Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 31, 2013

WEMA HAUOZI-43

Baada ya ile DvD ya mwanzo kumalizika, Mwanadada akageuka kumwangalia huyo mkuu wa kitengo cha upelelezi, na yule mkuu alikuwa bado yupo kwenye mshangao kwa yale alyoyaona kwenye DvD hiyo na badala ya kuongea yale aliyoyaona kwenye hiyo Dvd, huyo mkuu akawa anaongea jambo jingine kwa kusema;

‘Jana nilikuwa nakutafuta sana….’akasema huku akiitoa ile DVD kwenye laptop yake na kuhakikisha kaihifadhi vyema kwenye mfuko wa plastiki.

‘Ulikuwa unanitafutia nini, kwanini hukunipigia simu,…ndio nakumbuka  niliona ujumbe wa kwenye simu yangu,i lakini sikuwa  na uhakika ujumbe huo umetoka kwanani,…ila kwa sasa ndio nimegundua kuwa kweli ulitoka kwako, kwasababu namba iliyotumika ni ngeni kwangu, ni kwanini ukatuma huo ujumbe wa maneno kwenye namba ya simu isiyo ya kwako…. ?’

‘Sikujua kuwa sina salio kwenye simu yangu , kwani nilisha-andika huo ujumbe kwenye simu yangu, na nilipotuma nikagundua kuwa salio halitoshi, ndio nikaamua kuutuma huo ujumbe kwenye simu nyingine, …sikupenda kujiandika mimi ni nani, nikijua kuwa utaelewa kuwa ni mimi…’akasema huyo mkuu.

‘Kwa hali ilivyo sasa, inahitajika kuwa muangalifu, …..sikupenda kubahatisha, kwani kama ungelikuwa na umuhimu na mimi nailijua ungenipigia simu…’akasema mwanadada.

‘Ndio mimi niliyekutumia huo ujumbe,.. hiyo namba ni ya mke wangu, ambayo huwa haitumii mara kwa mara….nilikuwa nayo kwa muda ule’akasema huku akichukua ile DvD, nyingine, na akawa anaitoa kwa makini kwenye kasha lake.

‘Ulikuwa unanitafuta kwa jambo gani,….maana nakumbuka uliniambia nisiwe nakutana na wewe mara kwa mara, nina imani ulikuwa na jambo muhimu sana, japokuwa hukusisitizia…usilete ule utani wako…?’ akauliza mwanadada huku akitabasamu.

‘Hapana huo sio utani, hata hivyo, baadaye niliona hakuna umuhimu kwa hilo, kwani nilikuwa nimekutana na jambo jingine muhimu zaidi….’akasema huyo mkuu.

Mwanadada, akawa akawa anajaribu kuyachuja mambo kwenye akili yake, kama singelikuwa heshima kwa huyo mkuu, angemwambia atulia kwanza, kwani kuna kitu muhimu anataka kukiwaza,…lakini kwa heshima ya huyo mkuu, akaendelea kama atakavyo huyo mkuu.

‘Ni kuhusu hukumu ya kesi ya mwanadada…’akasema huyo mkuu wa askari kanzu na mwanadada ikabidi ayapuuze mawazo aliyokuwa nayo mwanzoni na kumgeukiwa huyo mkuu, na wakawa wanaangaliana, na huyo mkuu akageuka pembeni  kama vile hataki huyo mwanadada ajue hisia zake.

‘Kuna nini kuhusu kesi ya mwanadada,…kwani nijuavyo mimi, bado hukumu haijatolewa…. ?’ akauliza

‘Hukumu ilishapitishwa, …kama ujuavyo kuwa yule hakimu alishaisikiliza kilichokuwa kimebakia ni kutoa hukumu mbele ya mahakama, na kwa bahati mbaya, aliondoka kabla hajaitoa mahakamani…’akasema huyo mkuu.

‘Ndio lakini hiyo hukumu ni siri, mpaka itolewe mahakamani, sasa ilivujaje?’ akauliza mwanadada.

‘Kama ujuavyo huyu hakimu alihamishwa kwa haraka sana, kiasi kwamba hakupata muda, wa kukabidhiana na mwenzake, ….sasa sijui wakati anaondoka, ndipo mambo haya yalifanyika, au ni yeye mwenyewe alifanya hivyo, hapo nashindwa kuelewa maana namuamini sana yule hakimu, asingeliweza kufanya hivyo..’akasema huyo mkuu.

‘Sijakuelewa bado….’akasema mwanadada huku akiendelea kumwangali yule mkuu, ambaye alikuwa kaangalia pembeni.

‘Lakini hata hivyo, hakijaharibika kitu, maana huyu hakimu mpya kaona  aipitie hiyo kesi  upya, na mimi namuunga mkono kwa wazo hilo, ili kuondoa utata….’akasema.

‘Bado mimi sijakuelewa,…..’akalalamika mwanadada.

‘Unajua ilibidi hukumu hiyo ivuje, na hata mimi nisingeliweza kulifahamu hilo, lakini hakimu hiyo alituita upande wa usalama, na kuongea na sisi, …kwani alifanya hivyo,….. kumbe alishaisikia hii kesi wakati yupo huko alipokuwa, na yeye alikuwa na kesi kama hii, inafanana kwa kila kitu, unajua sasa hivi akina mama wameamuka kudai haki zao, na yeye aliweza kuhukumu vyema huko alipotoka,....’akatulia.

‘Nakusikiliza mkuu….’akasema wakili mwanadada, kwani hadi hapo alikuwa hajathibitisha ni nini hasa anachotaka kusema huyo mkuuna hakutaka kumuhoji kama mahakamani .

‘Alipofia hapa na kuliona hilo jalada la kesi hiyo, akashangaa …hakuamini, ikabidi akutane na wazee wa mahakama, na wahusika waliosimamia hiyo kesi…’akasema.

‘Wazee walikubali kuwa hiyi ndio hukumu halali,…ila kuna baadhi wakawa hawakubaliani, na hapo ikatia shaka,…na akaanza kufanya uchunguzi wa kwake binafsi, hakimu huyo sio mchezo, hakukubaliana na wazee, waliosema kuwa hukumu hiyo lipitishwa, kutokana na taratibu za mila na desturi…’akasema

‘Hakimu hakukubali, akaanza kufuatilia mwenyewe, ….na hapo akaanza kujenga chuki na baadhi ya wazee  ya mahakama hiyo,na baadhi ya wahusika  wengine kwenye ngazi za serikali kwenye kanda yetu hii,na hili limeshaanza kujitokeza wazi, kwani analalamika kuwa hapewi ushirikiano wa karibu, kitu ambacho anahisi kuwa kuna jamboo kubwa limejificha….’akasema

‘Mimi nimemshauri,….na wengi wameona hivyo, kuwa ili kuondoa fitina kesi hiyo isikilizwe upya…’akasema huyo mkuu.

‘Mkuu, samhani kidogo, kwani hukumu ilisemaje?’ akauliza Mwanadada, kwani ile DvD ilitaka kuanza, lakini akaisimamisha ili ikianza wawe wametuliza mawazo yao na kuona kilichopo. Mkuu huyu akatulia kwa muda kama anawaza jambo huku akiwa anaangalia ile laptop, kama vile anasubiri hiyo DvD ianze kucheza, na baadaye akamgeukia mwanadada, na kusema;

‘Pesa sio mchezo, nasema hivyo, kwasababu sioni kuwa kuna sababu nyingine ya kuweza kumbadili mtu, na kuiacha haki na ukweli kama sio pesa,labda kuna mambo yalitokea, lakini ….nilipopitia, na kuchunguza eneo hili, nimeona kuna mchezo mbaya unachezwa kwenye kanda yetu hii,…lakini hata hivyo,sio kwa yule hakimu, namfahamu sana, huenda kuna jambo kubwa zaidi ya hilo….’akasema huyo mkuu.

‘Hata kuhamishwa kwake, sio kwa kawaida….’akasema mwanada kusisitizia hilo.

‘Ndio hivyo…hata yeye mwenyewe alishangaa…’akasema huyo mkuu

‘Ina maana alishitukizwa…na je wakati anaondoka, uliwahi kumuuliza kuhusu hiyo hukumu?’ akauliza.

‘Mhh, hapana nisingeliweza kumuuliza kitu kama hicho, kwani najua sheria za kimahakama, hiyo ni siri, hadi hapo itakapotolewa mahakamani,…lakini ndio hivyo, yeye alipata barua usiku, na kesho yake anahitajika kwenda kwenye kitu kingine, eti kwasababu kuna kesi kubwa anahitajika akaisimamie…na huko ndio kutakuwa kituo chake cha kazi…’akasema mkuu huyo.

‘Sasa kama ni hivyo, huoni kuwa kama ni mchezo mchafu, utakuwa unawahusu wakubwa zaidi yake, labda na yeye awe anahusika….?’ Akauliza.

‘Nilipoangalia hii DvD, ….naona tunahitajika kuwa waangalifu sana,…na nakushauri, kukutana kwetu kuendelee kuwa kwa nadra, na usimwamini mtu yoyote kwa sasa…kuwa makini zaidi ya tulivyokuwa, na tujitahidi hi kesi ifanyike kwa haraka iwezekanavyo, kabla ushahidi haujapotea kabisa….’akasema.

‘Lakini hujaniambia hukumu hiyo ilikuwaje? Akauliza mwanadada, pale mkuu huyo alipoaka kuicheza ili Dvd, na mkuu huyu akatulia, na kuuondoa mkono wake, kwenye sehemu ya kuianzisha hiyo DvD.

‘Mwanamama, alishindwa kwenye hiyo kesi…’akasema huyo mkuu.

‘Eti nini, haiwezekani kabisa, …’akasema mwanadada, akimtolea macho huyo mkuu.

 ‘Hukumu aliyoikuta huyo hakimu, ilionyesha kuwa Mwanamama, alikuwa kashindwa kwenye hiyo kesi, na y a kuwa alitakiwa kukabidhi mali zote kwa wanafamilia, ….’akasema

‘Haiwezekani, …..haiji akilini hata kidogo, ina maana huyo hakimu ndivyo alivyohukumu hivyo, sizani kama yule hakimu ndio yeye aliyehukumu hivyo sizani…hapo  kweli kuna jambo…..’akasema mwanadada.

‘Sasa kama huamini, ….nenda kaumuulize mwenyewe huyo hakimu,…hata hivyo, huyo hakimu kasema ataipitia upya hiyo kesi, na ili kuondoa utata, anataka isikilizwe upya…na ndivyo hata sisi tulivyomshauri…’akasema

‘Isikilizwe upya kwasababu ipi..tuangalie na sheria, maana huwezi kusema kesi inasikilizwa upya, bila ya sababu za kimsingi…’akasema mwanadada.

‘Sababu ndio hizo…kwanza hakuna anayejua hukumu ilikuwaje,kwani haijasomwa mahakamani, haya tunayaongea kama uvumi….ujua hilo,…..’akasema huyu mkuu, akimwangalia mwanadada.

‘Na hata hivyo sababu zinaweza kutafutwa, hakishindikani kitu, na kwa vile sisi tunaona kuna umuhimu wa hilo, mimi naona bora iwe hivyo,,…hata mimi nilimshauri afanye hivyo, kwani kama ingelitolewa hukumu hiyo iliyokuwa imetolewa, sizani kama kungelikuwa na amani…na akiitoa yeye, unafikiri jamii itasemaje,…yeye ndiye kahukumu hivyo,sio mwenzake aliyeondoka…’akasema huyo mkuu wa upelelezi.

‘Kumbe ndio maana hawo jamaa walikuwa wakitamba…..lakini hapo najiuliza je hawa wenzetu walijuaje kuhusu hukumu hiyo, kuwa wameshinda, huoni kuwa kulikuwa na njama….aah,…’akasema wakili mwanadada akiwa kavunjika nguvu, na akaianzisha ile  DvD ya pili ianze kuonyesha

‘Mimi nitang’ang’ania nione hiyo hukumu ya mwanzo, na hapo ndipo nitakata rufaa kwenda mahakama ya juu, najua hapo haki itapatikana vyema, lakini kwanza tumalizane na hi kesi yetu inayotukabili…huenda ikasafisha kila kitu, na huenda hata kesi hiyo haitakuwa na msingi wa kuskilizwa upya,…lakini he hukumu halali ipo wapi, maana nahisi hiyo sio hukumu halali…?’ akawa kama anauliza mwanadada.

‘Mimi sioni haja ya kufanya hivyo….kuwa asome hukumu hiyo aliyoikuta halafu wewe ukate rufaa, cha muhimu, tumpe nafasi huyo hakimu mpya asafishe ofisi yake, mimi nina imani kuwa mahakama na utendaji wa eneo hili utabadilika, na wale wote wanaoiharibu mahakama hiyo na eneo hili kwa ujumla wataondolewa, mmoja baada ya mwingine….’akasema mkuu.

‘Mhh, ngoja tuona hii DvD kwanza, maana inaanza kwa mbwembwe, na kama vile inatuonyesha hili tunalolizungumzia…..samhani lakini mkuu’akasema mwanadada, na wote wakatulia kuiangalia…

**********

Mwanadada ambaye alichelewa kufika mahakamani, kama ilivyokuwa siku ya kesi iliyotangulia, alingia mahakamani na kama kawaida baadhi ya watu waliokuwemo humo, walisimama kutaka kumuona vyema, na hakimu akagonga rungu lake, kutaka utaratibu uwepo, na ilionekana kuwa kulikuwa na malumbano ya wakili mtetezi na waendesha mashitaka.

‘Muheshimiwa hakimu, kwanini kuna ukiritimba kwa hawa waendeshaji wa hii kesi, kwani huyo mwanadada ndiye nani, mpaka tumsubiri yeye…’sauti hiyo ilikatishwa, pale mwanadada huyo alipoingia, na ndipo watu wakainuka kumwangalia akiingia na hakimu kugonga rungu lake kutaka utaraibu uwepo.

‘Samahani nimechelewa, kwani ilibidi nikutane na mashahidi wapya waliojitokeza, na isingelikuwa busara kuwasikiliza kwanza, kabla hawajasimama kutoa ushahidi wao, na kwa mtizamo huo, naona tubadili kidogo, ratiba yetu, ….’akasema mwanadada,akiteta na wenzake.

‘Hakimu kakasirika sana,…’akasema mwenzake.

‘Usijali, yeye mwenyewe atakuja kurizika, akisikia ni sababu gani zilizonichelewesha,…hilo niachieni mimi….’akasema

‘Sawa kwahiyo unataka tumsimamishe nani kwanza?’ akauliza.

‘Mtamuona, hapa hata mwenyewe nashindwa nimuanze yupi, maana wote wana umuhimu, ngoje, nione, ….’akasema na kutuma ujumbe wa simu  kwa mtu anayesimamia mashahidi.

‘Lakini umesema kuna mashahidi wamejitokeza, kwani w atatusaidia nini kwenye hii kesi, tunaongeza mashahidi kabla hatujamalizana na hawa tulio nao, huoni kama tunajichanganya….’akasema mwenzake.

‘Niamini mimi, ….hautujichanganyi kabisa, wewe utaona, ….watakaochanganyikiwa ni hawo washitakiwa na wakili wao,….niamini mimi …’akasema na sauti ya hakimu ikasikika na kumkatiza.

‘Haya tuanze, kesi yetu, na natoa onyo kwa mara ya mwisho, kwa upande wa waendesha mashitaka, hii tabia isirejee tena, hatuna muda wa kupoteza, kwa  kumsubiri mtu mmoja, …’akasema hakimu kwa ukali, na mwanadada akasimama na kuinama kuonyesha unyenyekevu, akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, hali ya barabara zetu inajulikana, nilikutana na foleni, kwani kulitokea ajali mbele yetu,…’akajitetea.

‘Wenzako walifika vipi hapa acha vizingizio…haiyo haikubaliki…..?’ akauliza hakimu, lakini kabla mwanadada, hajijibu, hakimu akasema;

‘Haya tusipoteze muda, tuendelee, hilo nitalifanyia kazi baadaye, ….’akasema na mwanadada akatabasamu, akijua kuwa hiyo ya kulifanyia kazi baadaye haitakuwepo tena siku ya leo ikiisha…

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, hatutamsimamisha shahidi wetu wa kesi iliyopita kama tulivyokuwa tumepanga, kwani licha ya afya yake kuwa sio nzuri, lakini pia kuna mambo muhimu yamejitokea, na tumeona ni muhimu sana kwenye hii kesi,afike shahid wetu mwingine …’akasema mwanadada na wakili wa utetezi akatoa piangamizi.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, kwanini wenzetu wanapenda kuvuruga utaratibu, …wanatufanay sisi tuwe na wakati mgumu wa kujitetea, kwani tulishajiandaa kwa ajili ya shahidi aliyepita, ambaye kwa maneno ya wakili muendesha amshitaka,alisema huyu shahidi ana ushaidi, kwanini anaogopa kuutoa huo ushahidi….’akasema huyo wakili mtetezi.

‘Sisi ndio tunaoendesha hii kesi, na hilo halitavuruga kabisa utaratibu wa hii kesi, na huyo shahidi atasimama na ushahidi unaohitajika utawakilishwa, hilo lisikupe shida, ila kuna ufafanusi wa hilo, …ambao ni muhimu uwekwe wazi …ndio maana tunamuhitaji shahidi huyu atakaye simama sasa hivi….’akasema wakili mwanadada, na hakimu akaingilia kati na kusema.

‘Naona tusipoteze muda, na hakikisheni,kuwa huyo shahidi anaendeleza pale ulipoishia , na awe kweli anafafanua hicho alichokuwa akiwakilisha huyu shahidi aliyepita, ni kweli nimepokea taarifa kuwa shahidi aliyepita anaumwa, lakini dakitari kasema anaweza kufika, …ila hataweza kuongea kwa muda mrefu,…’akasema hakimu.

‘Muheshimiwa hakimu, sisi hatuna pingamizi na hilo, tunachohitajai ni ushahidi, …hasa kwa huyo shahidi kujiweka wazi, maana jinsi alivyokuja kwenye kesi iliyopita, ilikuwa kama tunamsikiliza shahidi aliyefichwa …..tunaomba huyo shahidi awe muwazi, tumone aje akiwa yupo wazi, ili tuhakikishe kuwa ndio yeye kweli…’akasema huyo wakili mtetezi.

‘Hilo litafanyika,…’akasema wakili muendesha mashitaka na hakimu akasema;

‘Haya muiteni huyo shahidi wenu mpya….’akasema hakimu, na wakati wanasubiria huyo shahidi kuingia  wakili mtetezi akainama kuongea na mteja wake, na ilionekana walikuwa wakibishana jambo, lakini wakili huyo akawa anamtuliza mteja wake.

Mlango wa mashahidi ukafunguliwa, na mara akaingia shahidi, na watu wote wakashindwa kujituliza na wengine wakasimama kumwangalia, na hata upande wa watetezi haukuweza kuvumilia, walijikuta wakisimama, na kuhakiki kile walichokiona….

NB: Je unahisi huyo shahidi ni nani?


WAZO LA LEO: Tetea haki, ukisimamia kwenye haki,  bila kuogopa, kwani haki yenyewe itakulinda.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Nancy Msangi said...

Haki ndio kila kitu Baba, haya ngoja tumwone huyo aliyeingia.