashukuru madakitari walinifanya upasuaji na sasa ninaendelea vyema….labda muda wa mimi kuhukumiwa ulikuwa bado, maana hapa najihisi ni mchafu…muuaji, japokuwa nilikuwa nafanya kama mtumwa…..anyway…, sasa nipo tayari kuelezea kila kitu, ..na ushahidi wote wa hii kesi nimeshakukabidhi….’akasema na wakili mwanadada akawageukiwa watu wa utetezi, na wakili wao, alikuwa bado akiteta na mteja wake, walionekana kuwa kuna kutokuelewana , kwani hawakuwa makini kusikiliza hicho anachoongea huyo shahidi.

‘Wakili mtetezi, mbona hampo makini na shahidi huyo, kuna tatizo gani……..?’ akuliza hakimu.

Wakili mtetesi akasema;

‘Samahani muheshimiwa  hakimu, mshitakiwa mzee, kiongozi wa kijiji, alikuwa akinikataza kumuhoji huyo shahidi, kwasababu zake, na mimi nimeona kama ananiingilia kazi yangu,lakini yeye bado anasisistiza kuwa anaomba kwanza aonane na ndugu yake, yaani mama mkunga, ili athibitishe kuwa ndio yeye kweli, na anahitaji kuongea na yeye kwani anahisi mengi yanayoongolewa hapo, anasingiziwa tu, na eti mimi siweki pingamizi,….

'Pili, anataka asimame mwenyewe kujitetea maana anaona kuwa mimi simtendei haki….kwahiyo...’akasema wakili wa utetezi na kabla hajamaliza, akaingia mwanasheria wa familia ya merehemu mume wangu, aliongea kidogo na mzee huyo na baadaye akamsogelea huyo wakili mtetezi, akamnong’oneza jambo, na huyu wakili akatikisa kichwa kukubali.

Na wakati huo hakimu, alikuwa akiandika jambo kwenye makabrsaha yake, na alipoinua kichwa aligeuka kumwangalia wakili mwanadada, na kuuliza;

‘Je mumemalizana na shahidi huyo?’ akauliza.

‘Niliona ni vyema niwapishe wenzangu wamuhoji shahidi huyu kwanza , kabla sijaendelea naye zaidi, na sioni kwanini wanang’ang’ania nimlete shahidi huyo mwingine, wakati huyu bado hajamaliza…’akasema wakili mwanadada.

‘Kwani wengine walikuwa wamemaliza, mfano  mama mkunga hatukupewa hata muda wa kumuuliza maswali, hakuwa amemaliza maelezo yake,….ilikuwa bado, imeonakena ni tabia yako kukatisha katisha mashahidi wako ili upate mwanya wa kutokuulizwa maswali kutoka kwa watetezi wa hii kesi, kwa namnahii haki haitatendeka vyme….’akasema wakili yule ambaye alionekana kuendelea na kazi yake baada ya kuongea na mwanasheria na mzee kukubali wakili huyo aendelee.

Muheshimwia hakimu, akamwangalia wakili huyo, na alionekana kukerwa na kauli yake hiyo, lakini hakusema neno, akamgeukia wakili mwanadada na kusema;

‘Naona bado una mashahidi wengi, je utamsimamisha lini shahidi wako ambaye mshitakiwa anahitajia kumuona?’ akaulizwa

‘Baada ya shahidi huyu, tukimalizana naye , tutamuita shahidi huyo wanayemuhitajia, nitamleta huyo mama, mbele yako muheshimiwa, na ushahidi wake, kuthibitisha haya yote yaliyotokea, na ataelezea jinsi gani ilivyotokea siku hiyo, ili muone unyana wa mshitakiwa mkuu na wenzake…’akasema wakili mwanadada  na wakili wa utetezi, akamgeukia mteja wake, wakawa wanateta kidogo, baadaye wakili huyo wa utetezi akageuka kumwangalia hakimu, na kusema;

‘Kwa shahidi huyo hatuna maswali naye kwa sasa kama alivyotaka mteja wangu, samahani sana muheshimiwa hakimu, kwani nilifikia hatua ya kusitisha azi yangu hii, lakini baada ya maongezi, imeonekana niendelee, lakini huenda huko mbele akaja wakili mwingine, ….samahani kwa usumbufu huu…’akainama kidogo na halafu akageuka kumwangalia wakili mwanadada, ambaye alikuwa akiwasubiri.

‘Kama hamna maswali naye, basi ngoja nimalizane na shahidi yangu huyu, kabla hatujamleta mama mkunga, kama muda utaruhusu….’akasema na hakimu,akaonekana kungalia saa na akawa anaandika jambo kwenye makabrsaha yake, halafu akasema;

‘Endeela na shahidi yako…’

‘Je katika kundi leni unapokea kazi kutoka kwa nani,?’ akaulizwa

‘Mara nyingi ni kutoka kwa kiongozi wetu wa kijiji….na mara chache kutoka kwa watu wengine’akasema

‘Watu wengine kama akina nani?’ akaulizwa

‘Viongozi wa kundi, yupo katibu, yupo, ….mtaalamu, hata hivyo sikuwa napokea kazi ovyo, kwani mimi ninapewa kazi iliyoshindikiana, na wakati mwingine ninaweza kupewa kazi, nikaona haina nguvu sana, …nakaamua kumtuma kijana wangu mwingine…..’akasema.

‘Kwahiyo kazi yako ilikuwa haiingialiani na majukumu ya jemedari?’ akaulizwa.

‘Hapana, jemedari ni kiongozi wa serikali, ya kijiji, mimi ni kiongozi, wa kundi la siri, ni vitu viwili tofauti…..’akasema.

‘Je kundi hilo unaloliita ni la siri lina mahali gani maalumu….yaani makao yenu yalikuwa ni wapi, au mlikuwa mkikutana nyumbani kwa mzee, kiongozi wa kijiji kama sehemu yenu maalumu?’ akaulizwa.

‘Hatukuwa na makao maalumu, ….kama kuna jambo tunaweza kuamua kukutana popote, hata mashambanii, maporini….ilimradi kusiwe na shuku yoyote….’akasema.

‘Je unahisi ni nani aliyekupiga hiyo risasi, maana watu wote unawafahamu ?’ akaulizwa.

‘Kwakeli hadi sasa nimeshindwa kumfahamu ni nani…..kwasababu hakuna anayefahamu ujio wangu kwako,…..labda ni watu wa usalama’akatulia kama anawaza.

‘Je katika kundi lenu ni nani mwenye shabaha, maana inaonekana kuwa risasi hiyo haikupigwa kwa karibu kama tulivyoona awali, uchunguzi uliofanyika tena kwa makini, umeonyesha kuwa risasi hiyo ilipigwa mbali kutoka jengo la pili, ….’akasema mwanadada na kumfanya huyo shahidi kushituka kidogo.

‘Ina maana nilipigwa risasi hiyo kutoka mbali, nilijua tu, ….lakini kwanini,ina maana watu wenu hawakuwa na utaalamu wa kugundua hilo,…nilijua tu,..nina utaalamu wa kujua nguvu ya risasi, hiyo ilikuja kutoka mbali, lakini sikuweza kuthibitisha pale mliposema kuwa mpigaji alipiga kwa kupitia dirishani,?’ akawa kama anasikitika au kulalamika.

‘Mwanzoni ilionekana hivyo, lakini uchunguzi uligundua tofauti, kwahiyo hilo dirisha huenda lilikatwa kimakosa kwa dhamira nyingine,au kama mbinu tu ya kuhadaa…..’akasema wakili mwanadada.

‘Sasa kwa vile unalifahamu vyema kundi lenu, kwa mtizamo huo, ….ni nani unayemfahamu anaweza kulenga shabaha, ndani ya kundi lenui …’hapo wakili wa utetezi akaweka pingamizi, lakini hakimu akasema swali hilo lijibiwe kwani muhimu sana kwenye kesi hiyo.

‘Ninayemfahamu sana, ni…mkuu wa kituo, wengine sina uhakika nao, maana hatujawahi kuwa na kazi kubwa ya namna hiyo ya kulenga shabaha kwa mbali….’akasema bila ya uhakika.

‘Ina maana viongozi wako wote hawajui shabaha, kiongozi wa kijiji, ndugu yake mtaalamu, na …..’aksema.

‘Kwakweli sina uhakika na hilo, haijawahi kutokea jambo kama hilo, japokuwa nafahamu kuwa wanajua kutumia silaha, …..’akasema huyo shahidi. Na wakili mwanadada akatoa vielelezo mbali mbali alivyokabidhiwa na huyo shahidi, na kila kimoja shahidi huyo alipewa nafasi ya kutoa maelezo yake, zikiwemo kanda mabli mbali za video, alizowahi kuzirekodi, kwa ajili ya ushahidi au kuwatishia watu….na ilikuwa ni ajabu kwa kambi ya utetezi, ambao walikuwa kimiya, wakiwa kama wasikilizaji tu

Wakili mwanadada alipotoa chupa mbili ambazo zilikuwa na mabaki kidogo ya kinywaji, alimgeukiwa shahidi na kumuuliza

‘Kati ya hizi chupa mbili ni ipi uliyoipeleka kwa Jemedari?’ akaulizwa.

‘Ni hiyo ya mkono wa kushoto….yenye kifuniko cheupe’akasema

‘Una uhakika gani , maana naona chupa zote zinafanana…?’ akauliza.

‘Kifuniko chake kilikuwa hakifungi vyema, nikabadilisha, …kama unavyoona vifuniko havifanani vyema…’akasema.

Wakili mwanadada akaziangalia zile chupa, na akataka kusema jambo, lakini akasita na kumsogelea msaidizi wake, akamnongoneza jambo, na huyu shahidi yake akaziangalai zile chupa na kutikisa kichwa, na hapo wakili mwanadada akasema;

‘Muheshimiwa hakimu, tumemalizana na shahidi huyu, lakini tulikuwa tunahitajia kufanya uchunguzi zaidi katika vielelezi hivi, tuna imani kuwa kuna jambo jingine limezuka, na huenda likatusaidia kuhakikisha kuwa haki inatendeka vyema…’akasema na hakimu akaonekana kushangaa na kuuliza.

‘Lakini mumeshawakilisha vielelezo hivyo kama ushaidi, kuna tatizo gani na ushahidi wenu huo, hamna uhakika nao?’ akauliza hakimu kwa sauti ya ukali.

‘Muheshimiwa hakimu, tutaelezea zaidi tukija kumsimamisha shahidi wetu aliyepita, ambaye ana utaalamu wa hizo sumu,…kwani inaonekana chupa, aliyopelekewa Jemedari, na huyu shahidi wetu, haikuwa na hiyo sumu, …na shahidi wetu anakiri kuwa aliondoka na chupa hiyo…lakini uchunguzi wetu ulikuta chupa ikiwa karibu na marehemu jemedari,…..’akatuliwa wakili mwanadada na hakimu akawa kama anawaza jambo.

‘Unataka kusema nini?’ akauliza hakimu, alipogeuka kuwaangalia watetezi, ambao hawakuwa makini na mazungumzo hayo.

‘Inaonekana kuna mchezo ulichezwa, inaonekena Jemedari hakufa na juisi aliyopelekewa na huyu shahidi, …atakuwa aliuwawa na sumu nyingine,….ina maana kuna mtu mwingine alikuja kuleta chupa yenye sumu, na alikuwa anafahamu kuwa huyu shahidi huenda hatafanya hilo alilotumwa, au alikuwa anajua kuwa juisi hiyo aliyopeleka huyu shahidi haikuwa na sumu….’akasema wakili mwanadada.

Hakimu akaangalia saa yake, na kusema;

‘Hakikisheni mnafanya uchunguzi wa kina kabla hamjaleta vielelezo vyenu, je kesho mnaweza mkawa mumekamlisha uchunguzi wenu huo?’ akaulizwa.

‘Muheshimiwa hakimu,….tuna uhakika na hilo….leo hii kila kitu kitakamila na kesho tutakuwa tayari na kielelezo hicho’akasema wakili mwanadada.

‘Sawa kesi yetu itaendelea kesho, tukianzia kwenye hivyo vielelezo na shaidi mama mkunga atasimama tena kukamilisha ushahidi wake, ….tunahitaji kesi hii iishe haraka iwezekanavyo maana inaleta hisia kubwa kwa raia, na hatupendi haki isitendeke kama wanavyodai watu…’akasema hakimu, na mawakili wote wakakubali na hakimu akasema;

‘Kesi imeahirishwa hadi kesho yake.....'akasema hakimu

Wakili mwanadada alipotoka hapo, akachukua simu yake na kuanza kuongea na vyanzo vyake vya haabari, huku akitembea kuelekea  kwenye chumba cha mashahidi, na alipofika aliwakuta watu kama wamesindia, na ni watu wote wakiwemo walinzi, akauliza kwa mshangao;

‘Mtaalamu yupo wapi?’ akauliza huku akiangalia huku na kule.

‘Ametoweka kiajabu…’akasema mlinzi ambaye alikuwa akipikicha macho na kupiga miayo

‘Kwa vipi ametoweka kijabu?’ akauliza mwanadada.

‘Hatuelewi, maana ilitokea kitu kama upepo, tukajikuta wote tumesinzia, na tulipofumbua macho , hatukumuoan tena….’akasema mmoja wa walinzi.

Wakili mwanadada akatoka nje, na kuanza kuwasiliana na vyanzo vyake vya habari na watu wa usalama wakawa wanahaha huku na kule kumtafuta huyo mtaalamu.

NB: Je kama mtaalamu katoweka, ni nani atathibitisha sumu hizo, je ni kweli hayo yanaweza kutokea….au wewe unahisi ni kisa cha kubuni tu. …kazi kwako, tuwe pamoja.

WAZO LA LEO: Tuchungeni sana uvumi usio na ushahidi, watu siku hizi wanaona ni jambo la kawaida tu kuongea, au kuandika, bila hata ya kuwa na ushahidi na hayo wanayoyaandika, ilimradi kasikia tu basi yeye anakuwa wakala wa propaganda potofu, ilimradi hayo anayoyaongea au kuyaandika yanakidhi haja zake…na anayaandika hayo kama taarifa ya kweli na sio hadithi ya kutunga.


Kwa kufanya hivyo, sio haki, tusihukumu kabla ya hukumu, tusiwazushie watu uwongo, kwa vile sio wenzetu, au sio ndugu, au sio mtu wa heshima,kwani kwa kutenda hivyo, tunakiuka miiko ya uandishi, tunakuwa tumetenda  dhuluma, na hii ni dhambi, na yatakayotokea baadaye ujue ni wewe uliyesababisha hivyo, na utawajibika kwa yote hayo,…napenda kuwaasa wenzangu na kujiasa mwenyewe, kuwa tuwe makini na `kalamu’….

Ni mimi: emu-three

No comments :