Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, July 22, 2013

WEMA HAUOZI-38Kesi ilianza tena, na watu waliofika siku hiyo ilikuwa haijawahi kutokea, japokuwa walipewa habari mapema kuwa hawataruhusiwa wasikilizaji , lakini watu hawakusikia hilo, habari ya kesi hii ilikuwa imetapaa sehemu kubwa, na kila mmoja alitaka kufika ajionee mwenyewe. 

Walianza kufika mtu mmoja mmoja, na kila aliyefika aliaambia asikaribie eneo hilo la mahakama kama haruhusiwi, lakini kika muda ulivyozidi kwenda ndivyo watu walivyozidi kufika, na hata ilipotimia muda wa kesi, umati wa watu ulikuwa umejezana, eneo karibu na mahakama,  ikawa ni kazi ya ziada ya walinzi wa usalama ambao walijitahidi kuhakikisha kuwa hakuna tatizo lolote lingeliweza kutokea tena.

‘Hatuwezi kuwaruhusu watu kuingia tena eneo hili mahakama, na mgari yote ya wahusika muhimu yataingia moja kwa moja ndani kwa kupitia mlango huu maalumu, nay a watu wengine ambao ni wasikilizaji tu , hatutaweza kuyaruhusu kuingia ndani au kusimama eneo hili la karibu ya mahakama…’tangazo likatolewa.

 Ni kweli lawama kubwa ilikuwa imeelekezwa kwa walinzi wa eneo hilo la mahakama kuwa wao walizembea hadi yule matu akafika eneo hilo na kusababisha ajali ambayo imekuwa ni gumzo la watu wengi, kila mmoja akisema lake..

‘Hebu jiulizeni, kwanini siku ile ya kesi mlango wakuingiza magari haukufunguliwa mapema, inaonekana kulikuwa na njama fulani zilipangwa…ili gari hilo la mwanadada, lisiingie mapema ndani na huyo mtu afike hapo na kumgonga, ilikuwa imepangwa hiyo……’wakawa wanasema watu. Hata hivyo uchunguzi uliofanyika haukugundua lolote kuhusiana na lawama hizo. Kilichoongelewa ni kuwa huyo jamaa alikuwa mlevi tu, ….

‘Haiwezekani, kuna kitu kinafichwa hapo…’wakasema watu walikuwa wakifuatilia sana hiyo kesi.

‘Lakini kama mahakama haiwezi kudanganya,..inawezekana ni kweli, na huyo mlevi mwenyewe wamemchukulia hatua gani?’ wakauliza watu.

‘Nasikia kawekwa ndani na pombe zilipoisha akawa anapiga mgaoti kuomba msamaha, kwani mwajiri wake anamfukuza kazi na yeye ndio katoka kuajiriwa karibu, na kukabidhiwa hilo gari, kwa ajili ya kumchukua bosi wake…’wakasema .

‘Yaani kumbe hata hilo gari sio lake….kweli hapo kaingia choo cha kike,huyo kazi hana…’mmoja akasema.

‘Nasikia huyo bosi walifika kumwekea dhamana, lakini akaambiwa dhamana kwa sasa haitakubalika, kwani kuna uchunguzi bado unafanyika…’akasema mtu mmoja.

‘Hamuoni kuwa hapo kuna jambo, kwanini kama ni mlevi tu, waendelee kumshikilia, …nahisi kuna jambo hawataki lijulikane, au ni kutokana na uzembe wao, au kuna uchunguzi ambao huenda wakiusema utaharibu mpangilio wa kesi yao…’wakazidi kuongea wachunguzi wa mambo.

‘Lakini yote tutayaona siku ya kesi,…tusubiri siku, ni mimi ni lazima nifike japokwua wametoa tanagzo kuwa wasikilizaji hawataruhusiwa, kuingia eneo la mahakama, lakini hata nikikaa nje, kusubiria inatosha.

‘Yaani uache shuguli zako kwa ajili ya hiyo kesi, halafu utapata nini, badala ya kuhangaika na kutafuta riziki ya watoto wako, wewe unahangaika na kesi za watu, ili kupata umbea….’akasema mwenzake.

‘Hii nayo ni ajira, hujui kuwa mimi ninauza taarifa kwa gazeti moja la udaku,…mjini hapa,…’akasema na wote wakacheka.

******

‘Hivi leo wakili mwanadada atakuwepo?’ ilikuwa swali la kila mtu, nawengi walifika hapo kwa ajili ya kumuona yeye, kwani kulikuwa na uvumi mwingi, wengine walifikia kudai kuwa wakili mwanadada alipogongwa, aliathirika ubongo, na hadi sasa hajijui…

‘Mna uhakika na hilo?’ wakaulizana watu.

‘Inawezekana kuna ukweli, maana tangu litokee lile tukio huyo mwanadada hajawahi kuonekana hadharani…’akasema mtu mmoja.

‘Inawezekana aliumia sana, lakini hospitalini hayupo tena, mimi nilifuatilia, nikaambiwa keshatoka, ila mimi nahisi wanafanya hivyo kwa ajili ya usalama wake, kwani imebainika kuwa kuna watu huenda wanataka kumuua..’akafafanua mtu mmoja.

‘Lakini kwanini watake kumuua, wakati ni mtetezi tu wa wanyonge?’ akauliza mwanamama mmoja.

‘Kama anatetea wanyonge, ina maana kuna watu hawapendi hivyo, kwasababu kwa yeye kufanya hivyo, hawatapata hicho wanachokitaka kwa hawo wanyonge,….’akasema mwanaume mmoja aliyekuwa karibu naye.

‘Hata wafanye nini, mimi nina imani kuwa mwisho wao umeshikafika, ni kutapatapa kwa mfa maji…’akasema huyo mama.

‘Usiseme hivyo wewe mwanamke, wewe unacheza na pesa, hawo wenye pesa wanaweza wakafanay hii kesi ikapigwa tarehe, hadi watu wakachoka, huoni ile kesi ya yule mwanadada aliyekuwa kadhulumiwa mali zake, mpaka sasa inapigwa tarehe…’akasema huyo mwanaume.

‘Lakini wametoa sababu za msingi, kuwa wanahusika na kesi ile , wengi wapo kwenye kesi hii, kwahiyo wameona cha msingi ni kumalizana na kesi hii, ambayo ina umuhimu wake sana. Halafu yule hakimu aliyekuwa akisimamia kesi hiyo alipata uhamisho, akaletwa hakimu mwingine, na huyo hakimu mwingine kabla hajaanza kazi, na yeye, akapatwa an dharura, mama yake yupo taabani, anaumwa sana ni wa kusikilizia, kwahiyo kaondoka kumuona mama yake.

‘Kwanini hayo yatokee …wewe hujiulize tu , unaweza ukaona ni mambo ya kawaida, lakini wenzetu wana kila mbinu…..wewe chezea na watu wenye pesa. Wewe huoni jinsi mataifa makubwa yanavyofanya, mfano huo tu, utakuonyesha kuwa, pesa inaongea. ….’akasema huyo mwanaume.

‘Sasa hayo ya mataifa makubwa yanahusiana vipi nah ii kesi…?’ akauliza huyo mwanamke.

‘Angalia kwa mfano wao wameanzisha demokrasia, kuwa wengi wape, lakini angalia pale wanapotaka mtu fulani asiwepo kwenye madaraka, demokrasia hiyo hiyo inaoat makengeza, utasikia visingizio kbao, na wakiona vipi, wanasimamia vikundi vya upinzani kuhakikisha nchi hiyo haina usalama….’akasema huyo mwanaume.

‘Lakini hayo yanahusiana vipi nah ii kesi?’ akauliza mama mwingine, akiona kama huyo jamaa anamchanganya.

‘Hilo nimekutolea mfano jinsi gani pesa ilivyo na nguvu…matajiri wana kila mbinu, za kuweza kubadili hali ya hewa…’akasema na wale akina mama wakaona huyo jamaa anawachanganya na mwanaume mmoja akauliza

‘Lakini kweli mbona kesi imeanza na huyo wakili mwanadada hajaonekana, inawezekana kweli anaumwa, au ….?’

Lakini hata kabla kabla mtu mwingine hajasema kitu, mara gari la wakili mwanadada likaingia mbele yake kukiwa na gari jingine, lilikuwa kama gari la waheshimiwa wanavyosindikizwa, na walipofika tu eneo la mahakama , mlango wa geti ukafunguliwa haraka, na magari hayo yakaingia ndani.

Gari la wakili mwanadada lilipofika tu, akatokea mtu mmoja, aliyekuwa kwenye gari la mbele na kuja kumfungulia wakili mwanadada, na huyu dada akatoka kwenye gari, hakugeuka kuangalia upande uli waliokuwepo watu, ambao walianza kusukumana kutaka kumuona vyema, …yeye kwa haraka akakimblia kwenye jengo la mahakama, kwani kesi ilikuwa ikiendelea na yeye alichelewa kufika.

*********

Baada ya utulivu kwenye mhakama, maana watu walishindwa kujizuia kuonyesha hamasa, zao pale mshitakiwa mkuu wa kesi hiyo alipoletwa mbele ya mahakama, kwani wengi walishafikia kusema mshitakiwa huyo ana nguvu za giza, na kila akitaka kukamatwa haonekani, lakini leo kafika, kwahiyo wengi walipomuona akiingizwa, wakashindwa kuvumilia na kuanza kusimama kumwangalia huyo mshitakiwa.

‘Ina maana nyie hamuoni mpaka msimame…’wakawa wanalalamika watu walio kuwa nyuma.

‘Ni maajabu, huyu mtu leo kuwepo hapa mahakamani….’akasema mama mmoja.

‘Wewe unacheza na sheria, sheria, haishindwi na nguvu za giza hata siku moja…’akasema mama mwingine

‘Nyie tulieni, mtaishia jela…’wakaonywa na mtu wa usalama aliyekuwa karibu yao.

*******
‘Ndugu hakimu, kutoka na maelezo yangu hayo, nahitimisha kwa kusema kuwa shutuma hizi dhidi ya mteja wangu ni za kusingiziwa, kwani hazina msingi wala ushahidi halisi, zote zimejengwa kwa hisia za chuki binafsi…’wakili akawa anataka kufungua ukurasa mwingine, lakini akagundua kuwa huo ndio ukurasa wa mwisho wa maelezo yake.

Wakili wa utetezi akahitimisha taarifa yake , na kuinama kidogo, kuonyesha adabu yake kwa muheshimiwa hakimu. Huyu alikuwa wakili ambaye alitafutwa kwa ajili ya kumtetea mjumbe wa nyumba kumi, baada ya wakili wa mwanzo kupatwa na ajali ya kugongwa na gari, akijaribu kumuokoa wakili mwanadada.

Kikawa kipindi cha kuwaita mashahidi wa pande zote mbili, waliitwa mashahidi mbali mbali, kutokana na mpangilia wa mwendesha mashitaka,  na kila aliyeitwa kila akimaliza kutoa maelezo yake, akiongozwa na mwendesha mashitaka, wakili wa utetezi alimuhoji, na kila alipomaliza kuhojiwa, kwa maswali ya kisheria, ilionekana kweli, huyo wakili mpya anaweza akabdili sura ya hiyo kesi.

‘Duuh, huyu wakili jembe, maana mashaidi wote wanaonekana kama vile wamatumwa  kuongea na maelezo yao hayana nguvu, ..’akasema mmoja wa watu waliokuwemo humo ndani, na wakati anaitwa shahidi mwingine, mara mlango wa mhakama ukafunguliwa, na watu wakajikuta wakigeuza shingo kuangalia ni nani aliyeingia.

Kila mmoja akajikuta kipumua, na hata hakimu, akajikuta na yeye akimwangalia huyo aliyeingia, na sekunde chache zikapita, kabala shahidi aliyekuwepo hapo kuendelea kuhojiwa na watetezi.

Huyu muendesha mashitaka mpya aliyeingia, alisogea hadi kwenye meza ya waendeshaji wa mashitaka, na kukaa kwenye sehemu yake, na muendesha mashitaka akamsogelea na kuanza kuteta naye, hawakujali kusikiliza huyo shahidi anavyohojiwa, na baada ya kuteta kidogo, hakimu akauliza kuwa kuna shahidi mwingine.

Hapo akasimama  muedesha mashitaka na kusema yupo shahidi mwingine, na alipotaka kumataja, mara akasimama huyo wakili aliyeingia na kumnong’oneza mwenzake, na mwenzake akatikisa kichwa na kurudi nyuma, na ilionekana kuwa huyo muendesha mashitaka mpya aliyeingia ndiye anataka kuendelea na hiyo kesi,  na kusema ;

‘Yupo shahidi mwingine muheshimiwa hakimu, …anaitwa Kijana.’na watu wakaanza kunong’ona, na kama tujuavyo minong’ona ya watu wengi, ni ngurumo, maana hata hakimu ilibidi agonge rungu lake na kusema watu watulie na kufuata taratibu za kimahakama.

********
Upande wa utetezi, ulikuwa kimiya, na mtu aliyeonekana kuathirika zaidi alikuwa ni mshitakiwa mkuu, ambaye ndio kwanza kesi yake ilianza leo, baada ya kukosekana kwenye kesi zilizopita kwasababu zilizokubalika na mahakama.

‘Hilo jina mbona ni la marehemu, mimi nina ushahidi kuwa kijana huyo alishafariki…’akasema huyo mshitakiwa mkuu.

‘Labda wana maana yao kuweka hilo jina, usiwe na wasiwasi nitapambana naye,….’akasema wakili wake ambaye likuwa mtu wa kujiamini sana.

‘Shahidi wetu mwingine ni Kijana, …’akasema tana huyo muendesha mashitaka aliyeingia alikuwa kavalia mawani, iliyoonyesha kuwa huenda kaja kuchukua nafasi ya mwanadada, na wengi walivunjika nguvu, wakijua mtu waliyetama kumuona hatakuwepo kwenye hiyo kesi, na mara watu wakaanza kunong’ona kila mmoja akisema lake, na hkimu akasema;

‘Tunahitaji ukimiya, na taratibu za mahakama zifuatwe, shahidi apite mbele..’akasema hakimu, na mara kutoka mlango wa wanaoingilia mashahidi akatokea kijana mmoja, ambaye kwanza likuwa kava kofia pana, lilofunikwa shemu kubwa ya kichwa chake, na akaamuriwa kulivua.

Alipolivua, kila mmoja alibakia kinywa wazi, na aliyeshindwa hata kujizuia alikuwa ni mshitakiwa mkuu, ambaye alijikuta akisema;

‘Haiwezekani,….ina maana huyu kijana hakufa…’akasema na wakili wake akasema;

‘Una wasiwasi gani, …wewe subiri jinsi gani nitakavyomtoa jasho,..’akasema huyo wakili wake mtetezi.

‘Kijana hebu elezea ilivyokuwa ……..’akasema mwongoza mashitaka, baada ya kumuuliza maswali kadhaa huyo kijana, wakati anamuongoza kutoa maelezo yake ya awali, na kabla hajajibu mlango ukafunguliwa, na watu wote wakageuza kichwa kumwangalia ni nani tena huyo aliyeingia, …..na haliikabadilika ghafla, maana wengine walishindwa kuvumilia na kuinuka kuhakiki macho yake, na ikawa ni hamsa iliyofanya dakika chache zipite, kabla hakimu hajaginga rungu lake, kuhakikisha utulivu na sheria za kimahaka, zinafuatiliwa.

‘Kwani ni nani huyo aliyeingia…?’ akauliza mshitakiwa mkuu, ambaye kutokana na kusimama kwa watu, hakuweza kumuona vyema huyo aliyeingia, na kipindi hicho hakimu anaamrisha watu watulie, upande ule wa waongoza mashitaka ulikuwa umekutana kwa pamoja, wakiteta jambo, na kuweza kumzuia huyo mashitakiwa mkuu kugundua  vyema huyo aliyeingia ni nani,

‘Ni wakili mwanadada…..!’ akasema wakili mtetezi wa huyo mshitakiwa mkuu.

‘Eti nini..haiwezekani….’akasema mshitakiwa mkuu, na kelele za watu wakirudi kwenye shemu zao kukaa, na wengi wao walioshindwa kujua wapo mahamani na kuanza kushangilia walitulia sasa wakisubiria ni nini kitafuta.

NB:Kesi hiyo, shahidi asiyetarajiwa akaingia, na wakili aliyesubiriwa kwa hamu naye akaingia, ni nini kitafuta. Sehemu hii ni kama utangulizi wa kesi yenyewe, tuwe pamoja kwenye sehemu ijayo, je kweli pesa ina nguvu kulika haki na ukweli? Na ni nini thamani ya wema.


WAZO LA LEO: Wengi wanadai kuwa pesa ni kila kitu, ukiwa na pesa unaweza ukafanya upendavyo, na hata kuinunua haki..Sio kweli, mbele ya haki, hata pesa, inaweza isiwe na thamani yake, ka lengo la hiyo pesa ni kuibatlisha haki. Elewa kuwa wakati wote haki na ukweli na ushuhuda usioshindwa kwa thamani ya pesa.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Nancy Msangi said...

Kama utakuwa Una pesa hlf hutendi haki sidhani km Ina maana na mwisho wa siku haki itaonekana tu,haya tusubirie kinachofuata.