Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, July 25, 2013

WEMA HAUOZI-40Baada ya maelezo ya shahidi kijana, wakili, au muendesha mashitaka, alisema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, wakili mtetezi anaweza kuendelea naye. Na wakili mtetezi, akatabasamu, na kusimama, kwanza alimgeukiwa mteja, na akamnong’oneza kitu, na mteja wake akaonekana kutabasamu, na akageuka kumkabili huyo shahidi, na akaanza kuuliza swali;

Wewe unadai ulikuwa upo kwenye kundi la ulinzi shirikishi, na bosi wako alikuwa ni Jemedari, ina maana  moja kwa moja ulikuwa ukiwajibika kwa huyo bosi wako Jemedari, ndio au sio? akaulizwa.

‘Ndio ….lakini….’kabla hajaendelea kuongea huyo shahidi wakili akasema.

‘Sijakuambia utoe maelezo..jibu kama nilivyokuuliza….’akasema huyo wakili akimtolea macho huyo shahidi, na huyo kijana akaonyesha kushangaa usoni, na kugeuka kumwangalia wakili mwanadada, na wakili mwanadada akatabasamu, kumpa moyo.

Wakili wa utetezi, akageuza jicho upande ule wa wakili mwanadada, huku akiwa bado anamtizama shahidi huyo, akauliza tena;.

‘Kwahiyo kazi zako huwezi kufanya mpaka huyo Jemedari awaamrishe mfanye kama atakavyo yeye,…?’ akaulizwa.

‘Ndio, …..na…na wakati mwingine tunaamrishwa na kiongozi wa kijiji…..’akasema kwa haraka wakati huo huyo wakili alikuwa akimzuia kwa ishara ya mkono.

‘Jibu swali kama nilivyokuuliza,….’akasema huyu wakili huku akijafanya anatabasamu

‘Wewe umesema mlitumwa kwenda kumkamata Mzee wa kijiji, kwasababu alikataa maagizo halali ya kijiji, ….je ni kweli kuwa kulikuwa na maagizo halali kutoka kwa kiongozi wa kijiji,?’ akaulizwa

‘Ndio yalikuwepo, ….’akasema na kabla hajafafanua huyo wakili akauliza swali jingine.

‘Na mlipokwenda kwa huyo mzee, alitii hayo maagiza halali ya serikali ya kijiji, au aliendelea kukaidi kama kawaida yake…?’ akaulizwa.

‘Sielewi hapo unaposema kama kawaida yake….’akalalamika huyo shahidi na huku akigeuka kumwangalai wakili mwanadada, na wakili mwanadada, alitaka kusema jambo, lakini akasita.

‘Jibu swali kama nilivyokuuliza..’akasema huyo wakili mtetezi na wakili mwanadada akatoa pingamizi kuwa wakili mtetezi analazimisha kujibiwa swali, ambalo shahidi hajalielewa, na hataki kumfafanulia vyema shahidi, na shahidi anakuwa hana uhuru wa kujitetea, na hapo hakimu akamuonya wakili aulize kwa mujibu wa sheria.

Wakili huyu akageuka kumwangalia wakili mwanadada,huku akitaabsamu, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo shahidi , akiwa kabadilika kwa kukunja sura, na kuuliza;.

‘Je mlipokwenda kwake, alifanya nini, alitii amari halali ya serikali ya kijiji,au aliendelea kukaidi..amri halali ya serikali ya kijiji?’ akauliza akiwa anasisitizia hayo maneno `amri halali ya serikali ya kijiji’.

‘Alisema hawezi kuondoka kwasababu analinda mali ya mtoto wake?’ akasema, hapo wakili mtetezi akamwangalia huyo shahidi kwa mshangao, halafu akauliza huku akionyesha mshangao

‘Ina maana  huyo mzee ni baba yake huyo mwanamama?’ akauliza huku akiwa kama kategesha sikio moja kumsikiliza huyo shahidi.

‘Hapana, …ila…’akasema

‘Ila alikuwa akiingilia familia za wenzake na kujifanya yeye ni mzazi wa huyo binti kwa maslahi yake, na kuendelea kuwa mkaidi wa serikali….ndio au sio?’akaongea kwa haraka, na akawa kama anauliza swali, huku wakili mwanadada akiwa anatoa pingamizi kwa kulalamika kuwa wakili anatoa maelezo yake binafsi badala ya shahidi .

Hakimu alimuonya tena huyo wakili, na kama kawaida yake huyo wakili aligeuka kwanza kumwangalia wakili mwanadada huku akitikisa kichwa kama anakubali jambo,, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo shahidi akiwa kakunja uso …kuonyesha kukasirika na kusema;

‘Je mlipofika kwake, na mkiwa na mkuu wa serikali ya kijiji, mkuu ambaye mlimchagua nyie wenyewe, na huyo mzee alifanya nini??’ akauliza

‘Alisema….’akataka kusema na huyo wakili akasema.

‘Je alitii amri?’ akauliza.

‘Hakutiii…’akasema

‘Alifanya nini?’ akauliza

‘Alisimama pale pale ndani….’akasema huyo shahidi.

‘Na ikawaje ?’ akauliza.

‘Kiongozi wa serikali ya kijiji aliendelea kumsihi, na wakawa na maongezi ya muda ….lakini mzee hakukubali kwa sababu alizozitoa ambao hutai nizieleze…’akasema shahidi na watu wakacheka.

Huyo wakili naye akacheka na kumwangalia wakili mwanadada kama vile anamzihaki,

‘Nyie mlichuku hatua gani?’ akauliza.

‘Kwa kipindi hicho, walikuwa wakiongea na kiongozi wa kijiji, na baadaye kiongozi wa kijiji, akatupa amri ya kumtoa nje, na sisi tulijaribu kumshika mkono, ….’akasema

‘Na yeye alifanya nini?’ akauliza.

‘Alikataa kata kata,…’akasema

‘Hakuwatishia kuwapiga…?’pingamizi likawekwa na hakimu akalikubali, kwani ilionekana wakili anamlisha shahidi majibu.

‘Unasema mliarifia mumutoe nje, kwa hiari,au sio? Akauliza.

‘Kama ni hiari angelikubali kwa kiongozi wa kijiji, lakini kwa vile alikataa, ndio maana kiongozi wa kijiji, akasema tumtoe, kwahiyo hapo hakukuwa na hiari tena…’akasema huyo shahidi.

‘Kama alikataa amri halali ya kijiji, na kiongozi anayetambulikana, akajaribu kutumia hekima yake, nab ado mtu huyo akaendelea kukata, wewe unafikiri, hapo mlitakiwa mfanye nini?’ akawa kama anauliza, lakini kabla huyo shahidi hajajibu,akauliza.

‘Je mlipomwambia kuwa atoke, alifanyaje…?’ akauliza.

‘Sisi hatukuwa lugha ya kumbembeleza, maana kiongozi alituambai tumtoe, sio tumbembeleze kwahiyo tulianza kwa kumshika mkono…’akasema huyo shahidi.

‘Unaona, bado serikali ilikuwa ikimbembeleza, na hawa mashababi, hawakutaka kwanza kutumia nguvu, wakamshika mkono, halafu ikawaje….’akauliza huyo wakili.

‘Alikataa kutoka kwenye hiyo nyumba, na tulipojaribu kumvuta kwa nguvu ili atoke nje, akagoma, kabisa, na hapo tukasikia mjumbe akisema kama tumeshindwa kumtoa, basi ataongeza nguvu nyngine’ akasema.

‘Ulisikia mkuu wa kijiji akisema mtumie njia nyingine..ya kutumia nguvu, kumpiga n a vitu kama hivyo…?’ akaulizwa.

‘Sikusikia,…ila…’akabla hajajibu huyo wakili akasema.

‘Kwa jinsi hiyo , nyie mlitumia njia ,mliyoona inaweza kumtoa huyo mzee kutokana na ujeri wake, au sio,..?’ akaulizwa.

‘Ndio unaweza kusema hivyo….’akasema.

‘Njia ambayo mliona nyie, kama walinzi, kuwa inafaa, sio kutoka kwenye kinywa cha kiongozi wenu, …’akawa kama anauliza lakini hata kabla shahidi huyo hajajibu swali, akamgeukiwa muheshimiwa hakimu na kusema;

‘Muheshimiwa hakimu, mara nyingi watu kama hawa wanapotumwa mahali, hasa hawa vijana wanaweza wakatiumia njia walizofundishwa, lakini ukikutana na mtu mkaidi, kama huyo mzee, bila ya kutumia nguvu,…huwezi kufanikiwa, na wao wasingeliweza kumtoa kwa hekima, ….hawa ndio wakaidi, wasiopenda kutii amri halali ya kijiji….

'Muheshimiwa hakimu, kama tuwajuavyo vijana, bado damu inachemka, wao huenda waliona kuafanya hivi au vile itasaidia, na kwa mzee kama huyo akiguswa kidogo tu, ….ndivyo kama ilivyokuwa, na hali kama hiyo, mkadii hataki , vijana wakamtoa kwa nguvu hataki,…wao wakatumia mbinu zao, na matokea yake wanamtwika kiongozi wa kijiji mzigo wote….’akasema wakili wa utetezi na mwanadada akasema.

‘Hatuhitaji maelezo yako, tunachohitajia kwasasa ni ushahidi, je wewe ndio umegeuka kuwa shahidi, au unataka shahidi akubaliane na matakwa yako kinyuma na ilivyokuwa..’akasema wakili mwanadada, na huyo wakili akasema.

‘Mimi nimetoa maelezo kwa muheshimiwa hakimu, ili aelewe hali ilivyokuwa, sioni kuna ubaya hapo,..’akasema huku akimwangalia hakimu, na hakimuw akawa anaandika jambo kwenye makabrsaha yake., na alipoona hakimu hajasema neno akamgeukia shahidi.

‘Wewe unasema wakati mwingine mlikuwa mnapewa kazi maalumu, je taarifa ya kazi maalumu huwa unapewa na nani?’ akauliza.

‘Kazi maalumu zinakuwa za siri, kwahiyo kuna ishara tunapewa, ni ishara za kiutendaji, na yule aliyekuwa akribu, au aliyepewa taarifa hizo, anakufahamisha kuwa tunahitajika kwa kazi maalumu, lakini mara nyingi ni kiongozi wetu wa karibu ndiye anaweza kuja kutufahamisha….’akasema.

‘Kiongozi wenu wa karibu ukiwa na maana Jemedari au sio…?’ akaulizwa.

‘Ndio….’akasema.

‘Siku unapodai kuwa mlikwenda kufanya kazi ya siri, ambayo unadai uliambiwa umwage mafuta kwenye nyumba ya mzee wa kijiji, ni nani alikuambia kuwa kuna kazi kama hiyo?’ akauliza.

‘Ni ….ni mlini mwenzangu, alisema amepewa taarifa kutoka….’kabla hajaendeelea wakili huyo akamkataizi na kusema.

‘Swali langu lilikuwa wazi, ni nani alikuamba wewe kuwa kuna kazi maalumu?’ akaulzwa tena.

‘Ni mlinzi mwenzangu…’akasema.

`Safi kabisa…jibu swali kama mtu aliyekwenda shule…’akasema huku akitabasamu, na kugeuza kichwa kwa haraka kumwangalia wakili mwanadada, na huku akiuliza swali.

‘Na je katika pilika pilika za kazi hiyo, ni nani aliyekuwa akiwasimamia?’ akaulizwa.

‘Alikuwepo msaidizi wa Jemedari,..lakini baadaye nilikua kufahamu kuwa mkuu….’akataka kusema na wakili akamkatiza.

‘Sijakuambia utoe maelezo, jibu swali ninavyokuuliza….’akasema wakili huyo.

‘Mwenzako au kiongozi wa tendo hilo, ambalo hukujua ni amri ya nani, … akakuambia uanze kumwanga mafuta ya taa kuzunguka jengo hilo, unaweza kusema ni kwanini ilitakiwa mfanye hivyo?’ akaulizwa.

‘Mimi nilifuata maagizo ya mtu wangu huyo wa karibu na sikuwa na amri ya kupinga, ama kwanini, kuna uvumi ulienea…’kabla hajamaliza maelezo yake, wakili mwanadada akapinga kwa maelezo kuwa shahidi alikuwa akitoa maelezo, kitu ambacho wakili hakumuuliza na hayo anayotaka kuongea ni uvumi sio uhakika…

‘Sizani kwamba kazi maalumu kama hizo zinafanyika bila sababu, je huyu mtu wako wa karibu hakukuambia ni kwanini ufanye hivyo? Akaulizwa.

‘Kwa muda huo hakukuwa na muda wa maelezo, ….’akasema.

‘Kwahiyo kumbe wewe uliweza kupokea amri yoyote kutoka kwa mtu wako wa karibu, na inawezekana isiwe imetoka kwa mkuu wa kijiji, inawezekana ilitoka kwa Jemdari, inawezekana ilitoka kwa yoyote mwenye nia mbaya, au uadui na huyo mzee…..’akasema na kugeuka kwa hakimu na kusema hapo nimemaliza.

Wakili mwnadada akasimama na kumuendea huyo shahidi, na kuuliza swali.

‘Wakati ulipojiunga na kundi hilo, uliambiwa ni nini majukumu yako ya kazi?’ akuliza.

‘Tulipewa mkataba wa kazi zetu, na tukafafanuliwa kwa maneno juu ya hayo yaliyoandikwa na kusisitiziwa kuwa tusije kukiuka hayo yaliyoandikwa hapo ….’akasema.

‘Kwenye mkataba huo, kuna maelezo gani ya kipengele cha kazi maalumu?’ akauliza

‘Kuna maelezo kuwa kazi maalumu, zitatolewa na kiongozi  wa kijiji, …na kiongozi wa kundi, atasimamia kazi hizo, kwa maslahi ya kijiji…..’akasema.

‘Kwahiyo kazi zote maalumu, kutokana na mkataba wenu, zilikuwa zimetoka kwa nani….?’ akauliza.

‘Kwa kiongozi wa kijiji….’akasema na wakili mwanadada akatabasamu.

‘J e katika utendaji wako wa kazi, ulishawahi kufanya kazi maalumu na baadaye ukagundua kuwa haikutoka kwa mkuu wa kijiji?’ akaulizwa.

‘Hapana haijawahi kutokea hata mara moja, maana wote tulikuwa tumefundishwa sheria na mkataba wa ajira yetu, na ni nini madhara yake kama utafanya kazi kinyume na utaratibu uliowekwa…’akasema.

‘Kwahiyo hata kazi hiyo ya kuchoma moto, ilitoka kwa mkuu wa kijiji?’ akauliza.

‘Ndio, ….’akajibu na wakili mtetezi akalalamika kuwa wakili anamlisha shahidi majibu, nahaki akasema shahidi aendelee

‘Na wakati mnampiga huyo mzee, mkuu wa kijiji alikuwa wapi?’ akauliza.

‘Alikuwa nje….na alipoona kuwa tumeshindwa kumtoa huyo mzee alituongezea watu tukawa watu saba, na wenzetu walipofika hawakukata kujua zaidi wakaanza kumpiga mzee kwa nguvu zote, hadi akawa kama anapoteza fahamu….’akasema.

‘Wewe ulifanyaje?’ akaulizwa.

‘Mimi nilikuwa nawasihi wasifanye hivyo, kwani katika mikataba yetu hatukuruhusiwa kumuumiza mtu ambaye hana silaha, au keshasalimu amri, hasa wazee na akinamama, labda kuwe na sababu maalumu ambayo itathibitishwa na kiongozi, ….mkuu wa kijiji..’akasema na wakili mwanadada akageukiwa wakili wa utetezi, na akawa kama anamuuliza. Na wakili mtetezi akatabasamu na kumgeukiwa shahidi

‘Unasema kwenye mkataba yenu, mliambiwa kuwa msitumie nguvu, labdakuwe na sababu maalumu  sababu kama ipi? akaulizwa.

‘Kama huyo mtu ana silaha, au akaanza kutupiga, …’akasema.

‘Je ,mlipofika kwa huyo mzee, alikuwa na silaha yoyote mkononi?’ akauliza

‘Alikuwa na panga…’alipojibu hivyo huyo wakili akamgeukiwa hakimu na kusema,

‘Ni hayo tu muheshimiwa, na wakili mwanadada, akamuendea shahidi nakuuliza.

‘Je unamfahamu vyema huyo mzee, tabia yake …?

 ‘Ndio ninamfahamu sana..’akasema

‘Je kila mara anakuwa na nini mkononi?’ akaulizwa

‘Kila mara anakuwa na panga mkononi…’akasema huyo shahidi na wakili mtetezi, alitaka kuuliza swali lakini akawa kama kakumbuka kitu, akasema;

‘Sina swali jingine muheshimiwa hakimu. Na hakimu akasema

‘Je kuna swali jingine kwa huyo shahidi, na wakili mwanadada, akasema,

‘Ndugu muheshimwa hakimu, tunaendelea na maelezo ya shahidi huyu, sehemu ya pili …..’akasema na wakili mtetezi akapinga, kwa kusema, huyo shahidi allishamaliza maelezo, kama kuna sehemu ya pili, basi shahidi huyo arudi, na atasimamishwa tena.

‘Kwani ni shahidi huyo ni wako au shahidi wangu, utatupangiaje utaratibu …’akasema wakili mwanadada.

‘Uliposema kuwa tumuulize maswali, ulikuwa umehitimsisha na huyo shahidi, hatukusikia ukisema kuwa utaendelea naye baadaye…..’akasema.

‘Huu ni utaratibu wetu,..na tunaweza kufanya tupendavyo, wewe kazi yako ni kujietetea kwa kuumuliza maswali, kwani una shaka gani anye…..?’ akauliza wakili mwanadada na huyo wakili akageuka kumwangalai hakimu, ili kutaka msaada, na hakimu, akatulia kama anawaza jambo, halafu akasema;

‘Sawa endelea…..lakini hata mimi sijafurahia na huo utaratibu wako, nakuonya usifanye hivyo tena…’

‘Ahsante muheshimiwa hakimu, tulifanya hivyo kama sehemu yetu ya kuhakikisha kila hatua inaeleweka vyema, lakini kama haitawezekana kwake yeye kuendelea kwa sasa, tunaweza kumpumzisha na tukaita shahidi mwingine, halafu tutakuja kumuita baadaye.Hakimu akageuka kuangalia upande wa upinzani na wakili mtetezi akasema;

‘Sisi tunaona amuite shahidi mwingine, na kama ni muhimu, basi atamsimamisha huyo shahidi baadaye maana hatukua kuwa kuna sehemu ya kwanza ya pili ya tatu……’akasema huyo wakili mtetezi akifanya ka mzaha, na watu wakacheka, na wakili mwanadada, akatabasamu na kuinua mkono juu kama kujipongeza, kitu ambacho kilimfanya wakili wa utetezi, amwangalie kwa mshangao.

‘Kabla shahidi mwingine hajaitwa hajasimama, ninatoa mapumziko ya dakika tano, halafu nawahitaji mawakili wa pande zote mbili nitete nao kidogo, dakika tano tu…’akasema .

 Kila kundi lilikutana na na kukawa na mazungumzo ya hapa na pale, na kipindi hicho, wakili mwanadada alikuwa kaondoka kama walivyoitwa na hakimu, hawakukaa sana, wakili mwanadada akarejea, na akasogea upande ula alipokuwa kakaa Mzee wa kijiji, kama wanavyomuita, au baba yangu wa kufikia, na wakawa wanaongea na mzee huyo, na mazungumzo yao yalionekana ni ya faragha, kwani walikuwa wameinama na kuongea kwa sauti ya chini kwa chini, na hapo, na baadaye kidogo wakili mwanadada akasema;

‘Natumai wakati umefika haina haja ya kusubiri….’nikasikia wakili mwanadada akiongea kwa sauti tofauti na alivyokuwa akiongea mwanzoni na huyo mzee.

‘Hata mimi naona hivyo, ….’akasema huyo mzee wa kijiji, na mimi pale nilipo nikahisi kuna jambo kubwa linataak kutokea, na nilipoangaangalia upande ule wa watetezi, nikaona mtu mwingine kaongezeka, na mtu huyo alikuwa naye kainama akiongea na mkuu wa kjiji, inaonekana walikuwa na furaha kubwa kama kuna jambo ambalo wameona litawasaidia, na yule mtu alipoinuka aliangalai upande watu.

‘Unamuona , shemeji kaweza kuja leo…’nikauliza na wakili mwanadada ambaye bado alikuwa akiteta na mzee wa kijiji, akainua kichwa na kuangalia upande ule wa washitakiwa  na huku akiuliza

‘Ni shemeji yupi huyo…?’ akauliza

‘Mchumba wako….’nikasema na wakili mwanadada akawa kama kashituka kusikia hivyo, akainua kichwa kuangalia upande ule, kwa haraka halafu akarudisha kichwa chini na kujifanaya anaendelea kuongea na huyo mzee, lakini nilihisi macho yao yakigongana, na nini kila mmoja wao anawaza ikawa siri yao.

 Mimi nikageuza kichwa kumwangalia shemeji yangu huyo, na macho yetu yakagongana, na yeye akajitahidi kutabsamu, mimi nikageuza kichwa haraka kumwangalia wakili mwanadada ambaye alikuwa katulia, na baadaye akasema;

‘Huyu naye kafuata nini , mtu anaumwa, badala ya kupumzika anakuja kujitakia mawazo mengine ya bure, hawajui hawo watu aliokuwa nao….angeliwajua asingeliwakaribia kabisa,….’akasema.

‘Atajua tu muda wao umefika kuumbuka…’akasema baba yangu wa kufikia, na kama vile tulipanga wote tukageuza vichwa kuwaangalia, na kumbe na wao walikuwa na wakituongela maana wote wakawa wanatuangalia sisi, na mara sauti ya ya hakimu ikatushitua pale aliposema;

‘Aletwe shahidi mwingine…’

Na  mlango wa mashaidi ukafunguliwa na wakati huu akaingia mwanamke akiwa kajifunika khanga sehemu zote, kuanzia kichwani hadi miguuni. Kwa jinsi alivyovaa, kila mtu akawa anamtizama yeye, na kwa mshangao, hata hakimu naye akajikuta akimtizama kwa mshangao, …

NB: Je ni nani huyu.


WAZO LA HEKIMA: Tuwe makini na marafiki, tuwe makini na taarifa zinazoletwa kutoka kwa wale tunawajua kama marafiki, ni vyema, tukafanya uchunguzi wa taarifa hizo, kwani sio kila taarifa inaweza kuwa kweli, eti kwa vile inatoka kwa hawo tunaoona ni marafiki. 

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Nancy Msangi said...

Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg

Nancy Msangi said...

Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg

Nancy Msangi said...

Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg