Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, August 6, 2013

WEMA HAUOZI-45Baada ya siku mbili, kesi ilitangazwa tena, na mshitakiwa mkuu, alikuwa amepata unafuu japokuwa dakitari alishauri kuwa mshitakiwa apate muda zaidi wa mapumziko, lakini kwa kauli ya mshitakiwa mwenyewe alisema hataki kusubiri, anataka kuhakikisha kesi hiyo aliyoiita ya kubambikiwa imekwisha

‘Nataka haki itendeke, nataka kumuona huyo anayejiita kuwa ni ndugu yangu…aonekane, na sio kujificha kwenye minguo, anaogopa nini’akasema.

‘Sisi tunahisi hataki kuonyesha jinsi gani alivyoungua….’akasema

‘Nyinyi mnasema tu, ule moto ulivyokuwa asingeliweza utoka mtu mle…..’akasema na wakili wake akamtizama huyo mzee, na kuuliza.

‘Ina maana wewe uliuona huo moto ulivyokuwa?’ akauliza.

‘Sijauona, lakini wewe mwenyewe kama uliwahi kuuona moto wa nyumba ulivyo, na ikizingatiwa nyumba ile ilikuwa ya mti na kuezekwa kwa makuti, huo moto utakuwa wa namna gani….?’ Akawa kama anauliza, na huyo wakili akatulia kwa muda, halafu akamuuliza mteja wake

‘Je kama kweli ni ndugu yako utasema nini?’ akaulizwa

‘Nitajua hapo nikithibitisha hilo, ..kwanza ni kuhakikisha kuwa kweli ni ndugu yangu…’akasema

‘Je utajuaje kuwa ni ndugu yako?’akaulizwa

‘Kama ni ndugu yangu nitamgundua kwa vile sote wawili tulikuwa na alama ya kuzaliwa zinazofanana ipo chini ya mkono wa kushoto, ….kama hii hapa’akasema akimuonyeshea huyo wakili wake alama nyeusi, iliyotuna, kama uvimbe, na wakili wake, akaitizama kwa muda, na baadaye akauliza.

‘Je wewe na ndugu yako mlikuwa vipi?akaulizwa

‘Mimi na ndugu yangu tulikuwa tunapendana sana,  unajua utotoni tena dada na kaka walivyo, …sikutarajia itatokea  tuje kutenganishwa kihivyo, lakini hayo ni ya zamani, na sisi kama watoto hatukuwa tunajua undani wa wazazi wetu kuwa hivyo, na mimi mwenyewe sikupenda kuyafutailia zaidi, lakini mimi nina mashaka kuwa huenda huyo asiwe huyo ndugu yangu, kama kweli yeye ni ndugu basi yaliyotokea ni bahati mbaya na mimi sikuwa na dhamira mbaya juu yake..’akasema.

‘Kwanini uwe na shaka kuw huyo sio ndugu yako?’ akauliza

‘Kwasababu hajawahi kuishi hapa, na kama aliwahi kuishi hapa kwanini asije kujitambulisha,…?’ akauliza

‘Je kama angelikuja kujitambulisha ungelimtambua?’ akaulizwa

‘Sijui…maana ni siku nyingi, hebu fikiria tulitengenishwa tukiwa na miaka minne, tuli[pisha kwa mwaka mmoja tu, …..sura zinabadilika, sura ya utoto sio sawa na ya sasa, sina uhakika sana na hilo….’akasema

‘Na ulikuwa na maana gani ya kusema hukuwa na dhamira mbaya juu yake na wakati wewe unashukuwa kuwa ndiye uliyeamrisha wale vijana wachome nyumba moto huku ukijua yeye yupo ndani….’akaambiwa.

‘Ni nani aliniona nikifanya hivyo…hebu tumia akili bwana, hilo hata mie ambaye sio hakimu, naweza kulipinga kwa hoja hiyo…usimezwe na hoja zao, ukiwasiliza hawo, utashindwa kunitetea,, tatizo nimegundua kitu…..’akatulia.

‘Umegundua nini?’ akauliza wakili wake akiangalia saa yake.

‘Nyie mnawasikiliza hawa wahuni…maana ni bora niwaite hivyo, wahuni, wao wamekaa na kubuni mambo yao, kwa vile wanaogopa kuumbuka, ….’akasema

‘Kuumbuka kwa vipi?’ akauliza wakili wake, akiwa anaonekana kukerwa na kitu fulani, lakini hakutaka kumkatisha mteja wake, akageuka kushoto na kulia, halafu akamgeukia mteja wake, ambaye alikuwa katulia, akimwangalai jinsi anavyogeuza kichwa kushoto na kulia.

‘Sikiliza wakili wangu hawa watu, wamemkosa aliyefanya hivyo, sasa ni lazima wafanye hivyo, na njia rahisi wakaona waninyoshee kidole mimi, kwa kunisingizia, eti kwa vile ni kiongozi wa kijiji….wewe hulioni hivyo, kuwa ukiwa kiongozi unakuwa jalala la matatizo yote ya watu,…wewe huoni hilo kuwa kama ni wakushukiwa basi angelikuwa ni huyo kiongozi wa kundi hilo la hawo vijana….huyo marehemu Jemedari, ndiye mshukiwa na angelikuwepo hai, angelithibitisha hayo,…..’akatulia akitikisa kichwa kicha kama kuthibitisha kuwa hayo aliyoongea ni ya kweli.

‘Sikiliza wakili wangu, cha muhimu, tena sana ukumbuke siku lilipotokea hilo tukio sikuwepo kabisa, nimekuaj kuhadithia ilivyokuwa, na walisema moto ulikuwa mkali sana, hakuna kiumbe angeliweza kupona, kama alikuwepo humo ndani,…..mimi siku hiyo sikuwepo, muulizeni hata mke wangu atathibitisha hilo…’akasema huku akiangalia pembeni.

‘Hiyo ni dhana ya kila mmoja wetu kwa sasa, ….kuwa wewe unahusika moja kwa moja na matukio hayo na ushahidi wa wenzetu una nguvu sana,…..cha muhimu ili kuwaweza kupinga ushahidi wao ni wewe kunitafuta ushahidi wa kuthibitisha kuwa kweli hukuwepo siku hiyo, mkeo hana nguvu sana za kisheria maana ni mkeo, inawezekana ulimpanga aseme hivyo, ….na pia hata kama hukumpanga, unaweza ukaaga kuwa unaondoka, lakini hukwenda huko ulipokusidia,….kwa kifupi hapo, nina maana kuwa mke wako peke yake hawezi kulithibitisha hilo, mpaka apatikane mtu mwingine ….je tunaweza kumpata huyo mtu mwingine?’ akaulizwa

‘Kwanini asipatikane, kuna njia nyingi tu, lakini kwa sasa kwa vile muda haupo, tunaweza kutumia pesa…tumia pesa, pesa sio tatizo, wewe weka yote kwenye madai yako, utalipwa na zaidi….’akasema na wakili wake, akatikisa kichwa.

‘Mzee, mimi ninachotaka ni ukweli….’akasema huyo wakili huku akiangalia saa yake, na huyo mzee naye akawa anamuangalia huyo wakili kwa mshangao.

‘Ina maana wewe huoni kuwa pesa inaweza kufanya lolote…?’ akauliza.

‘Mzee, kwanini kila jambo unakimbilia kutaja pesa, …sio kila jambo linahitajia pesa, nataka uniambie ukweli ulivyokuwa, ni nani atakayethibitisha kuwa kweli siku hiyo hukuwepo wakati hayo yanafanyika,….sio kutafuta mtu wa kumtengeneza, hapana nahitaji mtu ambaye ama kweli ulikuwa naye kwenye hiyo safari au alikuona wakati ukiondoka, na yeye awe na vithibitisho, je huyo mtu yupo au hayupo?’ akaulizwa

‘Wewe ni wakili wangu sio, na mimi ndiye ninayekulipa, kwahiyo huhitajiki, kuwa hakimu wangu, …kwa hivi sasa siwezi kumpata huyo mtu, maana wengi wamenigeuka,kwa hali kama hii utamwamini nani, na mimi nipo rumande, kama ningelikuwa nje, ningeliwapata wengi … huoni kuwa wengi kwasasa hawataki kusema ukweli, lakini nina uhakika ukiwapa kitu kidogo, watakubali kusem ukweli…hilo ndio wazo langu sikuwa na maana ya kumtengeneza mtu….eeh, wewe wakili bwana, ina maana huniamni tena’akasema na wakili wake, akatulia akiwaza jambo

‘Mzee, hebu niambie ukweli ulivyokuwa, nahisi unanificha jambo,na hali ilivyo kwasasa, hutakiwi kunificha jambo, sitaki nishitukiziwe na mambo, kama vile sijui,….kwahiyo una mawili, kuniambai ukweli ili niweze kujua jinsi ya kusaidia au ukae kimiya, mimi nitaiendesha jinsi nijuavyo mimi, lakini ….ujue kuwa itakula kwako?’ akamuuliza huku akimwangalia huyo mzee.

‘Hivi kweli huniamini wakili wangu, nimekutoa huko mbali, nikijua wewe ni mkali, jembe, la nguvu,….kama huniamini mimi basi sema nitafute wakili mwingine, nimeshakuona kuwa wewe hunifai, nimeona jinsi gani unavyowaachia hawo watu wanaongea tu, mpaka watu wanaamini kuwa kweli mimi ni mtu mbaya sana, hata pale ambapo ulihitajika kuweka pingamzi hufanyi hivyo, unakuwa kama mtu aliyepagawa, kwanini huyo mwanadada anakuzidi kiakili, yule ni mwanamke tu,…' akasema na kutulia kidogo, halafu akawa kama kakumbuka jambo, akasema

'Au wewe umeshampenda sana huyo dada nini....huyo ni mchumba wa mtu,....'akasema na huyo wakili akawa anatabasamu tu, na alipoona wakili wake hasemi kitu akaendelea kuongea kwa kusema

'Sasa amua moja, ufanye kazi yangu, ili ulipwe, au ujitoe nitafute mwingine, na nakuapia hutpati hata senti yangu moja, ukijitoa, na nitahakikisha kuwa uwakili wao hauna maana tena…’akasema akimkunjia uso huyo wakili, na huyo wakili akawa anatabasamu tu.

‘Usione kuwa nafanya utani, wewe…huwezi kumuachia huyo mwanadada kutamba, na kujiona kama yeye anaweza kutugaragaza , wanaume wazima tunashindwa na huyo mwanamke,  kwakweli umenidisapoiti sana…. 'akawa anatikisa kichwa kuashiria kusikitika.

'Na isingelikuwa kupata hiyo mishituko, nahisi  sasa hivi kesi ingelikuwa imekwisha na mimi nachezea kitanzi, na mimi sitakubali hilo…..’akatulia huku akishika mkono upande wake  wa kushoto, kuashiria maumivu.

Wakili wake akamwangalia huyo mzee kwa makini, na alipoona kuwa huyo mzee anaongea sana, na inaonyesha hatanii, kweli hali yake inaonyesha anapata maumivu makali akamuuliza.

‘Upo sawa kweli mzee, kama unaumwa useme, nikaiahirishe hii kesi…maana ikitokea tena hakimu anaweza akachukua maamuzi mengine, …..bado tuna safari ndefu, kama hujisikii vyema weka bayana, hiyo ni haki yako kisheria kama unaumwa, hulazimishwi kufika mahakamani, ninaweza kuongea hata jama haupo….,?’ akaumuuliza huku akimwangalia huyu mzee kwa mashaka.

‘Nipo sawa, ni maumivu ambayo huja na kuacha, yanauma upande huu wa kushoto, toka kidole cha gumba mguuni hadi kichwani..na vidole vinakuwa kama vimeumwa na nge….ni tatizo gani hili…naona linakuja kwa aksi kweli kweli…?’ akauliza na huyo wakili wake akasema

‘Huenda umepatwa na tatizo la Angina na dawa yake ni kuhakikisha unakwepa yale yatakayo kupeleka kuwaza sana, ….na kesi yenyewe hii inahitajika uwaze, hukutakiwa uwaze, ulitakiwa uniambie ukweli, ili mimi mawazo yako niyabebe mimi, …..mimi ndiye wakili wako, na nihitajai kujue ukweli, lakini nahisi kuwa unanificha mambo muhimu, na ukiyaficha ukabakia nayo moyoni, yatazidi kukuumiza, ni bora ukaniambai ili nijue jinsi gani ya kuyaweka sawa kisheria…’akasema

‘Kwahiyo unataka nikuambia ukweli ulivyokuwa…na utaweza kuyaweka mambo sawa sio ndio hivyo, mimi nakuaminia, na ni kweli, kama ninakulipa pesa nyingi, kwanini nisikuambie kila kitu, na pesa sio tatizo kwetu, ukifanikiwa kuyaweka haya mambo sawa, nitakupa pesa na eneo la shamba…hilo nakuahidi….hizo tulizokulipa ni cha mtoto…unanielewa lakini?’ akasema kwa kuuuliza.

‘Hiyo ndiyo kazi yangu uliyoniitia nije kuifanya, cha muhimu kwa sasa ni wewe uniambie ukweli ili nijue jinsi gani ya kuyaweka haya mambo sawa, swala la pesa na eneo hilo la shamba sio muhimu kwa sasa…..naomba unielewe hivyo mzee…’akasema huyo wakili wakawa wanaangaliana na huyo mzee, akainama chini na kusema

‘Nitakuambia na usikilize kwa makini, na ole wako ukinisaliti,….’akasema an yule wakili akachukua simu yake na kuanza kurekodi maneno ya huyo mzee

*************

‘Kooorti………’sauti ya kuashiria kuwa hakimu anaingia ilisikika, nakila mmoja akawa makini kusikiliza ni nini kinachotakiwa kuanza, kwani watu walishaanza kunongo’ona pale walipoona hakimu akichelewa kuingia, na hata kufikia kusema huenda kesi hiyo itaahirishwa tena,

‘Mnaona huyo mzee alivyo, ana nguvu za ajabu, anaweza akafanya kesi hii iharishwe hadi ije ifutwe…’akasema mtu mmoja.

‘Acha hizo imani wewe, imani kama hizo hazina maendelea kabisa,....hiyo kesi ipo, vinginevyo, tungelijua kuwa haipo, hawawezi kuwaweka watu hapa , halafu waje kusema kesi haipo…’akasem a mtu mwingine.

‘Kesi ilitakiwa ianze asubuhi na mapema, saa mbili na nusu, sasa ni saa nne, hebu jiulizeni kuna nini kinaendelea huko…..’akasema mtu mwingine.

‘Tuvuteni subira, mimi nina imani kuna jambo muhimu linatendeka, wasingelikaa kimiya bila kusema lolote…’akasema msemaji mwingine.

‘Haya ndio matatizo ya nchi yetu, hatujali muda, hatujali hisia za watu wengine, kwanini mmoja wao asiseme lolote, kuwa kuna tatizo gani, ili na sisi tuwe  na amani…’akalalamika mtu mwingine.

‘Mimi nina imani kuw hilo linalofanyika ni muhimu sana, ndio maana hata wao wamekaa kimiya…..’kabla hajamaliza, ndio sauti hiyo ya `kooortiii’, ikasikika.
Muheshimiwa hakim aliingia na taratibu za kimahakama zikafanyika, na hakimu alipotulia ikatajwa kesi hiyo, na hakimu akaanza kuongea;

‘Kuna mswala ya kisheria tulikuwa tukiyaweka sawa kuhusu kesi hii,…kama mnavyoona kesi hii imekuwa ya aina yake,..kwahiyo ilinibidi mimi nikutane na jopo la mahakimu wenzangu kuangalia baadhi ya mambo yaliyojitokeza, …kwahiyo msione kuwa nimechelewa kwa mambo mengine, hapana nilichelewa kwa mambo ya hii kesi….na sikuweza kutoka na kumwamba mtu aaje kuelezea ni nini kinaendelea, nikijua kuwa hicho kikao hakitachukua muda, lakini…tukajikuta tumetumia muda zaidi ya tulivyotajia…’akasema muheshimiwa hakimu

‘Sasa tuanze kesi yetu, na wakili mwanadada endelea na mashahidi wako,….’akasema hakimu, na wakili mwanadada akasogea mbele, na kusema;

‘Najua wengi wanahitaji tuendelee na shahidi wetu muhimu, ambaye alikuwa hajamalizia maelezo yake, lakini kwasababu zilizo nje ya uwezo wetu, shahidi huyo kapatwa na dharura, kama mjuavyo yule ni hakimu wa mahakama ya mwazo , na alikuja hapa kwasababu  h ii kesi, yetu, tunamtarajia kuwepo baadaye kwenye siku itakapotajwa …’akasema wakili mwanadada,

‘Hata hivyo hakijaharibika kitu, maana tuna mashidi wengi, na wote ni muhimu sana katika kesi yetu hii, na wanajua kila kitu kilichotokea kwenye kijiji hicho, kwahiyo kwasasa nitamuomba muongozaji wetu wa mashahidi amlete shahidi maalumu kwa leo….’akasema na kabla hajamaliza wakili mtetezi akaweka pingamizi.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, hii ni mara nyingine tunalalamika kuhusu tabia hii ya wenzetu, jinsi wenzetu wanavyofanya, …kila mara wanakuja na shihidi mpya, kabla haujamalizana na shahidi aliyetangulia, tukumbuke kuwa ilikuwa nafasi yetu sisi kama walalamikaji kumhoji huyo shahidi, …’akasema

‘Lakini umesiki kuwa shahidi huyo hayupo, na nilipokea taarifa hiyo, mkumbuke kuwa yule ni hakimu, wa mahakama ya mwanzo, ana ofisi yake huko alipohamishiwa, na alitarajia kuwa siku ile angelimaliza kila kitu, lakini kukatokea hilo lilotokea, hawezi kusubiria, wakati ofisi yake inamsubiria….’akasema hakimu

‘Sawa muheshimiwa hakimu, kwa huyo shahidi tunakubali ….hatuna pingamizi naye, tutakutana naye akija…,Je shahidi aliyetangulia kabla ya huyo, yeye ana sabau gani za kimsingi, ambazo zinamfanya asiweze kuwepo leo….tunamuhitajia afike amalizie sehemy yake, ili na sisi tuweze kumhoji,…na pia afika akiwa hajajifunika, ili tumuone vyema. Tutahakikishaje kuwa ndiye huyo mama mkunga…’akasema

‘Ina maana huiamini hii mahakama?’ akauliza hakimu

‘Sijasema siiamini mahakama hii, muheshimiwa hakimu, lakini ni haki yetu kudai kile tunachoona kinatufaa sisi kama watetezi…’akasema wakili huyo

‘Kwahiyo nyia mnataka nini hasa?’ akauliza hakimu

‘Tulikuwa tunataka asimamishwe shahidi huyo , yule aliyetambulikana kama mama mkunga, ili kwanza tuthibitishe wenyewe kuwa ndio yeye, na pili tuweze kumhoji’akasema na hakimu akamgeukia wakili mwanadada, na wakili mwanadada akasema;

‘Kwanini wenzetu mna wasiwasi, huyu shahidi yupo, lakini bado ana matatizo ya kiafya, hatuwezi kumsimamisha hapa kwa leo, kwa masaa mengi, ndio maana tunampa muda, ili aweze kuwa na afya njema na muda ukifika atakuwepo, na mtamuhoji vyovyote mpendavyo, na mtamuona kwa mapana…’akasema wakili mwanadada.

‘Kwahiyo bado anaumwa, kama bado anaumwa, mbona sijasikia muheshimiwa hakimua kisema kuwa kapokea taar?’ akauliza wakili mtetezi.

‘Bado yupo kwenye uangalizi wa dakitari, na yeye ndiye atakayemruhusu …lakini kwa leo dakitari kasema kuna vipimo, ambavyo alichukuliwa na majibu yake ni leo, baada ya hapo ndipo anaanza amtibabu stahiki,…na sikuhitajai kumwambia hakimu, kwa vile nilijua kuwa tunaendelea na shahidi mwingine, kutokuwepo kwake, leo,hakuzuii kesi yetu kuendelea…..’akasema wakili mwanadada.

‘Haya tusipoteze muda, waendesha mashitaka, tunahitajai shahidi wenu wa leo, na hatutavumilia malumbano yasiyo ya kisheria kwenye mahakama hii..’akasema hakimu na mara mlango wa kuingilia mashahidi ukafunguliwa…

Shidi aliyetokea, aliwafanya watu wote wainuke kwenye viti vyao,  hata hakimu aliyekuwa kashikilia rungu lake akitaka kuligonga kuashiria watu watulie, akajikuta akiwa kalishikilia hewani, na hata yeye alibakia mdomo wazi…

NB: Tengua kitandawili hiki ni nani shahidi huyu?


WAZO LA LEO: Tuweni makini sana tunapofanya makabidhiano au malipo iwe kwa pesa au kwa vitu. Ni vyema matendo hayo yawahusishe mashahidi, na maandishi ya kisheria, kuhesabiana nk. Kuna tabia ya watu wanapenda kukopeshana pesa bila mashahidi au maandishi, au kupeana pesa bila maandishi au mashahidi,au kuhesabu kile walichopewa au kulipwa, wakisema kuwa wanaaminiana, hiyo sio sahihi, kwani ubinadamu una mapunguzfu yake, kuna kusahau, na hujui hatima yako itakuwa lini, fanyeni kwa audilifu kwa kuhakiki, na kuandikishana mbele ya mashahidi.

Ni mimi: emu-three