Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, July 27, 2013

WEMA HAUOZI-41



Kumbuka tupo bado mahakamani, na sasa aliitwa shahidi,….shahidi ambaye uvaaji wake, ulikuwa sio wa kawaida, alikuwa mwanamama, ambaye alijitanda khanga mwili mzima, na kubakiza sehemu ndogo ya macho.  Hata hivyo, haikuwezekana kumwambia avue hizo nguo, je kwanini alivaa hivyo, ni kutokana na imani za dini, au kuna jingine na je huyu shahidi ni nani hasa, …tuendelee na kisa hiki.

*******

Wakili mwanadada akamsogelea shahidi wake, huku hakimu akiwa bado anamwangalia huyo shahidi kwa kuonyesha shauku au kushangaa, na alikuwa anataka kusema jambo, lakini akawa anasita, huenda ni kwa kuogopa kuingilia imani za watu, akageuka kumwangalia wakili mwanadada ambaye alikuwa akijiandaa kuongea, na mwihowe  akachukua kalamu yake na kuandika jambo, na wakati huo huo wakili mwanadada akaanza kuongea;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, natumai kila mmoja amekuwa na mawazo na shauku, ya kusikia mengi hususanai kwa shahidi yetu huyu, na najua kila mmoja ana dukuduku la kutaka kujua kwanini shahidi huyu kavaa kama anavyoonekana, na wengi watakimbilia kusema labda kava hivyo kwa ajili ya imanai za kidini, …nawaomba muwe na subira, mtakuja kufahamu ni kwanini baadaye….’akaanza kuongea na watu wakawa kama wanapumua. Kila mmoja mle ndani akili na macho yake yalikuwa pale mbele, kila mmoja akijaribu kuhakikisha hakosi kitu…

‘Katika maelezo yetu ya awali tulisema kuwa tutawaleta mashahidi, na ushahidi wao, na hata wakati tunaendelea na kesi  yetu hii wenzetu wamekuwa mara kwa mara wakidai ushahidi, na hata kusema kesi yetu hii imegubikwa na siasa na porojo nyingi, kuliko sheria, hili tunalainza sasa,  kuwa kila shahidi atakayesimama kuanzia sasa, atakuwa na ushahidi…’akasema na kumwangalia yule mwanamke aliyekuwa kakaa kwenye kiti.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, naomba nielezee kidogo,kama nilivyokuomba awali ..japokuwa huenda wenzetu wasikubaliane na hili, lakini ni kwa masilahi ya wote, maana tunasema usione mwenzako anafanyiwa ubaya ukacheka, kwani huwezi kujua ya leo na kesho,…utacheka, likitokea kwa mwenzako na hata kumlaumu, lakini kumbuka hakupenda, na huenda, imetoka hivyo kwasababu ya watu…ndio maana tunasema  leo ni kwake, kesho ni kwako…..’akatulia kidogo

‘Pia kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia maji….maana mabaya na ubaya hufanywa na watu, na huenda wakawa watu wako wa karibu tu….’akatulia na kuangalia upande huo wa wapinzani akitarajia pingamizi lakini wakili mtetezi alikuwa akiandika kitu kwenye makabrasha yake, aliyekuwa anaonekana kuongalia mbele , akimwangalai yule shahidi ni mteja wake.

‘Binadamu tumefikia hatua mbaya kabisa, hatua ambayo, tunaona maslahi ndio kila kitu, tunaona mambo yetu, ndio yana maana kuliko hata uhai wa mtu, mtu yuko tayari kutoa roho ya mwenzake kwasababu ya mali, pesa, sifa..…hali hii imekwenda mbali hata kutokijali wale wasio na hatia, wale ambao hawawezi hata kujitetea,..eti kwa vile sisi tuna madaraka, kwa vile sisi ni matajiri , kwa vile sisi ni mabosi, hatujali kabisa utu wa mtu, tonachojali sisi ni  tufanikiwe mambo yetu, nakujiona  tuna haki ya kila kitu….utasema nini kwa mwenye pesa, mwenye utajiri, bosi, …muheshiwa….tunajidanganya…’akatulia.

‘Shahidi huyu atakuwa kielelezo cha hayo ninayotaka kuyaelezeahapa, na ni vyema wanajamii mkalisikia hili, na kupata fundisho, ‘akageuka kumwangalia wakili wa utetezi ambaye alikuwa akiangalia saa yake, na kuendelea kusema.

‘Sio kwamba nahutubia hapa kupoteza muda, lakini inabidi nifanye hivyo kwa msilahi ya wanajamii, na nilishamuomba muheshimiwa hakimu kuhusu hili mbele ya wakili mtetezi, … lengo ni ili tuelimishane, ili hili na mengine yasitokee tena….’akasema na hakimu akaonyesha ishara kuwa wakili aendelee asipoteze muda.

‘Sisi ni binadamu, na hata tufanyeje hatuwezi kulibadili hili, na kama ni bianadamu, fanya  ufanyalo, penda upendavyo,ishi unavyopenda kuishi….lakini upo mwisho wa kila mtu. Na hizi tambo za utajiri, za kujiona, kuwa eeh, mimi ni mzuri, mimi ni bosi, kiongozi, muheshimiwa,  yote hayo ni hapa duniani tu, na malipo ni mbele ya mwenyezimungu…’akasema na kugeuka huku na kule.

‘ Kwahiyo nawaasa, na kujiasa mwenyewe, kuwa  ni vyema tukajiandaa, ni vyema tukajichunga nyendo, na taratibu zetu, ili ziendane na utu wa binadamu, na ni vyema tukachunga dhamana tulizopewa, kwani sio zetu,…wewe ni kiumbe tu kama viumbe wegine, tukumbuke kuwa kuna mwenye mamlaka zaidi yako,….akitaka liwe huwa, yule mwenye mamlka ya roho yako..’akatulia na mshitakiwa mkuu alionekana kukerwa, alikuwa kama anahangaika, lakini kwa muda ule hakuna aliyekuwa akimwangalai kila mtua alikuwa na shauku ya kuona au kusikia kutokana na shahidi huyo hapo mbele.

Kwa jinsi alivyokuwa akihangaika, watu wangelihisi mengine, lakini cha ajabu hata wakili wake, ambaye likuwa kakaa karibu naye, alikuwa hana mawazo na yeye, ….kama wengine, mawazo ya kila mtu  yalikuwa kule mbele.

‘Kuna imani zimejikita kwenye jamii zetu, na imani hizi zimetupaka matope, kidunia ,na hata kulichafua jina zuri la nchi yetu kuwa eti taifa letu ni miongoni mwa mataifa yanayo-ongoza kwa imani za kishirikina….hii sio sifa nzuri kabisa, mimi nasema huu ni uchuro, ….na ni kwanini tukafikia hapa…’akatulia na kuangalia,saa kwani alikumbuka kuwa alipewa dakika chache za kutoa huo muhutasari.

‘Mimi ninakubaliana na wale waliosema, kuwa sisi tunatatizo kubwa la Adui ujinga…’akataabsamu kidogo na kukuna kichwa.

‘Kuna maadui wengine, yupo adui, umasikini na maradhi,…hawa ni adui wakubwa sana, lakini huyu adui ujinga, amekuwa kikwazo kikubwa sana kuweza kupambana na maadui hawa wengine….kitu elimu, bado wengine hawajambua elimu ni kitu gani, je elimu ni kwenda darasani, na kukariri tu….hapana, elimu ni pana,..nasema hivi kwasababu…’akaatulia kidogo.

‘Nasema hivyo kwasababu wapo watu tunaowaita wasomi, bado wanaamini haya,…mchana wakiwa na suti zao, utawaona ni watu, wenye wadhifa wao, lakini usiku, wanakwenda kugonga milango ya wataalamu….msicheke haya yapo….na wengine wana hizo zinazoitwa hirizi….’ akawa anachezesha mikono na hapo watu wakawa wanacheka kidogo, lakini walinyamaza pale alipoendelea kuongea.

‘Wasomi hawa,wanaamini imani za kishirikina na hata kuzikumbatia, na kuzipigia chapuo, je huyu alikwenda shule kufanya nini…kama anafanya haya, anayaamini haya, na kuyapigia debe, basi …tunaweza kmfananisha na yule punda aliyebebeshwa vitabu vyenye hazina kubwa, lakini yeye hajui kuvitumia. Huyu kaenda shule, akasoma, akakariri, ili apate cheti, lakini hajaelimika, kaibeba elimu kichwani lakini haijui kuitumia, ni sawa na huyo punda, …ni kazi bure…’akasema na kuangalia huku na huku.

‘Elimu inatakiwa ikubadilishe bwana, elimu inatakiwa ikujenge uwe tofauti,..ili kila ulifanyalo uwe na uhakika nalo, usiwe mtu wa kubahatisha,…je imani hii ya kishirikiana ni ya uhakika au ni ya kubahatisha..hebu tujaribu kujiuliza wenyewe akilini na ukipata jibu utagudua kuwa nina maana gani?’ akawa kama anauliza.

‘Wewe unadiriki kumuita, ,eti mwenzako ni mchawi,  una uhakika gani na hilo, huoni kuwa ni chuki tu, husuda tu, ubinafasi tu, na mengi yamekuzwa na propaganda ambazo zilizopandikizwa, kwa ajili ya hiyo chuki tu na baadhi ya watu, na hili utaliona kwenye hii kesi, …’akatulia na uangalia saa yake.

‘Jamani utakuja kusema nini mbele ya mungu mtu kama wewe, uliyesoma uliyepewa majukumu, …na dhamana za watu nab ado hukutimiza wajibu wako…eti kwasababu ya chuki za imani, hasa hii ya kishirikiana, ambazo zimekwenda mbali zaidi….zimefikia hapo kwa vilezimejengwa na dhana ya kishetani…’ hapo alipaza sauti alipotamka neno `kishetani’

‘Watu wanafika hadi kukosana mtoto na mzazi wake, watu wanafika hadi kuuana,….jamani, mna ushahidi gani wa kisayansi kuwa huyu mtu mnayemshuku ni mchawi, onyesheni huo ushahidi tuuone huo au huyo mchawi akifanya hayo…ukichunguza zaidi utakuta hakuna ushahidi wowote zaidi ya dhana tupu, na ukichunguza zaidi utakuta ni chuki binafsi…jamani mtakuja kusema nini mbele ya mwenyezimungu…’mara hakimu akainua mkono juu, kuashiria kuwa muda umekwisha.

‘Sawa muheshimiwa hakimu, ni hayo kwa muhustasari…yanatosha, ngoja tuanze kuthibitisha hayo kwa vitendo…’akasema lakini  wakili mtetezi akaomba naye aongee kidogo. Na aliporuhusiwa akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu nimeona nisinyamaze tu, maana hili kwangu naliona ni tatizo…hapa ni mahakamani, hapa sio ukumbi wa kisiasa, mimi nilikubali kuwa mwenzangu labda anahitajia kutoa maelezo ya ushahidi wake, nilitarajia kuwa mwenzangu angelielezea ushahidi wake ili ueleweke vyema angelielezea jambo kuhusiana na hii kesi, lakini cha ajabu amegeuza mahakama ni uwanja wa siasa…’akatikisa kichwa kama anasikitika.

‘Sisi tutaendelea kudai, ushahidi na mashahidi, leteni ushaidi,…kwakweli nyie ndio mnaoendesha hii kesi kwa dhana…kama unahitajia kuielimisha jamii kwa hayo uliyoyaongea,…basi omba kibali nenda  akayaongelee kwenye viwanja vya siasa,….’akasema na kujipiga mikono kama kudharau.
Wakili mwanadada akatabasamu na kumwangalia muheshimiwa hakimu, ambaye alikuwa akiandika kitu, na baadaye akasema

‘Tuendelee…’

‘Sawa muheshimiwa, ujumbe umefika, na sasa tunaanza kazi, ndugu muheshimiwa hakimu, huyo hapa mbele yetu ana sifa zote mbili ya shahidi na ushahidi…’akasema na watu wakaguna, na huyo wakili wa utetezi, akacheka, hakimu akagonga rungu lake kuashiria utulivu.

‘Nawaonya kwa mara ya mwisho…kama utaratibu wa mahakama hautafuatwa hatua kali dhidi yenu zitatekelezwa, ..mnasikia…’akasema hakimu na mawakili hawa wawili wakainama na kusema

‘Tumesikia muheshimiwa hakimu….

‘Haya endelea na shahidi wako…’akasema hakimu.

Wakili mwanadada akamsogelea shahidi  wake na kwa unyenyekevu akamwiinamia na kumnongoneza kitu, na yule mwanamama akanyosha uso, kuangalai mbele kidogo, lakini kwa jinsi alivyokuwa amevaa usingeliweza kumuona vyema usoni, ni sehemu ndogo tu ya uso.

‘Shahidi unatakiwa  ujieleze kidogo, japokuwa umeshataja jina lako, lakini kwa hivi sasa elezea wewe ni nani na wanakujuaje watu wa eneo lako…’akasema wakili mwanadada.

Yule mwanamama, akakohoa kidogo, kuondoa kitu kooni na kuanza kuongea, huku akishikilia khanga inayofunika uso na kichwa isiondoke na hata uso wake ulikuwa unaonekana kidogo sana, ….sauti iliyokuwa ikitoka ilikuwa kama mtu kaweka kitu mdomoni, na maneno yake yalikuwa hayasikiki vyema, thi-thi…zilikuwa nyingi zaidi, hata hakimu naye akaonyesha kutaka kusema neno, kwanza akamwangalia wakili mwanadada…, lakini baadaye akatulia.

‘Samahanini sana sauti yake inasikika kwa shida,…tutakuja kuliona hili baadaye na ni  kwanini iwe hivyo, tunaomba utulivu na umakini wa kumsikiliza…’akasema.

‘Mimi naitwa Tabu, binti Saburi,,…..jina hilo kwa wengi, halijulikani sana, watu wengi wananitambua kwa jina la mama Mkunga….’akasema sauti ya `mama mkunga’ haikutoka vyema na wakili mwanadada akaomba alirudie tena hilo jina.

‘Mimi wananitambua kama ‘mama mkunga..’ alipotamka hivyo kwa uwazi, ukatokea mguno, na mshughuliko, maana wengi ambao walisikia, hawakuamini, na wale wasiosikia wakawa wanaulizana, na hali ikaanzisha kitu kama zogo. Lakini majina kama hayo hupewa wakina mama wengi wanaofanya hiyo kazi, kwahiyo bado ilibakia kitendawili kwa watu….

Hakimu akagonga rungu lake, na baadaye akamuita wakili muendesha mashitaka, na kumwambia.

‘Shahidi wako hawezi kuongea vyema, au huend hizo nguo alizovaa zinaweza kuwa ni sababu?’ akauliza

‘Kwa hali aliyo nayo hapo ndio sauti yake ya mwisho labda tungeliomba awekewe kipaza sauti…’akasema wakili mwanadada, na kweli hakimu akaamrishs kipaza sauti kiletwe,  na chombo hicho kikaletwa na kuwekwa mbele yake., na hapo sauti yake ikawa inasikika vyema japokuwa maneno mengi yalikuwa hayatoki kama yanavyotakiwa.

‘Haya hebu rudia maelezo yake …kwa kututambulisha kuwa wewe ni nan..’akasema wakili mwanadada.

‘Mimi naitwa Tabu, binti Saburi, lakini wengi hawanifahamu kwa jina hilo, wananifahamu kwa jina la mama mkunga…’akasema na hali ile ya mwanzo ikatoea tena, lakini baadaye kukatulia, na hakimu akawageukiwa wenzake na akawa anateta nao..

‘Haya tuendelee…lakini naonya tena, sheria zetu zinajulikana, …walinzi hakikiheni wote wanaokiuka sheria mnawatoa nje, na hatua kali zitawaandama…’akasema hakimu.

‘Kwanini wakawa wanakuita mama mkunga?’ akauliza wakili mwanadada.

‘Kwa vile nimekuwa nikifanya hiyo kazi ya kuzalisha wakina mama waja wazito?’ akasema.

‘Kwani kijijini kwetu hakuna zahanati, au hospitali ya kujifungulia akina mama ?’ akauliza.

‘Hakuna ni mpaka twende mjini…’akasema

‘Ujuzi huo umeupatia wapi?’ akaulizwa.

‘Ujuzi huo niliupatia kwa bibi, na mama yangu, ukoo au familia yetu imebarikiwa kujua kazi hiyo, na bibi yangu alinifundisha kila kitu, na yeye akanihakikishia kuwa nimekuwa mtaalamu kuliko hata yeye na mama…’akasema.

‘Najua wengi watasema..mnaona, kumbe bibi yake ndiye aliyemfundisha mambo hayo mnayoyamini ya kishirikina, lakini sivyo hivyo, huyu mama alitunukiwa kipaji cha kuweza kuwafunguza akina mama , na alifanya hayo na kuwaokoa wanawake wengi waliofikia muda huo, na wasingeliweza kufika hospitalini, kwa vile hospitali ipo mbali, nyote mnafahamu hali ya nchi yetu……Imebidi nifafanue hapo kwa vile kama mnavyosikia kuongea kwake.

Wakili wa utetezi akatoa pingamizi na kusema;

‘Mbona tunamsiki a, ..hicho kipaza sauti kimewezesha kumsikia vyema, usijifanye mjanja wa kuingizia maneno yako ya kisiasa, fuata sheria…’akasema wakili huyo na hakimu akasema

‘Endelea na shahidi yako wakili mwanadada, na fuata taratibu…’akasema hakimu.

‘Kwahiyo ukawa unafanya kazi hiyo kwenye kijiji, pamoja na bibi yako na mama yako, je hawo watu wapo hai?’ akauliza.

‘Hapana wameshatangulia mbele ya haki…’akasema huyo shahidi.

‘Pole sana yote ni matakwa  ya muumba, kwani kama wengelikuwepo hai huenda wangelisaidia hili kuonyesha kuwa imani walizokuwa nazo watu dhidi yako ni dhana potofu sio sahihi…’akasema na wakili wa utetezi alitaka kutoa pingamizi lakini wakili mwanadada akaendelea kumuongoza shahidi wake.

‘Je kazi hiyo ulikuwa ukiifanya mwenyewe, ….yaani anapotokea mtu anataka kujifungua kwa dharura na akaomba umsaidie, ..uliweza kuifanya kazi hiyo peke yako?’ akaulizwa.

‘Mara nyingi sana, nakuwa nawasaidizi wangu,….naweza kusema siwezi kuifanya kazi hiyo peke yangu bila msaidi, kutokana na kazi yenyewe ilivyo…’akasema.

‘Je kuna ugumu gani katika kuitekeleza k azi yako hiyo au ni magumu gani uliweza kukutana nayo katika kuitekeleza kazi yko hiyo?’ akaulizwa.

‘Yapo machache, na hayo machache yanatokea kama mzazi ana matatizo mengine ambayo mimi nisingeliweza kuyafahamu, kama vile ukosefu wa damu, au kutoka damu nyingi..au shinikizo la damu…na vitu kama hivyo.’akasema.

‘Sasa kama uliyajua hayo, uliwezaje kupambana nayo…?’ akaulizwa.

‘Kwanza ninapopata taarifa ya mja mzito, kitu kikubwa nawauliza wahusika au muhusika kama ana tatizo kama hilo, na je ameshawahi kwenda kiliniki, na kwanini wanaamua kumleta kwangu badala ya kumpeleka hospitalini. Lakini hayo hutokea, mara nyingi ni kwa vile mja mzito huyo kafikia muda wake na hakuna njia nyingine, ila nikumsaidia ajifungue…’akasema.

‘Kwahiyo ulikuwa ukiitwa kama hali ya kujifungua imeshafikia, na je kama utamkuta hali hiyo haijafikia ulifanayaje?’ akaulizwa.

‘Kama hali yake ya kujifungua haijafikia, huwa nawaomba wananduguu tuongozane, hadi hospitalini…’akasema.

‘Kwanini muongozane  nao?’ akaulizwa.

‘Ili kama atazidiwa njiani niweze kutoa huduma hiyo…’akasema.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, naona twende hatua kwa hatua, labda niwapishe wenzetu katika sehemu hiyo kabla sijaendelea naye sehemu ya pili, kama wapo tayari, kama hawana maswali ngoja mimi niendelee naye…’, na kabla hajamaliza, wakili wa utetezi akasema;

‘Nashukuru kwa taratibu zenu hizo za sehemu ya kwanza ya pili..haya tutafanyaje, na nyie ndio waendeshaji iwa hii kesi, lakini kwetu sisi hatuna shida,….ngoja nimuulize shahidi wako, ambaye umeamua kumficha …sijui na huu ndio utaraibu wenu mwingine,….’akasema huyo wakili na kumsogelea huyo shahidi huku watu wakijizuia kucheka, kwa jinsi alivyo kuwa akiigiza.

‘Mama wewe unasema ni mkunga wa jadi..je una kibali chochote cha kazi hiyo?’ akauliza.

‘Ndio ninacho..lakini kiliisha wakati wake, na kipindi nafuatilia kuongezwa muda, ndo yakanikuta haya…’akasema.

‘Unaweza kutuonyesha hicho kibali…’akauliza na wakili mwanadada akaingilia na kusema;

‘Kama utakihitaji hicho kibali sisi tutakionyesha kama moja ya ushaidi, kwa hivi sasa hana hicho kibali hapo alipo, kwasababu ambazo tutakuja kuzielezea baadaye….’akasema mwanadada na huyo wakili wa utetezi akawa anamwangalia huyo mwanamama kwa makini kama vile anataka kujua sura yake, lakini hakufanikiwa.

‘Je una zahanati, au una sehemu maalumu ambayo unaifadhi vyombo vyako, maana kazi hiyo inahitajia uangalifu wa hali ya juu, au zahanati yako ni kila mhali kwa wakati wowote..?’ akauliza.

‘Kazi ya ukunga wa jadi ni kama huduma ya kwanza..ndio ninavyo vifaa, lakini sina zahanati,…’akataka kuendelea lakini wakili mwanadada akaingilia kati.

‘Kama unahitajia kuviona vifaa vyake, na jinsi gani anavyofanya, hayo tutayatoa kama ushahidi baadaye…’akasema wakili mwanadada.

‘Wewe unasema kazi hiyo uliipata kwa bibi yako, je bibi yako licha ya kazi hiyo ya ukunga wa jadi, alikuwa akitambulikana kwa kazi gani nyingine….ambayo pia alikurisisha?’ akauliza.

‘Alikuwa mtaalamu wa tiba asilia..’akasema.

‘Alikuwa akitibia kwa uganga wa kienyeji, kama vile kuagua..kupiga ramli,….mashtani , na vitu kama hivyo?’ akauliza

‘Tiba asilia zinajulikana zilivyo….na kumbuka enzi zao, ilikuwa ndio tiba iliyotambulikana…na sasa watu wanaanza kuiletwa wazi kwa utalaamu wa kisasa..’akasema.

‘Je pamoja na tiba hiyo asilia, hakuwa na sifa nyingine, ambayo watu walikuwa wakimsifia nayo..?’ akauliza na watu wakaguna

‘Kama ipi, maana unavyoelezea ni kama vile unafahamu kuwa alikuwa na sifa nyingine..ambayo sijui ni ipi?’ akauliza.

‘Watu walikuwa wakimuogopa, kuwa ana nguvu za giza…ni kweli sikweli, kama walivyokuja kukuogopa wewe…’akasema na watu wakaguna na wengine kucheka.

‘Je unaamini hayo?’ Shahidi akauliza.

‘Nijibu swali langu…hujaambiwa uniulize swali mama…umemuomba muheshimiwa hakimu kuwa unataka kuniuliza swali….?’akasema huyo wakili.

‘Nitakujibu swali kutokana na imani yako, kama unaamini au huamini, kwasababu nikikujibu kiimani hizo na wewe huamini haitasaidia kitu..’akasema huyo mama.

‘Je mama yako aliwahi kushutumia, au kuongelewa kuwa na sifa hiyo ya nguvu za giza, ….?’ akaulizwa tena.

‘Hayo ni maneno ya watu,…ambayo yalianza baada ya mama na bibi kuondoka, lakini wakati wapo hai, watu walikuwa wakiwaheshimu kwa jinsii dawa zao zilivyokuwa zikiwasaidia watu, waulize wazee wa siku nyingi watakusimulia…’akasema.

‘Hayo maneno ya watu yalisema nini?’ akauliza.

‘Kama hivyo ulivyoosema wewe…’akasema na watu wakacheka.

‘Mama tusipoteze muda, jibu swali langu…’hapo wakili mwanadada akaingilia kati na hakimu akasema kuwa wakili wa utetezi aulize swali la msingi, asiulize swali la kusikia…’akasema hakimu.

‘Ni hayo kwasasa muheshimiwa hakimu….’akasema wakili wa utetezi na kurudi sehemu yake, na alipofika sehemu yake…akamsogelea mteja wake, ambaye alikuwa kainama kwenye kiti huku akiwa kaangalia mbele, kuonyesha kuwa alikuwa akimuangalia shahidi kama walivyokuwa wakifanya watu wengine…lakini ule ukaaji wake ulitia mashaka maana alikuwa katulia nakichwa kipo kama kimeinama kwa nyuma na macho hayapepesi.

Wakili huyo akajifanya kama hakuna kitu akasogea na kukaa sehemu yake, na hapo akamshika kwenye paja , ili watu wasimuone, na akawa kama anamtikisa, lakini jamaa yule alikuwa kakaa vile vile, na hapo wakili huyo akagundua kuwa kuna tatizo, akageuka kumwangalia, msaidizi wake na wakawa wanateta.

Wote wakamsogelea huyo mshitakiwa mkuu, na kujaribu kumuita na kumtikisa, lakini alikuwa kimiya..kimiya..hakimu kumbe naye alikuwa akiifuatilia ile hali, akauliza kuna tatizo gani

‘Muheshimiwa hakimu, mshitakiwa anaonekana ana tatizo…’akasema wakili.

‘Ana tatizo gani?’ akauliza hakimu, na mlinzi akamsogelea na kumchunguza halafu akageuka kumwangalia hakimu;

‘Anaonekana kapoteza fahamu….’akasema mlinzi

‘Watu wa huduma ya kwanza wafike wamuangalie, wengine wote mtulie kama mlivyo..’akasema hakimu.

‘Natoa dakika kumi, …baaada ya hapo tutaangalia kama tunaweza kuendelea au kuahirisha hadi siku nyingine..’akasema hakimu, na akawageukiwa watu wa huduma ya kwanza, ambao walikuwa wakitoa huduma zao kwa huyo mshitakiwa mkuu, na walipomaliza, akawauliza;

‘Mnasemaje, kuna tatizo lolote?’ akauliza.

‘Mshitakiwa kapoteza fahamu…anahitajika awahishwe hospitalini kwa matibabu…’wakasema

‘Basi kama ni hivyo, tutaahirisha hii kesi ..hadi kesho….na taarifa zaidi mtapatiwa…’akasema  na kesi ikaahirishwa.

NB:  Je ni kwanini huyo mshitakiwa akapoteza fahamu….na je itakuwaje.. tuzidi kuwemo kwenye kisa hiki kinachoendelea mwishoni.

WAZO LA LEO: Kuna tabia sasa hivi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, watu wanapiga hadi kuua, wanachoma atu na nyumba zao, je ina maana ubinadamu tena hakuna, na kati ya hawo, kuna wengine hawana kosa kabisa, walituhumiwa tu, au chuki zao zimakimbilia kupakaziana ubaya,….kwanini tunaamua kumuadhibu mtu bila kuhakiki kuwa kweli ni mkosaji, je tuna mamlaka gani ya kuchukua hatua hiyo..hiyo sio vyema, kwani kosa ni kosa pale linapothibitishwa kisheria kuawa ni kosa,na hukumu yake itaainishwa kisheria. Kama wewe utachukua sheria mikononi mwako ujue na wewe unatenda kosa.

‘                                                                                                      



Ni mimi: emu-three

1 comment :

Unknown said...

Mmh, majanga ndugu yng. Ngoja tusubiri tuone huyo alipoteza fahamu