Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, July 30, 2013

WEMA HAUOZI-42




Wakili mwanadada akiwa kwenye ofisi yake aliyokuwa ameifungua kwa muda kwa ajili ya kufuatilia kesi hizo, ni ofisi hiyo ilikuwa pembeni mwa duka la mwanadada, alichagua kukaa sehemu hiyo, ili kukutana na watu mbali mbali aliotaka kuwahoji, lakini baada ya tukio la kutaka kuuliwa kwa kugongwa na gari, ilibidi asiitumie tena sehemu hiyo kwa muda, lakini siku ya leo akafika hapo kwani aliahidiana kukutana na mtu aliyempigia simu kuwa anahitaji kuja kukutana naye.

Akiwa kakaa kwenye meza yake, akiwaza, na huku kaweka mikono yote miwili kwenye kidevu tayari kwa lolote litakalo tokea, alihisi joto, akavua koti alilokuwa kalivaa, na kubakia na kivazi kilichoacha sehemu ya mebega wazi, ...akalitundika koti lake ukutani, ....akataka kuchukua silaha yake iliyokuwa kwenye hilo koti, lakini akaona haina haja, akarudi na kukaa kwenye meza, huku akiwa kaweka mikono yake miwili kidevuni kama kwanza.

Badala ya joto, akaanza kuhisi ,mwili ukimsisimuka, na nywele kumsimama, akahisi kuna jambo, akahisi kuna mtu karibu yake,, na hapo akajilaumu, kwanini hakuchukua silaha yake akakaa nayo karibu, maana kama ni mtu yupo karibu, hataweza kuinuka, na kuichukua hiyo silaha kabla hajazurika, ...lakini hata hivyo , huyo mtu angelipitaje, wakati nje kuna askari wanalinda, na polisi wenyewe walimuahidi kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha. 

Inawezekana ni huyo mtu keshafika ..kama ni yeye walinzi wangemwambai kuwa kuna mtu anahitaji kuongea na yeye, asingeliweza kuingia bila kuonekana,....akageuka kuangalia huku na kule, hakuona dalili ya mtu, lakini hisia zake bado zilikuwa zikimtuma kuwa kuna mtu yupo karibu,....

'Isiwe taabu,..'akasema na kuinuka kwa haraka, akaliendea koti lake aliona ni bora aichukue hiyo silaha yake akae nayo karibu, maana huenda huyo mtu hana mema, na hali anayoiskia inamuashiria hatari...na wakati anainuka kwenda kuichua hiyo silaha, mawazo yake yakamrudisha nyuma na kukumbuka jinsi alivyoongea na huyo mtu ambaye aliahidi kuwa atakuja;

‘Unahitaji kukutana na mimi kwa tatizo gani na kwanini iwe usiku, huoni….’ akauliza

‘Siwezi kukuambia kwenye simu , ila nina uhakika litakusadia kwenye kesi yako hiyo, na sitaki nionekane na mtu..’akasema

‘Kesi ipi unayoizungumzia…?’ akauliza mwanadada.

‘Mwanadada, Mwanadada….kwani wewe una kesi ngapi,….?’ Akauliza huyo mtu.

‘Kwanini usiniambie kwenye simu….?’ Akauliza mwanadada, na huyo mtu akasema;

‘Mimi najua yote yanayoendelea kwenye hiyo kesi yenu, na mimi ninajua mengi yaliyofanywa na hawo watu, kwani walinitumia sana, lakini nimeona kuwa hawanifai, walikuwa wakinitumia tu, nawadai pesa nyingi sana, na sizani kama wataweza kunilipa, …nimezungushana nao sana, na imefika sehemu wanaanza kunitishia maisha,…’akatulia kidogo.

‘Kwahiyo kwa vile mnaanza kutapatapa, sasa mnazungukana, au ….?’ Akasema na huyo mtu akaendelea kuongea bila kujali anavyoongea mwanadada.

‘Mimi sikubali kudhulumiwa,, …maana nimefanya mengi ambayo hata sikutaka kuyafanya, lakini kwa shinikizo lao, kuwa nispofanya, wataniumbua, na familia yangu itakuwa hatarini, na kwa vile nilikuwa kijiweni muda mrafu sina kazi, ikabidi nikubali,…sikuwa na jinsi….lakini hata hivyo,nisingeliogopa kuwa maisha yangu yapo hatarini, lakini familia yangu….’akasema.

‘Kama unahisi hivyo , nakushauri ufike kituo cha polisi…uwaambia yote hayo, …’akasema.

‘Kabla sijaenda huko ngoja nikuambie hilo nililotaka kukuambia ,na kukupa  …maana hata huko polisi sikuamini sana, naweza nikauwawa huko huko, na hili ninalotaka kukuambia likapotea, na huenda wakawahi kuniua, ….mimi nawaambia ukweli, hamuwajui watu mnapambana nao, na hamuwajui ni watu gani,..hata hivyo, sitaki nife na kinyongo moyoni…’akasema

‘Sawa wewe fika kwenye ofisi yangu, utanikuta hapo, ila nakukanya kama una ajenda yoyote ya siri, utajijutia mwenyewe…’akasema mwanadada.

‘Usiwe na wasiwasi mwanadada,..hilo nakuhakikishia sina ajenda wala sina kibaya nilichokusudia juu yako, na wewe hawawezi kukuzuru kwa hivi sasa,…yaliyowahi kutokea yametokea na yananitesa sana…siwezi kuvumilia tena, na familia yangu ni muhimu sana…’akasema

‘Sawa nitakusubiri hapo….’akasema na kabla hajakata simu, akasikia huyo mtu akisema;

‘Utanikuta …usiwe na shaka…’akasema huyo mtu na kukata simu

*********

‘Una uhakika sio hawo watu wabaya wanaotaka kukuua?’ akaulizwa na Mzee wa kijiji

‘Nina uhakika sio hawo watu, na kama ni wao, nimeshawekewa walinzi, ambao watakuwa wakinilinda, msiwe na wasiwasi na hilo…’akasema.

‘Lakini mimi nitakuwa karibu yako,….sio lazima unione,.’akasema na mwanadada akacheka, na kusema;

‘Yaani baba, bado tu una wasiwasi na mimi….haya fanya uanavyoweza, lakini nakuomba usije ukaharibu, au ukajitumbukiza kwenye hatari,maana huyo mtu kasema kama kutakuwepo na mtu mwingine hataweza kusema hayo aliyokusudia kuniambia…’akasema

‘Usiwe na shaka, yeye hataniona na hata wewe mwenyewe hutaniona….’akasema baba huyo kwa kujiamini..

Mwanadada alipohisi mwili ukimsisismuka, akainuka na kusimama, akajifanya kama anapanga makabrasha 
yake huku akijaribu kutafuta njio ya kujihami, …au ni walinzi wanapita pita huko nje, au..na ghafla akasikia kama sauti ya kitu,….akageuka na mara akajikuta anaangalia na mwanaume , akiwa kavaa suti na briefcase mkononi na miwani ya meusi, machoni, na usiku kama ule, aliona ni kitu cha ajabu.

‘Wewe ni nani na umeingia saa ngapi humu ndani..mbona sijaambiwa na polisi?’ akauliza mwanadada.

‘Usijali, hapa niliingi baada yaw ewe tu kunikubalia tukutane hapa, jinsi nilivyoingia hata polisi wako hawajui, na hata wakati unaingia humu ndani nilikuwepo hapo nimejificha….’akaonyesha pembeni ya kabati, na mwanadada akajikuta akishangaa, maana kweli alipoingia hakuwazia kabisa kuwa kutakuwa na mtu ndani, kwahiyo hakujali kukagua humo ndani, ….lakini aliwezaje kupita getini, …’akawa anajiuliza.

‘Haya niambie ni nini ulichotaka kuniambia…maana kwa hli kama hiyo umeshaniweka kwenye wasiwasi, umewezaje kuingia hata bila walinzi kukuona?’ akauliza mwanadada.

Yule mtu akafungua briefcase yake na kutoa bahasha, na kumimina kilichokuwemo humo ndani, …kulitoka DVD mbili, na chupa moja ya maji ya kunywa na ndani yake kulikuwa na kitu kama soda, na hiyo chupa ilikuwa imefungwa vyema kwenye bahasha inayoonyesha ndani.

‘Usinione hivi mwanadada, mimi niliwahi kufanya kazi za usalama wa taifa nikafukuzwa…mimi ni komandoo….’akasema na kutabasamu.

‘Hata walipofikia hatua ya kunifukuza, walijuliza mara mbili tatu, maaan walijua kuwa wanafukuza jembe, walijua kuwa mimi sio mtu wa kawaida,na wakawa wananifuatlia kila mara, niliishi maisha kama jela, lkini baadaye wakachoka,na hapo ndipo hawa watu wakanitafuta… nilijuana na huyu mzee siku nyingi..na amekuwa akinitumia kwenye kazi zake za ujasusi….’akasema

‘Unazungumizia mzee yupi?’ akauliza.

‘Tusipotezeane muda, siwezi kukutafunia kila kitu, …’akasema huku akiangalia huku na kule, …kama vile anahisi kitu, halafu akasogea karibu na kabati akaweka kiti na kusimama, na kwa juu, akanyosha mkono, na kuchukua kikasha kidogo cha kuwekea pini za ofisi akakigeuza nyuma na akatoa kitufe kidogo.

‘Kumbe bado kipo, nilikiweka mimi hiki kitufe, nia ni kujua kila kitu unachokifanya..’akasema.

‘Bado sijakuelewa, …umavitoa hivi vitu hapa na kuvimwaga juu ya meza yangu, na sijui ni vitu gani, hujaniambia wewe ni nani na huyo mzee, aliyemzungumzia ni nani, niambie wewe ni nani ili tuweze kuelewana?’ akauliza mwanadada kwa suti ya ukali.

‘Mimi ni mtu wa karibu wa mshitakiwa mkuu wa hiyo kesi yako, na ninaweza kusema kila jambo ambalo linahusu usalama, ufuatiliaji, na…na, na….aaah’ pazia la dirisha lilitikisika kuonyesha kuwa kulikuwa na mtu kalifungua kwa haraka, na mlio mdogo, ukasikika na harufu ya risasi ikatapakaa ofisini, na mwanadada akawa kama anainama kukwepa, halafu akainua uso kumwangalia mwenzake ambaye alishadondoka chini….

Akatoka pale alipokuwa amekaa, na taaratibu aksogelea pale dirishani na kufunua pazia kwa taratibu, na lilipofunguka usawa wakuona kitu akagundua,…..sehemu iliyokatwa kwa ustadi,…halafu akasikia mtu akiguna, akageuka, na akagundua kuwa ni huyo jamaa yake,  alikuwa kalala chini,akilalamika maumivu … atakuwa kapigw risasi, anainama kumchunguza, ni kweli alikuwa kapigwa upande wa kushoto, kwa nyuma, na kitendo hicho kilichofanyika kwa haraka, na huyo mtu alijua ni nini anakifanya, huenda alishajiandaa, na huenda muda wote alikuwepo hapo….

Mwanadada hakuriski,akarudi pale kwenye dirisha na kuchunguza kwa makini akalifungua lile pazia, na lile dirisha lilikuwa limezungushiwa nondo na kuwekwa nyavu , alichofanya huyo mtu, ni kukata nyavu sehemu ndogo na kuachia nafasi ndogo yakuweza kupenyeza mkono…sijui hilo lilifanyika muda gani.Mwanadada akajaribu kuanglia nje, lakini hakuona mtu, na walinzi walikuwa kwa mbele ya nyumba, huku nyuma, kulikuwa kimiya.

Mwanadada akawazakuwa awaite walinzi, lakini akaona kuwa ni muhimu afanye kazi moja ya haraka, kwani walinzi wakifika hapo atakosa kila kitu, kwanza alimkagua huyo jamaa, ambaye kwa muda huo alikuwa katulia kimiya pale sakafuni huku kalala kicha kuelekea chini huku kaegeme mikono yake, na sehemu ya nyuma ambapo risasi ilipenya, kulikuwa kunavuja damu …na hapo mwanadada, akaona fanye jambo kumsaidia huyo mtu, kwa wakti huo alikuwa keshavaa soksi za mikononi,…akatoa kitambaa chake na kukiweka kwenye lile tundu la risasi na kujaribu kulzina lile shimo la risasi.

‘Aaah, naona wameniwahi….’akawa anasema kwa maumivu.

‘Ni akina nani hawo?’akauliza mwanadada.

‘Huyu anaweza akawa mmoja wa ….wa….wa, ..aaah’ akashindwa kumalizia, mwanadada akamsogelea na kujaribu kumweka vyema, na alihisi huenda keshafariki, na alipopima mapigo ya moyo kwa vidole viwili, aliona bado yupo hai, alikuwa kapoteza fahamu tu, na damu zikiwa zikitoka kwenye jeraha hilo la risasi, na mwanadada alitakiwa kufanya haraka kumuita dakitari, ili kama ikiwezekana aweze kumuokoa huyo mtu…akachukua simu na kumpigia dakitari mmoja anayemfahamu, alipomaliza akampigia mkuu wa usalama, aliyepangiwa kulinda eneo hilo.

Akarudi pale mezani na kuvitumbukiza vile vitu alivyopewa na huyo jamaa kwenye mfuko wa plastiki na kuhakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, akachukua ile briefcase ya yule mtu, na nakuifungua ndani kulikuwa na bastola, ….na vifaa vya kurekodia sauti…akavitoa na kuvitumbukiza kwenye mfuko huo wa plastiki, alihakikisha kuwa havigusi kwa mkono wake , kwani alikuwa kavaa sokosi za mikononi.

Akatoka nje na kumuita mmoja wa walinzi, na huyo mlinzi alipofika, huyo mlinzi akauliza.

‘Kuna tatizo lolote bosi….?’ Akauliza huyo mlinzi

‘Huyu jamaa kapigwa risasi,…na nina uhakika kazi hiyo imefanywa na mmoja wa walinzi wenu, kwani haiwezekani, mtu apite hapo bila nyie kujua,, sasa hakikisheni walinzi wote wanashikiliwa na kukaguliwa silaha zao, ….’akamwambia huyo mlinzi, ambaye alikuwa kama kashituliwa na umeme.

‘Haiwezekani, kapitia wapi, nyuma kote huko kuna ukuta,…na na, hebu ngoja kwanza, …’akasema na kukimbili huko nyuma na baadaye akidogo akarudi akiwa anahema kuonyesha kuwa alikuwa anakimbia, na wasiwasi ulikuwa umemjaa, akifahamu kuwa hapo atalaumiwa yeye kama mzembe, na huenda akingia matatani na wakati huo yule docta aliyepigiwa simu na mwanadada,a likuwa ameshafika.

‘Hapo ndani kuna jamaa kapigwa risasi, nijuavyo, hawa watu  wa usalama watachelewa kufika, mfanyie huduma ya kwanza, hakikisha huachi alama zako za vodole…..’akasema na huyo dakitari ambaye ilionekana kuwa kazi kama hizo keshazifanya sana, akaingia ndani, na haikuchukua muda akatoka.

‘Kila kitu kipo safi, …ila anahitajika kuwahishwa hospitali haraka iwezekanavyo, kwani…..bado yupo hai…’akasema  huyo dakitari

‘Naweza kuongea naye kidogo, maana wakija hawa waheshimiwa sitaweza kuongea naye tena,…..?’ akauliza mwanadada.

‘Unaweza…mmh,  ngoja nione  cha kufanya…’akasema na wakaingia ndani na mwanadada, na huyo dokitari akafanya mambo yake na huyu jamaa akawa kama anakoroma.

‘Halloh, unanisikia,mimi ni mwanadada, hebu niambie ni nani aliyekupiga risasi…?’ akauliza mwanadada, lakini yule jamaa alikuwa kama anakoroma tu, na dakitari akasema;

‘Anaweza akaongea,hapo inahitajia muda, mmh …lakini hujaniambia, maana hii sasa ni kesi ya kutaka kuua au mauaji,..kwahiyo unaniambia nini,  nisubiri polisi wafike au niondoke?’ akauliza.

‘Subiri polisi wafike….’na kabla hajamaliza wakasikia yule mtu akiwa anaweweseka, na hapo mwanadada akamsogela na kumsikiliza

 ‘Nenda haraka kao-ongee na yule dereva a-a-ali-yetaka ku-ku-ku-kuua,…ana mengi za-idi, mmh, ooh, lakini usimwa-mini mtu yo-yote, hasa polisi…aaaaah, …’akatulia, na mwanadada akasikia mlango ukigongwa na mkuu wa polisi,akiwa na watu wake walifika.

‘Oh,…yaani umeshamuita dakitari,..kwanini umefanya hivyo huoni utatuharibia taratibu zetu……..’ akaseama huyo mkuu wa kituo.

‘Tangu niwaite nyie,… mumetumia muda gani, huyu mtu yupo kwenye hali mbaya, anatakiwa kuwahishwa kwenye matibabu, ni lazima nifanye jambo ili kumuokoa..’akasema mwanadada.

‘Natumai hamjaharibu ushahidi, na wewe dakitari, usiondoke maana umeshajitumbukiza kwenye kesi hii, utawajibika….’akasema huyo mkuu wa polisi, kuonyesha kukerwa na kitendo kilichofanyika.

‘Mimi nashauri huyo mtu awahishwe hospitali, hali aliyo nayo anahitajia upasuaji wa haraka, ili tunaweza kumuokoa…’akasema huyo dakitari

‘Hiyo sio kazi yako kwasasa….’akasema huyoo mkuu wa kituo cha polisi, huku akiwaonyeshea vijana wake waanze kazi.

‘Mimi kama dakitari nimekuambia hilo, ili liwe kwenye kumbukumbu zenu, ili nikitoa ushahidi wangu itambulike nilisema hivyo, na wakili yupo hapa atathibitisha hivyo…’akasema huyo dakitari.

‘Hivi wewe unajiona unajau sana kazi kuliko sisi, unafikiri mimi hii kazi nimeanza leo,….tusifundishane kazi..hayo yafanye ukiwa kwenye anga zako, hii hapa ni anga yangu, tusiingliane, eeh,…kwani hata hukuhitajika kuwepo hapa kwani sisi wenyewe tumekamilika, nina dakitari wangu atafanya kila kitu, kama ni mtu wa kufa atakufa tu….’akasema huyo mkuu wa kituo cha polisi.

‘Kama mtamuwahisha hospitali mnaweza mukamuokoa, na anaweza kupona, lakini, mnavyozidi kupoteza muda hapa, mnamuweka katika hali mbaya sana, hilo nawashauri mimi kama dakitari…’akasema tena.

‘Hatuwezi kumchukua haraka hivyo, ….kuna mambo yanatakiwa yafanyike kwanza, au kuna mambo mumefanya, hapa, mnataka yasionekane naanza kuwatilia mashaka …’mara simu yake ikaita na alipoangalia na kuona jina la mpigaji, akatoka nje kwa haraka.

Mwanadada alipoona huyo mkuu katoka kwa haraka, aligeuka kuwaangalia waliopo humo ndani, na aligundua kuwa kila mmoja alikuwa akihangaika na shughuli yake, na yeye kwanza akajifanya kama anataka kupiga simu na taratibu akatoka nje. 

Baadaye yule mkuu wa kituo cha polisi akarudi, na alipoingia akawa anawaangalia watu wake wakiendelea na kazi, na akawa anawahoji mmoja mmoja, kuwa ni nini wamegundua, na sasa wanaendelea na jambo gani,baadaye akamsogelea yule dakitari, na kuanza kumhoji;

‘Nitahitajia maelezo yako…’akaanza kusema

‘Hamna shida mkuu…’akasema huyo dakitari na mara mkuu huyo akageuak huku na kule akitafuta jambo, na akasema;

‘Huyu wakili mwanadada yupo wapi?’ akauliza kwa mshangao.

‘Anapiga simu….’akasema huyo dakitari.

‘Ni nani kamruhusu kufanya hivyo, mbona mnafanya mambo kienyeji enyeji…’akasema kwa hasira na mara Mwanadada akingia huku akiwa bado kashikilia simu kuonyesha kuwa alikuwa kiongea na mtu, na hapo alikuwa akikata hiyo simu.

‘Wewe ni nani kakuruhusu kutoka nje…na kupiga simu…’akasema kwa hasira akimwangalia huyo mwanadada.

‘Sikumbuki kuniambia kuwa siruhusiwi kupiga simu, au kupokea simu…’akasema mwanadada.

‘Ina maana wewe hujui kuwa hayo hayaruhusiwi kwa mshukiwa wa mauaji, huoni wewe upo kwenye kundi la mshukiwa wa muaji…’akasema huyo mkuu.

‘Oh, nimeshakuwa mshukiwa tayari, basi nifungeni pingu…’akasema mwanadada akinyosha mikono yake, na yule mkuu akamwangalia kwa macho yaliyojaa hasira, na kusema;

‘Wewe binti, unajua, …ipo siku …’akashindwa kumalizia kwani simu yake iliita na yeye akaipokea bila kuangalia mpigaji na aliposikia sauti, akageuka kumwangalia mwanadada na kusema;

‘Baadaye….’akakata simu.

Mwanadada akamwangalia huku akitabasamu, tabasamu la dharau, huku akiangalia pembeni na kusema;

‘Naona wewe unarushusiwa kuonga na simu, lakini mimi kama mshukiwa siruhusiwi, kwanini uanogopa kuipokea hiyo simu?’ akauliza mwanadada na huyo mkuu wa kituoa akakunja uso kwa hasira akasema;

‘Ni nani kaumabia kuwa naogopa kuipokea, kwanini niogope, huoni hapa tupo kazini, na nikikalia kupkea simu, hatutaweza kufanya kazi….’akasema huku akiangalia saa yake.

‘Sawa mkuu, ujue tupo pamoja, mimi haps sifanyi kazi ya uwakili binafasi, nimeombwa na serikali kusaidi hii kesi, na nahisi kuna watu wa serikali wanahusika..watu weye dhamana…’akasema mwanadada.

‘Kwanini unasema hivyo, unajua nini wewe….wewe kazi yako ni huko mahakamani, hii hapa ni kazi yetu, kama kuna watu wanahusika, tutawagundua tu,…usitie shaka, mimi ninajua ni kitu ninachokifanya….’akasema.

‘Sawa mkuu, ..halafu sikujua kuwa wewe na kiongozi wa kijiji, mna mahusiano…’akasema mwanadada, na yule mkuu, alishituka, kiasi kwamba kile aliyemuona alihisi hivyo.

‘Eti nini….wewe unaota nini….kwanza hebu tokeni nje tifanye kazi yetu, tutawaita tukimaliza..’akasema.

‘Cha muhimu kwa vile mumeshachukua picha muwahisheni huyo mtu, labda kama hamtaki aishi…’akasema yule dakitari na huyo mkuu akamwamgalia kwa hasira na kusema;

‘Hiyo sio azi yako, tokeni nje haraka…’akasema

‘Mimi kama dakitari, niliyemuona huyo mgonjwa , nahitajika kukaa hapa ili nihakikishe, …maana loloye linaweza kutokea, nikasingiziwa mimi…’akasema huyo dakitari na huyo mkuu, akiwa kama kachanganyikiwa akasema;

‘Haya kaeni,….’akasema na yeye akatoka nje, na baadaye akaingia na wakati huo yule mtu aliyepigwa risasi alikuwa akiwekwa kwenye machela huku akiwa katundikiwa dripi ya kumsaidia na huduma nyingine zinastahiki

‘Muwahisheni hospitali ,maana naona hawa tu wanataka kuniharibia kazi, ….’aaksema huyo mkuu, huku akiwageukiwa mwanadada na dikatari..

‘Haya niambieni ilikuwaje…

*************

Mwanadada akiwa yupo kituo cha polisi, kwani ilibidi afike hapo kutoa maelezo kama alivyoamriwa na mkuu wa kituo cha polisi, na aliruhusiwa kuondoka, kwa kujidhamini yeye mwenyewe, na kabla hajaondoka akapitia kitengo cha upelelezi, na huko akakutana na mkuu wa kitengo hicho .

‘Naona niongee na wewe haraka, huu mzigi hapa, naomba uuhifadhi, na kama ikibisi tutafute sehemu , kuna mambo hapa yakifika kwa hapa jamaa, hatutayaona tena..’akasema wakili mwanadada., na mkuu huyo akaangalia vile vitu, na alikuwa kama anaogopa kuvigusa.

‘Huoni hilo ulilolifanya ni hatari…umevuruga taratibu za kipolisi…’akasema.

‘Hilo nalifahamu sana, lakini kama nisingelifanya hivi, mengi yanayohitajika kweney hii kesi yangelipotea, kama nilivyowahi kukuambia, mimi siamini kituo chenu hiki…’akasema wakili mwanadada.

‘Nafahamu hilo, lakini….’akasema na kuvaa soksi za mikononi, na akaanza kuvitoa vile vifaa, na alipoiona ile bastola, akashituka,…akawa anaishika kwa uangalifu sana, huku akiwa kakunja uso, na alipoikagusa, akaichukua na kuiweka kwenye platiki, ikiwa peke yake.

Akatoa chupa, iliyokuwa na itu kama soda au juisi,, akaiangalia kwa makini, na halafu akageuka kumwangalia Mwanadada, akasema

‘Hii sio soda, na kama ni soda, itakuwa imechanganywa na kitu kingine….’akasema

‘Hata mimi nahisi hivyo, na  ni moja ya vitu alivyotaka nivichukue huyo mtu kabla hajapigwa risasi, nahisi kuna jambo linalohusiana na hiyo soda isiyotambulikana…’akasema na huyo mkuu akaiweka kwenye mplastiki na kuandika kitu juu yake

‘Inabidi ifanyiwe uchunguzi wa haraka…’akasema na kuendelea kuchunguza vitu vingine, na zile DVD, akawa kaziacha mezani, halafu akasema;

‘Naona hapa kwasasa hakuna usalama, ….lakini moyo nahisi tutakuwa tumefanya kosa, kama hatutamshirikisha mkuu wa kituo…’akasema.

‘Kama nilivyokuambia, na kama hisia zangu zilivyokuwa toka awali, huyo mkuu, usimwamini tena, …nakuhakikishia hilo, maana nimemsikia mwenyewe akiongea na simu…’akasema mwanadada na mara mlango wa mkuu huoo huyo ukagongwa, na ulipofunguliwa mkuu wa kitua akaingia na alipomuona huyo mwanadada, akashituka.

‘Ina maana bado wewe upo?’ akauliza.

‘Mkuu, mbona huniamini, nimeshakuambia kuwa mimi nipo pamoja na nyie, kama mkinitenga, nitaweza kufanya kazi yangu, au umesahau kuwa mimi ni wakili uapnde wa serikali kwenye hii kesi, …’akasema mwanadada.

‘Ni sawa, lakini inapokuja katika mambo ya usalama, hata kama ni askari wetu, kakutwa kwenye tukio kaam hilo lililotokea kwako, hatuwezi kumwamini tena, mpaka ithibitishwe vinginenvyo,….’akasema.

‘Kwahiyo hata huo uwakili niuache, mana hamuniamini…’akasema

‘Sijasema hivyo…’akasema huyo mkuu, na akawa anaziangalia zile DVD, juu ya meza ya mkuu wa kitengo cha upelelezi, hakusema kitu, akageuka kutaka kuondoka.

‘Mkuu, nilijua kuwa umekuja kuniona,…’akasema mkuu wa kitengo hicho, lakini huyoo mkuu akawa keshatoka nje.

‘Nahisi anafahamu jambo kuhusiana na hizi DVD,..naona tufanya jambo la haraka, kabla hazijapotea,…’akasema huyo mkuu, na akachukua laptop yake na kuanza kuzinakili kwenye laptop  yake na kuhakikisha zimenakiliwa vyema, halafu akazichukua na kuziweka kwenye mfuko wa palatic, kwanza akatafuta DVD, nyingine tupu, akaziandika kama kama vile zilivyoandikwa hizo DVD, nakuziacha pale juu ya meza, halafu yeye na mwanadada wakaondoka, wakiwa wamechukua mzigo wao

********

‘Hebu niambie ilikuwaje?’ akauliza mkuu huyo walipofika nyumbani mwa mkuu huyo, na wakawa wanaanza kuangalia ni kitu gani kipo kwenye ile DVD,

‘Ninachoshukuru mungu, ni kuwa nipo salama, nahisi aliyefanya hivyo, hakuwa na lengo la kunimaliza mimi, ….alikuwa na lengo la kummaliza huyu mtu..na hili linanipa wazo kuwa adui yetu huenda tunaye…’akasema.

‘Una maana gani?’ akauliza huyo mkuu

‘Wewe huoni, kiongozi wa kijiji, yupo ndani, ..asingeliweza kuongea na hawa watu na kutoa amri hili lifanyike…..na ni nani alijua kuwa nitakutana na huyu mtu,…niliyemwambia ni mkuu wa kituo na wewe…’akasema na kutulia kidogo, halafu akakumbuka,

‘Kuna kifaa kilipandikizwa kwenye ile ofisi niliyokuwa nikiitumia, na aliyekiweka na huyo huyo jmaa aliyepigwa risasi, sasa sijui ,,….huenda kuna vifaa vingine zaidi, kwahiyo hawa watu wananifuatilia kwa karibu sana, na sio watu wa kawaida kama tunavyofikiria,….’akasema mwanadada.

‘Sawa nimkuelewa mwanadada, hilo niachie mimi,…mimi mwenyewe sipaamini tena hapa, na nafanya kazi katika mazingira magumu sana…nilipoongea na bosi wangu, aliniambia ataniongezea nguvu, kwahiyo wale vijana, waliokuja na mkuu wa kituo, ni hawo waliotokea Dar, nina imani nao, watagundua kila kitu, mimi najifanya sihusiki moja kwa moja..’akasema huyo mkuu wa kitengo cha upelelezi cha kituo hicho.

 ‘Umefanya la maana sana…kuviwahi hivi vitu, na pale ilibidi nikuambie hivyo, maana nahisi hata pale ofisini kuna vinagalizi vya nyendo zangu….’akasema huyo mkuu wa kitengo cha upelelezi

‘Kwanini?’ akauliza mwanadada.

‘Kuna mambo yanaendelea hapa na hata mimi yananitia wasiwasi, na kuna pendekezo kuwa nihamishwe kituo hiki, lakini nimeweza kuongea na bosi wangu huko juu, na kumwelezea hali halisi,..na kwa kuniamini ndio akanitumia hao vijana, na mimi nawaamini maana nilishawahi kufanya nao kazi nikiwa huko Dar, na nina uhakika watagundua mengi, lakini …huyo mkuu wa hapa, mmh, siwezi kusema neno, mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika…’akasema.

‘Hata mimi nimeshamtilia mashaka,…maana haya matukio yanayotokea kukiwa na walinzi, ..haiwezekani, nahisi kuna jambo, angalai yule mtu aliyetaka kunigonga, eti imegundulikana kuwa hana hatia,a likuwa ni mlevi tu, mimi sikukubaliana na hilo, nab ado nalifanyia kazi….’akasema mwanadada.

‘Nitakuja kukuambia jambo kuhusiana na hilo, lakini sio leo…’akasema huyo mkuu

‘Unajua kuwa nimegundua jambo jingine, wakati nasikiliza simu, ya huyo mkuu, akiwa anaongea na mtu mwingine,…’akasema mwanadada.

‘Umegundua nini?’ akauliza huyo mkuu

‘Huyo mkuu wako, inasemekana wanaudugu na  Kiongozi wa kijiji….mshitakiwa mkuu’akasema wakili mwanadada.

‘Unasema kweli…!!!, mamamama, mbona huyu mkuu, nijuavyo mimi, kwao ni mikoani,..na hata kumbukumbu zake zinaonyesha hivyo…’akasema huyo mkuu wa kitengo cha upelelezi.

‘Nimesikia kwa masikio yangu mwenyewe,….’akasema mwanadada

‘Kwani wewe uliskia ninii, cha kukuhakishia kuwa wana udugu, na huo udugu ni wa namna  gani?’ akauliza huyo mkuu

‘Kiongozi wa kijiji ni baba yake huyo bosi wako,…’akasema mwanadada.

‘Haiwezekani…labda awe ni baba kutoka kwa nyumba ndogo…’akasema huyo mkuu wa upepelezi.

‘Mhh,…labda, …’akaguna mwanadada na hapo ile DVD, ikaanza kuonyesha mambo, na kuwafanya watulie kuiangalia, hawauamini ….
Nb: Mambo yanazidi mambo…ni nini kimegundilikana tena, je kesi hii itakuwaje, …angalia dhamana zinavyochezewa sababu ya  umimi, udugu, ukabila….


WAZO LA LEO: Usije ukajidanganya kuwa wewe kwa vile ni muheshimiwa, au mkuu, uliye na dhamana, unaweza kufanya lolote ukiegemea wadhifa wako, ukawa unatenda madhambi ya kudhulumu, kuficha maovu ya ndugu zako, au ya jamaa zako, au kabila lako,..na wengine wanafikia hdi kuua, eti kuondoa ushahidi…kamwe usidhanie kuwa jambo hilo litaisha kiujanja ujanja tu.


Dhambi kama hiyo itakuandama milele, kwani siku zote uliowatendea hizo dhambi, ukawadhulumu, nafsi zao watakuwa wakimlilia mola wao,…na kila mja ana haki yake, na mola ni kwa wote, kwanini wasisikilizwe..ndugu yangu, jiepushe na dhambi kama hizo, maana kuua nafsi moja bila ya haki ni sawa nakuuwa nafsi za watu wote.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Unknown said...

Mmh emu 3 upo juu Sana batsman hata isiishe km nachek movie vile,

Yasinta Ngonyani said...

mmmmhhh nasubiri kwa hamu kuona kulikuwa na nini kwenye DVD....ila jamani tuaache ukabila, umimi na undugu tuwe kitu kimoja